Ruka hadi kwa yaliyomo
Printable page generated Alhamisi, 5 Des 2024, 00:54
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Alhamisi, 5 Des 2024, 00:54

Namba ya moduli 2: Kutalii Maendeleo ya Jamii

Sehemu ya 1: Kutambua mtandao (muingiliano) wa jamii

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kugundua mtandao wa jamii kwa kutumia igizo kifani, michoroti ya familia na wataalamu wenyeji?

Maneno muhimu: igizo kifani; tofauti; kutatua tatizo; madarasa makubwa, mtandao wa kijamii, michoroti ya familia.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kuanzisha majadiliano na kutumia michoroti ya familia kubainisha wana-familia wa karibu na wa mbali wa wanafunzi;
  • Kutumia igizo kifani na mbinu ya utatuzi-matatizo kutalii mtandao na mahusiano katika shule;
  • Kufanya kazi na wataalamu wenyeji ili kuboresha maarifa ya wanafunzi kuhusu mitandao ya kijumuiya.

Utangulizi

Watoto wanatoka katika familia, koo, makabila na jumuiya nyinginezo mbalimbali zinazowatambulisha wao ni kina nani. Ukiwa mwalimu, unahitaji kuwa makini na tofauti hizi na kujitahidi kuwajumuisha wanafunzi wako katika makundi yote haya katika jitihada za kuwa na mitandao mikubwa zaidi.

Katika sehemu hii, utatumia mbinu mbalimbali za ufundishaji na Nyenzo-rejea ili kuwasaidia wanafunzi wako kutambua mahusiuano yaona kuheshimu tofauti zao. Tunaanza na majadiliano na kuchora mchoro wa miti wa familia uoneshao mahusiano ya kifamilia. Utatumia shughuli za igizo kifani na mbinu ya utatuzi-matatizo ili kuwasaidia wanafunzi kutambua mahusiano yao ya kifamilia shuleni.

Mwisho, tunakushauri kuwa umkaribishe mtaalamu kutoka katika jumuiya ili aelezee mahusiano ya kifamilia makubwa zaidi ambayo huunda sehemu ya maisha ya wanafunzi.

Somo la 1

Sisi sote tuna mitandao tofauti ya kifamilia lakini kuna sifa na miundo ambayo tunaweza kuilinganisha. Wakati wa majadiliano ya mahusiano ya kifamilia, utagundua kuwa baadhi ya wanafunzi darasani kwako wanaweza kuwa wanatoka katika miundo ya familia ilyo tofauti ukilinganisha na wengine. Utahitaji stadi maalum kuwasaidia vijana hawa ili waweze kumudu tofauti zao na kuhakikisha kuwa vijana wengine darasani nao wanakubali tofauti hizi bila kinyongo.

Madarasa makubwa huibua matatizo maalum kwa walimu-hasa wakiwa wa madarasa tofauti. Mawazo yanatolewa katika Uchunguzi kifani 1 na Shughuli 1 kuhusu jinsi ya kutalii mitandao ya kifamilia; yatumie ukiwa na madarasa yenye idadi tofauti ya wanafunzi na wakiwa katika madarasa tofauti.Mbinu zilizotumika hapa ni uwasilishaji, majadiliano ya vikundi vidogo, na kutoa mrejesho.Nyenzo-rejea muhimu: Kufanya kazi na madarasa makubwa/madarasa tofauti huibua mawazo zaidi.

Uchunguzi kifani ya 1: Kuzungumzia aina za familia na darasa kubwa

Mama Ndonga kutoka Namibia ana darasa la wanafunzi 72. Darasa linashughulikia muingiliano wa jamii na anahitaji kutumia mbinu mbalimbali kuwasaidia wanafunzi wake kutambua aina mabalimbali za familia. Anafahamu kuwa ni muhimu kuwasaidia wanafunzi wake kugundua vitu wenyewe, badala ya kuwaeleza. Anaeleza kuhusu aina mbalimbali za familia na kuwauliza wanafunzi wake maswali mbalimbali kuhusu aina hizo. Hali hiyo inamwezesha kufahamu wanafunzi wake wanajua nini na kuwafanya wazipende habari hizo. Anagundua kuwa wanafunzi watatu wa kike waliokaa nyuma ya darasa hawakujibu maswali yake, na akaamua kuzungumza nao baada ya darasa. Kwa pamoja, wanafunzi walitambua makundi mbalimbali ya kifamilia ikiwa ni pamoja na

kiini cha familia na familia za mtandao mkubwa zaidi, mzazi mmoja na familia zinazoongozwa na watoto.

Wanafunzi wamekaa katika madawati ya watu watano watano na Mwalimu Ngunda aliwaacha wakae hivyohivyo. Vikundi vya wanafunzi waliokaa kwenye madawati ya aina hiyo havifai kwa majadiliano ya vikundi, lakini pia ndio njia pekee inayotumika, hasa darasa likiwa kubwa. Vikundi hivi huwa vimechanganyika - vina wanafunzi wenye umri tofauti na uwezo tofauti.

Kila kikundi kwenye dawati kinazungumzia hali halisi ya kwao na kinatambua aina tofauti za makundi wanamoishi. Vikundi vinatoa taarifa zao na Mwalimu Ndonga anaorodhesha ubaoni aina mbalimbali za familia. Wanafunzi wananakili orodha katika madaftari yao. Wanagundua kwa kuamsha mikono idadi ya aina mbalimbali za familia katika darasa lao. Wanajadiliana katika darasa kuhusu kwa nini ni muhimu kuheshimu tofauti za kila aina ya familia.

Katika somo linalofuata, Mwalimu Ndonga anakiuliza kikundi katika dawati lilelile kwa nini tunaishi katika makundi ya kifamilia. Sababu wanazotambua zimeoneshwa katika Nyenzo-rejea 1: Sababu za kuishi katika familia. Vikundi hivi pia vinajadili kuhusu nyumba wanamoishi na jinsi zilivyotengenezwa. Mwisho, wanaandika insha fupi kuhusu familia na nyumba zao na kueleza jinsi zinavyotofautiana na mwanafunzi mwingine darasani, hasa rafiki yake.

Shughuli ya 1: Majadailiano na mrejesho kuhusu mtandao wa kifamilia

Kuhusu tendo hili, unahitaji kutayarisha somo kutalii mtandao wa kifamilia., Ili uweze kutekeleza hili unahitaji kufikiria yafuatayo:

Kama una wanafunzi wakubwa au darasa kubwa, itafaa kutumia mbinu za maelezo na mrejesho kama alivyofanya Mwalimu Ndonga. Kama wanafunzi ni wadogo unaweza kutumia makundi au darasa zima kufanya majadiliano, lakini unaweza kuona kuwa kutumia mchoroti wa familia unaweza kuwafanya wanafunzi waelewe zaidi mahusiano ya familia zao. (Taz. Nyenzo-rejea 2: Mahusiano ya kifamilia .)

Kama una wanafunzi wadogo unaweza pia kutumia igizo kifani, wakijifanya wao ndio wana familia. Itafurahisha kuona ni nani mwenye familia ya watu wengi zaidi au nani mwenye familia yenye wanawake wengi zaidi. Unaweza kuhusisha hali hiyo na kazi za uchunguzi katika masomo ya Hisabati.

Chukua tahadhari kama una familia zinazoongozwa na watoto, kwa kuwa wanaweza kujiona tofauti na na hivyo kuona aibu au kufadhaika. Utahitaji kuwapa moyo vijana hawa na kuwasaidia wajisikie vizuri. Hakikisha kuwa wanafunzi wengine hawaathiriki kuona tofauti zao na kujihisi vibaya.

Utaanzaje darasa ili kupata usikivu wao? Utataka wanafunzi wafanye shughuli gani ili kupata matokeo ya ujifunzaji wa somo?

Ukipendezwa na andalio lako la somo, lifundishe.

Somo la 2

Watu, hususan vijana, hujisikia vizuri na salama wanapokuwa sehemu ya kundi. Hii ni kweli hasa nje ya familia. Shuleni, kwa mfano, makundi ya marafiki ni muhimu kwa vijana. Mara nyingi makundi ya marafiki huwa na matokeo chanya, lakini wakati mwingine yanaweza kuwa na athari hasi kwa baadhi ya vijana ambao hawakushirikishwa au wanaoonewa na wengine. Katika sehemu hii, utatumia igizo kifani na mbinu ya utatuzi wa matatizo ili kuwasaidia wanafunzi wako kutambua makundi yao na athari zinazosababishwa na makundi hayo katika maisha yao ya kila siku.

Utahitaji kutumia muda kiasi ukitayarisha maigizo kifani yanayofaa kwa kuzingatia umri wa wanafunzi wako darasani. Baadhi ya mapendekezo yametolewa katika Nyenzo-rejea 3: Maigizo kifani katika kutambua mtandao wa shule. Mapendekezo hayo yatakusaidia kuanza, lakini unaweza kufikiria mazingira halisi unayoweza kutumia. Wafikirie kwa makini wanafunzi wako darasani, fikiria matatizo yaliyokwisha tokea na hivyo kuwa makini unavyopanga maigizo.kifani.

Kwa vijana wadogo, ni muhimu kuwasaidia kujenga uhusiano mzuri na urafiki ili wajihisi kuwa kuja shuleni ni kunawaongezea ujuzi chanya. Kutumia hadithi kuhusu mazingira mbalimbali ni njia ambayo inaweza kuhamasisha mawazo ya jinsi ya kusaidiana.

Uchunguzi Kifani 2 inaonesha yaliyotokea wakati mwalimu mmoja alipotumia maigizo kifani na mbinu ya utatuzi wa matatizo darasani mwake.

Uchunguzi kifani ya 2: Makundi ya kirafiki

Mwalimu Mazura alitaka kuwasaidia wanafunzi wake wa darasa la 5 kujadili athari za makundi ya kirafiki. Kwanza alitayarisha kadi zenye matatizo halisi yanayozingatia umri wa wanafunzi wake. Alitumia muda mwingi akifikiria matatizo wanayoweza kuyapata wanafunzi wake, wenye umri wa miaka 11 hadi 12. Alijua kuwa hii ni miaka ya matatizo kwa vijana ambao wameanza kubadilika kimwili na wanaanza kuwa na muongezeko wa homoni. Alitaka pia kushughulikia tatizo kubwa alilokuwa nalo kuhusu kundi la wasichana ambao mara kwa mara walikuwa wakimsumbua msichana mmoja.

Katika mfulululizo wa masomo matatu, mwalimu Mazura aliyauliza makundi matatu kuwasilisha igizo ili kuonesha matatizo aliyoyaonesha katika kadi. Darasa lilikuwa na majadiliano ya kufurahisha baada ya kila wasilisho. Wakati mwingine kulitokea mabishano wakati wanafunzi walipokuwa na mawazo tofauti kuhusu utatuzi wa matatizo, lakini mwalimu Mazura aliwahimiza wasikilizane na waheshimu tofauti zao.

Kwa upande wa kazi ya nyumbani, mwalimu Mazura alilitaka darasa kufanya kazi wawili wawili na watatu watatu ili kufikiria mazingira ambamo wangependa kuigiza kwa ajili ya majadiliano darasani. Jambo hili lilikuwa nyeti, kwa kuwa mwalimu Mazura hakujua hali itakayojitokeza- na hivyo hakujitayarisha. Igizo lilihusisha michezo ya uonevu, kuwa na njaa, na kutokuwa na marafiki shuleni. Mwalimu Mazura alifurahia maigizo yao na alifurahi zaidi kwa kuwa hapakuwa na matatizo au hali ya mshangao.

Shughuli ya 2: Utatuzi wa matatizo katika muingiliano wa darasani

Makundi ya marafiki sio makundi pekee waliyonayo vijana shuleni. Hapa tunaonesha njia nzuri ya kupambanua makundi tofauti unapokuwa na darasa kubwa. Njia hii inahusisha vijana wote wakizunguka darasa wakati uleule, hivyo unahitaji kutunga kanuni ili kudhibiti darasa hilo. Utajikuta kuwa unahitaji filimbi.

Anza kwa kuwauliza wapo katika makundi yapi shuleni. Kila kijana anaandika jina la kundi alilomo katika kipande cha karatasi. Anakifunga nguoni mwake upande wa mbele. Kwa kutoa ishara wanafunzi wanazunguka darasani na kumtafuta kijana mwenzie wa kundi lake. Wape muda wa dakika tatu. Chunguza na kumsaidia kijana asiyekuwa na kundi au ambaye hakupata mwenzie. Piga filimbi tena na kila watu wawili watafute wenzi wao-wape dakika tatu pia. Endelea hivyohivyo mpaka makundi yote yaundwe. Watake wanafunzi wahesabu makundi na wayaandike ubaoni ili kubaini kundi lenye watu wengi/wachache, wasichana/wavulana wengi, n.k.

Watake wanafunzi wako wakae katika madawati yao. Halafu watake waandike wamegundua nini, kwa kumia taarifa iliyoandikwa ubaoni. Unaweza kuwa na majadiliano kuhusu kundi lipi linapendwa zaidi na kwa nini. Au ni kundi lipi lina wanafunzi wachache. Labda wanakundi hili wanaweza kuwasilisha taarifa fupi kuwaeleza wanafunzi wenzio darasani kuhusu shughuli zao. Ungeweza kuwahimiza baadhi yao kujiunga katika kundi jipya.

Kwa vijana wadogo utapenda kurudia haya kwa kufanya na kundi moja baada ya jingine na kuendeleza shughuli hiyo kwa wiki nzima, huku wewe ukiandika mawazo yako.

Somo la 3

Kuwakaribisha wanajamii shuleni kunaweza ku wasaidia wanafunzi na kuwahamasisha katika mafunzo yao na kufanya masomo yao yawe ya kufurahisha. Hali hiyo ikitekelezwa vyema itaifanya shughuli hiyo ikusaidie masomo ya stadi za maisha kuwa kamilifu kwa wanafunzi wako. Hii ni njia nzuri ya kuwatambulisha wanafunzi wako kwa baadhi ya maingiliano mbalimbali katika jamii.

Hata hivyo kuwakaribisha wanajamii kunaweza kuchukua muda kupanga-unahitaji kutambua watu wanaohusika, kufanya mipango nao na kuhakikisha kuwa wameelewa unachotaka kufanya. Inawezekana ukahitaji kutumia nyenzo-rejea kwa ajili ya wanafunzi wako ili wajifunze katika hali halisi.

Kumbuka kutathmini wanafunzi walichojifunza baada ya tukio hili. Si tu kuhusu mada ya mwalikwa, bali pia wamejifunza nini kuhusu kupanga tukio hilo. Unaweza kufanya jambo hili kwa njia mbalimbali-kuna mawazo katika Shughuli muhimu. Tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kuwatumia wanajamii/mazingira kama Nyenzo-rejea ili kukusaidia kupanga ugeni huo.

Uchunguzi kifani ya 3: Muingiliano (mtandao) wa jamii

Mwalimu Tomasi alizungumzia muingiliano wa jamii na darasa lake la sita. Wakiwa wawili wawili, wanafunzi walizungumzia wako katika makundi yapi tofauti ya kijamii au yapi waliyajua. Waliorodhesha ubaoni makundi tofauti yote:

Ukoo/kabila

Makundi ya kidini

Maskauti wavulana/wasichana (girl guides)

Klabu ya michezo Kundi la dansi Kwaya

Kundi la huduma ya kwanza.

Baada ya kujadili kila kundi lilikuwa na wanafunzi wangapi, darasa lilipiga kura ya kumkaribisha kiongozi wa Waislamu aje kuzungumza nao. Walifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na mwanafunzi wa Kiislamu mmoja tu na wengine walitaka kuwa na habari zaidi kuhusu Waislamu.

Kwanza mwalimu Tomasi alikwenda kwenye maktaba ya shule na kupata kitabu kinachohusu dini mbalimbali. Alijifunza kuhusu imani ya Kiislamu na kutayarisha somo kuhusu misingi ya dini ya Kiislamu. Alifanya hivyo ili darasa lipate maarifa ambayo ni msingi wa kujua waliyofundishwa na mgeni.

Wanafunzi waliandika insha fupi kuhusu imani ya Uislamu na mwalimu Tomasi aliziweka insha hizo katika meza maalum darasani ili kila mmoja azisome. Aliwaomba pia wanafunzi wake kutayarisha maswali ya kumuuliza mgeni na walikubaliana maswali mazuri ni yapi na nani wa kumuuliza mgeni.

Mgeni alipofika, alifurahi kuona kazi ya wanafunzi na kuona yapi ambayo walikuwa wakiyajua kuhusu imani ya Kiislamu. Aliwaletea sanaa za namna mbalimbali ili wazione na wanafunzi walivutiwa sana na majibu ya maswali yake na waliuliza maswali mengi zaidi.

Mwalimu Tomasi alifurahishwa na jinsi ugeni huo ulivyowahamasisha wanafunzi wake na aliamua kujaribu mbinu hiyohiyo katika masomo yao ya siku za usoni.

Shughuli muhimu: Kuwatumia wageni kuwahamasisha wanafunzi kujifunza

Bainisha wanafunzi wako wako katika makundi yapi ya kijumuiya. Unaweza kutumia mbinu aliyoitumia Mwalimu Tomasi, kwa majadiliano na darasa zima au kwa kutumia wanafunzi wachache, kwa kuzingatia idadi na umri wa wanafunzi.

  • Amua, kwa kushirikisha darasa zima, kundi lipi la kijumuiya ambalo ungependa kulijua zaidi.

  • Jitayarishe –utatakiwa kusoma zaidi.

  • Waeleze wanafunzi wako kuhusu somo husika

  • Jadili shughuli ambazo zinatakiwa kufanyika (kwa kutumia Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia wanajamii/mazingira kama Nyenzo-rejea).

  • Wasaidie wanafunzi wako kutayarisha maswali ya kumuuliza mgeni.

  • Waulize wanafunzi wanaojitolea (au wawili wawili au kundi) wa kutimiza shughuli hizo tofauti.

  • Waongoze wanafunzi wako wanapokuwa katika mchakato wa kukamilisha shughuli hii.

  • Baada ya mgeni kuondoka, wakumbushe wanafunzi wako kuandika barua za shukrani.

  • Fanya somo la mahitimisho ambapo utatambua wanafunzi wamejifunza nini. Hili laweza kufanywa kwa namna tofauti:

  • Kwa wanafunzi wakubwa –majadiliano, kuandika hadithi, maigizo kifani, jaribio;

Kwa wanafunzi wadogo-kuchora picha, igizo kifani.

Nyenzo-rejea ya 1: Sababu za kuishi katika familia - Orodha ya darasa ya mwalimu Ndonga

Mifano ya kazi za wanafunzi

  • Kuwalinda watoto

  • Kuwapa watoto chakula na malazi

  • Kuwafundisha watoto jinsi ya kuishi

  • Kuwafundisha watoto mambo wanayotaka kuyajua, kama uaminifu na heshima kwa watu wengine

  • Kwa sababu watoto hawawezi kujisaidia wenyewe

  • Kwa watu wazima kuwa na wenza

  • Kwa sababu binadamu ni wanamuingiliano na hawawezi kuishi pekee

  • Kuwa mfano wa watoto

  • Kushirikiana katika urafiki na mapenzi

  • Kushirikiana katika kazi.

Nyenzo-rejea ya 2: Muingiliano (Mtandao) wa familia

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Nakili mchoroti huu wa mti ubaoni. Wanafunzi wanaweza kuunakili katika daftrai zao, au katika karatasi za magazeti kama unahitaji kuonesha kazi zao.

Kila mtoto aorodheshe wanafamilia wake anaotaka kuwaonesha katika mchoroti na wachore idadi kamili ya masanduku. Hii inaweza kuonesha masanduku mengi au machache kuliko haya yaliooneshwa katika mchoroti hapa chini.

Nyenzo-rejea 3: Igizo la kutambua mtandao wa shule

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Haya ni mawazo ya kukusaidia wakati unapofikiria kuhusu maigizo kifani. Kwa fikra zaidi, utaweza kutumia mawazo haya na kufikiria juu ya igizo kifani linalowafaa wanafunzi wako. Kumbuka kufikiria juu ya maswali kwa ajili ya darasa lako, baada ya wanafunzi kumaliza kucheza igizo kifani lao. Inabidi uhakikishe kuwa wanajua wanachotakiwa kufanya na kusema. Hakikisha pia kuwa kila mmoja anapata nafasi ya kuigiza. Unaweza pia kuwauliza wanafunzi kama wanafikiri mwalimu naye ahusike katika mojawapo ya matatizo haya.

Watoto wadogo

1. Fatima na Rose wamekuwa marafiki tangu darasa la kwanza. Sasa wako katika           darasa la tatu. Mwanafunzi mgeni, aitwaye Elizabeth amejiunga na darasa hilo. Fatima ameamua kuwa hatakuwa rafiki na Rose zaidi kwa kuwa anaenda nyumbani kwa Elizabeth kucheza na mbwa wao. Rose anakosa raha kwa sababu Fatima si mtu mwenye huruma kwake. Anatumia muda wake mwingi wakati wa mapumziko kulia.

  • Rose afanye nini ili kutatua tatizo lake?

  • Fatuma afanye nini kama kweli anamjali Rose?

  • Elisabeth afanye nini kutatua hali hii?

2. Ahmed ni kijana mwenye soni. Anavaa miwani mizito kwa kuwa haoni vizuri. Hapendi michezo kwa kuwa si hodari wa michezo. Hamna kijana yeyote darasani kwake anayependa kufanya urafiki naye kwa kuwa hachezi mpira.

Mara nyingi yuko peke yake na anachukia shule kwa kuwa hana rafiki.

  • Unamshauri vipi Ahmed?

Wanafunzi wakubwa

  1. Isaac anapenda kushirikiana na vijana wanaojiita ‘Timu A’. Wanaonekena kuwa na furaha na wanazungukwa na wasichana. Baadhi huvuta sigara na kunywa pombe. Wanaiba pesa kutoka kwa wazazi wao kununua vitu hivi. Kama hawatapata pesa wanaiba kutoka katika duka la Allen Mushi. Wanasema kuwa kama Isaac anataka kuungana nao, basi lazima alete sigara na fedha.
    • Isaac afanye nini?
  2. Basma amekutana na mvulana ambaye ni mkubwa kwake. Basma ana umri wa miaka 13 na mwenzie ana umri wa miaka 16. Anampenda sana na anafikiria aolewe naye. Anataka kufanya mapenzi naye, lakini Basma hana hakika. Anataka akae naye kama mpenzi wake wa kiume lakini pia ana wasiwasi kuhusu kupata UKIMWI au kupata mimba. Anataka kujiunga na Chuo Kikuu.
    • Basma afanye nini?

Sehemu ya 2: Kuchunguza nafasi yetu katika jumuiya

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kutumia usimulizi wa hadithi, maarifa ya mahali husikana utamaduni husika ili kuboresha ujifunzaji?

Maneno muhimu: tamaduni; jumuiya; maigizo-kifani kifani; uvumbuzi; tabia;usimulizi wa hadithi.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii , utakuwa umeweza:

  • kujua zaidi kuhusu jumuiya husika kwa njia ya kujifunza kwa uvumbuzi;
  • kutumia maigizo-kifani kifani katika kubainisha tabia zinazokubalika katika mazingira mbalimbali;
  • kutumia usimulizi wa hadithi ili kukuza ufahamu wa wanafunzi wa tamaduni mbalimbali.

Utangulizi

Kujifunza kwa uvumbuzi, hadithi, na maigizo-kifani kifani ni njia za kiutendaji za kutalii jumuiya mbalimbali wanamoishi wanafunzi. Njia hizi huwafanya wanafunzi wachunguze vitu wao wenyewe, jambo ambalo ni bora zaidi kuliko tu wewe kuwaambia jinsi vitu vilivyo.

Lengo la kutumia hadithi na maigizo-kifani kifani ni kuchochea mjadala na kuwasaidia wanafunzi kuangalia mienendo na tabia zao wenyewe kwa njia ambayo haitishi. Kwa kuwa matukio ya kubuni ni tofauti na mazingira halisi ya wanafunzi, wanafunzi hawa wanaweza kuona kuwa wana uhuru zaidi wa kuzungumza.

Ni muhimu kwamba masomo ya stadi za maisha yasihubiri, ila yawasaidie wanafunzi kugundua mambo wao wenyewe na kutafakari kuhusu maisha na matamanio yao. Unatakiwa uelewe kwamba wanafunzi mbalimbali

‘watavumbua’ mambo mbalimbali yanayowahusu wao wenyewe, wanafunzi wengine pamoja na maisha yao. Katika Nyenzo-rejea 1: Jumuiya ni nini? kuna tini kuhusu jumuiya.

Somo la 1

Kujadiliana na kuandika hadithi huwasaidia wanafunzi kusema wanachokifikiria kuhusu hali mbalimbali. Hadithi zinaweza kusaidia wakati unapotaka wafikirie masomo magumu.

Lakini pia inachukua muda kuziandaa; unatakiwa ufikirie kuhusu jumuiya wanakotoka wanafunzi wako na uandae hadithi yako kwa uangalifu.Katika Uchunguzi Kifani 1, tunajifunza kuhusu Bibi Oto ambaye anafundisha darasa la sita katika shule kubwa ya msingi iliyopo Kampala.

Aliwataka wanafunzi wake wafikirie kuhusu mahusiano ya kijumuiya yaliyopo katika mazingira ya mji wao na kisha wachunguze kuhusu jumuiya iliyopo kijijini.

Kama unafanya kazi katika mazingira ya kijijini, unaweza ku wataka wanafunzi wako wachunguze hali ya mjini au ya mji.Shughuli 1 hutumia kujifunza kwa uvumbuzi ili kuwasaidia wanafunzi wako ‘kuvumbua’ zaidi kuhusu jumuiya zao wenyewe.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia uzoefu wako katika kujadili maisha ya jumuiya

Kwa kuwa Bibi Oto ametokea kijijini kilomita zaidi ya 200 kutoka Kampala, anajua vizuri mambo mengi kuhusu maisha ya kijijini. Kutokana na uzoefu wake wenyewe, aliweza kutunga hadithi kuhusu maisha yake ya pale na kisha kuzitumia na wanafunzi wake. Kutumia uzoefu wake wenyewe kulikuwa muhimu kwa Bibi Oto katika ufundishaji kwani ilimaanisha kuwa alikuwa anajiamini sana kuhusu ujuzi wa somo lake.

Bibi Oto aliwaambia wanafunzi wawili kutoka katika darasa la sita la shule ya msingi wasome hadithi alizoziandika kuhusu jumuiya moja ya kijijini kilichopo nchini Uganda na kisha wanafunzi wengine wawili wasome hadithi

moja kuhusu jumuiya ndogo ya mjini aliyoifahamu yeye. Alizichagua hadithi hizi kwa sababu zilikuwa na vipengele vingi vilivyofanana.Baada ya kusoma kila hadithi, aliwaambia wanafunzi wake wajadiliane katika vikundi vyao kimadawati kuhusu:

  • shughuli mbalimbali wanazozifanya watu katika kuendesha maisha yao; watu wanaowasaidia watu wengine katika jumuiya; matatizo ya kila jumuiya –matatizo yapi yanafanana? Matatizo yapi yaliyotofautiana?; viongozi wa jumuiya.

Bibi Oto alivi ambia vikundi kutoa mawazo yao na aliandika vipengele muhimu ubaoni. Walijadiliana kama darasa kuhusu mafanikio na matatizo ya jumuiya mbalimbali na jinsi ambavyo matatizo haya yangeweza kutatuliwa.Kama kazi ya nyumbani, Bibi Oto aliwaambia wanafunzi wafikirie kuhusu jumuiya zao wenyewe. Somo lililofuata, baada ya kila kikundi kuwa kimeshafanya utafiti kwa kiasi fulani (tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kufanyia utafiti darasani ) kila kikundi cha wanafunzi wannewanne kiliandika maelezo ya kikundi chao wenyewe juu ya jumuiya zao. Baadhi ya wanafunzi walilisomea darasa zima maelezo haya

Shughuli ya 1 :Kujifunza kwa njia ya uvumbuzi katika jumuiya husika

Liambie darasa lako libunge bongo kuhusu baadhi ya makundi makuu katika jumuiya husika. Makundi haya yanaweza kujumuisha AZISE, makundi ya kidini, marafiki, familia, viongozi wa jumuiya n.k.

  • Lipange darasa lako katika vikundi vyenye ukubwa wa kutosha. (Vikundi hivi vinaweza kufuata umri, uwezo au njia nyingineyo).

  • Waeleze kwamba watatakiwa kujua taarifa ya kundi mojawapo kati ya makundi hayo.

  • Kiruhusu kila kikundi kichague kundi la jumuiya. Kikundi zaidi ya kimoja kinaweza kuchunguza kundi au asasi hiyo hiyo moja kwani nia na maoni yatatofautiana.

  • Unaweza kuhitaji kufanya utafiti wewe mwenyewe au wanafunzi wako wanaweza kufanya wao ili kujua zaidi kuhusu kila kundi au kila asasi. Wewe au wao mnaweza kukusanya maandiko ya kuwasaidia katika chunguzi zao. Pia kila kikundi kinaweza kuandaa dodoso na kuwahoji watu wa asasi hiyo. Tazama Nyenzo-rejea 2: Sampuli ya maswali ambayo wanafunzi wanaweza kuuliza ili kujua zaidi kuhusu makundi ya jumuiya husika.

  • Wapatie wanafunzi muda wa kufanya uvumbuzi, au utafiti.

  • Somo linalofuata, kiambie kila kikundi kiandae wasilisho kuhusu asasi yao –wasilisho linaweza kuwa kwa njia ya andiko, bango, picha au njia nyingine yo yote ile ya onesho.

Kwa wanafunzi wadogo, ungeweza kuchunguza kundi moja tu na kumwalika mtu kutoka kwenye asasi hiyo kuzungumza na darasa na kutengeneza bango kwa pamoja. Ungeweza kurudia utaratibu huu baada ya muda fulani ili wanafunzi wako wapate kujua kuhusu asasi mbalimbali.

Somo la 2

Kuwaheshimu wengine na kutendeana kwa njia zinazofaa kati ya vizazi mbalimbali ni muhimu katika kufungamanisha jumuiya pamoja. Jinsi wanafunzi wako wanavyoongea na kushirikiana na kila mmoja darasani kwako kunaweza kuathiri malengo yao katika shule na katika kujifunza. Igizo kifani linaweza kutumiwa ili kuchunguza jinsi mtu anavyotenda kitabia katika hali mbalimbali. (Kwa mwongozo tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia Igizo kifani/majibizano/tamthiliya darasani).

Utahitaji kutumia muda ili kuandaa maigizo-kifani-kifani yanayofaa. Kumbuka, lengo ni kuwasaidia wanafunzi wako ili wachunguze imani, maarifa na mienendo yao wenyewe, na njia ya kufanya hivyo bila woga ni kwa njia ya igizo.

Uchunguzi Kifani 2 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyotumia igizo na wanafunzi waliokuwa wadogo zaidi ili kuchunguza kanuni za kimaadili ndani ya familia zao. Shughuli 2 inatumia igizo kifani ili kuchunguza mahusiano ya kijamii.

Uchunguzi kifani ya 2: Kanuni za familia

Bibi Mnagara anafundisha darasa la Tatu katika shule ya Msingi Themi. Aliwaambia wanafunzi wake wazungumze na babu na bibi zao au wanafamilia wengine wakubwa na kuwauliza kuhusu kanuni za kimaadili zinazotumika katika familia zao.

Siku iliyofuata, darasani, walilinganisha kwa pamoja kanuni hizi kutoka familia zao mbalimbali na kukuta kuwa kanuni nyingi zilikuwa zinafanana. Mtoto mmoja au wawili walikuwa na kanuni ambazo wengine hawakuwa nazo, na walizungumzia juu ya sababu za baadhi ya familia kuhitaji kanuni tofauti. Walikuta kuwa nyingi ya kanuni hizi zilikuwa ni kwa ajili ya watoto! ( Nyenzo-rejea 3: Kanuni za familia moja ina baadhi ya kanuni ambazo unaweza kuzijadili na darasa lako).

Bibi Mnagara alichagua vikundi vidogo vya wanafunzi kuigiza kwa vitendo moja ya kanuni hizi. Hii ililisaidia darasa kujadili tabia zilizooneshwa na vikundi hivi pamoja na wakati kanuni hizi zinapotumika.

Waligundua kuwa wakati mwingine kulikuwa na kanuni tofauti kwa ajili ya wavulana na wasichana. Walilizungumzia hili na kukuta kuwa kulikuwa na kazi maalum zilizofanywa na wavulana tofauti na zile za wasichana. Walihisi kwamba, kwa kiasi kikubwa, wasichana, hawakutendewa sawa na wavulana. Mwishowe, darasa zima lilikubali kuwa haikuwa haki na kwamba kanuni hizi lazima ziwe sawa kwa wote.

Mwishoni, Bibi Mnagara alieleza ni kwa nini kanuni hizi ni muhimu. Pia aliweka kumbukumbu katika kitabu chake kwa ajili ya kuandaa somo kuhusu masuala ya kijinsia ili kuendelea kuchunguza na yumkini kupinga tofauti katika makuzi ya wasichana na wavulana.

Shughuli ya 2: Kutumia maigizo-kifani kifani ili kuchunguza mahusiano ya kijumuiya

Andaa maigizo-kifani yanayohusu mazingira mbalimbali ya kijumuiya:

Godfrey anakutana na chifu

Bw. Eliasi muuza dukani

Yahsin na babu yake

(Kwa ufafanuzi zaidi kuhusiana na mawazo haya, angalia Nyenzo-rejea 4: Igizo kifani kuhusu mahusiano ya kijumuiya . Unaweza kuongezea shughuli zako mwenyewe.)

Waambie wanafunzi wako kufanya kila igizo kifani na kisha kuwa na mjadala wa vikundi au darasa kila baada ya kila igizo moja. Bainisha tabia nzuri na mbaya. Liulize darasa jinsi watu katika hadithi wanavyopaswa kuwa kitabia.Waambie wanafunzi, katika makundi, wafikirie hadithi yao wenyewe ya kuigiza. Waelekeze ili kuhakikisha kuwa wanafikiria hali halisi. Kiruhusu kila kikundi kiwasilisha igizo kifani lake, na rudia majadiliano ya kidarasa au ya kikundi ili kutafuta njia za kusuluhisha hali hizi.

Somo la 3

Kadiri wanafunzi wako wanavyokua, ni muhimu sana kuwasaidia ili wajifunze kuheshimu maoni na imani mbalimbali za watu. Hadithi ni njia nzuri za kuanzisha mjadala wa mawazo yanayohusiana na maingiliano ya kitamaduni pamoja na tabia nzuri au mbaya. Hadithi zinaweza kuwasaidia wanafunzi waelewe kanuni zinazotawala tabia za aina mbalimbali.

Ili kutumia hadithi vizuri, lazima uingize wahusika ambao wanatofautiana kitabia. Mjadala mrefu unaweza kutokana na hadithi iliyochaguliwa vizuri, lakini pia unahitaji kutafakari juu ya maswali ambayo unaweza kuwauliza wanafunzi.

Jambo hili pia linahusu maigizo-kifani kifani. Kwa kubuni wahusika na kuigiza kama wao, wanafunzi wanaweza kuchunguza aina za migongano ya kitamaduni inayoweza kutokea katika maisha halisi, lakini bila kuathiriwa na matokeo ya migongano hii. Hadithi na maigizo-kifani kifani yanaweza kuwasaidia wanafunzi wako kukuza welewa wao wa utofauti kwa njia ambayo haitishi. Nyenzo-rejea 5: Jumuiya zenye mwingiliano wa kitamaduni itakusaidia kuendeleza mawazo haya pamoja na wanafunzi wako.

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia usimulizi wa hadithi katika kuchunguza migogoro ya kijumuiya

Bwana Agoro aliamua kufundisha darasa lake kuhusu umuhimu wa watu kuheshimu wanajumuiya na nafasi mbalimbali walizonazo, pamoja na madhara yanayotokana na mgogoro. Alitumia hadithi ya mapigano baina ya makundi matatu ya kitamaduni yaliyoko Mpanga ili kujadili masuala haya. Tazama nakala ya hadithi hii katika Nyenzo-rejea 6: Mgogoro katika jumuiya ).

Kabla ya kusimulia hadithi hii, Bwana Agoro aliwaambia wanafunzi wake wasikilize vizuri na wajaribu kubainisha sababu yenyewe ya mgogoro huu. Baada ya kusikiliza hadithi hiyo, walishirikishana maoni yao na kuyaorodhesha ubaoni.

Kisha, aliwaambia, kwa vi kundi, kuelezana jinsi matukio yalivyojengwa hatua kwa hatua. Baada ya dakika kumi, walizungumza kama darasa na kukusanya hatua hizo mbalimbali na kuziandika ubaoni.

Baadaye Bwana Agoro aliwaambia wajadili jinsi ambavyo wangemaliza tatizo kwa kuangalia kila moja ya hatua hizi mbalimbali na kueleza jinsi ambavyo wangezuia kila moja. 

Mwisho, aliwaambia waorodheshe njia ambazo makundi haya matatu tofauti yanavyo shiriki na pia kushirikiana na jumuiya kwa njia chanya. Hii iliwasaidia kwelewa jinsi kila kundi lilivyokuwa muhimu kwa kundi jingine na jinsi ambavyo lisingeliweza kufanya kazi bila msaada wa makundi mengine.

Wanafunzi walijikuta wakilifurahia somo, na Bwana Agoro aliona jinsi walivyoanza kushughulikia masuala haya kwa umakini.

Katika somo lililofuata, wanafunzi walifanya tena kazi kwa vikundi katika kufikiria eneo lolote lile kwenye jumuiya yao lililokuwa na mgogoro na baadhi ya masuluhisho. Walitumia stadi za jinsi ya kupata ufumbuzi wa tatizo walizokuwa wamezitumia wakati walipokuwa wanashughulikia hadithi.

Shughuli muhimu: Kuigiza juu ya mwingiliano wa kijumuiya

Lipange darasa lako katika vikundi vitatu: kila kikundi kitawakilisha mojawapo ya jumuiya kutoka kwenye hadithi katika Nyenzo-rejea 6 . Waambie kwamba wataigiza kuhusu mgogoro na kisha watafute amani, hivyo wanatakiwa wafikirie jinsi watakavyofanya. Watatakiwa wafikirie kuhusu wajibu wa jumuiya yao, na jinsi ya kuwasilisha wajibu huu katika maigizo-kifani kifani wao.

Baada ya dakika 15 za maandalizi, kiambie kikundi cha wanafunzi sita (watu wawili kutoka kila jumuiya) kuigiza mgogoro, kama walivyouona, mbele ya darasa. Kisha, waambie wakae chini na watafute amani wakati darasa likiwa linawaangalia. Waambie wasikilize kwa makini rai za kila mmoja wao, na washughulikie rai hizi kwa makubaliano yo yote yale.

Kwa kushirikiana na darasa zima, bainisha na jadili:

  • majukumu mbalimbali ambayo kila jumuiya inayo;

  • masuluhisho mbalimbali yaliyofikiwa.

Waambie wabainishe mawazo ambayo wangeweza kuyatumia katika maisha ya kila siku. Ni mawazo gani ambayo unafikiri yalikuwa bora zaidi?

Mwishoni, waambie waandike hadithi kwa kutumia maneno yao wenyewe na waongezee jinsi mgogoro ulivyosuluhishwa.

Nyenzo-rejea 1: Jumuiya ni nini?

Usuli/welewa wa somo kwa mwalimu

Jumuiya ni kikundi cha watu ambao wanashiriki na kuchangia vitu fulani ambavyo vinafanana. Wanajumuiya wanaweza kuishi kwenye eneo moja na wanaweza kuwa na maadili na imani za pamoja. Kunaweza pia kuwa na vitu wanavyomiliki kwa pamoja.

Kama unajaribu kuelezea wazo la jumuiya kwa wanafunzi wako, unaweza kwanza kwa kutumia mifano wanayoifahamu. Njia nzuri ya kuanzia ni kuwaambia waeleze kuhusu familia zao, ikiwepo familia pana ya shangazi, wajomba na binamu. Wasaidie wang’amue kuwa familia zao zinaundwa na mtu mmoja mmoja, mkusanyiko wa watu, wanaoishi sehemu fulani – jumuiya ndogo.

Ili kuimarisha mawazo haya, unaweza kuwaambia kuongeza makundi mengine wanayoshirikiana nayo ambayo wanaunda sehemu ya jumuiya pana zaidi:

  • Majirani zao, wanaoishi kwenye mtaa mmoja;

  • Rafiki zao, wanaowaona kila situ.

  • Rafiki za wazazi wao, ambao wanawatembelea.

Ni mkusanyiko huu wa makundi mbalimbali ya watu ambao unaunda jumuiya, na ni jinsi wanafunzi wanavyoshirikiana na makundi haya kunakochangia jinsi walivyo na jinsi wanavyojiona wenyewe ndani ya jumuiya. Kubainisha mambo mbalimbali yanayosaidia kuelezea jumuiya kutawasaidia kwelewa nafasi waliyonayo katika makundi mbalimbali. Ungeweza kuwaambia waeleze:

  • eneo – mahali watu wanapoishi; lugha – jinsi watu wanavyoongea; utamaduni – watu wanavaa nguo gani, chakula wanachokula, dini zao; historia – matukio muhimu ambayo yametokea kwa kundi la watu

Nyenzo-rejea ya 2: Sampuli ya maswali ambayo wanafunzi wangeweza kuuliza ili kwelewa zaidi kuhusu makundi husika ya kijumuiya

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

  • Nini jina la kundi lako?

  • Nini lengo la asasi yako?

  • Unawasaidia wanajumuiya gani?

  • Unatoaje msaada huu?

  • Wanajumuiya yako ni nani?

  • Nani anaweza kuwa mwanakundi lako?

  • Mnakutana mara kwa mara? Kama ndiyo, lini na wapi?

Nyenzo-rejea ya 3: Sheria/Kanuni za familia moja

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Kanuni za familia moja

Watoto wanafanya kama walivyoambiwa. Wasichana

wanawasaidia mama zao kazi za nyumbani. Wavulana

wanawasaidia baba na wajomba zao shambani. Watoto

wanatulia na wanakuwa na hekima mbele ya wakubwa. Watoto

wanaondoka chumbani mgeni anapokuja.

Watoto hawawezi kucheza nje ya nyumbani siku ya Jumapili.

Watoto wakubwa wanawalea watoto wadogo.

Daima hakuna kusema uongo.

Nyenzo-rejea ya 4: Igizo kuhusu mahusiano ya kijumuiya

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Hapa pana baadhi ya maoni kwa ajili ya maigizo-kifani ambayo unaweza kuyafanya pamoja na wanafunzi wako. Ni Maoni tu ya kukufanya uweze kuanza somo. Je, unaweza kufikiria mazingira muafaka kwa ajili ya jumuiya na wanafunzi wako mwenyewe? Kama ndiyo, andika maigizo- kifani yako mwenyewe au rekebisha haya hapa chini. Unaweza kukatisha kila hadithi sehemu tuliyoachia na kuwaambia wanafunzi wamalizie wenyewe. Kwa njia hii, wanafunzi wanaweza kufanya kazi kwenye vikundi na kuja na masuluhisho ya matatizo mbalimbali. Au unaweza kumalizia kwa kuandika mwisho wako mwenyewe wa hadithi hiyo ili kueleza pointi unayotaka.

Godfrey akutana na Chifu

Godfrey alikuwa na tatizo na jirani yake ambaye alikuwa akiendelea kuwaruhusu mbuzi wake kwenye bustani ya Godfrey ambako waliweza kula mboga zake zote za majani. Ilikuwa imeshatokea mara nyingi. Godfrey alijaribu kuzungumza na jirani yake lakini hakumsikiliza. Mwanzoni jirani yake alikuwa mpole, lakini baadaye akawa mara nyingi kwenye sehemu za bia bila kujali sana kuhusu nyumba yake au rafiki zake.Godfrey aliamua kwenda kwa chifu kuomba ushauri. 

Bwana Elias muuza duka

Bwana Elias ana duka dogo ambalo huuza chakula na vyombo vya nyumbani. Duka lake ni msaada mkubwa kwa wanawake kijijini kwani linawaokoa kutembea hadi kwenye mji mwingine. Bwana Elias anasifikika kwa kumiliki friji na jenereta. Sasa anaweza pia kuuza vitu baridi kama, vinywaji baridi na maziwa – hata nyama. Vijana wanapenda kwenda dukani kwake kununua kola. Siku moja, Bwana Elias alipokuwa amekazania kumhudumia kijana mmoja kumuuzia pipi, vijana wengine wawili walifungua friji yake na kuiba chupa mbili za kola. Aliudhika sana na aliamua.

Yahsin na babu yake

Babu yake Yahsin ni mzee sana. Ana miaka 92! Anaishi na Yahsin na dada zake watatu na mama yake pamoja na shangazi na mtoto wa huyo shangazi. Muda mwingi babu hukaa chumbani kwake au kwenye kivi chake maalum nje ya mlango wa mbele chini ya kivuli cha mwembe. Mara nyingi anahamaki na kulalamika kuhusu kelele wanazopiga watoto. Mama yake Yahsin humwambia Yahsin kuwa hawana budi kumtunza babu kwani ni mkuu wa nyumba yao. Babu hupata malipo yake ya uzeeni kutoka serikalini, ambayo yanasaidia kununulia chakula chao. Yahsin anamwogopa sana babu yake na anapendelea kuwaachia dada zake ili wamtunze.

Siku moja, dada zake wote wanakwenda kuteka maji na mama anamwambia Yahsin kuwa ni lazima ampelekee babu yake mlo wake wa jioni. Yahsin anaogopa sana. Anachukua chakula na kisha

Nyenzo-rejea ya 5: Jumuiya zinazoingiliana kitamaduni

Usuli/welewa wa somo kwa mwalimu

Unavyowasaidia wanafunzi kueleza maana ya jumuiya zao, iwe ni familia zao, kijiji au shule, ni muhimu pia wajifunze kuheshimu maoni na imani mbalimbali za watu.

Wakumbushe wanafunzi kuwa wote ni watu kutoka kaya na familia mbalimbali kwa mfano wanaweza wasiweze wote kuzungumza lugha ya nyumbani au lugha mama inayofanana. Wazazi wao wanaweza kuwa na kazi tofauti tofauti; baadhi wanaweza kuwa vibarua; wengine wakulima; wachache wanaweza kuwa wafanya biashara, wauguzi n.k.

Lakini sisitiza ukweli kwamba wote ni wa jumuiya moja, yenye maslahi yale yale. Kutokana na hili, lazima waheshimu maoni ya watu wengine katika jumuiya hiyo.

Hatua ya kwanza ya kuheshimu watu wengine ni kusikiliza maoni yao na kung’amua thamani ya maoni hayo. Wanafunzi wanapojifunza kuhusu historia na imani za watu mbalimbali, wataweza kuheshimiana zaidi. Hawataogopa tofauti za kitamaduni. Pia watakuwa na welewa mkubwa wa wao ni nani.

Tofauti za kitamaduni wakati mwingine zinaweza kuwa ni vyanzo vya mgogoro ndani ya jumuiya. Ni muhimu kwa wanafunzi kwelewa sababu za mgogoro, kama vile mabishano juu umiliki wa ardhi, tabia, fedha na mahusiano. Sehemu muhimu ya elimu ya stadi za maisha ni kutafuta njia za kujaribu kuepusha mgogoro shuleni na kwenye jumuiya.

Nyenzo-rejea ya 6: Mgogoro katika jumuiya

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Ilitokea vita kubwa baina ya makundi matatu ya kitamaduni ya Mpanga, jumuiya ya kijiji iliyoko kando kando ya barabara kuu. Ilisababisha mauaji ya wanajumuiya kutoka makundi mbalimbali ya kitamaduni na iliathiri jumuiya vibaya sana.

Makundi haya matatu yalikuwa ni Wakwavi, ambao walikuwa wachunga ng’ombe; Wakete, ambao walikuwa wafanya biashara na anga, ambao waliendesha teksi na usafiri. Vita vilianza baina ya Wakete na Wapanga na kutokea hapa vilisambaa.

Wakete walisema kuwa Wapanga walikuwa wanawatoza fedha nyingi sana za kuwasafirishia bidhaa, na watu Wapanga walisema kuwa Wakete walitoza kiasi kikubwa kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea teksi zao.

Kwanza kulikuwa na mgomo wa teksi, na baadaye walisitisha kuwauzia vita. Siku moja, kulikuwa na mapigano kati ya dereva wa teksi na mfanyabiashara sokoni. Kisha madereva wote wa teksi walikwenda sokoni kuvunja mabanda yao, na mapigano makubwa yalianza.

Baada ya hili, Wapanga na Wakete walianza kushambulia makazi ya kila mmoja. Waliumizana vibaya. Watu walikufa na mali ilipotea. Familia za makundi haya mawili ziliyakimbia makazi yao kwa ajili ya kutafuta usalama.

Mwanzoni, wachunga ng’ombe wa Kwavi hawakuathirika sana kwa sababu walikuwa kwenye makazi yao na walikuwa wengi. Lakini mapigano yaliendelea kwa siku nyingine na walihusishwa.

Habari hizi za kusikitisha zilifika mapema katika maeneo ya makazi ya watu wa Panga na Kete kuhusu matatizo katika maeneo ya Kwavi. Wakazi waliwashambulia Wakwavi katika jumuiya zao wenyewe, huku wakiwaua ng’ombe.     Baadhi ya sehemu, wachunga ng’ombe waliuawa pia.

Hakukuwa na amani kwa siku kadhaa. Nyama haikupatikana majumbani kwa watu Wapanga na Wakete kwa sababu Wakwavi walikuwa wameondoka. Ariya kulikuwa hakuna teksi mitaani. Soko lilikuwa tupu kwa sababu vibanda vilivunjwa na hakukuwa na chakula kingine wala nyama iliyoweza kununuliwa kupelekwa nyumbani.

Viongozi wa jumuiya mbalimbali za Mpanga waliitisha mikutano na kuhutubia makundi yote matatu ya kitamaduni. Walionesha watu jinsi kila mtu alivyohitajiwa na mtu mwingine katika kujenga na kuendeleza jumuiya vizuri. Walieleza jinsi ilivyo muhimu kujifunza kusikiliza maoni ya kila mmoja, na kuwa wavumilivu kwa kila mmoja, kwa sababu kila mtu ana mambo mengi ya kujipatia toka kwa mtu mwingine.

Kisha walikaa na wawakilishi wa jumuiya mbalimbali na kujua chanzo cha tatizo. Walipata suluhisho na walileta amani miongoni mwa watu.

Sehemu ya 3: Njia za Uwajibikaji

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuoanisha maarifa ya nyumbani na ya shuleni ili kuleta mafanikio shuleni?

Maneno muhimu: kazi za vikundi; majadiliano; uwajibikaji; mafanikio; mashirikiano ya nyumbani

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii , utakuwa umeweza:

  • kutumia shughuli za mahusiano nyumbani na shuleni;

  • kutumia kazi za vikundi na majadiliano ili kubainisha jinsi imani na maadili vinavyohusiana katika mwenendo wa darasa;

  • kusaidia wanafunzi ili waweze kuunda kanuni zao wenyewe kwa ajili ya mwenendo wa darasa.

Utangulizi

Kuwasaidia wanafunzi wako wajali uwajibikaji katika kujifunza kwao wenyewe ni jukumu muhimu.

Mojawapo ya jukumu hili ni kuwashirikisha wanafunzi katika kusimamia darasa na rasilimali zake. Katika sehemu hii, unashirikiana na wanafunzi wako kupafanya darasani pawe ni mahali faafu zaidi, kwa kutoa ufafanuzi na kisha kupanga wajibu mbalimbali.

Vilevile, utawahimiza wanafunzi watengeneze kanuni zao wenyewe za darasani, kwa kuwaonyesha jinsi imani zao zinavyoweza kutumika katika mienendo yao ya darasani. Kuwa na kanuni hizi kutawanufaisha nyote; wewe na wao. Kuonesha heshima na imani kwa wanafunzi wako kutaleta athari chanya katika mitazamo yao kama watu na kama wanafunzi.

Ni vema kusoma Nyenzo-rejea 1: Faida za Kanuni/Sheria za Darasa kabla ya kuanza sehemu hii.

Somo la 1

Kila jumuia ina imani na maadili mbalimbali, yanayoongozwa na desturi za jamii ya kijadi. Imani na maadili haya husaidia kuamua mienendo gani inakubalika katika jumuia husika.

Kwanza wanafunzi watajifunza taratibu hizi nyumbani, na mafunzo hayo yaweza kuwa na manufaa kwako. Unaweza kuchukua mfano kutoka katika matarajio ya familia katika kusaidia kubainisha namna ambavyo wanafunzi na walimu wanatarajiwa watende shuleni wanapokuwa:

  • darasani;

  • katika viwanja vya michezo;

  • wanawasiliana na mwalimu;

  • wanawasiliana wao kwa wao.

Kuunda kanuni zihusuzo tabia njema kwa wanafunzi wako kutasaidia umakinifu wao wanapokuwa darasani. Watakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwa wasikivu wa jambo linalosemwa na kujali kuheshimiana.

Zaidi ya hapo, kwa kupata mawazo toka kwa wanafunzi wako, watajihisi kukubalika kwenye matarajio yoyote ya tabia njema. Watakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuheshimu matarajio haya kuliko kama ungewaambia tu kwamba ni lazima wafuate tabia fulani.

Kufanikisha hili kunahitaji mipango makini ambayo inaweza kuchukua muda mrefu kuitengeneza. Katika kila hatua, ni lazima usikilize mawazo ya wanafunzi wako kwa makini.

Uchunguzi kifani ya 1: Kanuni za darasa

Bibi Aber ni mwalimu wa Darasa la 4 nchini Uganda. Ana wanafunzi 63. Wakati wa wiki ya maelekezo ya mazingira, mwanzoni mwa muhula, aliwauliza wanafunzi wake kuhusu tabia wanazotarajiwa wazioneshe wakiwa nyumbani. Kwa kuwa ana darasa kubwa, aliwaweka wanafunzi katika kikundi cha watu wanane ili kulinganisha matarajio ya familia zao. Aliwataka wanafunzi kuorodhesha kanuni nne ambazo zinakubalika kwa wote.

Darasa lilitoa mifano mingi ya tabia ambazo familia zao zilizitarajia –nyingi kati ya hizo zilikuwa sawa kwa watoto mbalimbali. Bibi Aber aliandika baadhi ya tabia hizo ubaoni.

Halafu aliuliza kama ni lazima kuwepo na kanuni kama hizo za nyumbani kwa ajili ya tabia za darasani. Katika makundi, walichagua kanuni za nyumbani ambazo zingeweza kutumika darasani, na wakatoa sababu kwa nini wangetaka kuzitumia darasani. Baadaye walibadilishana mawazo kama darasa. Bibi Aber alifurahi, na akatumia mawazo haya kuunda sheria za tabia njema shuleni, ambazo zilijumuisha:jinsi tunavyotendeana; tabia zetu tuwapo darasani;tabia zetu wakati wa michezo;jinsi tunavyotunza vitu vyetu.

Walipigia kura kanuni sita ambazo walipenda kuzitumia.

Shughuli ya 1: Kuzifahamu Kanuni

Shughuli hii inweza kusaidia kueleza kwa nini tuna kanuni maalum, na jinsi zinavyomnufaisha kila mmoja.

  • Wapange wanafunzi wako katika makundi. Waambie wabainishe kanuni tano za nyumbani na tano za shuleni.

  • Chukua mfano mmoja wa kanuni ya nyumbani na mmoja wa kanuni ya shuleni kutoka katika kila kundi. Ziandike kanuni hizo ubaoni.

  • Waambie wanafunzi katika makundi wajadili:

  • kwa nini wanafikiri tuna kila kanuni;

  • Ni kwa namna gani kila kanuni inawasaidia.

  • Jadili mawazo yao kwa darasa zima. Andaa utaratibu wa kuuliza maswali ambayo yatawasaidia kutafakari zaidi kuhusu majibu yao.

  • Bainisha sheria mbalimbali toka kwenye kanuni, kwa kuliuliza darasa: k.m. usalama; kuwasaidia wengine; kusaidiana. Waambie waoanishe kila kanuni na sheria moja.

  • Mwambie kila mwanafunzi aandike aya moja kuhusu umuhimu wa kuwa na kanuni. Aya hizi zisomwe mbele ya darasa zima.

Maoni yao yalikuwa faafu kwa kiasi gani?

Somo la 2

Ni muhimu kwa wanafunzi wako kuelewa kwamba, kama ilivyo kwa walimu wao, na wao pia wana majukumu katika darasa lao.

Kwanza, lazima uwe mfano mzuri wa kuigwa. Onesha heshima katika kazi zako: wahi kufika kazini; andaa na hudhuria masomo; sahihisha kazi za kufanya nyumbani (mazoezi), n.k. Usipotimiza majukumu yako, usitegemee wanafunzi wako watayatimiza yao.

Pili, washirikishe wanafunzi katika kudumisha ubora wa darasa. Hili linahusu kuwahusisha katika:

  • kusafisha ubao;

  • kuliweka darasa katika hali ya usafi na mpangilio mzuri;

  • kutunza vitabu na samani, na kadhalika.

Kama watalitunza darasa lao wao wenyewe, wataanza kulionea fahari.

Tatu, washirikishe katika kupanga mafunzo yao wenyewe kwa njia ya shughuli ambazo unawapa. Jambo hili huwajumuisha katika:

  • kudhihirisha tofauti kati ya muda wa kazi na muda wa kucheza;

  • kupanga kazi za vikundi na vipindi vya kujisomea;

  • kuangalia wengine wanavyofanya kazi, na kadhalika.

Njia ya kawaida ya kuanza kutekeleza hili ni kwa kuwateua wanafunzi kama viranja wa madarasa na viongozi wa makundi, wenye wajibu wa kusimamia majukumu mbalimbali. Lakini wanatakiwa kufahamu kinachohitajika kwa kila wajibu.

Kwa maelezo zaidi tazama Nyenzo-rejea 2: Kuwatumia viranja wa darasa .

Uchunguzi kifani ya 2: Stadi na majukumu katika darasa

Bwana Sambwa ni mwalimu mwandamizi mwenye darasa kubwa la viwango vingi tofauti. Ana kundi la viranja wa madarasa kuanzia viwango vya juu ambao wana majukumu madogo madogo darasani na pia wanawasaidia wanafunzi wadogo. Viranja hawa wanasimamia makundi yao ili yawe tayari mwanzoni mwa kila somo, wanatunza vitabu na wanasafisha ubao kila siku. Kwa kweli wanasaidia sana.

Siku ya Ijumaa, ambayo ni siku ya usafi wa darasa, Bwana Sambwa anawaambia viranja wake wa darasa kufanya kazi katika makundi yao kuanzia madarasa ya chini kuorodhesha maeneo yanayohitaji utekelezaji. Kila kundi litoe pendekezo moja, ambalo linaandikwa ubaoni.

Kila kundi linajitolea kusimamia shughuli moja, na kwa kusimamiwa na kiranja wa darasa, linafanya kazi hiyo kila Ijumaa wakati wa mapumziko mpaka mwisho wa muhula.

Mwisho wa wiki, kila kundi linaeleza mbele ya darasa, walichofanya na walipoweka vifaa. Vile vile, wanawapa wanadarasa mapendekezo kwa ajili ya wiki itakayofuata ili kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu au kusaidia kutatua matatizo.

Mwisho wa muhula, wanapitia maendeleo ya kila kundi, na darasa zima linapiga kura kuchagua kundi lililoshinda kuliko yote.

Shughuli ya 2: Kuteua viranja wa darasa

Panga jinsi utakavyotambulisha suala la viranja wa darasa ili kulisaidia darasa.

  • Tambulisha hoja ya viranja wa darasa kwa darasa zima. Fafanua jinsi mfumo wa viranja wa darasa utakavyofanya kazi, na jinsi utakavyomnufaisha kila mmoja.

  • Pamoja na darasa lako, jadili na andika orodha ya majukumu yote ya darasani ambayo yanahitaji kutekelezwa mwanzoni, katikati na mwishoni mwa kila siku.

  • Bainisha majukumu ambayo utayatekeleza wewe, nay ale yatakayofanywa na wanafunzi.

  • Kama darasa, amuaeni kuhusu idadi ya viranja wa darasa inayohitajika na fikiria namna ya kuwachagua. Unaweza kuwabadili viranja wa darasa kila wiki ili kila mmoja apate nafasi ya kuwa kiranja na kutekeleza wajibu wake kwa wengine.

  • Teua kundi la kwanza la viranja wa darasa na eleza majukumu yao. Mwisho wa wiki ya kwanza, ukiwa pamoja nao, pitia kazi zao mbele ya darasa.

  • Waambie wapendekeze majukumu mapya ambayo watayatekeleza.

Kuchagua viranja wa madarasa kuna athari gani katika mwenendo wa shughuli za darasa lako? Je, wanafunzi wanaupenda mfumo huu? Je, unahitaji kupitiwa, na labda kufanyiwa marekebisho na darasa?

Somo la 3

Katika sehemu hii utatumia mawazo ya wanafunzi kuhusu taratibu bora za tabia ili kuwasaidia kuunda kanuni zao wenyewe za darasani.

Kuwasaidia wanafunzi kuunda kundi la kanuni kwa ajili ya darasa ni njia mojawapo ya kuimarisha ushirikishwaji na uwajibikaji, hususan kama wataandika kanuni hizi wao wenyewe. Uundaji wa kanuni zao wenyewe utawasaidia kuelewa mambo yanayotarajiwa na jamii.

Kuna makundi mawili ya kanuni yanayohitaji kufikiriwa. La kwanza ni kanuni za kijamii. Hizi zinajumuisha jinsi watu wanavyowasiliana na kutendeana.

La pili ni kanuni za kujifunza. Hizi zinajumuisha jinsi wanafunzi wanavyotenda wakati wa masomo nay ale wanayoweza kuyatenda ili wasaidiane katika kujifunza na kujisomea. Kwa kuwapanga wanafunzi wafanye kazi katika makundi utawapatia fursa ya kubadilishana mawazo na kukuza zaidi tabia ya kuheshimiana.

Ni muhimu kwamba kanuni hizi zitumike kwa mwalimu; na vilevile kwa wanafunzi. Unatakiwa kuonesha mfano mzuri kwa wanafunzi wako. Ukiwaheshimu wanafunzi wako darasani, na wao watajifunza kukuheshimu.

Uchunguzi kifani ya 3: Uundaji wa sheria za mwenendo

Bi. Mambo aliwaambia wanafunzi wake wa Darasa la III kutafakari kuhusu sheria za mwenendo walizozibainisha hapo awali na kwa namna gani sheria hizi zinaweza kuwasaidia kuunda kanuni zao wenyewe za darasani.

Aliwaambia wanafunzi kutafakari kuhusu majukumu yao mbalimbali. Mambo gani wanaweza kuyafanya ili kusaidiana kutimiza majukumu hayo?Kwanza walizungumza pamoja katika makundi ya wanafunzi wawili wawili, na halafu kama darasa. Mwishowe, katika makundi madogo madogo, aliwaambia waandike sentensi kwa kutumia: ‘Tunapaswa …’

Alizungukia kila kundi na kuwaambia wanafunzi wasome sentensi moja na kueleza kwa nini wameiandika hivyo. Kwa mfano: ‘Tunapaswa kuwa kimya darasani kwa sababu itatusaidia kusikiliza vizuri’.

Kama wanafunzi wakipendekeza katika ukanushi, kwa mfano ‘Usiongee darasani’, kwa pamoja wanabadilisha kuwa katika uyakinishi: ‘Tunapaswa kusikilizana kwa makini’.

Aliridhishwa sana na majibu yao, na alikusanya sentensi zao. Siku iliyofuata, alizipitia zote tena na alichagua sentensi nane. Kisha, Bi. Mambo aliziandika ubaoni na wanafunzi walizinakili daftarini mwao kwa ajili ya kumbukumbu.

Shughuli muhimu: Kuunda kanuni za darasani

Jadili na darasa lako kwa nini tunahitaji kanuni za darasani kwa ajili ya mwenendo na kwa ajili ya masomo. Jadili kwa nini wao – na si wewe –wataandika kanuni hizo.

Waache wanafunzi, katika makundi, wajadili mapendekezo yao kuhusu kanuni za kijamii na zile za kimasomo. Waambie waandike kanuni tano kila mmoja, kwa kutumia sentensi yakinishi. Kusanya mapendekezo kuhusu kanuni za kijamii toka katika kila kundi na kisha yaandike ubaoni. Waambie walieleze darasa kwa nini kanuni hizo ni muhimu.

Andaa upigaji wa kura: mwambie kila mwanafunzi achague kanuni sita mpaka nane kutoka ubaoni. Kama una kanuni nzuri, huhitaji kuwa na nyingi kupita kiasi. Soma kwa sauti kila kanuni, na hesabu idadi ya mikono iliyonyooshwa na wanafunzi kwa kila kanuni. Andika idadi ya mikono ubaoni na bainisha zile zilizochaguliwa na wengi zaidi.

Fanya hivyo hivyo kwa kanuni za kimasomo. Andaa darasa ili kutengeneza bango la kanuni zilizoandikwa. Organise the class to make a poster of the written rules. Libandike bango hilo kwenye mlango wa darasa ili kumkumbusha kanuni hizo kila aingiaye ndani ya darasa.

Fuatilia jinsi kanuni hizo zinavyofanya kazi kwa muhula mmoja, na pitia kanuni hizo, ikiwa ni lazima kufanya hivyo. Wewe na wanafunzi mtafanyaje kuzirekebisha?

Nyenzo-rejea 1: Faida za sheria za darasa

Taarifa za Msingi / welewa wa somo wa mwalimu

Kuna faida nyingi za kuwa na sheria zilizoundwa vema katika darasa lako. Fungu la miongozo iliyo dhahiri kuhusu ipi ni tabia nzuri na ipi ni tabia isiyokubalika katika darasa, linakusaidia kusimamia darasa vizuri zaidi. Kwa kufuata miongozo hii kama kanuni, utaweza kuzirejelea endapo zitahitajika. Hata hivyo, ili kanuni hizi ziweze kuwa faafu kwa mtazamo chanya, wanafunzi pia wanahitaji kufahamu kwa nini kanuni fulani ipo.

Miongozo hii inawasaidia wanafunzi kuelewa wanachotarajiwa wafanye. Wanafahamu tabia zipi zinatakiwa wakati wa masomo na wakati wa mapumziko. Pia wanafahamu kuhusu jinsi ya kuwasiliana na sababu za kuwasiliana. Fungu la miongozo kuhusu tabia linakurahisishia kupanga wanafunzi wakati wa kufanya shughuli za darasani. Watajua ni wakati gani wasikilize, wakati gani wazungumze, wakati gani wajibu maswali, na kadhalika. Kuwa na miongozo inayohusu tabia maana yake ni kwamba wanafunzi wanafunzi watajenga tabia ya kutendeana vizuri. Hali hii italifanya darasa liwe la amani na ushirikiano. Kwa kuwapa fursa wanafunzi waandike kanuni zao wenyewe na kuwajibika katika shughuli za darasani, utakuwa unawatia moyo waone fahari ya kujifunza. Aidha, watakuwa na nafasi kubwa ya kufuata kanuni hizo, ambazo kwa hakika, wameziandika wao wenyewe.

Hayo hapo juu yatachangia kuleta mazingira chanya ya ujifunzaji katika darasa lako. Utaweza kutumia muda mrefu zaidi katika ufundishaji na muda mfupi zaidi katika kulidhibiti na kulisimamia darasa. Wanafunzi watasikiliza vizuri darasani na watakuwa makini katika shughuli zao. Vilevile, watajifunza kusaidiana na kustahimiliana wenyewe katika masomo yao, jambo ambalo linatakiwa kuleta ubora zaidi wa mafanikio. Kwa jinsi wanavyopata maendeleo katika kujifunza kwao, watajisikia vizuri kama ilivyo kwa watu wengine, na hii itakufanya ufurahie kuendelea kuwafundisha.

Nyenzo-rejea 2: Kuwatumia viranja wa darasa

Taarifa za msingi / welewa wa somo wa mwalimu

Ukiwa mwalimu, unaweza kuwatumia wanafunzi ili wakusaidie katika shughuli za kila siku za usimamizi wa darasa lako. Kuna majukumu kadhaa rahisi ambayo unaweza kuwaambia wanafunzi wako wayatekeleze kwa niaba yako, nah ii inaleta faida mbili:

  • Inakuruhusu utumie muda zaidi katika kuandaa na kufanya ufundishaji mzuri, kuliko kutumia muda huo kulisimamia na kulipanga darasa;

  • Inawapa wanafunzi maeneo machache ya uwajibikaji, jambo ambalo linawatia moyo wa kuonea fahari masomo yao.

Kuna mambo machache unayohitaji kuyafikiria unapochagua viranja wa darasa. Unataka wanafunzi ambao watatekeleza majukumu yao vizuri, na ambao watakuwa tayari kukusaidia wewe na wengine.

Vilevile, unataka wanafunzi ambao watakuwa na jukumu la kuwasiliana vizuri na wengine. Wakati mwingine, wanafunzi wanaweza kuona kwamba kuwa kiranja wa darasa ni kama kuwa na nafasi ya nguvu dhidi ya wengine, na wanaweza kuitumia vibaya dhana hiyo. Ni muhimu kuwasaidia ili waelewe kwamba wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, na wewe hapa utakuwa mfano wa kuigwa. Wanafunzi wote lazima wapewe fursa ya majukumu haya ya ukiranja wa darasa. Ikiwa utawachagua wanafunzi wale wale kila mara, wengine watajihisi kutothaminiwa. Unatakiwa kutoa mwongozo na msaada kwa viranja wa darasa. Baadhi yao watahitaji msaada zaidi yaw engine katika hatua za awali.

Unahitaji kufikiri kwa makini kuhusu kila kazi kabla ya kuzitoa kwa wanafunzi. Kama si kazi ya kufanya kila siku, wanafunzi watachoshwa nayo na wataipuuza. Vilevile, inahitajika kuwepo na kusudi dhahiri kwa ajili ya kazi hiyo, kuliko kitu cha kupitisha wakati tu. Mwisho, utahitajika pia kutoa maelekezo thabiti.

Ni muhimu kugawa kazi na kumpa kila mwanafunzi zamu. Kama wanafunzi wengine hawashirikishwi, watakata tama na wanaweza hata kuvuruga utaratibu wa darasa ili wavute usikivu wa viranja wa darasa; yaani wawasumbue.

Kama ikiwezekana, waache wanafunzi wachague kazi wanazoweza kuzifanya ili kusaidia. Unaweza pia kufanya mikutano ya darasa ya mara kwa mara ambako wanafunzi wanaweza kutoa mapendekezo mbalimbali ya majukumu.

Mwisho, unahitaji pia kuwafuatilia na kuwasaidia. Wasifu pale unapoweza kufanya hivyo na wape mwongozo panapohitajika.

Sehemu ya 4: Kuchunguza Kujithamini

Swali Lengwa muhimu: Utatumiaje hadithi na shughuli nyingine kukuza na kutathmini kujithamini kwa wanafunzi?

Maneno muhimu: kujithamini; mahusiano; kazi za vikundi; shughuli za kijumuiya; tathmini; hadithi

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii , utakuwa umeweza:

  • umetumia shughuli na njia mbalimbali za kuwaweka wanafunzi katika vikundi ili kukuza kujithamini kwao;

  • umekuza welewa wako wa mambo yanayoweza kuathiri kujithamini;

  • umepanga shughuli yenye msingi wa kijumuiya;

  • umetumia njia za kutathmini ujifunzaji.

Utangulizi

Sehemu hii inahusika na jinsi ya kutoa utangulizi kwa wanafunzi juu ya hulka ya mahusiano mbalimbali na kuwasaidia waelewe kwamba mahusiano haya yanaweza ama kusaidia au kudhoofisha kujithamini. Athari ya mahusiano haya juu ya elimu ya wanafunzi inaweza kuwa kubwa. Ukiwa mwalimu, unao wajibu wa kujitahidi kadiri uwezavyo kutoa mazingira ya kujifunzia yenye msaada.

‘Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto’ (uk. 2) unasema kwamba:

‘Katika matendo yote yahusuyo mtoto yafanywayo na mtu yeyote au mamlak yoyote, maslahi bora ya mtoto yatakuwa ni zingatio la msingi…’

Washirika katika Mkataba huu watahakikisha, kwa kadiri watakavyoweza, uwezo wa kuishi, ulinzi na maendeleo ya mtoto’

Sehemu hii inaanzisha mjadala tu na wala haiingii kwa undani katika mchangamano wa mahusiano ya uonevu na tabia isiyofaa. Inatalii jinsi haya yanavyoweza kuathiri kujifunza na kujithamini kwa wanafunzi na inakupatia mwangaza kidogo katika nafasi na wajibu wako na haja ya kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu wengine unapohusika.

Mwishowe, tunajadili jinsi unavyoweza kuhamasisha wanafunzi kufanya kazi pamoja na kuwasaidia wale wenye matatizo.

Somo la 1

Kujithamini ni ufunguo muhimu kwa mafanikio katika maisha. Ukijihisi vyema kuhusu wewe ni nani, utajiamini zaidi katika kuungana na wengine, kupata marafiki wapya na kukabili hali mpya.Ukiwa mwalimu, una nafasi muhimu sana ya kukuza kujithamini miongoni mwa wanafunzi kwa jinsi unavyoingiliana nao. Unapaswa kuwa makini kuhusiana na hisia na mihemko ya wanafunzi, na unapaswa kuwa mwangalifu kuhusiana na mambo unayowaambia na jinsi unavyoongea nao.

Ni muhimu kuwa na mtazamo unaojenga na unaotia moyo, ukiwasifu wanafunzi kwa kazi yao nzito na mafanikio yao, na kutumia maneno ya ukarimu kila inapowezekana. Jaribu kuwakutiliza wakiwa wanatenda mema, badala ya kuwatega ili uwashike wakiwa wanatenda mabaya. Hii haimaanishi kuwa huna haja ya kuwatia nidhamu, lakini jinsi unavyofanya hivi ni muhimu ikiwa unataka kudumisha uhusiano mzuri wa kikazi nao.

Kila mara inafaa kuanza mada mpya kwa kutafiti mambo ambayo wanafunzi wako tayari wanayafahamu. Waombe mawazo juu ya kujithamini –unaweza kushangazwa na majibi mbalimbali watakayoyatoa.

Uchunguzi Kifani 1 na Shughuli 1 vinaonesha jinsi unavyoweza kutumia hadithi kwa njia mbalimbali ili kutalii wazo kama kujithamini.

Uchunguzi kifani ya 1: Kushughulikia masuala ya kujithamini

Joni Nvambo, aliye Naijeria, ana uhusiano mzuri na wanafunzi wake 36 wa darasa la nne. Siku moja, aling’amua kuwa si wanafunzi wake wote walikuwa wakichangia darasani. Baadhi walikuwa sasa wana soni na wakimya, na hawakumwuliza maswali. Aling’amua pia kuwa hili lilikuwa linaathiri alama zao. Kwa hiyo akaamua kulishughulikia tatizo hili.Kesho yake asubuhi, Joni alisimulia hadithi ya watoto watatu ili kuwasaidia waanze kufikiria wazo la kujithamini. (tazama Nyenzo-rejea 1: Hadithi juu ya kujithamini ).Kisha akaligawa darasa katika vikundi vitatu, A, B na CH, akikielekeza kila kikundi kuorodhesha sifa za mtu mwenye ama:

kujithamini vya kutosha;kujithamini kiwango cha chini; aukujithamini kupita kiasi.

Kisha, Joni aliwapanga watatuwatatu, mmoja kutoka kila kikundi, ili wabadilishane mawazo kabla ya kujadili kama darasa.Waliweza kubainisha sifa mbalimbali, na kwa nini zilikuwa nzuri au mbaya kwa watu husika. Kutokana na hili, waliweza kuzungumzia jinsi ya kupata uwiano wa kujithamini kwa kutumia shughuli kama ile iliyoko kwenye Shughuli 1.

Shughuli ya 1: Kukuza kujithamini

Tohoa Nyenzo-rejea 1 ili ikusaidie katika shughuli hii.

  • Gawa darasa katika vikundi. Vikundi hivyo viite ama A au B.

  • Uvitake vikundi vya A vimsaidie kijana mwenye kiburi abadilike awe na kujithamini kwenye uwiano.

  • Uvitake vikundi vya B vimsaidie kijana mwenye kujithamini kiwango cha chini kubadilika ili aanze kujiamini.

  • Fuatilia majadiliano ya vikundi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanashiriki.

  • Baada ya dakika 15, unda vikundi kwa kuchukua mtu wa kikundi A na kumuunganisha na mwingine wa kikundi B.

  • Watake wanavikundi kulinganisha mawazo na kupeana mapendekezo.

  • Baada ya dakika kumi, fanya majadiliano ya darasa zima kuhusu mawazo ya kumsaidia mtoto mwenye kiburi na kisha yule asiyejiamini.

  • Mwisho, kama darasa, orodhesha sifa kuu za kujithamini kunakofaa na jinsi kunavyowasaidia wanafunzi kufaidiana.

Je, shughuli hii imeathiri mwenendo wa wanafunzi katika mahusiano baina yao?

Somo la 2

Kwa bahati mbaya, kwa kadiri baadhi ya wanafunzi wanavyokua wanaweza kukutana na uhusiano uliojaa unyanyasaji. Aina hii ya uhusiano unaweza kuathiri vibaya ukuaji wao wa kijamii, kihisia na kimwili, na inachukua muda na juhudi nyingi kuwasaidia washinde uharibifu uliokwisha fanyika.

Dhana ya ‘unyanyasaji’ isichanganywe na lugha ya matusi na karaha. ‘Unyanyasaji’ kwa maana hii hutokea pindi watu wawatumiapo wengine kwa njia isiyo sahihi na isiyofaa. Mahusiano ya namna hii huacha kovu la kudumu la kisaikolojia, kihisia na kimwili kwa mtu aliyenyanyaswa. Kuna aina kadhaa za unyanyasaji, kwa mfano unyanyasaji wa kimwili na wa kiakili. Kuna mifano ya unyanyasaji wa aina hizi katika Nyenzo-rejea 2: Aina za unyanyasaji , ambayo huna budi kuisoma .

Ukiwa mwalimu, wajibu wako ni kuwasaidia wanafunzi kujifunza. Kama hawana furaha au wananyanyaswa, hawatajifunza. Dhima yako ni kuwalinda wanafunzi wako na unaweza kuhitaji kuwahusisha wengine wenye utaalamu zaidi na wanaoweza kutoa ushauri-nasaha. Nyenzo-rejea 3: Dhima ya walimu wa shule inatoa maelezo zaidi juu ya wajibu wako.

Njia bora ya kusaidia ni kutalii na wanafunzi wako mambo wanayofahamu kuhusu tabia sahihi na zisizo sahihi katika mahusiano. Hata hivyo, huna budi kufanya hivi kwa makini na uangalifu. Nyenzo-rejea 4: Kutafiti mambo ambayo wanafunzi wanafahamu tayari kuhusu mahusiano inaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyofanya jambo hili. Unaweza kutumia mbinu hii na wanafunzi wako..

Uchunguzi kifani ya 2: Ajira ya Watoto

Bwana Sele, mwalimu wa Darasa la 5 Shule ya Msingi Mlimani, alimleta Afisa wa Ustawi wa Jamii wa wilaya kuzungumza na darasa juu ya unyanyasaji.

Afisa wa Ustawi wa Jamii alianza kwa kuwaambia wanafunzi kwamba kuwatumia vijana kufanya kazi za biashara na shambani lilikuwa jambo la kawaida katika sehemu nyingi Afrika. Ilikuwa ni njia ya kuwakuza vijana wajifunze stadi na uwajibikaji, na kuweza kujitegemea.

Lakini baada ya ‘Mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Mtoto’ (tazama Utangulizi) kupitishwa, serikali haikuridhika na utumiaji wa watoto kama watembeza bidhaa mitaani na walimaji mashamba, ambako walinyonywa na kulazimishwa kufanya kazi kwa masaa mengi. Ni hatari kwa afya zao, na mara nyingine husababisha kifo. Watoto huachishwa shule na elimu, na mara nyingine husukumizwa kwenye uhalifu.

Afisa Ustawi wa Jamii alisema kuwa wazazi mara nyingine hutoa hoja kwamba wanawahitaji watoto kuleta chakula na fedha kwa ajili ya familia. Hata hivyo, alisema, serikali hulichukulia jambo hili kuwa kinyume na sheria, kwa kuwa watoto wote wana haki ya kupata elimu ya bure, na kwamba kila jumuiya inahitaji kushughulikia suala hili.

Kufuatia hotuba ya afisa wa ustawi wa jamii, siku iliyofuata, darasa la Bwana Sele liliwasilisha igizo kifani juu ya unyanyasaji wa watoto. Walilionesha kwanza kwa shule nzima, na kisha kwa kamati ya Chama cha Wazazi na Walimu (tazama Nyenzo-rejea 5: Jinsi igizo kifani lilivyopokewa) .

Shughuli ya 2: Igizo kifani juu ya unyanyasaji wa watoto

Andaa igizo kifani linalohusika na suala la unyanyasaji wa watoto kwa ajili ya darasa lako. Unahitaji kufikiri kwa makini juu ya hili. Linaweza kuwa suala nyeti sana kwa vijana, hivyo utahitaji kuwa mwangalifu katika uandaaji wa shughuli hii.

Kwanza, orodhesha aina mbalimbali za unyanyasaji wa watoto na matokeo yake. Chagua aina unayotaka kushughulikia darasani.

Fikiria jinsi utakavyoanzisha masuala haya darasani. Kuhusu igizo kifani, amua kuhusu nafasi mbalimbali za wanafunzi. Masuala yapi yanahusika na kila nafasi?

Panga ni wanafunzi wangapi watakuwa katika kila kikundi, na jinsi watakavyoandaa na kuigiza igizo kifani. Utawaelezaje jambo hili?

Mwisho, utaandaaje muhtasari wa mambo muhimu na wanafunzi baada ya kumaliza kuigiza igizo kifani? Utakuwa na mjadala? Utausimamiaje?

Kukusaidia, tumia Nyenzo-rejea kwa ajili ya sehemu hii na Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia igizo kifani/mazungumzo/tamthiliya darasani.

Somo la 3

Ni muhimu kwa wanafunzi kukuza njia za kufikiria jinsi mahusiano mbalimbali yanavyofanya kazi ili waweze kupata marafiki na kujilinda wasipatikane na madhara.

Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kuwasaidia wanafunzi wafanye kazi na jumuiya kushughulikia suala mahususi. Shughuli kama hizi huwaunganisha wanafunzi na jumuiya ili kutatua tatizo la kijumuiya. Wanafunzi hujifunza kuhusu mahusiano kwa kufanya kazi na wengine, kwa:

  • kubadilishana maarifa na wataalamu wa mahali husika; kujifunza jinsi vikundi vinavyofanya kazi; kujifunza jinsi ya kukubali na kutimiza majukumu; kujifunza jinsi ya kutendeana ifaavyo; kuunganisha mawazo mbalimbali ili kusaidia kutatua tatizo.

Kupanga na kuandaa shughuli ambapo wanafunzi hufanya kazi na watu wengine katika jumuiya kwaweza kuwa kugumu. Unahitaji kuandaa kazi ambayo wanafunzi wanaweza kuchangia kikwelikweli, na unahitaji kuchagua watu walio tayari kufanya kazi na watoto. Unahitaji pia kupanga nao namna mwingiliano utakavyofanya kazi –unaweza kuhitaji kufanyika kwa zaidi ya wiki mbili au tatu au zaidi. Ni muhimu kwa wote wanaohusika – watu wazima na watoto –wafahamu wanachotakiwa kufanya. Kabla ya kufanya sehemu hii, tunapendekeza usome Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia jumuiya/mazingira husika kama nyenzo

Uchunguzi kifani ya 3: Kampeni ya mazingira ya jumuiya

Bibi Msafiri alikuwa akizungumza na darasa la sita kuhusu jinsi ya kuweka mazingira yao safi. Aliwataka wafikirie vitu katika jumuiya ambavyo vilihitaji kusafishwa.

Jambo moja walilotaja ni mifuko ya plastiki mtaani. Mifuko hiyo ilisababisha matatizo kwa kuwa iliziba mifereji. Mara nyingine, ng’ombe na mbuzi waliila na kuugua.

Darasa la Bibi Msafiri liliamua kuanzisha kampeni ya kijumuiya. Walizungumza na afisa mazingira wa hapo ambaye alikuja kuwasaidia kupanga kampeni yao darasani. Walizungumza pia na kamati ya wafanya biashara wa sokoni na wakaandaa kampeni hiyo pamoja.

Afisa mazingira aliandaa tukio la kijumuiya na alipata udhamini toka kwa AZAKI ya mazingira ya hapo. Wafanya biashara waliwaeleza wateja wao juu ya jambo hilo. Baada ya kujadiliana masuala haya na afisa mazingira, Bibi Msafiri aliwaandaa wanafunzi wake wafanye yafuatayo:

  • kuchora bango la kampeni;

  • kutunga tamthiliya na wimbo;

  • kuandaa mdahalo kwa ajili ya tukio hili;

  • kuandaa kampeni ya usafi.

Tukio hili lilifanikiwa kabisa. Wafanya biashara walionyesha mabango magengeni, na walifafanua masuala husika kwa wateja wao.

Jumamosi moja, shule nzima iliokota mifuko yote mtaani na kwenye mifereji. Kwa msaada wa wafanya biashara na afisa mazingira, kijiji kilikuwa safi zaidi sasa.

Shughuli muhimu: Kutathimini ujifunzaji wa wanafunzi

Kwanza soma Nyenzo-rejea 6: Mwongozo wa kupanga shughuli yenye msingi wa kijumuiya na Nyenzo-rejea muhimu: Kutathmini kujifunza. Kama unataka kuandaa shughuli yenye msingi wa kijumuiya kwa ajili ya wanafunzi wako, panga jinsi utakavyotathmini watakayokuwa wamefaidi kutokana na uhusiano. Endesha shughuli na darasa lako.

Baadaye, watake wajadiliane na kuandika juu ya shughuli zao, wakieleza:

  • taarifa walizotumia;

  • shughuli walizofanya na stadi walizokuza;

  • walivyoingiliana na watu waliohusika, na nani alifanya nini;

  • jinsi walivyoandaa kazi yao.

Pindi wakishafanya hivi, unapaswa kuwa na ushahidi wa stadi na maarifa mapya waliyopata. Wahimize kufikiria jinsi tukio lilivyofanikiwa.

Sasa, waulize mambo yapi mapya wamejifunza. Waelekeze wayajadili katika vikundi na kisha andika orodha.

Mwisho, watake waeleze:

  • wanapanga kutumia vipi stadi zao mpya siku za usoni;

  • nani wangependa kufanya naye kazi baadaye.

Wanafunzi wameona kuwa shughuli hii yachangamsha? Unajuaje? Unawezaje kuitumia tena aina hii ya shughuli?

Nyenzo-rejea 1: Hadithi juu ya kujithamini

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili ya kupanga au kutohoa kwa matumizi na wanafunzi

Kulikuwa watoto watatu walioishi katika kijiji kimoja – wavulana wawili na msichana mmoja. Siku moja, wote walianza kwenda shule. Kwa kuwa walikuwa na umri sawa, waliingia katika darasa lilelile, ingawa walipokea mambo kwa kutofautiana sana.

Mvulana wa kwanza alikuwa na akili, na alianza kufanya vizuri shuleni. Aliweza kujibu maswali mengi na mara zote alipata alama nzuri. Kwa sababu hii, alianza kujiona. Hakutaka kusikiliza mawazo ya watu wengine. Akawa jeuri, na akafikiri alifahamu kila kitu. Alikuwa na dharau kwa wengine, na akaanza kupoteza marafiki.

Mvulana wa pili aliiona shule kuwa ngumu, na hakuelewa baadhi ya mambo. Lakini aliogopa kumuuliza mwalimu kwa kuogopa kuadhibiwa. Akabaki nyuma kabisa katika masomo yake. Kwa sababu hii, akajiona hafai. Alidhani kuwa wenzake darasani walikuwa wakimcheka. Alijiona hana faida, na akadhani anadharauliwa na mwalimu, kwa hiyo hakuongea darasani.

Msichana alifurahia kwenda shule toka mwanzo. Alipenda kufanya urafiki na wenzake, na akang’amua kuwa angejifunza mengi kwao. Alikuwa na uwezo mzuri wa kujifunza lakini alipenda kubadilishana mawazo na wengine. Alipenda kuwasikiliza wengine. Alikuwa mcheshi, lakini alijifunza kutopiga sana kelele. Aliweza kuuliza maswali ilipohitajika, lakini hakujua kudai usikivu kwa yeyote.

Nyenzo-rejea 2: Aina za unyanyasaji

Usuli / dokezo kwa mwalimu

Kuna aina mbalimbali za unyanyasaji – wa kimwili, kingono, kihisia na kisaikolojia. Aina hizi zinaweza kutokea baina ya watu wazima, baina ya watoto, au baina ya watu wazima na watoto.

Ni muhimu kwamba wanafunzi wako wawe na utambuzi wa aina hizi za unyanyasaji, kwa sababu wakiwa bado ni watoto kuna uwezekano mkubwa wa kudhurika. Huwaamini watu wazima, na kwa kawaida hufanya wanayowaambia, lakini wanapaswa kujua kwamba si kila kitu ambacho mtu mzima hufanya ni sahihi.

Unyanyasaji wa kimwili unahusisha kupiga mtu. Si lazima kuwe kwa nguvu, lakini kama unyanyasaji wa kimwili ni wa mara kwa mara unaweza kuwa na athari mbaya kwenye uhusiano.

Unyanyasaji wa kingono ni utumizi usiofaa wa mtu mwingine kwa nia ya kukidhi tamaa ya ngono, kwa kawaida bila kibali au kwa shinikizo la kisaikolojia au utumizi wa nguvu. Hii hutokea baina ya watu wazima, baina ya watu wazima na watoto, na pia baina ya watoto wanaoingia utu uzima. Fadhaa na madhara ya kisaikolojia yaweza kuwa mabaya kabisa, na wanafunzi wanaweza kuwa wagomvi sana au wakimya sana; wanaweza kuwa na wasiwasi wawapo na watu wazima au kuwa na mwenendo usiofaa na wanafunzi wenzao.

Unyanyasaji wa kihisia na kisaikolojia unahusisha kumtendea mtu kikatili kwa muda mrefu, hali inayomfanya ahuzunike na kusikitika. Unaweza kuhusisha kumtukana au kumkosea adabu, au kudhoofisha kujiamini kwake na kudunisha mafanikio yao.

Kuna mifano mingine pia, kwa mfano unyanyaswaji na wazazi. Huu unaweza kutokea, kwa mfano, kama baba atamrubuni mtoto wake wa kiume kwa kumwekea sigara mdomoni na kumwashia.

Unyanyaswaji wa namna hii pia waweza kuwa kumpiga mtoto kila mara na kwa nguvu na kumpatia majeraha na kumkandamiza na kumdhibiti kupita kiasi.

Kunaweza kuwa na unyanyasaji wa nyumbani – udhalilishaji wa wake au wafanyakazi wa nyumbani, hata kama wanafanya kazi kwa juhudi.

Unyanyasaji wa namna hii husababisha maumivu ya kimwili na kihisia, na yanaweza kusababisha huzuni na kutojiamini sana.

Nyenzo-rejea 3: Dhima ya walimu

Usuli / dokezo kwa mwalimu

Walimu wana nafasi ya kutambua pindi wanafunzi wanaponyanyaswa. Wana nafasi ya kumfahamu vizuri mwanafunzi mmoja mmoja, na hivyo kung’amua mabadiliko katika tabia au utendaji wa mtoto, ambao unaweza kuhusishwa na unyanyaswaji. Watoto pia wanaweza kufichua hali zao katika masomo ya stadi za maisha au sehemu nyingine za mtaala.

Kama mwalimu atashuku unyanyasaji, njia inayofaa kufuata ni hii:

  • Anza kukusanya taarifa pindi tu ushukupo unyanyasaji wa mtoto.

  • Endelea kufanya hivyo kwa uthabiti, andika taarifa zote unazokusanya.

  • Zichukulie taarifa hizi zote kuwa ni siri.

  • Jadili tuhuma zako na taarifa ulizokusanya na mwalimu mkuu (kama hahusiki)

  • Hakikisha usiri kwa kufungua jalada la pekee kwa mwanafunzi huyo. Jalada hilo lapaswa kuhifadhiwa mahali pa salama. 

  • Mwalimu mkuu na mwalimu lazima wachunguze orodha ya vigezo vya utambuzi wa aina mbalimbali za unyanyasaji kuthibitisha taarifa hiyo kabla ya kutoa madai ya unyanyasaji wa mtoto. Washirikishe wataalamu wenye uzoevu.

  • Usipendelee upande wowote wakati wote na usiruhusu mambo binafsi au hisia au mawazo uliyokuwa nayo kabla yaharibu uamzi wako.

  • Taarifa yoyote ihusuyo unyanyaswaji wa mtoto ni ya siri na lazima ishughulikiwe kwa busara.

  • Utoaji taarifa na uchunguzi wa unyanyaswaji wa mtoto lazima vifanyike kwa namna itakayohakikisha usalama wa mtoto.

  • Haki isihatarishwe, kanini wakati huo huo msaada ambao mtoto na familia yake wanahitaji usipuuzwe.

Mambo mengine muhimu ya kukumbuka unapoongea na wanafunzi ni:

  • Usimwambie mtoto anayefichua unyanyasaji kwamba humwamini.

  • Shadidia ujasiri wa mtoto kwa kufanya ufichuzi.

  • Mwambie mtoto unachotaka kufanya kuhusu aliyokwambia, na kwa nini.

  • Kama inawezekana, mwambie mtoto kitakachofuata. 

  • Ikilazimika, mtoto apate ushauri-nasaha.

  • Jiandae kutoa ushaidi mahakamani kama kuna mashataka.

Kuna mashirika mengi Afrika yote yaliyojitoa kwa ajili ya uzuiaji wa unyanyasaji wa watoto, kwa mfano Mtandao wa Afrika kwa ajili ya Uzuiaji na Ulinzi dhidi ya Unyanyasaji na Upuuzaji wa Watoto (African Network for the Prevention and Protection against Child Abuse and Neglect (ANPPCAN)). Tazama Wavuti www.anppcan.org/ kwa ajili ta taarifa zaidi.

Mkombozi ni shirika lililoanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto wa mitaani; sasa ni mojawapo ya mashirika maarufu yanayomlenga mtoto kaskazini mwa Tanzania. Nia yao ni ‘kutumia elimu, utafiti, utetezi, na elimu-masafa kuwasaidia watoto na vijana wenye uwezekano wa kudhurika kukua kiakili, kimwili na kiroho’. Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu kazi yao kwenye wavuti http://www.mkombozi.org/

Angalizo: Siku ya Unyanyaswaji wa Mtoto Duniani ni 19 Novemba kila mwaka.

Imetoholewa kutoka kwenye Nyenzo-rejea Zinazolenga Uzuiaji wa Unyanyasaji na Upuuzaji wa Watoto (Resources Aimed at the Prevention of Child Abuse and Neglect) (RAPCAN)

Nyenzo-rejea 4: Kutafiti mambo ambayo wanafunzi wanafahamu kuhusu mahusiano

Nyenzo ya mwalimu kwa ajili ya kupanga au kutohoa kwa ajili ya matumizi na wanafunzi

Rehema ni mwalimu mchapakazi kwenye shule ya jumuiya iliyopangiliwa vizuri katika kijiji katikati ya Tanzania. Kwa mkabala wake bainifu na kamilifu wa ufundishaji, alirahisisha maneno magumu ambayo wanafunzi wake wangeweza kukutana nayo katika uchunguzi wao wa mahusiano. Nia ni kuwahamasisha na kusaidia welewa wao.

Rehema anawataka wanafunzi wake wajadiliane katika vikundi:

  • kina nani wanahusiana nao kila siku nyumbani, na kwa nini;

  • kina nani wanabadilishana mawazo na uzoevu shuleni, na kwa sababu gani; 

  • kama wanahusiana na walimu wao, na kwa nini.

Baada ya kujadili mawazo haya katika vikundi, na kama darasa, mwalimu anawauliza kitu kinachofanya wahusiane na mchuuzi aliye nje ya lango la shule. Anawataka wafikirie watu gani katika jumuiya wanaowaona mara kwa mara, na kwa nini.

Wanajadili mawazo haya katika vikundi; kisha wanayajadili kama darasa. Kutokana na haya, Rehema anaweza kuwasaidia wanafunzi kuanza kutambua aina mbalimbali za mahusiano waliyo nayo na watu, na mienendo inayofaa kwa kila mojawapo.

Alitumia pia shughuli ifuatayo ya vikundi kuwasaidia wanafunzi wake kutalii mawazo kuhusu mahusiano.

  • Ligawe darasa lako katika vikundi unavyoweza kuvisimamia vizuri kwa kuzingatia mchanganyiko wa jinsia, aina za haiba na ujuzi, ili viyafanyie kazi maswali yafuatayo.

  • Kiruhusu kila kikundi kuchagua kiongozi wa kupanga kazi, na mwandishi wa kuandika mawazo yao.

  • Bainisha kwamba kazi ni ya dakika 15 tu na kila kikundi kitatoa taarifa kwa dakika tano.

  • Zungukazunguka chumbani kufuatilia maendeleo ya kila kikundi na kuhakikisha kwamba kila mwanakikundi anashiriki kikamilifu na wenzake.

  • Baada ya dakika 15, viite vikundi kwa zamu kutoa taarifa, wakati vikundi vingine vikiandika tini.

  • Ukishirikiana na wanafunzi, fanya muhtasari wa mawazo muhimu kwa ajili ya wanafunzi kuandika. Waelekeze wazingatie aina mbalimbali za mahusiano na kwa nini zipo.

Maswali kuhusu mahusiano

  • Una hisia gani kwa kaya/familia ambamo ulizaliwa?

  • Una hisia gani kwa dada/kaka yako nyumbani katika familia?

  • Ni kitu gani ambacho dada/kaka yako hukufanyia kinachomfanya awe karibu nawe?

  • Nani rafiki yako bora shuleni?

  • Kitu gani kinamfanya awe rafiki yako bora?

  • Kitu gani kinakufanya uhusiane na mwalimu wako?

Nyenzo-rejea 5: Jinsi Igizo kifani Lilivyopokewa

Usuli / dokezo kwa mwalimu

Soma simulizi lote juu ya mwitiko wa jumuiya kuhusu igizo kifani, na kisha fikiria miitiko muhimu ilikuwa ipi. Kungeweza kutokea miitiko gani badala ya hii?

Fikiria kama jumuiya hii ingekuwa yako – unafikiri miitiko ipi ingeweza kutokea? Ungeshughulikiaje hali yoyote ambayo ingetokea?

Jinsi jumuiya ilivyolipokea igizo kifani

Baada ya darasa la Bwana Sele kuigiza igizo kifani lake kwa jumuiya, kulikuwa na mwitikio mkubwa. Chama cha Wazazi na Walimu kiliamua kuandaa mdahalo juu ya suala hili, na kulikaribisha darasa liwasilishe mawazo ya watoto.

Wiki iliyofuata, Bwana Sele aliongoza darasa lake hadi kwenye ukumbi wa mikutano wa shule, mahali pa mkutano wa viongozi wa jumuiya na wawakilishi wa makundi ya wataalamu wa eneo hilo. Mwenyekiti wa kijiji alikuwa mwenyekiti wa mkutano, afisa wa ustawi wa jamii alikuwa mwandishi.

Kila kundi liliwasilisha msimamo wake kuhusu tatizo la unyanyasaji wa watoto, kundi moja baada ya jingine.

Wanafunzi walisema kwamba wanataka unyanyasaji wa watoto upigwe marufuku kwa sababu unavuruga elimu ya watoto na mchango wao kwa maendeleo ya taifa.

Mwalimu mkuu wa shule hii alisema kwamba unyanyasaji wa watoto umesababisha upunguaji wa watoto wanaoandikishwa kusoma shuleni na kwa hiyo shule yake haiwezi kutimiza wajibu wake wa kuandaa viongozi wa siku zijazo.

Askari polisi alisema kwamba wasichana wadogo wachuuzi huingia kwenye ajira ya ngono na kuwa changu-doa. Wavulana huishia katika uhalifu wa aina mbalimbali, pamoja na udokozi na ujambazi.

Rai ya afisa wa afya ilikuwa kwamba wafanyakazi wengi wa mitaani, pamoja na watoto, hawali chakula cha kutosha na cha kufaa, na huelekea kuvutika na utumizi wa madawa ya kulevya, ambayo huwasababishia matatizo makubwa ya kiakili na kimwili.

Wazazi na wachuuzi walitoa hoja kwamba huwatumia watoto wao kutafuta kipato kwa ajili ya familia, na kwamba bila kufanya hivyo, hawawezi kuishi.

Mwakilishi wa serikali na mwenyekiti wa kijiji walisema kuwa kijiji jirani hakina tatizo kama hili lililokuwa linawakabili. Waliuliza kwa nini.

Wanafunzi walipendekeza kuwa serikali itoe msaada wa kifedha kwa wachuuzi ili waanzishe maduka yao majumbani kwao, na kwa wakulima ili waajiri vibarua.

Wajumbe wengine waliona pendekezo la wanafunzi kuwa ni zuri, na wakalikubali.

Wanafunzi walirudi darasani kuchora picha ya mkutano wa viongozi wa jumuiya, wakizingatia makundi mbalimbali yaliyokuwa yamewakilishwa. Wanafunzi waliandika waliyojifunza kuhusu jinsi kila kikundi kilivyohusiana na kingine, na jinsi mahusiano yanavyoweza kukuzwa zaidi.

Nyenzo-rejea 6: Mwongozo wa kupanga shughuli yenye misingi ya kijumuiya

Nyenzo-rejea ya Mwalimu kwa ajili ya kupanga au kubadilisha na kutumia na wanafunzi

  • Bainisha suala la kijumuiya ambalo wanafunzi wako wanaweza kuzungumzia. Linahitaji kuwa na uhusiano na kujifunza kwao na liweze kusaidia jumuiya.

  • Bainisha watu katika jumuiya ambao watafanya kazi nao. Kama inawezekana, wadau hawa wawe na uzoevu wa kufanya kazi na watoto wa shule. Wanapaswa kuwa tayari kutoa mchango kwenye shughuli hii na kuwasaidia wanafunzi kwa kuwapa taarifa na mwongozo.

  • Panga namna na lini wana-jumuiya watashiriki, na washiriki na nani.

  • Panga jinsi utakavyoandaa wanafunzi kufanya shughuli hizi.

  • Panga jinsi utakavyozieleza shughuli kwa wanafunzi.

  • Amua jinsi utakavyowaangalia na kuwaongoza wanafunzi wako wakati wa hatua mbalimbali.

  • Sasa tekeleza shughuli na kisha fikiria iwapo imefanikiwa. Kama ungeifanya shughuli hii tena, ungebadili nini?

Sehemu ya 5: Njia za kudhibiti migogoro

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kudhibiti migogoro darasani kwako na kuwasaidia wanafunzi kukabili mafarakano?

Maneno muhimu: kazi za kikundi cha wawiliwawili; mbinu ya ufumbuzi wa tatizo; familia; kudhibiti mgogoro; jumuiya

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii , utakuwa umeweza:

  • Kukuza mbinu za kudhibiti migogoro darasani;

  • Kutumia kazi za wawiliwawili kubainisha sababu mbalimbali za migogoro na njia za kuitatua;

  • Kutumia mbinu ya ufumbuzi wa tatizo ili kusuluhisha migogoro.

Utangulizi

Kuweza kudhibiti tofauti za maoni na mgogoro ipasavyo ni muhimu kwetu sote. Sehemu hii ni utangulizi kuhusu dhana ya mgogoro kama ambavyo imeweza kutokea ndani ya:

  • Familia nyumbani;

  • Shule na darasani;

  • Jumuiya pana.

Tunabainisha baadhi ya sababu za migogoro na kuchunguza njia za kuidhibiti, na pia kufikiria njia za kuepuka migogoro. Kwa kuwa migogoro ndani ya darasa inaweza kuleta athari mbaya katika kujifunza, unahitaji kuimarisha mbinu za kupunguza migogoro darasani na kuboresha mazingira ambayo wanafunzi wako wote watayafurahia.

Somo la 1

Inawezekana wanafunzi wako wamekumbana na mgogoro ndani ya familia zao. Wanaweza kuwa wameshakuwa na ugomvi na kaka au dada zao; au kutokubaliana na wazazi wao. Wanaweza kuwa wameshashuhudia ugomvi baina ya ndugu wa familia zao, ukiwemo ugomvi baina ya mama na baba zao, na huu unaweza kuwa ni ugomvi wa maneno na pia mapigano.

Wanafunzi wanaweza kuwa hawahusiki moja kwa moja, lakini kama mwanafunzi anakumbana na mgogoro nyumbani, jambo hili linaweza kuathiri kusoma kwake kwa njia mbalimbali. Linaweza kuvuruga kule kujiamini na kujithamini kwake, anaweza kushindwa kumakinikia kazi yake na kuwafanya wakose raha na hatimaye kufadhaika.

Ni muhimu kwako kutambua jambo hili na kuwapatia wanafunzi wako msaada. Si mara zote itakuwa ni vizuri wewe kujihusisha na hali ya kifamilia, lakini, kama mwalimu wao, kuna mambo kadhaa ambayo unaweza kufanya ili kuwasaidia wanafunzi waendelee vizuri darasani. Kwanza, unaweza kulifanya darasa lako lisiwe katika mazingira ya migogoro ambapo wanafunzi watajiona kuwa wako salama na wanajiamini. Kwa kuanzisha kanuni za kimaadili za kupunguza migogoro, wanafunzi watakuwa na furaha pamoja na usalama.

Pili, unaweza kuwasaidia kihisia wale wanafunzi ambao wamekumbana na mgogoro nyumbani kwao. Msaada huu ni pamoja na wewe kuwa makini na hisia zao na kuhakikisha kuwa wanazungukwa na marafiki.

Tatu, unaweza kuwapatia wanafunzi stadi ili kuepuka migogoro wao kwa wao, na kupatana na kukomesha migogoro baina ya wengineShughuli hii inaweza kuwa changamoto, lakini ndiyo hasa itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Uchunguzi kifani ya 1: Kujadili mgogoro wa kifamilia

Bw. Okitiki nchini Afrika Kusini aliamua kujadili suala la mgogoro wa kifamilia na wanafunzi wake. Alisimulia hadithi sawa na ile iliyopo katika Nyenzo-rejea 1: Mgogoro wa kifamilia.

Aliwaambia wanafunzi wake wafikirie hadithi hii na kubainisha chanzo cha ugomvi huo. Aliwaambia wajadili, katika vikundi, jinsi ubishi ulivyotatuliwa. Baada ya dakika chache, walizungumzia ugomvi huo darasani. Wanafunzi walisema sababu za ugomvi zilikuwa: tabia ya kukopesha fedha kuwa ni tatizo; kwamba baba hakuwa na fedha za kutosha; kwamba mama hakutaka kumsikiliza;kwamba walikuwa hawawasiliani vizuri.

Waliamua kuwa masuluhisho yalipatikana kupitia njia zifuatazo: wanafunzi kuingilia kati;Mama kumsikiliza Baba na kusikia maelezo yake;Baba kumsikiliza Mama na kusikia maelezo yake;wote kusikia na kuelewa mtazamo wa kila mmoja.

Baada ya zoezi hili, Bw. Okitiki aliwapanga wanafunzi katika vikundi vya wanafunzi watatuwatatu ili kuigiza maigizo kifani yahusuyo hali ya mgogoro. Aliridhika na maigizo kifani wakati kila kikundi kilipowasilisha wiki iliyofuata. Kila igizo kifani lilijadiliwa na darasa zima, na walijifunza mengi kuhusu njia za kusuluhisha migogoro.

Shughuli ya 1: Kufasili Mgogoro

Ili kujua kile ambacho wanafunzi wako wanakijua wabunge bongo kuhusu mgogoro, uandike mawazo yao ubaoni au kwenye kipande cha karatasi. (tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia ramani za mawazo na kubunga bongo ili kutalii mawazo.)

Waambie wafikirie mazingira ya mgogoro ambayo nao walijikuta wamo, na, kila mmoja na mwenzake, wafikirie kuhusu maswali haya yafuatayo:

  • Watu wanagombania nini?

  • Nini sababu za ugomvi?

  • Je, kuna wakati mwingine ambao mnapigana?

  • Unapigana na nani?

  • Unapigania nini? Kwa nini?

  • Ugomvi unakufanya ujisikieje? Kwa nini?

  • Unamalizaje ugomvi wako?

Wahimize wanafunzi wafikirie kuhusu mazingira na tabia zao wenyewe. Waambie wanafunzi wawiliwawili waorodheshe mambo mbalimbali ambayo wangeweza kuyafanya ili kuepusha migogoro na familia au na rafiki. Kwa zamu kiulize kila kikundi moja kati ya mawazo yao na uyaandike ubaoni. Zungukia kila kikundi hadi urekodi majibu yote. Waulize wanafunzi: Yapi ni mawazo bora zaidi? Wangewezaje kuyatumia ili kuepusha au kutatua mgogoro?

Somo la 2

Unapokuwa na kundi kubwa la wanafunzi kwa pamoja, utakuwa na migogoro ya mara kwa mara itakayotokea baina yao. Hata hivyo, unaweza kupunguza uwezekano wa migogoro kwa kufanya jitihada ya kuwapatia wanafunzi wote mazingira yanayowasaidia. Mgogoro ukitokea ni vizuri sana kuutatua mapema iwezekanavyo. Huu ni wajibu wako kama mwalimu. Mgogoro ukiachwa bila kutatuliwa, unaweza:

  • kusababisha mazingira mabaya;

  • kuvuruga masomo ya kila mtu darasani;

  • kufanya darasa lisiwe mahali pazuri pa kukaa.

Mara nyingi, migogoro yo yote itakuwa baina ya wanafunzi wako, lakini lazima utambue pia kuwa mgogoro unaweza kuwa baina yako na mwanafunzi. Kwa sababu hii, unatakiwa uhakikisha kuwa kanuni nzuri za kimaadili pia zinakuhusu wewe. Jinsi unavyomwadhibu mwanafunzi lazima umwadhibu kwa kumheshimu mwanafunzi kwani kisichotakiwa ni tabia isiyopendeza ya huyo mwanafunzi na siyo mwanafunzi mwenyewe.

Ili kupunguza uwezekano wa mgogoro, lazima uweke kanuni wazi za mwenendo darasani, zinazohusu mahusiano ya kijamii na zinazohusu masomo. Kama wanafunzi watajua kutendeana vizuri, basi kutakuwa na uwezekano mdogo wa wao kupigana.

Pia ni lazima utambue tofauti kati ya wanafunzi wanaobishania hoja na wale wanaogombana au kupigana.

Njia rahisi kabisa ya kushughulikia mgogoro kwa haraka ni kuwatenganisha wale wanaohusika na kuwaweka sehemu tofauti za chumba. Lakini lazima upate sababu ya mgogoro wo wote ule. Waambie wanafunzi wakuelezee sababu za mgogoro. Tafuta suluhisho baina yao.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutatua mgogoro

Bibi Kweli ana wanafunzi wa darasa la Tano. Siku moja, aliwapanga kwenye vikundi vya watanowatano kwa ajili ya zoezi la kusoma na kuandika.

Aligundua kuwa wanafunzi wawili katika kikundi kimojawapo walikuwa wakisukumana. Ghafla waliacha, lakini pia waliacha kufanya kazi pamoja. Hii ilimaanisha kuwa wanafunzi wengine katika kikundi chao pia wasingeweza kufanya kazi vizuri, kwani kazi ilikuwa ni ya kikundi. Pia, wanafunzi katika vikundi vilivyokuwa pembeni/jirani vimekizungu kikundi hiki vilisumbuliwa na hali hii.

Kwa haraka Bibi Kweli alimaliza zoezi na kuanza kukagua majibu ya kila mwanafunzi. Kisha alimwambia wanafunzi wote wasimame, watembee na waunde vikundi vipya. Kwa njia hii aliwatenganisha bila tatizo.

Mwisho wa darasa, aliwaambia wale wanafunzi wawili wamwambie kuhusu ugomvi wao. Aligundua kuwa tatizo lilikuwa juu ya nani angesoma kitabu. Aliwaambia warejelee kanuni za darasa za ushirikiano na kuwaeleza kwa nini kanuni hizi ni muhimu kwa kila mtu. 

Pia aliwaambia wale wanafunzi wawili kwamba, waliwasumbua wanafunzi wengine, na kwamba wanatakiwa wawe makini. Aliwaambia wawe marafiki tena, na wakumbuke kwa nini walihitaji kushirikiana.

Shughuli ya 2: Wasilisho la darasa juu ya mgogoro

Wasaidie wanafunzi wako watalii zaidi kuhusu migogoro inayotokea shuleni.

Waambie wanafunzi, kwenye vikundi, kuorodhesha aina mbalimbali za migogoro inayotokea shuleni na kutoa mfano kwa kila mgogoro.

Kusanya mfano mmoja mmoja kutoka kila kikundi na uuandike ubaoni.Kiagize kila kikundi kuzungumzia kuhusu aina mojawapo ya mgogoro, kikibainisha: sababu za mgogoro;ungewezaje kuepukwa;ungewezaje kutatuliwa

Waambie watoe wasilisho kuhusu mawazo yao hayo mbele ya darasa. Baada ya kila wasilisho, viambie vikundi vingine viongezee mapendekezo yao ya njia za kutatua mgogoro.

Mwishoni, kiambie kila kikundi kiandike kwenye kadi njia bora za kuepuka aina ya mgogoro waliouchagua. Kusanya kadi hizi na kisha andaa onesho

Somo la 3

Kwa vikundi na watu wanaofanya kazi kwa pamoja, ni muhimu kukuza ufahamu wa nini kinachoweza kusababisha migogoro na jinsi ya kuiepuka.

Shule ni kitovu cha jumuiya yo yote ile, na walimu na wanafunzi huwakilisha sehemu zote za jumuiya hiyo. Kutokana na hili, shule ingeweza kuwa na.jukumu muhimu sana katika kuepusha au kutafuta suluhisho kwa migogoro mipana ya jumuiya.

Shule pia zinaweza kuwasaidia wanafunzi kufahamu zaidi juu ya vyanzo vya migogoro pamoja na masuala yanayoambatana na migogoro hiyo.

Baadhi ya wanafunzi wako wanaweza kuendelea na kuwa washiriki muhimu katika kusaidia katika migogoro inayohusiana na jumuiya.

Ili kuwasaidia wanafunzi wako wawe raia wanaojiamini unatakiwa:

  • uhakikishe darasa lako linakuwa na mazingira ya amani;

  • uwasaidie wanafunzi waelewe faida za kuwa na amani;

  • Uwapatie stadi za kusuluhisha migogoro.

Jambo muhimu ni kuwasaidia waelewe kuwa ni tabia mbaya isiyotakiwa na si yule mtu anayeifanya tabia hiyo.

Uchunguzi kifani ya 3: Kuwashirikisha wanafunzi katika kutafuta masuluhisho ya mgogoro wa kijumuiya

Abraham anafanya kazi katika shule iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Kulikuwa na mgogoro kati ya vijiji viwili vya jirani, Kitete na Mbulumbulu, uliohusu kugombania sehemu ya ardhi.

Mgogoro huu wakati mwingine ulisababisha matatizo shuleni, kwa sababu kuna wanafunzi walitokea katika vijiji hivi viwili na waliweza kuja shuleni baada ya kusikiliza watu vijijini kwao wakibishana.

Abraham aliamua kushughulikia tatizo hili pamoja na wanafunzi wake. Kwanza, aliwasaidia kubainisha mambo mbalimbali ambayo yanawaunganisha watu wa vijiji hivi viwili. Haya yanajumuisha: kwenda shule na kliniki moja; kutumia usafiri mmoja; kununua vitu katika soko moja.

Kisha aliwaambia wabainishe ni kitu gani ambacho kinakosekana kwa kila kijiji. Kitu kimoja ambacho wanafunzi walikibainisha ni uwanja wa mpira wa miguu pamoja na mchezo wa kukimbia.

Aliwauliza kama kulikuwapo na ardhi yo yote ili kuanzisha eneo la mpira wa miguu. Wanafunzi walipendekeza eneo lililokuwa katikati baina ya vijiji hivi.

Waliandaa wasilisho wakizungumzia sababu za kuhitaji uwanja wa michezo, na kwa nini eneo hili lilikuwa linafaa zaidi.

Walialika Chama cha Wazazi na Walimu (PTA) na kamati za vijiji ili wahudhurie, na baada ya wanafunzi kutoa wasilisho lao, watu walijadiliana.

Kamati zililikubali pendekezo. Vijiji vyote viwili vilipata uwanja wa michezo na jumuiya hizi mbili zilianza kushirikiana katika kujenga uwanja huo.

Shughuli muhimu: Migogoro ya kijamii

Kwa kazi ya nyumbani, waagize wanafunzi wako kila mmoja alete habari inayohusiana na mgogoro toka kwenye gazeti. Nyenzo-rejea 2: Mgogoro wa ng’ombe wasababisha mapambano makali inaonesha makala inayohusu mgogoro wa ardhi nchini Tanzania, lakini pia unaweza kutumia mifano tofauti.

  • Wanafunzi waelezane hadithi zao kwenye vikundi. Waambie wabainishe sababu za hiyo migogoro.

  • Waambie waangalie tena hizo habari na wapendekeze yapi yanaweza kuwa ni masuluhisho mbalimbali. Waambie waseme ni nani anawajibika kutafuta suluhisho.

  • Kisha, kiambie kila kikundi kichague habari moja na kiwasilishe mawazo yao juu ya kusuluhisha mgogoro huo darasani. Waambie wanafunzi wachangie katika mawasilisho ya wenzao na waseme kwa nini wanafikiri suluhisho lililopendekezwa linafaa au halifai.

  • Andaa orodha ya mapendekezo yaliyotolewa, na liambie darasa liandike kuhusu mapendekezo matatu watakayoyakumbuka na kuyatumia, na kwa nini.

Mapendekezo gani muhimu yaliyotolewa? Uliyataliije na wanafunzi?

Nyenzo-rejea 1: Mgogoro wa kifamilia

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili ya kupanga au kutohoa kwa matumizi na wanafunzi

Katika familia ya Kisongo, mume alikuwa akitoa fedha kwa ajili ya matumizi ya familia kila wiki. Siku moja, baba alimweleza mama kuwa hakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutoshelezea mahitaji yake. Mama hakutaka kumsikiliza baba. Alitoka chumbani kwa hasira na kubamiza mlango nyuma yake.

Asubuhi iliyofuata, hali ya nyumbani ilikuwa mbaya, kwani mama hakusikiliza maelezo ya baba. Baba aliendelea kujaribu kumweleza mama kwa nini hakuwa na fedha za kutosha, lakini mama hakumsikiliza.

Baada ya muda, baba aliwaomba watoto wazungumze na mama yao. Walifanya hivyo kwa kumwambia mama yao awe na subira. Mama aliwasikiliza na alikubali.

Mama alisikiliza kwa makini na alielewa kwa nini wiki hii baba hakuwa na fedha za kutosha – alilazimika kumkopesha kaka yake kiasi cha pesa kwa ajili ya kuwalipia watoto wake karo.

Mama aliposikia hivi, alilielewa tatizo lile. Lakini kwa upande wake, aliomba kwamba fedha kwa ajili ya chakula cha familia lazima zitengwe pembeni kabla ya kitu cho chote hakijatolewa kwa wengine, na pia ziongezwe kidogo ili kukidhi gharama za upandaji wa vyakula. Baba alikubali.

Hali ya wasiwasi nyumbani ilikwisha na kila mtu aliondoka nyumbani kwenda kwenye shughuli zake za kila siku akiwa na furaha. Mama alimkumbatia na kumbusu baba. Baba alitabasamu. Uhusiano uliokuwepo katika familia ulirudia kama kawaida

Nyenzo-rejea 2: Mgogoro wa ng’ombe wasababisha mapambano makali mwaka 2001’

Zaidi ya watu 400 wameyakimbia makazi yao Mashariki mwa Tanzania, mkoa wa Morogoro kwa kuogopa kuvamiwa na wafugaji wa Kimasai, baada ya mapambano ya kumwaga damu yaliyotokea tarehe 8 Desemba kati ya wafugaji na wakulima na kuacha watu 31 wengi wakiwa ni wanawake na watoto wakiwa wamekufa.

Mapambano kati ya Wamaasai wanaohamahama na wakulima mkoani Morogoro yalikuwa yakiendelea tangu mwishoni mwa Oktoba, lakini yalikuwa mabaya zaidi wakati wa siku nne za mapigano wiki iliyopita, Associated Press (AP) iliripoti siku ya Jumanne.

Associated Press ilisema kuwa shambulio la tarehe 8 Desemba lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa watu wawili wa kabila la Kimaasai na ng’ombe 35 ambako kulifanywa na wakulima. Mchanganyiko wa kulipiza kisasi pamoja na hasira kubwa ya kuchukuliwa mifugo yao kuliibua mgogoro mkubwa dhidi ya matumizi ya ardhi ambao haukuwa na suluhisho lililo wazi.

Gazeti la Kitanzania la Guardian toleo la Jumanne liliripoti kuwa mapigano yalianza baada ya wakulima wilayani Kilosa kuchukua kwa nguvu mifugo ambao walikuwa wakitangatanga mashambani mwao; wakulima walikuwa wakisubiri kulipwa fidia. Mazoea haya si mageni katika mkoa wa Morogoro, moja ya mikoa michache katika Tanzania isiyo na ukame sana, ambapo wafugaji na wakulima wanaishi pamoja. Kivutio cha ardhi ya malisho, kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, kimepelekea kuwepo kwa makundi ya mifugo ya Kimasai 250,000 katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Dk. E de Pauw, mshauri wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kwenye suala la matumizi ya ardhi aliliambia IRIN kwamba mgogoro umekuwa ukiendelea kwa miaka kumi hadi sasa. de Pauw alisema ‘Hakuna mpaka halisi unaotenga ardhi ya kilimo na ya ufugaji’. Alisema kuwa kutokana na wafugaji kumiliki idadi ya kutisha ya makundi ya ng’ombe kwa kule kulundikana kwao sana mkoani Morogoro, wanawachunga katika ardhi za kilimo, ama kwa kujua au kwa bahati mbaya, ambako kunachochea uhasama kwa upande wa wakulima.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la Afrika (PANA), serikali ya Rais Benjamin Mkapa imeweka nguvu mpya kwenye sekta ya mifugo. de Pauw alisema kuwa serikali imeunda sera ya kutenga maeneo ya wafugaji, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.

Wamaasai hufuata mtindo wa maisha wa nusu – unomadi wa kutoka eneo moja hadi jingine ili kutafuta malisho na maji. de Pauw aliliambia IRIN kuwa ‘Daima Wamasai wangependa kusaka ardhi bora [na] na hakuna wafugaji ambao wangependa kuwahamishia wanyama wao kwenye mikoa ambayo ina ukame. Mashindano ya kupata ardhi bora ni ya kuudhi hasa kipindi cha ukame.

Vyombo vya habari vya Tanzania vimeripoti kuwa sababu za kisiasa pia zinachangia katika tatizo hili. Gazeti la Guardian, toleo la Alhamisi, liliripoti kuwa wanavijiji wanadai kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO) ilikuwa imeshajua kuhusu huu mgogoro kati ya wafugaji wa Kimaasai na wakulima tangu mwaka 1997, wakati wawakilishi wa wakulima walipopeleka rufaa yao kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. Wanakijiji baadaye waliamua kuunda vikundi vya ulinzi wa jadi vilivyoitwa ‘sungusungu’.

‘Hata hivyo, sungusungu hawakufanya vizuri kwa sababu hawakupata ushirikiano wa polisi’, mwakilishi wa wakulima aliliambia The Guardian. Mkuu wa Wilaya wa Kilosa, Edith Tumbo, alisimamishwa kazi Jumatatu na Waziri Mkuu Frederick Sumaye, kwa mujibu wa Guardian.

Chanzo cha awali: EDC News 2001.