Ruka hadi kwa yaliyomo
Printable page generated Alhamisi, 12 Des 2024, 15:19
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Alhamisi, 12 Des 2024, 15:19

Namba ya moduli 3: Masuala ya Jumuiya na Uraia

Sehemu ya 1: Kubainisha uraia mwema

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kutumia njia mbalimbali za kuwahusisha wanafunzi ili kuendeleza welewa wao wa uraia?

Maneno muhimu: uendeshaji wa darasa; madarasa makubwa; kuthamini ujifunzaji; staid za kufikiri; uraia; haki; majukumu.     

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kukuza stadi zako ili kuweza kuhusisha maarifa ya awali ya wanafunzi na maarifa mapya kuhusu uraia;

  • Kutafuta mbinu nyingine za kuwasaidia wanafunzi ili wabaini majukumu ya jumuiya;

  • Umeandaa baraza la shule.

Utangulizi

Madarasa makubwa yana matatizo maalum kwa walimu - hasa kama yana mchanganyiko wa wanafunzi wa madarasa tofauti (tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kufanya kazi na madarasa makubwa na /au yenye mchanganyiko wa wanafunzi wa madarasa tofauti). Katika sehemu hii, tunatoa mapendekezo kuhusu kutumia mbinu tofauti za kuendesha darasa kwa ajili ya kuendeleza uelewa wa wanafunzi kuhusu uraia.

Kuwaelezea wanafunzi majukumu yao kama raia kuna athari ndogo kuliko kuwahusisha katika uzoefu hai. Sehemu hii inakusaidia kufikiria njia tofauti za kujua wanafunzi hao wanajua nini na kutumia ujuzi huo kuendeleza kuelewa kwao.

Somo la 1

Raia wote, pamoja na watoto, wana haki na majukumu, lakini yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Ili wanafunzi walielewe hili, wanahitaji kutambua haki na majukumu yana maana gani kwao. Wanahitaji kuelezana waliyoyatambua na kufikiria tofauti zao. Ili kutimiza hili, wanahitaji kuzungumza wakiwa darasa zima au wakiwa wawili wawili au wakiwa katika vikundi.

Uraia ni wazo gumu kwa wanafunzi wadogo na wanaweza wasilielewe mwanzoni. Ni vyema basi kulihusisha na kitu wanachokijua - kama kazi wanazozifanya wakiwa nyumbani. Kwa wanafunzi wakubwa, utaweza kutalii mada hii kwa undani na kuendeleza welewa wao kwa kufikiria wajibu na majukumu yao katika muktadha mpana zaidi wa jamii.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia makundi ya wanafunzi kama walivyokaa katika madawati kujadili haki na wajibu wa familia

Mwalimu Ngwinda ni mwalimu katika Shule ya Msingi Malbena katika jimbo la Eastern Cape Afrika ya kusini . Anafundisha darasa la 4 lenye wanafunzi 62 ambao hukaa katika vikundi vya wanafunzi watano watano wakizunguka madawati yao. Si rahisi kuwahamisha wanafunzi hao au kupangua madawati, kwa hiyo anatumia vikundi kufuata mpangilio wa madawati kujadili wajibu wa wanafunzi katika shughuli za nyumbani. Alitumia mbinu ya vikundi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi ya kuchangia mawazo yao.

Wakati wakijadili wajibu wao kwa muda wa dakika kumi, mwalimu Ngwinda huzunguka darasani akihakikisha kuwa hakuna anayetawala majadiliano na kukikumbusha kila kikundi kufikiria majukumu matatu ambayo watawaelezea wenzao.

Wanafunzi waliliona zoezi hili kuwa jepesi . Wakati wanafunzi wanawasilisha majibu yao mwalimu Ngwinda alikuwa anayaandika ubaoni. Anafurahishwa kuona kuwa wasichana wengi wanawasaidia mama zao majukumu ya nyumbani, kama kuosha vyombo na kupika na kuwaelea wadogo zao. Vijana wa kiume wanawasaidia baba zao na wajomba zao kuchanja kuni na kuchota maji, na wengine hufanya kazi katika bustani na mashambani. Walijadili mgawanyo wa kazi za nyumbani kwa msingi wa kijinsia.

Mwalimu Ngwinda aliwauliza kama wangesema mambo ambayo walikuwa huru kuyafanya katika familia zao. Wanafunzi waliliona zoezi hilo kuwa gumu, kwa hiyo aliwahimiza wajadili katika vikundi kabla ya kuwasilisha maoni yao. Mwalimu Ngwinda aliandika majibu yote ubaoni na kuwaeleza kuwa haya yote ambayo wako huru kuyafanya ni ‘haki’ yao. Alihakikisha wanaelewa tofauti kati ya wajibu na haki.

Tazama Nyenzo-rejea 1: Haki na wajibu wa watoto kwa ajili ya orodha ya haki na wajibu wa watoto nyumbani.

Shughuli ya 1: Vikundi vya wanafunzi wawili wawili kujadili haki na wajibu katika familia.

Waulize wanafunzi katika makundi yao ya wanafunzi wawili wawili, kujadili na kuorodhesha majukumu wanayopaswa kutekeleza nyumbani.

  • Baada ya dakika kumi kila kikundi , kwa zamu kieleze jukumu tofauti na uyaorodheshe majukumu yao ubaoni (wengi watakuwa na majukumu yanayofanana). Hakikisha kuwa wote wanaelewa kuwa haya ni majukumu yao. Mwambie kila mwanafunzi kurekodi orodha yao ya wajibu wao katika madaftari yao.

  • Baadaye, waulize wanafunzi katika makundi yao mambo ambayo wako huru kuyafanya katika familia zao (kama vile kusoma vitabu, kwenda kanisani/msikitini, kwenda shuleni, kucheza ndani au nje).

  • Orodhesha maoni yao ubaoni na talii welewa wao kuwa hizi ni ‘haki’ zao.

  • Watake kuorodhesha na kuchora mambo ambayo hupendelea sana kufanya -wajibu au haki. 

Je, umegundua kuwa kufanya kazi wawili wawili ni rahisi kutekeleza? Kama hivyo ndivyo, kwa nini? Kama sivyo, kwa nini?

Utabadilishaje shughuli hii ili kuiboresha wakati mwingine?

Maarifa na mawazo ya wanafunzi yanakushangaza?

Somo la 2

Sote huishi katika makundi au familia. Familia zetu ni sehemu ya makundi, kama vile vijiji au jamii. Ndani ya jamii tuna haki na wajibu. Hii maana yake ni kuwa inabidi kufanya mambo fulani ndani ya jamii na jamii lazima zifanye au zitufanyie mambo fulani. Nyenzo-rejea 2: Haki za mtoto itakusaidia kutayarisha mada hii.

Wanafunzi wanahitaji kukutana na wataalamu ambao wako tayari kuzungumza nao kuhusu maoni yao ya mada hii. Hii itawasaidia wanafunzi kuelewa wajibu wao katika jamii na kuwahamasisha kujifunza. Kabla ya mgeni kuja darasani kwako, ungependa kufikiria kupanga upya madawati ili kuifanya hali ya darasa kuwa vutivu. Hali hii itamfanya mgeni kujisikiavizuri na kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa sababu wanaweza kuona na kusikia vizuri zaidi. Kwa taarifa zaidi tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kuwatumia wageni kutoka kwenye jamii husika kama nyenzo.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutayarisha darasa ili kujadili majukumu ya jamii

Mwalimu Komba alitaka wanafunzi wake 48 wa darasa la nne kujadili kuhusu majukumu ya jamii. Aliamua kuwa jinsi darasa lilivyopangwa halisaidii kazi za majadiliano kwa hivyo alifanya mpango wa kurekebisha madawati yalivyopangwa.

Alijadiliana na mwalimu wake mkuu, ambaye alikubali mabadiliko hayo. Akisaidiwa na mwalimu mwenzake, aliunda makundi manane, kila moja likiwa na madawati matatu yaliyopangwa kukaliwa na wanafunzi sita. Kesho yake, wanafunzi walifurahi sana baada ya kuona mabadiliko ya darasa lao. Mwalimu Komba alieleza kuwa mpango wa darasa utawawezesha kuwa na majadiliano mengi zaidi.

Aliwataka wanafunzi wajadiliane, katika makundi yao, jamii inawapa nini - haki za watu wanaoishi katika jamii. Lakini kwanza aliwaeleza kuhusu kupeana zamu katika kujadiliana katika makundi yao na wasikilizane kwa kuheshimiana. Kila kundi lilitakiwa kutengeneza karatasi kubwa inayoonesha mambo mbalimbali yanayotolewa na jamii kama haki yao wakiwa wanajumuiya.

Wanafunzi wake walijua kuwa nao wana wajibu pamoja na haki. Hivyo, katika makundi yao walijadili wajibu wao katika jamii ni upi na baadaye waliandika maoni yao kwenye karatasi kwa rangi tofauti na kuonesha ufunguo. Makaratasi yote yalibandikwa ukutani ili makundi yaone maoni ya kila mmoja kabla ya kuwa na mjadala wa mwisho kuhusu ni maoni yapi yalikuwa yanaeleza haki na wajibu muhimu

Shughuli ya 2: Kuwatumia wataalamu kutoka katika jumuiya kuwahamasisha wanafunzi

Jadiliana na wanafunzi wako wajibu wao katika jamii.

Waongoze katika majadiliano yao kuhusu utunzaji wa mazingira, kuwaheshimu watu na mali, kusaidiana. Waweke wanafunzi katika makundi na watake wanafunzi kutengeneza karatasi kubwa (poster), andika shairi au hadithi au chora picha kuonesha maoni yao.

Jadili haki zao katika jamii- wasaidie waelewe kuwa wana haki ya kupata elimu, kupata huduma za afya, kuwa huru mitaani na mjumbani, na kutoa maoni yao.

Zungumzia viongozi na watu muhimu katika jumuiya. Orodhesha watu wote ambao wanasaidia katika jamii.

Amua ni yupi akaribishwe shuleni kuzungumzia kazi zake katika jamii. Anaweza kuwa kiongozi wa kijiji, kiongozi wa jamii, kiongozi wa siasa, nesi, mkutubi, afisa wa polisi au kiongozi wa dini.

Kwa msaada tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kuwatumia wanajamii kama nyenzo.

Baada ya ugeni, jadili na wanafunzi wako wamejifunza nini kuhusu kazi za mgeni.

Somo la 3

Ili kukubalika kuwa raia wa nchi yoyote unapaswa kuwa umekamilisha vigezo fulani. Vigezo hivi huandikwa katika katiba ya nchi. Jaribu kupata katiba ya nchi yako na zingatia inataja vigezo gani. Nyenzo-rejea 3: Nukuu kutoka katika Katiba inaorodhesha sifa za kuwa raia.

Njia mojawapo ya kutambua maoni ya wanafunzi wako kuhusu uraia imetolewa katika Uchunguzi Kifani 3.

Mabaraza ya shule yanaweza kuhitimisha mjadala kama njia mojawapo ya kuhamasisha wanafunzi. Namna ya kutayarisha baraza imeelezwa katika Shughuli muhimu.

Uchunguzi kifani ya 3: Ugeni wa kiongozi wa serikali za mitaa shuleni kujadili uraia

Mwalimu Notuka wa shule ndogo ya kijijini katika Tanzania, alimkaribisha Afisa wa Wilaya kutembelea darasa lake la tano lenye wanafunzi 56. Afisa huyo alileta picha ya rais, bendera ya taifa, nembo ya taifa, kitambulisho chake cha kazi na pasi ya kusafiria. Aliwaelezea wanafunzi umuhimu wa vitu hivi kwa Mtanzania. Alifafanua kila sehemu ya bendera inamaanisha nini. Waliimba pia wimbo wa taifa na kuorodhesha matukio yote ambayo wimbo huo huimbwa.

Baada ya ugeni huo, Mwalimu Natuko aliwapanga wanafunzi katika makundi madogo yanayozunguka madawati yao na kuwataka wajadili kwa nini ni muhimu kwao kuwa raia wa Tanzania. Alipitapita darasani na kuwaongoza wanafunzi wasijadili nje ya mada na kuorodhesha maoni ya kila mmoja.

Kisha aliwataka kila mmoja aandike maoni yake pekee katika vitabu vyao. Alikusanya kazi zao na aliweza kutathmini kila mmoja amejifunza nini kuhusu uraia.

Kuna wanafunzi watano ambao sababu zao hazikuendelezwa vizuri na Mwalimu Natuko alijadili sababu na wanafunzi hawa wakati wa mapumziko ili kuona kama wameelewa maoni hayo.

Shughuli muhimu: Kuwasilisha ujifunzaji katika baraza la shule

Zungumza na mwalimu mkuu kama unaweza kuwa na mkutano na baraza la shule kuhusu ‘Kuwa raia mwema’

Pamoja na darasa lako jadili maudhui ya baraza yatakuwa yapi

Kila kikundi kinatayarisha sehemu yake na nyenzo zitakiwazo. Itafaa uwashauri wanafunzi wako kuwa yafuatayo yanahitaji kuzingatiwa:

Raia ni nani?

Haki na wajibu nyumbani

Haki na wajibu katika jamii

Ishara za utaifa - bendera, wimbo wa taifa, kitambulisho, nembo, pasi ya kusafiria.

Kwa nini ni muhimu kuwa raia mwema?

Toa kazi mbalimbali na wape nafasi ya kujitayarisha - labda baada ya masomo kadhaa.

Ifanye kazi hiyo wazi, ili kila mwanafunzi aweze kutoa matokeo ambayo unaweza kuyatumia kutathmini ujifunzaji wao.

Wahamasishe waandike mashairi au aya za kusoma, kuchora bendera au tafuta aya ambayo wanapenda kusoma au kutumia.

Kubaliana na mtiririko wa uwasilishaji na fanya mazoezi.

Wasilisha baraza lako katika shule nzima

Baada ya hapo, jadiliana na wanafunzi yapi yamefanyika vizuri na yapi yangefanywa vizuri zaidi. Wana mawazo gani kuhusu jinsi shule nzima ilivyoelewa uraia –vizuri au vibaya?

Nyenzo-rejea ya 1: Haki na wajibu wa watoto- Orodha ya darasa ya mwalimu Nqwinda

Mifano ya kazi za wanafunzi

Wajibu wetu ni:Haki zetu ni:
Kusafisha nyumbaMalazi (nyumba ya kuishi)
Kuchanja kuni na kuchota majiChakula
Kuwalea wadogo zetuKulindwa (ili tusidhurike)
KupikaKulindwa na watu wazima
KulimaKutibiwa tukiwa wagonjwa
Kuwasikiliza na kuwatiiKwenda shule

Nyenzo-rejea ya 2: Haki za mtoto katika Tanzania

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Kwa kuzingatia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto ulioridhiwa mwaka 1991, haki za mtoto ni :

Mtoto katika Tanzania:

Anapaswa kuwa na haki sawa kama mtu mzima, bila kujali jinsia yake, dini, mila, kutoka vijijini au mijijini, uraia, kabila, jamii, hali ya ndoa ya wazazi wake au maoni.

Haki ya kukulia katika mazingira salama, uangalizi mzuri na mazingira salama, na kuwa na mahitaji ya msingi ya maisha, ikiwa ni pamoja na chakula, huduma za afya, mavazi na malazi.

Kuwa na jina na uraia.

Haki ya kujua wazazi wake ni nani na kufurahia maisha kuwa pamoja na familia au familia kubwa zaidi. Mahali ambapo mtoto hana familia au ameshindwa kuishi nao, basi anapaswa kupewa mbadala wa matunzo unaopatikana.

Haki ya kupewa kipaumbele katika mambo anayotaka katika uamuzi wowote uaofanywa kumhusu.

Haki ya kutoa maoni na kusikilizwa, na kushauriwa kwa kuzingatia welewa wake katika maamuzi ambayo yanamuathiri.

Haki ya kupata kinga ya afya yake kwa kupata chanjo na huduma nyingine za kiafya, na kufundishwa jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa. Anapokuwa mgonjwa, motto anapaswa kutibiwa kikamilifu.

Mtoto mlemavu ana haki ya kushughulikiwa kwa heshima kama watoto wengine na kupewa matunzo maalum, elimu na mafunzo panapohitajika ili kukuza kipaji chake na kujitegemea.

Haki ya kukataa kulazimishwa kuingizwa katika makundi ya kijamii na utamaduni ambayo yanaleta madhara (jando na unyago) ya kiafya.

Haki ya kutendewa kwa haki na kibinadamu katika mfumo wa sheria

Haki ya kulindwa dhidi ya aina zote za unyanyaswaji na unyonywaji.

Haki ya kupata elimu ya msingi.

Haki ya kupata burudani isiyo na madhara kimaadili; kushiriki katika michezo na shughuli za utamaduni chanya na sanaa.

Haki ya kutoajiriwa au kushiriki katika shughuli ambazo zinahatarisha maendeleo ya afya, elimu, akili, mwili na maadili

Mtoto, akiwa katika hali ya dharura ya kivita, mkimbizi au katika hali yoyote ya hatari, basi ana haki ya kuwa kati ya watu wa kwanza kuokolewa na kutunzwa.

Nyenzo-rejea 3: Nukuu kutoka katika Katiba: Sheria ya uraia ya ikionesha baadhi ya vigezo kwa wale ambao wana sifa za kuwa raia wa Tanzania.

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

SEHEMU YA II KUPATA URAIA SIKU YA AU KABLA YA SIKU YA MUUNGANO

4. Raia wa Tanzania bara na Zanzibar kabla ya siku ya Muungano anachukuliwa kuwa amekuwa raia wa Tanzania siku ya Muungano.

  1. Kila mtu ambaye, baada ya kuzaliwa Tanzania bara au Zanzibar kabla ya siku ya Muungano, alikuwa mara moja kabla ya siku ya Muungano raia wa Jamhuri ya Tanganyika au wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar atachukuliwa kuwa amekuwa, siku ya Muungano, na, kuanzia siku ya Muungano, kwa kuzingatia kifungu cha 30, kuwa ameendelea, na baada ya kuanza kwa sheria hii ataendelea, kuwa raia kwa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano

  2. Kila mtu, aliyezaliwa nje ya ama Tanzania bara au Zanzibar kabla ya siku ya Muungano, alikuwa mara moja kabla ya siku ya Muungano raia kwa kujiandikisha au kwa kuasiliwa na Jamhuri ya Tanganyika au wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar atachukuliwa kuwa amekuwa, siku ya Muungano, na, kuanzia siku ya Muungano, kwa kuzingatia kifungu cha 30, kuwa ameendelea,kuwa raia kwa kujiandikisha au vinginevyo, kwa kuasiliwa na Jamhuri ya Muungano, na baada ya kuanza kwa sheria hii ataendelea, kuwa raia kwa kuzaliwa, kwa kuasiliwa na Jamhuri ya Muungano, na baada ya kuanza kwa sheria hii atakuwa na ataendelea kuwa raia wa kuasiliwa wa Jamhuri ya Muungano.

  3. Kila mtu, aliyezaliwa nje ya ama Tanzania bara au Zanzibar kabla ya siku ya Muungano, alikuwa mara moja kabla ya siku ya Muungano raia kwa ukoo wa Jamhuri ya Tanganyika au wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar atachukuliwa kuwa amekuwa, siku ya Muungano, na, kuanzia siku ya Muungano, kwa kuzingatia kifungu cha 30, kuwa ameendelea kuwa raia kwa ukoo wa Jamhuri ya Muungano.

5. Watu waliozaliwa katika Jamhuri ya Muungano siku ya au baada ya siku ya Muungano

  1. Kwa kuzingatia sharti la kifungu kidogo cha (2), kila mtu aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya au baada ya siku ya Muungano atachukuliwa kuwa amekuwa na kuendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kuanzia siku ya kuzaliwa kwake, na kuanzia siku ya kuanzishwa kwa sheria hii atakuwa na kuendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 30.

  2. Mtu hatachukuliwa ni raia au kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa kifungu hiki kama wakati wa kuzaliwa kwake -

    • a.wazazi wake wote hawakuwa raia wa Jamhuri ya Muungano na baba yake, aliyeteuliwa kuwa mwakilishi, ana kinga ya madai na mchakato wa kisheria, ambayo hutolewa kwa mjumbe wa mamlaka ya nchi za nje, katika Jamhuri ya Muungano, au
    • b.mmojawapo wa wazazi wake ni adui na uzazi umetokea katika sehemu ambayo ilikuwa chini ya miliki ya adui.

6. Watu waliozaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano siku ya au baada ya siku ya Muungano

  1. Kila mtu aliyezaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano siku ya au baada ya siku ya Muungano atachukuliwa kuwa, kuanzia tarehe yake ya kuzaliwa, atachukuliwa kuwa na kuendelea kuwa, kwa kuzingatia mwanzo wa sheria hii atakuwa na kuendelea kuwa, raia wa Jamhuri ya Muungano ikiwa tarehe hiyo ya kuzaliwa kwake baba yake au mama yake ni au alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinginevyo licha ya ukoo, wa kuzingatia sharti la kifungu cha 30.

Sehemu ya 2: Njia za kuchunguza masuala ya kijinsia

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kutumia mikakati ya mtagusano kujadili masuala ya kijinsia?

Maneno muhimu: jinsia; igizo kifani; mitazamo pogofu; makundi ya jinsia moja; hojaji; wataalamu wa kijamii     

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • umechunguza mitazamo inayohusu jinsia kupitia shughuli za vikundi vya jinsia moja;

  • umetumia ‘igizo kifani kinyume’ kusisitizia mawazo pogofu kuhusu jinsia;

  • umetumia wataalamu wa kijamii na maonesho ya michezo ya kuigiza ili kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kijinsia.

Utangulizi

Kuna tabia fulani katika jamii ambazo mara nyingi huonekana kama ni faafu kwa ama wavulana au wasichana, lakini si kwa kila mmoja. Baadhi ya tabia hizi zinaweza kuwa na athari hasi katika hali za kujithamini na ari kwa wasichana na wavulana, na haitawafaa sana inapokuja kwenye ujifunzaji wa darasani. Watafiti wamegundua kwamba mara nyingi wasichana huona haya kuzungumza mbele ya darasa, na wakati mwingine hushindwa kujibu maswali, hata kama wanafahamu majibu.

Shughuli za sehemu hii zitakusaidia kuchunguza mawazo pogofu ya kijinsia pamoja na darasa lako, na kuyatazama majukumu ya kijinsia, yote mawili ya kiume na ya kike, kwa mtazamo chanya zaidi.

Nyenzo-rejea 1: Masuala ya kijinsia inatoa usuli kuhusu baadhi ya masuala yahusuyo jinsia.

Somo la 1

Mitazamo pogofu kuhusu jinsia, ingawa ni suala pana la kijamii, inaanzia nyumbani. Bila ya kuitambua, wazazi wengi katika familia zao huwatendea wavulana na wasichana namna tofauti –imeshakuwa kawaida kufanya namna hiyo; na wanaona hakuna sababu ya kubadili.

Matokeo yake, tabia hii yenye msimamo usiobadilika imesababisha, hususan kwa wasichana, kuamini kwamba hivi ‘ndivyo namna mambo yalivyo’ na hakuna chochote kinachoweza kufanyika hapo. Wavulana pia wanaikubali hali hii kwa sababu inaelekea kuwanufaisha.

Unaweza kuchunguza tofauti hizi pamoja na wanafunzi wako kwa kufanya kazi katika makundi ya jinsia moja ili kuwasaidia wanafunzi wako wazungumze kuhusu tabia na imani zao.

Katika Uchunguzi-kifani uliotangulia ( Moduli 2, Sehemu 2, Uchunguzi-kifani 2 ), mwalimu mmoja aliwaambia wanafunzi wake walete kanuni za familia darasani. Wakati walipoziwasilisha, darasa liliona kwamba kulikuwa na kanuni tofauti kati ya wavulana na wasichana. Mwalimu akaamua kuandaa masomo ya jinsia, baadaye katika muhula huo. Uchunguzi-kifani 1 unaonesha kilichotokea katika mojawapo kati ya masomo hayo.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia mchezo wa kuigiza ili kuchunguza masuala ya kijinsia

Mwalimu aliunda orodha ya kanuni za kifamilia toka katika somo lililopita. Alifikiria kuhusu namna ya kuchunguza masuala yanayojumuisha utendewaji tofauti kwa wavulana na wasichana katika familia, na aliamua kwamba mchezo wa kuigiza ungekuwa ni mbinu nzuri ya kufundishia. Angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumiaigizo-kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani kwa kupata mawazo.

Alilipanga darasa katika makundi ya ‘familia’ yenye ukubwa mbalimbali, huku wanafunzi wakiigiza nafasi mbalimbali za wanafamilia. Kundi moja lilikuwa na watu wane tu, kundi lingine lilikuwa na kumi na mmoja. Aliyaambia makundi yatunge mchezo unaohusu familia ili kuonesha jinsi wavulana na wasichana wanavyotendewa. Aliwapatia wanafunzi somo zima kuhusu mada hii na alizungukia kila kundi ili kuwasaidia na kuwapa moyo. Aliwauliza maswali kama ‘Kwa hiyo nini kitatokea baada ya hapo?’ ‘Unawezaje…?’

Aliwaagiza walete baadhi ya vitu ili kuweza kubainisha watu mbalimbali katika familia, na wafanye mazoezi ya michezo yao nyakati za mapumziko.

Katika vipindi vichache vilivyofuatia, kila kundi lilikuwa na zamu ya kufanya onesho la mchezo wao na baadaye darasa zima lilijadili wanayoyaona. Baada ya kutazama michezo yote na kuijadili, waligundua kwamba wasichana walikuwa na uhuru finyu zaidi wa kuchagua kuliko wavulana. Walipiga kura kuamua kama hali hii ni haki, na darasa lilikubali kwamba wavulana na wasichana lazima wapewe fursa sawa na wasinyimwe upataji wa shughuli na kazi kwa sababu za jinsia zao.

Shughuli ya 1: Kazi za makundi ya jinsia moja

Ili kuwasaidia wananfunzi wako kuchunguza na kufafanua hisia zao kuhusu majukumu ya kijinsia, shughuli hii inatumia makundi ya jinsia moja.

Andaa na wape hojaji katika Nyenzo-rejea 2: Jinsia –unafikiri nini? Kwa kila mwanafunzi na eleza kanuni kwa darasa zima.

Wape dakika kumi ili wakamilishe hojaji.

Kila mwanafunzi aoneshe majibu yake kwa jirani yake na wayajadili.

Panga darasa katika makundi ya jinsia moja ya kati ya wanafunzi watano na wanafunzi saba.

Kila kundi liandae orodha ya shughuli mbalimbali wanazozifanya:

katika siku za shule;

katika siku za wikiendi;

wakati wa likizo.

Makundi yawasilishe orodha ya shughuli zao –ambazo unaziandika ubaoni –kuunda orodha ya wasichana na nyingine ya wavulana.

Jadili orodha hizo pamoja na darasa. Uliza kuhusu usawa. Waulize kwa nini wanafikiri shughuli ziko tofauti.

Waambie wanafunzi waandike insha yenye kichwa ‘Ni kwa namna gani na kwa nini wasichana wanatofautiana na wavulana?’ Waambie watoe maoni yao wenyewe. Watoto wadogo wanaweza kuchora picha za shughuli wanazozifanya na kufanya ulinganifu miongoni mwao.

Somo la 2

Igizo kifani linaweza kuwa mbinu madhubuti sana katika kufundisha na kujifunza –hasa unaposhughulikia mada nyeti zinazohusu stadi za maisha au masomo ya uraia. Ni mbinu zinazofaa hasa unapochunguza masuala ya kijinsia pamoja na wanafunzi wako. Inaweza kuwasaidia wanafunzi kuzungumza kwa uhuru zaidi kwa sababu igizoni wanazungumza kuhusu tabia za watu wengine, na si tabia zao wenyewe. (Angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia igizo kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani .)

Ni muhimu kuchunguza mahali mtazamo pogofu kuhusu jinsia unapotokea. Wanafunzi wanahitaji kutambua ni wapi tabia ya mtazamo pogofu inashadidiwa. Mingi kati ya mitazamo hii inatokea katika familia, ni vema kuchunguza tabia yako mwenyewe. Je, unashadidia mitazamo pogofu ya kijinsia kwenye darasa lako? Je, mitazamo pogofu ya kijinsia ilishadidiwa kwenye familia yako mwenyewe? Uchunguzi-kifani 2 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyotumia uzoefu wake mwenyewe kuchunguza masuala ya kijinsia katika darasa lake.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia uzoefu wa utotoni katika kujadili jinsia

Bwana Awadh alitaka kufanya kazi na darasa lake kuhusu masuala ya kijinsia. Alitumia muda kutafakari kuhusu kitu cha kufanya. Alikumbuka kwamba alipokuwa mdogo, baba yake alikuwa akimwambia ‘tenda kama mwanaume’. Vilevile, anakumbuka kwamba dada zake wawili waligombezwa kwa ‘kutokuwa kama wanawake’. Aliamua kutumia mifano hii kutambulisha somo lake.

Aliandaa karatasi mbili zenye vichwa vya habari vifuatavyo: ‘Tenda kama mwanaume ’ na ‘Kuwa kama mwanamke’. Aliwaambia wavulana kueleza inamaanisha nini kutenda kama mwanaume. Wavulana walipomaliza kutoa mawazo yao, aliwauliza na wasichana. Alifanya hivyo hivyo kwa wasichana, akiwauliza wana maelezo au maneno gani wanaposikia mtu fulani anatenda kama mwanamke. Aliandika mawazo yao yote kwenye karatasi.

Alichora masanduku kuzunguka maneno fulani katika orodha zote mbili na akaeleza kwamba kuwa na tabia hizo kutazuia wanafunzi wanaotaka kufanikiwa. Walizungumza kuhusu jinsi ilivyo sawa kwa wavulana kupenda mitambo na michezo na kwa wasichana kupenda kupika na kutunza watoto, lakini tatizo linakuja tunapojihisi kuwa ni lazima tutimize majukumu haya ‘ili tukubalike’. Wasichana wengine wanaweza kutaka kufanya kazi za mitambo, n.k. na wavulana wengine wanaweza kutaka kutunza watoto au kuwa wapishi, lakini hawasemi wanavyotaka kwa sababu wanaweza kuchekwa.

Katika makundi madogo, wanafunzi walijadili kuhusu wakati walipojisikia kushurutishwa kutenda namna fulani ingawa wao hawakutaka. Walijadili kitu wanachoweza kufanya ili wakubalike kama walivyo, na pengine wafanye vitu tofauti na walivyofanya wazazi au walezi wao.

Shughuli ya 2: Igizo kifani kinyume

Katika shughuli hii, tunakutaka uandae maigizo kifani ambapo majukumu ya ‘kawaida’ yamebadilishwa (angalia Nyenzo-rejea 3: Igizo kifani kinyume kwa mfano). Hii itakusaidia kufikiri kuhusu mazingira mbalimbali ambamo unaweza kubadilishana nafasi kati ya majukumu ya kimapokeo yanayofanywa na wanaume na ya wanawake. Soma Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia igizo kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani .

Eleza darasa lako kuhusu shughuli hizi na madhumuni yake na kuhusu kutowacheka watu, bali kutafakari kuhusu masuala yanayoibuliwa wakati wakitazama. Baada ya kila igizo kifani, waambie wanafunzi wajadili, katika makundi ya jinsia changamano, maswali yafuatayo:

Unafikiri nini kuhusu hali hii? Ulijisikiaje ulipokuwa unaangalia igizo kifani hili, na kwa nini? Hisia zako zinaashiria nini kuhusiana na jinsi tunavyoyachukulia majukumu ya wanaume na wanawake katika jamii? Kama igizo kifani lingekuwa kinyume na lilivyooneshwa, je, ungejisikia tofauti?

Kama una wanafunzi wadogo, utatakiwa kuyafanya maigizo kifani yako rahisi kabisa. Vile vile, itakubidi baadaye, uwaongoze katika majadiliano yao, kuliko kuwaambia wajadili maswali katika vikundi.

Somo la 3

Kuna aina nyingi za tabia ya udhalilishaji na ni wanawake na watoto ambao mara nyingi ndio wahanga. Hii haina maana kwamba wavulana hawawezi kudhalilishwa pia; ni kwamba wasichana na wanawake wameelekea kuwa na majukumu hafifu katika jamii, wakati wanaume wamechukua yenye nguvu na madaraka zaidi.

Kama unataka kuchunguza sehemu hii pamoja na darasa lako, unahitaji kufanya maandalizi kwa uangalifu sana ili uweze kuwasaidia wanafunzi wako kwa vile baadhi ya hoja zinaweza kuwafanya wasijisikie vizuri na kuwasuta. Unaweza pia kukuta kwamba unatoa hadharani baadhi ya matukio ya udhalilishaji, ni lazima ujiandae kuwasaidia wanafunzi wako kwa umakinifu mkubwa wa namna ya kuzungumza na kwa uchaguzi mkubwa wa maneno ya kusema.

Unaweza kujiona hujitoshelezi kuzungumzia mada nyeti kama hii peke yako –hivyo unaweza kufuata mwongozo wa Bibi Umoru katika Uchunguzi-kifani 3 , ambaye alimwambia mtu mmoja toka Asasi isiyo ya Kiserikali ya kijamii kuja na kumsaidia kuendesha mjadala kuhusu udhalilishaji.

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia wataalamu wa kijamii katika kusaidia kujadili masuala nyeti

Kwa muda wa wiki kadhaa, darasa la V la Bibi Teri limekuwa likifanya kazi juu ya mitazamo pogofu kuhusu jinsia na jinsi inavyoweza kuathiri vibaya maendeleo ya msichana darasani na katika maisha. Ilikuwa wakati mgumu kwa Bibi Teri kwa sababu wavulana walijisikia hali ibaki hivyo ilivyokuwa na hawakuona kwamba kulikuwa na haja ya kuibadilisha.

Aliamua kupata msaada wa mtaalamu na akawasiliana na Asasi isiyo ya Kiserikali ya kijamii ambao walikuwa wakifanya kazi ya miradi ya maendeleo vijijini katika mji wao. Alikutana na mwanamke aliyeitwa Amina ambaye alikuwa mtaalamu wa jinsia.

Amina alikuja shuleni na alizungumza na darasa kuhusu udhalilishaji. Wanafunzi walitambua kwamba udhalilishaji unaweza kuwa wa kiakili, na vile vile wa kimwili na kijinsia. Amina alisimulia darasa kuhusu hadithi za vijana ambao wamedhalilishwa na wazazi wao, wanafamilia wengine, na hata watu kutoka katika makundi yao ya kidini. Alizungumza pia kuhusu njia ambazo wanafunzi hawa wamekuwa wakisaidiwa; na asasi ambazo ziko kwa ajili ya kuwasaidia watu. Maelezo yake yaliwafanya baadhi ya wanafunzi kuchukizwa sana kwamba watu wanaweza kuwa na tabia mbaya namna hiyo.

Wakati wa mazungumzo, Bibi Teri aliwaona wasichana wawili wakianza kulia. Baada ya ziara ya Amina, Bibi Teri aliwauliza wale wasichana wawili kama wangependa kwenda kuzungumza na Amina. Walikubali. Aliweka miadi ya Amina kukutana nao.

Katika somo lililofuatia, Bibi Teri aliwaambia wanafunzi wake waandike kuhusu udhalilishaji na waeleze hisia zao kuhusu tabia hiyo. Kutokana na zoezi hili, aliweza kuona ni kwa kiasi gani kila mwanafunzi alielewa, na aliweza kuona jinsi walivyoonesha hisia zao kutokana na hadithi za Amina.

Shughuli muhimu: Kuandaa tukio la shule kuhusu masuala ya kijinsia

Baada ya kuchunguza baadhi ya masuala darasani mwako kuhusiana na jinsia, toa pendekezo kwao kwamba wawaelimishe na wengine hapo shuleni kuhusu kile ambacho wao wamekipata.

Waulize watafanikishaje kazi hii. Wanaweza:

  • kutunga mchezo?

  • kufanya mhadhara?

  • kuandika habari hizi katika kitabu?

  • kuandika shairi?

Unaweza kufanya zaidi ya moja ya shughuli hizi ikiwa una darasa kubwa. Wanafunzi wanaweza kuchagua kikundi gani wajiunge nacho.

Mara watakapoamua nini cha kufanya, waambie wapange wanachotaka kukisema na kuchagua mbinu nzuri ya kukisema. Wakumbushe wawe makini na hadhira yao na wawe waangalifu kuhusu jinsi watakavyowasilisha mawazo yao.

Wape muda wa kuandika rasimu au kufanya mazoezi kuhusu wanachokifanya. Wakimaliza, waruhusu wawasilishe mchezo wao, kitabu, shairi au mhadhara mbele ya darasa, ili waweze kupata maoni faafu ambayo yatawawezesha kufanya marekebisho kabla hawajafanya onesho au uwasilishaji kamili mbele ya shule.

Baada ya tukio, wape wanafunzi wako fursa ya kutathmini athari ya tukio waliloonesha.

Tafakari jinsi utakavyowasaidia wanafunzi wako kuifanya kazi hii.

Nyenzo-rejea ya 1: Masuala ya kijinsia

Taarifa za msingi / welewa wa somo wa mwalimu

Jinsia inaeleza zile tabia za wanaume na wanawake ambazo zinatokana na shinikizo la kijamii na wala hazitokani na sababu za kimaumbile.

Hisia zilizooneshwa na wanafunzi wengi zilitokana na jinsi walivyolelewa kijamii, hali ambayo husababisha wawe na mtazamo pogofu wa kijinsia bila kujijua.

Kwa ujumla, katika familia wanaume huchukuliwa kama vichwa,na ufanyikaji wa maamuzi, kwa kiasi kikubwa, umetawaliwa na wanaume.

Kuna hali ya kutofautiana kabisa kijinsia katika upatikanaji wa elimu, fursa za kiuchumi na huduma za afya.

Kuna upendeleo wa kutoa elimu kwa wavulana, pamoja na masuala ya mimba za utotoni, matokeo yake ni kiwango kikubwa cha kuachishwa shule kwa wasichana.

Kuna hali ya kutolingana katika ajira kwa sekta na jinsia. Katika sekta ya kilimo, wanawake ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula.

Watu wanazaliwa kama wanawake au wanaume, lakini wanajifunza kuwa wasichana au wavulana ambao hukua na kuwa wanawake au wanaume.

Watu wanafundishwa tabia na mitazamo inayofaa, majukumu na shughuli zinazowastahili, na jinsi wanavyotakiwa kuhusiana na watu wengine. Tabia hii ya kujifunza ndiyo inayojenga utambulisho wa kijinsia na inayoamua kuhusu majukumu ya kijinsia.

Mambo ya kuzingatia katika ufundishaji wa jinsia

Masuala ya kijinsia ni nyeti hivyo kanuni lazima zidhibitiwe kwa msisitizo ili kuhakikisha kwamba mjadala haugeuki kuwa ugomvi kati ya wasichana na wavulana.

Unahitaji kusaidia jinsia zote kutambua vema mitanziko na nafasi za kuchagua walizonazo jinsia nyingine.

Ni muhimu kwa wanafunzi kuelewa jinsi mitazamo pogofu kuhusu jinsia inavyoshadidiwa na tabia za familia, shuleni na katika jamii.

Unatakiwa kuwasaidia wanafunzi wako kuunda mikakati na mbinu za kukabiliana na hali zisizosawa za kijinsia.

Nyenzo-rejea ya 2: Jinsia – unafikiri nini?

Matumizi ya mwanafunzi

Soma kila fungu la maelezo kisha chora kiduara kuzunguka tarakimu uliyochagua kuonesha ni kiasi gani unakubaliana au hukubaliani na maelezo.

5 inamaanisha unakubaliana kabisa.

1 inamaanisha hukubaliani kabisa.

Ikiwa huelewi chochote, unaweza kuzungushia 3.

aWavulana wana nguvu zaidi kuliko wasichana12345
bKupika ni kazi ya wasichana12345
cWasichana hawana muda wa kujisomea kwa sababu ya kazi zao za nyumbani12345
dWasichana huamka kabla ya wavulana12345
eShuleni, wasichana hufanya kazi nyingi kuliko wavulana12345
fWavulana wana akili zaidi kuliko wasichana12345
gElimu ni muhimu zaidi kwa wavulana kwa vile ni lazima wahudumie familia zao watakapokuwa wakubwa12345

Nyenzo-rejea 3: Igizo kifani kinyume

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

Bibi Mutiu amechelewa

Bwana Mutiu yuko kwenye hekaheka za kusafisha nyumba. Amembeba mtoto mgongoni kwa sababu mtoto haachi kulia. Anna, mwenye umri wa miaka mine, anamvuta Bwana Mutiu miguuni kwa sababu anataka kitu cha kula. Ni dhahiri Bwana Mutiu amechoka, lakini chakula cha jioni kinaiva katika moto mdogo. Anawaita watoto wakubwa nje waende kuongeza kuni. Anasema shida zake huku akiendelea na kazi. Ana wasiwasi kwamba chakula kinaweza kisitoshe mkewe atakaporudi nyumbani kutoka kazini kwenye baraza.

Bibi Mutiu anawasili nyumbani. Amekunywa kidogo na ana hasira kwa sababu chakula cha jioni hakiko tayari na nyumba si safi. Anamfokea Bwana Mutiu na wanakuwa na ugomvi, halafu Bibi Mutiu anampiga Bwana Mutiu na anatokomea nje ya nyumba akisema anakwenda kupata chakula chake cha jioni mahali pengine.

Sehemu ya 3: Kuchunguza kazi na ajira

Swali Lengwa muhimu: Njia mbalimbali za kuweka wanafunzi katika vikundi zita kuzaje welewa wa kazi na ajira?

Maneno muhimu: kazi za vikundi; ushirikiano; mdahalo; mazingira husika; kazi; ajira

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kutumia njia ya ‘fikiri-wawiliwawili-badilishana mawazo’ ili kuwasaidia wanafunzi wako kutambua umuhimu wa kazi nyumbani na katika jumuiya;

  • kuandaa shughuli za ubia na kutathimini ujifunzaji binafsi;

  • kutumia mazingira na nyenzo za mahali husika kuwahamasisha wanafunzi kuelewa juu ya kazi na ajira.

Utangulizi

Kuna tabia fulani katika jamii ambazo mara nyingi huonekana kama ni faafu kwa ama wavulana au wasichana, lakini si kwa kila mmoja. Baadhi ya tabia hizi zinaweza kuwa na athari hasi katika hali za kujithamini na ari kwa wasichana na wavulana, na haitawafaa sana inapokuja kwenye ujifunzaji wa darasani. Watafiti wamegundua kwamba mara nyingi wasichana huona haya kuzungumza mbele ya darasa, na wakati mwingine hushindwa kujibu maswali, hata kama wanafahamu majibu.

Shughuli za sehemu hii zitakusaidia kuchunguza mawazo pogofu ya kijinsia pamoja na darasa lako, na kuyatazama majukumu ya kijinsia, yote mawili ya kiume na ya kike, kwa mtazamo chanya zaidi.

Nyenzo-rejea 1: Masuala ya kijinsia inatoa usuli kuhusu baadhi ya masuala yahusuyo jinsia.

Somo la 1

Vijana na watu wazima hufanya shughuli mbalimbali kama kazi na ajira. Katika sehemu hii, tunapendekeza utumie mkabala wa ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kuwasaidia wanafunzi wako watalii maana na umuhimu wa kazi na ajira.

Kuchunguza ni wapi pesa inayotumika kununulia vitu nyumbani inakotoka ni mwanzo mzuri kwa mada hii.

Katika Shughuli 1 uwatake wanafunzi kufikiria aina mbalimbali za kazi na ajira katika jumuiya yenu na mjadili tofauti baina ya kazi na ajira. Uchunguzi kifani 1 unaonesha mawazo ya baadhi ya wanafunzi juu ya aina mbalimbali za ajira.

Uchunguzi kifani ya 1: Kikundi kikifanya kazi na mdahalo

Darasa la 5 la Bwana Petro huko Afrika Kusini lilikuwa likifanya kazi kwenye ajira mbalimbali nchini. Sasa alitaka wafanye kazi kwenye jumuiya ya mahali walipokuwa.

Bwana Petro aliligawa vikundi viwili. Alikitaka kikundi kimoja kubainisha waajiri wa mahali hapo na kuandaa hoja iungayo mkono kwa nini ni bora kuajiriwa. Alikitaka kikundi kingine kibainishe njia mbalimbali zisizo rasmi za kuchuma fedha na kiandae hoja iungayo mkono kwa nini ni bora kuchuma fedha kwa njia hii. Baada ya dakika 20 za maandalizi, kila kikundi kiliwasilisha orodha yake na Bwana Petro aliiandika ubaoni –akihakikisha kuwa harudii mawazo (tazama Nyenzo-rejea 1: Njia za kuchuma fedha kutoka kwenye orodha yao). Walijadili orodha hizi na kung’amua kuwa kazi ni ile ile katika baadhi ya mifano, iwe rasmi au si rasmi, iwe ya kulipwa au isiyo ya kulipwa.

Katika somo lililofuata, walifanya mdahalo, kila kundi likimteua msemaji kuwasilisha hoja yao. Mwishowe, walipiga kura kuhusu kama ajira rasmi au isiyo rasmi ni bora. Hata baada ya kupiga kura, wanafunzi waliendelea kujadili mawazo haya, jambo lililomfurahisha Bwana Petro.

Shughuli ya 1: Kutumia ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kutalii shughuli za kazi

Tumia mkabala wa ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kuwasaidia wanafunzi kutambua njia mbalimbali za kuchuma fedha na kutalii fursa za ajira za wanafunzi.

Uwatake wanafunzi kila mmoja afikirie njia mbalimbali zilizopo za kuchuma fedha. Mpatie kila mwanafunzi dakika tano.Kisha, waweke wawiliwawili kwa msingi wa ujirani na watake wabadilishane mawazo. (Kama wanafunzi wako wameketi watatuwatatu kwenye dawati, tumia kikundi cha watatu badala ya wawili). Wanaunganisha mawazo yao kufanya orodha ya wawiliwawili au watatuwatatu. Wape dakika kumi.

Kitake kila kikundi kiseme mawazo yao na kuyaorodhesha ubaoni.

Jadili tofauti baina ya kazi na ajira. Hakikisha wanaelewa kwamba watu lazima wafanye kazi majumbani na kwenye mashamba, na hili ni tofauti na kazi wanazofanya kama ajira ambazo ni za kulipwa. 

Watake wanafunzi wabadilishane mawazo jinsi wanavyotaka kufanya kazi katika siku za usoni.

Somo la 2

Kusikia kutoka kwa wengine kuhusu namna wanavyofanya shughuli zao mbalimbali kunaweza kuwasaidia wanafunzi wako kuelewa aina mbalimbali za kazi zilizopo na kazi gani wangependa wenyewe kufanya. Kukaribisha mgeni kuzungumza nao juu ya kazi wanayofanya kunaweza kusaidia wanafunzi kuelewa jinsi kazi mahususi inavyofanywa. Kuongea na wanafunzi nje ya shule kutawasisimua na kuwamotisha na kutilia uzito namna wanavyoziona kazi nyingi.

Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia jumuiya/mazingira ya mahali hapo kama nyenzo inatoa mwongozo kuhus kukaribisha wageni darasani kwako.

Uchunguzi kifani ya 2: Kuzungumzia kazi na ajira

Ili kuwasaidia wanafunzi wake kukuza dhana za kazi na ajira, na kuelewa umuhimu wa kazi, mwalimu wa darasa la 5 Bi. Maria alizungumza na wanafunzi juu ya kazi na siku za usoni. Aligundua kwamba wengi wa wanafunzi wake walitaka kwenda chuo kikuu ili waweze kupata kazi nzuri na kuchuma fedha nyingi. Wengi wao walitaka kuhamia jijini.

Kuwaonesha wanafunzi wake hali za maisha, Maria alimkaribisha mwuza duka wa mahali hapo aje shuleni kuwaeleza jinsi alivyoanzisha biashara yake. Walijifunza kwamba kuanzisha duka na kuliendesha ni kazi ngumu. Kunahitajika pia fedha; alipata mkopo kutoka serikalini kuanzisha bishara yake. Alikuwa karibu amalize kulipa mkopo huo na hivi punde atamiliki biashara yake.

Maria pia alimkaribisha rafiki yake, Jamila, ambaye aliishi kijijini kwao lakini akaenda kusoma chuo kikuu, na sasa alifanya kazi katika benki katika jiji. Jamila alieleza kuwa siku zote alitaka kufanya kazi katika benki na ilimpasa asome kwa juhudi ili aweze kuwa mhasibu.

Baada ya ugeni huo, darasa lilifanya mdahalo juu ya kama ni bora kubaki kijijini na kuendesha biashara yako au kwenda chuo kikuu na kupata kazi. Darasa lilijifunza mengi juu ya jinsi kazi na ajira vilivyohusiana na juhudi zao shuleni na katika jumuiya pana zaidi.

Shughuli ya 2: Kuzuru biashara ya mahali hapo

Lipeleke darasa lako (au katika vikundi vidogovidogo, kwa zamu) kwenye soko la mahali hapo na waache waone kinachotokea hapo. Waweke katika vikundi vya wawiliwawili kwa uangalifu kuhakikisha wanamakinika na shughuli hiyo na wasihangaike na mambo mengine wakiwa nje ya shule. Jitayarishe kwa shughuli hii kwa kupanga na wachuuzi wa sokoni kujibu maswali ya wanafunzi kuhusu biashara zao. Utahitaji kuandaa karatasi-kazi/hojaji kwa ajili ya wanafunzi wako (tazama Nyenzo-rejea 2: Karatasi-kazi ziara sokoni ). Kama huna nyenzo za kutengenezea karatasi-kazi, basi katika somo lililotangulia andika maswali ubaoni na wanafunzi wayanakili katika daftari zao –kwa kuacha nafasi kwa majibu watakayopata sokoni. Kadhalika, waulize wanafunzi wanachotaka kujua na ongeza maswali haya kwenye orodha.

Kama wadhani inafaa zaidi, unaweza kulipeleka darasa lako kwenye benki ya karibu au sehemu nyingine ya ajira, lakini utahitaji pia kupanga shughuli hii na kuwa na maswali au shughuli ambazo wanafunzi watafanya au kuuliza wakiwa huko. Baada ya ziara, wanafunzi wanaweza kuandika na/au kujadili waliyojifunza kuhusu kazi. Andaa muhtasari wa mawazo haya ubaoni.

Somo la 3

Katika shughuli zilizotangulia, wanafunzi wako wamejua zaidi kuhusu kazi na ajira kwa kazi za vikundi na pia wameelezwa uzoevu wa kimaisha wa watu walioajiriwa au wanaopata riziki.

Katika Shughuli Muhimu , unawapa wanafunzi fursa ya kuhusika katika kazi itakayopanua stadi zao na ambayo wanaweza kutumia ili kuchuma kipato.

Uchunguzi Kifani 3 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyoanzisha biashara ndogo ili kuwapatia wanafunziwake uzoevu wa kazi na ajira.

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia nyenzo za kienyeji zilizocheuzwa katika ushonaji na upataji wa kipato

Bibi Ngetu ni mwalimu wa mafunzo stadi wa shule ya msingi katika mji mdogo Tanzania. Karibu na shule kuna maduka matatu ya ushonaji. Eneo kuzungukia maduka ya ushonaji lilitapakaa vipande vidogovidogo vya nguo ambavyo mafundi ushonaji huvitupa. Bibi Ngetu na darasa lake waliwaza kwamba wangeweza kuvitumia vipande hivi kutengenezea vitu vya manufaa wakati wa masomo yao ya ushonaji. Aliwaomba mafundi ushonaji wamkusanyie vipande vyote vya nguo badala ya kuvitupa.

Bibi Ngetu alitumia vipande vya nguo kufundishia wanafunzi jinsi ya kushona. Walivikata, wakavipinda kwa unadhifu na kuvishona kutengeneza vitambaa vya mkono, skafu na vitambaa vidogo vya mezani. Kwa kuwa wanafunzi wengi hawakuwa na kitambaa cha mkono au skafu,

kila mwanafunzi alipewa kimoja. Vitambaa vya mkono na vitambaa vidogo vya mezani vilivyobaki viliuzwa kwa bei nafuu shuleni na kijijini.

Msichana na mvulana mmoja walichaguliwa kuweka rekodi ya kiasi cha fedha waliyolipwa. Walipaswa pia kulipia sindano na nyuzi walizotumia. Faida ilitumiwa kununulia sukari ya kutia katika uji wao. Wanafunzi walifurahi kwa sababu hapakuwa tena uchafuzi kutoka kwa mafundi ushonaji na sasa wanaweza kunywa uji wenye sukari.

Shughuli muhimu: Kuifanyia kazi shule yetu

Sasa ni wakati wa kuweka maarifa yote ya wanafunzi wako juu ya kazi na ajira kwenye jaribio kwa kufanya shughuli ambayo itanufaisha shule au nyumbani kwao.

Jadili na ubainishe shughuli ambazo wanaweza kuzifanya kama kazi-miradi ili ziwasaidie kukuza stadi, wakati huo huo zikiwa na manufaa kwa shule au nyumbani. Amueni pamoja mawazo mawili bora yanayoweza kutekelezwa. Mifano yaweza kuwa: kutengeneza vikapu, mikeka, kamba au fagio, au kukusanya mifuko na chupa za plastiki kwa ajili ya kuzicheuza. Aina ya shughuli itategemea mazingira ya shule.

Wanafunzi wanachagua kufanyia kazi mmojawapo wa miradi miwili iliyoteuliwa. Utahitaji kuwasaidia kupanga mradi na kukusanya nyenzo. Wataalamu wa mahali hapo na wana-jumuiya wanaweza kusaidia na kushauri juu ya nini cha kufanya.

Jadili na wanafunzi wanachoweza kufanya na mazao ya mradi wao (kama yanaweza kutumika shuleni, nyumbani au kuuzwa ili wachume fedha).

Jadili na wanafunzi manufaa ya miradi yao na stadi ambazo wamezipata.

Unaweza kutaka kupanga siku ya kuuza baadhi ya mazao na kutumia faida kununua vitu ambavyo vitalinufaisha darasa zima.

Waeleze wanafunzi kuwa shughuli wazifanyazo nyumbani na shuleni kama kazi zinaweza kuwasaidia kukuza stadi wanazoweza kutumia baadaye kupatia ajira.

Nyenzo-rejea ya 1: Njia za kuchuma fedha – Orodha ya darasa ya Bwana Petro

Mfano wa kazi ya wanafunzi

Njia rasmi za kuchuma fedha

  • Fanya kazi serikalini.

  • Fanya kazi kwenye kampuni.

  • Fanya kazi kwenye biashara ndogo ya mtu binafsi.

  • Endesha biashara yako.

  • Tengeneza vitu.

  • Fanya kazi kwenye AZAKI.

  • Fanya kazi kwenye kliniki.

  • Kuwa mwalimu.

  • Tengeza samani.

  • Fanya kazi kwenye gereji.

  • Kuwa fundi bomba.

Njia zisizo rasmi za kuchuma fedha

  • Uza vitu.

  • Panda vitu.

  • Uza chakula moto kwa wafanya kazi.

  • Shona.

  • Tengeneza magari.

  • Uchuuzi wa mitaani.

  • Kuwa mwelekezi wa mahali hapo.

  • Kuwa mtumishi wa nyumbani.

  • Kuwa mlima bustani.

Nyenzo-rejea ya 2: Karatasi-kazi kwa ajili ya ziara sokoni

1.Kuna magenge mangapi sokoni?

2.Mazao ya aina gani huuzwa huko?

3.Nani anamiliki/anasimamia soko?

4.Saa za kufungua soko ni zipi?

5.Soko jingine lililo karibu liko wapi?

Wanafunzi wanaweza kumuuliza mchuuzi mmoja:

1.Ulianzaje biashara yako?

2.Mazao unayouliza hutoka wapi?

3.Unakokotoaje bei zako za kuuzia

4.Unakokotoaje faida yako?

5.Unatumia usafiri gani kuja sokoni?

6.Kuna umbali gani kati ya soko na mahali unapoishi?

7.Tatizo kubwa kuliko yote kwa wachuuzi wa sokoni ni lipi?

Sehemu ya 4: Kutalii mazingira

Swali Lengwa muhimu: Utapataje takwimu ili kuendeleza ujifunzaji wa wanafunzi kuhusu mazingira

Maneno muhimu: mazingira, kukusanya data, tathmini, shajara, hadithi za maisha halisi.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kutumia hadithi halisi, umekusanya data na umeandika shajara ili kuendeleza welewa wa masuala ya mazingira;

  • Kupanga, kutekeleza na kutafakari utendaji kuhusu masuala ya mazingira;

  • Kutathmini ujifunzaji wa darasa na mafanikio ya mradi.

Utangulizi

Suala muhimu duniani ni athari za watu kuhusu mazingira. Tukit umia vibaya rasilimali na kuchafua mazingira kutakuwa na athari hasi kwa wanyama na mimea, na hivyo tutaifanya dunia iwe hatari kwa vizazi vijavyo.

Ukiwa mwalimu, na raia mwema, unahitaji kuelewa masuala ya mazingira na kuchukua hatua kama mfano kwa wanafunzi wako na kuwasaidia kuelewa masuala haya. Unaweza kufanya hivyo kwa kuwapa shughuli ambazo zinahusisha ukusanyaji wa taarifa kuhusu mazingira, katika sehemu zao au katika sehemu pana zaidi, na kutumia taarifa hizo kufikiria kuhusu matokeo ya matendo mbalimbali.

Somo la 1

Kujifunza baadhi ya dhana tata kuhusu mazingira kunakuhitaji wewe ukiwa mwalimu kuziweka dhana hizo katika vipengele vidogovidogo na kujenga picha kamili. Wanafunzi wanaelewa zaidi kama watafikiria juu ya mawazo wanayoyajua na kutumia mazingira yanayowazunguka kuwaonesha jinsi mawazo hayo yanavyohusiana na hali yao.

Kuna njia nyingi za kufanya hivi. Sehemu hii inatilia mkazo ukusanyaji wa taarifa kutokana na ujuzi wa wanafunzi kutalii dhana na majukumu na haki zao.

Uchunguzi kifani ya 1: Utafiti kuhusu matumizi ya maji katika jamii

Mwalimu Namhlane wa Nigeria alikuwa anaanza mada na wanafunzi wake wa darasa la pili, kuhusu mazingira akizingatia umuhimu wa maji katika maisha ya kila mmoja wetu.

Ili kuwahamasisha wanafunzi wake kuhusu mada hii, alianzisha mradi wa darasa. Kwanza, aliwataka waunde vikundi vya watu sita hadi wanane wanaoishi katika sehemu moja ya jamii na kuwaeleza kuwa kuna wageni watatu wanakuja shuleni siku inayofuata - mmoja akitoka kila sehemu ya jamii - ili kuzungumzia wanavyopata na kutumia maji. Aliwataka wanafunzi wake kufikiria na kuandika maswali watakayouliza. Makundi haya ya sehemu ya jamii yalishirikiana maswali yao ili kuhakikisha kuwa kila kikundi cha sehemu kingeweza kuona kama limefikiria vipengele vyote.

Kesho yake, kila mgeni alizungumza na wanafunzi wanaotoka katika sehemu yake ndani ya darasa au nje chini ya mwembe. Vikundi viliuliza maswali kwa njia tofauti - katika kikundi kimoja wanafunzi tofauti waliuliza swali moja kila mmoja, na katika kikundi kingine mvulana na msichana waliuliza maswali yote na waliobaki waliandika majibu.

Baada ya wageni kuondoka, wanafunzi walitakiwa kuorodhesha mambo matatu muhimu waliozingatia na kuwaelezea darasa zima. Mwalimu Namhlane alikitaka kila kikundi kwa zamu kuelezea walichogundua lakini bila kurudia jibu lililokwisha andikwa ubaoni.

Baada ya hapo walijadili matatizo yaliyokuwepo kuhusu maji na kufikiria jinsi ya kutatua. (Tazama Nyenzo - rejea 1: Matatizo ya kupata maji)..

Shughuli ya 1: Uwekaji wa kumbukumbu katika ‘shajara ya maji’

Watake wanafunzi wako kuweka kumbukumbu katika shajara kwa muda wa wiki moja. Wataandika (labda karatasi kubwa ya ukutani) kiasi cha maji wayatumiayo na kwa matumizi yapi (Tazama Nyenzo - rejea 2: Shajara ya matumizi ya maji kwa ajili ya kiolezo cha shajara).

Baada ya wiki moja, watake kufanya kazi katika vikundi na kuorodhesha katika yao matumizi yote ya maji na yaorodheshe kwa kuzingatia ni shughuli zipi zinatumia maji kwa wingi zaidi na zipi zinatumia maji kidogo. Bandika orodha hiyo ukutani na waruhusu kusoma kazi za wenzao kabla ya kuwa na majadiliano ya pamoja ya mwisho wakijadili masuala yahusuyo maji katika sehemu zao.

Itakuwa vyema kufikiria maswali kama: Maji yote yanapatikana kutoka wapi? Je, kila mmoja anapata maji? Je, maji yetu ni safi na salama? Huduma zetu za maji zinaweza kuboreshwaje? Tunaweza kusaidiaje?

Unaweza kuhusisha shughuli hii na kazi za tarakimu (kwa kuangalia data - kiasi cha maji kilichotumika), sayansi (kwa nini maji ni muhimu katika maisha yetu) na masomo ya jamii (matatizo ya kupata maji katika baadhi ya sehemu za Afrika).

Somo la 2

Kuchora ni njia nzuri ya kutambua mawazo ya wanafunzi kuhusu mada yoyote. Inawawezesha kuonesha mawazo yao bila kulazimika kuzungumza kwa sauti au kuweza kuandika. Ni njia nzuri kwa vijana wadogo na huwapatia njia ya kuzungumza maoni yao. Si lazima michoro iwe ya kiwango cha juu bali isimulie hadithi au ioneshe wazo. Kwa kutumia hadithi ni njia nyingine ya kuwaham asisha wanafunzi kufikiri kwa kina kuhusu tatizo. Inaondoa hali ya kumlenga mtu mmoja na badala yake inawawezesha wanafunzi kuzungumza kwa uwazi zaidi. Hadithi zinaweza pia kutoa taswira kubwa zaidi kwa wanafunzi na kuwahamasisha. Uchunguzi-kifani 2 na Shughuli ya 2 vinaonesha jinsi unavyoweza kutumia mbinu zote mbili katika darasa lako.

Uchunguzi kifani ya 2: Hadithi na masuala ya mazingira

Mwalimu Ngede aliwasomea wanafunzi wake Nyenzo-rejea 3: Hadithi ya mkulima mwenye ubinafsi ili kuhamasisha mawazo yao kuhusu ulimwengu na rasilimali zake.

Baada ya hapo aliwapa karatasi na kuwataka wachore picha ya ‘kwa nini mkulima alikuwa mbinafsi’.

Aliwaelezea wazo hili kwa makini na kuwahamasisha wasinakili, bali kufikiria juu ya mawazo yao. Baada ya wanafunzi kumaliza kuchora, walibandika picha zao ukutani. Mwalimu Ngede aliwataka baadhi ya wanafunzi kueleza picha zao zilihusu nini na alijaribu kukisia zingine zilihusu nini. Wanafunzi walifurahia sana zoezi hili.

Baadaye, aliongoza majadiliano kuhusu umuhimu wa kila mmoja kutunza ardhi. Waliorodhesha pamoja ubaoni jinsi watu katika jamii yao walivyotumia ardhi na jinsi walivyoitunza.

Baadaye aliwauliza maswali, ambayo waliyajadili katika vikundi. Kwa mfano:

Watu walitumiaje ardhi? Waliitunza? Ni kwa njia ipi mkulima angeitunza ardhi hii? Nani alifanya kazi? Je, ardhi ilikuwa na rutuba? Kama ndivyo kwa nini? Kama sivyo, kwa nini? Wanaweza kuboresha jinsi wanavyoitunza ardhi?

Mengi yanaweza kupatikana katika Nyenzo-rejea 4: Maswali kuhusu matumizi ya ardhi.

Kama darasa walifikiria maswali haya na kutoa mawazo yao.

Mwishoni mwa siku, Mwalimu Ngede aliwataka wanafunzi wakati wakiwa wanaelekea majumbani kwao waangalie njia mbalimbali za matumizi ya ardhi na kesho yake waje na mawazo yoyote ambayo yanaweza kuongezwa katika orodha yao.

Shughuli ya 2: Viongozi na mazingira

Shughuli hii inazingatia kwa upana zaidi umuhimu wa kutunza mazingira.

Nyenzo-rejea 5: Sebastian Chuwa anasimulia habari za Mtanzania mmoja aliyehamasisha jamii kujiunga pamoja kutatua matatizo ya mazingira. Soma habari hii kabla hujaanza kutayarisha somo.

Wasimulie habari hii wanafunzi wako. Andika ukutani tahajia za maneno, kwa mfano, ‘hifadhi’(ya mazingira).

Baada ya kusoma hadithi, jadili maneno hayo na maana zake.

Watake wanafunzi wako, wakiwa wawili wawili, wajifikirie kama Sebastian Chuwa. Ni masuala yapi ya mazingira ambayo wangependa kuyafanyia kazi? Wangefanyaje? Zunguka darasani na waulize wanafunzi walio katika vikundi vya watu wawiliwawili wenye mawazo mazuri kuyaeleza kwa wenzao darasani.

Watake wachunguze mazingira yao wakati wa kurejea nyumbani na waone kama kuna masuala mengine ambayo hawakuyaona kabla na wayazungumzie kesho yake. Orodhesha masuala matano wanayoyapendelea.

Somo la 3

Ukiwa mwalimu, unahitaji kuwasaidia wanafunzi wako kuelewa majukumu yao kuhusu mazingira katika hali ambayo inawahamasisha na kuendeleza mtazamo wa kuyatunza. Katika Shughuli Muhimu , bango linatumika kama kichocheo na katika Uchunguzi-kifani 3 , mradi mdogo umeelezwa ambao unaonesha jinsi vikundi tofauti vinavyoweza kushirikiana ili kuleta mabadiliko.

Wakati wanafunzi wanaendelea kushughulikia mradi huo, kazi yako ni kuwa umejitayarisha kutarajia baadhi ya mahitaji yao na kuwapa nyenzo ili kusaidia kujifunza kwao. Kama una darasa kubwa, unahitaji kufikiria jinsi utakavyowashirikisha wanafunzi wako wote na labda kugawanya kazi katika makundi. Kwa wanafunzi wa umri mdogo, utatakiwa kufanya shughuli za kiwango kidogo na washirikishe baadhi ya wanajamii wakusaidie zaidi.

Uchunguzi kifani ya 3: Upangaji na utekelezaji wa kampeni ya usafi

Darasa la shule ya Ngombe, Iringa, liliamua kampeni ya usafi. Mwalimu wao aitwaye mama Mboya amekuwa akiufanyia kazi mtaala mpana wenye kichwa cha habari ‘kulinda ardhi yetu’.

Baada ya kuzungukia shule asubuhi nzima na maeneo yanayoizunguka, Mwalimu Mboya na darasa lake walijadili waliyoyaona. Waliorodhesha mambo yote waliyoyapenda katika sehemu hizo na sehemu au mambo waliyotaka kubadili au kuboresha.

Waliamua kufanyia kazi sehemu ndogo mbili kwa kuzisafisha - uwanja wa shule wa michezo na kijito kilicho karibu na shule. Darasa liligawanywa katika makundi mawili yakiwa na timu mbili zikifanya kazi katika kila sehemu. Timu zilijadili wanachoweza kufanya halafu zilishirikiana mawazo na timu nyingine. Walikubaliana nani atafanya kazi gani na kila timu ilitekeleza mipango yake kwa muda wa juma zima, wakati wa saa za shule.

Darasa lilifanya usafi kwa muda wa wiki nzima. Baadaye walifanya maonesho katika ukumbi wa shule ambayo yalionesha:

Wingi na aina za takataka zilizokusanywa wakati wa kufanya usafi; Mipango ya kuendeleza hali ya usafi na kutokuwa na takataka katika siku zijazo; Jinsi ya kushughulikia takataka, ikiwa ni pamoja na kuzitumia tena kwa shughuli nyingine baada ya kuzipitisha katika mchakato mwingine au kuzifukia au kuzichoma;

Maonesho yalifanikiwa na wanafunzi wa madarasa mengine walifurahia kazi iliyofanywa na kusaidia kuweka shule safi zaidi.

Shughuli muhimu: Kuchukua hatua kuhusu masuala ya mazingira

Shughuli hii ni mwendelezo wa uhamasishwaji wa wanafunzi wa kushughulikia masuala ya takataka na inachukua mbinu ya hatua kwa hatua ya kujifunza kwa vitendo.

Hatua ya 1 –Watake wanafunzi (labda katika vikundi vya wawiliwawili) kutambua masuala ya takataka shuleni na karibu na shule. Chagua kipengele (labda kile kilichotajwa mara nyingi). 

Hatua ya 2 –Shirikiana na darasa kutayarisha ‘mpango wa utekelezaji’. Ili kufanya shughuli hii, kitake kila kikundi kupendekeza njia za kutatua matatizo. Hakikisha kuwa mpango wa utekezaji uliokubalika ni halisi na unaweza kutekelezwa na darasa. Wape wanafunzi katika vikundi kazi za kufanya. Uandike mpango wa utekelezaji katika bango likionesha mwisho wa utekelezaji, bango hilo linaweza kuwekwa katika ukuta wa darasa.

Hatua ya 3 –Chukua hatua: hii inaweza kuwa kazi ya siku au miezi mingi lakini hakikisha kuwa kila kikundi kinaweka kumbukumbu za kila wanachokifanya, lini na kwa utaratibu upi.

Hatua ya 4 –Wakiwa wanakamilisha kila sehemu ya mpango huo wa utekelezaji, watake warekodi maendeleo yao katika bango.

Hatua ya 5 –Wakati wakimalizia, tafakari mafanikio ya mpango pamoja na darasa. Wamejifunza nini? Kulikuwa na matatizo gani? Watafanya nini kuendeleza wazo hili? Je, sehemu imeendelea kuwa safi?

Nyenzo-rejea ya 1: Matatizo ya upatikanaji wa maji

Mfano wa kazi ya wanafunzi/Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

  • Umbali wa kusafiri/kutembea ili kupata maji.

  • Kuwaacha watoto wadogo nyumbani na kwenda kutafuta maji.

  • Wanafunzi kutokwenda shule kwa ajili ya kwenda kuchota maji.

  • Je, maji ni safi na salama?

  • Ujazo wa vyombo vya kuchotea maji na uzito wa kubeba kwa masafa marefu.

  • Muda unaotumika kutafuta maji unawazuia watu kufanya mambo mengine.

  • Maji yanayochotwa yanaweza kuwa yamechanganyika na uchafu na kutumiwa na wanyama.

  • Hatari ya maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na utumiaji wa maji machafu.

  • Ukame unaweza kukwamisha upatikanaji wa maji safi.

  • Ukosefu wa miundombinu k.v. mabomba na vyombo vya kuhifadhia maji yatokanayo na mvua, n.k.

  • Ukosefu wa mifumo ya kusafisha maji.

  • Ukosefu wa elimu kuhusu njia za kutumia na kutunza rasilimali asilia za maji/vyanzo vya maji.

  • Hakuna upatikanaji endelevu wa maji.

Nyenzo-rejea ya 2: Shajara ya matumizi ya maji

Matumizi ya wanafunzi

Kila wakati unapotumia maji kwa kunywa au kupikia, n.k. weka alama ya tiki katika kisanduku kinachostahili.

KunywaKupikiaKufuliaKusafishia nyumbaMengine
Jumatatu
Jumanne
Jumatano
Alhamisi
Ijumaa

Nyenzo-rejea 3: Hadithi ya mkulima mchoyo

Nyenzo rejea za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Kulikuwa na mkulima mmoja kijana. Alikuwa na mke na watoto wawili na waliishi katika kijiji kidogo. Mkulima alirithi shamba lake kutoka kwa babu yake aliyekuwa mchapakazi na ambaye alimpenda sana. Ingawa alikuwa na huzuni kwa kifo cha babu yake, mkulima aliridhika kwa kuwa mmiliki pekee wa ardhi yote.

Alikuwa ni kijana mchapakazi na aliweza kulitunza shamba vizuri, kama si vizuri zaidi, kuliko babu yake. Alijifunza mengi kutoka kwa babu yake lakini pia alijifunza vema shuleni na alisoma mambo mengi kuhusu njia mbalimbali za kuhifadhi maji na kutunza ardhi, jambo ambalo liliongeza mazao yake. Hata hivyo, hakuwa kama babu yake kwa kuwa hakuwagawia wakulima na wazalishaji wengine pale kijijini mawazo au mazao yake ya ziada.

Wanakijiji walishangaa walipokwenda kumwomba mbegu au ushauri kwa kuambiwa kwamba watoke katika ardhi yake. Mke wake hakupenda tabia hii lakini aliheshimu mawazo ya mumewe. Wanakijiji walitazama alichofanya na baadhi wakajaribu kuiga mambo aliyoyafanya bila kupata mafanikio makubwa. Wengine walicheka au kunung’unika kwa aliyoyafanya.

Wakati mmoja wa msimu wa kiangazi, mazao hayakustawi vizuri katika kijiji kile. Kulikuwa na maji kidogo kwa sababu kijito kilikauka hivyo kulikuwa na mwendo mrefu wa kilometa sita kuelekea kwenye chanzo kingine cha maji. Maana yake ni kwamba maji yaliyoletwa nyumbani yalitumika kwa kunywa tu.

Hata hivyo, mkulima mchoyo, alikuwa na maji na chakula kingi, lakini hakuwasaidia wanakijiji ambao walikuja kuomba msaada. Mkewe alimwomba awasaidie lakini hakubadili msimamo wake. Alitengeneza mifereji na kingo ili kukusanya maji ya mvua na aliyahifadhi katika mapipa makubwa ambayo alikuwa nayo. Kwa hiyo ukame ulipotokea aliweza kumwagilia mimea yake, ambayo ilikua vizuri kama kawaida.

Jinsi kulivyoendelea kuwa na joto na kiangazi kikali, mazao ya watu yalianza kufa na watu wengi wakapatwa na njaa. Mke alijaribu kumshawishi mumewe awasaidie wanakijiji. Watoto walijaribu kumshawishi baba yao, lakini hakuwasikiliza. Alisema alifanya kazi kwa bidii hivyo mazao ni mali yake, na wengine walikuwa wavivu au hawakuangalia yatakayotokea mbele.

Hata hivyo, siku moja, mtu aliyekonda sana na mwenye nguo zilizoraruka alifika shambani kuomba msaada wa chakula kwa ajili ya mke wake ambaye alikuwa mgonjwa. Mkulima alimfukuza kwa ukali lakini mke wake alimzuia na kusema: ‘Humtambui mpwa wako?’ Mkulima alipatwa na mshtuko kwa jinsi mpwa wake alivyoonekana amekonda na amezeeka. Mpwa alielezea jinsi alivyojaribu kutunza maji lakini alishindwa, na jinsi mazao yake yalivyokufa.

Mkulima akamweleza anachotakiwa kufanya wakati mwingine. Lakini mke wake akasema amedhoofika mno kiasi cha kushindwa kufanya hayo, vinginevyo umpe chakula yeye na mke wake. Mkulima alitulia na akampa mpwa wake chakula. Mpwa alirudi wiki iliyofuata akasema mkewe amepata nafuu na kuomba chakula zaidi. Mkulima alitaka kukataa, lakini mkewe akamwambia kwamba walikuwa na njaa sana kwa hiyo haikutosha kuwapa fungu moja tu la chakula. Mkulima aliwapa chakula, na katika kipindi cha siku chache zilizofuata, taratibu alibadilika mawazo yake baada ya kutafakari kuhusu uchoyo na utovu wa busara kuhusiana na kumbukumbu ya babu yake na shida ya majirani zake. Kwa hiyo aliwaita wanakijiji shambani kwake, akawagawia chakula na kuahidi kuwasaidia kujiandaa vizuri kwa ajili ya msimu ujao wa mazao.

Nyenzo-rejea 4: Maswali kuhusu utumizi wa ardhi

1.Ardhi inaweza kutumika kwa njia ngapi tofauti? Ziorodheshe.

2.Kwa nini ni muhimu kutunza ardhi?

3.Kwa nini watu wengine ni wachoyo zaidi kuliko wengine? Kwa nini ni lazima tugawane ardhi yetu?

4.Tunawezaje kuwahamasisha watu kuhusu tabia ya kugawana? Je, ni lazima tugawane kila kitu?

5.Je, tunatunza ardhi yetu vizuri?

6.Ni nani mwingine tunagawana naye ardhi yetu?

7.Ni kwa jinsi gani tunaweza kutunza ardhi yetu vizuri?

8.Sisi tukiwa wanadarasa, tunaweza kufanya nini ili tutunze ardhi ya shule?

Nyenzo-rejea 5: Sebastian Chuwa

Nyenzo rejea za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Sebastian Chuwa ni mtu mwenye ndoto kwa nchi yake, watu wake na vizazi vijavyo ambao watarithi urithi wao. Kwa miaka 30 amekuwa mstari wa mbele kusomea matatizo ya mazingira katika ardhi yake ya nyumbani Tanzania, Afrika ya Mashariki, na majawabu aliyoyapata yanatoa matokeo yanayonufaisha si ardhi peke yake, bali watu wote wanaotegemea ardhi kwa maisha na maendeleo yao. Mbinu zake ambazo zimejikita katika malengo ya msingi mawili ya uhamasishaji kwa vitendo katika jamii - kuratibu zoezi la watu kueleza matatizo yao katika ngazi ya mtaa, na elimu kwa vijana – ili kuhamasisha ufundishaji wa uhifadhi wa ardhi mashuleni, kuanzia ngazi ya shule za msingi.

Ametoa msukumo kwa makundi makubwa ya vijana wa kujitolea wa kijumuia kukaa pamoja na kutatua sio tu matatizo yao ya kimazingira, bali pia matatizo yao ya kupunguza umasikini, kuwawezesha wanawake na maendeleo ya vijana katika eneo la Mkoa wa Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania. Juhudi zake, kwa niaba ya shirika la African blackwood, zimeunda mpango wa kwanza wa kiwango cha juu wa kupanda upya wa spishi za mimea. Kwa sababu ya uanzishwaji wa bustani nyingi za miche ya miti za kijumuia na miradi kadhaa ya ushirika inayokusudia kuboresha kupanda upya kwa miti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, mwaka 2004 ABCP na makundi ya vijana walioshiriki katika kazi ya Sebastian, walisherehekea upandaji miti milioni moja.

Aina ya kazi yake, ambayo inapanuka kila wakati, imempa yeye na jumuia yake hadhi ya kuwa viongozi katika uwanja wa hifadhi ya Tanzania.

Historia ya Mradi wa Hifadhi wa African Blackwood (African Blackwood Conservation Project- ABCP)

Mwaka 1996, James Harris, mtaalamu wa kutengeneza mapambo kutoka Texas, USA, na Sebastian Chuwa walifadhili Mradi wa Hifadhi wa African Blackwood (ABCP), ili kuanzisha mpango wa elimu na upandaji upya wa miti, hasa kwa ajili ya spishi ya mmea uitwao mpingo (Dalbergia melanoxylon) katika eneo lake la nyumbani lililoko mashariki mwa Afrika. Mti wa mpingo unatumiwa sana na wachongaji wa Kiafrika na watengenezaji wa vifaa wa Ulaya kwa ajili ya kutengeneza zumari, filimbi, na vifaa vingi vingine vya muziki. Kwa sababu ya kuvunwa kupita kiasi, na kukosekana kwa juhudi zozote zinazoelekezwa kwenye kupanda upya kwa spishi hii, kuendelea kuwepo kwake kuko hatarini.

Mwaka1995, James Harris, ambaye anatumia mpingo katika sanaa zake za mikono, aliona filamu ya The Tree of Music huko Marekani na alidhamiria kufanya jambo kuhusiana na uhifadhi wa spishi hii. Aliwasiliana na Sebastian kwa barua pepe na alipendekeza washirikiane: angezindua mpango wa kuchangia mfuko miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa za miti, wanamuziki, wahifadhi misitu wa nchi za magharibi, na kisha kutuma fedha zitakazopatikana kwa Sebastian ili aanzishe bustani ya miti nchini Tanzania. Mradi uliidhinishwa na Bwana Chuwa kwa shauku kubwa. Tangu wakati wa mawasiliano hayo ya awali, ABCP imekuwa ndiyo nguvu inayoongoza uhifadhi wa mpingo kaskazini mwa Tanzania, inayofadhili bustani za mimea kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa miche ya mpingo na inayohamasisha kuhusu umuhimu wa spishi ya mpingo kimataifa.

Hifadhi ya Ngorongoro

*Kifaru mweusi huzuia magari barabarani katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Wakati wa utoto wake, nyumbani kwa Sebastian Chuwa kulikuwa kwenye mteremko wa kusini mwa Mlima Kilimanjaro katika kimo cha 4900’. Alijifunza kupenda mambo ya asili tangu utotoni kutoka kwa baba na mshauri wake, Michael Iwaku Chuwa, ambaye alikuwa mtaalamu wa mitishamba. Kwa pamoja walianzisha jitihada ya kusafiri na kufanya utafiti katika misitu ili kukusanya mimea ya madawa ambayo baba yake aliyatumia kwa kazi yake. Kutokana na safari hizi, katika kipindi cha miaka mingi alijifunza majina ya mimea na miti miongoni mwa mimea yote iliyosheheni katika eneo la Kilimanjaro. Upendo wake kwa dunia asilia unaendelea mpaka leo na ndio siri inayoongoza kazi yake.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alisoma katika Chuo cha Usimamizi wa Maliasili cha Mweka na baada ya kuhitimu aliajiriwa kama mhifadhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Katika kipindi cha miaka 17 cha ajira yake hapo, alijisomea na kuandika katalogi ya mimea ya sehemu ile, aligundua spishi mpya nne (ambazo kwa heshima yake, mbili kati ya hizo, zimeitwa jina lake) na amekusanya hodhimadawa ya mitishamba yenye aina 30,000 za mimea katika kituo cha wageni kwa ajili ya matumizi ya wageni na watumishi. Kwa sababu ya welewa wake mpana kuhusu mimea mingi ya eneo hilo, anafanya kazi na Mary Leakey katika eneo la jirani la Oldavai Gorge, kuitambua mimea kwenye eneo la ugunduzi wa mtu wa mwanzo la Leakey. Vile vile, katika Hifadhi ya Ngorongoro alianzisha mpango wa kuhifadhi vifaru weusi walio hatarini kutoweka; mpango ambao ulipata mafanikio. Mpango huu ulinakiliwa katika sehemu nyingine za Afrika.

Mbuga ya Ngorongoro ni eneo ambalo linasimamiwa kwa ushirika ambako jamii za Wamasai bado zinaishi na mifugo yao. Wakati wa kipindi chake cha ajira katika Mbuga, Sebastian alifanya kazi kwa karibu na Wamasai, akijifunza madawa yao na kuanzisha bustani za miti kwa ajili ya matumizi yao. Vile vile, alianzisha mpango wa kwanza wa elimu ya hifadhi ya misitu kwa vijana nchini Tanzania, hasa kwa ajili ya watoto wa Kimasai, uliohusu shughuli za kivitendo kama vile uanzishaji wa bustani za miche ya miti na miradi ya upandaji wa miti. Klabu hii ilifanikiwa sana hata ikiwa mfano kwa harakati za upandaji miti za nchi nzima; iliitwa Klabu ya Malihai ya Tanzania iliyoanzishwa mwaka 1985, ikiwa na ofisi katika Makao Makuu ya Mbuga ya Ngorongoro iliyoko Arusha; hivi sasa inafanya kazi nchi nzima na ina klabu zipatazo 1,000.

Ofisi na Tuzo

Mwaka 1999, Sebastian alitunukiwa wadhifa wa kuwa mwenyekiti wa Mfuko wa Dhamana ya Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira Kilimanjaro. na Mamlaka ya Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Ofisi hii, moja kwa moja inamfanya awe mjumbe wa Kamati ya Hifadhi ya Mazingira ya Mkoa. Kutokana na wadhifa huu, michango yake muhimu katika hifadhi ya mazingira itasambaa.

Imetoholewa kutoka: African Blackwood Conservation Project, Website

Sehemu ya 5: Mbinu makini za kukabili wu na ukimwi

Swali Lengwa muhimu: Utafundishaje mada nyeti kama VVU na UKIMWI katika mazingira chanya na yanayotia moyo?

Maneno muhimu: maandalizi; ujifunzaji changamfu; umakinifu; majaribio; igizo kifani; wu na ukimwi

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kujiandaa kwa kufundisha mada makini kama vile VVU na UKIMWI, kwa kutumia nyenzo-rejea mbalimbali; ikiwa ni pamoja na tovuti;

  • kutumia mbinu mbalimbali kama vile igizo kifani na wataalamu wa kijumuia ili kuhakikisha ujifunzaji changamfu unakuwepo;

  • kujenga mazingira makini ya kujifunza ili kukuza welewa wa VVU na UKIMWI.

Utangulizi

Ukiwa mwalimu wa shule ya msingi, utakuwa unafahamu kuhusu umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi wako kukabiliana na athari za VVU na UKIMWI katika maisha yao, kwa upande wa ujuzi kuhusu taarifa za VVU na UKIMWI, usalama wa afya zao wenyewe na afya za wengine.

Mada hii ni ngumu kuikabili kwa baadhi ya walimu na wanafunzi, na kwa sababu hiyo, walimu wengine hupendelea ‘kuwaachia wataalamu’. Hata hivyo, kuna njia mbalimbali ambazo unaweza kuunda mazingira makini ya ujifunzaji ili kuwasaidia wanafunzi wako kuchunguza mada hii ikiwa utaipanga kwa uangalifu. Sehemu hii itakusaidia kuandaa na kupanga matumizi ya nyenzo-rejea mbalimbali –walimu wenzako, wataalamu kutoka nje, maandiko na mtandao wa tovuti. Utakuza stadi za utumiaji wa igizo kifani katika ufundishaji wako kuhusu VVU na UKIMWI na kuunda kanuni za darasani ili kujenga mazingira yanayosaidia ujifunzaji. Sehemu hii haitoi kila kitu kinachohusiana na VVU na UKIMWI lakini inasaidia kuonesha mikabala unayoweza kuitumia.

Somo la 1

Huenda unakabiliwa na changamoto mbili mahsusi unapoandaa masomo ya VVU na UKIMWI. Ya kwanza ni kujiamini katika welewa wako na ya pili ni kwamba mada yenyewe ni nyeti na inaweza kuwa ngumu kuifundisha. Kama kuna shaka yoyote katika akili yako kuhusu kama elimu ya VVU na UKIMWI ifundishwe mashuleni au la, unatakiwa kujadili suala hilo na Mwalimu Mkuu wako. Hata hivyo, ni muhimu kwamba kila mtu afahamu kuhusu VVU na UKIMWI.

Ni muhimu sana ujiandae vizuri kabla hujaanza kuifundisha mada hii kwa wanafunzi wako. Lazima uzijue taarifa zinazohusika na ujiandae kujibu maswali ambayo yanaweza kuwa magumu kwako. Sehemu hii itakusaidia kujiandaa vizuri kwenye ufundishaji wa VVU na UKIMWI.

Aidha, ni lazima utafakari kuhusu wanafunzi kwenye darasa lako na jinsi gani kila mwanafunzi anaweza kuielewa mada hii. Utakachozungumzia, kwa kiasi kikubwa, kitatokana na umri wa wanafunzi wako na kwa kiasi gani unafikiri tayari wanafahamu kuhusu mada hii.

Uchunguzi kifani ya 1: Mpango wa kufundisha kuhusu VVU/UKIMWI

Bibi Shikongo wa nchini Tanzania alikuwa anajiandaa kufundisha Darasa lake la 4 kuhusu VVU na UKIMWI; na alikuwa amechanganyikiwa kidogo. Itakuwaje kama wanafunzi watamwuliza maswali ambayo atashindwa kuyajibu? Alifahamu ilikuwa ni muhimu kujiandaa vema na alitafakari kuhusu namna atakavyotekeleza jukumu hili. Aliandika madokezo ya mambo atakayohitaji kuyafanya.

  1. Kuzungumza na mwalimu wa Darasa la 5. Alihudhuria warsha ya VVU na UKIMWI iliyofanyika Nairobi. Uliza ikiwa ana madokezo yoyote ya warsha au nyenzo-rejea zozote ambazo zinaweza kuazimwa.
  2. Angalia katika maktaba ya shule ili kuona kama kuna vijarida vyovyote au habari nyingine za VVU/UKIMWI kwa ajili ya walimu na wanafunzi.
  3. Mwulize Mwalimu Mkuu kama kuna mwalimu mshauri wa VVU na UKIMWI katika sehemu yetu na wasiliana naye kwa ajili ya kupata taarifa za msingi.
  4. Chunguza kama kuna Asasi Zisizo za Kiserikali au kliniki zozote hapo mjini ambazo zina taarifa zinazohusiana na VVU na UKIMWI.
  5. Kusanya pamoja nyenzo-rejea, kisha panga muda wa kuzipitia na andaa madokezo kuhusu taarifa muhimu. Soma nyenzo-rejea huku ukizingatia umri wa wanafunzi wako na angalia kama unaweza kuzitumia.
  6. Tafakari jinsi ya kuwarahisishia wanafunzi wako kujifunza kuhusu mada hii na kuweza kuijadili kwa maoni yao wenyewe. Unawezaje kuhakikisha kwamba kujifunza kwao hakuzuiwi na aibu?
  7. Je, tunahitaji ‘kanuni’ maalum ambazo tutazitumia kujadili mada makini kama hii?

Fikiria jinsi ya kutathmini ni kwa kiasi gani wanafunzi wamejifunza.

Baada ya kumaliza maandalizi yake, Bibi Shikongo alifundisha somo lake la kwanza kuhusu VVU na UKIMWI. Darasa lake lilichanganyikiwa mwanzoni lakini jinsi darasa lilivyokuwa likiendelea wanafunzi walisikiliza na kushiriki vizuri. Wengi kati yao walizungumza kuhusu somo hilo wakati wa mapumziko. Wengine walimwuliza maswali ambayo alisema angeyajibu kwenye kipindi kitakachofuata

Shughuli ya 1: Maandalizi ya kufundisha VVU na UKIMWI

Jiandae kwa kutafiti taarifa zihusuzo VVU na UKIMWI na kutafakari kuhusu namna utakavyozifundisha kwa wanafunzi wako. (Tazama Nyenzo-rejea 1: VVU na UKIMWI katika Afrika kwa taarifa na mitandao faafu ya tovuti unayoweza kuitumia.)

Andika madokezo, ukitafakari kuhusu mambo yafuatayo:

Wasiliana na Mwalimu wako Mkuu kama anaridhia ufanye somo hili.

Utapata wapi taarifa?

Kuna mtu anayehusika na nyenzo-rejea katika shule yako? Mji? Wilaya?

Kuna Asasi Zisizo za Kiserikali au vituo vya afya vinavyoshughulika na elimu kuhusu VVU na UKIMWI?

Ni kwa namna gani utakusanya taarifa hizi?

Utaamuaje kuwa taarifa zipi zinawafaa wanafunzi wako?

Tafakari kuhusu umri wa wanafunzi na ukubwa wa darasa.

Ni jinsi gani utalipanga darasa na wanafunzi wako?

Je, wanafunzi wako wangefaidika kwa kuwa na mtaalamu wa kijumuia ambaye anakuja na kuzungumza nao ili kuendeleza ulichokiandaa kwa darasa lako? Wataalamu waje mwanzoni mwa kazi hii au baadaye?

Unaweza kupata nyenzo-rejea gani nyingine? Je, kuna chumba cha kompyuta katika shule yako ambako darasa linaweza kuunganishwa kwenye mtandao wa tovuti au ambako unaweza kukusanya taarifa?

Je, kuna wanafunzi wowote ambao wanaweza kuonesha hisia kali dhidi ya mada hii? Utakabiliana vipi na tofauti za uoneshaji wa hisia?

Panga utangulizi wa somo lako.

Somo la 2

Nidhamu ni muhimu kwa kila darasa. Hata hivyo, mada ya VVU na UKIMWI inaweza kuwafanya wanafunzi wakaipokea tofauti na jinsi wanavyokuwa katika masomo mengine. Katika Moduli 1, Sehemu ya 4 uliunda kanuni za darasa. Unaweza kukuta kuwa unatakiwa kupanua kanuni hizo ili kuruhusu majadiliano ya wazi kuhusu VVU na UKIMWI pamoja na tendo la kujamiiana. Kujadiliana na darasa lako sababu za kuhitaji kanuni maalumu na kuwaambia wanafunzi wapendekeze hizo kanuni wao wenyewe inaweza kuwa ni mwongozo wa kukusaidia katika mada yako.

Nyenzo-rejea 2: Hali ya darasa inakupa miongozo ya jinsi ya kuhakikisha kuwa darasa linakuwa na mazingira yanayowaruhusu wanafunzi wako kuweza kutalii mada ya VVU/UKIMWI.

Uchunguzi kifani ya 2: Kushughulika na wanafunzi watundu/wakorofi darasani

Twambo alikuwa amechoka sana - siku ilikuwa imeshakuwa ngumu. Yeye ni mwalimu mwanafunzi wa mazoezi ya ualimu katika shule ya msingi Bulongwa na mkaguzi wake alimwambia afundishe baadhi ya masomo juu ya VVU na UKIMWI kwa darasa la Nne, Tano na Sita. Alikuwa hajiamini sana.

Walikuwa wameshapewa vipindi vichache vya VVU/UKIMWI chuoni (angalia Nyenzo-rejea 2), ambayo ilimsaidia Twambo kujiandaa. Alikuwa anajiamini kuhusu kufanya kazi na wanafunzi wadogo, lakini alikuwa na tatizo kubwa na darasa la sita. Katika darasa hili kuna wavulana wengi wakubwa na Twambo alikuwa na uhakika kuwa wangeingilia kati masomo hayo.

Twambo alikuwa sahihi; kwani alikuwa tu ndiyo ameanza somo la kwanza wakati Thomas alipoanza kumwuliza maswali kuhusiana na maisha yake mwenyewe ya kimapenzi. Kwanza Twambo alishtuka, lakini akawahi kwa kumwambia Thomas kuwa asiwe mbinafsi na akaendelea na somo. Baadaye, kwenye kazi ya kikundi darasa lilikuwa na vurugu na makelele yaliyoambatana na kicheko na yule mshauri/mkaguzi wake akawa amekuja kuangalia kelele hizo zilikuwa zinahusu nini.

Twambo alikivunja kile kikundi cha wavulana wenye kelele, lakini wakati walipokuwa wanatoa maelezo Thomas na rafiki zake waliendelea bado kuelezea kwa uwazi mambo ya ngono hata kuwachekesha wanafunzi darasani na kumfanya Twambo atahayari. Twambo aliwakumbusha wanafunzi kanuni za darasa na alisema kuwa walikuwa kwenye hatari ya kutoshiriki kama wakikosa nidhamu. Aliweza kwenda nao vizuri kwa kutotilia maanani hoja zao nyingi au kwa kubadilisha hoja zao ili kueleza pointi ya ukweli. Lakini hali ilikuwa imeshachosha sana na kengele ya

kwenda nyumbani ilipogongwa Twambo alifurahi. Kipindi kingine kabla ya kuanza somo aliongea na wavulana hawa kuhusu heshima na kile ambacho angekifanya kama wangekosa adabu. Twambo alijaribu kuwasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa mada.

Shughuli ya 2: Kujenga mazingira yanayoruhusu kujifunza

Kwanza soma Nyenzo-rejea 2

Kuwaandaa wanafunzi wako na pia kujiandaa wewe mwenyewe ni sehemu ya maandalizi yako ya kufundisha darasa lako kuhusu VVU na UKIMWI. Hapo awali ulijifunza kuhusu kuunda kanuni za darasa za kusaidia ujifunzaji kwa ufanisi kwenye mada ambazo ni nyeti. Sasa unahitaji kufanya mambo yafuatayo na darasa lako.

Eleza darasani kwamba mtafanya kazi chache juu ya VVU na UKIMWI.

Durusu kanuni za darasa mlizonazo kwa kuligawa darasa kwenye vikundi ili kujadili kama kanuni hizi zinafaa.

Kiambie kila kikundi kifikirie kanuni za ziada zisizozidi tatu ambazo wanakikundi wangependa ziwepo wakati wa kufanya kazi hii. 

Kila kikundi kipendekeze kanuni zake za nyongeza , na kuziandika ubaoni.

Kama darasa, kubalianeni juu ya kanuni za nyongeza mnazozitaka.

Jadili kanuni zote na darasa, zikiwemo zile kanuni mpya, na hakikisha kuwa kila mmoja anaelewa vizuri sababu za kanuni hizi kuhitajika kwenye mada hii.

Utafanya nini iwapo watazipuuzia kanuni hizi? Kubalianeni na darasa lako kuhusu mipaka au vizuizi gani utakavyotumia.

Somo la 3

Iwapo wanafunzi wanatakiwa kujifunza kwa kuchangamka, basi wanatakiwa wawe wamechangamka ama kimwili au kiakili au vyote viwili! Kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia katika kuhamasisha kujifunza kwa uchangamfu ili kuhakikisha wanafunzi wako wanafaidika katika masomo yao. Kuhusu ni njia gani unazozitumia kufundisha juu ya VVU na UKIMWI kutategemea sana ukubwa wa darasa lako na umri wa wanafunzi wako –na kile unachokijua kuhusiana na njia hiyo ya kujifunzia wanayoipendelea.

Unajua kuwa igizo ni mbinu nzuri ya kutumia katika kuwasaidia wanafunzi kujadili mada ambazo ni nyeti. Kwenye masomo ya VVU na UKIMWI, itawafanya wanafunzi wajadili hali ambazo siyo zao lakini kwa kutafakari jinsi ambavyo hali hizi zinavyohusiana na uzoevu wao wenyewe. Njia hii inatumika kwenye Shughuli Muhimu.

Njia nyingine inayofaa ni jaribio (angalia Nyenzo-rejea 3: Jaribio kuhusu VVU na UKIMWI ). Katika Uchunguzi-kifani 3 , mwalimu mmoja anatumia, jaribio kama shughuli ili kujua ni kwa kiasi gani darasa lake la msingi linavyojua kuhusu VVU na UKIMWI.

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia jaribio kama shughuli ya kujifunzia kuhusu VVU na UKIMWI.

Maria alitumia mtandao ili kujiandaa kwa ajili ya kufanya kazi na wanafunzi wake juu ya VVU na UKIMWI. Ana bahati kwani anaongeza uwezo wake wa kufundisha kwa njia ya elimu ya masafa na anaruhusiwa kutumia chumba cha kompyuta kilichopo katika kituo cha kujifunzia. Alipata tovuti iliyoorodheshwa kwenye Nyenzo-rejea 1 na aliamua kujaribu moja ya shughuli zilizopatikana pale kwenye tovuti. Shughuli hii imepangwa kwenye Nyenzo-rejea 4: Uambukizo. Maria alifuata maelekezo na aligundua kuwa njia hii ilimsaidia sana katika kujua baadhi ya mitazamo potofu waliyokuwa nayo wanafunzi wake kuhusu VVU na UKIMWI. Pia alikuta kwamba njia hii inachukua muda mrefu sana kwa darasa lake kubwa lenye wanafunzi 56, ila alipoitumia kwa mara ya kwanza ilikuwa ni kero kidogo.

Hivyo, kipindi kilichofuata, aliligawa darasa lake katika vikundi viwili na akawa na kikundi kimoja kinachoandika kuhusu vitu walivyovijua au walivyovifikiria kuwa walivifanya kuhusiana na VVU na UKIMWI wakati wengine walikuwa wanafanya shughuli. Somo lililofuata vikundi vilibadilishana. Katikati ya masomo aliweza kutafakari kuhusu kile ambacho wanafunzi walikuwa tayari wanakijua au kufikiri kuwa walikuwa wameshakijua kuhusu VVU na UKIMWI na hii ilimsaidia Maria kupanga somo lililofuata.

Shughuli muhimu: Igizo-kifani kwa ajili ya masomo yanayohusu VVU na UKIMWI

Panga igizo kwa ajili ya baadhi ya masomo yanayohusu mada za VVU na UKIMWI (angalia Nyenzo-rejea 5: Igizo-kifani kwa ajili ya masomo ya VVU na UKIMWI) ambayo yanaendana na umri wa wanafunzi wako. Kama wanajihusisha na ngono, unaweza kulenga kwenye kuzuia. Hapa pana mifano ya vipengele vya kutumia:

  • John anasema kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Mary. Kwenye miadi, wakiwa wenyewe, John anajaribu kumshawishi Mary afanye naye mapenzi.

  • Angela, msichana mzuri na mjanja, hana vitu vizuri kama walivyonavyo baadhi ya wanafunzi wenzake. Mjomba wake alimtambulisha kwa rafiki yake ambaye anampenda Angela na anapenda ‘kumtuza’ Angela–lakini kama atafanya naye mapenzi.

Unaweza kwanza kutumia mpangilio huu wa matukio katika kujadili matatizo na baadaye kuwaambia wanafunzi wako waigize kuhusu njia za kushughulikia tatizo hili.

Ukiwa unafundisha watoto wadogo, unaweza kutunga maigizo yanayohusu fikra potofu kama vile:

  • Precious na Becky wako kwenye vyoo vya shule. Precious anataka kujisaidia lakini anasema kuwa atasubiri mpaka afike nyumbani au kwenye kichaka kwa sababu hataki apate UKIMWI.

Kamilisha mpango wako na endelea na somo hili. Mwishoni, jiulize: mpango umekwenda vizuri kiasi gani? Ulifanya kitu gani vizuri? Unawezaje kuboresha mbinu yako ili kuwasaidia wanafunzi waelewe na wajisikie salama?

Nyenzo-rejea ya 1: VVU na UKIMWI katika Afrika

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi

TOLEO LA WAVUTI:

http://www.avert.org

Huu ni ukurasa wa maskani wa wavuti wa shirika linaloitwa AVERT – Shirika la Kimataifa la kusaidia watu wenye VVU na UKIMWI lililoko Uingereza, lenye lengo la kuzuia VVU na UKIMWI duniani.

Utapata taarifa muhimu kwa walimu katika sehemu hii.

TOLEO LA MAKALA:

  • A.Ukweli pamoja na takwimu muhimu zinazohusu VVU na UKIMWI kwa nchi za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara

    Sehemu ya AVERT inatoa takwimu ambazo wanafunzi wako wanaweza kuuliza maswali juu yake. Pia ina mwongozo muhimu wa kuelewa takwimu.

    Hapa pana muhtasari wa takwimu kwa ajili ya Afrika. Utapata undani zaidi kuhusiana na nchi yako kwenye sehemu ya Wavuti hii.

    Afrika sehemu ya kusini mwa Jangwa la Sahara imeathiriwa sana na VVU na UKIMWI kuliko ukanda wo wote ule duniani. Mwishoni mwa mwaka 2005, ilikadiriwa kuwa watu milioni 24.5 walikuwa wanaishi na VVU na kiasi cha milioni 2.7 yalikuwa ni maambukizo mapya yalitokea katika mwaka huo. Katika mwaka uliopita tu mlipuko huo ulikatisha maisha ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 2 katika ukanda huu. Zaidi ya watoto milioni 12 ni yatima wa UKIMWI.

    Mama na mtoto katika hospitali ya Wilaya ya Nsanje, Malawi, wote wana VVU+.

    Ni sasa tu ambapo kiasi cha mlipuko kimeweza kuwa bayana katika nchi nyingi za Kiafrika, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye VVU wanaougua. Bila kufanya jitihada za kuzuia, kutibu na kuwatunza watu dhidi ya VVU/UKIMWI, inatarajiwa kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI itaendelea kupanda. Hii inamaanisha kuwa athari za mlipuko katika jamii hizi zitaonekana zaidi katika kipindi cha miaka kumi au zaidi ijayo. Madhara yake kijamii na kiuchumi tayari yameshaonekana, siyo tu katika sekta ya afya lakini pia katika elimu, viwanda, kilimo, usafiri, rasilimali watu na uchumi kwa ujumla.

    Nchi mbalimbali za Afrika zimeathirikaje?

    Kiwango cha kuenea kwa VVU kinatofautiana sana baina ya nchi za Afrika. Katika nchi za Somalia na Senegali kiwango cha kuenea ni chini ya asilimia moja (1%) cha idadi ya watu wazima, ambapo Afrika Kusini na Zambia ni kati ya asilimia 15-20% ya watu wazima ambao wameathirika.

    Katika nchi nne za kusini mwa Afrika, kiwango cha kuenea kwa VVU kwa watu wazima kitaifa kimepanda juu kuliko ilivyokuwa imefikiriwa na sasa kinazidi asilimia 20%. Nchi hizi ni Botswana (24.1%), Lesotho (23.2%), swaziland (33.4%) na Zimbabwe (20.1%).

    Afrika Magharibi ilikuwa haijaathirika sana na VVU, lakini viwango vya kuenea kwa VVU vinaongezeka. Kuenea kwa VVU kunakadiriwa kuzidi asilimia 5% katika nchi ya Kameruni (5.4%), Kodivaa (7.16) na Gaboni (7.9%).

    Mpaka hivi karibuni, kiwango cha kuenea kwa VVU na UKIMWI kilikuwa kiko chini katika nchi ya Nijeria, nchi ambayo ina watu wengi kuliko nchi zote za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara. Kiwango kilipanda taratibu kutoka chini ya asilimia 2% katika mwaka 1993 hadi asilimia 3.9% katika mwaka 2005. Lakini baadhi ya miji ya Nijeria tayari imeshakuwa na kiwango cha maambukizo ambacho ni kikubwa sawa na vile vilivyoko katika nchi ya Kameruni. Tayari kiasi cha Wanijeria milioni 2.9 wanakadiriwa kuwa wanaishi na VVU.

    Imechukuliwa kutoka: AVERTing AIDS and HIV, Website

  • B.Ukweli na takwimu muhimu kuhusiana na VVU na UKIMWI kwa Tanzania

    36, 766,356: Makisio ya idadi ya watu, Julai 2005.

    1,400,000: makisio ya watu waliokuwa wanaoishi na VVU/UKIMWI mwishoni mwa 2005.

    Makisio ya Asilimia 6.5% ya watu wazima (umri 15-49) waliokuwa wanaoishi na VVU/UKIMWI mwishoni mwa mwaka 2005.

    710,000: makisio ya idadi ya wanawake (umri 15-49) wanaoishi na VVU/UKIMWI mwishoni mwa 2005.

    110,000: Makisio idadi ya watoto (umri 0-14) wanaoishi na VVU/UKIMWI mwishoni mwa 2005.

    140,000: Makisio ya idadi ya vifo vilivyotokana na UKIMWI kwa mwaka 2005.

    1, 000,000: makisio ya idadi ya watoto waliopoteza mama au baba au wazazi wote wawili kwa UKIMWI na walikuwa hai na chini ya umri wa miaka 17 mwishoni mwa mwaka 2005.

    Vyanzo: Ripoti ya UNAIDS ya mwaka 2006 kuhusu Mlipuko wa UKIMWI Duniani -Mei 2006 (UNAIDS 2006 Report on the Global AIDS Epidemic – May 2006);; Kitabu cha CIA cha Kweli Duniani 2005 (CIA World Factbook 2005).

Nyenzo-rejea ya 2: Hali ya darasa

Usuli/welewa wa somo kwa mwalimu

Wanafunzi wanaweza kuyapokea masomo ya VVU na UKIMWI kwa njia tofauti. Wanaweza :

  • kuuliza maswali ili kujaribu kukuudhi;

  • kukaa kimya kwa sababu ya maudhi yao wenyewe;

  • kujaribu kushtuka au kushangaa kutokana kwa kueleza tabia ya ngono waziwazi;

  • Kukuliza maswali binafsi kuhusu maisha yako mwenyewe;

  • Kutoa hoja ambazo zenyewe zitaleta mzaha/bezo au ukosoaji kwa wanafunzi wengine.

Ili kukabiliana na hali hizi, ni muhimu uweke kanuni za darasa. Kanuni hizo lazima ziwe wazi kwa wanafunzi kabla ya kuanza darasa. Unaweza kuwaacha wanafunzi wajadiliane na kuweka kanuni zao wenyewe au unaweza kuanza na orodha ya kanuni na kuijadili kama ziko sahihi na kueleza sababu za kanuni hizo kuwa muhimu. Orodha yako inaweza kujumuisha kanuni kama vile:

  • Wanafunzi wanatazamiwa kuchukuliana vizuri na kujali hisia za kila mmoja.

  • Wanafunzi hawatakiwi kujadili mambo binafsi ya wenzao yaliyosemwa darasani na watu walioko nje ya darasa.

  • Wanafunzi lazima waepuke kuingilia kati mazungumzo ya wenzao.

  • Wanafunzi lazima wasikilizane na kuheshimu maoni ya wengine.

  • Wanafunzi na walimu wana uwezo wa kuendelea bila kuhoji au kujibu iwapo maswali yanamhusu mtu binafsi.

  • Hakuna kukatishana tama-hata kama hukubaliani na mtu kwa kiasi chochote, usicheke, usifanye utani dhidi yake au kutumia lugha ambayo itamfanya huyu mtu ajione mnyonge.

  • Wanafunzi watapewa fursa ya kutoa maswali yao kwa njia ya siri bila kujulikana kwa mwalimu.

  • Kumbuka kwamba kanuni hizi ni kwa ajili ya walimu na wanafunzi pia!

Mbinu zinazoweza katika ufanisi wa masomo

  • Mara nyingi vijana wanachekacheka kama mada inayohusu ngono. Hali hii ni lazima iruhusiwe mwanzoni kwani itapunguza vizuizi wakati wa kujadiliana suala la kujamiiana lakini itawasaidia ili wawe wasikivu.

  • Shughulikia kauli ambazo zinapinga au kudumisha mtazamo pogofu kuhusu waathirika waVVU (mf. kauli zinazoashiria kuwa baadhi ya makundi ya kikabila yanahusika na mlipuko wa UKIMWI) kwa kujadili madhara ya kauli kama hizi.

  • Kuwa na mamlaka unaposhughulikia hali ngumu – mf. Mada hiyo si sahihi/haiendani na darasa hili. Kama ungependa kuijadili, nitafurahi kuzungumza na wewe baada ya darasa.

  • Epuka kuwa mkali kuhusiana na majibu yanayotolewa ili wanafunzi wapate moyo wa kueleza maoni yao kwa uwazi na kwa uaminifu.

  • Elezea pande zote mbili za suala linalotatanisha.

  • Epuka kutoa hukumu kuhusu kile kilichosemwa.

  • Kuwatenganisha wavulana na wasichana wakati wa kufanya kazi kwa vikundi kunaweza kusaidia pale mjadala unapoweza kusababisha maudhi, au pale ambapo kwa kuwatenganisha huku hivi vikundi vitafanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Unajua kuwa wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha kwamba unafahamu ukweli unapofundisha kuhusu VVU na UKIMWI. Lazima ujiandae kikamilifu na hili litakusaidia ujiamini katika kushughulikia mada hii ngumu.

Inasaidia kufikiria kabla jinsi utakavyopokea taarifa za wanafunzi wanaoamini kuwa wameshaathirika. Ni muhimu kwamba upokee taarifa hizi kwa namna itakayowafanya wanafunzi wenye wasiwasi kujihisi faraja kutaka ushauri wako.

Ni muhimu kwamba umsikilize mwanafunzi yeyote anayekujia, pasipo kumlazimisha afuate maadili au mawazo yako, au kumhukumu. Jaribu usiulize maswali elekezi au dokezi (yanayoelekeza kwenye majibu) kuhusu mienendo yao.

Sehemu ya maandalizi yako yapasa kujumuisha kujua hudumu gani za VVU na UKIMWI zinazopatikana katika jumuiya yako. Tafiti ni kliniki au AZAKI zipi hutoa ushauri na msaada wa VVU na UKIMWI kwa vijana ili ujue wapi pa kuwaelekeza wanafunziwako ikilazimika.

Eleza shauku yako juu ya afya ya mwanafunzi husika, na, ikifaa, mwambie kuwa unafahamu kuhusu huduma zinazoweza kusaidia. Jitolee kuanza mchakato kwa kuwasiliana na kituo ambacho mwanafunzi anachagua.

Endeleza msaada wako kwa kumwuliza mwanafanzi mara kwa mara kama anahitaji taarifa zaidi, kama ameshachukua hatua zozote au bado ana shaka juu ya lolote kuhusiana na maongezi yenu.

Imetoholewa kutoka Elimu ya Afya Shuleni Kuzuia VVU & UKIMWI (1999), Shirika la Afya Duniani/UNESCO (School Health Education to Prevent AIDS & STD (1999) World Health Organisation/UNESCO).

Nyenzo-rejea 3: Jaribio kuhusu VVU na UKIMWI

Utumizi wa Mwanafunzi

Jaribio hili lipo mtandaoni kwenye http://www.avert.org/ generalquiz.htm na unaweza kulifanya mwenyewe hapo. Kama wanafunzi wako wanaweza kupata mawasiliano ya Tovuti, unaweza kuitumia nao. Kama haiwezekani, hapa kuna nakala ya matini. Weka tiki kwenye jibu udhanilo ni sahihi.

1. Je, VVU huathiri mashoga na wasagaji tu?
NdiyoHapanaMashoga tuWasagaji tu

2. Ni kadiri ya watu wangapi wanaoishi na VVU dunia nzima?
Milioni 38.6Milioni 25.8Milioni 3.5

3. Utatambuaje kuwa mtu ana VVU au UKIMWI?
Kutokana na jinsi wanavyotendaHuonekana wamechoka na wagonjwaHakuna njia rahisi ya kuwatambua

4. Unaweza kupata UKIMWI kwa kuchangia kikombe na mwathirika?
NdiyoHapanaKama kikombe hakikuoshwa

5. UKIMWI ulifafanuliwa kwa mara ya kwanza lini?
199719871982

6. Ni kitu kipi hukulinda zaidi dhidi ya uambukizo wa VVU?
Kondomu 

Vidonge vya Kuzuia

Uzazi

Jeli ya Kuua Manii

7. Dalili mahususi za UKIMWI ni zipi?
Hakuna dalili mahususiUpele toka kichwani hadi unyayoniUnaanza kuonekana mchovu

8. VVU ni nini?
KirusiBakteriaKuvu

9. Je, wadudu wanaweza kueneza VVU?
Mbu tuNdiyoHapana

10. MKN kirefu chake nini?
 

Maambukizi Kupitia

Ngono

 

Mganga Kabili wa

Ngono

 

Muuguzi Kamili wa

Ngono

11. Je, kuna tiba ya UKIMWI?
NdiyoHapanaZipo kwa agizo la daktari

12. Siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa lini?
1 Januari1 Desemba1 Juni

13. Duniani kote, UKIMWI umeathiri zaidi kundi la umri upi?
Miaka 0–14Miaka 15–24Miaka 25–34

14. Kuna tofauti baina ya VVU na UKIMWI?
Ndiyo, VVU ni kirusi kisababishacho UKIMWIHapana, VVU na UKIMWI ni kitu kile kileNdiyo, UKIMWI ni kirusi kisababishacho VVU

15. Ni asilimia ngapi ya wale walioambukizwa VVU ni wanawake?
Karibu 25%Karibu 50%Karibu 75%

16. Inawezekana kupunguza hatari ya mwanamke aliyeambukizwa VVU kukiambukiza kichanga chake?
Ndiyo, hatari inaweza kupunguzwa ikawa chini zaidiHapana, haiwezekaniKiasi tu

Majibu

Swali 1.

Jibu – Hapana

Swali 2.

Jibu – Milioni 38.6

Swali 3.

Jibu – Hakuna njia rahisi ya kutambua

Swali 4.

Jibu – Hapana

Swali 5.

Jibu – 1982

Swali 6.

Jibu – Kondomu

Swali 7.

Jibu– Hakuna dalili mahususi

Swali 8.

Jibu – Kirusi

Swali 9.

Jibu – Hapana

Swali 10.

Jibu – Maambukizi Kupitia Ngono

Swali 11.

Jibu – Hapana

Swali 12.

Jibu – 1 Desemba

Swali 13.

Jibu – Miaka 15–24

Swali 14.

Jibu – Ndiyo, VVU ni kirusi kisababishacho UKIMWI

Swali 15.

Jibu – Karibu 50%

Swali 16.

Jibu – Ndiyo, hatari inaweza kupunguzwa ikawa chini zaidi

Nyenzo-rejea 4: Uambukizo

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili ya kupanga au kubadilisha kwa ajili ya kutumia na wanafunzi/Matumizi ya wanafunzi

Unaweza kutumia mbinu hii kwa kundi lolote la rika kwa kubadili maswali yawiane na kiwango cha watoto. Maelezo haya yanawafaa zaidi wanafunzi wakubwa zaidi wa shule za msingi.

Madhumuni

  • Kutathmini viwango vya utambuzi wa jinsi VVU vinavyoenezwa.

  • Kuhimiza wana-vikundi kufikiria njia mbalimbali za uambukizo.

Vitu utakavyohitaji

Chumba chenye nafasi ya kutosha, ili kuruhusu upitaji huru wa hewa. Au unaweza kuwa nje.

Nakala ya karatasi ya maswali ya kweli/si kweli kuhusu Uambukizo na karatasi ya Majibu.

Karatasi mbili kubwa zenye maandishi ya wazi ‘NAKUBALI KABISA’ na ‘SIKUBALI KAMWE’.

Pini.

Muda – usiopungua dakika 60 kutegemea idadi ya kauli zilizotumiwa na ukubwa wa kundi.

Unafanya nini

  • Weka karatasi zenye maandishi 'NAKUBALI KABISA' na 'SIKUBALI KAMWE' kwenye kuta zinazokabiliana au kwenye kuta/miti uwanjani.

  • Waeleze wana-kundi kwamba utasoma mfuatano wa kauli, mojamoja. Kila mtu afikirie kama anakubaliana nayo au hakubaliani nayo, kisha aende upande wa chumba au nafasi iliyo na jibu husika. Ni sawa tu kukaa katikati kama hawana hakika.

  • Soma kauli ya kwanza. Baada ya watu wote kujongelea mahali/nafasi waliyochagua, watake wachague mtu aliye karibu wajadiliane nao kwa nini wamesimama hapo.

  • Sasa watake watu wachague mtu aliye mbali nao wajadiliane nao kauli, kila mmoja akieleza kwa nini amechagua kuwa hapo alipo.

  • Fanya hivyo kwa kauli nyingi iwezekanavyo kulingana na muda uliopo.

  • Kutana tena kama kundi, na, huku ukizungukazunguka, mtake kile mtu ataje jambo ambalo linamkanganya au ambalo halielewi vizuri. Watake wanakundi wafafanue masuala husika na usaidie tu pale inapolazimu.

Matokeo yanayowezekana

Mwishoni mwa zoezi hili, itakuwa wazi kuwa sehemu zenye mashaka zitabaki. Watu mmoja mmoja watakuwa wamepata nafasi ya kufikiria juu ya njia za kuambukiza VVU, na kujadili njia hizi na wanakikundi wengine. Itakuwa wazi pia kwamba njia za uambukizaji wa VVU ni mahususi sana, k.m. si ngono inayoambukiza virusi bali ngono isiyo salama inayohusisha mpenyo. Watu wanaweza mara nyingine kuwa wagomvi wakati wa kufanya zoezi hili, hivyo unahitaji kuingilia kati kuamua ugomvi.

Karatasi ya maswali ya kweli/si kweli
KweliSi kweli
1.Unaweza kuambukizwa VVU kwa kuwa mwasherati
2.Udungaji wa madawa ya kulevya kutakwambukiza VVU
3.Unaweza kupata VVU kwenye kikalio cha chooni
4.Kama u mzima huwezi kuambukizwa VVU
5.Wana-ndoa hawaambukizwi VVU
6.Kama utakuwa na mwenzi mmoja huwezi kuambukizwa VVU
7.Kama wanawake watatumia kingamimba hawawezi kuambukizwa VVU
8.Unaweza kuambukizwa VVU kwa kuchangia miswaki
9.Kama utafanya ngono na watu waonekanao wenye afya, hutaambukizwa VVU
10.Kama utafanya ngono na watu uwafahamuo tu, hutaambukizwa VVU
11.Ngono ya mkunduni baina ya wanaume wawili ni hatari zaidi kuliko ngono hiyo baina ya mwanaume na mwanamke
12. 

Unaweza kuambukizwa VVU

kutokana na kubusu

13.Mwanamme anaweza kuambukizwa VVU kama atamfanyia ngono ya kinywa mwanamke
14.Mwanamme anaweza kuambukizwa VVU kwa kufanyiwa ngono ya kinywa na mwanamke
15.Kondomu zinaweza kukomesha usiambukizwe VVU

Karatasi ya majibu ya Kweli/Si kweli

  1. 1. Tabia ya uasherati si hatari kama tabia, lakini kufanya ngono isiyo salama na mtu aliyeambukizwa ni hatari. Kwa kutumia kondomu kama inavyopasa na kuepuka ngono ya mpenyo, unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya uambukizo.

  2. Kama tu sindano au sirinji imechafuliwa kwa VVU kabla.
  3. Hakuna uambukizo wa VVU unaofahamika kutokana na kukalia vikalio vya vyoo.
  4. Uwe mwenye afya au uwe na matatizo ya kiafya, kama ukishiriki ngono isiyo salama kuna uwezekano wa kuambukizwa.
  5. Hii inategemea washirika wahusika, waliyotenda kabla ya kukutana, kama mmojawao alishiriki ngono isiyo salama nje ya ndoa, au kama walijidunga madawa kwa kutumia zana zilizoambukiwa.
  6. Kama kwa Na 5.
  7. Ni kondomu tu zinazotoa ulinzi dhidi ya uambukizo wa VVU; na hata kondomu si salama kikamilifu. Njia nyingine za kinga ya mamba hazitoi ulinzi wowote dhidi ya VVU.
  8. Hakuna ushahidi wa uambukizo kwa njia hii, lakini ni vema kutochangia miswaki kwa sababu za kiafya kijumula.
  9. Watu wengi wenye VVU huonekana wenye afya kabisa. Hivyo, mwonekano ni njia isiyofaa ya kutathmini hatari.
  10. Kumfahamu mtu vizuri si jambo lakutegemea katika kufahamu kama mtu ameambukizwa VVU au la.
  11. Ngono ya kinywani ni hatari pia ifanyike baina ya wanaume wawili au baina ya mwanaume na mwanamke.
  12. Hakuna ushahidi wa uambukizo wa VVU kwa njia hii, ingawa kubusiana wakati kukiwa na vidonda mdomoni kunaweza kuwa hatari.
  13. VVU viko kwenye ute wa mlango wa kizazi na uke kadhalika na damu ya hedhi, hivyo upo uwezekano wa kuambukizwa kwa njia hii.
  14. VVU viko katika shahawa, hivyo kuna uwezekano wa uambukizo kwa njia hii.
  15. Kondomu zikitumika ipasavyo husaidia kuzuia uambukizo wa VVU kutoka kwa mshirika aliyeambukizwa kwenda kwa mshirika ambaye hajaambukizwa. Hata hivyo, kondomu si salama asilimia 100%. Vilainisho vikitumika vyapasa viwe vya majimaji kwani kama ni vya mafuta vitadhoofisha kondomu. Wakati wa kununua kondomu kagua tarehe ambapo kondomu hiyo inapaswa kuwa imeuzwa.

Nyenzo-rejea 5: Igizo kifani kwa masomo ya VVU na UKIMWI

Usuli / dokezo kwa mwalimu

Unapofikiria matatizo kwa ajili ya maigizo kifani, hakikisha unawapa nafasi wanafunzi kulenga miitikio au mienendo chanya. Utafiti umeonesha kuwa ujumbe hasi na unaoogofya hauhimizi badiliko chanya la tabia mara zote. Katika igizo kifani, wanafunzi huigiza hali kwa msukumo wao wenyewe. Hii ina maana kwamba huchukua nafasi na kuamua watakachofanya na kusema papo kwa papo. Hawafanyi mazoezi au kutumia andiko. Huwezi kubashiri kwa hakika namna nafasi itakavyoendelezwa. Maigizo kifani yanaweza:

  • kusaidia kupambanua mitazamo ya watu tofautitofauti;

  • kusaidia wanafunzi kutalii mienendo ya vikundi au watu binafsi;

  • kusaidia wanafunzi kuona kuwa watu wana matatizo yanayofanana;

  • kusaidia wanafunzi kukuza stadi za jinsi ya kuhusiana baina ya mtu na mtu;

  • kutoa fursa ya kushughulikia matatizo nyeti;

  • kusaidia wanafunzi kuona mambo kutumia mitazamo ya watu wengine;

  • kusaidia wanafunzi kufanya mazoezi ya kutenda na kusema kwa uthabiti;

  • kuwapa nafasi wanafunzi kutalii hali zinazowahusu bila kufichua jambo lolote binafsi kuhusu maarifa yao, imani zao, uzoevu au hali zao.

Vidokezo kwa ajili ya maandalizi na uendeshaji wa maigizo kifani

  • Andika tatizo ubaoni au kwenye karatasi.

  • Wape nafasi wanafunzi wasome na kuifikiria hali.

  • Mpe kila mwanafunzi ‘kadi ya nafasi’ ikieleza nafasi yao na wape nafasi wafikirie watasema nini. Maandalizi haya yanaweza kufanywa katika vikundi vya wanafunzi wenye ‘nafasi’ ile ile. (Njia hii inawafanya wanafunzi walenge ‘nafasi zao’ na si hali nzima na hivyo inaweza kutoa igizo kifani lililo changamani zaidi.)

  • Mvulana anaweza kucheza nafasi ya msichana, na msichana ile ya mvulana.

Toa muda kwa ajili ya majadiliano, yatakayohimizwa na maswali kama: Mhusika fulani (…) angetendaje tofauti na alivyotenda? Ni sababu zipi zilizomfanya fulani (…) atende kama alivyotenda? Wahusika wengine walijihisije?