Ruka hadi kwa yaliyomo
Printable page generated Jumatano, 13 Nov 2024, 18:57
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Jumatano, 13 Nov 2024, 18:57

Namba ya moduli 1: Kusoma na Kuandika kwa madhumuni mbalimbali

Sehemu ya 1: Kuhamasisha na kutathmini usomaji na uandishi

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuhamasisha ujifunzaji kusoma na kuandika na kutathmini maendeleo?

Maneno muhimu: kujua kusoma na kuandika katika hatua za mwanzo; nyimbo; mashairi; chapa za kimazingira; tathmini; kazi ya kikundi; usomaji wa ushirika.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kutumia nyimbo na mashairi kufundisha wanafunzi wa kiwango cha mwanzo kusoma;
  • kutumia ‘chapa za kimazingira’ na bidhaa za dukani kufundishia usomaji, uandishi na uchoraji;
  • kutalii njia za kuhamasisha ujifunzaji kwa kutumia kazi ya kikundi;
  • kukuza uwezo wako wa kutathmini ujifunzaji.

Utangulizi

Msomaji na mwandishi mfanisi anatakiwa ajue na aweze kufanya nini? Kama mwalimu, unatakiwa uweze kujibu swali hili ili uweze kuwaongoza wanafunzi wako. Kujifunza kusoma na kuandika kwa ufanisi kunahitaji mazoezi. Hivyo, ni muhimu kutumia mikabala na shughuli mbalimbali ambazo zitawafanya wanafunzi wafurahie. Ni muhimu kutathmini maendeleo ya wanafunzi na kujiuliza mwenyewe kama unakidhi matakwa yao. Sehemu hii inatalii mawazo haya kwani inaangalia ujifunzaji kusoma na kuandika katika hatua za awali.

Somo la 1

Kujifunza kusoma na kuandika ni kazi ngumu! Kwa sababu unataka wanafunzi wazingatie masomo ya kusoma na kuandika, ni muhimu ufanye darasa lako –na shughuli ambazo zinahamasisha ujifunzaji kusoma na kuandika –liwe la kusisimua kadiri iwezekanavyo.

Nyenzo Rejea 1: Wanachotakiwa kukijua wale wasomaji na waandishi wafanisi inaeleza kwamba wanafunzi wanahitaji kujua jinsi ya kuhusisha sauti na herufi, herufi na maneno, maneno na sentensi. Nyimbo na mashairi ambayo wanafunzi wanayajua vizuri –na ambayo wanaweza kuyaimba na kuyaghani kwa kuonesha vitendo –yanawasaidia kujenga mahusiano haya. Pia kushirikishana na wanafunzi wako katika usomaji wa kitabu cha hadithi chenye chapa kubwa kunajenga mahusiano. Unapokuwa unasoma, acha kuwaonesha kila picha na waulize wanafikiri kitu gani kitatokea au kitafuata baadaye. Unapokuwa umemaliza, tumia hiki kitabu kwa shughuli za ugunduzi wa herufi na maneno ambazo utawaambiwa wanafunzi wenyewe waonesha na wasome herufi na maneno fulani. Kumbuka kuwapatia wanafunzi fursa nyingi ili wazungumzie kuhusu hadithi hii –wahusika, kilichotokea, wanavyojisikia kuhusiana na hadithi n.k.

Uchunguzi kifani ya 1: Kuwapatia wanafunzi utangulizi kuhusu usomaji

Bibi Nomsa Dlamini anafundisha wanafunzi wa darasa la 1 wa Nkandla, Afrika Kusini, kusoma na kuandika KiisiZulu. Nomsa huwasomea vitabu vya hadithi, kutoka kwenye baadhi ya vitabu alivyoandika na kufafanua mwenyewe kwa sababu vipo vitabu vichache vya KiisiZulu.

Mwanzoni mwa mwaka, anahakikisha kwamba kila mwanafunzi anaelewa jinsi kitabu kilivyotungwa –jalada, jina la kitabu, hadithi ilivyojengwa –kwa sababu anajua kuwa baadhi yao hawakuwahi kushika kitabu kabla ya kuanza shule. Amegundua kwamba utabiri wa shughuli, ambapo wanafunziwanapendekeza kile kitakachofuata katika hadithi, una umuhimu na huchangamsha wanafunzi wake.

Nomsa amegundua kwamba wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi ili kuwafanya wajiamini katika usomaji. Hutengeneza nakala nyingi za machapisho ya mashairi au nyimbo za KiZulu ambazo wanazijua vizuri na nyingine ambazo anajua kuwa ni mahsusi kwa ajili ya ufundishaji wa ugunduzi wa herufi-sauti. Wanafunzi huzisema au huziimba na kuonesha vitendo kuhusiana na nyimbo na mashairi hayo (angalia Nyenzo Rejea 1: Mifano ya nyimbo na mashairi ). La muhimu zaidi, aliwaambia wanafunzi wenyewe waguse na kusoma herufi na maneno. Baadhi ya wanafunzi waliona kuwa kazi hii ni ngumu hivyo alinukuu majina yao na herufi au maneno waliyoona yanawapa shida. Aliandaa kadi zenye picha, herufi na maneno ili kuzitumia kwa njia nyingine na wanafunzi hawa, ama kwa mmojammoja au katika vikundi vidogovidogo, wakati wanafunzi wengine wakiwa wanafanya shughuli nyingine. Nomsa anafarijika kuona kuwa zoezi hili lilisaidia katika kuwafanya wanafunzi hawa wajiamini na kusonga mbele.

Shughuli ya 1: Kutumia nyimbo na mashairi katika kufundisha usomaji

Waambia wanafunzi:

Wachague wimbo au shairi wanalolipenda;

wauimbe/waghani;waangalie kwa makini, unaposema maneno na kuyaandika ubaoni (au kwenye karatasi /ubao ili uweze kuyatumia tena);wasome wimbo/shairi ulilonalo (fanya hivi mara nyingi);waoneshe kwa kugusa herufi fulani (mojamoja) au maneno au alama za uandishi (herufi kubwa, kituo, alama ya kuuliza);waamue vitendo mtakavyofanya mkiwa mnaimba wimbo/kughani shairi ; wafanye vitendo hivi mkiwa mnaimba tena wimbo/kughani tena shairi; wakae kwenye vikundi vya wannewanne na mpeane zamu za kusomeana wimbo huu/shairi hili.

Zunguka darasani, ukiangalia wanafunzi wanaopata matatizo katika usomaji.

Malizia kwa kuliambia darasa zima liimbe tena wimbo au lighani tena shairi, na kuonesha vitendo.

Somo la 2

Baadhi ya wanafunzi wanakulia katika nyumba ambazo zina utajiri wa chapa na maumbo: maboksi ya bidhaa za dukani, pakiti na makopo, vitabu kwa ajili ya watoto na watu wazima, magazeti hata kompyuta/ngamizi. Wengine wana vifaa hivi kwa uchache nyumbani kwao. Changamoto yako kama mwalimu ni kulipatia darasa lako mazingira yenye utajiri wa chapa . Njia moja ya kufanya hivi ni kukusanya vifaa vyovyote popote vinapopatikana. Vifaa vya kufungashia (maboksi ya mbao, pakiti na makopo) mara nyingi vinaandikwa sana na hata wanafunzi wadogo mara nyingi hutambua maneno muhimu kwa zile bidhaa ambazo zinatumika sana nyumbani. Kwa wasomaji wazoevu, magazeti ambayo wanajumuiya wameshamaliza kuyasoma yanaweza kutumiwa kwa shughuli nyingi darasani.

Sehemu hii inatalii njia za kutumia chapa kama hizi katika kusaidia kujifunza kusoma.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia orodha ya vitu vya dukani kwa shughuli za kujifunza kusoma na kuandika

Precious Muhaji hufundisha Kiingereza kwa wanafunzi 45 wa Darasa la 4 lililopo Lushoto katika Milima ya Usambara. Hawajazoea sana Kiingereza lakini wanatambua herufi na baadhi ya maneno ya Kiswahili yaliyopo kwenye vifaa vya kuhifadhia bidhaa ndogondogo za nyumbani.

Precious alimwomba jirani yake maboksi/makasha, pakiti na makopo matupu. Alivileta vitu hivi shuleni ili kuvitumia katika shughuli za kujifunza kusoma na kuandika.

Mchezo unaopendwa na wanafunzi wake ni mchezo wa ‘ugunduzi wa maneno’. Precious alilipanga darasa katika vikundi tisa vya wanafunzi watanowatano na kukipa kila kikundi boksi, pakiti au kopo lilelile. Aliwaambia wanafunzi waandike namba kuanzia 1 mpaka 5 na kisha aliuliza maswali matano (angalia Nyenzo Rejea 3: Maswali ya mfano ya kuuliza kuhusu vitu vya nyumbani ). Wanafunzi walilinganisha majibu wenyewe na waliamua kuhusu jibu la kikundi. Precious alijadili yale maswali na darasa zima. ‘Mshindi’ alikuwa ni kikundi kilichomaliza cha kwanza na kuweza kutoa majibu sahihi zaidi.

Wakati mwingine Precious alikikaribisha kila kikundi ili kiweze kuuliza swali linalohusiana na ugunduzi wa neno.

Ili kuwahamasisha wanafunzi wafikiri kwa makini, wakati mwingine aliuliza swali kuhusu mchoro wa kifaa kinachohifadhia bidhaa na ujumbe uliopo kwenye tangazo.

Precious aligundua kuwa wanafunzi wengine hawakushiriki, hivyo wakati mwingine walipocheza mchezo huu, alimwambia kila mwanafunzi aandike maneno manne kutoka kwenye kontena la kuhifadhia bidhaa za dukani kabla ya kurudi kwenye viti vyao vya kawaida. Wakiwa wamesharudi kwenye viti vyao alimwambia kila mmoja amsomee mwenzake orodha yake. Aligundua wanafunzi sita ambao walihitaji msaada zaidi na alifanya nao kazi baada ya saa za shule kwa nusu saa, kwa kutumia vitu vilevile na kuwapatia muda wa kufanya mazoezi ya kubainisha herufi na maneno.

Precious aligundua kuwa kuzoea herufi na maneno katika vifaa vya kuhifadhia bidhaa huwasaidia wanafunzi kubainisha herufi na maneno haya katika matini nyingine walizozisoma, kama vile hadithi. Kwa kunakili maneno kutoka katika vitu hivyo, wanafunzi pia hujifunza kuandika herufi na maneno kwa kujiamini zaidi na kwa usahihi zaidi.

Shughuli ya 2: Kutumia orodha ya bidhaa za dukani kwa shughuli za usomaji na uandishi

Leta makopo/mikebe, pakiti au maboksi ya kutosha darasani ili kila kikundi cha wanafunzi watanowatano au sitasita kipate kitu kimojawapo cha kukifanyia kazi au liambie darasa lako likusaidie katika ukusanyaji wa vitu hivi.

Andika maswali ubaoni kuhusu maneno na picha zinazoonekana kwenye pakiti, kopo au boksi ( angalia Nyenzo Rejea 3 ). Ama waambie wanafunzi wayasome au uwasomee.

Ama chezesha mchezo wa ugunguzi wa maneno katika vikundi (angalia Uchunguzi Kifani 2) au waambie wanafunzi waandike majibu wenyewe. Panga muda wa ziada wa mazoezi na wa kutoa msaada zaidi kwa ajili ya wanafunzi ambao hawawezi shughuli hii.

Katika somo linalofuata, waambie wanafunzi wafanye kazi katika vikundi vilevile wabuni maandishi na taarifa zinazoonekana kwa ajili ya kifaa cha kweli au picha ya bidhaa za dukani.

Kiambie kila kikundi kioneshe na kuzungumzia kuhusu ubunifu/mchoro wao kwa wanafunzi wote darasani.

Wanafunzi wamejifunza nini kwa kusoma orodha ya bidhaa za dukani na kwa kuchora na kuonesha vifaa vyao wenyewe vya kuhifadhia bidhaa hizo? Linganisha mawazo yako na mapendekezo yaliyopo katika Nyenzo Rejea 3 .

Somo la 3

Kusoma na kuandika kunaweza kusisimua na kuchangamsha sana, lakini baadhi ya wanafunzi wanajenga mtizamo hasi kuhusiana na shughuli hizi. Sababu inaweza kuwa ni kwa vile wanagundua kuwa kusoma na kuandika ni kugumu, labda kwa sababu wanaweza kuchoshwa na kazi za usomaji na uandishi ambazo zinafuata ruwaza zilezile daima, au labda hawaoni thamani kubwa katika usomaji na uandishi. Moja ya changamoto zako kama mwalimu ni kuamsha ari ya wanafunzi katika usomaji na uandishi na kuwafanya wahamasike.

Uchunguzi Kifani 3 na Shughuli Muhimu vinapendekeza shughuli ambazo zinaweza kuwasaidia wanafunzi wafurahie na wajiamini zaidi katika usomaji na uandishi.

Uchunguzi kifani ya 3: Kusoma alama zinazopakana jirani na eneo lako na kuandika maelezo kuhusiana na alama hizo

Bwana Richard Limbunga hufundisha Kiswahili Darasa la 5 jijini Dar es Salaam. Dar es Salaam ni eneo lenye watu wengi na mifano mingi ya chapa za kimazingira kuzunguka shule –mifano mingi zaidi ni ya Kiswahili lakini pia kuna mifano kutoka katika lugha mbalimbali za asili.

Ili kuongeza kipato watu wameanzisha ‘biashara za uani’ kama vile maduka ya bidhaa ndogondogo za dukani, sehemu za kunyolea, warepeaji magari na vibanda vya simu. Sehemu zote hizi zina alama na baadhi pia zina matangazo ya kibiashara kwa ajili ya bidhaa mbalimbali. Hizi ni shule, kliniki, sehemu na kumbi za kuabudia, ambazo nyingi yazo zina alama na mbao za matangazo. Katika barabara kuu, kuna alama sehemu nyingi, zikiwemo Chuo Kikuu maarufu cha Dar es Salaam.

Bwana Limbunga alipanga safari kuzunguka Dar es Salaam ambayo ingewapatia wanafunzi fursa ya kusoma na kutengeneza kitini na michoro kuhusu mifano mbalimbali ya chapa na maumbo yanayoonekana. Pia aliandaa orodha ya maswali ili kuongozo uchunguzi wao.

Bwana Limbunga anao wanafunzi 58 katika darasa lake, wakiwemo kumi ambao wamewasili hivi karibuni kutoka Burundi. Aliamua kuwaomba wastaafu wawili wanaojua lugha nyingi wamsaidie katika shughuli hii. Mmoja anaongea Kirundi, lugha ya wanafunzi kutoka Burundi. Vikundi vitatu vya darasa lile vilikwenda safari.

Marafiki wa Bwana Limbunga walishiriki katika mjadala darasani na kwenye shughuli zilizofuata za usomaji na uandishi. Kufikia mwishoni mwa wiki, watu wale watatu walikubali kuwa wanafunzi wamejua zaidi jinsi taarifa inavyoweza kuwasilishwa kwa njia mbalimbali na kwa lugha mbalimbali na baadhi walionekana wamefurahia zaidi usomaji na uandishi kuliko hapo awali.

Shughuli muhimu: Kusoma Alama

Kabla ya somo, soma Nyenzo Rejea 4: Kujiandaa kwa matembezi ya kijumuiya ili kupanga matembezi na kuandaa maswali yako. Andika maswali ubaoni.

Ili kuanza somo, waambie wanafunzi kuhusu matembezi na, kama wanaweza, waambie wanakili yale maswali kutoka kwenye ubao. Kama hawawezi, andaa orodha ya maswali kwa kila kiongozi wa kikundi kwa ajili ya kuwauliza katika matembezi.

Wachukue kwa ajili ya matembezi yaliyopangwa mpaka kwenye jumuiya yenu mnayokaa.

Wakiwa wanatembea, lazima watoe au waandike majibu ya maswali na wachore mifano ya chapa au picha wanazoziona.

Baada ya muda, waambie wanafunzi kwenye vikundi washirikishane kile walichokiona, walichokiandika na walichokichora. Liambie darasa zima liripoti na lirekodi pointi muhimu ubaoni.

Kiambie kila kikundi kichore, kiandike jina na kichore alama, ilani au tangazo wanalofikiri ni muhimu kuwapo katika jumuiya zao. Wasaidie katika maneno yoyote magumu. Watoto wadogo wanaweza kuhitaji kufanya kazi kwenye vikundi vidogo vyenye mtu mzima wa kuwasaidia.

Kiambie kila kikundi kioneshe mchoro wao darasani kisha kieleze uteuzi wa lugha, maumbo na taarifa.

Onesha michoro hii darasani ili wanafunzi wote waisome.

Nyenzo­rejea ya 1: Kitu ambacho waandishi na wasomaji wafanisi wanatakiwa kukijua

Usuli/ welewa wa somo wa mwalimu

Lugha wanayotarajiwa kujifunzia usomaji na uandishi

Kama wanafunzi wanatakiwa wajifunzie kusoma na kuandika katika lugha ambayo si lugha ya nyumbani, hali hii itafanya kazi iwe ngumu zaidi. Katika hali hii, walimu wanatakiwa waanze na kazi za kuongea na uundaji wa msamiati katika lugha hii ya nyongeza, kwa kutumia vitendo na picha. Pindi tu watakapokuwa na uelewa wa baadhi ya yanayosemwa wanaweza kutarajiwa kutumia uelewa huo kwa usomaji na uandishi.

Msimbo wa maandishi

Wanafunzi wanahitaji kuelewa jinsi herufi kwenye ukurasa unavyowakilisha sauti fulani na jinsi zinavyoungana katika kuwasilisha maana kwa njia ya maneno. Hii ndiyo sababu ya umuhimu wa walimu kwa kiasi fulani kuzingatia ‘foniksi’ – herufi inayowakilisha sauti fulani – wanapowafundisha wasomaji wa kiwango cha mwanzo. Kwa kuchukua mfano toka katika lugha ya Kiswahili, kama mwalimu ungeweza kutumia picha ya mbwa pamoja na herufi tofauti za m b w a na kisha neno m b w a chini yake. Kwanza waulize wanafunzi wanaona nini katika picha (mbwa), kisha onesha kila herufi na kuitamka; kisha tamka neno zima. Baadaye pima welewa wa wanafunzi kwa kuonesha herufi ambazo hazijaunganishwa na kuwaambia waunde manenokwa kutumia kila moja ya sauti. Baadaye, waambie wakuambie maneno mengine yanayoanza na sauti m. Pia wapatie mifano yako mwenyewe.

Kanuni za uandishi

Wanafunzi wanahitaji kuelewa jinsi maneno yanavyoungana kuunda maana katika sentensi, aya, na matini ndefu (mf.kitabu kizima cha hadithi) na jinsi matini zinavyoandikwa kwa njia nyingi na kwa madhumuni mbalimbali (mf. Mapishi ni tofauti na jinsi hadithi inavyoandikwa). Katika miaka ya mwanzo, wanafunzi wanaanza kujifunza jinsi uandishi unavyopangiliwa, lakini hili ni jambo wanalojifunza zaidi katika masomo yao. Wanafunzi wanatakiwa wasome kitabu chote ili waweze kuona jinsi maneno yalivyoungana na jinsi hadithi au dai linavyoendelezwa. Hii ndiyo maana hakutoshi kushughulikia sauti tu.

Jinsi ya kusoma michoro, picha­vivuli, vielelezo na jinsi ya kutengeneza mahusiano baina ya maumbo haya na maneno ya maandishi

Wanafunzi wanahitaji kufundishwa jinsi kugundua yale yaliyopo katika michoro, picha­vivuli na vielelezo. Unaweza kuwasaidia kwa kuwauliza maswali kama vile ‘babu ameshika nini?’ ‘Kiboko ana nini mgongoni mwake?’

Kuhusu dunia na jinsi inavyojiendesha

Kadiri mwalimu anavyowasaidia wanafunzi kupanua maarifa yao ya jumla ya dunia na jinsi inavyofanya kazi, ndivyo hivyo inavyowarahisishia wanafunzi kusoma kuhusu kile kigeni na kile wasichokijua kwa sababu wanaweza kuunganisha kati ya kile ambacho tayari wana uzoevu nacho au wameshajifunza na hii taarifa mpya.

Zaidi ya yote, ni muhimu wanafunzi wafurahie kusoma na kuandika – hata wanapokutana na changamoto.

Nyenzo­rejea ya 2: Mifano ya nyimbo na mashairi 

Nyenzo Rejea ya mwalimu kwa upangaji au kurekebisha kwa ajili ya kutumia na wanafunzi

Mfano wa wimbo wa Kiswahili

Wimbo wa kubembelezea mtoto wa ‘Kua’, unahusu mzazi anayekazania kumwambia mtoto wake mdogo akue. Zingatia mdafao wa marudio ya herufi na sauti zilezile.

Unaimbwa hivi:

‘Kua mwanangu, kua. Kua ili nikupe mawaidha ili kwamba niweze kukupa kundi la ng’ombe na mbuzi, ili upate maziwa. Kua mwanangu, kua. Kua ili uwe mkubwa. Kua upesi kama mgomba kwa sababu mnazi unachelewa. ‘Kua mwanangu, kua.

Katika unaweza kuusikia wimbo huu.

Vyanzo vya asili: [BBC Radio 3 On Your Stree], Website

Shairi la Kiswahili lililotafsiriwa kutoka lugha ya Kiiingereza ambalo linafurahisha likighanwa harakaharaka

Siagi ya Manjano na Mary Ann Hoberman

Siagi ya manjano jeli ya zambarau jemu nyekundu mkate mweusi

Ipakaze kwa wingi

Iseme kwa haraka

Siagi ya manjano jeli ya zambarau jemu nyekundu mkate mweusi

Ipakaze kwa wingi sana

Iseme kwa haraka sana

Siagi ya manjano jeli ya zambarau jemu nyekundu mkate mweusi

Sasa irudie

Ukiwa unaila

Siagi ya manjano jeli ya zambarau jemu nyekundu mkate mweusi

Usiongee mdomo ukiwa umejaa!

Shairi la vitendo

Mimi ni chombo kidogo cha sukari, kifupi na imara

Huu ni mpini wangu, huu ni mdomo wangu

Ninapopata joto

Hapo ninapayuka

Nipindue

Nimwage.

Wimbo wa mnyama dunia – wimbo kutoka Kongo

Angalizo: Wimbo huu unahusu harakati na sauti za kiitikio zinawakilisha harakati za viumbe.

MSIMULIAJI: Samaki huenda

KIITIKIO: Hip!

MSIMULIAJI: Ndege huenda

KIITIKIO: Viss! MSIMULIAJI: Nyani huenda KIITIKIO: Nyan!

SAMAKI: Ninaanzia kushoto,

Ninageuka kulia.

Mimi ni samaki

Anayeponyoka majini,

Anayeteleza,

Anayenengua,

Anayechupa!

MSIMULIAJI: Kila kitu kinaishi,

Kila kitu hucheza dansi,

Kila ktu huimba.

KIITIKIO: Hip!

Viss!

Nyan!

NDEGE: Ndege huruka mbali,

Huruka, huruka, huruka,

Huenda, hurudi, hupita,

Hupanda, huelea, hutua.

Mimi ni ndege!

MSIMULIAJI: Kila kitu huishi,

Kila kitu hucheza dansi,

Kila kitu huimba.

KIITIKIO: Hip!

Viss!

Nyan!

NYANI: Nyani! Kutoka tawi

hadi tawi

Hukimbia, huchupa, huruka,

Akiwa na mkewe na mtoto,

Mdomo ukiwa umejaa chakula, mkia hewani,

Huyu ni nyani!

Huyu ni nyani!

MSIMULIAJI: Kila kitu huishi,

Kila kitu hucheza dansi,

Kila ktu huimba.

KIITIKIO: Hip!

Viss!

Nyan!

Vyanzo vya asili: [Siagi ya manjano – Shairi/wimbo wa jadi; Kiingereza Kipya cha Mafanikio, Darasa la 6, Kitabu cha Kusoma], [Oxford University Press]

[ Wimbo wa mnyama dunia – Wimbo wa jadi kutoka Kongo], [Ushairi wa Kiafrika kwa Shule, Longman]

Nyenzo­rejea ya 3: Maswali ya mfano ya kuuliza kuhusu bidhaa za dukani

Nyenzo Rejea ya mwalimu kwa kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

  1. Ndani ya kopo/pakiti/boksi mna nini?
  2. Unajuaje hivi?
  3. Ni neno au maneno gani yameandikwa kwa herufi kubwa zaidi yaherufi zote? 
  4. Unafikiri kwa nini hili neno au haya maneno yameandikwa kwa herufi kubwa kuliko herufi zote?
  5. Maneno mangapi yanaanza kwa herufi kubwa?
  6. Maneno gani yameandikwa zaidi kwenye kifaa hiki cha kuhifadhia bidhaa kisha kuandikwa mara moja?
  7. Neno lipi hutumika sana?
  8. Nini uzito wa bidhaa hii (gramu/kilogramu)?
  9. Maneno na picha zote zinakuambia nini kuhusiana na bidhaa hii?

Maswali yanayohamasisha kufikiri kwa makini

  • Unakubaliana au unapingana na kile unachoambiwa na maneno na picha hizi?

  • Kama ungekuwa na fedha, ungependa kununua bidhaa hii? Kwa nini ndiyo?, au kwa nini hapana?

Angalizo 1: Baadhi ya bidhaa zina maneno ambayo yako kwenye lugha zaidi ya moja. Kama hivi ndivyo kwa baadhi ya bidhaa unazotumia, ungeweza kuwauliza wanafunzi ni lugha gani ambazo zimekuwa zikitumika na kwa nini wanafikiri lugha hizi zilikuwa zikitumika.

Angalizo 2: Maswali haya ya mfano ni ya jumla sana. Kuna maswali mengine mengi ungeweza kuuliza, kama kuna picha za watu kwenye bidhaa, je, ni wanaume au wanawake, je ni vijana au wazee? Kwa nini watu hawa wawepo kwenye pakiti/kopo/boksi?

Wanafunzi wanaweza kujifunza nini kutokana na kutumia orodha ya bidhaa za dukani

  1. Wasomaji wa kiwango cha mwanzo wanaweza kutumia maneno yaliyopo kwenye orodha ya bidhaa za dukani ili kupata ujasiri na stadi katika kutambua muundo wa herufi kubwa na ndogo wa alfabeti na katika kuunganisha maumbo ya herufi na sauti.
  2. Kwa kunakili herufi na maneno kutoka kwenye kitu hicho, mwandishi wa kiwango cha mwanzo, anaweza kupata ujasiri na stadi za kuandika herufi na maneno haya kwa usahihi.
  3. Wasomaji wa ngazi ya juu wangeweza kusoma ‘ujumbe’ uliopo kwenye kitu hicho na kutafakari maana yake. Wangeweza kuanza kuwa wasomaji makinifu.
  4. Kwa kufanya kazi ya kubuni baadhi ya orodha ya bidhaa za dukani katika vikundi, wanafunzi wangeweza kufaidika kutokana na mawazo ya wenzao, kujifunza vitu vinavyohusika katika kuchora bidhaa, kutumia fikra zao na kufanya mazoezi ya kuandika na kusoma.
  5. Baadhi ya wanafunzi wanaona ni vigumu kuzungumza darasani kwa sababu hawajui wazungumzie nini. Ukiwa na kielelezo cha kitu kwa ajili ya kuelezea darasani kinawapa wanafunzi mada ya kuzungumzia.
  6. Kila kielelezo cha kikundi kinawapatia wanafunzi wengine vitu vingine vya kusoma.
  7. Ungeweza kutengeneza kadi za kusomeshea zenye herufi/maneno ambayo baadhi ya wanafunzi wanayaona ni magumu kuyasoma. Weka picha ya kuwasaidia kwenye kila kadi. Tumia kadi hizi kwa ajili ya mazoezi ya kusoma ya mwanafunzi mmojammoja au kwa kikundi kidogo kwa muda muafaka.

Nyenzo­rejea ya 4: Kujiandaa kwa matembezi ya kijumuiya – kipindi hicho wanafunzi watagundua chapa za kimazingira

Nyenzo Rejea ya mwalimu kwa kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Hatua 1: Kama darasa lako ni kubwa sana, unaweza kuwaomba watu wazima kutoka kwenye jumuiya wakusaidie kufanya matembezi na vikundi vya wanafunzi. Kama unawaomba, kutana nao kabla ya matembezi kuwaeleza kile unachotaka wao wafanye. Lazima wajue ni maswali gani utawauliza wanafunzi na ni mifano gani ya chapa za kimazingira unataka wanafunzi wazigundue. Wanaweza pia kuwa na mapendekezo ya kukupa.

Hatua 2: Panga shughuli kwa kutembelea mazingira yote yanayoizunguka shule yako. Kwa baadhi yenu eneo hili linaweza kuwa ni kijiji, kwa wengine sehemu ya jiji lenye shughuli nyingi. (Angalizo: Kama shule yako ipo sehemu ambayo imejitenga, unaweza kuhitaji kusaidiana na wanajumuiya ili kupanga usafiri wa wanafunzi kwenda sehemu ambayo wanaweza kuona chapa mbalimbali za kimazingira). Angalia kila mfano wa chapa ya kimazingira unaoweza kuwavutia wanafunzi na panga njia ambayo wewe na wanafunzi mtapitia wakati wa matembezi. Aina za chapa na maumbo/picha, kwa hakika, itatofautiana sana kutoka kwa eneo jirani moja na jingine lakini zinaweza kujumuisha majina (mf.shule, kliniki, msikiti, kanisa, ukumbi wa jumuiya, duka, mto, mtaa); alama (mf. Alama ya SIMAMA); matangazo kwenye mabango makubwa au kwenye kuta za maduka; taarifa za kijumuiya (mf. mabango ya uchaguzi au taarifa kuhusu mikutano au matukio ya kijamii au michezo).

Hatua 3: Andaa orodha ya maswali watakayoyajibu wanafunzi. Haya yanaweza kujumuisha:

  • Alama au jina hili linatuambia nini?

  • Unafikiri kwa nini limewekwa hapa?

  • Limeandikwa kwa lugha gani?

  • Unafikiri kwa nini limeandikwa kwa lugha hii?

  • Unapata taarifa gani kutokana na mchoro au picha kivuli hii unayoiona?

  • Ni alama ipi ambayo ni rahisi kuisoma? Kwa nini?

  • Unapenda alama ipi? Kwa nini?

  • Unawezaje kuboresha baadhi ya alama hizi?

  • Ni majina gani mengine, alama, matangazo, mabango, taarifa ambazo ungependa kuwa nazo katika mazingira ya hapa jirani? Kwa nini ungependa kuwa nazo hizi?

Sehemu ya 2: Kuchochea hamasa katika usomaji wa hadithi

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuwahamasisha wanafunzi wapende kusoma hadithi na vitabu?

Maneno muhimu: usomaji wa kushirikishana; majibu ya ubunifu; kusoma kimya; mianzo na miisho; kuchochea hamasa.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kutumia njia ya kushirikishana katika usomaji wa hadithi kwenye ufundishaji wako ili kusaidia wasomaji wanaoendelea;
  • kutumia shughuli zinazolenga mianzo na miisho mbadala katika usomaji;
  • kutalii njia mbalimbali za kukuza Usomaji Kimya Endelevu katika darasa lako.

Utangulizi

Inawezekana zaidi kwa wanafunzi kujifunza kusoma kwa ufanisi kama wanafurahia kusoma na kuandika mara nyingi iwezekanavyo. Ukiwauliza rafiki zako wanafurahia nini katika kusoma, majibu yao yanaweza kutofautiana kuanzia kwenye kurasa za magazeti ya michezo mpaka kwenye mapishi, riwaya za mapenzi, hadithi za upelelezi au wasifu –au wanaweza wasisome kabisa! Kama walivyo rafiki zako, wanafunzi mbalimbali wanaweza kufurahia kusoma aina tofauti za matini. Watavutiwa na kile wanachosoma kwa njia mbalimbali. Kazi yako ni kuwahamasisha wanafunzi wote katika darasa lako wasome kwa ufanisi na wafurahie usomaji.

Sehemu hii inalenga kuwasaidia wanafunzi wapate raha katika usomaji na wavutiwe na hadithi.

Somo la 1

Aina ya hadithi na shughuli za usomaji wa hadithi ambazo wanafunzi wanazifurahia huenda zikatofautiana kufuatana na umri wao na ujuzi wao wa lugha iliyotumika katika hadithi hiyo. Wanafunzi wadogo zaidi na wanafunzi ambao ndio wameanza kujifunza lugha ya ziada wanafurahia wakisomewa hadithi mara kadhaa –hasa kama wana fursa ya kushiriki katika usomaji. Kwa kusoma hadithi mara nyingi na kuwatia moyo wanafunzi wasome sehemu za hiyo hadithi pamoja na wewe, unawasaidia wazoee maneno mapya na wajiamini kama wasomaji.

Lengo la Shughuli 1 ni kuandaa na kufundisha somo la kushirikishana katika usomaji. Madhumuni ya shughuli hii ni kuongeza kujiamini kwako na ujuzi kama msomaji, na kuwafanya wanafunzi wapende kusoma vitabu.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia uzoevu wa hadithi za utotoni ili kuandaa shughuli za darasani

Wakati Jane Dlomo alipofikiri kuhusu enzi za utoto wake huko Rasi ya Mashariki ya Afrika Kusini, alikumbuka ni kwa kiasi gani alivyofurahia hadithi za bibi yake. Vitu viwili vilimjia akilini: kwanza kabisa, jinsi gani alivyofurahia kusikiliza hadithi zilezile na tena zaidi na zaidi na pili, jinsi gani yeye na kaka na dada zake walivyofurahia kujumuika kwenye hadithi. Wakati mwingine bibi yake aliuliza, ‘Mnafikiri kulitokea nini baadaye?’ Wakati mwingine aliwataka watoto kuonesha vitendo.

Jane aliamua masomo yake ya usomaji kwa Darasa la 4 nne yawe karibu na jinsi alivyofanya bibi yake katika hadithi. Pia aliamua kuwajaribishia shughuli ambazo zingewahusisha wanafunzi washirikiane naye katika usomaji.

Alipomwambia rafiki yake Thandi kuhusu uamuzi wake, Thandi alipendekeza kuwa washirikiane kupata vitabu vya hadithi vinavyofaa, kufanya mazoezi ya kusomeana hadithi kwa sauti na katika kufikiria njia za kuwashirikisha wanafunzi katika usomaji. Walimu wote wawili waligundua kuwa kushirikishana katika maandalizi kuliwasaidia katika kujiamini zaidi darasani. (angalia Nyenzo-rejea 1: Maandalizi kwa ajili ya usomaji wa kushirikishana ).

Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia usimulizi wa hadithi darasani inakupa mawazo zaidi.

Shughuli ya 1: Kushiriki kwa pamoja raha iliyo katika kitabu kizuri cha hadithi

Soma Nyenzo-rejea 1 na fuata hatua zifuatazo hapa chini: Andaa kazi ya mazoezi mengine kwa baadhi ya wanafunzi ili wayafanye wakati mnapofanya usomaji wa kushirikishana kikundi cha wanafunzi 15 au 20.

Toa maelezo ya usuli kuhusu mada ya hadithi kabla ya kuisoma hiyo hadithi.

Unaposoma, waoneshe wanafunzi vielelezo na waulize maswali kuhusiana na vielelezo hivyo. Tumia sauti yako na vitendo ili kuvuta usikivu wa wanafunzi.

Waalike wanafunzi wajiunge katika usomaji kwa kurudia maneno au sentensi kadhaa ulizoandika ubaoni na kwa kuonesha vitendo.

Mwishoni, jadilini hadithi hii na wanafunzi wako. (Angalia Nyenzo-rejea 2: Maswali ya kutumia katika usomaji wa vitabu.)

Ulijisikiaje kuhusu usomaji wako wa hadithi? Je, wanafunzi waliifurahia hadithi? Unajuaje? Unaweza kufanya nini ili kuboresha stadi zako za usomaji?

Somo la 2

Bruno Bettelheim (1976), mtaalamu wa saikolojia ya watoto, anaamini kwamba kama watoto watakutana na ‘maajabu’ katika hadithi, kwa hakika watapenda kujifunza kusoma. Anatoa hoja kuwa kama watoto anaamini hasa kwamba kuweza kusoma kutafungua dunia yenye uzoevu na welewa wa ajabu, watafanya jitihada kubwa kujifunza kusoma na wataendelea kusoma.

Kusoma pamoja hadithi za kufurahisha na wanafunzi ni njia moja ya mwalimu ya kufanya usomaji uwe ni jambo lenye mvuto. Kitu kingine ni kuchochea udadisi na ubunifu kwa kuwahimiza watafute miisho mbadala ya hadithi (na wakati mwingine mianzo) na kushirikishana mianzo na miisho hii na wanadarasa wenzao. Uchunguzi kifani 2 na Shughuli 2 vinaeleza jinsi unavyoweza kuwasaidia wanafunzi wako wawe watunzi wa hadithi kwa ajili ya wenzao.

Uchunguzi kifani ya 2: Usomaji wa hadithi; uandishi wa miisho mipya ya hadithi

Bibi Miriam Pharouk hufundisha Kiingereza Darasa la 6 katika shule ya Tanga. Siku moja aliwaambia wanafunzi wake wafikirie hadithi ambazo wameshasoma naye na wamwambie ni mwisho upi wa hadithi waliupenda sana na upi waliuona si mzuri au haukuwaridhisha. Aligundua kuwa walikuwa na hadithi tofautitofauti walizozipenda. Hata hivyo, kulikuwa na hadithi moja ambayo wanafunzi wengi hawakuipenda kwa sababu hawakujua kilichotokea kwa wahusika watatu ambao ‘walitoweka’ kwenye hadithi. Miriam aliwaambia wapendekeze nini kinaweza kuwa kiliwatokea wahusika hawa na aliandika mawazo yao ubaoni. Baadaye aliwaambia

wanafunzi wamchague mhusika mmoja kati ya hawa watatu na waandike sehemu ya mwisho ya mhusika huyu katika hadithi hii. Aliwahimiza wanafunzi kutumia mawazo yao wenyewe, na pia yale yaliyoandikwa ubaoni, na waingize michoro kwenye uandishi wao. Kisha alisoma tena ile hadithi ili kuwakumbusha mandhari, wahusika na matukio makuu.

Ingawa Miriam aliwaambia wanafunzi kila mtu aandike mwenyewe, pia aliwahimiza kusaidiana kwa mawazo, msamiati na muenelezo wa maneno. Alizunguka darasani huku wanafunzi wakiwa wanaandika na kuchora, akitoa msaada palipohitajika. Alifarijika alipogundua kuwa wengi wa wanafunzi wake wanapenda kwa dhati wazo la kuwa watunzi na la kuiandikia hadhira halisi (wanadarasa wenzao). Aling’amua kuwa walikuwa waangalifu sana katika kufanya kazi yao kwa sababu wanadarasa wenzao wangesoma kazi zao.

Katika somo lililofuata, wakati wanafunzi wanasoma mwisho wa hadithi ya mwenzao, mwalimu aligundua kuwa wengi wa ‘wasomaji wake waliokuwa wanasitasita’ walikuwa makini kusoma kile ambacho wanadarasa wenzao walikuwa wamekiandika na kuona kile walichokuwa wamekichora.

Shughuli ya 2: Uandishi wa mianzo na miisho mipya ya hadithi

Andika kwenye ubao wako hadithi fupi katika Nyenzo-rejea 3: Hadithi . Futa kichwa cha hadithi na sentensi mbili za mwisho.

Soma hiyo hadithi wewe na wanafunzi wako. Jadilini maneno yoyote magumu.

Waambie wajibu maswali kama yaliyoko kwenye Nyenzo-rejea 3.

Panga darasa katika vikundi vya wannewanne –wawili waandike mwanzo wa hiyo hadithi na wawili waandike mwisho wa hiyo hadithi. Wanafunzi wawiliwawili wachore mchoro wa kufafanua sehemu yao ya hadithi. (Zoezi hili linaweza kuchukua zaidi ya kipindi kimoja.)

Kiambie kila kikundi kisome hadithi yao yote na kuonesha michoro yao kwa darasa zima. Jadilianeni na wanafunzi kitu wanachokipenda katika hadithi za wenzao.

Mwishoni, wasomee wanafunzi wote kichwa cha hadithi ya awali na zile sentensi mbili za mwisho. (Huenda wakashangaa kwamba inahusu soka!)

Tafuta hadithi nyingine ili kurudia zoezi hili.Shughuli hii ilifanikiwa vizuri kwa kiasi gani? Wanafunzi walizipokeaje hadithi za wenzao?

Somo la 3

Walimu lazima wawe mifano mizuri kwa wanafunzi wao. Wanafunzi wako wanaweza kuhamasika zaidi katika usomaji kama wanakuona wewe ukisoma. Kila siku jaribu kutenga muda (angalau mara tatu kwa wiki) kwa ajili yako na wanafunzi wako wa kusoma kimya darasani. Unaweza kuchukua mfano huu kutegemeana na umri wa wanafunzi wako. Kwa mfano, wanafunzi wenye umri mdogo wangeweza kuangalia kitabu cha picha na wenzao au kumsikiliza mtu akiwasomea katika vikundi vidogo.

Usomaji Kimya Endelevu au Usomaji wa Kina (Sustained Silent Reading) huwasaidia wanafunzi wazoee kujitegemea katika usomaji na kwa kasi yao wenyewe (ambayo inaweza kuwa ya haraka sana au taratibu sana kuliko baadhi ya wanadarasa wenzao). Mlengo ni kwenye hadithi yote (au sura yote kama hadithi ni ndefu sana) na kwenye miitikio binafsi ya wanafunzi kuhusiana na kile wanachosoma. Usomaji Kimya Endelevu unaweza kufanywa kutumia kitabu cha kusoma darasani, idadi mbalimbali ya vitabu ambavyo wanafunzi wamevichagua katika maktaba ya darasa au ya shule, au kwa kutumia magazeti (kama wanafunzi wanaweza kuyatumia) – angalia Nyenzo-rejea 4: Usomaji Kimya Endelevu .

Uchunguzi kifani 3 na Shughuli Muhimu zinaonesha njia za kutathmini maendeleo ya wanafunzi kama wasomaji. (Angalia pia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutathmini ujifunzaji .)

Uchunguzi kifani ya 3: Uzoevu wa walimu kuhusu Usomaji Kimya Endelevu

Chama cha Usomaji Tanzania kilipanga warsha iliyofanyikia Dar es Salaam, ili kuwapatia walimu utangulizi kuhusu Usomaji Kimya Endelevu. Ilielezwa kuwa moja ya malengo makuu ya Usomaji Kimya Endelevu ni kujenga ‘utamaduni wa kusoma’ miongoni mwa wanafunzi.

Walimu walialikwa kushiriki katika Usomaji Kimya Endelevu na kisha kutafakari uzoevu wao. Kila mwalimu alichagua kitabu au gazeti na kusoma kimya kwa dakika 20. Baada ya kusoma, walikuwa na dakika kumi za mjadala na wenzao watatu kuhusu kile walichokisoma na jinsi walivyoipokea ile matini. Waliporudisha vitabu na magazeti yao waliandika majina yao kwenye kitabu cha rejesta na, pembeni mwa majina yao, waliandika maoni mafupi kuhusu matini hiyo.

Walimu hawa waliamua kuwa Usomaji Kimya Endelevu ni muhimu kwa ajili ya kujenga umakinikaji na nidhamu ya mtu, kwa kujifunza msamiati mpya na mawazo mapya na kutoa maudhui ya kujadiliana na wanafunzi. Walifikiri kuwa wanafunzi wataifurahia shughuli hii na kuona fahari watakapokuwa wamemaliza kukisoma kitabu. Baadhi ya walimu waliamua kujaribu kuendesha zoezi hili kwa kutumia kikundi kidogo kimojakimoja na kuzunguka darasani kwa sababu walikuwa na vitabu vichache tu darasani.

Shughuli muhimu: Usomaji kimya endelevu

Kusanya vitabu vinavyosisimua, magazeti na hadithi ambazo zinalingana na kiwango cha wanafunzi wako. Washirikishe wanafunzi na jumuiya katika kukusanya matini zinazofaa au tumia vitabu ambavyo wanafunzi wametengeneza darasani (angalia Nyenzo-rejea 4 ). Tenga dakika 15–20 kila siku au mara tatu kwa wiki kwa ajili ya Usomaji Kimya Endelevu. Waambie wanafunzi wachague matini ya kusoma kwa ukimya. Jisomee mwenyewe wakati wanafunzi wakiwa wanasoma. Mwishoni, kama hawakumaliza kusoma vitabu vyao, waambie watumie alama zilizopo kitabuni ili watakaposoma tena iwe rahisi kujua walipoishia.

Mwambie kila mwanafunzi atoe au achangie kwenye rekodi ya usomaji (angalia Nyenzo-rejea 4).

Kila wiki, watake wanafunzi, katika vikundi vidogo, waambiane kuhusu walichokuwa wanakisoma.

Zungukia vikundi kusikiliza wanayosema wanafunzi. Kagua rekodi zao za usomaji.

Je, wanafunzi wamefurahia shughuli hii na wanasonga mbele katika usomaji wao?

Unawezaje kusaidia zaidi?

Nyenzo-rejea ya 1: Kitu ambacho waandishi na wasomaji wafanisi wanatakiwa kukijua

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Chagua hadithi yenye wahusika na matukio ambayo unafikiri yatawasisimua wanafunzi wako.

Fikiria maelezo ya usuli ambayo wanafunzi watayahitaji ili waelewe na wafurahie hadithi. Amua jinsi utakavyoyatoa kabla ya kuanza usomaji wa hadithi. Kwa mfano, wanafunzi wenye umri mdogo katika baadhi ya sehemu za Afrika watamfahamu kiboko, lakini wengine wanaweza wasielewe, hivyo kabla ya kusoma hadithi ya Kiboko Mkali utatakiwa uchunguze wanafunzi wanajua nini kwa njia ya kuwauliza maswali kama haya:

Maswali ya kujua maarifa waliyo nayo

  • Kiboko anafananaje?
  • Je, kiboko anaweza kukuogopesha? Kwa nini ni ‘ndiyo’ , au kwa nini ni ‘hapana’?
  • Unaweza kumwona kiboko wapi?
  • Kiboko anakula nini? Swali la kwanza linalotabirika
  • Hadithi hii inaitwa Kiboko Mkali. Angalia mchoro kwenye jalada la mbele. (Mchoro unaonesha kiboko akijaribu kujikinga kwa majani ya jamii ya mchikichi.) Unafikiri hadithi itahusu nini?
Imechukuliwa kutoka: Dixie Elementary Magnet School, Book Jackets; Website

Angalizo: Wakati maswali haya yanarejelea hadithi ya Kiboko Mkali, maswali hayahaya yanaweza kuwahusu wanyama, watu, mahali au shughuli zinazohusiana na hadithi yoyote ile.

Fanya mazoezi ya kusoma hadithi kwa sauti kabla ya kuitumia kwenye darasa lako. Fikiria jinsi ya kuigiza sauti za wahusika na vitendo utakavyoweza kuvitumia ili hadithi ionekane kama ya kweli. Kama kwenye hadithi kuna michoro, amua namna ya kuitumia utakapokuwa unasoma hadithi hii darasani kwako.

Angalia sehemu za hadithi ambazo wanafunzi wanaweza kushiriki mara tu watakapoifahamu hadithi hii. Kwa mfano, katika hadithi moja, Tembo Eddie alijaribu kuigiza vitendo vya wanyama wengine au vitendo vya binadamu na kila mara ashindwapo hulia ‘Wah! Wah! Wah! Boo! Hoo! Hoo! Natamani ningejua kitu ambacho ninaweza kufanya!’ Unaweza kuandika kiitikio kama hiki ubaoni kwako ili wanafunzi waweze kufuatilia.

Tafuta mahali kwenye hadithi ambapo unaweza kuwauliza wanafunzi baadhi ya maswali ya utabiri kama vile: ‘Unafikiri Eddie atafanya nini baadaye?’ au ‘Kiboko Mkali atatatuaje tatizo lake?’

Nyenzo-rejea ya 2: Maswali ya kutumia wakati wa usomaji wa kitabu – usomaji wa kwanza, wa pili na wa tatu

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Hapa pana maswali machache unayoweza kuuliza kabla ya kusoma hadithi na wanafunzi na pia mifano ya maswali ya kuuliza baada ya usomaji kumalizika. Aidha pana maswali ya kuwauliza wanafunzi baada ya kuwa wamesoma kitabu mara ya pili au zaidi.

KIPINDI CHA KWANZA CHA USOMAJI

Kabla ya usomaji

  1. Je, jalada linakufanya upende kusoma hiki kitabu? Kwa nini? au kwa nini hapana? Unafikiri jalada linakuambia kitabu kinahusu nini? Kwa vipi?
  2. Niambie kuhusu kile unachokiona katika ukurasa wa kwanza wa hadithi.

Wakati wa kusoma

Uliza maswali kuhusu jinsi hadithi ilivyoundwa na jinsi maneno na picha yanavyochangia katika muundo wa hadithi hii.

Baada ya kusoma

  1. Umependa nini na hukupenda nini kuhusu hiki kitabu?
  2. Je, kuna kitu kilichokushangaza kuhusiana na kitabu hiki? 
  3. Je, kuna ruwaza zozote ambazo umezigundua?
  4. Picha gani unayoipenda zaidi? Unaweza kuniambia unaona nini katika picha hii?
  5. Unafikiri jalada linafaa kuhusiana na kile kilichotokea katika hadithi hii?
  6. Je, maneno au picha zinasisimua? Je maneno yanaeleza hadithi kwa njia mbalimbali? Je, maneno yangekuwa mazuri bila picha? Je, picha zingeendelea kuwa nzuri bila maneno?
  7. Je, hadithi imesimuliwa kwa picha au vyote viwili? Je, hali hii ndivyo ilivyo kwa kitabu kizima?

KIPINDI CHA PILI NA CHA TATU

(Angalizo: Hivi ni lazima viwe vimepishana kwa wiki kadhaa )

Kabla ya kusoma

  1. Umeshafikiri kuhusu kile kitabu tangu tulipokisoma kwa mara ya mwisho?
  2. Ungependa kukisoma tena?
  3. Nisimulie unachokumbuka zaidi kuhusiana na kile kitabu.

Wakati wa kusoma

Uliza tena maswali kuhusu muundo wa hadithi na jinsi maneno na picha vinavyochangia katika muundo huu.

Baada ya Kusoma

  1. Umegundua kitu chochote wakati huu ambacho hukukigundua kabla? 
  2. Unajisikiaje kuhusiana na hadithi hii baada ya kuisoma tena?
  3. Unapofikiria kitabu hiki sasa, ni kitu gani muhimu kuliko vyote kwako kuhusiana na kitabu?

Baada ya kuwa umekisoma kitabu hiki zaidi ya mara moja, je, ungependekeza wanafunzi wengine pia wakisome zaidi ya mara moja na mwalimu wao?

Imechukuliwa kutoka: Swain, C. Gazeti Msingi la Kiingereza (The Primary English Magazine)

Nyenzo-rejea 3: Hadithi

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Andika hadithi ubaoni, lakini usiandike kichwa cha hadithi wala sentensi mbili za mwisho (‘Alitoa shuti – chini kuelekea kulia. Goli zuri!’) ubaoni mpaka sehemu ya mwisho kabisa ya somo lako.

[Kukimbilia utukufu na Mark Northcroft (umri miaka 12 )]

Alikimbia tena na tena. Miguu yake iliuma kama tindikali. Aliweza kusikia waliokuwa wanamfukuzia wakiwa wanamkaribia. Alihisi kuwa asingeweza kukaa nao sana na kwa muda mrefu lakini alijua lazima afanye vile. Hatua zilikuwa zinamkaribia. ‘Haraka! Haraka!’alilia. ‘Siwezi! Siwezi!’ alijibu. Alijisikia nguvu kutoka sehemu fulani ndani ya mwili wake. Sasa alijua kuwa atafanikiwa.

Ghafla mtu alitokea kusikojulikana. ‘Nipate sasa au nisipate kabisa,’ alifikiri.

[Alipiga shuti – chini kuelekea kulia. Goli zuri!]

Tanbihi

‘Miguu yake iliuma kama tindikali’ – Tashbiha hii au ulinganisho huu si rahisi kuueleza lakini unaweza kusema kuwa mwanaume au mvulana huyu alijisikia maumivu katika miguu yake kana kwamba kulikuwa na mchanganyiko wa kemikali iliyokuwa inachemka.

Maswali ya kuwauliza wanafunzi katika maandalizi ya uandishi wa mwanzo na mwisho mbadala wa hadithi hii

  1. Unafikiri ‘A’ ni nani?
  2. Unafikiri yuko wapi?
  3. Unafikiri nini kitamtokea?
  4. Nani ‘mwanamume’?
  5. Watu gani wengine wanaweza kuwa sehemu ya hadithi hii? 
  6. Kutakuwa kumetokea nini kabla ya sehemu hii ya hadithi?
  7. Nini kinaweza kutokea baadaye?

Nyenzo-rejea 4: Usomaji kimya endelevu

Usuli/welewa wa somo wa mwalimu

Kukuza Usomaji Kimya Endelevu darasani kwako ni muhimu katika kuwahamasisha wanafunzi wako wapende kusoma na kuboresha stadi zao za usomaji. Ili Usomaji Kimya Endelevu ufanikiwe kunahitajika kuwe na mpango makini kabla ya usomaji wenyewe. Utahitaji kukusanya pamoja Nyenzo-rejea kwa ajili ya kusomwa na darasa au kikundi chako. Vitu hivi vinaweza kuwa makala toka magazetini, vitabu, n.k. Unatakiwa uwe mbunifu katika kukusanya vitu hivi na pia kuvihifadhi ili visipotee au visiharibike.

Kama una Nyenzo-rejea kwa darasa zima, unaweza kufanya Usomaji Kimya Endelevu mara moja kwa wiki mwanzo au mwisho wa siku. Kama una idadi ndogo ya Nyenzo-rejea, unaweza kuendesha shughuli ya usomaji kwa kutumia kikundi kimoja kwa kila siku na pia kushirikiana na darasa lako kutengeneza vitabu zaidi vya darasa vya kusoma.

Maswali ya kuuliza

Hii ni mifano ya maswali ambayo yanaweza kuulizwa kuhusu aina na viwango mbalimbali vya vitabu vya hadithi, lakini unaweza pia kuwauliza wanafunzi wakupatie maoni mafupi.

  1. Kumetokea nini katika sehemu ya kwanza (utangulizi, mwanzo) wa hadithi hii?
  2. Kumetokea nini katika sehemu ya kati (wapi pana utata au migogoro katika hadithi hii)?
  3. Kumetokea nini katika sehemu ya mwisho (suluhisho)?
  4. Je, kuna tatizo linalohitaji kutatuliwa?
  5. Nini lengo la mhusika mkuu au wahusika?
  6. Kumetokea nini kwa wahusika katika sehemu mbalimbali za hadithi? Wamekumbwa na matatizo gani?
  7. Je, umeshawahi kukutwa na jambo kama hilo?
  8. Kama jaribio lao la kwanza halikufanikiwa, je, mhusika mkuu alipata nafasi nyingine ya kujaribu kufikia lengo lake?
  9. Mwishoni kimewatokea nini wahusika?
  10. Unajisikiaje kuhusiana na hii hadithi? Je, imekufanya utafakari kuhusu maisha yako mwenyewe au ya mtu mwingine? Kama ndivyo, kwa vipi?

Kutunza rekodi ya usomaji

Wanafunzi wanapokuwa wanafanya Usomaji Kimya Endelevu ni muhimu kwao kutunza kumbukumbu ya vitabu ambavyo wameshavisoma na kutoa maoni ya kitu gani walikipenda au hawakukipenda kuhusiana na vitabu hivyo. Pia ni njia ya kujua aina ya vitu wanavyovisoma na aina ya vitu vinavyowasisimua. Utunzaji wa rekodi unakueleza wewe kuhusu wanafunzi wamesoma kwa kiasi gani, hasa ikiwa unawahimiza pia kusoma vitabu, magazeti, n.k ambavyo wanavisoma nyumbani au mahali penginepo. Kwa magazeti, unaweza kupendekeza kuwa wayaongeze kama wanayasoma mara kwa mara na waseme wameyasoma mara ngapi. Wanaweza kupendelea kuongeza makala kutoka kwenye magazeti fulani.

Kutunza kumbukumbu kusiwe kwa kuchosha kwani kutawafanya wanafunzi waache kusoma. Inatosha tu kuandika jina la kitabu na la mtunzi na labda mchapishaji kama unataka kukiweka kitabu hiki katika sehemu yake ya kukihifadhia (kama una bajeti). Wanafunzi wanaweza pia kusema kama walikipenda kitabu na kwa nini, na kama wangependekeza kisomwe na wengine.

Kumbukumbu inaweza kuwa ya darasa moja, ambapo kichwa cha kila kitabu cha maktaba kipo juu ya karatasi na kila wakati mtu anaposoma kitabu hiki anatia saini katika orodha hii na kuandika maoni mafupi. Njia nyingine ni kwa kila mwanafunzi kuwa na ukurasa mwishoni mwa daftari lake ambapo kunakuwa na orodha ya vitabu alivyosoma na kila mara anapomaliza kusoma kitabu au kusitisha kusoma kitabu anaandika maoni pembeni mwa jina la kitabu na jina la mtunzi. Itakuwa vizuri kama wanapotoa maoni waandike tarehe ili uweze kuona wanamaliza kusoma kitabu lini n.k.

Ukusanyaji na uoneshaji wa vifaa kwa ajili ya Usomaji Kimya Endelevu

Kama unahitaji kuanzisha maktaba yako mwenyewe ya darasa, hitaji la kwanza ni kukusanya vitabu na magazeti. Yapo mashirika ambayo yanaweza kuzisaidia shule kupata vitabu. Hapa kuna mawasiliano muhimu:

Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania

Katibu Mtendaji

CBP

S.L.P 78245

Dar Es Salaam, Tanzania simu: (255) 22-2760750

nukushi: (255) 222-761562

baruapepe: cbp@raha.com

Chama cha Kimataifa cha Usomaji

Makao Makuu

800 Barksdale Rd

S.L.P 8139

Newark, DE 19714-8139

Marekani

simu: +1 302-731-1600

Nukushi: +1 302-731-1057 baruapepe: pubinfo@reading.org

Huduma za Maktaba Tanzania

Mkurugenzi Mkuu

S.L.P Box 9283

Dar es Salaam

simu: (255) 22 2150048 9 baruapepe: tlsb@africaonline.co.tz

Kwa taarifa zaidi juu ya Usomaji Kimya Endelevu, wavuti hii inaweza kukusaidia:

www.trelease-on-reading.com

Wakati mwingine balozi za nchi za nje au mashirika yanayohusiana na balozi hizi, kama vile British Council, zinaweza kutoa mchango wa vitabu. Mashirika ya kutoa huduma kama vile Rotary Clubs pia hukusanya na kutoa mchango wa vitabu. Kama huwezi kuwasiliana na kampuni yoyote kwa ajili ya kuomba msaada, basi jaribu kuwaomba wenzako na rafiki zako wakupatie vitabu na magazeti ambayo watoto au wanafamilia wao wameshamaliza kazi nayo. Baadhi ya shule zinawaomba wazazi wawasaidie walimu kuendesha shughuli ya kuchangisha fedha na kisha wanazitumia fedha hizo ambazo zimechangwa kununulia vitabu. Nyenzo- rejea Muhimu: Kuwa mwalimu mbunifu katika hali zenye changamoto inatalii zaidi jambo hili.

Mara tu utakapokuwa na vitabu na magazeti ya kuwatosha wanafunzi wote darasani kwako kwa usomaji binafsi wa wanafunzi, unatakiwa utafakari namna ya kuvitunza vifaa hivi ambavyo ni vya thamani. Kama una shubaka, au unaweza kujitengenezea shubaka (au kutengenezewa na mtu mwingine), unaweza sasa kutandaza vitabu na magazeti hayo ili kuwavutia wanafunzi. Mashubaka yanaweza kupangwa pembeni au nyuma ya darasa lako. Ndani ya daftari la mazoezi andika vichwa vya habari vya vitabu na magazeti ili uendelee kuvifuatilia. Mwisho wa kipindi cha Usomaji Kimya Endelevu, kuwa makini katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanarudisha vitabu kwenye shubaka.

Kama huna mashubaka, hifadhi vitabu na magazeti hayo kwenye maboksi. Unaweza kuwatumia baadhi ya wanafunzi kama watunzaji wa vitabu kwa kukusaidia kugawa vitabu kila kipindi cha usomaji kinapoanza na kuvihifadhi kwenye maboksi baada ya kipindi kumalizika.

Sehemu ya 3: Njia za Usomaji na upokeaji wa taarifa za matini

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kujiongezea stadi za uulizaji maswali ili kuwasaidia wanafunzi kutumia kwa njia inayofaa taarifa za matini

Maneno muhimu: taarifa za matini; ufahamu; muhtasari; maswali; tathmini

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kujiongezea uwezo wa kutunga maswali na kazi ambazo zinahimiza usomaji wa matini kwa makini na majibu binafsi;
  • Kugundua njia za kufundisha wanafunzi namna ya na kuandika juu ya taarifa zinazotolewa kwa muundo tofauti;
  • Kuwasaidia wanafunzi kuendeleza stadi zao zinazohitajika kufupisha matini;
  • Kutumia njia hizi kutathmini ujifunzaji.

Utangulizi

Katika ‘muda wa taarifa’ sote tunahitaji kuweza kusoma na kushughulikia taarifa ziwasilishwazo katika miundo mbalimbali. Kusoma taarifa kutoka katika jedwali au mchoro kunahitaji stadi tofauti ukilinganisha na usomaji wa hadithi.

Ukiwa mwalimu, kazi yako ni kuwasaidia wanafunzi kuelewa wanachokisoma, kufanya muhtasari wa mawazo muhimu ya matini na kutoa maoni yao. Ingawa ni muhimu kwa wanafunzi kuweza kuandika majibu ya maswali kuhusu walichosoma, wengine watatoa kazi bora zaidi kama watapewa nafasi ya kuonesha walichoelewa kwa kutumia shughuli nyingine, k.m. kutengeneza mabango au chati.

Sehemu hii inapendekeza njia za kuwasaidia wanafunzi kuimarisha stadi za ufahamu na muhtasari.

Somo la 1

Mazoezi ya ufahamu ni ya kawaida sana, lakini yanasaidiaje stadi za usomaji wa mwanafunzi?

Uchunguzi kifani 1 inaonesha kuwa unahitaji kufikiri kwa makini hasa kama kweli maswali ya ufahamu katika usomaji wa vitabu yanasaidia kujua wanachoelewa wanafunzi kutokana na usomaji huo. Unahitaji kutunga maswali au shughuli ambazo zinahitaji wanafunzi kusoma taarifa za matini kwa uangalifu. Shughuli 1 inakuonesha mifano ya kujaribu na kuitumia wakati unapotunga maswali yako na shughuli nyinginezo. Nyenzo Rejea Muhimu: Kutumia maswali ili kusaidia kufikiri inakupa mawazo zaidi.

Uchunguzi kifani ya 1: Kufiria upya kuhusu ‘ufahamu katika usomaji’

Katika warsha huko mjini Lusaka, Zambia, walimu wa Kiingereza kama lugha ya nyongeza walisoma matini ambayo haina maana na kujibu maswali kuhusu matini hiyo. Sentensi ya kwanza katika matini hii ilikuwa: ‘Some glibbericks were ogging blops onto a mung’ na swali la ufahamu lilikuwa nani alikuwa ‘ogging blops onto a mung?’ Kila mwalimu alijua jibu ‘some glibbericks’ . Katika majadiliano yao, waligundua kuwa wangeweza kutoa jibu sahihi kwa sababu walijua kuwa katika Kiingereza ‘some glibbericks’ ilikuwa ni kiima cha sentensi. Hawakuhitaji kujua nani au ‘glibberick’ kilikuwa ni kitu gani ili kutoa jawabu!

Baada ya majadiliano, walifanya kazi katika vikundi, ya kutunga maswali na kazi nyinginezo ambazo zingewaonesha kama wanafunzi wanaelewa au hawelewi matini iliyotumika katika kazi hizi. Walijifunza kuwa maswali yasiruhusu wanafunzi kunakili tu taarifa ya sentensi moja katika matini.

Walitayarisha kazi ambapo wanafunzi walijaza jedwali, walitengeneza bango au kutayarisha muhtasari wa kutumia katika mdahalo kama njia ya kuonesha walichojifunza kutoka katika matini waliosoma.

Walitafakari kuwa maswali waliyouliza na shughuli nyingine walizotayarisha zilimaanisha kuwa waliweza kutathmini welewa wa wanafunzi.

Shughuli ya 1: Kufahamu na Kupokea taarifa za matini

Soma Nyenzo rejea 1: Matini kuhusu takataka . Toa nakala za makala na kazi au andika aya na kazi ubaoni.

Zifunike.

Kabla ya wanafunzi kusoma makala, uliza maswali ya utangulizi. Maswali yako yawasaidie wanafunzi kuoanisha wanayoyajua na taarifa mpya iliyomo katika matini (Angalia Nyenzo rejea 2: Maswali ya utangulizi ). Kama wanafunzi ni wenye umri mdogo au unahitaji kuwasomea matini, unaweza kuandika majibu yao ubaoni.

Baada ya hapo, funua makala na kazi ulizotayarisha, na kuwataka wanafunzi wasome makala hiyo kimya na kuandika majibu ya kazi hizo. Watakapokuwa wamemaliza, kusanya vitabu vyao na tathmini majibu yao

Rudisha vitabu na /au toa maoni yako kwa darasa zima kuhusu waliyofanya vizuri na jadili matatizo yoyote waliyokumbana nayo. Angalia majibu ya kazi hii yaliyopendekezwa katika Nyenzo rejea 1 )

Katika somo linalofuata, watake wanafunzi wafanye kazi katika makundi madogo madogo kutengeneza bango linalokataza utupaji ovyo wa takataka na lioneshe darasani (Angalia Nyenzo rejea 3: Mabango mazuri ).

Somo la 2

Fikiria taarifa mbalimbali za matini ulizokwisha soma. Taarifa hizi ama zikiwa katika kurasa za vitabu, au katika vipeperushi vya matangazo, au katika skirini za kompyuta, mara nyingi huambatanisha vielelezo,chati, grafu, michoro, picha au ramani. Kufanikiwa kama wasomaji, wewe pamoja na wanafunzi wako mnahitaji kuelewa jinsi maneno, tarakimu na sanamu zionekanazo (kama picha au michoro) zinavyofanya kazi pamoja kuwasilisha taarifa. Sasa waandishi wengi wa elimu wanasisitiza umuhimu wa vielelzo vya kufundishia kusoma na kuandika. Kujifunza jinsi ya kusoma na kuitika picha na michoro ni sehemu mojawapo ya kujua kusoma na kuandika. Kusoma na kuitika michoro, grafu na vielelezo ni njia nyingine. Chati ya pau na pai ni baadhi ya chati rahisi kuelewa na kutengeneza ili kufanya muhtasari wa taarifa.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutengeneza chati ya pai kuwasilisha namba ya tarehe za kuzaliwa za wanafunzi kwa kila mwezi

Mwalimu Maria Mutagwa anapenda kuwafanya wanafunzi wake wa Darasa la 6 kujisikia vizuri. Darasani kwake ana karatasi kubwa ikionesha mwezi na siku ya kuzaliwa kwa kila mwanafunzi. Kila siku ya kuzaliwa ya wanafunzi mmojawapo wanafunzi wenzake huimba wimbo wa “heri ya siku ya kuzaliwa.” Siku moja, mwanafunzi mmoja alitoa hoja kuwa katika baadhi ya miezi wanaimba wimbo huo mara nyingi kuliko miezi mingine. Maria aliamua kutumia hoja hiyo kufanya hesabu na kazi ya maonesho ya kihesabio katika chati za pai.

Kwanza, aliandika jina la mwezi ubaoni na baadaye aliwataka wanafunzi wamweleze ni wanafunzi wangapi walikuwa na siku yao ya kuzaliwa kwa kila mwezi. Aliandika namba mbele ya mwezi husika (k.m. Januari 5; Februari 3, na kadhalika).

Baadaye alichora mduara mkubwa ubaoni na kuwataka wanafunzi kufikiria kuwa hiyo ilikuwa chati ya pai na kwa kuwa walikuwa wanafunzi 60 darasani kutakuwa na sehemu 60 katika chati ya pai, moja kwa kila mwanafunzi.

Sehemu zitaunganishwa kutengeneza vijisehemu (vipande). Kutakuwa na vijisehemu 12, kwa sababu kuna miezi 12 kwa mwaka. Kila kijisehemu kitawakilisha idadi ya wanafunzi waliokuwa na siku ya kuzaliwa katika mwezi husika, lakini kila kijisehemu kitakuwa na ukubwa tofauti. Alianza na mwezi palipoangukia siku za kuzaliwa nyingi. –mwezi wa Septemba. Katika mwezi wa Septemba, wanafunzi 12 walikuwa na siku zao za kuzaliwa.

Wanafunzi walipata wazo haraka la kutengeneza vijisehemu 12 vya ukubwa tofauti ndani ya mduara ili kuwasilisha idadi ya siku za kuzaliwa za kila mwezi kama asilimia ya darasa. Walinakili chati ya pai katika daftari zao na kuchora kila kijisehemu kwa rangi tofauti.

Wanafunzi walizungumzia taarifa nyingine ambazo wangeweza kuziingiza katika chati ya pai na waliamua kutambua wanafunzi wangapi walicheza michezo tofauti, wangapi waliunga mkono kila timu katika michuano ya mashindano ya mpira Tanzania na wanafunzi wangapi wanazungumza lugha tofauti katika sehemu zao.

Shughuli ya 2: Kufahamu na kutengeneza chati ya pai

Nakili chati ya pai ya Nyenzo rejea 4: Chati ya pai ubaoni .

Waulize wanafunzi kwa nini mchoro huu unaitwa chati ya pai.

Tunga maswali (sehemu b) kuhusu chati ya pai ubaoni na waulize wanafunzi kufanya kazi katika jozi na kuyajibu.

Jadili majibu darasani.

Tumia ubao wako kuwaonesha wanafunzi jinsi ya kubadili majibu haya katika aya kuhusu wikiendi ya Thomas. Watake wanafunzi wako wachore chati ya pai.Kwa kazi ya nyumbani watake wanafunzi kuchora chati ya pai kuonesha jinsi wanavyotumia muda wao wa wikiendi.

Baada ya kukagua kazi za nyumbani, watake wanafunzi wabadilishane chati zao na wenzao na kuandika aya kuhusu wenzao wanavyotumia muda wao wa wikiendi. Umejifunza nini kuhusu shughuli hizi? Utafanya kitendo gani wakati ujao kinachohusiana na shughuli hizi? (Angalia Nyenzo rejea 4 kwa mawazo zaidi).

Somo la 3

Kujifunza kutafuta na kufanya muhtasari wa mawazo makuu kutoka katika sura za vitabu na vitini vingine kunakuwa muhimu kwa wanafunzi kwa jinsi wanavyopanda madarasa shuleni. Stadi hizi zinahitaji mazoezi kuzimudu.

Shughuli Muhimu na Nyenzo rejea 5: matini kuhusu mbuyu inatoa mifano ya njia ya kuwasaidia wanafunzi jinsi ya kufanya muhtasari wa taarifa za matini. Utahitaji kufanya shughuli hiyo mara nyingi. Kwa wanafunzi wakubwa, unaweza kuwaomba wenzako kukuonesha wanafunzi unaowafundisha wanahitaji kusoma nini katika masomo mengine kama vile masomo ya jamii au sayansi. Baadaye unaweza kutumia aya kutoka masomo ya fani ya jamii au vitabu vya sayansi kwa ajili ya kufanya kazi ya muhtasari katika somo la lugha kwa kufuata hatua zilizomo katika Shughuli Muhimu.

Uchunguzi kifani ya 3: Kufupisha mawazo muhimu kutoka katika sura za vitabu

Wanafunzi wa darasa la Mwalimu Emmanuel Chadwali walikuwa na wasiwasi kuhusu mitihani inayofuata. Walimwambia kuwa hawelewi walimu wao walimaanisha nini walipowaambia kupitia (kudurusu) sura za vitabu vyao. Emmanuel aliamua kutumia matini ya taarifa kutoka katika kitabu cha Kiingereza ili kuwapa wanafunzi wake baadhi ya mawazo kuhusu jinsi ya kutafuta na kuandika mawazo muhimu ya matini.

Aliwauliza wanafunzi wake kumwambia shabaha ya jedwali la yaliyomo, vichwa vya sura na sura ndogo katika vitabu vyao. Ilikuwa wazi kutokana na ukimya wao kwamba wanafunzi wengi walikuwa hawajawahi kufikiria jambo hilo. Wachache waliweza kusema kuwa majedwali haya humsaidia msomaji kupata mawazo kuhusu mada muhimu za kitabu. Emmanuel aliwaambia wanafunzi kuwa ili kusoma tena sura, wanapaswa kuandika vichwa vya habari katika ukurasa, wakiacha nafasi kati ya kichwa kimoja na kingine, wafunike daftari zao na kujaribu kuandika mawazo muhimu katika yale waliyosoma.

Baadaye, wanapaswa kucheki maelezo yao waliyoandika dhidi ya mawazo yaliyomo katika kitabu na kufanya masahihisho katika maandishi yao kwa kuongezea chochote muhimu walichosahau au wafute kile ambacho wameandika kwa makosa. Emmanuel alisema kuwa wanafunzi wengine hupendelea kuandika mawazo yao kwa njia ya michoro ya ramani ya mawazo ambapo kuna uhusiano wa mawazo muhimu. (Angalia Nyenzo rejea 5 na Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia ramani ya mawazo na)

Mwisho, aliwakumbusha kuwauliza walimu wao kuelezea chochote ambacho hawakukielewa. Emmanuel aliwaelezea pia jinsi alivyoandika kumbukumbu kuhusu mambo ya wanafunzi wake aliyoyagundua na ujifunzaji wao ili kumsaidia kupanga masomo zaidi.

Shughuli muhimu: Kuboresha stadi za kuandika muhtasari

Kabla ya somo , nakili matini kutoka Nyenzo rejea 5katika mbuyu au iandike ubaoni. Jaribu shughuli hizo kabla.

Kwa kuwaonesha wanafunzi kurasa za magazeti na majarida, waulize kwa nini matini yana vichwa vya habari na yanawaambia nini wasomaji wake.Watake wapendekeze kwa nini vitabu vyao vina vichwa vya habari na vichwa vidogo vya habari.

Watake wanafunzi wasome matini ya taarifa kuhusu mbuyu na kufanya kazi katika jozi kuamua ni aya zipi zinajadili mada ileile. Watake waandike kichwa cha habari kinachofupisha aya kwa kila mada. Watake baadhi ya wanafunzi wako kusoma kwa sauti vichwa vyao vya habari na kuviandika ubaoni.

Kubalianeni ni vichwa vipi bora vya habari kwa kila aya vinavyohusu mada ileile. Viache vichwa vya habari bora ubaoni ukiacha nafasi kwa kila kimoja. Watake wanafunzi washauri mawazo muhimu kutoka kwenye aya na kuyarekodi. Waonesha wanafunzi jinsi ya kuhusisha vichwa vya habari na mawazo muhimu katika ramani ya mawazo ili kuwasaidia kukumbuka kuhusu mbuyu.

Nyenzo-rejea ya 1: Matini kuhusu takataka

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Takataka

Takataka ni aina ya vitu vilivyoachwa au mabaki ya vitu visivyofaa ambavyo watu hawaviweki mahali pake, kama vile kwenye pipa la takataka. Watu ambao wanadondosha takataka kama vile ganda la tunda au kopo tupu kwenye udongo wana hatia ya kuchafua mazingira. Wakati mwingine tunawaita watu hawa “wadudu waharibifu”.

Takataka hazitokei tu

Watu ndio wanaohusika na takataka. Takataka kama kipande cha karatasi inayofungia chokoleti, si takataka kama kitatupwa katika pipa la takataka. Kinakuwa takataka kama kitatupwa ovyo kwenye ardhi, anakiacha

kikielea kwenye ardhi ambapo amekuwa akikaa au anakitupa nje ya dirisha.

Takataka zinaweza kuleta madhara kwa watu

Glasi zilizovunjika na vipande vya mabati vyenye ncha kali ambavyo vimeachwa katika sehemu ambazo watu wanapita- na hasa watoto wadogo wanapochezea- vinaweza kuwakata. Sehemu hizi zilizokatwa zinaweza kuleta maambukizo ya hatari. Takataka za matunda na mboga kuna wakati huteleza na kama watu wakizikanyaga wanaweza kuanguka na kuvunja mguu au mkono. Takataka zinaweza kuleteleza ajali barabarani wakati madereva wanapotaka kuendesha magari yao au malori kuepuka vifaa vyenye ncha kali vinavyoweza kupasua matairi ya magari yao. Mifuko ya plastiki na vipande vya mbao hupeperuka mbele ya kioo cha mbele cha gari na huzuia madereva kuona vizuri.

Takataka zinaweza kuwa hatari kwa wanyama na ndege

Vipande vya glasi na makopo vinaweza kukata miguu au midomo ya wanyama wafugwao au wa porini wakati wakiwa machungani. Nyavu za nailoni za kuvulia zinazotupwa ardhini au kwenye maji zinaweza kusokota midomo au miguu ya ndege na zinaweza kusababisha vifo vyao kwa sababu hawawezi kutembea au kula. Wanyama wa baharini, kama vile sili na papa, wanaweza kunaswa katika nyavu chakavu za kuvulia. Kama hawakujinasua watakufa.

Hatari za plastiki

Takataka za plastiki zinaleta matatizo kwa samaki, ndege na watu. Katika mito na baharini, zinaweza kuleta madhara kwa samaki kwa sababu wanaweza kukanaswa na kushindwa kutoka. Takataka zilizoko ufukoni mwa bahari zimesababisha vifo vya shakwe wa baharini. Hata mifuko ya plastiki, ambayo huwekwa mboga na matunda, inaweza kuwa hatari kwa ndege. Ndege hawa huingia ndani yake na wanashindwa kupata njia ya kujitoa kwa kuwa plastiki ni ngumu. Vipande vya plastiki au mifuko ya plastiki inaweza kujipenyeza kwenye injini za boti na zinaweza kusababisha injini kutofanya kazi.

Kama tunataka kuweka nchi yetu katika hali ya usafi na inayopendeza na kuwalinda watu wetu na wanyama, lazima tuache kutupa takataka ovyo. Si vigumu kutupa kopo, chupa, mfuko wa plastiki au kipande cha karatasi kwenye pipa la takataka badala ya kuvitupa ardhini.

Kazi za uandishi kuhusu Takataka

Orodhesha aina saba za takataka zinazotajwa katika makala (kujibu swali hili kwa uhakika wanafunzi wanahitaji kutafuta taarifa katika aya mbalimbali, kwa hiyo wanapaswa kusoma kwa makini).

Fafanua maana ya takataka. (wanafunzi wanaweza kunakili jawabu kutoka katika aya ya kwanza ya matini bila kujua maana ya neno hilo lakini swali linalofuata linaweza kukusaidia kujua welewa wao kwa sababu unawataka watumie neno au maneno kutoka kwenye lugha wanazozifahamu - kwa wanafunzi lugha yao ya awali.)

Ni neno lipi (au maneno yapi) yanayotumika kwa neno takataka katika lugha nyinginezo unazozijua.

Orodhesha aina tatu za takataka ambazo zina madhara kwa ndege. (Ndege wametajwa mara nyingi katika aya, sio tu katika aya yenye kichwa cha habari kinachoelezea ndege. Wanafunzi wanahitaji kutafuta kila rejeo kuhusu ndege na hivyo kuhusisha tofauti hii na tofauti mbalimbali za takataka na matatizo yayosababishwa na takataka hizo.

Kwa maneno yako mwenyewe fafanua njia tatu ambazo watu wanaweza kudhurika nazo. (Wanafunzi watumie vichwa vidogo kuwaelekeza na wajaribu kuelezea maudhui ya aya katika maneno yao wenyewe badala ya kunakili kutoka katika aya. Hii itakusaidia kung’amua kama wameelewa walichosoma).

Unakubaliana na mwandishi kuwa si vigumu kutupa takataka katika pipa la takataka? Toa sababu za jibu lako. (Hili ni swali linalohitaji maoni ya wanafunzi binafsi kutafakari na kuelezea maoni yao).

Pendekeza kinachoweza kufanywa kuhusu mazao ya takataka kama vile vichupa, karatasi, plastiki, maganda ya matunda na mboga mboga (hili nalo ni swali linalohitaji majibu binafsi na linahimiza majadiliano darasani kuhusu mada za mzunguko wa mazingira).

Zingatia kuwa majibu ya swali la 1 mpaka la 5 yanahitaji wanafunzi wasome matini kwa uangalifu wakati swali la 6 hadi la 7 yanawahitaji kutumia maoni yao.

Majibu ya kazi za kuandika

Maganda ya matunda na mbogmboga, vichupa, makopo, plastiki, neti za kuvulia, makaratasi, vipande vya mbao.

Takataka ni vitu visivyohitajika ambavyo watu hawaviweki katika mahali pake panapohitajiwa (kama vile katika pipa la takataka).

Maneno yatokanayo na lugha zinazotumika darasani mwako.

Nyavu za nailoni za kuvulia, mifuko ya plastiki, vikapu vya kusuka na mifuko ya matunda.

Watu wanaweza kujikata kutokana na chupa zilizovunjika au makopo yenye ncha kali. Watu wanaweza kuteleza kutokana na takataka za matunda na mbogamboga na wanaweza kuvunja mikono au miguu. Watu wanaweza kupata ajali za barabarani wakati madereva wakitaka kukwepa takataka barabarani au ikiwa hawawezi kuona kwa sababu ya takataka zilizopeperushwa katika kioo cha mbele cha gari. Watu wanaosafiri baharini na boti wanaweza wasifike salama nchi kavu kama injini ya boti imeharibiwa na palastiki. (Njia nne zimeelezwa hapa.) Hili ni swali ambalo wanafunzi wahimizwe kutoa maoni mbalimbali. Kwa mfano, haiwezekani kuweka takataka katika pipa la takataka kama hakuna mapipa hayo katika uwanja wa shule au mitaani.

Kazi zinakupa wewe na wanafunzi nafasi ya kujadili njia mbalimbali za kutumia tena bidhaa ambazo zinakuwa takataka. Kwa mfano, maganda ya mbogamboga na matunda yanaweza kufanywa lundo la mbolea au kuwekwa moja kwa moja katika udongo shambani ili kurutubisha udongo. Plastiki zinaweza kusukwa katika mikeka au mazulia. Katika baadhi ya majiji na miji vipande vya chupa, kopo, na karatasi au vipande vya mbao vinaweza kuchukuliwa katika sehemu ambapo vinakusanywa na kutumika upya na watu wanaweza kulipwa kwa takataka wanazo kusanya na kuzipeleka katika mahali husika.

Imetokana na Taitz, L. et al New Successful English, Learner’s Book, Oxford University Press

Nyenzo-rejea ya 2: Maswali ya utangulizi

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Uliza maswali haya kabla ya kuanza kusoma ili kuwasaidia wanafunzi kuhusisha yale wanayoyajua na yale watakayosoma katika matini ya taarifa kuhusu takataka.

Je, kuna aina yoyote ya takataka katika eneo la shule au katika mazingira ya nyumbani?

Takataka hizo zilifikaje hapo?

Kama hakuna takataka, ni sababu ipi ya usafi wa mazingira hayo kuzunguka mazingira ya shule au nyumbani?

Ni neno gani lingine la takataka ambalo linatumika shuleni au mitaani? (kama wanafunzi hawajui, onesha ‘takataka’ ubaoni au katika nakala ya makala.)

Je, ni matatizo gani yanayoweza kusababishwa na takataka?

Nyenzo-rejea 3: Mabango mazuri

Usuli/taarifa ya msingi/ welewa wa mwalimu

Sifa za bango zuri

Karatasi yote inatumiwa.

Maneno yameandikwa kwa herufi kubwa.

Mara nyingi maneno si sentensi zote.

Picha zinapaswa kuwa rahisi, wazi na zenye mvuto (nguvu).

Rangi za maneno na picha zivutie uangalifu.

Nafasi ya maneno na picha katika karatasi lazima zivutie uangalifu. (Hii inaitwa ‘muundo’ wa bango.)

Mfano wa bango/picha iliyotayarishwa na mtoto nchini Tanzania.

Imechukuliwa kutoka: Rehydration Project, Website

Ndama anywe maziwa ya ng’ombe.

Kichanga cha binadamu anywe maziwa ya (mama yake) binadamu.

Hatua za kufuata katika somo la kuchora na kuwasilisha mabango na ni kitu gani wanafunzi wanaweza kujifunza kutokana na shughuli hii.

Waambie wanafunzi kuwa watafanya kazi katika vikundi kuchora bango linaloelezea kutotupa takataka ovyo.

Anza na majadiliano ya darasa zima. Ni kitu gani kinafanya bango kuwa zuri? Ni taarifa zipi zitafaa katika bango ambazo zitawahimiza watu kuacha kutupa takataka ovyo?

Kipe kila kikundi karatasi kubwa au kadi na hakikisha kuwa wana penseli na peni.

Wakati vikundi vinafanya kazi, zungukazunguka darasani kusaidia ikiwa ni lazima na kuzingatia wanafunzi wanavyojifunza.

Wakati vimemaliza kazi, watake kila kikudi kuonesha kazi zao darasani na kuzungumzia kwa nini wametengeneza mabango yao katika hali hiyo.

Yabandike ukutani mabango hayo darasani au shuleni. Wanafunzi wanaweza kuonesha kuwa wanajifunza:

Jinsi ya kufanya kazi kwa kushirikiana katika vikundi vidogo;

Msamiati mpya;

Kuna aina gani za takataka (kwa kuelewa taarifa kutoka katika matini na kwa kutumia ujuzi wao);

Kunaweza kufanyika nini kuzuia kutupa takataka ovyo;

Jinsi ya kuzungumzia mabango yao.

Wanafunzi wameonesha ujifunzaji upi?

Umejuaje?

Ni sehemu zipi wanazohitaji marekebisho?

Utawasaidiaje?

Nyenzo-rejea 4: Chati ya pai

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

a) Chati ya pai: Jinsi Thomas anavyotumia muda wake wakati wa mwisho wa juma (wikiendi)

taarifa muhimu kulala 30%

kutembelea marafiki 15%

kucheza mpira 15%

kusaidia kazi za nyumbani na shambani 5%

kuangalia televisheni 10% kufanya kazi za nyumbani 2%; kutengeneza gari 5% kumtembelea babu 10%;

kula 8%

b) Maswali kuhusu chati ya pai.

Chati ya pai inatwambia nini? (Jinsi Thomas anavyotumia muda wake wakati wa wikiendi)

Thomas anatumia muda wake mwingi zaidi akifanya nini? (Kulala)

Anatumia muda mchache zaidi akifanya nini? (kazi za nyumbani)

Anafanya nini kwa muda sawa kama aangaliavyo televisheni? (Kumtembelea babu).

Anafanya nini kwa muda awa kama asaidiavyo kazi za nyumbani na shambani? (Kutengeneza magari ya waya)

Wakati akiwa macho, ni mambo gani mawili ambayo Thomas hutumia muda mwingi kufanya? (Kuwatembelea marafiki na kucheza mpira)

Ukitengeneza chati ya pai ya kuonesha unavyotumia muda wako wakati wa wikiendi, Je, chati hiyo itafanana na ya Thomas au itakuwa tofauti? (majibu ya aina mbalimbali yatatokea)

c) Aya kuhusu wikiendi yaThomas

Thomas anapenda wikiendi. Anafurahia kukaa ndani ya kitanda cha joto kwa muda mwingi kuliko asubuhi siku za shule na kula chakula na familia. Anatumia muda wake mwingi akiwatembelea marafiki na kucheza mpira. Anaangalia televisheni na familia yake wakati wa jioni na wakati mwingine anakaa sana usiku. Jumamosi asubuhi yeye na dada zake huwasaidia wazazi kusafisha nyumba au kusaidia kazi za shambani.

Wanapomaliza, dada zake hupendelea kwenda madukani lakini yeye hupenda kuwatembelea marafiki zake au hutumia sehemu ya muda wake akitengeneza magari ya waya na malori ili kumuonesha babu yake anapomtembelea siku ya Jumapili. Kwa kawaida anahitaji kupata wakati siku ya Jumapili jioni kufanya kazi zake za nyumbani.

Baadhi ya taarifa katika aya hii haziwezi kupatikana kutoka katika chati.Waandishi wameongezea vipengele kutokana na ujuzi wao na data iliyotolewa. Unahitaji kugundua hili pamoja na wanafunzi wako. Waulize wanachoweza kusema kutokana na chati na ni vipengele gani vimeongezwa.

d) Mnaweza kujifunza nini wewe na wanafunzi wako kutokana na shughuli hizi.

Kusoma taarifa za chati ya pai.

Kulinganisha kipengele kimoja cha taarifa na kingine kutoka katika chati.

Kutengeneza chati ya pai ili kufupisha taarifa.

Kuelewa kuwa taarifa ileile inaweza kutolewa kwa namna mbalimbali.

Kutumia taarifa kutoka katika chati ya pai ili kuandika aya.

Kujifunza namna ya kueleza muda (k.m. kutumia maneno ‘mara nyingi’, ‘wakati mwingine’).

e) Mawazo kwa ajili ya shughuli nyinginezo

Ili kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi kuhusu chati za pai, wanaweza kutengeneza nyingine- labda kuhusu tarehe za kuzaliwa za wanafunzi au timu za michezo wanazoshabikia au lugha wanazozizungumza. Unaweza pia kuwaonesha njia nyingine za kuwasilisha taarifa kama vile kutumia grafu ya baa au jedwali kama una taarifa nazo. Marafiki zako wanaweza pia kukusaidia.

Nyenzo rejea 5: Matini kuhusu mbuyu

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Kabla hujaanza Shughuli muhimu, unaweza kutumia Nyenzo rejea 1 kama mfano na kujadiliana na wanafunzi wako jinsi vichwa vidogo vya habari vinavyoweza kufanya muhtasari wa mawazo muhimu.

Mbuyu

Mbuyu sio mti wa kawaida. Baadhi ya watu hufikiria kuwa ni mbaya kwa kuwa ni mnene na muda mwingi huwa hauna majani. Unaonekana pia kutukua kwa utaratibu mzuri juu. Kwa hakika baadhi ya watu wanaishi katika sehemu ambazo kuna miti hii wanasema kuwa hukua kinyume matawi yake yakiwa ardhini na mizizi yake ikiwa juu.

Mbuyu unafanya vitu tofauti ukilinganisha na miti mingine. Miti mingi hushiriki mchavuko kwa kusaidiwa na nyuki na ndege ambao huchukua punje za chavua toka mti mmoja hadi mwingine ili miti irutubishwe na kutengeneza maua mengine, matunda au kokwa. Mibuyu husaidiwa na popo. Wakati wa mwanzo wa kiangazi mti huu hutoa maua makubwa yenye petali.

Maua huchanua usiku wakati popo wanapotokea. Popo hufyonza nekta na husafirisha chavua kutoka mti mmoja hadi mwingine katika mabawa yao na mwilini.

Mbuyu huishi kwa muda mrefu. Baadhi ya mibuyu mikubwa inaweza kuwa na umri wa miaka zaidi ya 3,000. 

Mbuyu una matumizi mengi. Miaka iliyopita baadhi ya watu wa kabila la Khoi na San wa Afrika ya kusini walitumia mibuyu kujengea nyumba. Waliweka moto ndani ya mti wa mbuyu ili kulainisha sehemu za ndani ya mti, na kutengeneza tundu ambamo waliishi. Pamoja na kuwa na shimo kubwa ndani, mti huo uliendelea kukua.

Ganda la mti lina matumizi mengi. Linaweza kutumiwa kutengeneza zulia, karatasi na uzi. Unyuzi wa ganda unatengeneza kamba ngumu.

Sehemu nyingine za mti zina matumizi mengine. Mizizi ikisagwa, inatengeneza uji laini. Sehemu laini ya ndani ni kinywaji cha wanyama wenye kiu wakati wa majira ya ukame . Mbegu zikivundikwa majini kwa siku kadhaa, zinakuwa dawa za kutibu homa. Majani yakikaushwa na kusagwa, yanatengeneza kahawa nzuri lakini chungu. Majani yakichemshwa yanafanana kama kabeji na yanaweza kuliwa. Nchini Tanzania, wakati mwingine maganda yakisagwa yanatumika kama dawa ya kusugulia meno.

Kuna hadithi nyingi kuhusu mbuyu. Watu wa Venda Afrika ya kusini wanasema kuwa miti hii ilikuwa ni mahali pa maficho ya mizimu. Halafu mungu alikuja na kuchimbua miti hiyo toka ardhini na kuipanda upya kinyume, yaani mizizi juu na matawi chini. Kutokana na kitendo hicho, mizimu haikuweza kujificha katika miti hiyo.

Watu wengine husema kuwa ukifyonza mbegu hutashambuliwa na mamba, na ukinywa kinywaji kilichotengenezwa kutokana na maganda ya mbuyu utakua hadi kuwa mtu mkubwa na mwenye nguvu (cheo.) Mbuyu ni mti wa maajabu. Ni mmojawapo wa miujiza ya Afrika.

Vichwa vidogo vya habari vilivyopendekezwa kwa ajili ya matini ya mbuyu

Aya 1: Mbuyu hufananaje?

Aya 2: Jinsi poleni zinavyosafirishwa kati ya miti ya mbuyu?

Aya 3: Maisha ya mbuyu

Aya 4, 5, 6: Matumizi ya mbuyu

Aya 7, 8: Hadithi na imani kuhusu mibuyu

Zingatia: Hakuna taarifa katika aya ya mwisho. Aya hiyo inaonesha angalizo la mwandishi, akitoa maoni yake kuhusu mti huo.

Muhtasari wa ramani ya mawazo ya mbuyu

Imechukuliwa kutoka: Ellis, R. & Murray, S. Let’s Use English, Learners’ Book 5

Sehemu ya 4: Njia za kuwasilisha mtazamo wako

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuwasaidia wanafunzi wako wawe wawasilishi wa mawazo wanaojiamini na makini?

Maneno muhimu: hisia binafsi, mitazamo, mdahalo, barua, gazeti, uhusishaji

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kuwasaidia wanafunzi katika kueleza mawazo yao katika mazungumzo na maandishi;
  • Kuimarisha uwezo wako kuwasaidia wanafunzi kuelewa hali za watu wengine, hisia na maoni yao;
  • Kutumia majadiliano kuchunguza masuala ya uhusishaji.

Utangulizi

Sehemu hii inahusika na jinsi tunavyoeleza hisia na kuwasilisha mitazamo yetu. Ni muhimu kuwa walimu na wanafunzi kuweza kutenda hili kwa kujiamini, kwa mazungumzo na kwa maandishi, ili kushiriki katika kutoa maamuzi katika familia, shule na jamii pana. Ukiwa mwalimu, una wajibu mkubwa katika shauri hili. Unahitaji kuweza kutoa hoja kuhusu shauri lako shuleni katika masuala kama nyenzo na njia za kufanya kazi, na pia unahitaji kuwasaidia wanafunzi wako kadiri wanavyokuza stadi hizi.

Ni muhimu kuwa wanafunzi wajihisi wanashirikishwa darasani na katika jamii, licha ya hali zao za kiafya, haIi zao za nyumbani au kutojiweza kwa aina yoyote.

Somo la 1

Sehemu hii inatalii njia za kufanya kazi zitakazowasaidia wanafunzi kuelezea hisia zao na kugundua mawazo yanayohusu mambo mengi, ikiwa ni pamoja na yanayohusu maisha yao. Inazingatia jinsi ya kushughulikia migongano na mikanganyiko kwa njia iliyo bora zaidi.

Mara nyingi, unapoanza mada ambazo zinagusa masuala nyeti, inasaidia kuacha wanafunzi wagundue kwa siri mawazo yao kwanza. Kwanza, kuandika mawazo kuhusu suala kunaweza kusaidia kuchochea fikira. Hii ni mbinu ambayo inaweza kutumiwa kwa mada nyinginezo ili kugundua wanachojua wanafunzi kwanza.

Uchunguzi kifani ya 1: Uandishi ili kueleza hisia na mawazo

Mwalimu Mariam Uledi wa Dar es Salaam, alijadiliana na wanafunzi wake wa darasa la 7 mambo ambayo yanawafanya wajihisi tofauti na/au kutengwa.

Baadaye, aliwataka waangalie picha ya mtoto aliyekaa peke yake wakati wenzake wakicheza ( Nyenzo-rejea 1: Mtoto ‘alitengwa’ ), na kuwataka kuandika kuhusu mtoto huyu.

Aliwauliza pia kama zamani walikwisha jihisi kama watu waliotengwa au wako tofauti na wengine au kama sasa wanajihisi hivyo. Aliwataka waandike kuhusu hisia hizo.

Halafu walicheza michezo ambayo iliwasaidia kupata ujuzi wa hali yamtu mlemavu (Angalia Nyenzo-rejea 2: Michezo inayowezesha kusaidia kuelewa ulemavu wa viungo) .

Baadaye, walizungumzia jinsi ulemavu huo unavyoweza kuwafanya watoto kujisikia tofauti na wakati mwingine kuwafanya watengwe na wenzao wa darasa. Walizungumzia juu ya watoto ambao wanaishi na virusi vya VVU/UKIMWI, au wale ambao wazazi wao wamekufa kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Mariamu aliwataka waandikie kuhusu ujuzi wao wakati wa michezo. Walijisikiaje kuwa na ulemavu?

Baada ya haya, kabla ya kuanza mada nyeti, mara nyingi Mariam huwataka wanafunzi wake kuandika au kuzungumza wawiliwawili au katika vikundi vidogo ili kutalii mawazo yao kwanza.

Shughuli ya 1: Kuandika ili kuibua mawazo na hisia

Wakati wa kuanza mada nyeti na wanafunzi ni vizuri kwanza kutalii mawazo na hisia zao.

Chagua picha, shairi au hadithi ili kuamsha hamasa ya kufikiri kwao. (Angalia mfano mmoja kutoka katika Nyenzo-rejea 1 ).

Waoneshe/wasome shairi au hadithi na uwatake wafikirie lina maana gani kwao.

Watake waandike au wazungumze na wenzao kuhusu mawazo yao na husisha na hisia zao pia.

Wakumbushe kuwa hakuna mtu yeyote atakayesahihisha au kuhukumu wanayoelezana. Ni kwa ajili yao kwa wakati huo kufikiri juu ya wanayofikiri na kuhisi.

Halafu, jadili pamoja na wanafunzi wanafikiri ni ujumbe upi unapatikana katika picha hizo.

Somo la 2

Kujifunza namna ya kushiriki katika midahalo kunawasaidia wanafunzi (na walimu) kueleza maoni yao, kusikiliza maoni ya wenzao na kufikiri kwa umakinifu. Unapochagua mada za midahalo darasani kwako, hakikisha unachagua mada ambazo ni muhimu kwa wanafunzi wako ili waweze kueleza maoni yao.

Katika Shughuli ya 2 utawaeleza wanafunzi wako sheria na kanuni za kufanya mdahalo na kuwasaidia wanapojitayarisha kufanya mdahalo huo. Katika Uchunguzi-kifani 2, mdahalo unahusu kushirikishwa darasani. Kwa watoto wadogo, unaweza kuendesha majadiliano rahisi au mdahalo kuhusu masuala kama kutopigana.

Nyenzo-rejea 3: Muundo wa hotuba za midahalo na Nyenzo-rejea 4: Sheria na kanuni za kuendesha midahalo utakupa mwongozo. Unaweza pia kuziona sheria na kanuni hizi kuwa za manufaa kama ni mwanachama wa chama cha kuendesha midahalo.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutayarisha na kuendesha midahalo

Baada ya mwalimu Mariam Uledi na wanafunzi wake kuandika juu ya ‘kutengwa/kutoshirikishwa’, walijadili hasa kuhusu watoto ambao hawakuwa shuleni kwa sababu kadhaa. Baadhi ya wanafunzi hawa walikuwa walemavu, wengine hawakuwa na wazazi na walikuwa ndio wanaolea/wanaosimamia familia na wengine hawakuja shuleni kwa kuwa walikuwa masikini kiasi cha kutoweza kununua sare ya shule.

Mariam alianzisha wazo la kufanya midahalo katika darasa, na kuwasilisha mada yenye kichwa kinachosema: ‘ Darasa hili linaamua kuwa “vijana wote walio nje ya shule”, waliotengwa kwa sababu ya vizingiti vya kujifunza, lazima warudishwe shuleni.’

Aliwaweka wanafunzi 36 katika vikundi sita, na akawataka nusu ya vikundi kujadili mawazo yanayounga mkono mada ya mdahalo na nusu kujadili mawazo yanayopinga mada ya mdahalo.

Baadaye aliwapa mwongozo wa kutayarisha hotuba yao (Angalia Nyenzo-rejea 3). Kila kikundi kiliandika hotuba yake, ama ya kuunga mkono au ya kupinga mada ya mdahalo, na kumchagua msemaji kutoka katika wanachama wa darasa. Mwalimu Mariam aliziangalia hotuba zao wakati wa muda wa chakula, na akawashauri wazungumzaji jinsi ya kuziboresha. Wakazirekebisha zaidi nyumbani.

Mdahalo ulifanyika siku iliyofuata. Mariamu alifurahishwa na kiwango cha juu cha ushiriki wa wanachama wote wa darasa. Hoja ilipita, na wanafunzi walianza kuwasiliana na watoto ambao hawakuwa mashuleni, na kufanya kazi na walimu wao na mwalimu mkuu ili kuwarejesha shuleni. Mariam aligundua kuwa mdahalo umeleta nafasi nzuri kwa wanafunzi kuendeleza na kueleza hoja zao na kushughulikia suala muhimu la kijamii.

Shughuli ya 2: Kufanya mdahalo wa hoja; kueleza maoni

Wafafanulie wanafunzi kuhusu kushiriki katika mdahalo

Changiana mawazo kuhusu mada zinazowafurahisha na wasaidie kujieleza katika muundo wa hoja. Amua mada za mdahalo (Angalia Nyenzo-rejea 3 ).

Fafanua sheria na taratibu za kufanya mdahalo, kwa kutumia taarifa iliyomo katika Nyenzo-rejea 4.

Andika sheria kuu na kanuni/taratibu ubaoni ili wanafunzi wazinakili kwa ajili ya marejeo katika siku za usoni.

Watake wanafunzi watayarishe hotuba za mdahalo katika vikundi na mchague msemaji mmoja kuwasilisha majadiliano yao.

Unaweza kuwasaidia kwa kuwaeleza taarifa ya utangulizi ili waitumie katika hotuba zao.

Hakikisha kama vikundi viko tayari kuanza mdahalo (labda mwishoni mwa wiki) na fuata sheria na kanuni/taratibu.

Watake wanafunzi wakueleze walichojifunza kutokana na tajiriba hii na itumie taarifa hiyo kupanga masomo ya siku za usoni na nafasi za kujadili mawazo.

Kwa watoto wadogo, unaweza kufanya mdahalo na mada zinazohusu shule, kama kwa mfano ni lazima wawe na kanuni za darasa. Unaweza kuwasaidia kujifunza namna ya kupeana nafasi ya kuzungumza na kusikiliza maoni ya wengine.

Somo la 3

Ni muhimu kujifunza namna ya kueleza hoja kwa uwazi, ukithibitisha mawazo yako. Hii ni stadi inayofaa wakati wa kuandika insha za wanafunzi, lakini pia, unapokuwa mtu mzima, kama unaandika barua kuhusu mada ya mdahalo wa kijamii au wa kitaifa hasa barua ya kuchapishwa katika gazeti.

Barua ya gazetini inaweza kulinganishwa na sehemu ya kwanza ya mdahalo.

Mara nyingi mtu mwingine atajibu barua iliyochapishwa gazetini na atatoa hoja mbadala. Katika Nyenzo-rejea 5: Mfano wa barua kuna barua katika gazeti ambayo wanafunzi wanaandika kuhusu masuala muhimu ya kuwaingiza wanafunzi wote shuleni.

Uchunguzi-kifani 3 na Shughuli muhimu inatoa mwongozo wa jinsi ya kufanya kazi na wanafunzi ili watoe hoja kwa njia ya barua.

Uchunguzi kifani ya 3: Kujifunza kuandika barua kwa mwalimu mkuu au katika gazeti

Miezi michache baada ya mwalimu Mariam Uledi kutoa wazo la kuwarudisha wanafunzi shuleni, kulikuwa na wanafunzi wageni wawili darasani kwake. Mmoja alikuwa hasikii, na mwingine alikuwa na mkono mmoja. Yeye na wanafunzi walikuwa wanaanza polepole kuwashirikisha darasani, kuzungumza nao, na kuwasaidia bila kuwafanya kujihisi kuwa wao ni ‘tofauti’ kabisa. Aliwashauri wanafunzi kuandika barua kwa mwalimu mkuu au gazetini kuhusu mada ya umuhimu wa kuwarudisha wanafunzi wote shuleni. Wangeweza kutuma barua yao kwa mwalimu mkuu au katika gazeti la Nipashe jijini Dar es Salaam, au katika gazeti la Tanzania Daima . Watapaswa kuandika kwa Kiswahili.

Wanafunzi walilipenda wazo hili na walijadiliana kuhusu watakayosema. Waliandika vidokezo vya barua.

Dhamira: Shule zijitahidi kuwarejesha shuleni ‘watoto ambao hivi sasa hawasomi.

Sababu.

‘Njia za kukabili maoni ya kupinga

Tajiriba yetu.

Kufaulu na changamoto.

Kurudia dhamira.

Mariam aliwaelekeza wanafunzi aina za virai vya kutumia, hasa namba 2 na 3, ambapo walikuwa wakiwasilisha mawazo. Walimuomba mwalimu aliyekuwa na kompyuta kuwachapia kazi yao, na kutuma nakala magazetini (Angalia barua katika Nyenzo-rejea 5 ).

Shughuli muhimu: Barua kwa mwalimu mkuu au gazetini ili kutoa hoja

Chagua mada ambayo imekwisha jadiliwa na wanafunzi katika mijadala yao na toa hoja ya kutoa mawazo yao katika barua kwa mwalimu mkuu au, kama kuna gazeti la mahali hapo, itume katika gazeti.

Uwatake wabunge bongo, katika vikundi, mambo wanayotaka kuyaandika. Baadaye andika muundo wa barua ubaoni ukitumia vidokezo vilivyomo katika Uchunguzi-kifani namba 3 (ingawa dhamira yako inaweza kuwa tofauti).

Wanafunzi wanaweza kuandika barua hii katika lugha nyingineyo (k.m. Kiingereza) hivyo wasaidie kuwapa virai vya kutumia katika utangulizi na katika hoja zao (Tazama Nyenzo-rejea 6: Virai vinavyotumika katika ‘majadiliano’ )

Vitake vikundi kutathmini barua zao na barua za watu wengine, na amua ipi ni bora ya kutuma kwa mwalimu mkuu au katika magazeti (Tazama Nyenzo-rejea 6 kwa maelekezo). Utahitaji kufanya uhariri kabla hujatuma barua, lakini jitahidi kubakiza maneno ya wanafunzi.

Fikiria wanafunzi wamejifunza nini katika kubadili majadiliano ya mdahalo hadi kwenye barua. Kwa watoto wadogo au wale wasiojiamini na wasiokuwa na uwezo wa kuandika, unaweza kulifanya kama zoezi la darasani ukiandika mawazo yao. Tumia shughuli hii kuendeleza msamiati wao katika lugha husika.

Nyenzo-rejea ya 1: Mtoto ‘aliyetengwa’

Nyenzo ya Mwalimu kwa ajili ya kupanga/kurekebisha na kutumia na wanafunzi

Vyanzo vya asili: Umthamo 6, Chuo Kikuu cha Fort Hare, Mradi wa Elimu ya Masafa Marefu

Nyenzo-rejea ya 2: Michezo inayohimiza uelewa wa ulemavu wa viungo

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia na wanafunzi kwa ajili ya kupanga/kurekebisha

Unaweza kuwasaidia wanafunzi kuelewa baadhi ya matatizo ambayo wanafunzi wenye ulemavu wanayapata katika kucheza michezo kama inayoelezwa hapa chini:

  1. Leta shuleni baadhi ya soksi ndefu za zamani au vipande vya kamba au sufu. Wape vifaa hivi wanafunzi na watake kuifunga mikono yao wanayoitumia kuandika nyuma ya migongo yao. Mpe kila mwanafunzi kipande cha karatasi. Waeleze kuwa mchezo huu unahusu kutaka kujua nani anaweza kuandika kwa mwandiko mzuri sentensi ambazo uko karibu kuzitaja kwa haraka. Zisome sentensi hizo na sasa angalia kutatokea nini! Baada ya kumchagua mshindi, jadiliana na wanafunzi wako walivyojisikia wakati wakicheza mchezo huu na hali ikoje kwa wanafunzi wenye ulemavu au wanaopungukiwa mkono, kama hawawezi kuandika, watake kuchora mti.
  2. Leta shuleni baadhi ya vipande vya nguo au skafu (au waambie wanafunzi kuleta vifaa hivyo) ili nusu ya wanafunzi hao waweze kufunika macho na vipande hivyo. Lichukue darasa nje. Watake wanafunzi kufanya kazi wawiliwawili. Yule ambaye amefungwa macho yake anatakiwa kutembea akipita katika vizingiti mbalimbali ulivyoweka, huku akiongozwa na mwenzake. Katika zoezi hili unaweza kutumia madawati na viti.
  3. Zingatia muda kwa kila kikundi. Kama darasa lako si kubwa sana watake wanafunzi wako wabadilishane majukumu hayo na zingatia muda tena kwa kila kikundi. Mshindi ni kikundi cha wawiliwawili waliomaliza majukumu yote kwa muda mfupi zaidi, bila kujikwaa katika kizingiti chochote. Baada ya hapo, waulize wanafunzi walijisikiaje kwa kufunikwa macho na kumtegemea mwenzao.
  4. Leta shuleni manyoya ya pamba ya kutosha kwa kila mwanafunzi ili waweze kuweka manyoya masikioni mwao ili kuwazuia kusikia vizuri. Halafu watake wanafunzi kukusikiliza wakati ukiwapa wanafunzi taarifa ya kuandika. Mshindi ni mwanafunzi wa kwanza kumaliza kuandika taarifa bila makosa. Baadaye waulize wanafunzi walijisikiaje walipokuwa hawasikii vizuri na wangefanya nini kumsaidia mwanafunzi mwenye matatizo ya kusikia.
  5. Kama shule yako inaweza, nunua pipi nyingi. Mpe za kutosha kila mwanafunzi ili midomo yao iwe imejaa pipi. Waambie wasimung’unye wala kumeza pipi yoyote bali kumwambia mwenza taarifa uliyoandika ubaoni. Hili ni gumu kulifanya na watagundua inakuwaje unapokuwa na matatizo ya kuzungumza ambayo yanamzuia mtu kusema vizuri. Mwishoni, wanakula pipi hizo!

Nyenzo-rejea ya 3: Muundo wa hotuba za mdahalo

Usuli/taarifa ya mwanzo/uelewa wa mwalimu

Maelezo ya hoja

Bungeni, au katika kamati muhimu, wakati wajumbe wanatoa maamuzi, mmoja anaweza kutoa hoja ya kujadiliwa. Hoja ni tamko kuhusu kitu kinachopaswa kufanywa au kujadiliwa. Mdahalo unatalii sehemu zote za mjadala. Kwa mfano, kama mbunge akisimama na kusema: ‘Natoa hoja kuwa adhabu ya viboko ifutwe,’ wazo hili linajadiliwa na uamuzi unafikiwa, ambao unatoa suluhisho linalotakiwa kutekelezwa au kutotekelezwa.

Taarifa zifuatazo ni mifano ya masuala unayoweza kutumia shuleni. Unaweza kurekebisha hizi kwa kutegemea ukubwa wa darasa lako na umri wa wanafunzi wako.

Wazazi wasitumie adhabu ya viboko kuwafundisha nidhamu watoto. Tunayojifunza nyumbani ni muhimu kuliko tunayojifunza shuleni.

a) Wanaounga mkono mada ya mdahalo

Eleza mada: Nakubaliana na hoja kuwa vijana wote walio nje ya shule, wanatengwa kwa sababu ya vizingiti vya kujifunza, warudishwe shuleni.

Fafanua istilahi. Katika hali hii utahitaji kueleza una maana gani unaposema vijana walio ‘nje ya shule’, na vizingiti vya kujifunza. (Hili linapaswa kufanywa na mzungumzaji wa kwanza)

Toa sababu za kuunga mkono mada: k.m. sababu yangu ya kwanza katika kuunga mkono mada hii ni........

Sababu ya pili, …

Sababu ya tatu, …

Fanya hitimisho ya sababu zako za kuunga mkono mada: Kwa ufupi au kwa kuhitimisha ....

Eleza tena mada ya mdahalo: Kwa hiyo narudia tena au kwa hiyo nawasihi nyote kuunga mkono mada ambayo inasema kuwa.......

b) Wanaopinga mada ya mdahalo

Eleza msimamo wako kuhusu mada: Napinga mada inayosema kuwa........AU Nawaunga mkono wanaopinga mada kwamba........

Fafanua istilahi. Katika hali hii utahitaji kueleza una maana gani unaposema vijana walio ‘nje ya shule’, na vizingiti vya kujifunza. (Hili linapaswa kufanywa na mzungumzaji wa kwanza). Wote wanaohusika wanahitaji kukubali ufafanuzi wa istilahi.

Toa sababu zako za kupinga mada: k.m. sababu ya kwanza ya kupinga mada hii ni...

Sababu ya pili,...

Sababu ya tatu, …

Fanya hitimisho la sababu zako za kupinga mada: Kwa ufupi au kwa kuhitimisha...

Eleza tena msimamo wako: Ninarudia tena AU ninawasihi nyote kutounga mkono mada inayodai kuwa .........

Nyenzo-rejea ya 4: Sheria na taratibu za kuendesha mdahalo

Usuli/taarifa ya mwanzo/uelewa wa mwalimu

Mdahalo ni mashindano, au, labda, ni kama mchezo ambapo wazungumzaji wawili au zaidi hutoa hoja zao kwa nia ya kushawishiana...

Kwa nini tunafanya midahalo?

Kwa kujitayarisha na kushiriki katika midahalo wanafunzi wanajifunza kutumia taarifa kuunga mkono hoja zao. Wanajifunza namna ya kuwasilisha mawazo yao kwa uwazi na kwa ushawishi mkubwa.

Kwa kushiriki katika midahalo, wanajifunza kuelewa mawazo ambayo ni tofauti na yao kwa sababu, wakati wa kufanya mdahalo, wanaweza kujadiliana kwa kutoa hoja kwa jambo ambalo hawakubaliani nalo kikamilifu, na wanapaswa kuelewa mawazo ya wenzao wa timu ya wasiokubali hoja zao.

Matayarisho

Wafanya midahalo wazuri wanajitayarisha vizuri. Mdahalo unaofanya darasani unaweza usiwe rasmi, lakini unaweza kuwajenga wanafunzi katika hali inayowafanya wanafunzi wako wafanye mdahalo rasmi katika mashindano.

Kabla ya kuandaa hotuba, wafanya midahalo wanakusanya taarifa nyingi kwa kadri iwezekanavyo, kutoka katika maktaba, magazetini, na kwa kujadiliana na watu.

Wanafikiria hoja zote zinazounga mkono mada yao, na zile zinazopinga hoja yao. Kwa maana nyingine ni kuwa, wanaelewa hoja za wapinzani wao pamoja na hoja zao. Wanajitayarisha kwa maswali yoyote wanayoweza kuulizwa na wapinzani wao, na changamoto zozote zinazoweza kutolewa.

Wafanya midahalo wazuri wanatayarisha hoja zao katika muundo mzuri wa ushawishi. Wanawasikiliza watu wengine wanaofanya mdahalo, ili wajifunze ufundi na stadi za kufanya mdahalo. Wanajiunga na vyama vya kufanya midahalo, na kufanya midahalo mara kwa mara.

Mchakato

Kuna timu mbili, kila timu ina wazungumzaji wawili au watatu. Timu moja (chanya) inaafiki hoja, na timu nyingine (hasi) inapinga hoja.

Kuna mwenyekiti, ambaye anaendesha utaratibu.

Hotuba na muda wa hotuba hizo unagawanywa sawasawa kwa timu zote mbili.

Kila mzungumzaji anatoa hotuba upande wake umeandaa kuunga mkono hoja zao.Pande zinazungumza kwa zamu, wakianza na anayependekeza hoja (chanya, hasi, chanya, hasi). Kila mzungumzaji ana muda maalum wa kuzungumza (k.m. dakika tatu au tano)

Baadaye mdahalo unaweza kufunguliwa kwa washiriki wengine, kwa wasemaji kusimama na kutoa hoja zao za kuunga mkono au kupinga mada ya mdahalo. Kila mzungumzaji kutoka upande wa wasikilizaji anapewa muda maalum wa kuzungumza ( k.m. dakika moja au dakika tatu).

Kila timu inaweza pia kuzungumza kwa kujibu hoja za wapinzani wao, baada ya kila timu kupewa muda kidogo wa mashauriano. Hii ina maana kuwa wana nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wapinzani wao. Kila timu inaweza kupewa nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wenzao mara moja au zaidi. Nafasi ya kwanza ya kupinga hoja wanapewa wale wanaopinga mjadala na nafasi ya mwisho inatolewa kwa wanaunga mkono mjadala.

Kanuni muhimu

Timu inayounga mkono mjadala haitakiwa kubadili hoja zao. Aidha ile inayopinga mjadala nayo pia hairuhusiwi kubadili hoja zao. Wanapaswa kupinga kabisa mjadala licha ya maoni yao binafsi).

Ikiwa mzungumzaji anatoa tamko, wanatakiwa kutoa ushahidi au sababu za kuunga mkono tamko hilo.

Taarifa zinazotolewa katika mdahalo lazima ziwe sahihi.

Wazungumzaji hawaruhusiwi kuleta hoja mpya wakati wa kujibu/kupinga hoja za wenzao.

Hoja ya utaratibu na hoja ya taarifa

Yeyote anayehusika na mdahalo anaweza kuingilia kati wakati msemaji akizungumza kwa kunyoosha mikono na kusema kuwa ‘anataka kutoa hoja’. (Hii ni ‘hoja ya utaratibu’). Hii ina maana kuwa anataka kueleza kuwa moja ya kanuni za mdahalo imevunjwa (k.m. mzungumzaji amezidisha muda wake wa maongezi, au hana ushahidi wa kuthibitisha hoja zake).

Wana-mdahalo wanaweza pia kunyoosha mikono yao wakitaka kutoa ‘hoja ya taarifa’ (swali au taarifa za ziada wanazoweza kutoa). Msemaji anaweza kuamua kumruhusu mwanachama kuzungumza, lakini halazimiki.

Uamuzi

Timu inayoshinda katika mdahalo inaamuliwa na jaji au majaji kwa kutegemea ubora wa mjadala.

Aidha inaweza pia kuamuliwa kwa kupigiwa kura.

Vyanzo vya asili: Trivium Pursuit, Website.

Nyenzo-rejea ya 5: Mfano wa barua- iliyoandikwa na darasa la mwalimu Mariam

Mfano wa kazi za wanafunzi

Barua hii ni kwa ajili ya kutumwa katika gazeti, lakini unaweza kuandika barua yako kwa mwalimu mkuu kuhusu jambo jingine ukitaka.

Mhariri

Nipashe

Dar es Salaam

Ndugu

Yah.: Shule ziwalete wanafunzi wanaokaa majumbani

Katika Tanzania, elimu ya msingi ni bure. Ni kwa ajili ya watoto wote. Lakini bado kuna watoto ambao wamekaa majumbani, bila kusoma. Baadhi wana ulemavu, wengine wana wazazi wao wenye virusi vya UKIMWI, na wazazi wengine ni masikini mno kiasi cha kutoweza kuwanunulia watoto wao sare za shule.

Shule lazima ziwalete watoto hawa mashuleni, ili wapate elimu na wenzao. Kwa nini tunasema hivyo?

Kwanza, ni haki yao ya kidemokrasia kuelimishwa. Waziri wa elimu anasema kuwa watoto wote lazima wajumuishwe darasani.

Pili na muhimu zaidi, wahitaji kuwa na marafiki na kuwa sehemu ya maisha.

Baadhi wanasema kuwa walimu hawajui kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu. Wengine wanasema kuwa wazazi hawataki watoto wao kuwa na marafiki ‘walemavu’ Lakini hatutaki jumuiya yetu iwe ile ya kubagua. Kila mmoja lazima ashughulikiwe kwa namna ileile.

Watoto wanaweza kuwasaidia wenye ulemavu, na kulifanya kuwa jambo jepesi kwa mwalimu.

Darasa la saba katika shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam iliwakuta watoto wawili wakiwa peke yao nyumbani. Tuliwahimiza kuja shuleni. Kibena alikuwa na mkono mmoja. Tunamsaidia kujifunza kuandika na kucheza michezo. Ni hodari na anajifunza kwa haraka.

Masanja ni mlemavu asiyesikia, lakini akikuangalia midomo yako, anaweza kusikia. Anajitahidi. Pia amekuwa hodari wa kusoma. Tunaweza kumuandikia ujumbe. Tunajifunza mambo mengi kutoka kwa watoto hawa, na marafiki zetu.

Bado ni vigumu kwao, na mwalimu anawapa msaada wa ziada baada ya shule. Kamati ya shule inawasaidia pia kwa kuwanunulia sare za shule. Bado hawana sare za shule.

Tunafurahi kuwa wamekuja darasani mwetu, na tunataka kuziambia shule nyingine kufanya kama tulivyofanya sisi.

Wako

Darasa la 7, Shule ya msingi Bunge

Nyenzo-rejea ya 6: Vifungu vya utoaji hoja

Usuli/maarifa ya somo kwa ajili ya uelewa wa mwalimu

Vifungu vya mabishano

Tunasisitiza kuwa ... …

Sababu zetu kwa kusema haya ni: Kwanza, ............Pili,.......Mwisho na muhimu zaidi, ................ …

Katika (jina la gazeti), la (tarehe), (jina la mtu) ameandika kuwa .....AU (jina la mwandishi/mtunzi), katika kitabu chake (jina la kitabu), anasema ... hii inaonesha kuwa.....AU hii inathibitisha kuwa .....

Wengine wanasema kwamba ...... Lakini sisi tunaamini kuwa.......

Uzoefu wetu umeonesha kuwa.........

Maswali ya tathmini

Je, barua inaanza kwa kueleza waziwazi hoja, au majadiliano? Inawasilisha hoja za kuunga mkono kauli hii?

Inajumuisha baadhi ya taarifa ambazo zinahusisha hali ya mazingira ya mahali panapohusika au matukio na kuyaeleza kibinadamu?

Inaeleza hoja tena, kwa uhakika zaidi, katika aya ya mwisho?

Je, ina muundo mzuri, imegawanywa katika aya, kila aya ikiwa na wazo kuu?

Je, ni sahihi, bila kuwa na makosa ya sarufi, tahajia au uakifishi?

Sehemu ya 5: Njia za kuwa msomaji na mwandishi makinifu

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuendeleza stadi za umakinifu wa kufikiri wa mwanafunzi wakati wa usomaji na uandishi

Maneno muhimu: usomaji makinifu; uandishi makinifu; maoni/mitazamo; uulizaji (maswali); tathmini     

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kutumia maswali kuwasaidia wanafunzi wako kuwa wasomaji makinifu wa matini mbalimbali;
  • Kuwasaidia wanafunzi wako kubuni na kuandika hadithi, matini na barua za taarifa ambazo zinatokana na matini walizosoma kwa umakinifu na hivyo kukuza stadi za kufikiri;
  • Kutumia njia mbalimbali za kutathmini ujifunzaji.

Utangulizi

Waandishi wote - wawe wa hotuba za kisiasa, matangazo ya biashara, makala za magazeti, vitabu vya shule au vyuo (vikuu), hadithi za watoto, au aina nyingine yoyote ya matini - huandika kwa kuzingatia mtazamo fulani na kwa nia fulani. Ni muhimu kuweza kubainisha mtazamo wa mwandishi na kuamua kama unakubaliana nao au hukubaliani nao.

Kufikiria uzoevu wako na imani zako na uliyojifunza katika masomo yako kunaweza kukusaidia kuuliza maswali makinifu kwa kila kitu unachosoma. Itakusaidia kama mwalimu kukumbuka kuwa wanafunzi wako wanaweza kuwa na mawazo ambayo ni halali kama yako. Ukiwafundisha wanafunzi wako kuuliza maswali kuhusu wanachosoma na kufikiria misimamo mbalimbali, utakuwa unawasaidia kuwa raia wanaofahamu kwa makini mambo mengi.

Unaweza kuanza jambo hili hata kama wanafunzi ni wadogo. Ukiwa unawasomea hadithi, wahimize wajadiliane yapi wanayakubali na yapi hawayakubali.

Shughuli tatu katika sehemu hii ni mifano ya njia za kuwasaidia wanafunzi wako kuwa wasomaji na waandishi makini wa matini.

Somo la 1

Wakati wewe na wanafunzi wako mnasoma hadithi, unaweza kuwasaidia kutambua nani amehusishwa katika hadithi na amehusishwaje, na nani hakuhusishwa.

Unaweza kuwasaidia kuona jinsi mandhari ya hadithi (shule, kijiji, mji, n.k.) yanavyoelezwa. Unaweza pia kuwasaidia wanafunzi kwelewa mtazamo au msimamo wa mwandishi, kufikiria kama kunaweza pia kukawa na maoni mengine na, kama yapo, ni yapi.

Unapofanya hivyo na wanafunzi, unawasaidia kuendeleza stadi za kufikiri na stadi za kuuliza maswali makinifu. Utajifunza pia wanafunzi wanapendelea nini na misimamo yao ni ipi. Unaweza kutumia njia hii kutimiza zaidi matakwa yao.

Uchunguzi kifani ya 1: Kusimulia hadithi kutokana na misimamo tofauti

Mwalimu Pinkie Motau wa Soweto, Afrika ya Kusini ana makasha matatu ya vitabu vya hadithi darasani mwake. Wakati mwingine anasoma vitabu hivi kwa darasa lake la 4 na wakati mwingine wanafunzi wanasoma wenyewe. Hadithi zinahusu watoto na familia, zinahusu wanyama na zinahusu viumbe vya kufikirika kama vile mazimwi.

Siku moja alipokuwa akisoma hadithi kuhusu mamba, Sizwe alisema alijisikia vibaya kuhusu mamba kwa kuwa kila wakati mamba alionekana ‘mbaya’. Wengine walisema kuwa hii ilikuwa sahihi kwa kuwa mamba ni mnyama hatari, lakini wengine walisema hii haikuwa halali kwa sababu mamba wanapaswa kujilinda kama wanyama wengine wanavyofanya. Hali hii ilimpa wazo mwalimu Motau. Aliwataka darasa kutoa maoni ya jinsi hadithi ingesimuliwa kutokana na msimamo wa mamba mwenyewe. Wanafunzi walikanganyikiwa, kwa hiyo akasema, ‘Jifikirie kuwa wewe ni mamba katika hadithi hii. Unataka kuwaambia nini wanyama wengine kuhusu hali yako?’ Swali hili liliwasaidia wanafunzi kutoa maoni. Baada ya majadiliano darasani, mwalimu Motau aliwataka kufanya kazi katika vikundi vya watu watanowatano, kuchora na kuandika hadithi ambayo itaonesha kuwa mamba ni mnyama ‘mzuri’.

Kwa kubadilishana mawazo, waliandika hadithi na kuchora picha na vielelezo kuhusu hadithi hizo zenye ubunifu wa hali ya juu.

Wakati mwalimu Motau alipokuwa akisoma hadithi hizo, alifikiria maneno na michoro ‘vilimwambia’ nini kuhusu uwezo wa wanafunzi wa kubuni hadithi kutumia msimamo wa mamba mwenyewe. Siku iliyofuata, alisoma hadithi za kila kikundi kwa sauti na kuonesha picha na vielelezo. Baada ya kusoma kila hadithi, aliliambia darasa zima kikundi kimefanikiwa katika mambo yapi, na pia aliwataka wanafunzi kutoa maoni yao kuhusu maandishi na picha za kila kikundi.

Mwishowe, hadithi hizo zilitengenezwa kitabu kwa ajili ya maktaba ya darasa.

Shughuli ya 1: Kuwa msomaji makinifu wa hadithi

Tafuta hadithi ambapo wahusika, mandhari na matukio vimeandikwa na kuchorwa kutokana na msimamo mmoja (k.m. wanyama wazuri, wazazi wa mwanafunzi mtukutu).

Isome hadithi hii kwa wanafunzi darasani, ukihakikisha kuwa umewaonesha michoro.

Waulize maswali yanayowachochea kufikiri kimakinifu kuhusu hadithi ilivyoandikwa na vielelezo vilivyochorwa. (Angalia Nyenzo-rejea 1: Uulizaji wa maswali kwa mifano ya maswali ambayo ungetumia.)

Baadaye, watake wanafunzi kufanya kazi katika vikundi vya wawiliwawili kwa kuandika barua kwa mhariri, wakifafanua wanachotaka/wasichotaka kuhusu jinsi barua waliyosoma ilivyoandikwa na vielelezo vilivyochorwa. Andika barua ubaoni na jadili mawazo na wanafunzi kabla ya wanafunzi katika vikundi vyao kuanza kuandika barua (angalia Nyenzo-rejea 2: Vidokezo vya barua kwa mwandishi ) au kwa watoto wadogo iandike rasimu hiyo pamoja.

Wanafunzi wamefanikisha nini katika masomo haya ya usomaji na uandishi makinifu? Umejuaje? Una ushahidi gani?

Wamefanya kitu chochote kilichokushangaza, kilichokupendeza au kilichokuchukiza? Kuna kitu ambacho ungefanya tofauti kama ungekuwa unafundisha masomo haya tena?

Somo la 2

Hadithi zote husimuliwa kwa kuzingatia msimamo fulani. Maoni yetu kama waandishi na wasomaji yanaweza kuathiriwa na hali mbalimbali; maoni haya hutegemea kama ni sisi vijana au wazee, wanaume ama wanawake, ni wanachama wa chama fulani cha siasa, ni waumini wa dini Fulani, tunafurahia shughuli fulani, tuna afya njema au afya mbovu, tunafanya kazi au hatufanyi kazi, n.k. Ni muhimu wanafunzi wakajifunza kuwa hadithi zinaweza kuhadithiwa kwa njia mbalimbali kwa kuhusishwa na msimamo fulani au kutohusishwa nao. Ni kweli pia kuwa katika maisha halisi kuwa kuna njia zaidi ya moja ya kulitazama suala fulani na njia mbalimbali za kutatua tatizo.

Unaweza kuwasaidia wanafunzi wakajifunza hili kwa kuwapa nafasi ya kusimulia hadithi ileile au hadithi inayofanana kutokana na mitizamo tofautitofauti au kwa kubadilisha hadithi.

Uchunguzi kifani ya 2: Kumbadilisha ‘mhusika wa nje’ kuwa mhusika mkuu katika hadithi.

Mwanafunzi mmojawapo aitwaye James katika darasa la 6 la Mwalimu Fortunate Mabuso, ameumia sana kutokana na ajali ya gari na angeweza kutembea kwa magongo. Siku moja, alimwambia mwalimu Mabuso kuwa alijisikia vibaya kwa kuwa hadithi zote kuhusu wavulana zilieleza namna walivyofurahia shughuli ambazo hawezi kuzifanya. Mwalimu Mabuso alighadhabika kwa kuwa hakuwahi kulifikiria jambo hili. Alimuuliza alikuwa akifanya nini wakati akiwa nyumbani na akagundua kuwa alikuwa mwanamuziki hodari ambaye alijua kupiga ngoma na filimbi ya chuma. Alimuuliza anaweza kucheza kwa kutumia filimbi hiyo darasani. Kwanza alikuwa na aibu kuhusu jambo hili lakini mwisho akakubali kuwa anaweza.

Katika somo lake lilifuata la Kiingereza, Mwalimu Mabuso aliwaambia kuwa anataka kuwapa mawazo ya kuandika hadithi. Alimwomba James kuwachezea ngoma. Wanafunzi walishangaa na kufurahia uhodari wa James.

Mwalimu Mabuso aliwataka wafikirie hadithi ambapo James, mwanamuziki, alikuwa mhusika mkuu. Darasa zima lilibadilishana mawazo halafu wakafanya kazi wawiliwawili na kuanza kuandika hadithi na/au kuchora

Wakati wa somo, baadhi ya wanafunzi walikwenda kwa James na mwenzake kuomba ushauri wa mambo zaidi ya kuandika hadithi yao. Katika somo lililofuata, wanafunzi katika vikundi vya wawiliwawili, waliendelea na majadiliano yao na kuandika na kuchora hadithi zao binafsi.

Wakati mwalimu Mabuso alipokuwa akisoma hadithi, aligundua kuwa kulikuwa na wanafunzi wengine darasani ambao labda nao walijisikia ‘kutengwa’ katika hadithi katika vitabu vya kiada na vitabu vya hadithi vya darasa. Alianza kupanga njia za kuwashirikisha wanafunzi hawa pia.

Shughuli ya 2: Kuandika hadithi kwa kuzingatia mitazamo tofauti

Tumia hadithi ileile kwa shughuli ya 1 au nyingine uliyochagua.

Isome na wanafunzi na jadili jinsi ambavyo ingesimuliwa tofauti. Kwa mfano, wahusika wapya wangeongezwa au wahusika waliopo wangeshiriki kwa uhusika tofauti. Katika ya familia, baba angebaki nyumbani na kupika wakati ambapo mama angekuwa akifanya kazi katika gereji. Familia ingekuwa na mtoto au mtu mzima ambaye ana ulemavu au upungufu wa akili. Watake wanafunzi wafanye kazi katika vikundi vidogo kuandika na/au kuchora kwa namna mbalimbali za hadithi mliyosoma. Zungukia darasa, ukizingatia mambo yapi yanawafurahisha wanafunzi. Kama kuna kikundi chenye matatizo, kisaidie.

Vikundi vikisha maliza, mtake mwanafunzi mmoja kutoka katika kila kikundi kusoma hadithi hiyo mpya darasani na kuonesha picha. Kusanya hadithi hizo kwa ajili ya kuzitathmini. Unaweza kuzichapisha hadithi hizo katika kitabu kwa ajili ya maktaba ya darasa au ziweke kwenye maonesho darasani. Hadithi zinakuonesha nini kuhusu mawazo ya wanafunzi na hatua yao ya maendeleo ya kuandika.

Somo la 3

Matangazo katika mabango, redio, televisheni na skrini ya kompyuta, magazeti na majarida, katika maduka au katika barua za posta, hujaribu kutufanya tutende kwa njia fulani - hasa kutumia pesa. Ni muhimu kwako na kwa wanafunzi kwelewa jinsi matangazo yanavyojaribu kufanya hili ili wewe na wanafunzi wako muyasome kwa umakinifu na pia mtambue namna ya ujanja unaotumika katika matangazo hayo.

Mwitiko wa wanafunzi katika Shughuli Muhimu zitakuonesha kama wameanza kwelewa au hawajaanza kwelewa jinsi ya kusoma matangazo kwa umakinifu.

Uchunguzi kifani ya 3: Kujifunza kusoma matangazo kwa umakinifu

Wakati mwalimu Stella Mapuga aliposhiriki katika programu ya maendeleo ya walimu, alivutiwa na shughuli za kusoma kwa umakinifu. Yeye na wenzake walilinganisha matangazo ya bidhaa ileile katika magazeti kwa ajili ya wasomaji tofauti (vijana au wazee, au watu waliotoka katika ‘jamii’ au makundi ya vipato tofauti). Waligundua kuwa picha na maneno yaliyotumika katika kutangaza bidhaa yalikuwa tofauti katika magazeti tofauti na kwamba baadhi ya bidhaa yalitangazwa katika gazeti moja tu kati ya magazeti hayo. Walimu waliangalia lugha iliyotumiwa na watangazaji. Waliangalia pia picha au michoro katika matangazo hayo. Rafiki yake na mwalimu Stella alilalamika kuwa wanawake waliotumiwa walikuwa vijana na wenye umbo la kuvutia! Mwishowe, walijadili jinsi matangazo yalivyochanganya maneno na picha katika ukurasa na walimu waliona nini kwanza walipoangalia matangazo.

Mhadhiri wao alipowauliza walichojifunza, walimu walisema wamejifunza kuangalia matangazo kwa umakinifu zaidi siku za usoni. Walijifunza kuwa wasanifu wa matangazo huteua maneno na picha ili kuwahimiza wasomaji kununua bidhaa. Wasanifu hawa huteua maneno na picha zenye ukubwa tofauti na huziweka katika ukurasa katika njia ambayo inawahimiza wasomaji kuona zaidi baadhi ya maneno au picha.

Baadhi ya walimu walisema kuwa wana hamu ya kuwaonesha wanafunzi wao jinsi matangazo yanavyojaribu kushawishi wasomaji kuchukua hatua-hasa hatua ya kununua - na kuwahamasisha kuwa wateuzi.

Shughuli muhimu: Kusoma matangazo kwa umakinifu

Tayarisha shughuli hii na iwasilishe kwa wanafunzi kwa kufuata hatua kama zilivyo kwenye Nyenzo-rejea 3: Usomaji wa matangazo kwa umakinifu. Unahitaji kukusanya maandishi ya matangazo mbalimbali au andika baadhi uliyokwishaona katika maduka ya mitaani au sokoni.

Wape matangazo hayo vikundi na watake wajadili maswali yafuatayo:

Ni bidhaa gani inayotangazwa?

Ni nani mlengwa wa kununua bidhaa au huduma hiyo?

Watangazaji wanajaribuje ‘kuuza’ bidhaa au huduma? Rejelea mawazo yaliyo katika orodha ya ubaoni

Nani haihussishwi katika tangazo hili?

Ungetaka kuwauliza maswali gani watangazaji?  

Baada ya dakika kama 15, viulize baadhi ya vikundi kutoa majibu yao.

Kwa kazi za nyumbani, watake wanafunzi kutafuta tangazo, waliweke katika daftari zao na waandike majibu ya maswali (1-5) yanayohusu tangazo hilo.

Baada ya kusahihisha kazi zao za nyumbani, panga na fundisha somo jingine ambapo wanafunzi watapanga na kutengeneza matangazo yao wenyewe. Angalia Nyenzo-rejea 4: Utengenezaji wa matangazo kwa mapendekezo ya jinsi ya kutathmini na kupanga shughuli hiyo.

Nyenzo-rejea ya 1: Uulizaji wa maswali – kuwahimiza wanafunzi kufikiri kwa umakinifu kuhusu hadithi

Nyenzo ya Mwalimu kwa ajili ya kupanga/kurekebisha na kutumia na wanafunzi

Mfano A: Hadithi kuhusu familia

Unaweza kuuliza maswali kama:

  • Ni wanafamilia wapi waliomo katika hadithi?

  • Wapi wanaonekana muhimu? Unawatambuaje?

  • Je, familia yako inafanana na hii? Kama hivyo ndivyo, kwa njia zipi? Kama sivyo, inatofautianaje?

  • Wanafamilia wanafanya nini? Je, watu katika familia yenu wanaweza kuwa na mwenendo kama huo?

  • Unafikiri mwandishi anataka watu waamini nini kuhusu familia?

Mfano B: Hadithi iliyotayarishwa shuleni

Unaweza kuuliza maswali kama:

  • Shule katika hadithi inafanana na shule yetu?

  • Ni kwa njia zipi majengo yanafanana? Ni kwa njia majengo ni tofauti?

  • Ni kwa njia zipi watu - mwalimu mkuu, walimu, wanafunzi - wanafanana na wale wa shuleni kwetu? Ni kwa njia zipi wanatofautiana?

  • Je, watu katika hadithi wana mwenendo au wana matendo kama watu wa shuleni kwetu au wana mwenendo au wanatenda tofauti? Toa mifano kuthibitisha jibu lako.

  • Unafikiri mwandishi katika hadithi anawataka wasomaji kuamini nini kuhusu shule?

Angalizo: Unaweza kuuliza maswali kama haya kuhusu kijiji, mji, jiji ambapo hadithi kama hii inatolewa. Lengo ni kuwafanya wanafunzi kulinganisha kati ya yale wanayoyajua na wanayosoma juu yake.

Nyenzo-rejea ya 2: Vidokezo vya barua ya mwandishi

Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia na wanafunzi kwa ajili ya kupanga/kurekebisha

Mwandishi anaweza kuwa mwanafunzi darasani kwako. Kama mna vitabu mnavyochangia na darasa jingine, mwandishi anaweza kuwa darasa hilo au mwanafunzi katika darasa hilo.

Bwana ………

Tumesoma ……… (kichwa cha habari cha hadithi) darasani kwetu. Tulifikiri kuwa ungependa kujua maoni yetu kuhusu hadithi hii.

Kwanza, tunapenda……… (sentensi moja au mbili hapa). Tunapenda hii kwa sababu……… (wanafunzi waandike sababu zao).

Tunapenda pia……… (sentensi moja au mbili hapa). Tulifurahia hadithi hii kwa sababu……… (wanafunzi wanaandika sababu zao).

Lakini , hatukupenda ……… (sentensi moja au mbili hapa). Hatukupenda hili kwa sababu (wanafunzi waandika sababu yao).

Tunatarajia kuwa utakapoandika hadithi nyingine ………….(wanafunzi wanatoa mapendekezo yao).

Wako

(jina la darasa)

Nyenzo-rejea ya 3: Usomaji makinifu wa matangazo

Usuli/taarifa ya mwanzo/uelewa wa mwalimu

Orodha iliyopo hapa chini imetayarishwa kwa ajili ya usomaji wa matangazo kwa umakinifu zaidi lakini inaweza kurekebishwa kutumiwa katika usomaji wa matini nyinginezo kama mashairi, picha au barua kutoka kwa watu wanaohusika na masuala ya shule k.m. ofisa ya elimu wilayani.

Misingi na maswali unayouliza yanaweza kubadilishwa kwa sababu hii ili kukidhi zaidi haja ya muktadha lakini bado itawasaidia wanafunzi kusoma kwa ajili ya kupata maana ya ndani zaidi.

  • Kusanya au andika matangazo ya kutosha toka gazetini, matangazo ya maduka, masoko ya mitaani n.k. kwa kila kikundi cha wanafunzi wanne darasani ili kila kikundi kiwe na mfano mmoja wa kufanyia kazi.

  • Kabla ya kuvipa vikundi matangazo haya, watake wanafunzi wazungumze na wenzao kuhusu maana ya kutangaza vitu fulani na jinsi wanavyoweza kutangaza shule yao kwa wazazi ambao wangependa kuandikisha watoto wao katika shule hiyo.

  • Watake wanafunzi waliambie darasa zima walichojadili. Halafu watake wanafunzi kupendekeza watangazaji wanachofanya ili kufanya bidhaa zao kuwavutia wanunuzi.

  • Andika mapendekezo yao ubaoni.

Hapa kuna mifano ya wanayofanya watangazaji:

  • Tumia picha au michoro inayovutia.

  • Tumia rangi inavyotakiwa .

  • Andika maneno na kuweka picha au michoro katika sehemu ya ukurasa panapovutia nadhari.

  • Jaribu kuwavutia wasomaji ambao wanathamini moja au zaidi ya haya:

    • Uwezekano wa kununuliwa - bidhaa hii si aghali au ni bei nzuri.
    • Upatikanaji kwa urahisi - bidhaa hii inaondoa usumbufu.
    • Uzuri/uimara - bidhaa hii inakupendeza na inadumu.
    • Utajiri - bidhaa hii itakufanya uwe tajiri.
    • Afya - bidhaa hii itakufanya uwe mwenye afya.
    • Furaha - bidhaa hii hukufanya ujisikie mwenye furaha.
    • Ubora - bidhaa hii ni bora kuliko zote za aina yake.
    • Usalama - bidhaa hii inakufanya uwe salama.
    • Umashuhuri – bidhaa hii itakufanya upendwe na watu.
    • Ladha – bidhaa hii ina ladha nzuri.

    Imerekebishwa kutika: Focus on English, Grade 10

Mifano ya matangazo ya biashara kutoka Tanzania.

Chanzo chake cha asili: PIETERFOURIE, Website.

Chanzo chake cha asili: Leeryanmiller, Website.

Chanzo chake cha asili: BBC World, Website.

Nyenzo-rejea ya 4: Kutengeneza matangazo

Nyenzo-rejea ya Mwalimu kwa ajili ya kupanga/kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Tathmini ya mwitiko wa wanafunzi katika kujibu maswali yanayohusu matangazo.

Tumia maswali haya kutathmini kazi za wanafunzi:

  1. Kuna ushahidi kuwa wanafunzi wameelewa kazi waliyotarajiwa kuifanya? Kwa mfano, mwanafunzi amechagua/hakuchagua tangazo; mwanafunzi amejaribu/hakujaribu kujibu swali?
  2. Ni maswali yapi ambayo mwanafunzi amejibu kwa mafanikio zaidi? Kuna ushahidi upi unaoonesha kuwa majibu ni ya mafanikio?
  3. Ni maswali yapi ambayo mwanafunzi hakujibu vizuri au kwa usahihi? Ni kitu kipi kinakosekana katika majibu yake au ni makosa yapi yaliyomo katika majibu yake?

Masomo ya ufuatiliaji

  • Warudishie wanafunzi kazi zao na toa maoni ya jumla kuhusu kazi walizozifanya vizuri na ni mahali papi ambapo wangepaboresha zaidi.

  • Watake wanafunzi wafanye kazi katika vikundi vilevile kama walivyofanya katika somo la kujibu maswali kuhusu matangazo.

  • Kipe kila kikundi karatasi kubwa na, kama inawezekana, kalamu za kuchorea au rangi pamoja na brashi.

  • Watake wafikirie bidhaa mpya (k.m. aina ya chakula, gari, kifaa cha nyumbani, nguo) na wapange jinsi ambavyo wangechora au wangeandika tangazo. Wanatakiwa kufikiria juu ya maswali waliyojibu katika somo lililopita.

  • Watake wachore na kutengeneza tangazo la bidhaa hii mpya.