Katika Kipindi kilichopita ulijifunza kuhusu anatomia na fiziolojia ya mfumo wa uzazi wa kike. Homoni za estrojeni na projesteroni ziliangaziwa kwa kifupi. Katika Kipindi hiki, utajifunza mengi zaidi kuhusu wajibu wa homoni hizi na zingine muhimu zinazohusika katika udhibiti wa mzunguko wa hedhi kwa binadamu, utoaji wa ova (mayai) na wanawake wa umri wa uzazi na uandaaji wa uterasi kwa kufaa kuupokea ujauzito.
Baada ya Kipindi hiki unapaswa uweze:
4.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote maalumu yalioandikwa kwa herufi nzito. (swali la kujitathmini 4.1)
4.2 Kueleza michakato ya kifiziologia na mabadiliko yanayotokea wakati wa mzunguko wa hedhi. (maswali ya kujitathmini 4.1 na 4.2)
4.3 Kueleza udhibiti wa homoni katika mfumo wa uzazi wa kike. (maswali ya kujitathmini 4.3 na 4.4)
Jinsi unavyoweza kukumbuka kutoka katika somo lako la biolojia katika shule ya upili hapo awali, majukumu mbalimbali ya mwili hudhibitiwa na mfumo wa neva na wa homoni. Mifumo hii miwili huhusika katika udhibiti wa shughuli za mfumo wa uzazi wa kike kwa mfuatano wa matukio ya kila mwezi yaitwayo mzunguko wa hedhi, jinsi tutakavyoelezea.
Unapaswa kukumbuka kutoka katika Kipindi cha 3 kwamba homoni ni kemikali ya kutuma ishara ambayo hutengenezwa mwilini na kuenea katika damu. Homoni tofauti hudhibiti shughuli za seli au ogani tofauti. Majukumu ya homoni tano kuu zinazodhibiti mfumo wa uzazi wa kike yameelezewa katika Kisanduku 4.1 na kisha jinsi zinavyoingiliana kuelezewa katika mchoro 4.1.
Homoni itoayo gonadotropini hutolewa na sehemu ya ubongo iitwayo hipothalamasi. Homoni hii ieneapo katika damu husababisha kutolewa kwa homoni mbili muhimu (tazama hapa chini na pia mchoro 4.1) kutoka kwa tezi ya pituitari iliyo katika sehemu nyingine maalumu ya ubongo.
Homoni Chochelezi ya Foliko (HCF) hutolewa na tezi ya pituitari katika nusu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi. Homoni hii huchochea ukuaji wa foliko pevu ya ovari na kudhibiti utoaji wa ova na manii kwa mwanamke na mwanamume mtawalia.
Homoni ya lutea pia hutolewa na tezi ya pituitari iliyo ubongoni. Homoni hii huchochea ovari kutoa estrojeni na projesteroni. Pia huchokonoa ovulesheni (kutolewa kwa ova pevu kutoka kwenye ovari) na kuendeleza kukua kwa kopasi luteamu.
Je, kopasi luteamu ni nini? (Kumbuka Kipindi cha 3)
Jina kopasi luteamu humaanisha ‘mwili wa manjano,’na hukua katika ovari baada ya ovulesheni kutoka kwa foliko za ovari zilizokua na kutoa ova.
Mwisho wa jibu
Estrojeni ni homoni ya uzazi wa kike ambayo hutolewa hasa na ovari kwa mwanamke asiye na ujauzito. Homoni hii huendeleza upevukaji na utolewaji wa ova katika kila mzunguko wa hedhi. Pia hutolewa na kondo wakati wa ujauzito.
Projesteroni hutolewa na kopasi leteamu katika ovari. Jukumu la homoni hii ni kuandaa endometriamu (bitana ya uterasi) kwa kupokea na kukuza ova iliyotungishwa. Pia hukomesha utoaji wa estrojeni baada ya ovulesheni.
Muda wa mzunguko wa hedhi huwa ni takribani siku 28 lakini unaweza kuwa wa kubadilika. Muda huu unaweza kuwa mfupi kama wa siku 21 au mrefu kama wa siku 39 kwa wanawake wengine. Mzunguko huu wa hedhi hueleweka vizuri tukilenga kwanza shughuli zinazotendeka katika ovari kisha zinazotendeka katika uterasi. Tutaeleza kila moja ya hizi.
Mzunguko katika ovari ni mfuatano wa shughuli za kila mwezi zinazohusiana na upevukaji na uachiliaji wa ova, maandalizi ya utungisho na pandikizo kwenye uterasi (ikiwa kutatokea utungisho). Unaweza kuwa unashangaa ni kwa nini udhibiti wa mfumo wa uzazi wa kike ni changamano jinsi ilivyoonyeshwa katika mchoro 4.1. Sababu ni kuwa mzunguka katika ovari sharti uanzishwe kisha usitishwe kwa utaratibu uliodhibitiwa sawasawa kila mwezi. Katika sehemu hii tutaeleza jinsi haya yanavyotimizwa.
Mzunguko katika ovari huwa katika awamu mbili zinazofuatana. Kila awamu huchukua muda wa takribani siku 14. Matukio hubainishwa kutoka siku ya 1 ambayo ndiyo siku ya kwanza ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi.
Mfuatano ulioonyeshwa katika mchoro 4.1 umeanza na hipothalamasi kutoa homoni itoayo gonadotropini, ambayo huichochea tezi ya pituitari kutoa Homoni Chochelezi ya Foliko (HCF) na homoni ya lutea ambazo kisha huiathiri ovari kwa kuzifanya foliko za ovari kuhitimisha upevukaji wa ova. Katika kipindi hiki, foliko chache za ovari zilizo na ova zisizopevu hukua na kupevuka kutokana na uchochelezi wa Homoni Chochelezi ya Foliko na homoni ya lutea. Kwa kawaida, kufikia siku ya 14, ni foliko moja tu ambayo huwa pevu na tayari kuitoa ova iliyo ndani yake. Foliko zingine zote zilizokuwa zimeanza kupevuka katika awamu hii ya mzunguko wa ovari kua nyeusi mara tu baada ya ovulesheni.
Fahamu kuwa ni kipindi kimoja tu kisichobadilika kwa kiasi kwa wanawake wote, nacho ni muda kati ya ovulesheni na mwanzo wa hedhi ambacho ni sawa kwa wanawake wote na huchukua kwa kawaida karibu siku 14 hadi 15. Hata hivyo wakati wa ovulesheni hubadilika na ni vigumu kuubashiri kwa usahihi.
Awamu hii ndiyo kipindi cha shughuli ya kopasi luteamu ambapo uterasi huandaliwa kwa ujauzito iwapo utatokea. Baada ya ovulesheni, kopasi luteamu huanza kutoa projesteroni pamoja na kiwango cha chini cha estrojeni. Projesteroni hudumisha uterasi katika hali thabiti inayofaa kwa kupokea na kukistawisha kiinitete. Bitana ya uterasi (endometriamu) hunenepa na kustawishwa na mishipa ya damu kwa wingi na kuwa pokezi sana kwa ova iliyotungishwa. Projesteroni pia husitisha utolewaji zaidi wa Homoni Chochelezi ya Foliko na homoni ya lutea kutoka katika tezi ya pituitari.
Ovulesheni hivyo hufuatwa kwa haraka na ongezeko la kiwango cha projesteroni huku kopasi luteamu ikichukua jukumu la kutoa homoni hii. Projesteroni huenea katika damu mwilini kiwango chake kinapoongezeka. Kiwango cha juu cha homoni hii kinapoifikia hipothalamasi kwenye ubongo, utoaji wa homoni itoayo gonadotropini kutoka kwa hipothalamasi husitishwa.
Je, ni nini kitakachofanyika hipothalamasi inapoacha kutoa homoni itoayo gonadotropini? (Tazama mchoro 4.1)
Tezi ya pituitari itakoma kutoa Homoni Chochelezi ya Foliko na Homoni ya Lutea.
Mwisho wa jibu
Je, hii itakuwa na athari gani kwa ovari?
Upevukaji wa ova zaidi utakomea hapo.
Mwisho wa jibu
Aina hii ya mfumo dhibiti ambapo kuongezeka kwa kemikali moja ya mwili (kwa muktadha huu projesteroni) husitisha kutolewa kwa kemikali nyingine ya mwili (kwa muktadha huu homoni itoayo gonadotropini) huitwa mwitiko hasi kwa utaratibu wa utendaji. Hata hivyo, kopasi luteamu ina maisha mafupi na kwa hivyo, baada ya kukoma kutoa projesteroni, mwitiko huu hasi kwa hipothalamasi husita na kuiwezesha tena kuanza kutoa homoni itoayo gonadotropini. Hivyo basi mzunguko wa ovari huanza tena.
Kisha tutaangazia matukio kwenye uterasi kwa kipindi hicho hicho cha muda wa siku 28 sawa na matukio yaliyoelezewa kuhusu ovari. Mzunguko katika uterasi huonyesha mfuatano wa mabadiliko yatendekayo kwenye uterasi kwa kuitikia uchochelezi wa homoni za uzazi wa kike ambazo ni projesteroni na estrojeni.
Ikiwa utungisho haukutendeka baada ya ovulesheni, kopasi leteamu itasawijika na utoaji wa projesteroni kupungua na hatimaye kichochelezi kinachoidumisha endometriamu nene kupotea. kupunguka kwa kiwango cha projesteroni husababisha kukwangulika kwa bitana nene ya endometriamu. Ukuta wenye misuli wa uterasi (miometriamu) hunywea ili kusaidia kukatiza kuletwa kwa damu kwenye endometriamu na kuifanya kujitenga kutoka kwa uterasi. Endometriamu inapochanguka na kutokea ukeni huwa imechanganyika na damu kiasi kwa sababu awali ilikuwa na mishipa mingi ya damu kwa ustawishaji wa fetasi iwapo kungetokea ujauzito. Mchanganyiko wa tishu na damu hutolewa kupitia ukeni kama kioevu cha hedhi kwa kawaida kwa muda wa takribani siku 3 hadi 5. Majina mengine ya hedhi ni kutokwa na damu kila mwezi au kipindi cha hedhi.
Hedhi hutoka kila mwezi kwa muda wote wa miaka ya uzazi isipokuwa wakati wa ujauzito ampapo husitishwa na mwanamke hawezi kupata ujauzito mwingine hadi mtoto atakapozaliwa. Unyonyeshaji wa mtoto pia husitisha hedhi bali kunayo hatari kwamba ovulesheni na ujauzito vinaweza kutokea.
Kiwango cha estrojeni kwenye damu huongezeka katika kipindi hiki kufuatia mwisho wa hedhi huku ovari zikijiandaa kwa ovulesheni itakayofuata siku ya 14 hivi. Hii huitwa awamu ya kuongezeka kwa sababu katika kipindi hiki endometriamu hunenepa na kustawishwa sana na mishipa ya damu kwa maandalizi ya uwezekano wa utungisho na ujauzito.
Katika awamu hii, kiwango cha projesteroni katika damu huongezeka na kusababisha ukuaji wa mishipa mingine ya damu kwenye endometriamu. Hii huiweka endometriamu katika nafasi nzuri ya kupokea ova iliyotungishwa. Ikiwa ova itatungishwa na kiinitete kujipandikiza kwenye endometriamu na kondo kukua, kondo hii itatoa Homoni Ya Binadamu ya Korioni ya Gonadotropini katika muda wote wa ujauzito. Ugunduzi wa homoni hii katika mkojo wa mwanamke ndio msingi wa vipimo vingi vya ujauzito.
Homoni ya Binadamu ya Korioni ya Gonadotropini huichochea kopasi luteamu kuendelea kutoa projesteroni ili kudumisha endometriamu katika ujauzito. Viwango vinavyoongezeka vya projestoreni hutenda kazi kama mwitiko hasi kwa utaratibu wa utenda kazi wa hipothalamasi na tezi ya pituitari kwa kuzuia kutolewa kwa Homoni Chochelezi ya Foliko na Homoni ya lutea na kisha kuzuia ovulesheni zaidi.
Je, ni nini hutendeka iwapo utungisho haukutokea?
Kopasi luteamu kua nyeusi na kiwango cha projesteroni kupungua. Kutokana na haya, endometriamu huchanguka na kisha mwanamke huyo kupata hedhi - hii ni ishara kuwa hakupata ujauzito katika mzunguko huo wa hedhi.
Mwisho wa jibu
Huenda unajua kuwa kuvunja ungo (hedhi ya kwanza), kwa wastani, huanza kati ya umri wa miaka 12 hadi 15 katika bara la Afrika. Hata hivyo, katika hali zingine huenda ianze baadaye kwa kuchelewa kati ya umri wa miaka 17 hadi 20 au mapema kati ya umri wa miaka 8 hadi 9. Baadhi ya mambo yanayoathiri umri wa kuvunja ungo ni ya kibayolojia na mengine ni ya kitamaduni.
Kuvunja ungo (hedhi ya kwanza) huanza hipothalamasi kwenye ubongo inapochochewa kuanza kutoa homoni itoayo gonadotropini katika umri wa takribani miaka 12 hadi 15. Hata hivyo, imethibitishwa kuwa homoni itoayo gonadotropini inaweza kuanza kutolewa kwa umri wa chini kwa wasichana waliostawishwa vyema na kutangamana na mambo yanayozidisha hamu ya ngono kama vile kutazama filamu za ngono na kuongea kuhusu ngono. Huenda hedhi ya kwanza (kuvunja ungo) ichelewe hadi umri wa miaka 17 hadi 20 kwa wasichana wasiostawishwa vyema, na wasiotangamana sana na mambo yanayozidisha hamu ya ngono. Magonjwa yanayoathiri hipothalamasi na tezi ya pituitari au ovari na uterasi yanaweza pia kuathiri umri wa hedhi ya kwanza.
Katika umri wa kuvunja ungo, homoni za uzazi wa kike, estrojeni na projesteroni huwajibika katika kukuza sifa za baadaye za kijinsia kwa mwanamke. Hizi ni:
Pamoja na hedhi ya kwanza, kujitokeza kwa sifa za baadaye za kijinsia hudhihirisha kipindi kiitwacho ubaleghe – kipindi cha maisha (hasa kati ya umri wa miaka 10 hadi 15) ambapo viungo vya uzazi hukua kikamilifu na kuweza kutenda majukumu yao. Sifa za baadaye za kijinsia huitwa ‘za baadaye’ kwa sababu hutokea baada ya sifa za mwanzo za kijinsia zinazowatofautisha wanawake na wanaume.
Taja baadhi ya sifa za mwanzo za kijinsia za wanawake.
Tayari ulisoma kuzihusu katika Kipindi cha 3 cha somo -ndivyo viungo vya nje vya jenitalia ya kike (kwa mfano labia ndogo na kisimi), na viungo vya ndani vya uzazi wa kike (kwa mfano ovari,uterasi na uke).
Mwisho wa jibu
Hedhi huendelea kutoka kila mwezi isipokuwa wakati wa ujauzito hadi mwanamke huyo atakapofikia ukomohedhi kati ya takribani umri wa miaka 48 hadi 50 ambapo hedhi hukoma. Unaweza kukumbuka kutoka katika Kipindi cha somo cha 3 kuwa wakati wa kuzaliwa, ovari za mtoto mchanga wa kike anapozaliwa tayari huwa na takribani ova 60,000 zisizopevu na hawezi kutoa zingine zaidi maishani mwake. Anapofikia ukomohedhi, uwezo wake wa kupevusha ova hufika mwisho.
Tutaelezea katika Kipindi cha 5 cha somo kinachotendeka ova inapotungishwa na kujipandikiza kwenye uterasi na kukua hadi itakapokuwa fetasi.
Umejifunza katika Kipindi cha 4 cha somo kuwa:
Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, unaweza kutathmini ni kwa kiwango kipi umeweza kuyatimiza malengo ya masomo ya Kipindi hiki kwa kujibu maswali haya. Yaandike majibu katika shajaradaftari lako kisha uyajadili na mkufunzi wako katika mkutano utakaofuata wa masomo ya kusaidiana. Unaweza kuyalinganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.
Safu yakushoto ya Jedwali 4.1 inaonyesha majina ya awamu tofauti zilizo kwenye mzunguko wa hedhi. kamilisha safu ya kushoto kwa kujaza kipindi sahihi tangu kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi.
Awamu ya mzunguko wa hedhi | Siku (1 = siku ya kwanza ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi) |
---|---|
Awamu ya foliko ya mzunguko katika ovari | |
Awamu ya lutea ya mzunguko katika ovari | |
Awamu ya hedhi ya mzunguko katika uterasi | |
Awamu ya kuongezeka ya mzunguko katika uterasi | |
Awamu ya unyesaji ya mzunguko katika uterasi |
Awamu ya mzunguko wa hedhi | Siku (1 = siku ya kwanza ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi) |
---|---|
Awamu ya foliko ya mzunguko katika ovari | 1-14 |
Awamu ya lutea ya mzunguko katika ovari | 15-28 |
Awamu ya hedhi ya mzunguko katika uterasi | 1-5 |
Awamu ya kuongezeka ya mzunguko katika uterasi | 6-14 |
Awamu ya unyesaji ya mzunguko katika uterasi | 15-28 |
Je, kwa nini unafikiri kuwa mwanamke anaweza kuhisi maumivu ya mbano kwenye fumbatio lake wakati wa hedhi?
Mwanamke anaweza kuhisi maumivu ya mbano kwenye fumbatio lake wakati wa hedhi kwa sababu kuta zenye misuli za uterasi (miometriamu) hubana ili kusaidia kukatiza damu iendayo kwenye endometriamu na kuifanya itengane na uterasi.
Mwisho wa jibu
Je, unaweza kupendekeza jinsi viwango vya juu vya estrojeni na projesteroni bandia zipatikanazo kwenye tembe za kuzuia mimba zinavyozuia ujauzito kwa wanawake wanaozitumia tembe hizi mara kwa mara na walivyoshauriwa?
Kiwango cha juucha estrojeni na projesteroni bandia kwenye tembe za kuzuia mimba huzuia ujauzito kwa kuleta mwitiko hasi kwa utaratibu wa utendaji kazi wa hipothalamasi iliyo kwenye ubongo. Kiwango hiki cha juu cha estrojeni na projesteroni huiga hali inayotokea wakati wa ujauzito. Homoni hizi hukandamiza utoaji wa homoni itoayo gonadotropini kwenye hipothalamasi na kwa hivyo tezi ya pitutari hukoma kutoa homoni chochelezi ya foliko na homoni ya lutea. Hii hatimaye hukomesha ovari kupevusha ova zozote zaidi na kisha mwanamke huyu kamwe hawezi kupata ujauzito almradi anakunywa tembe hizi za kuzuia ujauzito mara kwa mara jinsi alivyoshauriwa.
Mwisho wa jibu
Eleza ni kwa nini hedhi hukoma wakati wa ujauzito.
Kwa mwanamke mjamzito, kondo huendelea kutoa homoni ya binadamu ya korioni ya gonadotropini inayoichochea kopasi luteamu kwenye ovari kutoa projesteroni katika muda wote wa ujauzito. Projesteroni hudumisha endometriamu kama rusu nene yenye mafuta na kwa hivyo hedhi hukoma wakati wa ujauzito kwa sababu endometriamu bado imejishikiza kwenye uterasi huku ikisaidia katika kustawisha na kuilinda fetasi inayokua.
Mwisho wa jibu.