Skip to main content
Printable page generated Saturday, 5 October 2024, 11:36 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Saturday, 5 October 2024, 11:36 PM

8. Kutambua Ujauzito na Kujifunza Historia ya Mwanamke Mjamzito

Kipindi cha 8 Kutambua ujauzito na Kujifunza Historia ya Mwanamke Mjamzito

Utangulizi

Kipindi hiki kinaanza kwa kukupa maarifa ya kutambua mwanamke awapo mjazito. Utajifunza kutofautisha kati ya ishara na dalili zinazoweza kuashiria ujauzito, zinazoelekea kuashiria ujauzito na zile chanya. Dalili ni kiashiria cha hali fulani (kama vile ujauzito), au ugonjwa au tatizo kinachogunduliwa na mhusika, na anachoweza kuelezea mwenyewe, au ukiuliza maswali mwafaka. Kwa upande mwingine, ishara ni kiashiria kinachoweza kugunduliwa na mtaalam wa maswala ya afya tu, au kwa kupima.

Ili kumpa mwanamke mjamzito utunzaji bora, unahitaji pia kujua kuhusu hali yake ya kiafya kwa jumla na ujauzito wa hapo awali na ni mara ngapi ameweza kuzaa na hali ya ujauzito huu kufika sasa. Habari hizi huitwa historia ya kitiba. Mchakato wa kukusanya habari yote na kuinakili kwa kutumia maswali wazi na yanayoeleweka huitwakuchukua historia. Katika Kipindi hiki utajifunza jinsi ya kuuliza maswali barabara kuhusu historia ya kiafya ya mwanamke mjamzito. Maarifa haya yatakusaidia kutoa ushauri mwafaka na wa kibinafsi ili kuuwezesha ujauzito na uzazi huu kuwa salama iwezekanavyo. Pia utatambua umuhimu wa kudumisha imani ya mwanamke kwa kuweka anayokuambia kwa siri.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 8

Baada ya kipindi hiki unapswa kuweza:

8.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yalioandikwa kwa herufi nzito. (Maswali ya Kujitathmini 8.1 na 8.4)

8.2 Kueleza kwa nini ni muhimu kupata imani na uhakika wa mwanamke anayekuja kwako kwa utunzaji katika ujauzito, na utoe mfano wa jinsi unavyoweza kudumisha au kupoteza imani yake. (Swali la Kujitathmini 8.1)

8.3 Kutofautisha kati ya ishara za ujauzito zinazoweza kutokea, zinazoelekea kutokea na zile chanya, na uamue ikiwa mwanamke ana uwezekano au anaelekea kuwa mjamzito kwa msingi wa uchunguzi kifani wa kubuni. (Swali la Kujitathmini 8.2)

8.4 Kuuliza maswali wazi nawanayoelewa ili kukusaidia kupata habari kuhusu dalili za ujauzito zinazoweza kuonekana au visababishi vya hatari vinavyotokea sana na vinavyoweza kuathiri afya ya mwanamke mjamzito au mtoto wake. (Maswali ya Kujitathmini 8.1 na 8.5)

8.5 Kutambua visababishi vikali vya hatari vinavyoweza kupelekea mwanamke huyo kuhitaji kuzalia kwenye kituo cha afya kuliko nyumbani. (Maswali ya Kujitathmini 8.3 na 8.4)

8.1 Kupata imani ya mwanamke katika utunzaji katika Ujauzito

Ili kufanya utambuzi bora wa kubainisha iwapo mwanamke ni mjamzito au kujifunza kuhusu historia yake ya kitiba kama kipengele cha utunzaji wake katika ujauzito, lazima kwanza upate imani yake na umfanye ajihisi mtulivu kuongea nawe kuhusu habari zake za kibinafsi. Anza kwa kujitambulisha na kumwuliza kwa heshima kuongea kuhusu mambo yanayomhusu yeye binafsi na historia yake ya kitiba. Mwanzoni huenda asitake kufanya hivyo. Iwapo ataona haya kuhusu mwili wake au ngono, inaweza kuwa vigumu kwake kukueleza mambo unayohitaji kujua kuhusu afya yake. Jaribu kumsaidia atulie na kuwa na imani nawe kwa kumsikiza kwa makini, kujibu maswali yake kwa lugha anayoielewa, ukiweka anayokueleza siri na kumheshimu.

  • Je, nini kinachoweza kutendeka ukiambia wengine alichokuambia kuhusu historia yake ya kibinafsi?

  • Anaweza kupoteza imani nawe kama mhudumu wa afya. Anaweza kukosa ari ya kuongea nawe kwa uaminifu wakati mwingine utakapomwona.

    Mwisho wa jibu

  • Je, kupoteza kwake kwa imani nawe kunawezaje kusababisha hatari zaidi kwa afya yake au ya mtoto wake?

  • Huenda asikuambie habari muhimu kuhusu ujauzito wake ambayo ingekusaidia kutambua visababishi vya hatari kabla havijakithiri. Anaweza hata kusitisha safari zake za utunzaji katika ujauzito kwa sababu hakuamini.

    Mwisho wa jibu

Utakuwa ukiandika yale unayojifunza kuhusu kila mwanamke mjamzito katika kadi yake ya kumbukumbu za utunzaji wa ujauzitoni. (Mchoro 8.1)

Mchoro 8.1 Uandikaji wa muhtasari mzuri ni muhimu unapochukua historia ya kitiba ya mwanamke mjamzito.

Habari hii inaweza kuhitajika baadaye katika ujauzito huo, leba na kuzaa au baada ya mtoto kuzaliwa (kipindi cha baada ya ujauzito). Mwondolee shaka kuwa hautaruhusu mwingine yeyote isipokuwa wahudumu wengine wa afya kuona uliyoyaandika kumhusu.

Kwanza tutapendekeza aina za maswali unayoweza kuuliza ili kukusaidia kutambua ikiwa mwanamke ni mjamzito. Kisha tutaeleza habari nyingine utakayohitaji kuuliza kumhusu. Hii ni ili uweze kutambua visababishi vyovyote vya hatari anavyoweza kuwa navyo na umtunze ipasavyo katika ujauzito huo.

8.2 Kutambua iwapo mwanamke ni mjamzito

Viashiria vya ujauzito vimeainishwa kijumla katika makundi matatu:

  • Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito: mabadiliko katika mwili wake ambayo mwanamke anaweza kutambua mwenyewe na akuambie kuhusu yanayoweza kumaanisha kuwa ni mjamzito lakini yanaweza pia kusababishwa na jambo jingine. Ripoti ya dhahania ya mwanamke huyo ndiyo uliyo nayo tu ya kukusaidia katika utambuzi wako. Hata hivyo, katika kituo cha afya, dalili zinazoweza kutokea huwa ndio ushahidi uliopo katika miezi ya kwanza mitatu hadi sita.
  • Ishara na dalilizinazoelekeakuashiria ujauzito: baadhi ya viashiria hivi huripotiwa na mwanamke huyo lakini pia unaweza kujionea mwenyewe. Pia kuna kipimo cha ujauzito unachoweza kufanya au kinachoweza kufanywa katika kituo cha afya cha kiwango kinachofuata.
  • Dalili chanya za ujauzito: hizi ni ithibati kamili ya ujauzito kwa msingi wa utambuzi halisi.

8.2.1 Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito

Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito zinazoripotiwa sana na wanawake mwanzoni mwa ujauzito pia huitwa ‘ishara za kukisiwa’ kwa sababu mara nyingi ujauzito ‘hukisiwa’ na mhudumu wa afya kwa msingi wa ripoti hizi za dhahania. Lakini ni muhimu kukumbuka kuwa hizi ni ishara zinazoweza tu kuashiria ujauzito.

Kukosa kipindi cha hedhi (amenorea)

Kukosa kipindi cha hedhi mara nyingi huwa ndiyo dalili ya kwanza ambayo wanawake hutambua wanapokuwa wajawazito. Ikiwa mwanamke atakuambia kuwa amekosa kipindi cha hedhi (amenorea) au alikoma kupata hedhi kwa miezi kadhaa, hii ni ishara nzuri ya ushikaji mimba kwa wanawake ambao huwa na mzunguko wa hedhi wa kawaida. Visababishi vingine vya amenorea vinaweza kuwa lishe duni, matatizo ya kihisia, au ukomohedhi (mabadiliko katika maisha) kwa wanawake wakongwe.

Mabadiliko kwa matiti

Wanawake wajawazito wanaweza kuripoti kuhisi matiti kuwa laini, yaliyojaa, yanayonywea, utanukaji na areola (tishu nyeusi ya mviringo inayozunguka chuchu) kuwa nyeusi. Mwanzoni mwa ujauzito tezi za areola hutanuka kutokana na uchochelezi wa homoni na ukubwa wa matiti huongezeka polepole kujitayarisha kutengeneza maziwa ya mtoto. Lakini kumbuka kuwa ukubwa wa matiti mara nyingi huongezeka muda tu kabla ya kipindi cha hedhi cha kila mwezi kwa wanawake wasio wajamzito.

Kichefuchefu na kutapika

Dalili hii inayotokea sana hutokea katika takriban asimilia 50 ya ujauzito katika miezi mitatu ya kwanza. Huwa kali zaidi asubuhi na ndiyo sababu iliyopelekea hisia hii kuitwa maradhi ya asubuhi. Lakini inaweza kutokea wakati wowote na inaweza kuchochewa na harufu za upishi na za viungo vya upishi. Wanawake wengine wajawazito huhisi kichefuchefu siku nzima. Visababishi vingine vya dalili hii vinaweza kuwa maradhi au vimelea. Kutapika sana mara kwa mara ni dalili ya hatari kwa sababu mwanamke huyo anaweza kupoteza uzani kwa haraka. Utajifunza mengi kuhusu haya katika Kipindi cha 12.

Uchovu

Mwanzoni mwa ujauzito wanawake wanaweza kuripoti kujihisi wachovu na wenye usingizi wakati wa mchana na kutaka kupumzika mara kwa mara kuliko kawaida wanapofanya kazi zao. Visababishi vingine vinaweza kuwa anemia (tazama Kisanduku 8.1), lishwe duni, matatizo ya kihisia, au kazi nyingi za sulubu.

Kisanduku 8.1 Anemia

Anemia ni ugonjwa wa damu ambao unaweza kumfanya mtu ajihisi mchovu kila wakati. Damu huwa na chembe nyekundu ambazo hubeba oksijeni kuzunguka mwili, zikipeleka kwa misuli na ogani ambapo hutumika kutengeneza nguvu. Mtu aliye na anemia hana chembe nyekundu za damu za kutosha na kwa hivyo mwili wake hupungukiwa na oksijeni na hauwezi kutengeneza nguvu za kutosha kufanya kazi ya kawaida. Kuna visababishi kadhaa vya anemia lakini kile kinachojulikana sana ni ukosefu wa ayoni kwenye mlo. Ayoni huhitajika kutengeneza upya chembe nyekundu za damu. Anemia husababisha matatizo katika ujauzito na kuzaa lakini inaweza kuzuiliwa kwa kula vyakula vya kutosha vilivyo na protini na ayoni. Wanawake wajawazito huhitaji ayoni nyingi na kwa hivyo kidesturi hupewa tembe za ayoni. Utajifunza kuhusu lishe na ujauzito katika Kipindi cha 14. Utambuzi na matibabu ya anemia vimeelezewa katika Kipindi cha 18.

Kukojoa mara kwa mara

Wanawake wajawazito mara nyingi huripoti kuwa wao huhitaji kukojoa mara kwa mara, hasa katika miezi mitatu ya kwanza na mwezi mmoja au miwili ya mwisho wa ujauzito. Visababishi vingine vya dalili hii vinaweza kuwa mfadhaiko, maambukizi ya kibofu au kisukari (ugonjwa wa sukari kwa damu). Utajifunza kuhusu utambuzi wa kisukari katika Kipindi cha 9 na maambukizi ya kibofu katika Kipindi cha 18.

Ishara za kwanza za uhai wa mtoto zinazohisiwa na mama

Wanawake wengi wajawazito huanza kuhisi mtoto wao akisonga kwa mwendo mwepesi ndani yao kabla ya kutimiza nusu ya muda wa ujauzito. Hisia hii hujulikana kama mtoto kutoa ishara za kwanza za uhai. Wanawake ambao wamepata mtoto hapo awali huwa makini kwa mienendo hii midogo mapema kuliko wanawake walio wajawazito kwa mara ya kwanza. Kutambulika kwa kwanza kwa mienendo hii ya fetasi kwa kawaida hutokea katika juma la 18-20 la ujauzito kwa primigravida (wanawake wenye ujauzito wa kwanza) lakini inaweza kuwa mapema kama juma la 14-16 kwa maltigravida (wanawake waliowahi kuwa na ujauzito hapo awali). Kisababishi kingine cha dalili hii kinaweza kuwa gesi kwenye tumbo.

Kloasma (au ‘barakoa ya ujauzito’)

Weusi wa ngozi kwenye paji la uso, sehemu juu ya pua, au vitefute huitwa kloasma. Hupatikana sana kwa wanawake weusi (Mchoro 8.2). Madoadoa meusi yanaweza kutokea kwa titi na tumbo, hasa kwenye mstari wa kati chini ya kitovu. Kwa kawaida dalili za kloasma hutokea baada ya majuma 16 ya ujauzito (ujauzito wa miezi minne) na huongezeka kwa kuwepo kwa mwanga wa jua. Hata hivyo, mabadiliko haya ya ngozi si viashiria vya kuegemewa vya ujauzito.

Mchoro 8.2 Kloasma inaweza kuashiria ujauzito lakini pia inaweza kuwa ni athari ya mwanga wa jua.
  • Je, unaweza kuamua kuwa mwanamke ni mjamzito awapo na dalili zote zilizo hapo juu?

  • Hauwezi kuwa na uhakika kuwa ana ujauzito kwa sababu mabadiliko mengine ya mwili ya kawaida au matatizo ya afya hujitokeza sawa na dalili hizi zinazoweza kuashiria ujauzito.

    Mwisho wa jibu

8.2.2 Dalili na ishara zinazoelekea kuashiria ujauzito

Hizi ni za kutegemewa sana kuliko dalili zinazoweza kutokea lakini si ishara kamili za ujauzito.

Kutanuka kwa fumbatio

Kuna kutanuka kwa fumbatio (tumbo) hatua kwa hatua kutoka juma la 7 hadi la 28 la ujauzito. Katika juma la 16 hadi la 22, ukuaji unaweza kuonekana kuwa wa haraka sana uterasi inapoinuka juu kwenye fumbatio.

  • Je, unaweza kupendekeza mambo mengine yanayoweza kusababisha utanukaji wa fumbatio?

  • Dhahiri mno ni kuwa mwanamke huyo ananenepa tu. Lakini pia unapaswa kuwazia ikiwa anaweza kuwa na saratani au aina nyingine ya uvimbe tumboni mwake.

    Mwisho wa jibu

Kipimo cha ujauzito cha korioni ya gonadotropini ya binadamu

Homoni hii hutolewa na sehemu ya kiiinitete siku nane tu baada ya utungisho, kisha na plasenta muda wote wa ujauzito. Inaweza kuguduliwa na vipimo vya kemikali ambavyo kwa kawaida vinaweza kufanywa tu katika vituo vya afya vya kiwango cha juu. Vifaa vya kupima ujauzito vinaweza kununuliwa kutoka kwa maduka mengine ya dawa ingawa ni ghali.

Homoni hiyo inaweza kugunduliwa katika damu na mkojo wa mama siku 8 hadi 10 baada ya utungisho au siku 40 baada ya kipindi cha mwisho cha hedhi. Watu wanaposema ‘kipimo cha ujauzito’, wao humaanisha kipimo cha mkojo cha korioni ya gonadotropini ya binadamu. Ingawa hutoa kiashiria bora cha ujauzito kwa watu wengi, vifaa vya kupima vinaweza kutoa matokeo yasiyo ya kweli, hasa ikiwa havikuwa vimehifadhiwa vizuri, au vimepitisha tarehe. Pia kuna magonjwa mengine yasababishayo kutolewa kwa korioni ya gonadotropini ya binadamu.

Minyweo ya uterasi isiyo na maumivu

Uterasi inapotanuka huwa ya mviringo na mara nyingi huzunguka kuelekea upande wa kulia. Minyweo ya uterasi isiyo na maumivu huhisika kama mkazo au shinikizo. Huanza ujauzito ukiwa na umri wa majuma 28 na kuongezeka katika idadi ya marudio. Minyweo hii hupotea kwa kutembea au kufanya mazoezi wakati minyweo ya leba halisi huongezeka kwa udhabiti.

8.2.3 Dalili chanya za ujauzito

Utambuzi chanya wa ujauzito unaweza kufanywa kwa msingi wa dalili hizi ambazo wakati mwingine huitwa dalili ‘hakika’. Kamwe haziwezi kutambulika hadi baada ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.

Mipigo ya moyo wa fetasi
Mchoro 8.3 fetoskopu ya sikio moja

Kiwango cha kawaida cha mpigo wa moyo wa fetasi ni mipigo 120-160 kwa dakika. Mpigo wa moyo unaweza kugunduliwa baada ya majuma 18-20 ya ujauzito kwa kuweka fetoskopu (Picha 8.3) kwenye fumbatio la mama na kusikiza. Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Kipindi cha 11 na masomo yako ya ujuzi tendaji. Wakati mwingine hospitali huwa na mashine inayoitwa Doppler ya kushika kwa mkono inayoweza kutambua mpigo wa moyo wa fetasi mapema hata kama baada ya majuma kumi ya ujauzito.

Utomasaji wa fetasi

Unapaswa kuweza kuhisi (kutomasa kwa mikono yako) fetasi ikisonga kupitia kuta za fumbatio la mama, ujauzito ukiwa na takriban majuma 18, na baada ya majuma 22, umbo la mtoto linaweza kuhisika. Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Vikao vya 10 na 11 vya Somo na katika masomo yako ya ujuzi tendaji.

Uchunguzi wa kutumia mawimbisauti

Uchunguzi wa kutumia mawimbisauti (au uchunguzivijisauti) ni mojawapo ya visaidizi bora sana vya kiufundi katika kutambua na kufuatilia ujauzito, hata hivyo, unaweza kufanywa tu katika kituo cha afya kwa kutumia vifaa mwafaka. Mawimbi makali sana ya sauti usiyoweza kuyasikia hupitishwa kwenye fumbatio la mama kwa mashine hiyo na kurushwa kurudi nyuma mbali na mtoto. Tarakilishi hugeuza mawimbi haya ya sauti kuwa picha ya umbo la fetasi; plasenta na kiungamwana pia zinaweza kuonekana. Hali njema ya fetasi inaweza kufuatiliwa kwa kutumia vijisauti ujauzito unapoendelea.

  • Je, ni zipi kati ya ishara na dalili za ujauzito zilizo katika Sehemu 8.2.1 hadi 8.2.3 unazoweza kutumia katika kebele yako kukusaidia kutambua ujauzito katika jamii?

  • Unaweza kutegemeza utambuzi wako kwa mchanganyiko wa dalili zinazoweza kuashiria ujauzito ambazo wanawake wanakueleza (amenorea, mabadiliko ya matiti, kichefuchefu na kutapika, hasa magonjwa ya asubuhi, kukojoa mara kwa mara, uchovu wakati wa mchana, ishara za kwanza za uhai wa fetasi, na kloasma); na ishara na dalili zinazoelekea kuashiria ujauzito za kutanuka kwa fumbatio na mwanamke kuwa na minyweo ya uterasi isiyo na maumivu. Ishara chanya unazoweza kutambua katika kiwango cha jamii majuma 18-22 baada ya utungisho ni kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi kwa fetoskopu na kutomasa fetasi kupitia ukuta wa fumbatio la mama.

    Mwisho wa jibu

Zoezi 8.1 Kuuliza maswali kuhusu ishara zinazoweza kuashiria ujauzito

Tenga takriban dakika 10 kwa zoezi hili.

Andika katika Shajara yako ya Masomo maswali ambayo ungemwuliza mwanamke ikiwa unajaribu kujua iwapo huenda awe na ujauzito. Kumbuka kutumia lugha ya heshima na maneno anayoweza kuelewa.

Jadili maswali yako na Mkufunzi wako katika Mkutanao saidizi wa Masomo utakaofuata.

Zoezi hili linahusiana na Swali la Kujitathmini 8.5 mwishoni mwa Kipindi hiki.

8.3 Kutambua mambo yanayoweza kusababisha hatari katika ujauzito

Wacha tuchukulie kuwa umeamua kuwa huenda mwanamke ana ujauzito na kuwa unahitaji kuchukua historia yake ya kitiba ili uweze kupangia utunzaji wake wa ujauzitoni. Lengo muhimu la kuchukua historia ni kutambua ikiwa anaweza kuwa na visababishi vyovyote vya hatari vinavyoweza kusababisha matatizo katika ujauzito, au leba na kuzaa, au katika kipindi cha baada ya kuzaa. Kuuliza maswali maalum hukusaidia kufanya haya.

8.3.1 Je, ana miaka mingapi?

Ujauzito unaweza kusababisha matatizo kwa wanawake wa umri wowote. Lakini wanawake wa umri mdogo sana na wenye umri mkubwa sana huwa na matatizo zaidi.

Wasichana wanaopata ujauzito kabla ya umri wa miaka 17 wanaweza kuwa hawajamaliza kukua. Huenda pelvisi ya msichana haijakua vya kutosha kuweza kuzaa kikawaida. Wasichana wana uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo pia - kama priklampsia (tazama Jedwali 8.2), leba ya muda mrefu na watoto wanaozaliwa mapema sana. Wasichana wanaopata ujauzito wakiwa wachanga sana wanaweza kuwa mama wazuri sana na watunzaji, hata hivyo wengi wao watahitaji ushauri na usaidizi zaidi.

Inaweza kuwa salama kwa wanawake walio na umri mkubwa sana na wenye umri mdogo sana kuzalia katika kituo cha afya kilicho na vifaa, kuliko nyumbani.

Wanawake wakongwe wanaweza pia kuwa na matatizo zaidi katika ujauzito na kuzaa.

Kisanduku 8.2 Priklampsia na eklampsia

Priklampsia ni hali hatari inayojulikana kwa shinikizo la juu la damu (hipatensheni), kufura mikono, miguu na hata uso, na kiwango cha haja cha protini katika mkojo (protinuria). Kwa kawaida hutokea katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito. Wanawake walio na ugojwa huu huhisi kuugua sana na mara nyingi wao huripoti maumivu makali ya kichwa, kichefuchefu, na kutapika.

Ukishuku kuwa mwanamke mjamzito ana priklampsia, unapaswa kumpa rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu mara moja.

Priklampsia isipotibiwa inaweza kuendelea na kuwa eklampsia ambapo dalili hizo zote huwa mbaya zaidi na mwanamke huyo kupata kuchanganyikiwa kiakili, matatizo katika kuona na matukutiko. Eklampsia ni hatari kwa maisha ya mwanamke na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.

Eklampsia, priklampsia, na aina zingine za magonjwa yanayosababishwa na shinikizo la juu la damu hujulikana kama magonjwa ya hipatensheni, yamejadiliwa kwa kina katika Kipindi cha 19.

8.3.2 Je, amezaa watoto wangapi awali?

Wanawake ambao tayari wamewahi kuzaa mtoto mmoja au wawili, na ambao watoto wao walizaliwa wakiwa hai na wenye afya kwa kawaida huwa na matatizo machache katika kuzaa. Wanawake wengine wanaweza kuwa na matatizo zaidi. Mara nyingi kuzaa kwa mara ya kwanza huwa mgumu kuliko kuzaa kwa baadaye. Kuwa mwangalifu kwa dalili hatari na uwe na usafiri tayari wa dharura.

Kwa sababu hii, inaweza kuwa vyema kwa mwanamke anayepata mtoto wake wa kwanza au ambaye amepata watoto watano au zaidi kuzalia katika kituo cha afya.

8.3.3 Je, ujauzito wake umewahi kuharibika?

Wanawake wengine hupata ujauzito unaoharibika mmoja baada ya mwingine, na huenda usijue kisababishi. Mpe rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu ili kujua kisababishi na pia kumsaidia kubeba ujauzito huu hadi mwisho.

Kuharibika kwa ujauzito (ujauzito kutoka wenyewe) ni ambapo ujauzito unatoka kabla ya mwanamke kufikisha majuma 28, mtoto akiwa angali mdogo sana kuweza kuishi nje ya mama bila huduma maalum ya dawa za uangalizi makini wa wagonjwa hospitalini. Uharibikaji wa ujauzito hutokea sana na mara nyingi hutendeka hata kabla ya mwanamke kujua kuwa ana ujauzito.

Huwa vigumu kujua sababu ya kuharibika kwa ujauzito. Lakini visababishi vingine vinaweza kukingwa. Malaria, maambukizi ya zinaa, jeraha, vurugu na dhiki vyote vinaweza kusababisha kuharibika kwa ujauzito.Wakati mwingine, kuharibika kwa ujauzito hutokea mwanamke anapotangamana na sumu au kemikali zenye sumu. Kwa mfano, wanawake wanaofanya kazi kwenye mashamba hupumua au kushika dawa za kuua wadudu mara kwa mara. Hivyo basi kupelekea uharibikaji mwingi wa ujauzito kuliko wanawake wasiotangamana na kemikali hizo. Baadhi ya uharibikaji wa ujauzito unaweza kuzuiwa kwa kuwatibu wanawake walio na magonjwa au maambukizi, au kuwasaidia kuepuka kemikali au dhuluma.

8.3.4 Je, amewahi kutoa mimba?

Mwanamke aliyekuwa mgonjwa, aliyepata jeraha au aliyetokwa na damu nyingi baada ya aina yoyote ya uavyaji wa ujauzito anaweza kuwa na kovu kwenye uterasi yake zinazoweza kusababisha matatizo katika ujauzito huu au kuzaa. Huenda ni salama kwake kuzalia hospitalini.

Ikiwa mtu yeyote au mwanamke mwenyewe atafanya lolote kwenye mwili wake ili kuuharibu ujauzito, itaitwa utoaji wa mimba. Ambapo uavyaji wa mimba ni halali na unapatikana, mwanamke anaweza kuavya mimba salama na kutohatarisha ujauzito utakaofuata.

Mahali ambapo utoaji wa mimba si halali, mwanamke anayejaribu kuharibu ujauzito anaweza kujidhuru au kumwendea mtu asiyeweza kuavya mimba kwa usalama (Jedwali 8.4). Uavyaji mimba usio salama unaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi, maambukizi mabaya, utasa, au hata kifo. Kipindi cha 20 kitakufundisha jinsi ya kumhudumia mwanamke baada ya utoaji mimba usio salama.

Picha 8.4 Maambukizi ni hatari sana hasa kutokana na utoaji mimba usio salama kwa sababu vidole au vyombo vichafu vinaweza kuingizwa kwenye mwili wa mwanamke huyo.

8.3.5 Je, amewahi kupata matatizo yoyote ya kuzaa au ujauzito wa awali?

Ikiwa mwanamke amekuwa akipata matatizo ya kuzaa au ujauzito hapo awali, anaweza kupata matatizo hayo tena. Mwambie mama akuhadithie kuhusu kuzaa na ujauzito wa awali. Mhimize akueleze kila kitu: mazuri na mabaya. Kisha uliza maswali haya ili kujua zaidi kuhusu matatizo ya awali katika ujauzito na jinsi ya kujitayarisha kwa ujauzito huu. Nakili utakayojifunza. Matatizo haya yote yameelezewa kwa kina katika vikao vingine vya somo katika Moduli hii.

Je, alikuwa mchovu, mdhaifu au mwenye anemia?

Kuchoka sana au udhaifu katika ujauzito kwa kawaida husababishwa na anemia (tazama Jedwali 8.1). Ikiwa alikuwa na anemia katika ujauzito wa awali, kuna uwezekano wa kupata tena wakati huu.

Je, alikuwa na shinikizo la juu la damu, kuvimba au matukutiko?

Ikiwa alikuwa na shinikizo la juu la damu katika ujauzito wa hapo awali, kuna uwezekano wa kupata tena. Shinikizo la juu la damu linaweza kuwa dalili ya priklampsia (tazama Jedwali 8.2). Chunguza shinikizo la damu na dalili zingine za priklampsia mara kwa mara na ujitayarishe kumpa rufaa kwenda hospitalini.

Ikiwa alikuwa na matukutiko katika kuzaa au ujauzito wa hapo awali, huenda alikuwa na eklampsia (Jedwali 8.2) na ni dhahiri kuwa anafaa kuzalia hospitalini.

Je, alikuwa na kisukari melitasi?

Ikiwa alikuwa na kisukari melitasi (sukari nyingi sana kwenye damu) katika ujauzito wa awali, kuna uwezekano wa kuupata tena. Kiwango cha sukari kinapokuwa juu sana kwenye damu, kiasi fulani huingia kwenye mkojo damu inapochujwa kwenye figo. Unafaa kupima mkojo wa mwanamke mjamzito ili kubaini iwapo kuna sukari. (Tutakufunza jinsi ya kufanya haya kwenye Kipindi cha 9). Kipimo cha kutegemewa kinaweza kufanywa katika kituo cha afya. Kisukari melitasi kinaweza kuwa kisababishi cha kuharibika kwa ujauzito au matatizo mengine kwa mama au mtoto baada ya kuzaa.

Je, alikuwa na leba iliyokaa muda mrefu sana au awamu ndefu ya kusukuma mtoto?

Je, leba yake ilichukua zaidi ya saa 24 kwa mtoto wa kwanza au zaidi ya saa 12 kwa watoto wengine? Je, alisukuma mtoto kwa zaidi ya saa mbili? Je, mtoto alikuwa katika nafasi yenye ugumu au alikuwa mkubwa sana? Je, alikuwa na woga mwingi? Uliza ikiwa hiyo leba yake iliyokaa kwa muda mrefu ilisababisha matatizo kwake au mtoto wake. Ikiwa uzazi ulikuwa salama kwa mama na mtoto, basi huenda asiwe na tatizo katika kuzaa. Ikiwa kulikuwa na ugumu wa kuzaa, uliza ikiwa anajua kisababishi cha leba kuchukua muda mwingi. Je, alikuwa na anemia?

Je, alikuwa na fistula?

Je, ikiwa alipata leba kwa muda mrefu, ilisababisha fistula (mwanya usio wa kawaida, baina ya uke na labda kibofu cha mkojo, rektamu, urethra au ureta)? Kuna uwezekano wa hili kutokea kwa wanawake waliopitia desturi inayodhuru ya ukeketaji walipokuwa watoto. Mkojo au kinyesi hupita kwenye fistula hadi kwenye uke na kuvuja kwa mfululizo, isipokuwa fistula izibwe kwa njia ya upasuaji.

Historia ya fistula hapo awali inamaanisha ni dhahiri kuwa anapaswa kuzalia hospitalini.

Je, alipata uchungu wa kuzaa (leba) kwa muda mfupi sana (chini ya saa 3)?

Ikiwa mama alipata leba ya muda mfupi sana hapo awali, hakikisha yeye pamoja na familia yake wanajua la kufanya iwapo utachelewa kumfikia na hawawezi kumpeleka katika kituo cha afya. Unaweza kuifunza familia jinsi ya kuzalisha mtoto kwa hali ya dharura. Utajifunza jinsi ya kufanya haya kwenye Moduli inayofuata ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa.

Je, alizaa mapema kabla ya muda?

Ikiwa alipata mtoto aliyezaliwa mapema kwa mwezi mmoja, chunguza ikiwa mchozo ulitoka ukeni mwake. Hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi kwenye uke ambayo yanaweza kusababisha kuzaa kabla ya muda kamili wa ujauzito kukamilika. Kuwa tayari ikiwa mtoto atawasili kabla ya muda na umakinikie dalili za leba zilizoelezewa kwenye moduli inayofuata ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa.

Je, alipata mtoto mdogo (chini ya kilo 2.5 au pauni 5)?

Chunguza ikiwa mtoto alizaliwa mapema (ni kawaida kwa watoto wanaozaliwa mapema kuwa na uzani wa chini). Ikiwa mtoto alikuwa mdogo lakini alizaliwa kwa wakati unaofaa, chunguza ikiwa mama alikuwa na anemia ( Jedwali 8.1), shinikizo la juu la damu au priklampsia (Jedwali 8.2). Chunguza pia ikiwa alipata chakula cha kutosha, ikiwa alivuta sigara au kutumia madawa. Moja ya mambo haya huenda lilisababisha mtoto huyo kuwa na uzani wa chini.

Chunguza ukubwa wa fumbatio lake ili kuona ikiwa mtoto anakua kikawaida. (Utajifunza jinsi ya kufanya haya kwenye Kipindi cha 11). Ukifikiri kuwa huenda mtoto huyu ana uzani wa chini ikilinganishwa na umri wa ujauzito, mama anastahili kuzalia hospitalini kwa sababu watoto wadogo wanaweza kupata matatizo mengi ya kiafya kuliko walio na uzani wa kawaida. (Moduli ya Utunzaji wa baada ya kuzaa itaelezea sababu na jinsi ya kutoa usaidizi).

Je, alipata mtoto mkubwa (zaidi ya kilo 4 au pauni 9)?

Chunguza ikiwa alikuwa na matatizo wakati wa kuzaa. Iwapo hakupata, labda uzazi huu utakuwa salama pia. Lakini, kuwa na mtoto mkubwa kunaweza kuashiria kuwa mama anaugua kisukari melitasi. Chunguza kwa makini uone ikiwa mtoto huyu anaonekana kuwa mkubwa pia. Pima sukari kwenye mkojo wa mama na ikiwezekana aweze kupimwa kisukari melitasi kwenye kituo cha afya.

  • Je, unaweza kueleza ni kwa nini mtoto anaweza kuwa mkubwa iwapo mama ana kisukari?

  • Hapo awali tulisema kuwa mama kuugua kisukari melitasi husababisha ongezeko la sukari kwenye damu. Mtoto hulishwa virutubishi kutoka kwa damu ya mama na kwa hivyo anapata sukari nyingi na huenda akanenepa.

    Mwisho wa jibu.

Je, alivuja damu nyingi kabla au baada ya kuzaa?

Ikiwa alivuja damu nyingi hapo awali kabla au baada ya kuzaa, kuna uwezekano wa kutokea tena. Mhimize akueleze yote anayokumbuka kuhusu kuvuja huko kwa damu. Je, alihitaji usaidizi wa kiafya? Je, alipata anemia baadaye? Je, alikuwa mdhaifu hadi kushindwa kusimama? Majibu ya haya maswali yatakusaidia kujitayarisha kwa yanayoweza kutokea wakati huu. Kuwa tayari kumtibu ikiwa atavuja damu sana baada ya kuzaa. Utajifunza jinsi ya kufanya haya katika Moduli ya Utunzaji katika leba na kuzaa.

Ikiwezekana, mwanamke aliyevuja damu hapo awali anafaa kuzalia hospitalini.

Je, alikuwa na matatizo ya plasenta (baada ya kuzaa)?

Itakuwa vyema ikiwa mwanamke ambaye plasenta yake ilisalia ndani baada ya kuzaa hapo awali atazalia kwenye hospitali ujauzito utakaofuata.

Ikiwa plasenta ya mwanamke huyo haikutoka kwa urahisi hapo awali, tatizo hilo linaweza kutokea tena. Mwambie amakinikie dalili za kuvuja damu katika ujauzito huu na kutafuta usaidizi mara moja kutoka kwa mtaalam wa afya haya yakitokea.

Je, alikuwa na joto jingi mwilini au maambukizi kwenye uke au uterasi?

Kuzaa huku kunaweza kuwa sawa. Lakini ikiwa alikuwa na maambukizi kwenye uke au uterasi katika au baada ya kuzaa hapo awali, kuna hatari ya maambukizi tena wakati huu. Kuwa tayari kuchunguza dalili za maambukizi ya uke. (Kipindi cha 9 kitakufundisha jinsi ya kufanya haya).

Je, alihuzunika (alipata dipresheni) baada ya kuzaa?

Dipresheni ya baada ya kuzaa ni tatizo kubwa sana la kiafya. Kwa hivyo, ni lazima apewe rufaa aende katika kituo cha afya cha kiwango kinachofuata.

Ikiwa mwanamke huyo alipata dipresheni hapo awali baada ya kuzaa, inaweza kutokea tena. Kuwa tayari kutoa usaidizi haya yakitendeka. (Ushauri umeangaziwa katika Kipindi cha 14.)

Je, mtoto aliugua au kufariki kabla, katika na baada ya kuzaliwa?

Ukidhani kuwa kutakuwa na hatari kwa mtoto wake atakayefuata, mpe rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu.

Chunguza visababishi vya mtoto huyu kuugua au kufariki. Je, wataalam wa afya walimwambia kisababishi iwapo alihudumiwa nao? Je, anayo maoni yake kuhusu yaliyotendeka?

Je, mtoto wake alikuwa na kasoro za kuzaliwa?

Kasoro zingine za kuzaliwa hutokea tu na hakuna anayejua sababu. Zingine ni za kifamilia (za kurithiwa). Uliza kuhusu aina ya kasoro na ikiwa kuna mtu yeyote kwenye familia ya mama au ya babake mtoto aliye na kasoro hiyo ya kuzaliwa. Huenda mtoto anayefuata akawa na matatizo hayo hayo. Kasoro zingine husababishwa na maradhi kama vile hepesi au rubela. Ikiwa mwanamke alikuwa na hepesi au rubela katika ujauzito wa awali, mhakikishie kuwa huenda maambukizi haya yasisababishe kasoro za kuzaliwa katika ujauzito huu. Wanawake wajawazito wanapaswa kujaribu wasitangamane na watu wagonjwa. Visababishi vingine vya kasoro za kuzaliwa ni kutangamana na kemikali zenye sumu, madawa au dawa, au zinaweza pia kutokana na lishe duni katika ujauzito. Ulaji wa lishe bora katika ujauzito umeangaziwa katika Kipindi cha 14.

Je, alifanyiwa upasuaji (kuzaa kwa njia ya upasuaji)?

Katika upasuaji wa kuzaa, daktari hukata na kufungua fumbatio na uterasi ya mwanamke ili kumtoa mtoto. Wakati mwingine upasuaji hufanywa kwa sababu mtoto hatoshei kwenye pelvisi ya mama. Vile vile, wakati mwingine hufanywa kwa sababu mtoto yumo hatarini na ni lazima azaliwe kwa haraka. Baada ya mtoto kutoka, daktari hushona uterasi na kufunga fumbatio. Kovu hubaki kwenye uterasi na la pili kwenye fumbatio (Mchoro 8.5).

Ni salama kabisa kwa mwanamke aliyefanyiwa upasuaji awali kuzalia hospitalini tena katika ujauzito utakaofuata.

Mchoro 8.5 Upasuaji wa kuzaa huacha kovu moja kwenye fumbatio (kushoto) na kovu jingine kwenye uterasi (kulia).

Wanawake wengi wanaweza kuzaa kwa njia ya kawaida kupitia ukeni hata ikiwa walizaa kwa njia ya upasuaji hapo awali. Lakini, kuna uwezekano mdogo kuwa kovu lililo kwenye uterasi linaweza kupasuka wakati wa leba. Haya yakitokea, mwanamke pamoja na mtoto wake wanaweza kufariki kutokana na mama kuvuja damu ndani ya mwili.

8.3.6 Je, anayo matatizo mengine yoyote ya kiafya?

Wanawake wengi ni wenye afya na wanaweza kuzaa bila hatari yoyote kuwapata pamoja na watoto wao. Hata hivyo, ni sehemu muhimu ya jukumu lako kama mtaalam wa afya kuwajua wanawake walio katika hatari kubwa kwa sababu ya matatizo waliyo nayo au waliyokuwa nayo. Ikiwa mwanamke mjamzito ni mgonjwa anayekumbwa na mojawapo ya matatizo haya, wakati huu au uliopita, anafaa kupata usaidizi wa kiafya ili kupangia mahitaji yake katika ujauzito na kuamua ikiwa atazalia hospitalini:

  • Kisukari melitasi
  • VVU/ UKIMWI
  • Maambukizi ya kibofu au figo
  • Malaria
  • Kiwango juu cha joto zaidi ya sentigredi 37.5 (100.4 F) kwa zaidi ya siku mbili, au kiwango juu cha joto cha mara kwa mara
  • Shinikizo la juu la damu
  • Priklampsia na eklampsia
  • Ugonjwa wa ini (hepatitisi hasa hepatitisi B)
  • Matatizo ya moyo
  • Kifua kikuu ambacho hakijatibiwa
  • Ulemavu kwenye nyonga au chini ya mgongo.

8.3.7 Maswali yako mwenyewe

Huenda unayo maswali yako mwenyewe ambayo unataka kuwauliza wanawake wajawazito unaokutana nao lakini, hatukuyaweka kwenye Kipindi hiki. Kwa mfano, ikiwa kuna hepatitisi B kwenye jamii yako, unaweza kutaka kumwuliza ikiwa ana ugonjwa huo au kumweleza jinsi ya kuuzuia. Fikiria kuhusu habari unayotakiwa kujua ili kumpa huduma bora katika ujauzito na ujitayarishe kwa leba, kuzaa na kipindi cha baada ya kuzaa.

Baadaye katika moduli hii, Kipindi cha 13 kitaelezea ratiba ya awamu nne za kupokea utunzaji bora katika ujauzito, na mwongozo wa kufuata katika kila awamu. Utajifunza jinsi ya kuandika maelezo wazi na taratibu kwenye kadi ya utunzaji changamani utakayojaza kila unapomtembelea mwanamke mjamzito, katika leba, kuzaa na baada ya kuzaa. Lakini kwanza unahitaji kujua jinsi ya kumchunguza pamoja na mtoto wake, jinsi vikao vya somo vinavyofuata vilivyoeleza.

Muhtasari wa Kipindi cha 8

Katika Kipindi cha 8, umejifuna kuwa:

  1. Ni muhimu kudumisha imani ya mwanamke unapomhoji kuhusu historia ya afya yake, ficha unachonakili na usimfichulie yeyote.
  2. Maswali unayouliza yanafaa kuwa ya heshima na kwa lugha anayoelewa.
  3. Utambuzi wa ujauzito hufanywa kwa msingi wa dalili zilizoripotiwa na mwanamke, ishara na dalili zinazoelekea kuashiria ujauzito na hata zile chanya unazoona mwenyewe au zinazoweza kudhibitishwa kwa uchunguzi wa kimwili au kipimo cha kemikali.
  4. Dalili zinazoweza kuashiria ujauzito mapema katika ujauzito zinazoripotiwa sana ni kukosa hedhi, mabadiliko kwa matiti, kichefuchefu na kutapika hasa asubuhi, kuhisi uchovu, kukojoa mara kwa mara, kuhisi ishara za kwanza za kuwepo kwa mtoto (kumsikia mtoto akisongasonga), na kloasma.
  5. Ishara na dalili zinazoelekea kuashiria ujauzito ni ongezeko katika ukubwa wa fumbatio, matokeo chanya ya kipimo cha ujauzito cha homoni ya binadamu ya korioni ya gonadotropini na minyweo isiyo na maumivu ya uterasi. Dalili chanya ni kutambua mipigo ya moyo wa fetasi, kutomasa fetasi na kutazama picha zitokanazo na uchunguzi wa kutumia mawimbisauti palipo na vifaa.
  6. Wanawake wachanga sana au wakongwe, kina mama wa mara ya kwanza na wanawake waliozaa mara nyingi hapo awali wana uwezekano zaidi wa kupata matatizo katika ujauzito na wanafaa kupewa rufaa kwenda katika kituo cha afya kwa leba na kuzaa.
  7. Ni muhimu kumuuliza mwanamke maswali maalumu ili kutambua visababishi vingine vya hatari kama vile uharibikaji au utokaji wa ujauzito hapo awali, watoto waliozaliwa wakiwa wakubwa mno au wadogo sana, leba iliyokaa kwa muda mrefu au muda mfupi sana, fistula, upasuaji wa kuzaa au kutokwa na damu nyingi kabla au baada ya kuzaa, plasenta iliyosalia ndani, mfadhaiko wa baada ya kuzaa, mtoto aliyezaliwa akiwa amefariki au aliyekuwa na kasoro za kuzaliwa, au historia ya hali za kiafya kama vile shinikizo la juu la damu, kisukari melitasi, anemia, priklampsia au eklampsia, maambukizi, na matatizo ya moyo, figo au ini.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 8

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyofanikisha malengo ya mafunzo kwa kujibu maswali yanayofuata utafiti kifani 8.1. Andika majibu yako kwenye shajara yako ya masomo na ujadiliane na mkufunzi wako katika Kipindi saidizi cha masomo kitakachofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya maswali ya kujitathmini mwishoni mwa moduli hii.

Utafiti kifani 8.1 Je, Bi X ni mjamzito?

Bi X ana umri wa miaka 39 na ameishi katika ndoa kwa miaka 15. Amejaliwa mtoto ambaye alizaliwa miaka kumi iliyopita na ana matumaini kuwa yeye ni mjamzito tena. Bi X anasema kuwa yeye na mumewe hawajatumia uzuiaji mimba na hafikirii kuwa ujauzito wake umewahi kuharibika kwa wakati huo. Hajapata hedhi kwa majuma tisa yaliyopita. Unapomhoji kuhusu mabadiliko kwenye mwili wake tangu hedhi ya mwisho, anasema kuwa hajagundua chochote, lakini amekuwa akihisi uchefuchefu anapoamka asubuhi na yeye huwa na uchovu mwingi sana. Bi X anakuambia kuwa mtoto wake wa kwanza alizaliwa baada ya leba ya saa 30 na alikuwa na uzani wa kilo 4. Pia anakumbuka kuwa alipewa tembe za ayoni lakini hajui sababu.

Maswali ya kujitathmini 8.1 (yanatathmini Malengo ya Somo 8.1, 8.2 na 8.4)

  • a.Je, ni nini kibaya na kumwuliza Bi X ikiwa alipata priklampsia katika ujauzito uliopita?
  • b.Je, kumwuliza swali kwa kutumia maneno hayo kunawezaje kuharibu uaminifu wake kwako?
  • c.Andika swali hili tena ili kuepuka kusababisha matatizo uliyotambua.
Answer
  • a.Mtu ambaye si mtaalam wa afya hawezi kuelewa maana ya priklampsia. Kwa hivyo, hawezi kuelewa swali hilo. Anaweza kusema ‘la’ kwa sababu hataki ufikiri kuwa hajui. Unaweza kukosa kujua habari muhimu kuhusu visababishi vya hatari ikiwa maswali yako hayaeleweki.
  • b.Anaweza kuwa na wasiwasi kuwa unaweza kufikiria yeye ni mjinga kwa sababu hajui neno hili la kitiba.
  • c.Hatujui jinsi ulivyoandika tena swali hilo (kuna njia nyingi bora za kulisema) lakini huenda ulitumia maneno kama;

‘Je, katika ujauzito uliopita, mtaalam wa afya aliwahi kukuambia kuwa una shinikizo la juu la damu au kuwa una protini kwenye mkojo? Je, uliwahi kupitia maumivu makali ya kichwa, kichefuchefu au kutapika na kuvimba nyayo, mikono au uso?’

Mwisho wa jibu

Maswali ya kujitathmini 8.2 (yanatathmini Malengo ya Somo la 8.3)

  • a.Je, ni dalili zipi zinazoweza kuashiria ujauzito zilizo katika utafiti kifani wa Bi X?
  • b.Je, kuna lolote katika historia yake linaloashiria kuwa huenda hana ujauzito?
  • c.Je, angewezaje kujua kwa haraka iwapo huenda ana ujauzito?
Answer
  • a.Bi X anaripoti dalili tatu zinazoweza kuashiria ujauzito: amenorea (kukosa hedhi kwa majuma tisa); kichefuchefu asubuhi na uchovu usio wa kawaida wakati wa mchana.
  • b.Ametaka mtoto mwingine kwa miaka kumi iliyopita lakini hata kwa kutotumia uzuiaji mimba, bado hajashika mimba, na kwa hivyo huenda asiwe na ujauzito.
  • c.Njia ya haraka ya kujua iwapo ana ujauzito inaweza kuwa kuenda katika kituo cha afya kilicho karibu ambapo wanaweza kupima ujauzito kwa kutumia mkojo wake kuchunguza ikiwa una homoni ya korioni ya gonadotropini ya binadamu, ambayo hutolewa na kiinitete na plasenta. Kipimo hiki si ushahidi wa mwisho, bali kinaweza kuashiria ujauzito.

Mwisho wa jibu.

Maswali ya kujitathmini 8.3 (yanatathmini Malengo ya Somo 8.5)

Je, kuna lolote kwenye historia ya Bi X linaloonyesha kuwa anafaa kushauriwa kuzalia kwenye kituo cha afya wakati huu ikiwa ujauzito wake utadhibitishwa? Eleza ni kwa nini ndivyo au sivyo.

Answer

Ikiwa Bi X ni mjamzito, anafaa kushauriwa kuzalia kwenye kituo cha afya wakati huu kwa sababu ya umri wake (ni mama mkongwe kidogo wa miaka 39), alikuwa na leba kwa muda mrefu (zaidi ya saa 24), na mtoto wake wa kwanza alikuwa mkubwa (kilo 4). Visababishi vyote vitatu vya hatari vinaonyesha kuwa huenda akawa na ugumu katika kuzaa mtoto wake wa pili.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 8.4 (linatathmini Malengo ya Somo 8.1 na 8.5)

Eleza ni kwa nini Bi X alipewa tembe za ayoni katika ujauzito wa hapo awali. Je, hii ni ishara kuwa alikuwa na kisababishi kikali cha hatari wakati huo?

Answer

Bi X alipewa tembe za ayoni katika ujauzito wake wa kwanza kama utaratibu wa kumkinga dhidi ya kupata anemia (upungufu wa seli nyekundu za damu). Ayoni huongeza usambazaji wa seli nyekundu za damu ambazo hubeba oksijeni kwenye mwili wake na ule wa mtoto anayekua. Wanawake wote wajawazito wanafaa kupewa tembe za ayoni. Kwa hivyo hiki si kisababishi cha hatari kwa Bi X.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.5 (linatathmini Malengo ya Somo la 8.4)

Je, ni maswali yapi uliyoandika katika Shajara yako ya Masomo ulipokamilisha zoezi 8.1? Je, ulitumia lugha ambayo wanawake kwenye jamii yako wataelewa?

Answer

Hatuwezi kutabiri maswali uliyoandika kwenye Shajara yako ya Masomo wala maneno uliyotumia. Kwa hivyo, maswali yako yanaweza kuwa tofauti kidogo na yetu, na bado yawe bora. Kilicho muhimu ni kuwa lugha uliyotumia inafaa kueleweka kwa wanawake kwenye jamii yako. Unafaa kuuliza maswali kama;

  • Je, hedhi yako ya mwisho ilikuwa lini? Je, umekosa kwa mwezi mmoja?
  • Je, matiti yako yamekuwa makubwa hivi karibuni au yamekuwa laini?
  • Je, umeugua, hasa asubuhi unapoamka?
  • Je, umehisi uchovu usio wa kawaida au kuhisi usingizi wakati wa mchana?
  • Je, umehisi kutaka kukojoa zaidi ya kawaida?
  • Je, umehisi kitu kikisonga kwenye fumbatio lako?
  • Je, fumbatio lako limekuwa kubwa hivi karibuni?

Mwisho wa jibu