Skip to main content
Printable page generated Sunday, 6 October 2024, 5:16 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Sunday, 6 October 2024, 5:16 AM

9. Kutathmini Mama Mjamzito kijumla

Kipindi cha 9 Kutathmini Mama Mjamzito kijumla

Utangulizi

Kipindi hiki kinakuonyesha jinsi ya kutathmini kwa jumla hali ya afya ya mama mjamzito anapotembelea kliniki ya wajawazito. Unapaswa kufanya utathmini huu kila wakati unapompatia huduma ya wajawazito. Kwa kila utathmini, kwanza tunaelezea ishara na dalili zinazoonyesha kwamba mjamzito yuko katika afya nzuri. Kisha tunaelezea ishara na dalili za hatari zinazoweza kusababisha matatizo ya afya ambazo zinaweza kuleta matatizo makali ya ujauzito, zikiwa ni pamoja na anemia, ugonjwa wa kisukari, lishe duni, upungufu wa iodini, shinikizo la juu la damu, joto jingi mwilini, maambukizi, na matatizo ya mapavu na figo.

Baadaye katika moduli hii, utajifunza kuhusu matatizo makali zaidi ya ujauzito kwa undani zaidi - maambukizi ya VVU katika Kipindi cha 16; kupasuka mapema kwa membreni ya fetasi katika Kipindi cha 17; anemia, malaria, na magonjwa ya njia ya mkojo katika Kipindi cha 18; shinikizo la juu la damu, prekilampsia, na eklampsia katika Kipindi cha 19; na kutokwa na damu katika kipindi cha mwanzo na cha mwisho cha ujauzito katika Vipindi vya 20 na 21.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 9

Utakapokamilisha Kipindi hiki, unapaswa kuwa na uwezo wa:

9.1 Kufafanua na kutumia kwa ufasaha maneno yote muhimu yaliochapishwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 9.1)

9.2 Kutambua jinsi ya kutathmini mjamzito kwa weupe, hali ya lishe, kiwango cha mdundo kwa mshipa, shinikizo la damu, joto, upungufu wa pumzi na sukari katika mkojo. (Maswali ya Kujitathmini 9.2 na 9.3)

9.3 Kutambua ishara na dalili za afya bora na zile hatari zinazoweza kuathiri ujauzito, kulingana na tathmini hizi. (Maswali ya Kujitathmini 9.2 na 9.3)

9.1 Kuangalia dalili za lishe duni au ukosefu wa madini ya iodini

Unapoanza huduma ya ujauzito, mmoja kati ya mambo unayopaswa kuuliza kwanza mjamzito ni kama ana dalili zozote zinazoashiria lishe duni au ukosefu wa madini ya iodini kwa mlo wake. Hii ni muhimu sana, kwa sababu lishe duni kwa mama huhusishwa na matokeo duni ya mimba kama vile mtoto mdogo, na anaweza kuwa mfupi. Maswali unayomuuliza lazima ya lenge kugundua iwapo ana dalili hatari zifuatazo (yaani, mambo anayoyaona yeye mwenyewe):

Dalili hatari

  • Kutokuwa na hamu ya kula
  • Kutoongeza uzito
  • Udhaifu na magonjwa ya kimwili kwa ujumla
  • Vidonda, vipele, au matatizo mengine ya ngozi
  • Kidonda au kutokwa na damu kwa ufizi
  • Matatizo ya tumbo au kuhara
  • Joto au kufa ganzi miguuni.

Madhara ya upungufu wa madini ya iodini ni:

Mchoro 9.1 Tezi inaweza kuwa ishara ya hatari ya ukosefu wa madini ya iodini kwa chakula.
  • Tezi (uvimbe mbele ya shingo unaosababishwa na upungufu wa madini ya iodini; Mchoro 9.1)
  • Watoto wafupi
  • Watoto viziwi
  • Watoto walio na ukretini, ulemavu unao athiri fikira.

Kama unashuku kuwa afya ya mjamzito ni duni kutokana na lishe duni, au ukosefu wa virutubishi kwa mlo wake, mshauri kuhusu lishe bora na nyongeza ya iodini. Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika Kipindi cha 14 la Moduli hii.

9.2 Kuangalia uzito wake

Ongezeko bora la uzito

Mama aliye na afya bora huongezea uzito kwa utaratibu kati ya kilo 9-12 wakati wa ujauzito. Hii ni sawa na kilo 1 - 2 kila mwezi. Hata hivyo, kupima uzito kwa kawaida si muhimu kwa huduma ya ujauzito kwa sababu si kiashiria cha uhakika wa matokeo ya mimba. Mama aliye na ongezeko mdogo tu wa uzito anaweza kuwa na matokeo mazuri ya mimba, ingawa hii si kawaida.

Dalili hatari Mjamzito anayeongeza uzito kwa ghafla karibu na kipindi cha mwisho cha ujauzito lazima apewe rufaa kwa kituo cha afya kilichoko karibu.

Kama mama anaongeza uzito kwa ghafla karibu na kipindi cha mwisho cha ujauzito, inaweza kuwa ni ishara ya mapacha, au prekilampsia (shinikizo la juu la damu na protini katika mkojo inayoonekana kwa mara ya kwanza wakati wa ujauzito).

9.3 Kuangalia joto lake

Joto la mwili ni kipimo cha jinsi tishu za ndani za mwili zilivyo moto au baridi. Ingawa inatofautiana kidogo wakati wa joto au baridi, au kama mtu amevaa nguo nyingi au chache mno, au anapofanya kazi nzito ya kimwili, inakaa kwa ujumla karibu na kiwango kinachojulikana kama joto ya 'kawaida', isipokuwa kama mtu ni mgonjwa. Joto la mwili hupimwa kwa kutumia chombo kitwacho kipimajoto (Kielelezo 9.2a), ambacho kina 'balbu' katika sehemu moja ya mwisho, kwa kawaida iliyojazwa na kiowevu cha chuma cha fedha inayoitwa zebaki. (Baadhi ya vipimajoto vilivyo vya glasi huwa na rangi nyekundu badala, na zingine hutumia teknolojia ya tarakimu. Angalia Kielelezo 9.2b) Katika kipimajoto cha glasi, wakatibalbu ya zebakiinapashwa joto na mwili wa mtu, zebaki inapanuka na kupanda hadi kwa tyubu nyembamba ya glasi, ambayo ina alama zilizo na nambari zinazoonyesha hali ya joto katika mwili wa mtu.

Kielelezo 9.2 (a) Kipimajoto cha glasi kinaweza kupima kwa Selisiasi(juu) au Farenhaiti (chini). (b) Kipimajoto cha tarakimukinachonyesha joto kama nambari iliyo kwa dirisha.

Joto la kawaida

Joto la kawaida ni karibu Nyuzi 37, au ni chini ya Farenhaiti 98. Hauhisi joto unapomgusa mama.

Ishara hatari

Mama ana joto jingi mwilini - joto zaidi ya Nyuzi 37.5 (au 100 Farenhaiti ). Unahisi joto unapomgusa mama.

Mchoro 9.3 Unaweza kuhisi kwa urahisi kama ni moto zaidi kukuliko.

9.3.1 Jinsi ya kupima joto lake

Kama huna kipimajoto, wekelea nyuma ya mkono wako mmoja juu ya paji la uso wa mama, na nyingine juu yako mwenyewe, au kwa mtu mwingine aliye na afya (Mchoro 9.3). Ikiwa mama ana joto jingi mwilini, unaweza kuhisi kuwa ngozi yake ni moto zaidi kuliko ile ya mtu mwenye afya.

Mchoro 9.4 Tingisha zebaki hadi chini Nyuzi 36.

Iwapo una kipimajoto cha glasi, kisafishe vizuri kwa sabuni na maji safi, au spiriti. Shikilia kipimajoto upande wa 'balbu' iliyo na zebaki ya fedha ikiangalia mbali na mkono wako. Kitingishe kwa kusongesha kifundo (Mchoro 9.4), mpaka juu ya safu nyembamba ya zebaki ya fedha inaanguka chini ya halijoto ya mwili la 'kawaida', hii ni, chini ya Nyuzi 36 (au Farenhaiti 96 ).  

Weka mwisho wa balbu ya kipimajoto chini ya ulimi wa mama au katika kwapa lake, na ukiwache hapo kwa dakika tatu. Mama anapaswa kufunga kinywa, au kuweka mkono karibu na mwili wake.

Toa kipimajoto na ukigeuze mpaka uone mstari wa fedha. Pahali ambapo fedha inasimama inaonyesha kiwango cha halijoto. Kawaida kuna alama ndogo pahali pa kiwango cha 'kawaida'.

  • Halijoto inayoonekana katika Kielelezo 9.2a ni ngapi?

  • Zebaki imepanda hadi karibu Nyuzi 39.6 – joto jingi mwilini.

    Mwisho wa jibu

Kila wakati safisha kipamajoto ukitumia sabuni na maji baridi, au na spiriti, baada ya kutumia. Usitumie maji moto - yanaweza kuvunja kipimajoto! Zebaki ni chuma iliyo na sumu sana. Kuwa makini na vipimajoto vya glasi, na vikivunjika, usichukue zebaki kwa mikono yako wazi. Fagia zebaki na utie ndani ya chupa na uizike. Usiwaruhusu watoto kucheza na vipimajoto au zebaki. Tafuta kipimajoto cha tarakimu kama unaweza (Kielelezo 9.2b).

9.3.2 La kufanya iwapo mama ana joto jingi mwilini

Joto jingi mwilini inaweza kusababishwa na:

  • Ugonjwa - kwa mfano, homa au malaria
  • Maambukizi kwa sehemu ya mwili - kama vile maambukizi kwa kibofu cha mkojo, au uterasi
  • Joto kiasi pia inaweza kusababishwa na upungufu wa maji mwilini (upotezaji wa viowevu mwilini kutokana na kutokunywa maji ya kutosha).

Kama joto jingi mwilini halijashuka chini katika masaa nane, rufaa mama kwenye kituo cha afya.

Joto jingi mwilini inahitaji kupunguzwa mara moja. Ili kupunguza joto jingi mwilini:

  • Mpe paracetamol (miligramu) 500 - 1000 kwa kinywa kila baada ya saa 4-6
  • Anywe kikombe kimoja cha maji kila baada ya saa
  • Mwoshe mwili na kitambaa kilichowekwa katika maji baridi

9.4 Kuchunguza mipigo yake kwa mshipa

Kielelezo 9.5 Tumia vidole viwili au vitatu (kamwe si kidole cha gumba) kuhisi mipigo katika shingo au ndani ya kifundo.

Mpigo kwa mshipa itakuonyesha jinsi moyo inapiga. Kila wakati moyo inapopiga (jikaza) inasukuma damu ndani ya mishipa. Unaweza kuhisi kila 'mpigo kwa mshipa' kwa kufinya polepole mshipa wa ateri na vidole. Mpigo kwa mshipa ya kila mtu ni tofauti. Hiyo ni kawaida. Unaweza kupata mpigo katika shingo au kifundo, kama inavyoonyeshwa katika Kielelezo 9.5.

Mipigo kwa mshipa ya kawaida

Kiwango cha kawaida cha Mipigo kwa mshipa ni kama 60-80 kwa dakika wakati mama anapumzika.

Ishara hatari

Kiwango cha mipigo kwa mshipani 100 au zaidi kwa dakika wakati mama anapumzika.

9.4.1 Jinsi ya kupima kiwango cha mipigo kwa mshipa

Subiri hadi mama apumzike na kutulia. Weka vidole viwili juu ya mshipa (Mchoro 9.6). Usitumie kidole cha gumba, kwa sababu kuna mpigo mdogo katika kidole hiki ambacho kinaweza kukuchanganya.

Mchoro 9.6 Hakikisha mama ameketi katika hali ya utulivu wakati unapima kiwango cha mipigo kwa mishipa.

Kama una saa iliyo na mkono wa sekunde, hesabu kiwango cha mipigo kwa mshipa wa mama kwa dakika moja. Andika idadi.

Mara ya kwanza, uwe na mtu wa kukuangalilia saa, na kukwambia wakati dakika moja imepita. Wengi huwa na ugumu wa kuhesabu kwa ufasaha wakati wanaangalia saa. Wanamwelekeo wa kuhesabu mpigo mmoja kila sekunde, haijalishi kwa kweli haraka ya mpigo kwa mshipa.

Kama huna saa iliyo na mkono wa sekunde, angalia mipigo hata hivyo. Unaweza kujifunza kufahamu kama ikawa ni polepole, kawaida, au haraka ikilinganishwa na mipigo yako mwenyewe, na yale ya kina mama wengine.

9.4.2 La kufanya iwapo mama ana mipigo kwa mshipa ya haraka

Kama hujui ni nini inayosababisha kiwango cha juu cha mpigo kwa mshipa (zaidi ya 100 kwa dakika), rufaa mama kwa kituo cha afya kilichoko karibu.

Kama mipigo yake ni ya kiwango cha 100 au zaidi kwa dakika, anaweza kuwa na moja au zaidi ya matatizo yafuatayo:

  • Mfadhaiko, hofu, wasiwasi, au kuhuzunika
  • Anemia
  • Maambukizi kama vile malaria
  • Maambukizi kwa kibofu cha mkojo au katika uterusi
  • Kuvunja damu sana
  • Matatizo ya tezi
  • Matatizo ya moyo

9.5 Kuchunguza dalili za anemia

Wakati mtu ana anemia, kawaida inamaanisha kwamba hajaweza kula vyakula vilivyo na madini ya ioni ya kutosha. Madini ya ionihusaidia seli za damu nyekundu kubeba oksijeni kutoka kwa hewa tunayovuta hadi kwa sehemu zote za mwili. Baadhi ya aina za anemia husababishwa na ugonjwa, si ukosefu wa ioni. Na baadhi ya aina zingine hurithiwa (maumbile) na haziwezi kutibiwa kwa kula vyakula vyenyeioni au kutumia dawa za ioni. Utajifunza kupima damu, na matibabu ya anemia wakati wa ujauzito, katika Kipindi cha 18, baadaye katika Moduli hii.

Mchoro 9.7 Weupe unaweza kuwa ishara ya anemia.

Ishara na dalili za afya

Afya njema na nguvu nyingi kwa jumla. Mama hana weupe (angalia sehemu inayofuata).

Ishara na dalili za hatari

  • Weupe - weupe ndani ya kope, kucha na ufizi nyeupe (Mchoro 9.7)
  • Kizunguzungu au kuzirai
  • Udhaifu au kuchoka
  • Mpigo kwa mshipa wa mwendo wa kasi (zaidi ya mipigo100 kwa dakika)
  • Ugumu wa kupumua (upungufu wa pumzi).

9.6 Kuchunguza upungufu wa pumzi

Upumuaji wa kawaida

Baadhi ya upungufu wa pumzi, hasa wakati wa kipindi cha mwisho cha ujauzito, ni ya kawaida. Wanawake wengi hupata upungufu kiasi cha pumzi wakati wako na mimba ya miezi wa 8 au 9.

  • Je, unafikiri hii husababisha na nini?

  •  Mtoto anapokuwa mkubwa, anabana mapafu hivyo nafasi ya kupumua hupunguka. Upumuaji unaweza kuwa rahisi wakati mtoto anapoteremka chini katika tumbo muda mfupi kabla ya leba kuanza. 

    Mwisho wa jibu

Mchoro 9.8 Upungufu wa pumzi unaweza kuwa dalili ya hatari.

Dalili hatari

Kama upungufu wa pumzi unamfanya mjamzito kukosa utulivu, hii ni dalili hatari, hasa kama ana dalili zingine za ugonjwa (Mchoro 9.8).

Upungufu wa pumzi pia unaweza kusababishwa na:

  • Anemia
  • Matatizo ya moyo
  • Kifua kikuu
  • pumu
  • Maambukizi ya mapafu
  • Damu kuganda katika mapafu
  • Aleji.

Iwapo mjamzito ana matatizo ya kupumua wakati wote, au tatizo kali hata mara moja, au kama unashukuanaweza kuwa na ugonjwa wowote uliotajwa, mwelekeze kwenye kituo cha afya.

9.7 Kuchunguza shinikizo lake la damu

Shinikizo la damu inamaanisha hali ambapo damu 'inasukuma' kuta za mishipa mikubwa ya damu inaposukumwa ndani ya mwili na moyo. Shinikizo la damu hupimwa kwa milimita ya zebaki (kiowevu cha chuma cha fedha, ambacho kina alama ya Hg ya kemikali), hivyo vipimo vya shinikizo la damu inaandikwa kama mmHg ikifuatiwa na nambari. Tutakuonyesha jinsi ya kupima shinikizo la damu katika Sehemu ya 9.7.1.

Madaktari na wauguzi huita nambari iliyo juu shinikizo la sistoli, na ya chini la diastoli.

Kipimo cha shinikizo la damu ni nambari mbili zilizoandikwa mmoja juu ya nyingine. Nambari iliyo juu itakueleza shinikizo la damu ya mama kwa wakati huyo moyo wake 'unapopiga' na kusukuma damu kwa mwili wake. Nambari ya chini itakueleza shinikizo la damu yake wakati moyo wake inapopumzika katikati ya mipigo, ili iweze kujaa damu tena.

Shinikizo la damu la kawaida

Shinikizo la damu la kawaida huwa kati ya mmHg 90/60 (useme hii kwa sauti ‘milimita tisini kwa sitini’ za zebaki,) na chini ya mmHg 140/90 (‘milimita mia moja arubanini kwa tisini’ za zebaki). Huwa haiongezeki sana wakati wa ujauzito.

Dalili za hatari

Shinikizo la juu la damu linajulikana kwa tiba kama hipatensheni na ni dalili ya hatari. Mama ana shinikizo la juu la damu ikiwa mmoja kati ya haya ni kweli:

  • Nambari ya juu ni 140 au zaidi.
  • Nambari ya chini ni 90 au zaidi.

Shinikizo la chini mno la damu (chini ya mmHg 90/50) pia ni daliliyahatari, ambayo kwa kawaida husababishwa tu na kuvuja kwingi kwa damu au mshtuko (upungufu hatari wa damu mwilini). Hali hii ni hatari sana.

Mama ambaye ana shinikizo la chini la damu anapaswa kupewa rufaa kwenye kituo cha afya kilichoko karibu mara moja.

Moyo ni kama pampu, inayosukuma damu mwilini. Shinikizo la juu la damu inamaanisha kwamba moyo lazima ifanye kazi kwa nguvu ili kusukuma damu kupitia mishipa zilizokazwa au nyweka (vena na ateri). Kiasi cha shinikizo la damu huonyesha ugumu ule damu inasukumwa. Kumbuka kwamba shinikizo la damu, si sawa na mpigo kwa mshipa. Unaweza kuwa na mpigo iliyo ya chini na shinikizo la juu la damu.

Ni muhimu sana kuchunguza shinikizo la damu ya mama kila anapotembelea kliniki ya wajawazito na kumpa rufaa kwenye kituo cha afya kama iko juu sana.

Wakati mama ana shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito, ni vigumu kwa damu yake kuleta chakula na oksijeni kwa mtoto kupitia plasenta. (Ulijifunza kuhusu haya katika Kipindi cha 5.) Kisha mtoto hukua polepole mno. Shinikizo la juu mno la damu linaweza pia kusababisha mama kuwa na matatizo ya figo, kuvuja damu kwa uterasi kabla ya kuzaa, au kuvuja damu kwa ubongo (kiharusi). Inaweza pia kuwa ni ishara ya prekilampsia, ambayo inaweza kusababisha kuzaa kabla ya wakati, kufuja damu, msukosuko, au hata kifo kwa mama.

9.7.1 Jinsi ya kupima shinikizo la damu

Kuna aina kadhaa za vifaa vya kupimia shinikizo la damu (Kielelezo 9.9).

Kielelezo 9.9 Kifaa cha kupimia shinikizo la damu kinaweza kuwa na geji ndefu (kushoto) au iliyo mviringo (katikati). Pia utahitaji stethoskopu (kulia).

Unapopima shinikizo la damu ya mama, kwanza mwambie utakachofanya, na ni kwa nini. Hakikisha kwamba ameketi au amelala vizuri na anajihisi kuwa ametulia. Kielelezo 9.10 inaonyesha mchakato wa hatua kwa hatua.

Kielelezo 9.10 Michoro 1 - 7 Zinakuonyesha jinsi ya kupima shinikizo la damu.

Vile hewa inavyotoka nje, utaanza kuhisi mipigo kwa mshipa ya mama kupitia stethoskopu yako. Tazama pahali mshale upo (tazama Kielelezo 9.11), au pale safu ya zebaki itasimama kama unakifaa chenye geji ndefu (kama juu iliyo kushoto wa Kielelezo 9.9).

Kielelezo 9.11 Geji hii ni ya mviringo, na shinikizo linaloonyeshwa na mshale. Aina nyingine ya kifaa cha kupimia shinikizo la damu huwa na geji ndefu na safu uliowima ya zebaki fedha na nambari kwa upande (picha iliyo kushoto wa Kielelezo 9.9). Juu ya safu ya fedha inaonyesha shinikizo la damu.

Ikiwa shinikizo la damu ya mama iko zaidi ya 140/90, basi iko juu mno na inaweza kuwa dalili ya hatari. Anahitaji kupewa rufaa kwa kituo cha afya.

Unaweza kurekodi shinikizo la damu ya mama:

  • Utakapoanza kuhisi mpigo kwa mshipa (hii itakuwa nambari ya juu), na
  • Wakati mpigo itatoweka au kupungua (hii itakuwa nambari ya chini). Pima shinikizo la damu ya mama kila anapotembelea kliniki.
Kielelezo 9.12 Rekodi shinikizo la damu ya mama kama inavyooneshwa katika mfano huu.
  • Andika shinikizo la damu kwenye kadi yake ya kurekodi ya kipindi kabla ya kuzaa hivyo unaweza kuangalia mabadiliko yanavyoendelea (tazama mfano katika Kielelezo 9.12). Ikiwa shinikizo lake la damu linaenda juu, mshauri aje kila wiki mpaka uwe na uhakika kwamba haiendelei kupanda.
  • Angalia kwa makini Kielelezo 9.12. Je, kuna mwezi ambayo

    shinikizo la damu ya mama huyu ilikuwa juu kutosha kuwa dalili ya hatari?

  • La. Nambari iliyo juu haizidi 110, na nambari ya chini kamwe haizidi 72. Ni kawaida kwa nambari kutofautiana kidogo mwezi baada ya mwezi.

    Mwisho wa jibu

9.8 Kuchunguza ugonjwa wa kisukari

Wakati mama ana ugonjwa wa kisukari, mwili wake hauwezi kutumia sukari yote kwa damu, hivyo inakaa juu sana na baadhi yake inaweza kuonekana kwa mkojo wake.

Ishara na dalili za hatari

Kama mama ana baadhi ya dalili za hatari zifuatazo, anaweza kuwa na ugonjwa wa kisukari. Kina mama wanaougua ugonjwa wa kisukari kwa kawaida hawana ishara hizi zote. Lakini vile mama ana dalili zaidi, ndivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba ana ugonjwa wa kisukari.

Mchoro 9.13 Kukojoa mara kwa mara kunaweza kuwa onyo la dalili ya ugonjwa wa kisukari.
  • Alikuwa na ugonjwa wa kisukari katika ujauzito wa awali.
  • Mmoja wa watoto waliozaliwa alikuwa mkubwa sana (zaidi ya kilo 4); hii ni kwa sababu sukari nyingi katika damu ya mama humfanya mtoto kuongeza uzito kupita kiasi.
  • Mmoja wa watoto wake alikuwa mgonjwa sana au alikufa wakati wa kuzaliwa bila kujua sababu.
  • Yeye ni mnene.
  • Yeye hupatwa na kiu kila wakati.
  • Yeye huwashwa mara kwa mara na ana harufu mbaya inayotoka kwa uke wake.
  • Majeraha yake hupona polepole.
  • Yeye hukojoa mara kwa mara zaidi kuliko wajawazito wengine (Mchoro 9.13).
  • Uterasi yake ni kubwa kuliko ya kawaida kutokana na ile miezi amekuwa mjamzito.

9.8.1 Vipimo vya mkojo kwa ugonjwa wa kisukari

Kuna kipimo cha mkojo kwa ugonjwa wa kisukari ambacho unaweza kufanya kwa kituo kidogo cha afya na kipimo kinachoaminika kinachoweza kufanywa tu kwa kituo cha afya.

Kupima kwa kutumia kijiti

Ikiwa mama ana dalili za hatari au dalili zilizotajwa hapo juu, na unashuku kuwa anaweza kuwa na ugonjwa wa kisukari, pima mkojo wake kwa njia zifuatazo. Utahitaji 'vijiti vya kutumbukiza' vya kupimia mkojo vilivyotolewa kwa kituo chako kidogo cha afya. Vijiti vya kutumbukiza vina mistari ya kemikali mwishoni ambavyo vinabadilisha rangi wakati vinapatana na sukari.

  • Mwambie mama akojoe kwa chombo kisafi. Kama inawezekana, chukua sampuli ya mkojo 'katikati ya mkondo' (yaani, ile mkojo inayotoka baada ya mchururo wa kwanza; wacha kabla amalize kukojoa).
  • Shikilia kijiti upande wa mwisho usiokuwa na mistari wa kemikali, na utumbukize mwisho ulio na mistari ya kemikali katika mkojo uliotoka wakati huo. Itoe nje mara moja.
  • Ondoa mkojo uliozidi kutoka kijiti cha kupima kwa kupitisha kwa ukingo wa chombo.
  • Shikilia kijiti sambamba kabla ya kusoma matokeo.
  • Kama sukari imezidi kwa mkojo, itaathiriana na kemikali kwenye kijiti. Rangi itabadilika kutoka kijani kuwa kahawia, kulingana na kiasi cha sukari katika mkojo.
Kipimo rahisi cha mkojo ambacho anaweza kufanya nyumbani
Mchoro 9.14Mchwa huvutiwa na sukari katika mkojo wa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari.

Ikiwa mama ana dalili na ishara za hatari zilizotajwa kwa ukurasa uliopita, lakini anaonekana hana nia ya kutembelea kituo cha afya ili apimwe damu, au huna vijiti vya kupima mkojo wake, unaweza kumshauri kuhusu njia rahisi anayoweza kujipima nyumbani. Mwambie akojoe kwenye chombo kisafi kama vile jagi au kikombe, na aiwache chombo nje. Iwapo mchwa wataingia ndani ya chupa (Kielelezo 9.14), pengine kuna sukari kwa mkojo wa mama - dalili ya ugonjwa wa kisukari. Mweleze mama ahakikishe amekwambia ikiwa dalili ipo! Akishuhudia mwenyewe anaweza kushawishika kwenda kwa kituo cha afya ilikuthibitisha utambuzi huo na kupewa matibabu.

9.8.2 Jinsi ya kumsaidia mama aliye na ugonjwa wa kisukari

Ukishuku kwamba mama ana ugonjwa wa kisukari, anapaswa kupata usaidizi wa matibabu. Anapaswa kupanga kuzaa mtoto wake hospitalini.

Wakati mwingine ugonjwa wa kisukari katika kipindi cha ujauzito inapungua ikiwa mama atakula chakula bora na kufanya mazoezi. Lazima ale vyakula mbalimbali vilivyo na virutubishi, ajiepushe na pipi, sukari, na ale milo midogo midogo mara kwa mara. Lakini ugonjwa wa kisukari unaweza kumfanya mama awe mgonjwa zaidi na kuzaa kwake kuwe hatari zaidi. Mtoto wake anaweza kuwa mkubwa sana, kuwa na matatizo ya kuzaliwa nayo, au anaweza kuwa mgonjwa sana na kufa baada ya kuzaliwa. Wakati mwingine dawa inahitajika ili kuzuia matatizo makali.

9.9 Kuchunguza maambukizi ukeni

Mchozo wa kawaida ukeni haunuki, iko kiasi kidogo, na haiweki doa wala kulowesha chupi.

Dalili za hatari

Ikiwa mama ana maambukizi ukeni, ishara ni:

  • Mchozo mweupe unaoonekana kama maziwa ya mgando
  • Mchozo ulio na harufu mbaya
  • Kuwasha kwa sehemu ya nje ya uzazi (angalia nyuma katika Mchoro 3.2 kwa Kipindi cha 3 ili kujikumbusha kuhusu anatomi ya sehemu ya jenitalia ya wanawake)
  • Vulva inaweza kuwa na uvimbe
  • Kunaweza kuwa na uchungu wakati wa kukojoa
  • Mama anaweza kuripoti ana maumivu wakati wa ngono

Ikiwa mama anamchozo ambayo sio ya kawaida, au anaripoti dalili zozote zingine zilizotajwa hapo awali, mpe rufaa kwenye kituo cha afya kilicho karibu haraka iwezekanavyo.

9.10 Hitimisho

Katika Kipindi hiki, umejifunza jinsi ya kufanya utathmini wa kawaida kwa mama mjamzito anapotembelea kliniki ya wajawazito, na kutambua dalili za afya au dalili na ishara hatari na hatua ambazo unaweza kuchukua. Umejifunza jinsi ya kutathmini kina mama kwa hali duni ya lishe, weupe, ugumu wa kupumua, shinikizo la juu la damu, joto jingi mwilini, ugonjwa wa kisukari, na maambukizi ukeni. Umejifunza jinsi ya kupima joto, mpigo na shinikizo la damu, na kupima sukari kwa mkojo. Katika Kipindi kijacho, utajifunza jinsi ya kufanya uchunguzi wa fumbatio ya mama mjamzito kupima ukubwa wa uterasi yake. Hii inakusaidia kutambua kama fetasi inakuwa kwa njia ya kawaida wakati wa ujauzito.

Muhtasari wa Kipindi cha 9

Katika Kipindi cha 9, umejifunza kwamba:

  1. Kila wakati mama anapotembelea kliniki ya wajawazito, unapaswa kutathmini wajawazito wote kwa ishara na dalili za lishe duni au upungufu wa madini ya iodini, pamoja na weupe, ukosefu wa nguvu na uwepo wa tezi.
  2. Wanawake wengi huongeza kilo 9-12 wakati wa ujauzito wa kawaida, lakini ongezeko la uzito si kiashiria cha uhakika wa matokeo ya mimba. Ongezeko la uzito kwa ghafla karibu na kipindi cha mwisho wa mimba ni onyo la kuwa kuna uwezekano wa hali prekilampsia na lazima apewe rufaa kwenye kituo cha afya.
  3. Joto jingi mwilini (joto zaidi ya Nyuzi 37.5) inapaswa kutibiwa mwanzo na viowevu, paracetamol, na kupanguza mwili kwa maji baridi. Mpe mjamzito rufaa kwenye kituo cha afya kama hali yake ya joto itabaki juu. Anahitaji kuchunguzwa kwa magonjwa kama vile malaria.
  4. Kama kiwango cha mpigo wa mshipa kitaongezeka zaidi ya midundo 100 kwa dakika moja, ni ishara ya ugonjwa na anahitaji rufaa kwenye kituo cha afya.
  5. Ishara na dalili za anemia ni pamoja na weupe, uchovu, mpigo kwa mshipa wa haraka, na ugumu wa kupumua. Rufaa wajawazito walio na hali hizi.
  6. Upungufu wa pumzi huwa kawaida karibu na kipindi cha mwisho cha ujauzito vile mtoto anayekuwa hufinya mapafu ya mama. Mpe rufaa iwapo itasababisha usumbufu mkubwa.
  7. Kama shinikizo la damu ya mama mjamzito itafika mmHg 140/90 au zaidi, ana shinikizo la juu la damu. Kila shinikizo la juu la damu katika ujauzito ni ugonjwa mkali, ambayo inahitaji rufaa mara mojakwa kituo cha afya.
  8. Mchozo usio wa kawaida kutokea ukeni, kuwashwa au uvimbe wa viungo vya uzazi, na uchungu wakati wa kukojoa au wa ngono, ni dalili za maambukizi kwa uke, na ni lazima apewe rufaa.

Maswali za Kujitathmini ya Kipindi cha 9

Kwa vile umekamilisha Kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyopata mafanikio yake ya Matokeo ya Kujifunza kwa kujibu maswali haya. Andika majibu yako kwa Shajara lako la Somo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Mkutano ujao wa Somo Saidizi. Unaweza kulinganisha majibu yako na Maelezo kwa Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa moduli hii.

Swali la Kujitathmini 9.1 (linatathmini Malengao ya Somo la 9.1)

Linganisha kila utambuzi na ishara au dalili hatari inayohusishwa.

Using the following two lists, match each numbered item with the correct letter.

  1. Weupe

  2. Uvimbe shingoni

  3. Joto jingi mwilini

  4. Uterasi kubwa kuliko iliyotarajiwa kwa hatua ya mimba

  5. Shinikizo la juu la damu

  • a.Ugonjwa wa kisukari

  • b.Tezi

  • c.Prekilampsia

  • d.Malaria

  • e.Anemia

The correct answers are:
  • 1 = e
  • 2 = b
  • 3 = d
  • 4 = a
  • 5 = c

Swali la Kujitahmini 9.2 (linatathmini Malengo ya Somo 9.2 na 9.3)

Je, taarifa zipi zifuatazo si kweli? Katika kila hali, sema kwa ni nini sio sahihi.

  • A.Tezi kwa wajawazito husababishwa na upungufu wa madini ya ioni.
  • B.Ugonjwa wa kisukari kwa wajawazito mara nyingi husababisha mtoto kuzaliwa akiwa mkubwa.
  • C.Upungufu wa pumzi inaweza kusababishwa na anemia, matatizo ya moyo, maambukizi ya mapafu, au kuganda kwa damu.
  • D.Shinikizo la damu ya mmHg 90/50 ni dalili ya afya bora.
  • E.Kiwango cha mpigo kwa mshipa wa midundo 80 kwa dakika au chini inawezea kuwa ishara hatari ya anemia.
  • F.Shinikizo la damu na kiwango cha mdundo kwa mishipa zinapaswa kupimwa wakati mama ameketi akiwa ametulia.
Answer

A si kweli. Tezi husababishwa na upungufu wa madini ya iodini, na si ya ioni.

B ni kweli. Kisukari kwa mjamzito matokeo yake mara nyingi huwa ni mtoto mkubwa kwa sababu mama ana sukari nyingi mwilini, ambayo inamfanya mtoto awe mnene

C ni kweli. Ugumu wa kupumua unaweza sababishwa na anemia, matatizo ya moyo, maambukizi kwa mapafu, au donge la damu.

D si kweli. Shinikizo la damu la mmHg 90/50 liko chini sana, na ni ishara ya hali ya kutokwa na damu nyingi au mshtuko. Katika hali kama hiyo mama lazima apewe rufaa kwenye kituo cha afya mara moja.

E si kweli. Mdundo kwa mshipa wa kawaida wakati mama anapopumzika huwa mipigo 60-80 kwa dakika. Mipigo ya kasi (midundo 100 kwa dakika au zaidi) inaweza kuwa ishara ya anemia.

F ni kweli. Shinikizo la damu na kiwango cha Mpigo zinapaswa kupimwa wakati mama ameketi akiwa ametulia.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitahmini 9.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 9.2 na 9.3)

Wakati wa kipindi kabla ya kuzaliwa unapoenda kumwona Zufan, nakili vipimo vifuatafuatavyo:

  • Joto: Nyuzi 37.2
  • Kiwango cha mipigo kwa mshipa: midundo 96 kwa dakika
  • Shinikizo la damu: mmHg 142/100

Je, unapaswa kumpa Zufan rufaa kwa kituo cha afya? Eleza ni kwa nini unapaswa au haupaswi kumpa Zufan rufaa kwa kituo cha afya.

Answer

Unapaswa kumpa rufaa Zufan mara moja. Ingawa joto lake liko karibu na ya kawaida na hatoi waziwazi, mipigo yake kwa mshipa wako kwa kiwango cha kasi kuliko ya kawaida, na shinikizo lake la damu liko juu sana – nambari ya juu na ya chini zote zimezidi kiwango cha onyo ya mmHg 140/90.

Mwisho wa jibu