Skip to main content
Printable page generated Thursday, 8 Dec 2022, 22:25
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2022 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 8 Dec 2022, 22:25

10. Kukadiria Umri wa Ujauzito kutoka kwa Kipimo cha Urefu wa Fandasi

Kipindi cha 10 Kukadiria Umri wa Ujauzito kutoka kwa Kipimo cha Urefu wa Fandasi

Utangulizi

Katika kipindi hiki, utajifunza jinsi ya kuchukua kipimo muhimu ambacho kinapaswa kufanywa katika kila safari ya utunzaji katika ujauzito - kupima urefu wa sehemu ya juu ya uterasi ya mama kama njia ya kukadiria ikiwa mtoto wake anakua kikawaida. Tutakufundisha njia mbili za kufanya hivi - kutumia vidole na kutumia chenezo laini. Hii hukuwezesha kukadiria kipindi cha ujauzito wake, na kuchunguza usahihi wa tarehe anapotarajiwa kuzaa ikikokotolewa tangu kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi cha mama. Kisha tutajadili sababu zinazoweza kuifanya uterasi kukua haraka sana au polepole sana na hatua unazopaswa kuchukua ukishuku kuwa huenda kuna tatizo.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 10

Baada ya kusoma katika kipindi hiki unapaswa uweze:

10.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyochapishwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 10.1)

10.2 Kujua jinsi ya kupima urefu wa fandasi kwa kutumia mbinu ya vidole na chenezo laini. (Swali la Kujitathmini 10.1)

10.3 Kufasili vipimo vya urefu wa fandasi ili kukadiria ukuaji wa kawaida wa fetasi kulingana na umri wa ujauzito. (Swali la Kujitathmini 10.2)

10.4 Kutambua mambo yanayoweza kusababisha vipimo visivyo vya kawaida vya urefu wa fandasi na uchukue hatua mwafaka. (Swali la Kujitathmini 10.3)

10.1 Je, kupima urefu wa uterasi ya mama hutueleza nini?

Lengo la kupima urefu wa uterasi ya mama ni kubaini iwapo mtoto anakua kikawaida katika kila kipindi cha ujauzito. Unapopima uterasi, unachunguza kujua ilipo sehemu ya juu ya uterasi.

Ishara bora

 • Urefu wa uterasi hulingana na umri wa ujauzito, yaani, idadi ya majuma au miezi ya ujauzito.
 • Sehemu ya juu ya uterasi huinuka kwenye fumbatio la mama kwa takriban upana wa vidole viwili au sentimita 4 kila mwezi.

Ishara za hatari

 • Urefu wa uterasi haulingani na idadi ya majuma au miezi ya ujauzito.
 • Sehemu ya juu ya uterasi inainuka zaidi ya au chini ya upana wa vidole viwili au sentimita 4 kila mwezi.
 • Je, unakumbuka jina la sehemu yenye umbo la kuba juu ya uterasi? (Ulisoma haya katika Kipindi cha 3.)

 • Huitwa fandasi.

  Mwisho wa jibu

Unapopima sehemu ya juu ya uterasi ilipofika kwenye fumbatio la mama, unapima urefu wa fandasi. Hii ni njia sahihi zaidi ya kukadiria ukuaji wa fetasi kuliko kupima uzani wa mama. Kupima urefu wa fandasi hukuonyesha mambo matatu:

 • Idadi ya miezi ambayo mwanamke huyo amekuwa mjamzito.
 • Tarehe anayotarajiwa kuzaa. Iwapo uliweza kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa tangu hedhi yake ya mwisho, kupima urefu wa sehemu ya juu ya uterasi kunaweza kukusaidia kujua ikiwa tarehe anayotarajiwa kuzaa ni sahihi. Iwapo hukuweza kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa kutoka kwa kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, kupima urefu wa fandasi kunaweza kukusaidia kujua tarehe anayotarajiwa kuzaa. Hii inafaa kufanywa katika uchunguzi wa kwanza wa utunzaji katika ujauzito.
 • Kiwango cha ukuaji wa mtoto. Katika kila uchunguzi katika ujauzito, pima urefu wa fandasi ili kujua ikiwa mtoto anakua kwa kiwango cha kawaida. Iwapo anakua haraka sana au polepole sana, huenda kuna tatizo.

Mtoto anapokua ndani ya uterasi, unaweza kuhisi uterasi ikikuwa kubwa kwa fumbatio la mama. Sehemu ya juu ya uterasi husonga takriban upana wa vidole viwili au sentimita 4 zaidi kila mwezi (Kisanduku 10.1).

Kisanduku 10.1 Mabadiliko kwa urefu wa fandasi katika ujauzito wa kawaida

Baada ya takriban miezi mitatu (majuma 13-14), sehemu ya juu ya uterasi huwa juu ya mfupa wa kinena wa mama (ambapo vuzi huanzia).

Baada ya takriban miezi mitano (majuma 20-22), sehemu ya juu ya uterasi huwa kwenye kitovu cha mama.

Baada ya takriban miezi tisa (majuma 36-40), sehemu ya juu ya uterasi karibu inafikia sehemu ya chini ya mbavu za mama.

Watoto wanaweza kuteremka chini katika majuma machache kabla ya kuzaliwa. Unaweza kutazama Picha 7.1 katika Kipindi cha 7 uone mchoro wa urefu wa fandasi katika majuma tofauti ya umri wa ujauzito.

10.2 Jinsi ya kupima urefu wa fandasi

Ili kuhisi uterasi, mama anapaswa kulala chali na awe na viegemeo chini ya kichwa na magoti. Mweleze utakayofanya (na sababu ya kufanya hivyo) kabla ya kuanza kugusa fumbatio lake. Mguso wako unapaswa uwe thabiti lakini wa upole. Songesha vidole vyako kuelekea juu upande wa fumbatio (Mchoro 10.1) hadi utakapohisi sehemu ya juu ya fumbatio lake chini ya ngozi. Itahisika kama mpira mgumu. Unaweza kuhisi sehemu ya juu kwa kuzungusha vidole vyako pole pole kwenye fumbatio.

Mchoro 10.1 Mwanamke akiwa amelala chali, anza kwa kutafuta sehemu ya juu ya uterasi kwa vidole vyako. Kisha ujue mwanamke ana ujauzito wa miezi mingapi kwa kulinganisha idadi ya vidole na Mchoro 10.2 (kila mstari ni takriban upana wa vidole viwili).

10.2.1 Jinsi ya kupima urefu wa fandasi kwa mbinu ya kutumia vidole

Ikiwa sehemu ya juu ya uterasi iko chini ya kitovu, pima ni vidole vingapi vitakuwa chini ya kitovu. Ikiwa sehemu ya juu ya uterasi iko juu ya kitovu, pima ni vidole vingapi vitakuwa juu ya kitovu.

Mchoro 10.2 Kupima urefu wa fandasi kwa kutumia vidole. Mwanamke amelala chali. Kila mstari unawakilisha upana wa vidole viwili.
 • Tazama kwa makini Mchoro 10.2. Iwapo mtoto anakua kikawaida, je, uterasi inapaswa kuongezeka kwa upana wa vidole vingapi katika trimesta ya pili (miezi 3-6 ya ujauzito, au majuma 15-27 yaliyokamilika ya ujauzito)?

  Mchoro 10.3 Urefu wa fandasi baada ya miezi 7 ya ujauzito.
 • Urefu wa fandasi unapaswa kuongezeka kwa upana wa vidole 6 (upana wa vidole viwili kila mwezi) katika trimesta ya pili.

  Mwisho wa jibu

 • Je, ni upana wa vidole vingapi juu ya kitovu inapostahili kuwa sehemu ya juu ya uterasi baada ya miezi 7 ya ujauzito?

 • Tazama Mchoro 10.3 kupata jibu.

  Mwisho wa jibu

 • Je, utaelezaje mahali pa mstari wa nukta baada ya miezi 9 katika Mchoro 10.2 chini ya mstari unaoonyesha urefu wa fandasi baada ya miezi 8 ½ hadi 9?

 • Watoto wanaweza kuteremka chini majuma machache kabla ya kuzaliwa (tazama Kisanduku 10.1).

  Mwisho wa jibu

 • Tazama michoro katika Mchoro 10.4 (a) na (b). Je, ujauzito wa wanawake hawa ni wa majuma mangapi kwa mujibu wa mbinu ya kutumia vidole kupima urefu wa fandasi iliyoonyeshwa katika Mchoro 10.2?

  Mchoro 10.4 (a) na (b) Je, unafikiri michoro hii inaonyesha miezi mingapi ya ujauzito?
 • Katika Mchoro 10.4 (a) mwanamke ana takriban miezi 4 ½ ya ujauzito. Katika Mchoro 10.4 (b), yuko na takriban miezi 6 ½ ya ujauzito (vidole vitatu juu ya kitovu).

  Mwisho wa jibu

Unapopima urefu wa fandasi katika kila safari ya utunzaji katika ujauzito nakili idadi ya vidole ulivyotumia kupima urefu wa uterasi kwenye kadi yake. Weka alama ya ‘+’ (kuongeza) mbele ya nambari hiyo ikiwa sehemu ya juu ya uterasi iko juu ya kitovu. Weka alama ya ‘-’ (kutoa) mbele ya nambari hiyo ikiwa sehemu ya juu ya uterasi iko chini ya kitovu.

 • Je, ni vipi utakavyonakili vipimo vilivyoonyeshwa katika Picha 10.4 (a) na (b)?

 • Kipimo kilicho katika Mchoro 10.4 (a) kitaandikwa kama -2. Kipimo kilicho katika Mchoro 10.4 (b ) kitakuwa +3.

  Mwisho wa jibu

Upungufu wa mbinu ya kutumia vidole

Unapaswa kujua kuwa mbinu ya kutumia vidole kukadiria umri wa ujauzito (idadi ya majuma/miezi ya ujauzito) ina upungufu fulani unaoathiri usahihi wake.

 • Tazama mikono yako. Je, unaweza kusema ni kwa nini mbinu ya kutumia vidole inaweza kutoa makadirio tofauti ya umri wa ujauzito ikiwa wahudumu wa afya wawili tofauti walitumia mbinu hii kupima urefu wa fandasi ya mwanamke mmoja?

 • Kutokana na tofauti kubwa katika unene wa vidole vyetu, kunaweza kuwa na tofauti ya hadi majuma matatu kati ya kipimo cha urefu wa fandasi ya mwanamke mmoja kilichofanywa na watu wawili tofauti. (Hii huitwa ‘tofauti katika mitazamo ya wachunguzi,’yaani tofauti kati ya wachunguzi tofauti.)

  Mwisho wa jibu

Hata mhudumu mmoja akipima urefu wa fandasi ya mwanamke mmoja mara kadhaa kwa siku moja, huenda jibu likawa tofauti kila wakati kwa sababu mbinu ya kutumia vidole haina usahihi kamilifu. (Hii huitwa ‘tofauti katika mitazamo ya mchunguzi mmoja’, yaani tofauti kwa mchunguzi mmoja katika nyakati tofauti.)

Mwishowe, huenda umegundua kuwa umbali kati ya kinena simfisisi (mfupa wa kinena) na kitovu ni tofauti kati ya wanawake wakati hawana ujauzito na tofauti hii huathiri usahihi wa kipimo cha urefu wa fandasi kwa mbinu ya kutumia vidole. Kwa mfano, inachukulia kuwa umbali kati ya kinena simfisisi na kitovu ni sentimita 20 katika ujauzito wa majuma 20 bali inaweza kuwa ndefu sana hadi sentimita 30 na fupi sana hadi sentimita 14.

Kukabiliana na upungufu huu, imependekezwa kuwa upime urefu wa fandasi kwa chenezo laini iwapo unayo, jinsi ilivyoelezwa hapa chini.

10.2.2 Jinsi ya kupima urefu wa fandasi kwa chenezo laini

Unaweza kutumia mbinu hii sehemu ya juu ya uterasi inapokua kufikia kitovu cha mwanamke.

Katika nusu ya pili ya ujauzito, ukubwa wa uterasi kwa sentimita huwa karibu na idadi ya majuma ambayo mwanamke amekuwa mjamzito. Kwa mfano, kama imekuwa majuma 24 tangu kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, urefu wa uterasi huwa sentimita 22-26. Uterasi inapaswa kukua kwa sentimita 1 kila juma, au sentimita 4 kila mwezi.

 1. Weka kitambaa au chenezo laini ya plastiki kwenye fumbatio la mama ukiwa umeshikilia alama ya 0 (sifuri) kwa chenezo hiyo kwenye sehemu ya juu ya mfupa wa kinena (tazama alama ya mshale katika Mchoro 10.5a).
 2. Fuata mkunjo wa fumbatio lake na ushikilie chenezo kwenye sehemu ya juu ya uterasi (Mchoro 10.5b).
 3. Andika idadi ya sentimita kutoka sehemu ya juu ya mfupa wa kinene hadi kwenye sehemu ya juu ya uterasi.
Mchoro 10.5 (a) Alama ya mshale imeelekezwa sehemu ya juu ya mfupa wa kinena. Weka alama ya 0 (sifuri) ya chenezo hapa. (b) Fuata mkunjo wa fumbatio la mwanamke na ushikilie chenezo kwenye sehemu ya juu ya uterasi.

Madaktari, wauguzi, na wakunga wengi hufundishwa kuhesabu muda wa ujauzito kwa majuma badala ya miezi. Wao huanza kuhesabu siku ya kwanza ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi, ingawa mwanamke anaweza kuwa alipata ujauzito majuma mawili baadaye. Kuhesabu hivi hufanya ujauzito mwingi kuwa na muda wa majuma 40 (au unaweza kusema kuwa muda wa kawaida wa ujauzito ni majuma 40).

10.3 Je, na ikiwa ukubwa wa uterasi si ulivyotarajia?

Iwapo unapima kwa usahihi na hupati sehemu ya juu ya uterasi unapoitarajia kuwa, kwa mujibu wa tarehe aliyokupa mwanamke huyo ya kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, inaweza kumaanisha mambo matatu tofauti:

 • Tarehe anayotarajiwa kuzaa uliyopata kwa kuhesabu kutoka kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi huenda haikuwa sahihi.
 • Huenda uterasi (na mtoto) inakua haraka sana.
 • Huenda uterasi (na mtoto) inakua pole pole sana.

10.3.1 Tarehe anayotarajiwa kuzaa uliyopata kwa kuhesabu tangu kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi si sahihi

Kuna sababu kadhaa za uwezekano wa tarehe ya kutarajia kuzaa tangu kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi kutokuwa sahihi. Wakati mwingine wanawake hawakumbuki tarehe ya kipindi chao cha mwisho cha kawaida cha hedhi kikamilifu. Wakati mwingine mwanamke hukosa hedhi kwa sababu nyingine, na kisha apate ujauzito baadaye. Mwanamke huyu anaweza kuwa na ujauzito mchanga kuliko ulivyofikiria na kwa hivyo uterasi ni ndogo kuliko unavyotarajia. Au wakati mwingine mwanamke anatokwa na damu kidogo baada ya kupata ujauzito. Iwapo alichukulia kuwa hiyo ilikuwa kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, mwanamke huyu atakuwa na ujauzito wa mwezi moja au miwili zaidi ya ulivyofikiria. Uterasi itakuwa kubwa kuliko unavyotarajia.

Kumbuka kuwa tarehe za kutarajiwa kuzaa si kamili kabisa. Mara nyingi wanawake huzaa hadi baada ya au kabla ya majuma mawili au matatu kutoka tarehe wanayotarajiwa kuzaa. Hii huwa salama.

Ikiwa tarehe ya kutarajia kuzaa hailingani na ukubwa wa uterasi katika safari ya kwanza, nakili. Subiri na upime tena uterasi baada ya kati ya majuma mawili au manne. Iwapo uterasi itakua kwa takriban upana wa vidole viwili au sentimita 1 kwa mwezi, tarehe ya kutarajia kuzaa uliyopata kwa kuhisi sehemu ya juu ya uterasi inaweza kuwa si sahihi. Huenda tarehe ya kutarajia kuzaa uliyopata kutoka kwa kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi si sahihi.

10.3.2 Uterasi inakua haraka sana

Ikiwa uterasi inakua zaidi ya upana wa vidole viwili kwa mwezi, au zaidi ya sentimita 1 kwa juma, kuna uwezekano wa visababishi kadhaa tofauti:

 • Huenda mama ana pacha.
 • Huenda mama ana kisukari melitasi.
 • Huenda mama ana maji mengi (kiowevu cha amnioni) kwenye uterasi.
 • Huenda mama ana ujauzito bandia (tyuma badala ya mtoto).

Ukifikiri kuwa huenda kukawa na pacha, hata ikiwa kuna mpigo mmoja tu wa moyo, mpe mwanamke huyo rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu.

Huenda mama ana pacha

Inaweza kuwa vigumu kujua kwa hakika kuwa mama ana ujauzito wa pacha.

Ishara za pacha ni:

 • Uterasi hukua haraka au huwa kubwa zaidi ya kawaida.
 • Unaposhika fumbatio la mama, unaweza kuhisi vichwa viwili au matako.
 • Unaweza kusikia mipigo miwili ya moyo. Hii si rahisi kutambua, lakini inaweza kutambulika katika miezi miwili ya mwisho.

Tutakuonyesha jinsi ya kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi kupitia kwa fumbatio la mama katika Kipindi cha 11. Kwa sasa, tunalenga pacha kama kisababishi cha uterasi kuwa kubwa zaidi ya inavyotarajiwa. Hapa kunazo njia mbili za kusikiza mipigo ya mioyo ya pacha:

Mchoro 10.6 kupiga kwa mioyo ya fetasi kwa mwendo sawa kunaweza kukuonyesha ikiwa mtoto ni mmoja au wawili.
 1. Tafuta mpigo wa moyo wa mtoto mmoja. Mwambie msaidizi asikize sehemu zingine ambako mpigo wa moyo ni rahisi kusikika. Akisikia mpigo wa moyo, mwambie asikize sehemu moja huku nawe ukisikiza sehemu nyingine. Kila mmoja wenu anaweza kutumia mkono wake kupiga mpigo wa moyo. Ikiwa midundo ni sawa, huenda mnasikiza mtoto mmoja. Ikiwa mipigo si sawa, huenda mnawasikiza watoto wawili tofauti (Mchoro 10.6).
 2. Ikiwa huna msaidizi, bali una saa iliyo na mshale wa sekunde au kipima saa cha kujitengenezea, jaribu kupima kila mpigo wa moyo kivyake. Ikiwa mipigo hiyo ya moyo si sawa, huenda unasikiza watoto wawili tofauti.

Kwa kuwa uzazi wa pacha ni mgumu au hatari kuliko ule wa mtoto mmoja, ni salama kwa mwanamke kwenda hospitalini kwa kuzaa. Kwa kuwa pacha wana uwezekano mkubwa wa kuzaliwa mapema, mama anafaa kuwa na usafiri tayari wakati wote baada ya mwezi wa sita wa ujauzito. Ikiwa hospitali iko mbali sana, ni vyema mama kusonga karibu katika miezi ya mwisho ya ujauzito. Hakikisha una mpango wa jinsi ya kupata usaidizi wakati wa dharura.

Huenda mama ana kisukari melitasi

Ulijifunza kuhusu ishara za hatari za kisukari katika Kipindi cha 9.

 • Je, ni nini utakachotarajia kupata iwapo mwanamke ana ishara zote za hatari za kisukari?

 • Mpe mwanamke huyo rufaa aende katika kituo cha afya ukishuku kuwa huenda ana kisukari melitasi.

  Alikuwa na kisukari katika ujauzito uliopita. Mmoja wa watoto wake wa hapo awali alizaliwa akiwa mkubwa sana (zaidi ya kilo 4), au alikuwa mgonjwa au alifariki akizaliwa na hakuna anayejua sababu. Ni mnene. Anahisi kiu kila wakati. Anajikuna mara kwa mara na harufu mbaya kutoka ukeni mwake. Vidonda vyake vinapona pole pole. Anakojoa mara kwa mara zaidi ya wanawake wengine wajawazito. Uterasi yake ni kubwa zaidi ya kawaida kulingana na umri wa ujauzito. Unapofanya uchunguzi wa dipstick, kuna sukari kwenye mkojo wake (Sehemu ya 9.8.1 ya Kipindi cha 9).

  Mwisho wa jibu

Maji mengi sana kwenye uterasi

Maji mengi sana (kiowevu cha amnioni) si tatizo wakati wote, bali yanaweza kufanya uterasi kutanuka sana. Kisha uterasi haiwezi kunywea ipasavyo ili kusukuma mtoto nje, au kuzuia kutoka kwa damu baada ya kuzaa. Katika hali chache mno inaweza kumaanisha kuwa mtoto atakuwa na matatizo ya kuzaliwa. Jaribu kumpa mwanamke huyu rufaa aende katika kituo cha afya kinachoweza kumpa sonogramu (uchunguzi wa mawimbi ya vijisauti) ikiwa kipimo cha uterasi ni kikubwa sana na hutarajii pacha.

Ujauzito bandia (tyuma)

Wakati mwingine mwanamke hupata ujauzito, bali tyuma hukua badala ya mtoto. Hii huitwa ujauzito bandia (Mchoro 10.7). Madoadoa ya damu na tishu (wakati mwingine zenye umbo la zabibu) vinaweza kutoka ukeni mwake.

Mchoro 10.7 Ujauzito bandia (tyuma) ukikua kwenye uterasi badala ya mtoto.

Ukitambua ishara na dalili za ujauzito bandia, mpe mwanamke huyo rufaa aende hospitalini haraka iwezekanavyo. Tyuma hiyo inaweza kuwa saratani na kumwua, wakati mwingine haraka sana. Daktari wa upasuaji anaweza kuondoa tyuma hiyo ili kuokoa maisha ya mwanamke huyo.

Dalili zingine za ujauzito bandia ni:

 • Mpigo wa moyo wa fetasi hausikiki.
 • Mtoto hawezi kuhisika.
 • Mwanamke amekuwa na kichefuchefu muda wote katika ujauzito.
 • Ana madoadoa ya damu, na tishu zenye umbo sawa na mkungu wa zabibu kutoka ukeni.

10.3.3 Uterasi inakua polepole sana

Ukuaji wa pole pole wa uterasi unaweza kuwa dalili ya mojawapo ya matatizo haya:

 • Huenda mama ana kiasi kidogo cha maji (kiowevu cha amnioni) kwenye uterasi. Wakati mwingine ni kiasi kidogo cha maji kuliko kawaida na kila kitu bado kiko SAWA. Wakati mwingine, kiasi kidogo sana cha maji kinaweza kumaanisha kuwa mtoto si wa kawaida, au anaweza kuwa na matatizo katika leba.
 • Huenda mama huyo hupata lishe duni. Chunguza chakula ambacho mama amekuwa akila. Ikiwa hana uwezo kabisa wa kupata chakula kizuri cha kutosha, jaribu kupata njia ya kumsaidia yeye na mtoto wake. Kina mama na watoto wenye afya huimarisha jamii.
 • Huenda mama ana shinikizo la juu la damu (hipatensheni). Shinikizo la juu la damu linaweza kumfanya mtoto asipate lishe anayohitaji ili kukua vizuri. Ulijifunza jinsi ya kuchunguza shinikizo lake la damu katika kipindi kilichopita.
 • Huenda mama hunywa pombe, huvuta sigara au hutumia madawa. Haya yanaweza kufanya mtoto kuwa mdogo. Jaribu kutafuta mbinu za kumsaidia kuacha mienendo hii inayodhuru.
 • Huenda mtoto amefariki. Watoto waliofariki hawakui na kwa hivyo uterasi hukoma kukua.

Ikiwa huna kifaa kinachofaa kuchunguza shinikizo lake la damu, na uterasi inakua pole pole sana, mpe rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu kwa uchunguzi.

Jinsi ya kujua ikiwa mtoto amefariki

Ukishuku kuwa huenda mtoto amefariki, mpe mama rufaa aende katika kituo cha afya kwa uzazimfu.

Ikiwa mama ana ujauzito wa miezi 5 au zaidi, mwulize ikiwa amemsikia mtoto akisonga hivi karibuni. Ikiwa mtoto hajasonga kwa siku mbili, huenda kuna tatizo. Ikiwa mama ana ujauzito wa zaidi ya miezi saba, au ikiwa ulisikia mpigo wa moyo wa mtoto katika safari ya awali, sikiza mpigo huo tena.

Mwanake akiripoti kutosonga kwa fetasi na huwezi kuusikia mpigo wa moyo, huenda mtoto amefariki. Iwapo hivyo, ni muhimu kwa mtoto aliyekufa (uzazimfu) kuondolewa haraka kwa sababu huenda mwanamke huyo akatokwa na damu kuliko kina mama wengine, na yuko katika hatari zaidi ya maambukizi.

Mama anapompoteza mtoto, anahitaji upendo, utunzaji na kueleweka (Mchoro 10.8). Hakikisha kuwa hapitii leba pekee yake. Akizaa mtoto mfu hospitalini, mtu anayemwamini anafaa kukaa naye wakati wa uzazi huo.

Mchoro 10.8 Mama anapompoteza mtoto wake, anahitaji upendo, utunzaji na kueleweka.

10.4 Hitimisho

Katika kipindi hiki, umejifunza jinsi ya kupima urefu wa fandasi kwa kutumia vidole vyako au chenezo. Pia umejifunza jinsi ya kufasili matokeo ya vipimo na kuchukua hatua mwafaka. Katika kipindi kinachofuata, utajifunza jinsi ya kuchunguza mtoto alipo kwa kutomasa (kuhisi) fumbatio la mama na kusikiza mahali ulipo mpigo wa moyo wa fetasi.

Muhtasari wa Kipindi cha 10

Katika Kipindi cha 10, umejifunza kuwa:

 1. Kupima urefu wa fandasi hukufahamisha umri wa ujauzito, jinsi mtoto anavyokua na siku anayotarajiwa kuzaliwa.
 2. Kumbuka kumlaza mama ifaavyo kabla ya kupima urefu wa fandasi. Fandasi ya uterasi hukua kwa wastani wa upana wa vidole viwili kwa kila mwezi wa ujauzito.
 3. Ikiwa urefu wa fandasi haulingani na umri wa ujauzito, unafaa kuchunguza muda wa ujauzito tangu kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi. Kuwa na tarehe isiyo sahihi ni mojawapo ya sababu kuu za tofauti kati ya urefu wa fandasi na umri wa ujauzito.
 4. Ikiwa urefu wa fandasi ni mkubwa zaidi ya inavyotarajiwa kwa umri wa ujauzito huo, huenda mama alikupa tarehe isiyo sahihi ya kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, au ana pacha, kisukari melitasi, maji mengi sana kwenye uterasi, au ujauzito bandia.
 5. Ikiwa urefu wa fandasi ni mdogo zaidi ya inavyotarajiwa kwa umri wa ujauzito huo, huenda mama alikupa tarehe isiyo sahihi ya kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi, huenda ana kiasi kidogo sana cha kiowevu cha amnioni kinachozunguka fetasi, shinikizo la juu la damu, lishe duni, huenda anakunywa pombe au anatumia madawa mengine yanayodhuru, au huenda mtoto ni mfu.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 10

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini ni kwa kiasi kipi umeweza kutimiza Malengo yake kwa kujibu maswali yanayofuata uchunguzi maalum 10.1. Andika majibu yako kwenye Shajara yako ya Masomo na ujadili na mkufunzi wako katika mkutano saidizi wa masomo utakaofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Uchunguzi Maalum 10.1 Abebech

Abebech ni mwanamke mjamzito ambaye umri wa ujauzito wake ni miezi sita kulingana na kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi. Unapomchunguza, unaweza kuhisi kuwa fandasi yake iko upana wa vidole vinne juu ya kitovu chake na unaweza kuusikia mpigo wa moyo vizuri.

Swali la Kujitathmini 10.1 (linatathmini Malengo ya Somo 10.1 na 10.2)

 • a.Je, umri wa ujauzito wa Abebech ukitumia kipimo cha urefu wa fandasi ni upi?
 • b.Je, fumbatio la Abebech lingekuwa sentimita ngapi kutoka kwa mfupa wa kinena hadi juu ya uterasi yake ili kuthibitisha kipimo chako cha urefu wa fetasi?
Answer
 • a.Umri wa ujauzito huu kulingana na kipimo cha urefu wa fandasi ni miezi saba.
 • b.Ikiwa kweli Abebech ni mjamzito wa miezi saba, utatarajia fumbatio lake kuwa sentimita 28 kutoka kwa mfupa wa kinena hadi juu ya uterasi, yaani, takribani sentimita 1 kwa kila juma la ujauzito tangu kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi. Kumbuka kuwa kipimo kinaweza kuwa kati ya sentimita 26 na 30.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 10.2 (linatathmini Lengo la Somo 10.3)

Je, umri wa ujauzito wa Abebech kulingana na kipimo cha urefu wa fandasi unalingana na umri wa ujauzito huo uliokokotolewa tangu kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi?

Answer

Umri wa ujauzito kulingana na urefu wa fandasi ni mwezi mmoja zaidi ya inavyotarajiwa tangu tarehe ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi. Kwa hivyo, uterasi ni kubwa zaidi ya inavyotarajiwa tangu tarehe ya kipindi cha mwisho cha kawaida cha hedhi.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 10.3 (linathmini Lengo la Somo 10.4)

Je, ni maelezo yapi unayoweza kutoa kwa matokeo yako katika kisa cha Abebech, na ni hatua zipi utakazochukua?

Answer

Huenda uterasi ni kubwa zaidi ya inavyotarajiwa kwa sababu tarehe ya kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi inaweza kuwa si sahihi, na kwa hakika Abebech ana ujauzito wa miezi saba. Hili si tatizo, lakini ni muhimu kuchunguza maelezo mengine yoyote. Kwa mfano, huenda ana kiowevu kingi cha amnioni (maji) kinachomzunguka mtoto kwenye uterasi; mpe rufaa aende kwenye kituo cha afya kwa uchunguzi wa mawimbi vijisauti kujua iwapo hili ndilo tatizo. Au huenda ana ujauzito wa pacha. Unaweza kusikia vizuri mpigo mmoja wa moyo wa fetasi, kwa hivyo tafuta mtu mwingine akusaidie kusikiza kwenye fumbatio la Abebech ili kuona ikiwa mtasikia mipigo miwili ya mioyo ya fetasi. Ukishuku kuwa ana pacha, mpe rufaa aende kwenye kituo cha afya kilicho karibu.

Mwisho wa jibu.