Katika kipindi hiki tunazingatia uchunguzi wa mwili wa mama ili kujua kuhusu mkao na afya ya mtoto wake. Utajifunza jinsi ya kuchunguza fumbatio la mama ili kubaini iwapo mtoto amelala kichwa juu, kichwa chini au kingamo kwenye uterasi yake. Kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi pia kunaweza kukufahamisha kuhusu mkao na hali njema ya mtoto. Mwishoni mwa kipindi hiki tunakupa mwongozo kuhusu la kufanya ukishuku kuwa mkao wa mtoto unaweza kusababisha ugumu au hatari katika kuzaa, au ukishuku kuwa mwanamke huyo ana pacha.
Baada ya kipindi hiki, unapaswa uweze:
11.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyochapishwa kwa herufi nzito. (Swali la kujitathmini 11.1)
11.2 Kujua jinsi ya kutambua mkao wa kawaida na usio wa kawaida kwa utomasaji na oskalitesheni. (Maswali ya kujitathmini 11.1 na 11.2)
11.3 Kujua jinsi ya kutathmini hali njema ya fetasi kwa oskalitesheni na kucheza kwa fetasi. (Maswali ya kujitathmini 11.1, 11.3 na 11.4)
11.4 Kutambua hali za fetasi zinazohitaji kupewa rufaa kwenda katika kituo cha afya kilicho karibu. (Swali la kujitathmini 11.4)
Mkao wa mtoto kwenye uterasi huitwa mlalo wa fetasi. Lengo la kujua mlalo wa fetasi ni kutambua iwapo kuna dalili zozote za hatari zinazoweza kuleta ugumu katika leba na kuzaa, na kumweka mama na mtoto hatarini.
Kuna mbinu mbili za kujua mkao wa mtoto - kuhisi fumbatio la mama (utomasaji), na kusikiza (oskalitesheni) ambapo sauti ya mpigo wa moyo wa fetasi ni kubwa. Unaweza kuhitaji kutumia mbinu zote mbili ili kuwa na uhakika wa mkao wa mtoto.
Inaweza kuwa vigumu kujua mkao wa mtoto kabla ya miezi sita au saba ya ujauzito, na si muhimu hadi majuma 36 (miezi minane) kwa sababu ni kawaida mtoto kuzunguka hadi mwezi wa mwisho. Mara tu ujauzito unapotimiza miezi sita au saba, itakuwa rahisi kuhisi mtoto na kujua mkao wake kwenye uterasi.
Kwanza, msaidie mama kulala chali na umwekee viegemeo chini ya magoti na kichwa chake. Hakikisha ametulia. Maswali unayojaribu kujibu unapomchunguza ni:
Watoto wengi huwa wamelala wima kufikia mwezi wa saba, kichwa kikiwa kimeelekea kwenye seviksi ya uterasi. Huu ndio mkao salama kabisa kwa uzazi wa kawaida. Ili kujua iwapo mtoto yuko wima, weka mkono bapa kwa kila upande wa fumbatio la mama. Finya kwa upole lakini kwa uthabiti, kwanza kwa mkono mmoja na kisha huo mwingine (Mchoro 11.1a). Chunguza umbo kwa makini. Je, miisho ya mtoto inaonekana kuwa kwenye pande za mama (Mchoro 11.1b)? Ikiwa ni hivyo, mtoto anaweza kuwa amelala kingamo. Watoto wengi hulala kingamo katika miezi ya kwanza lakini wengi hujigeuza kichwa chini kufikia miezi minane au zaidi. Watoto hawawezi kuzaliwa kupitia ukeni wakiwa katika mlalo wa kingamo. Mtoto aliyelala kingamo, na hawezi kugeuzwa leba inapoanza lazima azaliwe kwa upasuaji wa kuzaa hospitalini.
Mtoto akilala kingamo baada ya miezi minane ya ujauzito, mpe mwanamke huyo rufaa aende katika kituo cha afya.
Inaweza kuwa vigumu kuhisi mkao wa mtoto kwenye uterasi iwapo mama ana misuli yenye nguvu sana au iwapo ana mafuta mengi kwenye fumbatio lake. Iwapo itakuwa vigumu kuhisi nafasi ya mtoto mwambie mama avute pumzi nzito kisha aachilie polepole na alegeze mwili wake huku ukitomasa fumbatio lake.
Kisha hisi fumbatio la mama kupata umbo kubwa gumu (mgongo wa mtoto). Iwapo utalihisi (Mchoro 11.2a), mtoto ameangalia upande wa mgongo wa mama. Iwapo huwezi kuhisi mgongo wa mtoto, tafuta vibonge vingi vidogo (Mchoro 11.2b). Iwapo unahisi vibonge vingi vidogo badala ya umbo kubwa gumu, huenda unahisi mikono na miguu ya mtoto, inayokuonyesha kuwa mtoto ameangalia upande wa mbele wa mama.
Kufikia mwezi wa mwisho kabla ya kuzaliwa, watoto wengi huwa wamelala kichwa kikielekea kwenye seviksi ya uterasi (Mchoro 11.3a). Hali ya kichwa chini huitwa mlalo wa kutanguliza kichwa, na iwapo sehemu ya fuvu la kichwa iitwayo veteksi itatangulia kwenye njia ya uzazi, huu ndio mlalo bora zaidi kwa uzazi wa mtoto. Madaktari na wakunga huiita sehemu ya mtoto inayotangulia kwenye seviksi ya uterasikitangulizi. Katika Mchoro 11.3a, kitangulizi ni kichwa cha mtoto na katika Mchoro 11.3b, kitangulizi ni matako ya mtoto. Utajifunza kuhusu milalo mingine (uso, paji la uso, bega) katika Moduli kuhusu Utunzaji katika Leba na kuzaa.
Je, veteksi ni sehemu ipi ya fuvu la kichwa? (Kumbuka Kipindi cha 6. Unaweza kutaka kutazama tena Mchoro 6.5 unaoonyesha mifupa ya fuvu la kichwa cha fetasi).
Veteksi ndiyo sehemu ya fuvu la kichwa cha fetasi kati ya utosi wa mbele (nafasi kati ya mifupa kwenye sehemu ya mbele ya kichwa cha mtoto), na utosi wa nyuma (nafasi kati ya mifupa kwenye sehemu ya nyuma ya kichwa cha mtoto).
Mwisho wa jibu
Kufikia mwezi wa saba au wa nane, kichwa cha mtoto kimeteremka chini kwenye pelvisi ya mama. Hii ndiyo jinsi ya kuhisi kichwa cha mtoto:
Usipohisi chochote kwenye upande wa chini wa fumbatio la mama, huenda mtoto amelala kingamo.
Kumbuka Kipindi cha 10. Je, unapaswa kufanya nini ukishuku kuwa mwanamke ana pacha?
Mpe mama huyo rufaa aende katika kituo cha afya mara moja.
Mwisho wa jibu
Madaktari na wakunga huchukulia kucheza kwa fetasi kama ishara ya hali njema ya fetasi na pia inaweza kuashiria mlalo wa fetasi.
Huku ukihisi fumbatio la mama, jaribu kuwazia milalo tofauti ya mtoto kwenye uterasi. Wazia sehemu ambapo huenda mikono na miguu ya mtoto ipo. Wazia jinsi kila mlalo unavyoweza kumuathiri mama mtoto anapocheza. Kisha mwulize mama anakohisi mtoto akicheza kwa nguvu sana na anapohisi akicheza polepole. Je, hii ndiyo sehemu unayodhani miguu na mikono inaweza kuwa (tazama Mchoro 11.9)?
Mpe mwanamke rufaa aende katika kituo cha afya ikiwa hahisi mtoto akicheza ndani yake.
Mtoto akiwa na afya na anapata virutubishi vya kutosha kutoka kwa mama, yeye hucheza katika uterasi kwa njia ambayo mwanamke atamhisi. Kucheza kwa mtoto mara nyingi huhisika vizuri baada ya mama kula na baada ya kupumzika vizuri sana na amelala kwa upande.
Mwanamke akikuambia kuwa mtoto hasongi kama hapo awali, au hasongi kabisa, anaweza kuwa mgonjwa au amefariki.
Mpigo wa moyo wa mtoto hukufahamisha kuhusu mlalo wa mtoto ndani ya mama na kuhusu afya ya mtoto. Sikiza mpigo wa moyo katika kila safari yake ya utunzaji katika ujauzito kuanzia miezi mitano. Mara nyingi madaktari na wakunga hurejelea mpigo wa moyo.
Kufikia miezi miwili ya mwisho ya ujauzito, unaweza kusikia mpigo wa moyo wa fetasi mara nyingi ukiwa katika chumba kisicho na kelele kwa kuweka sikio lako kwenye fumbatio la mama (Mchoro 11.10a). Ni rahisi kusikia mpigo wa moyo kwa stethoskopu (Mchoro 11.10b) au fetoskopu (Mchoro 11.10c na d). Iwapo huna fetoskopu, unaweza kujitengenezea moja kutoka kwa mbao, mchanga au mwanzi.
Mpigo wa moyo wa fetasi ni tulivu na wa haraka. Unaweza kusikika kama mpigo mwepesi wa saa chini ya mto, ingawa kwa kasi. Mpigo wa moyo wa fetasi ni takriban mara mbili zaidi ukilinganishwa na wa moyo wa mtu mzima - kwa kawaida mipigo 120 hadi 160 kwa dakika. Hamna haja ya kuhesabu mipigo ya moyo hadi mwanamke atakapoanza leba. Kusikia mpigo dhahiri wa moyo wa fetasi wakati wa safari ya utunzaji katika ujauzito hudhibitisha kuwa mtoto yuko hai.
Ukisikia sauti ya mtindo fulani (shee-oo, shee-oo, shee-oo), huenda unasikia mpwito wa ateri wa mtoto kwenye kiungamwana. Sauti kwenye kiungamwana hukuonyesha jinsi moyo wa mtoto unavyopiga haraka, bali hazikusaidii kujua mkao wa mtoto kwenye uterasi.
Mpigo wa moyo ukiwa polepole, huenda unasikia mpwito wa ateri wa mama badala ya ule wa mtoto. Jaribu kusikiza kwenye sehemu tofauti kwa fumbatio lake.
Wazia upande ambao huenda mtoto amelalia. Kisha uanze kusikiza mpigo wa moyo karibu na sehemu unapofikiria moyo wa mtoto unapaswa kuwa. Unaweza kuhitaji kusikiza katika sehemu nyingi kwenye fumbatio la mama kabla ya kupata sehemu ambapo sauti ya mpigo wa moyo ni mkubwa na dhahiri (Mchoro 11.11).
Je, sauti ya mpigo wa moyo ni kubwa zaidi juu au chini ya kitovu cha mama? Ukisikia sauti kubwa zaidi ya mpigo wa moyo chini ya kitovu cha mama, huenda mtoto yuko katika hali ya kichwa chini (Mchoro 11.12a). Ukisikia sauti kubwa zaidi ya mpigo wa moyo juu ya kitovu cha mama, huenda mtoto yuko katika mlalo wa kutanguliza matako (Mchoro 11.12b).
Wakati mwingine, mtoto akiwa ameangalia upande wa mbele wa mama, ni vigumu kupata mpigo wa moyo kwa sababu mikono na miguu ya mtoto huzuia. Sikiza karibu na pande za mama, au moja kwa moja katikati mwa fumbatio lake ili kuusikia mpigo wa moyo wa fetasi.
Watoto waliotanguliza matako mara nyingi huzaliwa bila matatizo yoyote, hasa ikiwa mama amewahi kuzaa watoto wengine na alizaa kwa urahisi. Lakini watoto waliotanguliza matako wana uwezekano mkubwa wa kukwama, au kuwa na matatizo mengine hatari.
Iwapo mtoto ametanguliza matako kufikia juma la 36 (miezi 8), mpe mwanamke huyo rufaa aende katika kituo cha afya. Usijaribu kumgeuza mtoto aliyetanguliza matako (tazama Kisanduku 11.1).
Ni mkunga, afisa wa afya au daktari aliyefunzwa kugeuza mtoto aliyetanguliza matako anayepaswa kujaribu kufanya hivyo na inapaswa kufanyika hospitalini. Kujaribu kugeuza mtoto kwa kufinya uterasi ni hatari sana. Hata mkunga, afisa wa afya au daktari asijaribu kumgeuza mtoto ikiwa kiowevu cha amnioni cha mama hakijatoka, au ikiwa ametokwa na damu ukeni, amekuwa na shinikizo la juu la damu, upasuaji kwenye uterasi yake, au upasuaji wa kuzaa.
Iwapo mtoto hayuko katika hali ya kichwa chini leba inapoanza, ni salama zaidi kwa mama kuzalia hospitalini. Mkunga, afisa wa afya au daktari anaweza kutumia fosepu (vifaa vya kuvuta) mtoto akikwama. Au wanaweza kufanya upasuaji wa kuzaa.
Watoto waliolala kingamo hawawezi kutoshea kwenye pelvisi ya mama ili kuzaliwa (Mchoro 11.13). Ukijaribu kuzalisha mtoto bila upasuaji, uterasi ya mama itapasuka wakati wa leba, na yeye pamoja na mtoto watafariki bila huduma ya matibabu. Mtoto akigeuka na kutanguliza kichwa wakati wowote - hata siku ambapo leba ya mama itaanza - ni SAWA kwake kuzalia nyumbani au kwenye kituo cha afya.
Mtoto aliyelala kingamo lazima azaliwe kwa upasuaji wa kuzaa hospitalini. Usijaribu kumgeuza mtoto aliyelala kingamo kwa mkono. Hii ni hatari kama kujaribu kumgeuza mtoto aliyetanguliza matako, na inapaswa kufanywa tu na daktari hospitalini.
Kumbuka uliyojifunza katika Kipindi cha 10 kuhusu ujauzito wa pacha.
Je, dalili tatu za ujauzito wa pacha ni zipi?
Uterasi hukua haraka au kubwa kuliko kawaida. Unaweza kuhisi vichwa viwili au matako mawili unapohisi tumbo la mama. Unaweza kusikia mipigo miwili ya moyo (hii si rahisi, lakini inawezekana katika miezi michache ya mwisho).
Mwisho wa jibu
Je, njia mbili za kujaribu kusikia mipigo ya mioyo ya pacha ni zipi?
Tafuta mpigo wa moyo wa mtoto mmoja. Mwambie msaidizi kusikiza sehemu zingine ambapo mpigo wa moyo ni rahisi kusikia, na nyote mgonge mipigo ya mioyo. Tumia saa kukusaidia kuhesabu mipigo hiyo miwili ya moyo.
Mwisho wa jibu
Baada ya kumaliza kuchunguza fetasi na mama, na kufuata maagizo ya ishara zozote za hatari, chunguza iwapo mwanamke huyo ana maswali mengine, au anahitaji kuzungumzia kingine chochote. Iwapo ana ishara zozote za hatari, mweleze kwa makini kuhusu ishara hiyo ya hatari na atakachofanya kujitunza. Iwapo alikuwa amerudi kwa uchunguzi katika ujauzito, tathmini ulichomfanyia katika uchunguzi wa awali. Amua kingine chochote ambacho ungehitaji kumfanyia. Iwapo anahitaji rufaa ya kwenda katika kituo cha afya cha ngazi ya juu, hakikisha anajua kwa kwenda na wakati mwafaka wa kwenda.
Katika kipindi hiki, umejifunza jinsi ya kuchunguza fumbatio la mwanamke mjamzito ili uweze kutambua mkao wa mtoto kwenye uterasi, kitangulizi (kichwa au matako au ikiwa amelala kingamo), na jinsi ya kuchunguza hali njema ya fetasi kwa kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi na kumwuliza mama kuhusu kucheza kwa fetasi.
Katika Kipindi cha 11, umejifunza:
Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyotimiza malengo ya masomo haya kwa kujibu maswali haya. Andika majibu katika shajara yako ya masomo na ujadiliane na mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi wa Masomo yatakayofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.
Je, ni kauli ipi kati ya hizi isiyo sahihi? Eleza kisicho sahihi katika kila kauli.
A Sahihi. Kusikiza mpigo wa moyo wa fetasi kwa stethoskopu huitwa oskalitesheni.
B Sahihi. Kichwa cha fetasi kikiwa upande wa chini na matako ya fetasi hiyo yawe upande wa juu kwenye fandasi, huitwa mlalo wima.
C Si sahihi.Katika mlalo wa kutanguliza veteksi kitangulizi ni kichwa cha mtoto.
D Sahihi. Kiwango cha mpigo wa moyo wa fetasi huwa takriban mipigo 120 hadi 160 kwa dakika.
E Si sahihi. Katika mlalo wa kutanguliza matako, sauti ya mpigo wa moyo wa fetasi ni mkubwa zaidi juu ya kitovu cha mama.
Mwisho wa jibu
Soma kwa makini uchunguzi maalum ufuatao kisha ujibu maswali ya kujitathmini 11.2 hadi 11.4.
Bekelech alikuja kwa uchunguzi katika ujauzito akiwa na ujauzito wa miezi minane. Ulipotomasa fumbatio lake, ulipata umbo gumu la mviringo kwenye fandasi ya uterasi na umbo laini kubwa karibu na kinena simfisisi. Bekelech alikuambia kuwa kucheza kwa mtoto kulikuwa kumepungua katika juma lililopita na uliposikiza kwenye fumbatio lake kwa fetoskopu hukusikia mpigo wa moyo wa fetasi.
Mwisho wa jibu
Je, ni wapi utakaposikiza mpigo wa moyo wa fetasi kuthibitisha utambuzi wako wa jinsi mtoto wa Bekelech alivyojilaza, na kwa nini?
Utasikiza mpigo wa moyo wa fetasi juu ya kitovu cha Bekelech kwa sababu iwapo mtoto ametanguliza matako, sauti ya mpigo wa moyo wake itakuwa kubwa zaidi hapo. (Tazama tena Mchoro 11.12 ikiwa huna uhakika.)
Mwisho wa jibu
Je, unadhani mtoto wa Bekelech yuko katika hali gani, na ni hatua ipi unayopaswa kuchukua?
Huenda mtoto huyo ni mgojwa au hata amefariki, kwa sababu Bekelech anasema hachezi na huwezi kusikia mpigo wa moyo wa fetasi. Unapaswa kumpa rufaa aende katika kituo cha afya mara moja.
Mwisho wa jibu