Katika sehemu ya 1 ya Moduli Utunzaji katika Ujauzito, umejifunza kimsingi kuhusu muundo wa kimaumbile wa mfumo wa uzazi wa mwanadamu na jinsi unavyofanya kazi, awamu za kawaida za ujauzito na mabadiliko ya kuwezesha kubeba mimba, uchunguzi wa kijumla kuhusu jinsi mimba inavyoendelea na jinsi ya kutambua matatizo madogo. Katika sehemu ya 2 ya Moduli yaUtunzaji katika Ujauzito, utajifunza kuhusu kanuni za kimsingi za utunzaji maalum katika ujauzito.
Kipindi hiki kitaanza kwa kueleza dhana na kanuni za utunzaji maalum katika ujauzito na tofauti za kimsingi baina ya huduma hii na mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito. Kipindi hiki kitaangazia vipindi vingine katika sehemu ya 2 ambavyo vyote huwa katika Utunzaji Maalum katika Ujauzito. Pia utajifunza malengo ya kila mojawapo ya ziara nne za utunzaji maalum katika ujauzito. Kipindi hiki kitahitimisha kwa hatua ambazo wewe binafsi na mama mjamzito mnapaswa kutekeleza katika kuzaa; mashauri kuhusu jambo la kufanya iwapo matatizo yataibuka na maelekezo ya jinsi ya kuandika arifa ya rufaa ikiwa mama anapaswa kuhamishwa hadi katika kituo cha afya.
Baada ya kuhitimisha kipindi hiki, unatarajiwa:
13.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 13.1)
13.2 Kujadili kanuni za utunzaji maalumkatika ujauzito na kutaja jinsi unavyotofautiana na mtazamo wa kitamaduni. (Swali la Kujitathmini 13.1)
13.3 Kueleza ratiba, malengo na taratibu zinazofuatwa katika kila mojawapo ya ziara nne za utunzaji maalum katika ujauzito, za wanawake katika kipengele cha kimsingi. (Maswali ya Kujitathmini 13.2 na 13.3)
13.4 Kuwashauri wanawake wajawazito kuhusu maandalizi ya kuzaa pamoja na vifaa watakavyohitaji. (Swali la Kujitathmini 13.4)
13.5 Kutoa muhtasari wa vipengele muhimu vya kujitayarishia matatizo na kupangia matukio ya dharura, ikijumuisha kuwashauri watoaji damu na kuandika arifa ya rufaa. (Swali la Kujitathmini 13.3)
Kihistoria, kielelezo cha kitamaduni cha utunzaji katika ujauzito kilianzishwa miaka ya kwanza ya 1900. Kielelezo hiki huchukulia kuwa ziara za kila mara na kuwaainisha wanawake wajawazito katika viwango vya hatari ya chini na hatari ya juu kwa kutabiri matatizo kabla ya wakati, ndiyo njia mwafaka ya kumtunza mama na fetasi. Utunzaji maalum katika ujauzito ulichukua nafasi ya mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito - huu ni mtazamo wa kimalengo uliopendekezwa na watafiti mnamo mwaka wa 2001 na kuanza kutumiwa na Shirika la Afya Duniani mnamo mwaka wa 2002.
Kusudi la utunzaji maalum katika ujauzito ni kukuza afya ya kina mama na watoto wao kupitia ukaguzi uliolengwa kwa wanawake wajawazito ili kusaidia:
Pia, utunzaji maalum katika ujauzito hukusudia kumpa kila mwanamke utunzaji wa kibinafsi ili kudumisha hali ya kawaida ya kuendelea kwa ujauzito kupitia uelekezi na ushauri wa wakati unaofaa kuhusu:
Katika utunzaji maalum katika ujauzito, wahudumu wa afya husisitiza makadirio ya kibinafsi na hatua zinazohitajika ili mhudumu na mama mjamzito waweze kufanya uamuzi kuhusu utunzaji katika ujauzito. Hivyo basi, badala ya kufanya ziara za kila mara za kitamaduni za utunzaji katika ujauzito kuwa desturi kwa wote, na kuwaainisha wanawake kwa kuzingatia kiashiria hatari cha kidesturi, wahudumu wa utunzaji maalum katika ujauzito huongozwa na hali ya kibinafsi ya mwanamke.
Mtazamo huu pia hufanya utunzaji katika ujauzito kuwa jukumu la familia. Mhudumu wa afya hujadili na mwanamke na mumewe kuhusu matatizo ambayo mama anaweza kukumbana nayo; pamoja wanapanga kujitayarishia kuzaa na kujadili utunzaji wa baada ya kuzaa pamoja na maswala ya uzazi wa baadaye. Wanawake wajawazito hupata utunzaji wa asili wakiwa nyumbani na katika kituo cha afya; familia pamoja na wahudumu wa afya hutambua matatizo mapema; na hatua za kuingilia kati huanzishwa kwa wakati unaofaa hivyo kuwa na matokeo bora zaidi kwa akina mama na watoto wao.
Kisanduku 13.1 kinatoa muhtasari wa kanuni za kimsingi za utunzaji maalum katika ujauzito.
Utunzaji maalum katika ujauzito umepata umaarufu kwa sababu ya manufaa yake katika kupunguza vifo vya kina mama na uwezo wa kufa na maradhi(ugonjwa, matatizo au ulemavu) ya kipindi kinachokaribiana na kuzaliwa. Uwezo wa kufa katika kipindi kinachokaribiana na kuzaliwa ni idadi ya jumla ya uzazimfu (watoto wanaozaliwa wafu baada ya wiki 28 za ujauzito) ikijumlishwa na idadi ya jumla ya watoto wachanga (watoto wazawa) ambao hufariki katika siku 7 za kwanza za maisha. Kima cha vifo katika kipindi kinachokaribiana na kuzaliwa ni idadi ya watoto wanaozaliwa wafu na vifo vya watoto wachanga vinavyotokea kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai, na ni kipimo kilichotambulika ulimwenguni kote cha kiwango cha utunzaji katika ujauzito.
Ufasili wa uwiano wa kiwango cha vifo vya kina mama ni upi? (Ulijifunza haya katika Kipindi cha 1 cha Moduli hii.)
Uwiano wa kiwango cha vifo vya kina mama ni idadi ya jumla ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya ujauzito au kuzaa, kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai.
Mwisho wa jibu
Utunzaji katika maalum ujauzito ni mtazamo mwafaka kwa nchi zisizo na raslimali za kutosha ambapo wataalamu wa afya ni wachache na miundo msingi ya afya ni duni. Hususani, wanawake wengi wajawazito hawawezi kukimu gharama ya ziara za kila mara kama inavyohitajika katika mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito. Katika mtazamo wa kimipango na kifedha, mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito hauwezi kutekelezwa katika wanawake wengi wajawazito na ni mzigo kwa mfumo wa afya. Kwa hivyo, mataifa mengi yanayoendelea yanachukua mtazamo wa utunzaji maalum katika ujauzito.
Utafiti (kwa mfano, tazama Kisanduku13.2) umeonyesha kuwa ziara za kila mara za kipindi cha ujauzito kama ilivyo katika mtazamo wa kitamaduni haziboreshi matokeo ya ujauzito. Hususan, wanawake wajawazito unaoitajika kuwa na 'hatari ya chini' au 'wasio na hatari' katika mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito huenda wasipate ushauri kuhusu dalili za hatari. Hivyo, mara nyingi wanawake hawa hawatambui dalili za hatari hivyo hawawaarifu wataalamu wa afya haraka iwezekanavyo.
Kwa kuchukua kutokea kwa leba iliyokwama kama mojawapo ya kiashiria, utafiti wa mwaka wa 1984 nchini Zaire katika wanawake 3,614 wajawazito ulionyesha kuwa asilimia 71 ya wanawake walio na leba iliyokwama walikuwa wameainishwa kama 'wasio na hatari' hapo awali, wakati asilimia 90 ya wanawake waliogunduliwa kuwa 'katika hatari' hawakupata leba iliyokwama. Hii ni asili moja ya ushahidi kuonyesha kuwa matatizo mengi ya ujauzito hayawezi kutabirika na hutokea katika awamu za mwisho.
Mifano mingine ya matatizo ya ujauzito yasiyoweza kutabirika ambayo hutokea katika awamu za mwisho zaidi za ujauzito hujumuisha visababishi vitatu vikuu vya vifo vingi vya kina mama:
Mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito umeshindwa kutambua kwa hakika wanawake walio ’katika hatari' ya kupata hali hizi zinazotishia maisha. Mtazamo huu hutambua baadhi ya wanawake kama walio na 'hatari ya chini' ambao baadaye hupata dalili za hatari zinazohitaji wataalamu kuingilia kati kwa dharura.
Jedwali 13.1 kinatoa muhtasari wa tofauti za kimsingi baina ya mtazamo wa kitamaduni wa utunzaji katika ujauzito na utunzaji maalum
Matumizi ya dawa za kulevya hujumuisha tumbaku, vileo, miraa, dawa zilizopigwa marufuku, bangi, kokeini na dawa nyinginezo
Sifa | Utunzaji wa kitamaduni katika ujauzito | Utunzaji maalum katika ujauzito |
---|---|---|
Idadi ya ziara | 16 - 18 bila kuzingatia hali ya hatari | 4 kwa wanawake walioainishwa katika kipengele cha kimsingi (kama ilivyoelezwa baadaye katika kipindi hiki) |
Mtazamo | Wima: maswala ya ujauzito pekee ndiyo yanayoshugulikiwa na wahudumu wa afya. | Huunganishwa na kuzuia kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi mtoto, ushauri kuhusu dalili za hatari, hatari za kutumia dawa za kulevya, kupima VVU, kuzuia malaria, lishe, chanjo na kadhalika. |
Dhana | Ziara za mara nyingi zaidi za wanawake wajawazito na kuwaainisha katika vikundi vya hatari ya juu/chini husaidia kutambua matatizo. Huchukulia kuwa ziara zinapokuwa nyingi, matokeo huwa bora zaidi. | Huchukulia kuwa ujauzito wowote unaweza kuwa 'na hatari'. Ziara mahususi na za kibinafsi husaidia kutambua matatizo |
Matumizi ya viashiria vya hatari | Hutegemea viashiria hatari vya kidesturi kama vile urefu wa mama <150cm, uzito wa <50kg, edema ya miguu, hali mbaya ya fetasi kabla ya wiki 36, na kadhalika | Haitegemei viashiria hatari vya desturi. Huchukulia kuwa hatari kwa mama na fetasi inaweza kutambulika muda unavyopita |
Hutayarisha familia | Kuwategemea wahudumu wa afya pekee | Kugawa majukumu ya kujitayarishia matatizo na maandalizi ya uzazi |
Mawasiliano | Mawasiliano ya upande mmoja(elimu ya afya) kwa wanawake wajawazito pekee | Mawasiliano ya pande mbili (ushauri) kwa wanawake wajawazito na waume zao |
Gharama na wakati | Mtazamo huu huwagharimu na kufanya wanawake wajawazito pamoja na wahudumu wa afya kutumia wakati mwingi kwani hauteui maswala | Huwa na gharama ya chini na huokoa wakati. Wanawake wachache huhitaji ziara za kila mara au rufaa kwani mimba nyingi huendelea bila matatizo |
Athari | Hutoa fursa ya upuuzi wa wahudumu wa afya na familia ya wale wasio ‘hatarini’ na kufanya familia kutojua na kusita punde matatizo yanapotokea | Hutahadharisha wahudumu wa afya na familia kuhusu matatizo yanayoweza kutokea wakati wowote wa ujauzito |
Utunzaji maalum katika ujauzito una awamu tatu zifuatazo:
Kisanduku 13.3 kinatoa muhtasari wa hatua za utaratibu huu.
Katika utoaji huduma ya utunzaji maalum katika ujauzito vipengele muhimu vitakavyozingatiwa ni:
Kielelezo cha utunzaji maalum katika ujauzito huwaainisha wanawake wajawazito katika vikundi viwili: wanaostahiki kupata utunzaji wa kidesturi katika ujauzito (kikundi kinachoitwa kipengele chakimsingi), na wanaohitaji utunzaji maalum kulingana na hali yao hasa ya afya au vipengele vya hatari (kipengele maalum). Vigezo vilivyowekwa awali (kama inavyoelezwa hapa chini) hutumika kuamua kuhusu wanawake wanaostahiki kuingia katika kipengele cha kimsingi. Wanawake waliochaguliwa kuwa katika kipengele cha kimsingi huchukuliwa kama wasiohitaji ukaguzi zaidi au utunzaji maalum wakati wa ziara ya kwanza, bila kuzingatia umri wa ujauzito ambao mama alianza ratiba ya utunzaji katika ujauzito.
Wanawake huulizwa maswali na kuchunguzwa katika ziara ya kwanza ili kufahamu iwapo wana vipengele vyovyote vifuatavyo vya hatari:
'NDIO' kwa MOJAWAPO ya maswali yaliyoko hapo juu humaanisha kuwa mwanamke huyo hastahiki kuwa katika kipengele cha kimsingi ya utunzaji katika ujauzito. Mwanamke huyu ataainishwa katika kipengele maalum na anahitaji kuangaliwa kwa makini zaidi na kupewa rufaa kwa utunzaji wa kitaalamu.
Utawapa rufaa wanawake walio katika kipengele maalum ili wafuatiliwe kwa makini zaidi katika kituo cha afya cha kiwango cha juu zaidi na kupewa utunzaji maalum utakaoamuliwa na wataalamu katika nyenzo hizo, hali ukiendelea kufuata hatua zilizoko katika kipengele cha kimsingi.
Kielelezo 13.1 ni mwongozo wa habari unayopaswa kukusanya katika kila mojawapo ya ziara nne za utunzaji katika ujauzito. Mwanzoni mwa kila ziara, mwulize mama ikiwa amepata dalili zozote za hatari tangu kuchunguzwa. Mkumbushe kuja kukuona ikiwa ataanza kuvuja damu ukeni, kuwa na kiwaa, maumivu ya tumbo, homa au dalili yoyote ile ya hatari. Utajifunza jinsi ya kumshauri kuhusu dalili za hatari katika Kipindi cha 15.
Wakati mwingine, mwanamke mjamzito huja kuchunguzwa kwa mara ya kwanza ya utunzaji katika ujauzito wakati ujauzito tayari umeendelea. Hata hivyo, unapaswa kujumuisha hatua zote za ratiba ya utunzaji wa kimsingi na hatuazote za ziara ya kwanza hata kama mama yuko katika trimesta ya pili au ya tatu ya ujauzito.
Ziara ya kwanza ya utunzaji maalum katika ujauzito inapaswa kutendeka kabla ya wiki 16 za ujauzito. Unapaswa kutimiza malengo yafuatayo:
Inamaanisha nini ikiwa kuna tofauti ya wiki kadhaa baina ya umri wa ujauzito uliokadiriwa kwa kutumia kipimo cha urefu wa fandasi na kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida?
Kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 10, hii inaweza kumaanisha kuwa mwanamke hajakumbuka vyema tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida, lakini inaweza pia kumaanisha kuwa fetasi haikui kwa njia ya kawaida (urefu wa fandasi ukiwa chini ya kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida) au pia inawezekana kuna kiowevu cha amniotiki kingi zaidi kinachoizingira fetasi, au kuna ujauzito wa pacha au mtoto mkubwa zaidi (urefu wa fandasi ni zaidi ya kadirio la kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida.)
Mwisho wa jibu
Ratibu ziara ya pili ya utunzaji maalum katika ujauzito kati ya wiki ya 24-28 ya ujauzito. Fuata taratibu zilizoelezwa katika ziara ya kwanza. Aidha:
Ziara ya tatu ya utunzaji maalum katika ujauzito inapaswa kutendeka karibu na kipindi cha wiki ya 30- 32 ya ujauzito. Malengo ya ziara hii ya tatu ni sawa na yale ya ziara ya pili. Aidha: unapaswa:
Kumbuka kuwa wanawake wengine huenda wakapata leba kabla ya ziara inayofuata. Washauri wanawake wote kukuita mara moja au kuja kwako punde tu wanapoanza leba. Usingoje!
Unapaswa pia kusisitiza umuhimu wa ziara ya kwanza baada ya kuzaa ili kuhakikisha umemhudumia akiwa nyumbani kwake au kituoni cha afya baada ya kuzaa. Kipindi kilicho muhimu zaidi baada ya kuzaa ni saa 4 za kwanza; matukio mengi ya kuvuja damu baada ya kuzaa hutokea wakati huu. (Utajifunza kuhusu kuvuja damu baada ya kuzaa katika Moduli ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa.)
Ziara ya nne ya utunzaji maalum katika ujauzito inapaswa kuwa ya mwisho kwa wanawake walio katika kipengele cha kimsingi na hupaswa kufanyika kati ya wiki ya 36- 40 ya ujauzito. Unapaswa kuzingatia hatua zote zilizoelezwa katika ziara ya tatu. Aidha:
Kutanguliza matako, na mkao wa kukingama humaanisha nini? (Ulijifunza haya katika Kipindi cha 11.)
Kutanguliza matako ni hali ambapo kichwa cha mtoto kinaelekea juu katika uterasi, huku matako, miguu au nyayo zikielekea chini kwenye seviksi ya mama wakati ujauzito unapokaribia mwisho. Mkao wa kukingama ni hali ambayo mtoto amejilaza kutoka upande mmoja hadi mwingine katika fumbatio.
Mwisho wa jibu
Mtoto aliyetanguliza matako huenda azaliwe kupitia uke katika kituo cha afya. Mtaalamu wa kiukunga anaweza kumrekebisha mtoto aliyejilaza kwa kukingama hadi arejelee hali ya kawaida ya kutanguliza kichwa au veteksi, au ni sharti azaliwe kwa upasuaji.
Ratiba ya kibinafsi ya kuzaa ni mwongozo wa wahudumu wa afya inayoanzishwa kwa kujadiliana na mwanawake binafsi na mwenzi wake au wasaidizi wakuu. Mwongozo huu huonyesha jinsi wangependa kuzaa. Baadhi ya wachumba huchagua kuzalia nyumbani chini ya utunzaji wako kwa sababu wao huchukulia kuzaa kama jambo la kawaida maishani. Wengine huchagua kuzalia hospitalini au katika kituo cha afya. Ratiba ya kuzaa ya wanawake walio na VVU inapaswa kuwa kuzalisha katika kituo cha afya kama ilivyo katika Mwelekezo wa Kitaifa wa kuzuia kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi mtoto (kama ilivyoelezwa katika Kipindi cha 16).
Kujitayarishia kuzaa ni utaratibu wa kupangia mwanamke kuzaa kwa njia ya kawaida. Kujiandalia matatizo ni kutazamia hatua zinazohitajika ikiwa jambo la dharura litatokea. Kupangia matukio ya dharura ni utaratibu wa kutambua na kukubaliana kuhusu hatua zote zinazohitaji kuchukuliwa upesi dharura ikitokea, na maelezo yake kueleweka na kila mmoja anayehusika, na mipango inayohitajika kufanywa. Kwanza tutazingatia kujitayarishia mwanamke kuzaa kwa njia ya kawaida.
Muelimishe mama na familia yake kubaini ishara za kawaida za leba. Mwanamke anaweza kuzaa siku kadhaa au hata wiki nyingi kabla au baada ya tarehe iliyotarajiwa, kulingana na tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida. Mwanamke anapofahamu maana ya leba, ataweza kufahamu kitakachotokea. Ufahamu huu kisha humsaidia kutulia zaidi na kuwa na ujasiri katika siku au wiki za mwisho za ujauzito.
Toa maagizo dhahiri ya jambo la kufanya leba inapoanza (kwa mfano ikiwa atakuwa na maumivu ya mkakamao wa misuli ya fumbatio au kuvuja kwa kiowevu cha amniotiki). Hakikisha kuwa kuna mtu atakayekuita wewe au mtaalamu mwingine ili kuzalisha haraka iwezekanavyo. Ambatanisha ushauri wako wa kiusemi kwa maagizo yaliyoandikwa kwa lugha asili ya mteja.
Maandalizi ya kuzaa pia yanafaa kuzingatia:
Vifaa vya kuzalishia ambavyo mwanamke mjamzito na familia yake wanapaswa kushauriwa watayarishe kabla ya kuzaa ni (tazama Mchoro 13.2):
Kama ilivyodokezwa hapo awali, kujiandalia matatizo ni utaratibu wa kutazamia hatua zinazohitajika ikiwa jambo la dharura litatokea, na pia kufanya mpango wa dharura (Kisanduku 13.5). Matatizo yanayohusiana na ujauzito kama vile shinikizo la juu la damu na kuvuja damu yanaweza kutokea wakati wowote katika ziara za utunzaji katika ujauzito, na ugonjwa wowote unaweza kutokea wakati wa ujauzito. Hali hizi zinapokisiwa katika awamu yoyote ya ujauzito, unapaswa kumpa mwanamke huyo rufaa mara moja na urudie kumshauri aje kukuona au kutafuta huduma ya kitabibu haraka iwapo dalili za hatari zitaonekana.
Hakikisha kuwa mwanamke na mumewe pamoja na watu wengine katika familia wanajua mahali pa kutafuta usaidizi.
Sehemu muhimu ya kupangia matukio ya dharura ni kutazamia matukio yanayoweza kusababisha kukawia kunakoweza kuepukwa kwa mipango bora.
Kuna aina tatu ya kuchelewesha usaidizi. Zote zinaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto wake:
Kuchelewa huku husababishwa na vipengele kadhaa, vikiwemo vikwazo vya kimipango na kifedha, na ukosefu wa maarifa kuhusu maswala ya kiafya ya kina mama na watoto wazawa. Kwa mfano, mama, familia yake na hata majirani wanaweza kuhisi kuwa ni mume tu au mtu mwingine wa familia aliyeheshimiwa anayeweza kumpa ruhusa mama akuite au apate huduma ya matibabu ya haraka katika kituo cha afya. Lakini kukawia huku kunaweza kuhatarisha maisha yake na ya mtoto.
Kuchelewa kuamua kutafuta huduma kunaweza kusababishwa na kushindwa kutambua dalili za matatizo, maswala kuhusu gharama, matukio mabaya ya awali kuhusu mfumo wa huduma ya afya na matatizo ya kiusafiri. Kuchelewa kufikia huduma kunaweza kusababishwa na umbali wa nyumba ya mwanamke mjamzito hadi kwenye kituo cha afya au mhudumu wa afya, hali ya barabara au ukosefu wa usafiri wa dharura.
Kuchelewa kupata huduma mwafaka kunaweza kupelekea upungufu wa vifaa vya kimsingi, ukosefu wa wataalamu wa afya na ujuzi duni wa wahudumu wa afya. Visababishi vya kukawia huku hutokea mara nyingi na vinaweza kutabirika. Hata hivyo, wanawake wajawazito, familia na jamii, wahudumu na vituo vya afya vilivyo karibu ni sharti wajitayarishe mapema kuchukua hatua za haraka iwapo dharura itatokea.
Hatimaye, unapaswa kufahamu hatua ya kuchukua unapofanya rufaa - kumhamisha mgonjwa ili apate huduma zaidi ya kiafya na utunzaji maalum katika kituo cha afya cha kiwango cha juu zaidi. Unapaswa kujaza fomu ya rufaa kikamilifu na utie sahihi na tarehe, kisha uhakikishe inaambatana na mteja kwenye kituo cha afya ulichomhamishia; fomu hii pia ina nafasi ya majibu kutoka kituoni kuhusu matibabu waliyompa mgonjwa.
Ikiwa hauna fomu sanifu ya rufaa, unapaswa kuandika arifa iliyo na taarifa muhimu (Kisanduku 13.6).
Hii ndiyo tamati ya mjadala wetu kuhusu utunzaji maalum katika ujauzito. Katika vipindi vinavyofuata katika Moduli hii, utajifunza zaidi kuhusu vipengele maalum vya utunzaji katika ujauzito katika maandhari mahususi, pamoja na maswala ya uhamasisho wa kiafya katika ujauzito, kumshauri mwanamke mjamzito kuhusu dalili za hatari, kuzuia kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi mtoto, utambuzi na udhibiti wa malaria, anemia na maambukizo ya mfumo wa mkojo, shinikizo la juu la damu, huaribikaji wa mimba na kuvuja damu katika awamu za kwanza na za mwisho za ujauzito. Moduli ya Utunzaji katika ujauzito inamalizia kwa kueleza jinsi ya kuingiza kanula na neli ndani ya mishipa ya vena ili kutia viowevu moja kwa moja katika mkondo wa damu na jinsi ya kuingiza katheta ya mkojo ili kumsaidia mama mjamzito kukojoa. Vipindi vya mafunzo ya kiutendaji vitahakikisha kuwa umepata maarifa haya.
Katika Kipindi cha 13 umejifunza kwamba:
Kwa kuwa sasa umekamilisha kikao hiki, jibu maswali yafuatayo ili kubaini jinsi ulivyotimiza Malengo ya Masomo ya kipindi hiki. Andika majibu yako katika shajara yako ya masomo na uyajadili na mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi wa Somo unaofuata. Unaweza kudhibitisha majibu yako ukilinganisha na vidokezo ulivyoandika katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.
Ni elezo lipi ambalo si kweli?? Katika kila kauli, eleza lisilo la kweli.
A si kweli. Utunzaji maalum katika ujauzito hauwalengi wanawake wajawazito pekee (hili lilitendeka katika mtazamo wa kitamaduni). Utunzaji maalum katika ujauzito hujumuisha mwenzi wa mwanamke na hata familia yote kumtunza mama wakati wa ujauzito, kuchunguza dalili za hatari na kujiandalia kuzaa, kujitayarishia matatizo na kupandia matukio dharura.
B ni kweli. Wanawake katika sehemu ya kimsingi huwa na ziara 4 tu katika utunzaji maalum katika ujauzito, isipokuwa ishara au dalili za tahadhari zinapogunduliwa katika awamu yoyote.
C sikweli. Mwanamke mjamzito anapaswa kujitayarishia leba na kuzaa kwa kukusanya nguo safi kabisa, wembe mpya, uzi mpya ulio safi, sabuni na burashi ya kusugua, maji safi ya kuosha na kunywa, ndoo na bakuli, vifaa vya kutengenezea vinywaji na tochi.
D si kweli. Ratiba ya kuzaa katika utunzaji maalum katika ujauzito huwa ya kibinafsi kwa kila mwanamke na mwenziwe na huheshimu matakwa na hiari ya mama. Ratiba hii hujadiliwa katika ziara ya tatu na kurudiwa inapohitajika katika ziara ya nne.
E ni kweli. Proflaksisi katika utunzaji maalum katika ujauzito hulenga kukinga magonjwa ya zinaa pamoja na kusambazwa kwa VVU kutoka kwa mama hadi mtoto, malaria, upungufu wa kilishe, anemia, maambukizi katika mfumo wa mkojo na pepopunda.
Mwisho wa jibu
Tuseme kwa mfano kwamba mwanamke mjamzito aliye na umri wa miaka 27 anayeitwa Aster amekuja kukuona. Yeye anakueleza kuwa ana mimba ya kwanza na alipata hedhi ya mwisho wiki 25 zilizopita. Ni hatua gani utakazochukua katika ziara hii ya kwanza? Kwa kawaida, ziara ya pili ya Aster itakuwa lini?
Kwa vile Aster ana mimba ya wiki 25, unapaswa kufanya huduma zote za ziara ya kwanza na ya pili za utunzaji maalum katika ujauzito. Makinika katika kuchunguza historia yake ya kimatibabu na kiukunga na ufanye uchunguzi kamili wa mwili ikiwa ni pamoja na shinikizo la damu, mpigo wa moyo, halijoto, pumzi, uchunguzi wa tumbo ili kupima urefu wa fandasi, sikiliza mpigo wa moyo wa fetasi, tazama kutanguliza na mkao wa fetasi na ukague matokeo ya vipimo vya mkojo. Kusudi la hatua hizi ni kutambua iwapo Aster anafaa kufuata sehemu ya kimsingi ya utunzaji. Pia mshauri kuhusu lishe, usafi na mapumziko.
Iwapo ana afya njema na mimba inaendelea kwa hali ya kawaida, mweleze kuwa ziara itakayofuata ni kati ya wiki ya 30- 32 ya ujauzito, lakini ni sharti atafute usaidizi mara moja iwapo atapata dalili zozote za hatari, kama vile kuvuja damu, mchozo unaonuka kutoka ukeni, homa, kiwaa au kisulisuli na kuchanganyikiwa.
Mwisho wa jibu
Tuseme Aster amekuja kwako akiwa na mimba ya wiki 32. Unatambua kuwa shinikizo lake la damu ni mmHg 120/60, ana konjaktiva iliyokwajuka kidogo na urefu wa fandasi ni wa kipimo cha fandasi ya wiki ya 38. Ishara hizi zinaonyesha nini na ni hatua zipi utakazochukua?
Konjaktiva iliyokwajuka inaonyesha kuwa huenda Aster ana anemia, hivyo mwulize kuhusu lishe yake- anakula nini na ni kiwango kipi cha chakula anachopata kila siku? Chukua vipimo vingi vya mkojo kwa kutumia kijiti cha kupimia ili kujua iwapo mkojo una sukari zaidi au protini. Ikiwa kipimo cha mkojo ni cha kawaida, mshauri kuboresha lishe na umpe tembe za foleti na ayoni.
Kwa vile fandasi ina urefu uliopita matarajio ya kawaida katika wiki ya 32 ya ujauzito, inaweza kuashiria kuwepo kwa pacha au hali ya kipatholojia na Aster anapaswa kupewa rufaa ili achunguzwe katika kiwango cha juu zaidi. Hivyo basi, unapaswa kuandika arifa ya rufaa na umshauri kuenda katika kituo cha afya au hospitali iliyo karibu. Aster anaweza kuhitaji usaidizi katika kupangia usafiri au fedha za kusafiri. Mshauri Aster kuhusu kujiandalia kuzaa, kujitayarshia matatizo na kupangia matukio ya dharura.
Mwisho wa jibu