Skip to main content
Printable page generated Thursday, 25 April 2024, 9:50 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 25 April 2024, 9:50 AM

14. Masuala ya Uendelezaji wa Afya Katika Ujauzito

Kipindi cha 14 Masuala ya Uendelezaji wa Afya Katika Ujauzito

Utangulizi

Uendelezaji wa afya ni shughuli yoyote inayolenga kutimiza afya bora katika jamii au nchi. Huhusisha elimu ya kiafya kwa watu binafsi ili kuwawezesha kudhibiti na kubadilisha mitindo yao ya kimaisha ili kuboresha afya yao. Hili ndilo lengo kuu la Kipindi hiki katika muktadha wa jukumu lako kama mwalimu wa afya wa wanawake wajawazito katika safari za utunzaji katika ujauzito. Lakini jinsi unavyojua kutoka katika Kipindi cha 2 cha Moduli hii, shughuli za uendelezaji wa afya huenda zaidi ya kulenga mienendo ya mtu binafsi na huhusisha tatuzi anuwai za kijamii na kimazingira zinazoboresha afya na hali njema kwa jamii na vile vile watu binafsi. Uendelezaji wa afya pia huhusisha uzuiaji wa magonjwa - Vitendo vinavyotekelezwa ili kuzuia magonjwa kuendelea, na uchunguzi wa kiafya - utaratibu wa kupima watu binafsi ili kujua ikiwa wamo katika hatari ya kukumbwa na tatizo la kiafya. Uhusiano kati ya uendelezaji afya, elimu ya kiafya, uzuiaji wa magonjwa na uchunguzi wa kiafya umeelezwa katika Picha 2.1 katika Kipindi cha 2.

Utunzaji katika ujauzito (Utunzaji kamili katika ujauzito, Kipindi cha 13) unatoa kiingilio kikuu kwa huduma anuwai za uendelezaji wa afya na uzuiaji wa magonjwa. Ni muhimu kwa wanaotoa utunzaji wa kiafya na wanawake kuongea kuhusu masuala muhimu yanayoathiri afya ya mwanamke na ujauzito wake.

Katika kipindi cha ujauzito, unaweza kuendeleza afya ya wanawake walio chini ya utunzaji wako na afya ya watoto wao kabla na baada ya kuzaliwa kwa kuwaelimisha kina mama kuhusu manufaa ya lishe bora, kupumzika vya kutosha, usafi, upangaji uzazi na unyonyeshaji wa mtoto pasipo kumpa chakula kingine chochote, chanjo na juhudi zingine za uzuiaji wa magonjwa. Lengo lako ni kukuza ufahamu za wanawake kwa masuala haya ili waweze kufanya uamuzi bora unaoathiri matokeo ya ujauzito wao - lakini kamwe usisahau wala kupuuza ugumu utakaowakabili wanawake wengine katika harakati za kuboresha mitindo yao ya kimaisha.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 14

Baada ya kujifunza somo hili unapaswa uweze:

14.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote maalumu yaliyochapishwa kwa herufi nzito (Maswali ya kujitathmini 14.2 na 14.4)

14.2 Kueleza sehemu kuu za mlo kwa afya bora kwa mwanamke mjamzito, kuwashauri wanawake kula vizuri hata wakiwa na fedha chache na ueleze matatizo yatokanayo na lishe duni. (Maswali ya kujitathmini 14.1 na 14.2)

14.3 Kueleza faida za usafi bora na shughuli zingine za kujitunza katika ujauzito (Swali la kujitathmini 14.3)

14.4 Kueleza faida za chanjo dhidi ya tetanasi. (Swali la kujitathmini 14.3)

14.5 Kueleza faida za kuanza unyonyeshaji mapema na pasipo kumpa mtoto chakula kingine chochote kwa mama na kwa mtoto wake. (Maswali ya kujitathmini 14.3 na 14.4)

14.6 Kueleza faida za upangaji uzazi ili kutimiza uzazi wa majira na kujadili uzuiaji wa ujauzito baada ya kuzaa na wanawake wajawazito. (Swali la kujitathmini 14.4)

14.1 Lishe katika ujauzito

Katika sehemu hii (iliyo kubwa zaidi katika Kipindi hiki), tutaeleza mahitaji ya kilishe katika ujauzito kwa kina na kueleza jinsi unavyoweza kuwashauri wanawake kuhusu kula vizuri hata wakiwa na pesa kidogo za chakula cha zaidi.

14.1.1 Kula vizuri

Kula vizuri humaanisha kula vyakula bora vya aina tofauti na pia kula chakula chakutosha. Mchanganyiko huu husaidia mwanamke mjamzito na mtoto wake kuwa wenye afya na nguvu kwa sababu:

  • Humsaidia mwanamke kukingana na maradhi katika ujauzito wake na baada ya kuzaa
  • Hudumisha meno na mifupa ya mwanamke
  • Humpa mwanamke nguvu za kufanya kazi
  • Humsaidia mtoto kukua vizuri kwenye uterasi ya mama
  • Humsaidia mama kurudisha nguvu zake haraka baada ya kuzaa
  • Husaidia katika utengenezaji wa maziwa mengi bora ya mama ili kustawisha mtoto.

Kula vyakula vya aina tofauti

Ni muhimu kwa wanawake wajawazito (kama kila yeyote yule) kula vyakula vya aina tofauti (tazama Picha 14.1): vyakula vikuu (kabohidrati), vyakula vya kukuza au vijenzi (protini), vyakula vilinzi (vitamin na madini), na vyakula vitoavyo nguvu (mafuta na sukari), pamoja na viowevu kwa wingi. Tutaelezea kila mojawapo ya makundi haya kwa kina baadaye katika Kipindi hiki.

Mchoro 14.1 Kula vizuri ni kula vyakula vya aina tofauti ili kupata virutubishi vyote vinavyofaa hasa katika ujauzito na unyonyeshaji na kula chakula cha kutosha kwa afya bora

Kula chakula zaidi

Wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha huhitaji kula zaidi ya kawaida. Chakula cha ziada huwapa nguvu za kutosha na kusaidia watoto wao kukua. Wanahitaji kuongeza chakula wanachokula kikawaida kwa angalau kalori 200 kwa siku au hata zaidi iwapo walikuwa na uzani wa chini kabla ya kupata ujauzito. Kuna njia nyingi za kuongeza chakula cha kila siku kwa kiwango hiki: kwa mfano, kipimo kimoja zaidi cha uji wa mahindi na karanga 12 kwa siku kinaweza kutimiza hitaji hili la ziada.

Wanawake wengine wajawazito huhisi kichefuchefu na kwa hivyo wasipende kula. Hata hivyo, wanawake wajawazito wanahitaji kula chakula cha kutosha - hata wakiwa wagonjwa. Vyakula vya kawaida kama injera au mchele vinaweza kuwa rahisi kwa wanawake hawa kula. Kwa wanawake wanaokumbwa na kichefuchefu, wahimize wale chakula kidogo mara kwa mara.

Matatizo yatokanayo na lishe duni

Lishe duni inaweza kusababisha uchovu, udhaifu, ugumu katika kupigana na maambukizi na matatizo mengine makali ya kiafya. Lishe duni ni hatari hasa katika ujauzito. Inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba au mtoto kuzaliwa akiwa mdogo sana au akiwa na kasoro za kuzaliwa. Pia huongeza uwezekano wa mtoto au mama kufariki katika au baada ya kuzaa.

14.1.2 Kuzungumza na wanawake kuhusu chakula

Unapokutana na wanawake kwa huduma za utunzaji katika ujauzito au katika mikutano ya vijiji na sherehe au sokoni, jaribu kupata njia za kuwahoji kwa makini kuhusu vyakula wanavyovila. Ni bora kwa wanawake wajawazito kuanza kula vyakula bora mapema, kwani hii huwawezesha kuishi wakiwa wenye afya, kuzaa kikawaida, na kupata watoto wenye afya. Ili kujua ikiwa mwanamke anakula vizuri, mwulize chakula anachokila, na kiasi gani. Kwa mfano mwulize: ‘Je, ulikula nini jana?’ Hakikisha unamweleza kilicho bora kuhusu anachokila. Tilia mkazo juhudi bora anazofanya kwa kula vizuri. Kisha kukiwa na haja, pendekeza jinsi anavyoweza kula chakula bora zaidi.

Kumbuka kuwa elimu kuhusu chakula kivyake haitoshi kubadili mazoea ya kula. Hata ikiwa mwanamke anajua vyakula vilivyo bora kwa afya huenda akakosa kuvila. Familia nyingi haziwezi kumudu kununua vyakula vya kutosha au vya aina tofauti. Ili kumsaidia mwanamke kula vyema, pendekeza vyakula bora anavyoweza kumudu na atakavyopendelea.

14.1.3 Kula vizuri kwa garamakidogo

Kisababishi kikubwa cha lishe duni ni umaskini. Familia maskini sana inaweza kula vizuri kwa kutumia pesa kwa hekima na bila kutumia vibaya kidogo walicho nacho. Baba anayenunua pombe, tumbaku na miraa anaweza kununua chakula bora au kuku wa kutaga mayai badala ya hivyo vingine. Mama anayewanunulia watoto wake peremende na soda anaweza kununua mayai, maharagwe au vyakula vingine bora vya bei ya chini badala ya hivyo vingine. Hapa kuna maoni ambayo familia zinaweza kutumia ili kula vyema kwa garama kidogo.

Mchoro 14.2 Panda maharagwe mwaka huu na upande mahindi papo hapo mwaka ujao.

Maharagwe, kunde na ndengu

Maharagwe, kunde na ndengu huwa katika familia ya mboga iitwayo jamii kunde. Jamii kunde zote huwa na protini na vitamini kwa wingi na huwa hazigharimu fedha nyingi. Hata zina vitamini nyingi zikioteshwa kabla ya kuliwa. Upandaji wa jamii kunde huurutubisha udongo. Mazao mengine kama vile mahindi hukua vyema zaidi shambani ambapo jamii kunde zimekuzwa hapo awali (Mchoro 14.2).

Nyama na bidhaa za wanyama za bei nafuu

Damu na nyama za viungo kama ini, moyo, na figo zina ayoni nyingi na zinaweza kuwa na bei ya chini kuliko nyama zingine. Samaki na kuku ni bora pia kama nyama zingine na huwa na bei ya chini, hasa kwa familia inayovua au inayofuga kuku. Mayai yana protini, ayoni na vitamini A kwa wingi. Mayai hutoa protini nyingi kwa garama kidogo kuliko karibu chakula kingine chochote.

Nafaka nzima

Nafaka kama tefu, ngano, mchele na nafaka huwa na virutubishi zaidi wakati hazijasafishwa (kusindikwa ili kuondoa rangi). Uondoaji wa rangi huondoa vitu bora pia. Mkate mweupe na mchele mweupe vina vitamini, madini na protini chache kuliko mkate au mchele wa kahawia. Tefu nyeusi na injera ya kahawia zina virutubishi zaidi kuliko zenye rangi hafifu (isiyoiva).

Mboga na matunda

Mboga zinapochemshwa au kupikwa kwa mvuke, vitamini zingine kutoka kwa vyakula hivyo huenda kwa maji ya kupika. Tumia maji haya kutengeneza supu.

Majani ya nje ya mimea mara nyingi hutupwa lakini wakati mwingine yanaweza kuliwa. Majani ya mmea wa muhogo yana vitamini na protini nyingi kuliko mizizi yake. Matunda mengi ya mwituni na matunda madogo madogo huwa na vitamini na sukari asilia zinazotoa nguvu.

Maziwa ya mama

Maziwa ya mama hayagharimu chochote na yana jumla ya lishe inayohitajika kwa mtoto. Watoto wachanga wanaonyonyeshwa bila kupewa chakula kingine chochote hawahitaji maziwa wala vyakula vingine vilivyosindikwa hadi watimize umri wa miezi 6.

14.2 Makundi ya vyakula na virutubishi vyao

Vyakula vikuu (kabohidrati)

Katika sehemu nyingi duniani, watu hula aina moja ya chakula kikuu kwa kila mlo. Chakula hiki kikuu kinaweza kuwa injera, mchele, mahindi, ngano, mtama, mihogo, ndizi, kocho, bulla, godere, shenkora, gishta, shelisheli au chakula kingine cha wanga cha bei nafuu kilicho na kabohidrati. Vyakula hivi hupatia mwili nguvu. Hata hivyo, mwili unahitaji aina zingine za vyakula pia ili kukua na kudumisha afya.

Vyakula vya kukuza au vijenzi (protini)

Nyama, samaki, na jibini ni vyakula vyenye virutubishi lakini hubeba vimelea au ugonjwa vikiliwa kabla ya kupikwa. Wanawake wajawazito wanapaswa kula samaki, nyama, au jibini baada ya kupikwa au kuondolewa vijidudu tu.

Vyakula vya kukuza (vijenzi) huwa na protini inayohitajika kwa kukuza misuli, mifupa na damu dhabiti. Kila mtu anahitaji protini ili kuwa mwenye afya na kukua. Vyakula vingine vijenzi vilivyo na protini nyingi ni:

  • Jamii kunde (maharagwe, kunde, soya na ndengu )
  • Mayai
  • Jibini, maziwa na mtindi
  • Njugu na mbegu
  • Nafaka, ngano, na mchele
  • Nyama, kuku, na samaki

Vyakula vitoavyo nguvu (sukari na mafuta)

Vyakula vitoavyo nguvu huwa na sukari na mafuta, ambavyo huupa mwili nguvu. Kila mtu huhitaji vyakula hivi ili kudumisha afya. Vyakula vingine vitoavyo nguvu vilivyo na sukari nyingi ni:

  • Matunda
  • Asali

Vyakula vingine vitoavyo nguvu vilivyo na mafuta kwa wingi ni:

  • Njugu zingine (kwa mfano karanga) na mbegu zingine (kwa mfano alizeti)
  • Parachichi
  • Mafuta ya mboga, siagi, na mafuta ya nguruwe
  • Nyama yenye mafuta
  • Maziwa na jibini
  • Mayai
  • Samaki.

Siku hizi watu wengi hula sukari na mafuta mengi kuliko wanavyohitaji. Hii ni kwa sababu watu wengi hunywa soda yenye sukari au hula vyakula wanavyopata vikiwa vishatayarishwa badala ya vyakula vinavyotengenezwa nyumbani. Vyakula vilivyotayarishwa, vyenye sukari na mafuta ni ghali na si bora kama bidhaa mbichi. Pia huharibu meno. Ni bora kula vyakula vyenye nguvu vya asilia kuliko vilivyotayarishwa.

Vyakula vilinzi (vitamini na madini)

Vyakula vilinzi huwa na vitamini na madini na huusaidia mwili kupigana na maambukizi na kudumisha afya na uthabiti wa macho, ngozi na mifupa. Vitamini na madini pia huitwa virutubishi vidogo kwa sababu ni vidogo mno. Matunda na mboga huwa na vitamini na madini kwa wingi. Ni muhimu wanawake wajawazito kula aina nyingi za matunda na mboga iwezekanavyo. Katika sehemu itakayofuata tutajadili aina tano za vitamini na madini muhimu ambazo wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanapaswa kula kila siku.

14.2.1 Aina tano muhimu za vitamini na madini

Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji aina hizi tano za vitamini na madini kwa wingi kuliko watu wengine - ayoni, asidi ya foliki, kalisi, ayodini na vitamini A. Wanapaswa kujaribu kupata aina hizi za vitamini na madini kila siku.

  • Kwa nini unafikiri mwanamke mjamzito anahitaji vitamini na madini haya kwa wingi?

  • Mtoto huhitaji virutubishi hivi ili kukua na kuwa mwenye afya na kuzuia kasoro za kuzaliwa. Mwanamke mjamzito huvihitaji ili kuwa na nguvu za kutosha za kujitunza yeye na familia yake, kupigana na maambukizi na kumpa nguvu za kuweza kuubeba ujauzito huo hadi mwisho, kuzaa kwa usalama na kumnyonyesha mtoto baadaye.

    Mwisho wa jibu

Ayoni

Ayoni husaidia katika kudumisha afya ya damu na kuzuia anemia (utajifunza kuhusu kutambua na kutibu anemia katika Kipindi cha 18 cha Moduli hii). Mwanamke mjamzito anahitaji ayoni kwa wingi ili kuwa na nguvu za kutosha, kuzuia kutokwa na damu sana wakati wa kuzaa, na kuhakikisha kuwa mtoto anayekua anaweza kutengeneza damu bora na kujiwekea ayoni ya kutumia miezi michache ya kwanza baada ya kuzaliwa. Pia ni muhimu kwa utengenezaji wa maziwa bora ya mama.

Mchoro 14.3 Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanapaswa kujaribu kula angalau mlo mmoja ulio na ayoni kila siku.

Vyakula hivi vina ayoni kwa wingi (Mchoro 14.3):

  • Kuku
  • Samaki
  • Alizeti, boga, na mbegu za boga
  • Maharagwe, kunde, na ndengu
  • Majani ya mboga ya rangi ya kijani kibichi nzito
  • Viazi vikuu
  • Boga gumu
  • Nyama (hasa ini, figo, na nyama ya viungo vingine)
  • Bidhaa za nafaka nzima
  • Matunda yaliyokaushwa
  • Njugu
  • Mkate uliosindikwa kwa ayoni
  • Kiini-yai

Kumeza tembe za ayoni

Inaweza kuwa vigumu kwa mwanamkwe mjamzito kupata ayoni ya kutosha hata akila vyakula vyenye ayoni kila siku. Anapaswa pia kutumia tembe za ayoni (au matone ya ayoni) ili kuzuia anemia. Dawa hizi zinaweza kuitwa ferrous sulfate, ferrous gluconate, ferrous fumerat, au majina mengine (jina ferrous linatoka kwa jina la Kilatini la Ayoni)

Tembe au matone ya ayoni yanaweza kupatikana katika maduka ya dawa au vituo vya afya. Hata hivyo, kote Afrika, utawapa wanawake wajawazito tembe za ayoni kidesturi kama sehemu ya mpango wa Utunzaji katika Ujauzito. Mwanamke anafaa kupata milligramu 300 hadi 325 za ferrous sulphate mara moja kwa siku kupitia kinywani, hasa pamoja na chakula. Kipimo hiki huwa katika tembe moja iliochanganywa na folati (tazama hapa chini)

Tembe za ayoni zinaweza kusababisha kichefuchefu au uyabisi wa utumbo na kinyesi chake kinaweza kugeuka kuwa cheusi. Hata hivyo, ni muhimu mwanamke huyo kuendelea kumeza tembe za ayoni kwa sababu anemia inaweza kusababisha matatizo wakati wa ujauzito, kuzaa na baada ya mtoto kuzaliwa. Ni bora kwa mwanamke huyo kumeza tembe ya ayoni pamoja na chakula, kunywa viowevu vingi, na kula matunda na mboga kwa wingi ili kuzuia kichefuchefu na uyabasi wa utumbo. Rangi nyeusi ya kinyesi ni athari ya kawaida ya ayoni na haidhuru.

Folati (asidi ya foliki)

Ukosefu wa folati unaweza kusababisha anemia kwa mama na kasoro kali za kuzaliwa kwa mtoto. Ili kuzuia matatizo haya, ni muhimu ikiwezekana mwanamke huyu apate asidi ya foliki ya kutosha kwa mlo wake kabla ya ujauzito na anapaswa kufanya hivi katika miezi michache ya kwanza ya ujauzito.

Vyakula vilivyo na folati ambavyo wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanapaswa kujaribu kula kila siku (Mchoro 14.4) ni:

Mchoro 14.4 Vyakula hivi huwa na folati kwa wingi.
  • Majani ya mboga ya kijani kibichi
  • Nafaka nzima (mchele wa rangi ya kahawia, ngano nzima)
  • Nyama (hasa ini, figo, na nyama ya viungo vingine)
  • Samaki
  • Ndengu na maharagwe
  • Mayai
  • Alizeti, boga na mbegu za boga
  • Uyoga.

Pamoja na kula vyakula hivi kwa wingi iwezekanavyo, wanawake wote wajawazito wanapaswa pia kumeza tembe za asidi ya foliki za mikrogramu 400 kila siku wakati wa ujauzito. Anapaswa aweze kupata tembe hizi kutoka kwako kama sehemu ya utunzaji katika ujauzito.

Kalisi

Mchoro 14.5 Vyakula vilivyo na kalisi

Mtoto anayekua anahitaji kalisi kwa wingi ili kutengeneza mifupa mipya hasa katika miezi michache ya mwisho ya ujauzito. Wanawake huhitaji kalisi ili wawe na mifupa na meno thabiti. Vyakula hivi vina kalisi nyingi (Mchoro 14.5):

  • Mboga za rangi ya manjano (boga gumu, viazi vikuu)
  • Maji ya majivu ya kaboni
  • Maziwa, magandi, mtindi, na jibini
  • Mboga za kijani kibichi
  • Mlo wa mifupa na maganda ya mayai
  • Molasi na soya
  • Sadini.

Wanawake wanaweza pia kupata kalisi kwa:

  • Kulowesha mifupa au maganda ya mayai kwa siki au juisi ya ndimu kwa saa chache kisha watumie majimaji haya kutengeneza supu au wale kwa vyakula vingine.
  • Kuongeza juisi ya ndimu, siki, au nyanya unapopika mifupa.
  • Kusaga maganda ya mayai kuwa poda laini na kuchanganya na chakula.
  • Kulowesha mahindi kwa maji ya majivu ya kaboni kabla ya kuyapika.

Aidini

Mchoro 14.6 Chumvi yenye ayodini ndiyo njia rahisi sana ya kupata aidini ya kutosha katika mlo.

Aidini huzuia tezi-shingo (uvimbe kwenye shingo) na matatizo mengine kwa watu wazima. Ukosefu wa aidini kwa mwanamke mjamzito unaweza kusababisha ukretini (ulemavu unaoathiri akili na maumbile) kwa mtoto wake.

Njia rahisi sana ya kupata aidini ya kutosha ni kutumia chumvi iliyoaidinishwa (yenye aidini) badala ya chumvi ya kawaida (Mchoro 14.6). Chumvi hii hupatikana kwa pakiti iliyoandikwa “chumvi iliyo aidinishwa” katika masoko mengi.

Vitamin A

Vitamin A huzuia uwezo duni wa kuona wakati wa usiku au ukali wa mwanga unapokuwa chini na husaidia kupigana na maambukizi. Ukosefu wa vitamini A pia husababisha upofu kwa watoto. Mwanamke anahitaji kula chakula kilicho na vitamini A kwa wingi wakati wa ujauzito na akinyonyesha.

  • Mboga za rangi nzito ya manjano na kijani kibichi na mtunda ya rangi ya manjano huwa na vitamini A kwa wingi. Taja baadhi ya mboga na matunda haya.

  • Karoti, maembe, spinachi, kabeji (Huenda umetaja mifano mingine bora)

    Mwisho wa jibu

Vyanzo vingine vya vitamini A ni ini, mafuta ya ini na ya samaki, maziwa, mayai na siagi.

Viowevu

Pamoja na kula vyakula bora, wanawake wanapaswa kunywa maji safi kwa wingi pamoja na viowevu bora vingine kila siku. Juisi za matunda, maziwa ya wanyama, na vinywaji vingi vitokananvyo na kulowesha au kuchemsha mimea ya mwituni ni viowevu bora vya kunywa.

14.3 Usafi katika ujauzito

Wakati wa ujauzito, wanawake wanapaswa kuwa waangalifu hasa kuhusu usafi wao wa kibinafsi. Wanawake wajawazito hutoa jasho zaidi na hutokwa na mchozo zaidi ukeni kuliko wale wasio wajawazito (kutokana na mabadiliko ya homoni) na wanaweza kuwa wepesi wa kupata maambukizi kutokana na vijidudu vilivyo kwenye mazingira. Kudumisha usafi wa mwili husaidia kuzuia maambukizi. Kuosha mikono kwa sabuni ndilo tendo bora sana analoweza kufanya ili kudumisha usafi hasa kabla ya kutayarisha chakula na baada ya kwenda chooni. Ikiwezekana, mwanamke mjamzito anafaa kuosha mwili wake kwa maji safi kila siku – hasa sehemu ya jenetalia.

Usafi wa meno ni muhimu hasa wakati wa ujauzito kwa sababu viwango zaidi vya estrojeni vinaweza kusababisha kufura na uwezo zaidi wa kupitisha hisi katika tishu za ufizi. Asafishe meno yake kwa kijiti au mswaki na dawa ya meno, mwanake huyo mjamzito anapaswa kufanya hivyo mara kwa mara.

14.4 Kuishi kwa mtindo bora wa maisha

Pamoja na kula vizuri na kudumisha usafi, mwanamke mjamzito anahitaji kupata usingizi na kupumzika vya kutosha kila siku. Hii itamsaidia kujiepusha na shinikizo la juu la damu (imejadiliwa kwa kina katika Kipindi cha 19 baadaye katika Moduli hii), na edema (kuvimba kwa miguu na vifundo kutokana na kiowevu kujikusanya katika tishu). Kupumzika vizuri pia humsaidia kuimarika na kuipa fetasi nafasi nzuri ya kuzaliwa ikiwa yenye afya.

Mchoro 14.7 Familia zinazomhimiza mwanawake mjamzito kupumzika mara nyingi humsaidia yeye na mtoto wake kuwa wenye afya.

Wanawake wengi lazima wafanye kazi kwenye mashamba, makampuni au maduka na aidha nyumbani kwao muda wote wa ujauzito. Hii inaweza kuwa ngumu hasa kwa wanawake wakati wa ujauzito kwa sababu wanachoka zaidi ya kawaida – hasa katika majuma machache ya mwisho. Waeleze pamoja na familia zao kuwa mwanamke huyo anafaa kujaribu kupumzika kwa dakika chache baada ya kila saa 1 hadi 2 (Mchoro 14.7). Hii pia itamsaidia kufurahia ujauzito wake.

Mchoro 14.8 Chochote mama anachoweka mwilini mwake humfikia mtoto wake.

Hakikisha wanawake wanaelewa kuwa chochote wanachokiweka mwilini mwao hupita kwenye plasenta na kumfikia mtoto (Mchoro 14.8). Moshi wa sigara, pombe, na madawa haramu kama afyuni, heroini, kokeini na dawa za usingizi ni hatari kwa kila mtu lakini ni za kudhuru hasa kwa fetasi inayokua. Hata kinywaji kimoja au viwili vyenye pombe wakati wa ujauzito vinaweza kupelekea mtoto kuzaliwa akiwa mdogo sana au akiwa na kasoro au ulemavu wa kuzaliwa unaoathiri ubongo.

Anapaswa pia kushauriwa kuepukana na:

  • Uinuaji wa vitu vizito
  • Watu wagonjwa, hasa ikiwa wanatapika, wanahara au wana upele
  • Kemikali kali au manukato yake (kwa mfano, kemikali zinazotumiwa kuua wadudu shambani)
  • Dawa zisizo muhimu
  • Dawa kama shira za kikohozi, haluli, na za kupunguza maumivu ambazo hajaandikiwa na muhudumu wa afya (Mchoro 14.9).
Mchoro 14.9 Wanawake wajawazito wanapaswa kunywa dawa ambazo ni salama tu katika ujauzito na ambazo kwa hakika zinahitajika.

14.5 Chanjo dhidi ya tetanasi

Tetanasi ni maambukizi hatari sana yanayohatarisha maisha na huharibu mfumo wa neva na husababishwa na bakteria katika mazingira, kwa mfano udongoni. Chanjo ya tetanasi ndiyo kinga bora zaidi dhidi ya tetanasi kwa mwanamke na mtoto wake. Kwa hivyo, ni muhimu sana kwake kuchanjwa kulingana na ratiba iliyo kwenye kadi yake na kuleta kadi yake kila anapokuja kwa utunzaji katika ujauzito. (Mchoro 14.10).

Picha 14.10 Hakikisha wanawake wote wajawazito wanapata chanjo dhidi ya tetanasi.

Katika Moduli ya Utunzaji wa Baada ya kuzaa utajifunza kuwa usafi wa gutu ya kiungamwana unapaswa kudumishwa na isiwe na unyevu hadi itakapoanguka. Hii ni mojawapo ya sababu za umuhimu wa mwanamke na familia yake kupanga na kujitayarisha kwa mtoto kuzaliwa mahali safi na salama na kuhudumiwa na mhudumu wa afya mwenye ujuzi kama wewe.

14.6 Faida za kuanza kunyonyesha mapema bila kumpa mtoto chakula kikinge chochote

Hali nzuri za kunyonyesha na kujishikiza vyema kwa mtoto yameelezewa kwa kina katika Moduli ya Utunzaji wa Baada ya kuzaa, lakini unapaswa kuweka misingi na wanawake wajawazito wakati wa safari za utunzaji katika ujauzito — hasa wanaopata mtoto kwa mara ya kwanza. Ikiwa mama ameamua kumnyonyesha mtoto wake au kumpa chakula mbadala, unapaswa kuheshimu uamuzi wake. Lakini hawezi kufanya uamuzi huu ikiwa hujamfahamisha vizuri kuhusu faida za kuanza kunyonyesha mapema bila kumpa mtoto chakula kingine chochote. Mweleze kuwa:

  • Humpa mtoto mzawa lishe bora zaidi
  • Hufyonzwa kwa urahisi na kutumika vizuri mwilini mwa mtoto
  • Hukinga dhidi ya maambukizi na maradhi mengine
  • Hukinga dhidi ya mizio.
  • Ni ya bei nafuu
  • Huendeleza uhusiano kati ya mama na mtoto
  • Humpa mwanamke kinga dhidi ya ujauzito kwa kiwango fulani (ingawa ina ubora wa chini ya asilimia100) ikiwa ananyonyesha mtoto bila kumpa chakula kingine chochote hadi kipindi cha kwanza cha hedhi kitakaporudi baada ya kuzaa.

14.6.1 Imani na mazoea duni kuhusu ulishaji wa watoto wazawa

Katika nchi zingine kunazo imani kuhusu ulishaji wa watoto wazawa ambazo ni hatari kwa afya ya mtoto. Kwa mfano katika sehemu zingine, mtoto hupewa chakula au viowevu kama vile maji yaliyo na sukari, asali, mimea ya mwituni, viungo, na maziwa ya wanyama katika siku 3 za kwanza baada ya kuzaliwa kabla mwanamke huyo kuanza kunyonyesha. Kiowevu chepesi cha maji maji kiitwacho kolostramu kitolewacho na matiti katika siku hizi 3 za kwanza kinaweza kutupwa kwa sababu huchukuliwa kutokuwa safi.

  • Je, faida za kumpa mtoto mzawa kolostramu ni zipi? (Ulijifunza kuhusu haya katika Kipindi cha 7 cha Moduli hii)

  • Kolostramu ina protini na antibodi (protini spesheli zinazotolewa na mfumo wa kingamwili wa mama zinazosaidia kumkinga pamoja na mtoto wake dhidi ya maambukizi).

    Mwisho wa jibu

Hata baada ya maziwa ya mama kuanza kutoka watu wengine huendelea kulisha mtoto viowevu vingine na asali pamoja na kunyonyesha.

  • Je, unafikiri ni nini sababu za kufanya hivi na kuna hatari zipi kwa kufanya hivi?

  • Watoto wanaonyonyeshwa wanaweza kutaka kula mara kwa mara na kwa hivyo huenda mama akafikiri kuwa maziwa yake pekee hayatoshi. Kumlisha mtoto viowevu vingine na asali si muhimu kwa lishe na huongeza hatari za maambukizi kutoka kwa kijiko au chupa inayotumika.

    Mwisho wa jibu

14.6.2 Kanuni za kijumla za kuanza kunyonyesha mapema pasipo kumpa mtoto chakula kingine chochote

Kwa kina mama ambao hawana VVU:

  • Watoto wanapaswa kuanza kunyonya mapema iwezekanavyo (hasa katika saa ya kwanza) na kuendelea kwa angalau miezi 6 ya kwanza ya maisha.
  • Kolostramu ambayo ndiyo maziwa ya kwanza, inapaswa kupewa mtoto na bali si kutupwa.
  • Mtoto anapaswa kunyonyeshwa bila kupewa chakula kingine chochote kwa miezi 6 ya kwanza ya maisha. Mtoto asilishwe wala kunyweshwa kitu kingine chochote katika wakati huu.
  • Mtoto anapaswa kunyonyeshwa kila anapotaka, iwe usiku au mchana (anapodai) na hii huchochea matiti kutoa maziwa ya kutosha.

Utajifunza jinsi ya kuwashauri kina mama walio na VVU katika Kipindi cha 16 cha Moduli hii kilicho juu ya uzuiaji wa maambukizi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto.

14.7 Upangaji uzazi baada ya kuzaa

Majadiliano kuhusu njia tofauti za upangaji wa uzazi baada ya kuzaa yanapaswa kuanza katika kipindi cha ujauzito. Habari na huduma za upangaji wa uzazi ni sehemu muhimu ya utunzaji bora katika ujauzito. Matukio haya hutoa nafasi kwa wahudumu wa afya kujadiliana na wanawake faida za uzazi wa majira (kuwa na angalau nafasi ya miaka 2 kati ya uzazi) kwa afya yao na ya watoto walio nao na watakaowapata baadaye. Wasaidie wanawake wajawazito na kina mama wa mara ya kwanza kuamua jinsi watakavyojizuia kupata ujauzito baada ya kuzaa.

14.7.1 Kunyonyesha na uzuiaji wa ujauzito

Kurudi katika hali ya kuweza kupata ujauzito baada ya kuzaa hakutabiriki kabisa na kupata ujauzito kunaweza kutokea kabla mwanamke kuanza tena kipindi chake cha kwanza cha hedhi. Mwanamke ambaye hanyonyeshi bila kumpa mtoto chakula kingine chochote anaweza kupata ujauzito haraka kama majuma 4 hadi 6 baada ya kuzaa mtoto na anapaswa kuanza mbinu yoyote ya uzuiaji ujauzito kabla ya kuanza kushiriki ngono tena. Kunyonyesha kikamilifu bila kumpa mtoto chakula kingine chochote hutoa kinga dhidi ya ushikaji ujauzito, lakini hakuwezi kutegemewa kufaa kwa asilimia 100. Mwanamke anayenyonyesha hukingwa tu dhidi ya ujauzito ikiwa:

  • Hajapitisha miezi 6 baada ya kuzaa
  • Ananyonyesha tu bila kumpa mtoto chakula kingine chochote (mara 8 au zaidi kila siku pamoja na angalau mara moja usiku; hakuna kunyonyesha mchana kwa muda unaoachana kwa zaidi ya saa 4 na hakuna kunyonyesha usiku kwa muda unaoachana kwa zaidi ya saa 6; hakuna vyakula na viowevu vingine vya ziada anavyopewa mtoto)
  • Mzunguko wake wa hedhi haujaanza tena.

Mbinu nyingi salama za uzuiaji ujauzito kwa wanawake wanaonyonyesha zinapatikana.

14.7.2 Faida za uzazi wa majira

Kwa kinga kamili, wanawake baada ya kuzaa wasingoje hadi kurudi kwa hedhi ili kuanza mbinu ya kuzuia ujauzito, bali waanze mara tu mwongozo salamu wa mbinu waliyochagua unaporuhusu. (Kanuni zingine za kimsingi za uzuiaji ujauzito baada ya kuharibika kwa ujauzito au kutoka kwa mimba zimeelezwa katika Kipindi cha 20 cha Moduli hii. Majadiliano ya kina juu ya mbinu zote za uzuiaji ujauzito na miongozo vimetolewa katika Moduli ya Upangaji Uzazi katika mtalaa huu.)

Muda wa angalau miaka 2 kati ya uzazi huwa na faida za kiafya kwa mwanamke na mtoto (Kisanduku 14.1).

Kisanduku 14.1 Uzazi wa majira unaofaa hupunguza hatari ya:
  • Kifo cha mama
  • Kifo cha fetasi (kuharibika kwa mimba au kuzaa mtoto mfu), kifo cha mtoto mchanga
  • Anemia kwa mama katika ujauzito utakaofuata
  • Inflamesheni ya bitana ya endometriamu kwenye uterasi baada ya kuzaa
  • Kupasuka kwa mapema kwa membrani za amnioni zinazoizunguka fetasi
  • Kuzaa kabla ya kutimiza muda
  • Ucheleweshaji wa ukuaji wa bitana ya ndani ya uterasi na kuzaa mtoto aliye na uzani wa chini
  • Utapiamlo kwa watoto wazawa na wachanga kutokana na kutopata maziwa ya mama ya kutosha

Linganisha safari zako za huduma za upangaji uzazi na ratiba ya chanjo ya mtoto. Na kumbuka kuwa unyonyeshaji bora hutoa faida mara tatu: uimarikaji wa nafasi za kuishi kwa mtoto na afya yake, afya bora kwa kina mama, na uzuiaji wa ujauzito kwa muda.

Katika Kipindi kitakachofuata, utajifunza kuhusu kanuni za ushauri bora ili uweze kuwasilisha jumbe za uendelezaji wa afya kwa makini kwa wanawake wajawazito wakati wa utunzaji katika ujauzito na kuzungumzia matatizo na imani zao kuhusu ujauzito na kuzaa.

Muhtasari wa Kipindi cha 14

Katika Kiako cha 14 ulijifunza kua:

  1. Kula vizuri wakati wa ujauzito na kunyonyesha humaanisha kula aina tofauti za vyakula na vya kutosha - angalau kalori 200 zaidi kila siku.
  2. Kula vizuri ukiwa na pesa kidogo kunawezekana kwa kununua vyakula bora kama maharagwe na nyama za viungo kwa bei nafuu, kukuza jamii kunde, kufuga kuku, kutumia nafaka nzima na kutengeneza supu.
  3. Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji kula aina tofauti ya vyakula vikuu (kabohidrati), Vyakula vya kukuza/vijenzi(protini), vyakula vitoavyo nguvu (sukari na mafuta) na vyakula vilinzi (vitamini na madini hasa ayoni, folati, kalisi, aidini na Vitamini A).
  4. Wanamake wajawazito wanapaswa kupewa tembe za ayoni na za folati (asidi ya foliki) kama sehemu ya utunzaji taratibu katika ujauzito.
  5. Usafi wa kibinafsi, hasa kuosha mikono na kudumisha usafi wa sehemu ya jenitalia husaidia kuzuia maambukizi wakati wa ujauzito (na wakati wote).
  6. Kuweza kupumzika na kulala kwa wingi na kuepukana na pombe, sigara, madawa haramu, kemikali kali, na watu wanaoweza kukuambukiza husaidia kumkinga mwanamke mjamzito na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.
  7. Chanjo dhidi ya tetanasi inapaswa kuwa sehemu ya utunzaji taratibu katika ujauzito.
  8. Kumpa mtoto kolostramu na kuendelea kunyonyesha kikamilifu bila kumpa chakula kingine chochote ndiyo lishe bora zaidi na pekee ambayo mtoto huhitaji katika miezi 6 ya kwanza ya maisha.
  9. Kunyonyesha kikamilifu bila kumpa mtoto chakula kingine chochote kunaweza kumkinga mwanamke dhidi ya ujauzito mwingine kwa muda wa hadi miezi 6 baada ya kuzaa lakini ni ikiwa tu unyonyeshaji ni wa mara kwa mara na kipindi chake cha hedhi hakijarudi.
  10. Uzazi wa majira wa angalau miaka 2 ni bora kwa afya ya mwanamke, mtoto wake na watoto wowote wakubwa alionao – kwa hakika kwa jamii yote.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 14

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki , unaweza kutathmini ni kwa kiwango kipi umeweza kuyatimiza malengo ya masomo ya Kipindi hiki kwa kujibu maswali haya. Yaandike majibu katika shajara yako ya masomo kisha uyajadili na mkufunzi wako katika mkutano saidizi utakaofuata wa masomo. Unaweza kuyalinganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la kujitathmini 14.1 (linatathmini Malengo ya Somo 14.2)

Pendekeza njia za kuwasaidia wanawake ambao hawawezi kumudu vyakula vingi vya aina tofauti jinsi wanavvyoweza kupata kalori za kutosha na aina tofauti za vyakula.

Answer

Maharagwe, ndengu na kunde ni vyakula vya bei nafuu, vyenye virutubishi tele na rahisi sana kukuza. Nyama za viungo kama ini, moyo na figo zina ayoni nyingi na zinaweza kununulika kwa bei nafuu kuliko nyama zingine. Mkate na mchele wa rangi ya kahawia na teff nyeusi huwa na virutubishi zaidi kuliko nafaka za rangi hafifu (isiyoiva) na huwa za bei nafuu ikiwa hawezi kukuza mwenyewe.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 14.2 (linatathmini Malengo ya Somo 14.1 na 14.2)

Kamilisha Jedwali 14.1. Baadhi ya makundi yameachwa mapengo ya kuandika majibu yako.

Jedwali 14.1 kwa Swali la Kujitathmini 14.2
Kundi la vyakulaVilivyomoMifano mitatu
Vyakula vikuuKabohidrati
Protini
Vyakula vitoavyo nguvu
Vitamini na Madini
Answer

Jedwali lililo hapa chini ni jedwali 14.1 lililokamilishwa. Hatujui hasa ni mifano gani mitatu uliyochagua kwa kila kundi la vyakula, kwa hivyo huenda umetaja mifano mingine mizuri.

Kundi la vyakulaVilivyomoMifano mitatu
Vyakula vikuuKabohidratiInjera, mchele, mahidi, nk
Vyakula vya kukuza (vijenzi)ProtiniMaharagwe, mayai, nyama, nk
Vyakula vitoavyo nguvuSukari na mafutaMatunda, asali, njugu, nk
Vyakula vilinziVitamini na MadiniSamaki, mboga za kijani kibichi, nyama, nk

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 14.3 (linatathmini Malengo ya Somo 14.3, 14.4 na 14.5)

Je, ni ushauri upi unaopaswa kumpa mwanamke mjamzito kuhusu jinsi ya kuepuka maambukizi kwake yeye au kwa mtoto wake mzawa? Fikiria angalau hatua tatu tofauti anazoweza kuchukua.

Answer

Baadhi ya hatua unazoweza kumshauri mwanamke mjamzito kuchukua ili kuepuka maambukizi kwake yeye na kwa mtoto wake mzawa ni:

  • Kunawa mikono yake kwa sabuni hasa kabla ya kutayarisha chakula na baada ya kutumia choo.
  • Kuosha mwili wake kila siku kwa maji safi hasa sehemu yake ya jenitalia.
  • Kuosha meno yake kila siku kwa kijiti cha meno au mswaki.
  • Kupata chanjo dhidi ya tetanasi.
  • Kudumisha usafi na ukavu wa gutu la kiungamwana cha mtoto mzawa hadi litakapoanguka.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 14.4 (linatathmini Malengo ya Somo 14.1, 14.5 na 14.6)

Je, ni gani kati ya kauli hizi isiyo sahihi? Eleza kisicho sahihi kwa kila kauli.

  • A.Unyonyeshaji hufaa kwa asilimia 100 kwa kuzuia ujauzito mwingine.
  • B.Kolostramu inapaswa kupewa mtoto mzawa bali si kutupwa.
  • C.Kuanza kunyonyesha mapema na bila kumpa mtoto chakula kingine chochote humaamisha kumlisha maziwa ya mama pekee kutoka saa ya kwanza ya maisha ya mtoto hadi angalau umri wa miezi 6.
  • D.Hata kipindi cha hedhi kikirudi wakati wa kunyonyesha bila kumpa mtoto chakula kingine chochote, mwanamke hahitaji kuanza mbinu nyingine ya uzuiaji ujauzito.
  • E.Faida za uzazi wa majira wa angalau miaka 2 ni kupunguza hatari za kifo cha mama na cha fetasi.
Answer

A si sahihi. Kunyonyesha hakufai kwa asilimia 100 katika kuzuia ujauzito mwingine. Kunyonyesha kikamilifu na bila kumpa mtoto chakula kingine chochote hutoa kinga bora dhidi ya ujauzito lakini haiwezi kutegemewa kuwa inayofaa kwa asilimia 100 - hasa baada ya miezi 6 tangu kuzaa au ikiwa kipindi cha hedhi kimerudi.

B ni sahihi. Kolostramu inapaswa kupewa mtoto kwa sababu ina virutubishi vingi na hutoa kinga dhidi ya maambukizi.

C ni sahihi. Kuanza kunyonyesha mapema bila kumpa mtoto chakula kingine chochote humaamisha kumlisha maziwa ya mama pekee kutoka saa ya kwanza ya maisha ya mtoto mpaka angalau umri wa miezi 6.

D si sahihi. Mwanamke anayenyonyesha bila kumpa mtoto chakula kingine chochote hahitaji kuanza mbinu nyingine ya uzuiaji ujauzito iwapo kipindi chake cha hedhi kimerudi.

E ni sahihi. Uzazi wa majira wa angalau miaka 2 hupunguza hatari za kifo cha mama na cha fetasi.

Mwisho wa jibu