Skip to main content
Printable page generated Friday, 29 March 2024, 12:04 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Friday, 29 March 2024, 12:04 AM

15. Kuwashauri Wanawake Wajawazito kuhusu Dalili za Hatari

Kipindi cha 15 Kuwashauri Wanawake Wajawazito kuhusu Dalili za Hatari

Utangulizi

Kipindi hiki kitakupa maarifa ya jinsi ya kuwashauri wanawake wajawazito kuhusu dalili za hatari zinazotokea sana zinazoweza kuwakumba baadhi yao katika ujauzito. Ushauri bora katika lugha wanayoweza kuelewa utawawezesha kujua wanapohitaji kupata usaidizi wa dharura kutoka kwako au katika kituo cha afya ikiwa mojawapo ya dalili hizi itatokea.

Tayari umeelewa tofauti kati ya dalili na ishara katika Kipindi cha 8, na katika Kipindi cha 9 ulijifunza kuhusu ishara na dalili za hatari zinazotokea sana katika ujauzito. Kipindi hiki kitaanza kwa kukueleza kwa kifupi kanuni za kijumla na sehemu maalumu za kuwashauri wanawake wajawazito. Kisha tutatoa muhtasari wa dalili zinazohusiana au zisizohusiana na ujauzito ambazo wanawake wajawazito wanaweza kuhisi au kutambua kulingana na umri wa ujauzito. Baadaye katika kipindi hiki, tutakuelekeza jinsi na unapofaa kuwashauri wanawake wajawazito kwa mujibu wa dalili hizi za hatari, na kusisitiza umuhimu wa kuwahusisha waume/ wenzi wao katika ushauri huu.

Malengo ya Somo la Kipindi 15

Baada ya kipindi hiki, unafaa uweze:

15.1  Kueleza na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa katika herufi nzito. (Swali la kujitathmini 15.2)

15.2  Kujadili kanuni za kijumla za kutoa ushauri na kutoa muhtasari wa ujuzi na mitazamo ya mshauri bora. (Maswali ya kujitathmini 15.1, 15.3, 15.4 na 15.5)

15.3  Kueleza umaalumu wa kuwashauri wanawake wajawazito. (Maswali ya kujitathmini 15.1 na 15.3)

15.4  Kueleza dalili za hatari zinazotokea sana zinazoweza kuhisiwa au kutambuliwa na wanawake wajawazito, umri wa ujauzito ambapo kila dalili ina uwezekano mkubwa wa kutokea, na hatua ambayo mwanamke huyo anafaa kuchukua (Maswali ya Kujitathmini 15.2 na 15.5)

15.5  Kutambua wakati bora wa kutoa ushauri kuhusu aina tofauti za dalili za hatari kwa mujibu wa umri wa ujauzito. (Swali la kujitathmini 15.3)

15.6  Kueleza umuhimu wa kumhusisha mume au mwenzi katika ushauri kwa wanawake wajawazito kuhusu dalili za hatari. (Swali la kujitathmini 15.4)

15.1  Kanuni za kijumla katika ushauri wa mwanamke mjamzito

Kumshauri mwanamke mjamzito ni mawasiliano ya njia mbili kati ya watu wawiliambapo unamsaidia kujua kuhusu matatizo yanayoweza kumkumba katika ujauzito na kisha afanye uamuzi wake wa jinsi ya kuyatatua. Mnapoanza majadiliano haya mkiwa mmefahamiana vyema haimsaidii tu mwanamke huyo kujua matatizo yanayoweza kumkumba, bali pia hujenga uaminifu kati yenu. Pia, njia hii ya mawasiliano humtuliza mwanamke huyo na kumwezesha kuwasilisha wasiwasi na matakwa yake kwako akiwa huru.

Kumbuka kuwa mwanamke mjamzito ni mtaalam pia katika matakwa na hali yake. Amejifunza mengi Kivyake (wakati mwingine sahihi na mwingine yasiyo sahihi). Kwa hivyo, usimpinge kuwasilisha kwako imani na mawazo yake kutoka mwanzo - unafaa kustahimili imani na maadili ya kila mwanamke huku ukijaribu kuondoa kwa upole na kimakini mambo yoyote potovu sana anayoweza kuwa nayo. Heshima na ustahimilivu kwa imani potovu haimaanishi kuwa unazikubali na haziwezi kubadilishwa. Umakini na ustahimilivu ni mbili za sifa bora bainifu za mshauri bora.

Kisanduku 15.1 kinatoa muhtasari wa ujuzi na mitazamo unayohitaji ili kuanzisha mawasiliano bora na mteja yeyote, wakiwemo wanawake wajawazito. Mchakato wa kushauri hupitia awamu hizi: kujenga uhusiano na wanawake wajawazito, kuchunguza matatizo yao, kuwezesha mbadilishano wa habari na kutamatisha mchakato huu wa mashauriano kwa furaha na miadi.

Mchoro 15.1   Kudumisha usiri hujenga uaminifu.

Kisanduku 15.1  Ujuzi na mitazamo kwa mawasiliano bora ya njia mbili

  • Mkaribishe mwanamke na aketi karibu nawe akikutazama.
  • Tabasamu na muweze kuangaliana ana kwa ana.
  • Mhakikishie tena kuwa mtakayozungumza yatawekwa siri (Mchoro 15.1).
  • Usihusishe mtu wa tatu kwenye mkutano huu bila idhini yake.
  • Tumia lugha rahisi isiyo ya kitabibu wakati wote ili aweze kuelewa na uhakikishe mara kwa mara kuwa ameelewa.
  • Msikize kwa makini kwa kutumia ishara na kuzungumza ili kuonyesha kuwa unasikiza yote anayoyasema.
  • Mhimize aulize maswali, aeleze matakwa na shaka alizonazo na kuuliza asipoelewa.
  • Kikawaida anafaa kuongea kwa theluthi mbili za muda wote nawe uzungumze theluthi moja (tazama Mchoro15.2). Utafiti umeonyesha kuwa wataalamu wa afya mara nyingi huongea sana badala ya kuwapa wateja muda wa kutosha wa kutoa maoni na matakwa yao.
Mchoro 15.2 Wahudumu wa afya wanapaswa kuongea kwa muda mfupi na kuwahimiza wateja wao kuongea zaidi.

15.2  Je, nini cha muhimu kuhusu kuwashauri wanawake wajawazito?

Kwa mwanamke mjamzito, kusudi la kijumla la kupata ushauri ni kumpa habari muhimu kwa kuendeleza au kudumisha afya yake pamoja na ya mtoto wake kabla na baada ya kuzaa. Mahususi, ushauri utamsaidia mwanamke mjamzito kuishi mwenye afya kwa kumshauri kuhusu masuala ya uendelezaji wa afya kama vile lishe (ulijifunza haya katika Kipindi cha 14) na pia kujua dalili zitokeazo sana za hatari za kiafya zinazoweza kumdhuru yeye na mtoto wake. Mbali na haya, ushauri ni kiingilio kwenye familia hasa kwa mume/ mwenziwe ili pia wajue hatari zinazoweza kutokea katika ujauzito na kujitayarisha kisaikolojia na kiuchumi. Kisanduku 15.2 kinatoa muhtasari wa matokeo bora ushauri kuhusu dalili za hatari katika kipindi cha ujauzito.

Mchoro 15.3  Ikiwa mwanamke mjamzito atakuamini, anauwezekano wa kuja na kupata huduma ya utunzaji kabla ya kuzaa.

Kisanduku 15.2  Kushauri kuhusu dalili za hatari

Kushauri kumefanikiwa ikiwa mwanamke mjamzito:

  • Anahisi amepata usaidizi aliohitaji.
  • Anaelewa dalili za hatari zinazotokea sana.
  • Anajua la kufanya na kujihisi mjasiri kuwa anaweza kuja karibuni apatapo mojawapo ya dalili za hatari.
  • Anahisi kuheshimiwa, kusikizwa na kuthaminiwa.
  • Atarudi anapohitaji usaidizi wako (anakuamini, tazama Mchoro 15.3)

15.3  Je, dalili za hatari zitokeazo sana katika ujauzito ni zipi?

Kutokea kwa dalili hizi za hatari zinazoweza kuhisiwa au kugunduliwa na mwanamke mjamzito hutofautiana kulingana na umri wa ujauzito.

  • Je, ni nini maana ya trimesta ya kwanza, ya pili na ya tatu ya ujauzito?

  • Trimesta humaanisha ‘kipindi cha miezi mitatu’. Trimesta ya kwanza ni miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito (yaani, tangu utungaji mimba hadi mwisho wa juma la 14 la ujauzito, muda huo ukipimwa tangu kipindi chake cha mwisho cha kawaida cha hedhi); trimesta ya pili ni kutoka miezi 3 hadi 6 (yaani, kuanzia majuma 15 hadi 27); trimesta ya tatu ni miezi 3 ya mwisho ya ujauzito (yaani, kuanzia majuma 28 hadi kuzaa ambapo ni hata hadi baada ya majuma 42).

    Mwisho wa jibu

Tayari umejifunza kuhusu uchunguzi wa matatizo yanayohusiana na ujauzito na afya kwa kuchukua historia ya mwanamke na kufanya uchunguzi wa kimwili (kumbuka Vipindi vya 8 na 9). Hata hivyo, unaweza tu kutambua hatari za kiafya kwa mama au mtoto katika uchunguzi wa ujauzitoni, kwa hivyo ni muhimu kumsaidia mama kutambua dalili zozote kivyake na kujua anapopaswa kuja kwako haraka.

Kwanza unahitaji kujua vizuri sana wakati ambapo matatizo yanayohusiana na ujauzito au ya kiafya hutokea kwa kuchukua umri wa ujauzito kama muda muhimu (tazama Jedwali 15.1). Pili, unapaswa kuwa makini usije ukampa mwanamke huyo habari nyingi kwa wakati mmoja. Tatu, kumbuka kuwa utoaji wa ushauri si tukio la wakati mmoja - unafaa kuwa tayari kurudia ujumbe kuhusu dalili za hatari kila unapomhudumia na kuhakikisha kuwa ameelewa vizuri.

Tayari unajua kuhusu baadhi ya matatizo yaliyoorodheshwa katika Jedwali 15.1 ( k.m ujauzito wa nje ya uterasi na ujauzito bandia). Baadaye katika Moduli hii, utajifunza kwa kina kuhusu visababishi vingine vya vifo vya kina mama na vya fetasi, na kuugua katika ujauzito: hiparemisisi gravidaramu ilikuwa katika Kipindi cha 12; urarukaji wa mapema wa membreni umejadiliwa katika Kipindi cha 17; malaria, anemia, na maambukizi ya mfumo wa viungo vya mkojo yamejadiliwa katika Kipindi cha 18, maradhi ya kihipatensheni ya ujauzito yako katika Kipindi cha 19; kuharibika kwa ujauzito na utokaji wa ujauzito, na kutokwa na damu ukeni mwanzoni na mwishoni mwa ujauzito yako katika Vipindi vya 20 na 21 mtawalia.

Uchungu wa mara kwa mara kwenye sehemu ya chini ya fumbatio pekee hutokea sana mwanzoni mwa ujauzito na kivyake si dalili ya hatari.

Jedwali 15.1  Dalili za hatari katika ujauzito

Dalili ambazo mama hupitia

(maneno yaliyo katika herufi za mlazo ndiyo muhimu sana)

Huenda akawa na hali hii ya kiafya
Utungaji mimba hadi majuma 20 ya ujauzito
Kutapika kunakodumu, kupoteza uzito

Hiparemesisi gravidaramu

Inayoonyeshwa kwa kutapika mara kwa mara, kupoteza kilo 5 au zaidi za uzani, uchunguzi wa mkojo unaonyesha ketoni 2+ au zaidi (Ulisoma haya katika Kipindi cha 12; jinsi ya kufanya uchunguzi wa mkojo katika Kipindi cha 19)

Kutokwa na damu (mbichi) ukeni, huenda ikawa na madonge ya damu au nyama, na uchungu kwenye sehemu ya chini ya fumbatio Utoaji mimba (kali)

Aina zote za uharibikaji wa ujauzito ni matukio makali na ya ‘ghafla’ isipokuwa utoaji potelelevu (Utasoma kuhusu utoaji katika Kipindi cha 20

 
Dalili za ujauzito zinapotea, fumbatio halikui au hata linapungua kwa ukubwa, huenda kukawa na kuvuja kwa damu nzito

Utoaji potelelevu

Fetasi au tishu ya fetasi inapokuwa kwenye uterasi wakati hakuna ishara za uhai na seviksi imefungwa kabisa

 
Kuvuja damu ukeni, (kama vile hedhi), maumivu kwenye sehemu ya chini ya fumbatio, kukosa hedhi au hedhi isiyo ya kawaida

Ujauzito wa nje ya uterasi

(umeangaziwa katika Vipindi vya 5 na 12)

Kutokwa na damu ukeni

 Kutokwa na damu (mbichi), kupita kwa tishu zinazofanana na barafu iliyochafuliwa kwa damu (tishu zinazofanana na zambarau), ukuaji wa haraka wa fumbatio

Ujauzito bandia

 

 (imejadiliwa katika Vipindi vya 10 na 20)

Umri wa majuma 20 hadi mwishoni mwa ujauzito
Maumivu ya kichwa, hisia ya kuungua kwa epigastriamu (Mchoro 15.4) kiwaa, Kuvimba kwa mwili (kunakohusisha mgongo, ukuta wa fumbatio, mikono na uso), kupungua kwa kiasi cha mkojo

Matatizo ya kihipatensheni ya ujauzito (Priklampsia na eklampsia yalitangulizwa katika Vipindi vya 8 na 9, utajifunza zaidi katika Kipindi cha 19) 

Mchoro 15.4

Kutokwa na damu ukeni mwishoni mwa ujauzito, hata kiasi kidogo

Kuharibika kwa mimba mwishoni mwa ujauzito (majuma 20 hadi 27) au kutokwa na damu katika ujauzito (majuma 28 na zaidi) (Utajifunza zaidi katika Kipindi cha 20)
Kuvuja kwa viowevu vya majimaji kutoka ukeni na kulowesha chupi zake pakubwa na kunaweza kukithiri

Upasukaji wa mapema wa membreni

(Utajifunza kuhusu urarukaji wa mapema wa membreni katika Kipindi cha 17)

Kuongezeka kunakoendelea kwa maumivu yanayosukuma chini kwenye sehemu ya chini ya fumbatio kabla ya miezi 9 ya ujauzito

Leba ya mapema

(Imeangaziwa katika Moduli ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa)

Hakuna mabadiliko katika ukuaji wa fumbatio, kusonga kwa fetasi kunasikika chini ya mara kumi kwa saa 12. (Idadi yoyote ya kusonga kwa fetasi kwa dakika moja, huhesabiwa kama moja)Vizuizi dhidi ya ukuaji wa fetasi kwenye uterasi (Imeangaziwa kwa kifupi katika Kipindi cha 7)

Fetasi kukosa kusonga kwa zaidi ya saa 6

Fetasi kufia ndani ya uterasi

Wakati wowote katika ujauzito

Kiwango juu cha joto, maumivu ya kichwa, kutetemeka, kuhisi baridi, kutokwa na jasho, kuhisi kiu, kuhisi maumivu kwa mwili wote, kukosa hamu ya kula

Malaria, kipindupindu, homa ya chawa au homa ya vipindi

(Utajifunza kuhusu maambukizi haya katika Moduli ya Magonjwa ya kuambukiza)

Mchoro 15.5 Maambukizi katika sehemu hii ya figo husababisha dalili za hatari.

Kukojoa kwa mara kwa mara kwenye uchungu na, na huenda mkojo ukawa na damu au uwe kama usaha

Maambukizi ya mfumo wa viungo vya mkojo (Maambukizi ya mfumo wa viungo vya mkojo, uvimbe wa kibofu au urethraiti)

(Utajifunza kuhusu maambukizi ya mfumo wa viungo vya mkojo katika Kipindi cha 18)

Maumivu mbavuni, joto jingi, kutapika, mkojo wenye damu, kukazwa na kukojoa mara kwa mara

Pielonefritisi (Inflamesheni ya figo) kali (Mchoro 15.5 unaonyesha sehemu maalum kwenye figo ambapo maambukizi haya yanaweza kutokea)

Macho kuwa na rangi ya manjano, kukosa hamu ya kula, kuchukia harufu ya vyakula vyenye vikolezo, anahisi uchovu kichefuchefu, na kutapika

Ugonjwa wa ini

Anahisi kiu, anakunywa maji mengi, anakojoa mara kwa mara, anahisi njaa, kupoteza uzani kwa mfululizo,

Kisukari Melitasi

Kukohoa

Ugonjwa wa mapafu na moyo

Jedwali 15.1 ni muhtasari wa kina unaofaa kusoma kama mhudumu wa afya. Haitakuwa bora wala muhimu kumuonyesha mwanamke mjamzito katika safari za utunzaji katika ujauzito.

  • Je, unaweza kueleza ni kwa nini sivyo?

  • Jedwali hili linatumia lugha ya kitiba ambayo huenda mwanamke asielewe (ila naye pia ni mhudumu wa afya), na inaweza kumjaza kwa habari nyingi zaidi kwa wakati mmoja na kumpa wasiwasi wa kutazamia hatari nyingi zinazoweza kumkumba yeye na mtoto wake.

    Mwisho wa jibu

Jedwali 15.2 ni muhtasari uliorahisishwa na kuwekwa katika sehemu mbili unaoweza kujadiliwa na wanawake wajawazito katika kipindi kinachofaa cha ujauzito. Wanawake walio katika awamu ya kimsingi ya utunzaji katika ujauzito, ulioelezwa katika Kipindi cha 13, wanafaa kuhudumiwa kwa safari ya kwanza kabla ya majuma 16 ya ujauzito, na kwa safari ya pili kati ya majuma 20-24). Hakikisha kuwa kila mwanamke anajua dalili za hatari zinazotokea sana katika ujauzito zilizo na uwezekano mkubwa wa kutokea katika kila kipindi.

Jedwali 15.2 Dalili za hatari ambazo kila mwanamke mjamzito anafaa kujua.
Katika safari zote kabla ya majuma 20Safari zote baada ya majuma 20

Kutapika mara kwa mara

Kutokwa na damu ukeni

Hakuna mabadiliko katika ukuaji wa fumbatio

Joto jingi

Kutapika

Maumivu ya kichwa

Hisia ya kuungua kwa epigastrimu (tazama Mchoro 15.4)

Kiwaa

Kutokwa na damu ukeni

Kuvuja kwa kiowevu

Hakuna mabadiliko katika ukuaji wa fumbatio

Kutapika mara kwa mara

15.4 Kuwaeleza wanawake wajawazito kuhusu dalili za hatari

Unafaa kufahamu kuwa wanawake wajawazito wanayo majukumu mengi nyumbani, hasa mashambani na huenda wakawa wamejazwa na habari nyingi kuhusu ujauzito huu. Jedwali 15.2 linawasilisha mambo ambayo mama anastahili kujua kwanza, lakini kamwe usimweleleze kila kitu kwa wakati mmoja. Kumshauri mwanamke mjamzito kulingana na vipindi vya ujauzito ni mkakati unaofaa kutokana na mtazamo wa uelewaji wa mwanamke huyo na utumiaji wa muda wako ifaavyo. Yaani, unafaa kujadiliana naye dalili za hatari zinazotokea sana, kwa kuzingatia kipindi cha ujauzito. Kwa mfano, mwanamke anayekuja kwa ajili ya utunzaji katika ujauzito kabla ya umri wa majuma 20 ya ujauzito anafaa kushauriwa kuhusu dalili za hatari za kuharibika kwa ujauzito zinazojitokeza kwa kutoka kwa damu ukeni. Pia anafaa kujua dalili za hatari za matatizo ya kiafya yanayotokea sana yanayoweza kutokea wakati wowote katika ujauzito - kama vile yanavyoweza kutokea kwa mtu yeyote.

Matatizo mengi makali yanayohusiana na ujauzito hutokea katika trimesta ya tatu. Kwa hivyo, ni wakati mzuri wa kumshauri mama kuyahusu katika trimesta ya pili ili kumpa muda wa kujiandaa mapema. Unaweza kutumia maagizo yaliyochapishwa, michoro, picha ukiwa nazo, kwani zinaweza kumsaidia kuelewa na kuongeza uwezo wake wa kukumbuka mambo muhimu. Hii ni njia bora ya kumkumbusha kuhusu mlichojadili katika safari za utunzaji katika ujauzito hapo awali (tazama Jedwali 15.3).

Kisanduku 15.3 Kufuatilia ujumbe wa ushauri wa awali

Katika safari zitakazofuata za huduma ya ujauzitoni, kumsaidia mwanamke kupitia mliyoyajadili awali kutakusaidia:

  • Kutambua alivyoelewa swala hili
  • Kutambua anayoweza kukumbuka kwa usahihi
  • Kujua ikiwa amekubali na yuko tayari kutumia maarifa hayo
  • Kujua sehemu alizoelewa vibaya

Pia, kutamsaidia kueleza shaka na hofu alizonazo, ili muweze:

  • Kujadili maswala yoyote ambayo hayakueleweka au kupokelewa vyema
  • Kupanga kwa pamoja mtakachofanya, kwa kumhusisha mume/mwenziwe.

15.5 Umuhimu wa kumhusisha mume/mwenzi katika ushauri wa ujauzitoni

Matatizo mengi yanayohusiana na ujauzito hayawezi kutabirika na hutokea baadaye. Kwa upande mwingine, ufahamu wa wana nchi kuhusu hatari za kiafya kwa mama na fetasi zinazohusiana na ujauzito ni mdogo sana. Chini mwa Sahara, mume au mwenzi wa kiume huwa na ushawishi mkubwa, uwezo wa kiuchumi na kukubalika kijamii kuliko mwanamke. Kuwashauri wanawake wajawazito wengi iwezekanavyo ni njia moja ya kuufikia umma kwa kumhusisha mumewe ambaye anaweza kuwa ajenti wa pili kwa usambazaji wa hatari zinazoweza kutokea katika ujauzito kwa umma.

Kwa hivyo, kumhusisha mume/mwenzi katika safari za utunzaji katika ujauzito kuna manufaa mengi (Kisanduku 15.4).

Kisanduku 15.4 Kumhusisha mume/ mwenzi katika safari za huduma katika ujauzito

  • Humsaidia mwenzi/mume kujua dalili za hatari ambazo mwanamke anaweza kupata katika ujauzito.
  • Kutamfanya awe mwenye kujali zaidi na kujihusisha.
  • Humsaidia kuchukua hatua (kuripoti mapema) dalili za hatari zinapotokea.
  • Hummakinisha kuweka akiba ya pesa kwa uwezekano wa dharura, kwa mfano kumsafirisha hadi kwenye kituo cha afya.
  • Huimakinisha familia kuamua pahali wanapopendelea pa kuzalia.
  • Huisaidia familia kujiandaa kumtunza mama na mtoto wake baada ya kuzaa.
  • Ni hatua zaidi ya kuongeza ufahamu wa wana nchi kuhusu hatari zinazoweza kutokea katika ujauzito.

15.6 Orodha ya kukagulia baada ya kila kipindi cha ushauri katika ujauzito

Mwisho, tunatamatisha kipindi hiki kwa orodha ya kukagulia unayoweza kutumia kutathmini ujuzi na mitazamo yako ya utoaji ushauri (Jedwali 15.3). Imechukuliwa ili kutumika katika kuwashauri wanawake wajawazito, bali inashirikisha kanuni za kijumla za kutoa ushauri unazoweza kutumia kwa mteja yeyote aliye chini ya utunzaji wako wa kiafya.

Jedwali 15.3 Oroaha ya kukagulia ya ‘KUSANYA’ ujuzi wa kutoa ushauri (imerekebishwa kwa wanawake wajawazito).
SalimuJe:

Ulimkaribisha kila mwanamke mjamzito alipowasili?

Mlijadiliana mahali penye starehe na faraghani?

Ulimhakikishia mwanamke mjamzito usiri wa mtakayo ya zungumza?

Ulionyesha kujali na kumpokea kwa maneno na ishara katika mkutano?

Ulieleza cha kutarajiwa?

UlizaJe:

Ulimwuliza mwanamke huyo mjamzito sababu ya safari hii?

Ulimhimiza mwanamke huyo mjamzito kuongea theluthi mbili za maongezi?

Uliuliza maswali ‘wazi’ kwa wingi?

Ulimakinikia yaliyosemwa na mteja huyo na jinsi yalivyosemwa?

Ulijiweka katika nafasi ya mwanamke huyo — ukionyesha kuelewa aliyoyasema bila kumkosoa vikali wala kumhukumu?

Uliuliza anavyohisi?

Uliuliza kuhusu mapendeleo yake?

Je:

Ulianza majadiliano kwa kuzingatia mapendeleo ya mwanamke mjamzito?

Ulijadili dalili za hatari za ujauzito kulingana na umri wa ujauzito?

Ulitoa habari kuhusu dalili za hatari za ujauzito ili kumsaidia kufanya uamuzi wake mwenyewe?

Uliepuka kumpa habari nyingi zaidi kwa wakati mmoja?

Ulitumia maneno anayoweza kuelewa?

Ulijadili umuhimu wa kuripoti mapema ikiwa atakumbana na dalili za hatari katika ujauzito?

UsaidiziJe:

Ulimjulisha kuwa uamuzi ni wake?

Uliwasaidia wanawake wajawazito kuweza kutambua dalili za hatari zinazotokea sana?

Ulimsaidia kuweza kuwazia athari kwa maisha yake na ya mtoto wake?

Uliwashauri wanawake wajawazito bila kuwakandamiza wala kuwavunja moyo?

Ulimuacha mwanamke huyo mjamzito kufanya uamuzi?

Ulihakikisha kuwa uamuzi wa wanawake wajawazito unatokana na kuelewa vyema?

Uliorodhesha sababu zozote za kiafya, kijamii, kitamaduni na kidini kwa kufanya uamuzi tofauti – labda tofauti na ambayo ungependa kutimiza?

ElezaJe:

Ulitoa alichohitaji mteja huyo ikiwa hakuna sababu ya kiafya ya kutofanya hivyo?

Ulieleza wakati mwanamke huyo anafaa kukutembelea mojawapo ya dalili za hatari ikitokea?

Ulimsaidia kueleza kwa maneno yake jinsi anavyoelewa kila dalili ya hatari katika ujauzito?

Ulieleza kwa kutumia maagizo yaliyochapishwa, picha na michoro?

KurudiJe:

Mlipanga wakati wa safari itakayofuata?

Ulijadili na mwanamke huyo mjamzito kuwa anaweza kurudi na mumewe au mwenziwe?

Ulimhakikishia mwanamke huyo mjamzito kuwa anapaswa kurudi wakati wowote, kwa sababu yoyote?

Ulimhakikishia arudi karibuni hata ikiwa alikosa kuja siku aliyoratibiwa kwa sababu asizoweza kuepuka?

Ulimhakikishia kuwa ni haki yake kamili kwenda katika kituo chochote kingine cha afya wakati wowote?

Ulimshukuru mwanamke huyo mjamzito kwa kutembelea huduma ya utunzaji katika ujauzito?

Muhtasari wa Kipindi cha 15

Katika Kipindi cha 15 umesoma kuwa:

  1. Utoaji wa ushauri ni mchakato wa siri wa njia mbili za mawasiliano kati ya watu wawili unaowasaidia wanawake wajawazito kuchunguza maswala yao ya kibinafsi, kufanya uamuzi na kupanga jinsi ya kuchukua hatua ikiwa watapata dalili za hatari.
  2. Ujuzi wa kimsingi katika utoaji wa ushauri ni kusikiza kwa makini, kumhimiza mwanamke mjamzito kuongea, kuuliza maswali kwa uwazi na kumakinikia maswala husika yanayohusiana na dalili za hatari na umri wa ujauzito.
  3. Kila mwanamke mjamzito ana haki ya kuamua kitakachotendeka kwa ujauzito wake.
  4. Habari yote ambayo mwanamke mjamzito atatoa wakati wa majadiliao inafaa kuwekwa siri.
  5. Makosa ya kawaida katika utoaji wa ushauri ni kumkatiza mwanamke anapozungumza, kutazama kando mara kwa mara, kukosoa vikali maadili ya tamaduni na dini yake, kummalizia sentensi na kumhukumu.
  6. Mchakato wa utoaji ushauri hupitia awamu hizi: kufungua na kujenga uhusiano, kuchunguza maswala, kufanikisha mabadiliko, na kufunga.
  7. Mwanamke mjamzito anafaa kushauriwa kuja kwako mara moja ikiwa atapata mojawapo ya dalili hizi:
    • Kwa kawaida nusu ya kwanza ya muda wa ujauzito: kutapika mfululizo, kupoteza uzani, kutokwa na damu ukeni, na kukosa mabadiliko katika ukuaji wa fumbatio.
    • Kwa kawaida katika nusu ya pili ya muda wa ujauzito: maumivu ya kichwa, kiwaa, hisia ya kuungua kwa epigastriamu, kutokwa na damu ukeni, kuvuja kiowevu ukeni kukosa mabadiliko katika ukuaji wa fumbatio kupungua au kukosa kusonga kwa fetasi.
    • Wakati wowote katika ujauzito: joto jingi, kutapika, uchungu kwenye mwanya wa fupanyonga, macho kuwa manjano au kukohoa kulikodumu.
  8. Kumhusisha mume au mwenzi katika safari za utunzaji katika ujauzito huufanya utunzaji wa mwanamke mjamzito kuwa swala na jukumu la familia na pia huwasaidia kuwa macho kwa dalili za hatari zinazohitaji hatua ya haraka.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 15

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyoafikia Malengo yake ya Mafunzo kwa kujibu maswali yafuatayo. Andika majibu kwenye shajara yako na kuyajadili na mkufunzi wako katika mkutano utakaofuata wa masomo. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari kuhusu Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la kujitathmini 15.1 (linatathmini Malengo ya Somo 15.1 na 15.2)

Kwa kila kauli, onyesha ikiwa ni kweli au la. Eleza kisicho sahihi kwa kauli yoyote ambayo si kweli.

  • A.Kusema karibu, kutabasamu, kumhimiza kueleza wasiwasi na shaka alizo nazo humsaidia mama kutulia na kuwa na imani nawe.
  • B.Lazima umweleze kuwa asipokuja siku aliyoratibiwa, hutamhudumia wakati mwingine wowote.
  • C.Usimruhusu kuuliza maswali hadi utakapomaliza kumweleza anachofaa kujua.
  • D.Unaweza kumshauri mwanamke mmoja aliyekaa nawe huku ukiendelea kumfanyia yule mwingine uchunguzi.
  • E.Akikuambia kuwa binti zake wawili walipashwa tohara siku alipo zalia nyumbani, mwambie kwa ukali kuwa asifanye hivyo tena na ikiwa anapanga kurudia hayo kwa mtoto huyu iwapo ni wa kike, asirudi tena kwa safari zingine zozote.
  • F.Kumshauri mwanamke mjamzito kuhusu dalili za hatari ni muhimu katika kila safari.
Answer

A ni kweli. Kumkaribisha mama, kutabasamu na kumhimiza kueleza wasiwasi na shaka alizonazo humsaidia kutulia na kuwa na imani nawe.

B si kweli. Si jambo rahisi kwa wengi wa wanawake wajawazito chini mwa Sahara kuja siku waliyoratibiwa, hasa kutokana na majukumu yao mengi ya kibinafsi na ya kijamii. Ni haki yao kuja kabla au baada ya siku waliyoratibiwa, au hata wasije kabisa. Ni wajibu na jukumu la mtaalam yeyote wa afya kuwakaribisha kwa mkono mkunjufu siku au wakati wowote ule watakapokuja kwa uchunguzi.

C si kweli. Huduma ya afya kimsingi ni haki ya mteja/mgonjwa. Wajibu wa wataalam wa afya ni kutoa huduma ya kumtuliza na kumridhisha. Kwa hayo, unafaa kujitayarisha kuulizwa maswali na kufanya juhudi kuwahimiza wanawake kuuliza maswali wasiyoelewa.

D si kweli. Kwa kanuni zake, utoaji ushauri ni kujadili maswala ya kibinafsi ambayo mteja hatapendelea yakijadiliwa na yeyote nje ya familia. Kwa hivyo, hata ukiwa na haraka, si vyema kumshauri mwanamke mmoja huku ukimchunguza mwingine. Katika mazingira kama hayo, anayeshauriwa hataweza kueleza hisia na wasiwasi wake kwa uwazi kwako.

E si kweli. Huwezi kuhimiza mabadiliko ya kitabia kwa watu wazima kwa kukosoa vikali, kuwapinga, kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa wazi wazi. Mwanamke huyu hatahisi kuheshimiwa na huenda asirudi kwa huduma zaidi ya utunzaji katika ujauzito. Ili kuleta mabadiliko bora kwa mienendo duni, mbinu bora zaidi kwa watu wazima ni majadiliano ya wazi ukiwajuza hatari/hasara na kuwapa fursa ya kukadiria chaguzi walizonazo wenyewe na kufanya uamuzi wao.

F ni kweli. Katika kila safari ya huduma katika ujauzito, wanawake wajawazito wanafaa kupewa ushauri kuhusu dalili za hatari katika ujauzito ili waweze kuchukua hatua ya haraka kunapotokea dharura.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 15.2 (linatathmini Lengo la Somo 15.3)

Kutokana na uliyosoma katika Jedwali 15.1, linganisha kila dalili ya hatari na hali mwafaka ya kiafya.

Using the following two lists, match each numbered item with the correct letter.

  1. Kuvuja kwa kiowevu ukeni

  2. Kutokwa na damu ukeni

  3. Joto jingi

  4. Kupungua kwa ukubwa wa fumbatio

  5. Maumivu kwenye fupanyonga

  6. Maumivu ya kichwa yanayodumu

  • a.Utokaji potelelevu

  • b.Pielonefritisi kali

  • c.Malaria

  • d.Upasukaji wa mapema wa membreni

  • e.Hipatensheni

  • f.Kutokwa na damu kabla ya kuzaa

The correct answers are:
  • 1 = d
  • 2 = f
  • 3 = c
  • 4 = a
  • 5 = b
  • 6 = e

Swali la kujitathmini 15.3 (linatathmini Lengo la Somo 15.4)

Kwa kila kauli, eleza ikiwa ni kweli au la. Eleza kisicho sahihi kuhusu kila kauli isiyo kweli.

  • A.Mshauri anastahili kumweleza mwanamke mjamzito kuhusu dalili zote za hatari za ujauzito katika safari yake ya kwanza ya utunzaji katika ujauzito kabla ya majuma 16 ya ujauzito.
  • B.Kumhimiza mwanamke mjamzito kurudia yaliyojadiliwa katika ushauri kutaongeza kumbukumbu yake (uwezo wa kuendeleza kuwepo) ya hoja muhimu.
Answer

A sikweli. Kipengele wanachohitaji kushauriwa kukihusu kinafaa kulingana na umri wa ujauzito kwa sababu:

  • Matatizo tofauti yanayohusiana na ujauzito hutokea katika vipindi tofauti vya ujauzito.
  • Si rahisi kwa wateja kuelewa na kuhifathi habari nyingi hasa isipokuwa muhimu kwao wakati huo.
  • Kuongea kuhusu dalili zote za hatari katika safari moja kutachukua wakati wako mwingi.
  • Habari nyingi zaidi kuhusu hatari inayoweza kutisha inaweza kuwazidi wateja na kuwazuia kuuliza maswali yao na ufafanuzi.

B ni kweli. Kurudia yaliyojadiliwa/yaliyosemwa kutasaidia:

  • Mwanamke mjamzito kukumbuka alichosikia.
  • Mhudumu wa afya kuchunguza kiwango cha kuelewa cha mwanamke huyo.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 15.4 (linatathmini Lengo la Somo 15.5)

Orodhesha manufaa ya kumhusisha mume/mwenzi katika ushauri wa kabla ya kuzaa kuhusu dalili za hatari.

Answer
  • Kumshauri mume/mwenzi kuhusu dalili za hatari katika safari za huduma ya utunzaji katika ujauzito inamaanisha kuwa hata yeye anaweza kuzimakinikia na kutafuta usaidizi wa haraka wakati wa dharura.
  • Kuwahusisha waume/wenzi ni njia moja ya kujulisha wana nchi kwa upana kuhusu hatari zinazoweza kuwakumba wanawake na watoto katika ujauzito.
  • Ikiwa mume/mwenzi atajua dalili zinazoweza kutokea katika ujauzito, anaweza kujali zaidi na kuhusika kwa kumtunza mkewe.
  • Ana uwezekano mkubwa wa kukubali kumpeleka mkewe mjamzito kwa mhudumu wa afya ikiwa dalili za hatari zitaibuka.
  • Kumshauri mume/mwenzi kutamuwezesha kujiandaa kisaikolojia na kifedha kukabiliana na dharura zinazohusiana na ujauzito.

Mwisho wa jibu

Maswali ya kujitathmini 15.5 (yanatathmini Malengo ya Somo 15.1 hadi 15.5)

Soma kwanza Uchunguzi Maalum 15.1 kwa makini kisha ujibu maswali yanayofuata.

Uchunguzi maalum 15.1 Kisa cha Bi. H

Bi. H ni mwanamke mwenye umri wa miaka 25 aliye katika ujauzito wa pili na alimtembelea mhudumu wa afya nje ya hospitali kwa mara ya kwanza baada ya majuma 34 ya ujauzito. Mhudumu huyo wa afya aliuliza mahali alikozalia awali. Shinikizo la damu na uzani vilipimwa na afya yake ilionekana kuwani njema; fumbatio lake lilichunguzwa na ujauzito kuonekana kuendelea kikawaida. Mwisho, aliagizwa kurudi baada ya majuma 3.

Majuma mawili baadaye, alianza kuvuja kiowevu cha majimaji ukeni. Aliwajulisha jirani zake na wakamwambia asihofu. Kwa kuwa kiliendelea kuvuja, siku ya tatu baada ya kuanza kuvuja, alimrudia mhudumu huyo wa afya na kupata ushauri huo huo alioupata nyumbani. Siku ya tano, alipata joto jingi sana (sentigredi 39) na kiowevu kinachonuka kutoka ukeni.

  • a.Je, nini kibaya na safari ya huduma ya utunzaji katika ujauzito baada ya majuma 34 ya ujauzito kwa mtazamo wa kumshauri mwanamke mjamzito ipasavyo?
  • b.Je, kwa nini Bi. H alivuja kiowevu ukeni?
  • c.Je, kwa nini alingoja siku tatu kabla ya kuripoti kwa mhudumu wa afya nje ya hospitali baada ya kuanza kuvuja?
  • d.Je, nini ambacho kingefanywa na mhudumu wa afya nje ya hospitali Bi. H alipowasili akivuja kiowevu ukeni?
  • e.Je, kwa nini Bi. H alipata kiwango cha juu sana cha joto na kiowevu kinachonuka ukeni?
Answer
  • a.Bi. H hakushauriwa kuhusu dalili za hatari za ujauzito katika umri wa majuma 34 ya ujauzito. Alipokuwa na wasiwasi kuhusu dalili alizokuwa nazo aliomba ushauri kutoka kwa majirani. Walifikiri (bila usahihi) kuwa kuvuja kiowevu cha majimaji ukeni katika juma la 36 ilikuwa ni kawaida kuliko matatizo mabaya yanayohusiana na ujauzito.
  • b.Kiowevu cha majimaji kilivuja kutokana na kupasuka kwa mapema kwa membreni za fetasi ambazo ndizo kifuko kinachoweka fetasi na kiowevu cha amnioni. Kwa hivyo ni kiowevu cha amnioni kilichokuwa kikivuja kupitia membreni zilizopasuka.
  • c.Alingoja siku kadhaa kabla ya kutafuta usaidizi kwa sababu hakujua kuwa kuvuja kwa kiowevu ni dalili ya hatari ya kupasuka kwa mapema kwa membreni na majirani walimhakikishia kuwa si tatizo.
  • d.Mhudumu wa afya nje ya hospitali angempa rufaa aende katika kituo cha afya au hospitali kwa uchunguzi na matibabu.
  • e.Bi. H alipata kiwango cha juu sana cha joto na mchozo unaonuka kutoka ukeni kwa sababu maambukizi yaliweza kupanda ukeni hadi kwenye uterasi baada ya kupasuka kwa membreni.

Mwisho wa jibu.