Skip to main content
Printable page generated Tuesday, 3 Aug 2021, 14:07
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Tuesday, 3 Aug 2021, 14:07

19. Magonjwa ya Kihipatensheni ya Ujauzito

Kipindi cha 19 Magonjwa ya Kihipatensheni ya Ujauzito

Utangulizi

Magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito ni mojawapo ya visababishi vitatu vikuu vya maradhi na vifo (pamoja na kutokwa na damu, na maambukizi) kwa kina mama. Mchango wa hipatensheni (shinikizo la juu la damu) kwa vifo na maradhi ya fetasi na watoto wachanga pia ni mkubwa. Magonjwa ya kihipatensheni yanaweza kutatiza hadi asilimia 10 ya ujauzito wote, huku kiwango kikubwa zaidi cha asilimia hiyo kikitokea katika wanawake walio na ujauzito wa kwanza (primigravida). Hipatensheni hufafanuliwa kama shinikizo la damu zaidi ya 140/90mmHg, ambapo nambari ya juu ndiyo shinikizo la sistoli na nambari ya chini ndiyo shinikizo la diastoli.

Shinikizo la damu hupimwa kwa milimita za zebaki (mmHg)kwa sababu vifaa vya kwanza vilikuwa na zebaki.

 • Je, unakumbuka kinachomaanishwa na shinikizo la sistoli na la diastoli?

 • Shinikizo la sistoli ni shinikizo la damu katika mishipa ya damu moyo unaponywea. Shinikizo la diastoli hupimwa moyo unapolegea katikati ya mipigo.

  Mwisho wa jibu

Jukumu kuu la huduma yako ya utunzaji katika ujauzito ni kuwafahamisha wanawake wajawazito kuhusu dalili za hatari za magonjwa ya kihipatensheni, kuchunguza shinikizo lao la damu katika kila safari (ulijifunza jinsi ya kufanya hivi katika Kipindi cha 9), na kufanya utambuzi wa hipatensheni kwa wakati unaofaa na kuwapa rufaa wanawake walioathiriwa mapema iwezekanavyo.

Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu mabadiliko katika mwili wa mwanamke kutokana na hipatensheni na jinsi yanavyoathiri mama na fetasi, uainishaji wa hipatensheni, visababishi vikuu, jinsi ya kutambua aina tofauti, na hatua utakazochukua ili kuzuia matatizo yanayokithiri na hata kifo.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 19

Baada ya kusoma somo hili, unapaswa uweze:

19.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliochapishwa kwa herufi nzito. (Maswali ya Kujitathmini 19.1, 19.2 na 19.3)

19.2 Kueleza kwa kifupi kinachotendeka kwenye mishipa ya damu na viowevu vya mwili kwa wanawake walio na hipatensheni, na jinsi kinavyoweza kuidhuru fetasi. (Maswali ya Kujitathmini 19.1 na 19.2)

19.3 Kufafanua aina tofauti za magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito. (Maswali ya Kujitathmini 19.2 na 19.3)

19.4 Kuorodhesha visababishi vikuu vya hipatensheni inayohusiana na ujauzito. (Swali la Kujitathmini 19.3)

19.5 Kueleza dalili za kiafya zinazotokea sana za priklampsia kali. (Swali la Kujitathmini 19.3)

19.6 Kutambua matatizo yanayotokea sana ya magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito kwa mama na fetasi/mtoto mchanga. (Swali la Kujitathmini 19.3)

19.7 Kutoa matibabu saidizi ya kimsingi na kuwezesharufaa ya mapema, hasa kwa wanawake walio na magonjwa makali ya kihipatensheni ya ujauzito. (Swali la Kujitathmini 19.3)

19.1 Je, hipatensheni huathiri vipi ujauzito?

Kisababishi hasa cha hipatensheni inayohusiana na ujauzito bado hakijulikani. Hata hivyo, hipatensheni inajulikana kusababisha magonjwa katika sehemu tofauti za mwili; hasa huathiri ubongo na uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu, damu, figo, na ini.

19.1.1 Athari kwa mishipa ya damu na viowevu vya mwili

Tukio linalojulikana sana kwa mwanamke anayepata hipatensheni katika ujauzito ni kuwa kuta za misuli za mishipa ya damu mwilini mwote hunywea, na kwa hivyo nafasi ndani ya mishipa hupungua. (Jina maalum la hali hii ni msongo wa mishipa kote mwilini.) Msongo huu wa mishipa husababisha shinikizo la juu la damu katika mishipa ya damu, na hii ni sababu moja ya kiowevu kutoka kwa damu kusukumwa nje kupitia kuta za mishipa na kukusanyika kwenye tishu za mwanamke huyo.

 • Je, uvimbe unaotokana na kukusanyika kwa kiowevu kwenye tishu huitwaje, na ni wapi ambapo uvimbe unaoneka sana kwa wanawake wajawazito walio na hipatensheni? (Ulijifunza kuhusu haya katika Kipindi cha 7 na cha 8, hasa Kisanduku 8.2.)

 • Uvimbe huu huitwa edema na ni ishara ya hatari ya hipatensheni katika ujauzito. Huonekana mara nyingi katika sehemu ya chini ya miguu, vifundo na nyayo; pia mikono, na kwenye uso na mgongo katika hali kali sana.

  Mwisho wa jibu

19.1.2 Athari za hipatensheni ya mama kwa fetasi

Aina yoyote ya hipatensheni katika ujauzito ina athari kubwa kwa ukuaji na kuishi kwa fetasi. Hii hutendeka kutokana na kupungua kwa kiasi cha damu ya mama, jambo ambalo baadaye hupunguza uletaji wa damu kutoka kwa ateri za endometria hadi kwa plasenta. Ateri za endometria huleta damu ya mama kwa plasenta, na kuleta oksijeni kutoka kwa mapafu na virutubishi kutoka kwa mfumo wake wa umeng'enyaji hadi kwa fetasi. (Unaweza kuyaona ukitazama nyuma katika Mchoro 5.5 katika Kipindi cha 5.)

 • Je, ukuaji wa fetasi utaathiriwa vipi iwapo kiasi cha damu ya mama inayoingia kwenye plasenta kitapungua?

 • Upelekaji wa oksijeni, virutubishi, na viowevu kwenda kwa mtoto utapungua na kwa hivyo hatakua kikawaida. Ukuaji wa fetasi unaweza kuzuiliwa (hipatensheni katika ujauzito ni mojawapo ya visababishi vikuu vya uzuiaji wa ukuaji kwenye uterasi).

  Mwisho wa jibu.

Kiwango cha kiowevu cha amnioni kinachozunguka fetasi pia kitakuwa kidogo kuliko kawaida kwa sababu damu inayofika kwenye figo za mtoto imepungua na kwa hivyo hutengeneza kiasi kidogo cha mkojo. Mwishoni mwa ujauzito, kiasi kingi cha kiowevu cha amnioni hutoka kwa mkojo wa mtoto. Fetasi inaweza kufariki kutokana na ukosefu wa oksijeni na virutubishi, au kutokana na kupungua kwa kiowevu cha amnioni. Iwapo fetasi itaishi muda mrefu kwenye uterasi huku ikipata oksijeni kidogo, ubongo unaokua unaweza kuathiriwa vibaya sana. Kutokana na hayo, mtoto huyu anaweza kuwa punguani baadaye iwapo atazaliwa akiwa hai na kuongoka katika maisha ya mapema utotoni.

Pia fetasi inaweza kufariki kwa sababu plasenta huzeeka mapema sana na kusababisha usambazaji duni wa damu kwa fetasi, kwa hivyo plasenta inaweza kujitenga mapema na kuta za uterasi. (Mtengo wa mapema huitwa kuachia kwa plasenta na utajifunza kuuhusu katika Kipindi cha 21.) Leba ya mapema inaweza kuanza yenyewe (Kipindi cha 17) na maisha ya mama pia yanaweza kuwa hatarini kutokana na kuachia kwa plasenta ambapo damu nyingi inaweza kupotezwa.

19.1.3 Matatizo yanayotokea sana ya priklampsia kali kwa mama

Matatizo ya aina yoyote ya magonjwa ya kihipatensheni kwa mama yanahusiana sana na msongo wa mishipa na usambazaji tena wa viowevu vya mwili (viowevu zaidi nje ya mishipa ya damu na kidogo ndani ya mishipa). Tukio hili husababisha:

 • Kuletwa kwa kiasi kidogo cha damu kwenye ogani zake muhimu (ubongo, moyo) na ogani zisizo muhimu sana kwa kuishi kwa muda mfupi (figo, ufereji wa utumbo likiwemo ini, misuli ya skeletoni na ngozi).
 • Kiowevu kujikusanya kwenye ogani zake (ini, ubongo, kaviti ya fumbatio, macho, mapafu), ambazo huvimba na hata vinaweza kuraruka.
 • Mishipa ya damu miembamba au yenye msongo, inayochangia kuharibika kwa seli za damu, hasa pleteleti (muhimu kwa ugandaji wa damu kukiwa na mraruko au kidonda kwenye tishu), na seli nyekundu za damu.
 • Je, mwanamke atapata hali gani ya kiafya iwapo kiasi kikubwa cha seli nyekundu za damu yake kitaharibika?

 • Atapata anemia.

  Mwisho wa jibu.

19.1.4 Muhtasari wa matatizo ya mama na fetasi ya priklampsia kali

Jedwali 19.1 Matatizo ya priklampsia kali yanayotokea sana kwa mama na fetasi.
Matatizo kwa mamaMatatizo kwa fetasi
EklampsiaKuachia kwa plasenta
Kutokwa na damu ndani ya kichwa (kutoka damu ndani ya fuvu la kichwa)Asifiksia ya ndani ya uterasi (ukosefu mkubwa wa oksijeni kwenye uterasi)
AnemiaUzuiaji wa ukuaji ndani ya uterasi
Idadi ya chini ya pleteleti, ugandaji duni wa damu, na hatari ya kutokwa na damuKuzaa kabla ya muda kamili kutimia
Figo kutofanya kaziFetasi kufariki ndani ya uterasi
Ini kutofanya kazi, au hata kuraruka kwa iniUgumu katika kupumua baada ya kuzaliwa (asifiksia ya mapema ya mtoto mchanga)
Kiowevu kwenye mapafu (edema ya mapafu)Upunguani
Moyo kutofanya kazi
Upofu kamilifu wa muda

19.2 Uainishaji wa hipatensheni katika ujauzito

Hipatensheni katika ujauzito inaweza kuwa ya mara ya kwanza, au inayoendelea au inayozidi kukithiri iliyokuwepo kabla ya ujauzito huo. Iwapo hipatensheni itatambuliwa kabla ya ujauzito au katika majuma 20 ya kwanza ya ujauzito, au ikiendelea kwa majuma sita baada ya mtoto kuzaliwa, hii hufafanuliwa kama hipatensheni sugu.

'Sugu' hueleza hali ya kiafya inayoendelea kwa muda mrefu.

Sababu ya kuainisha hipatensheni katika ujauzito ni kukuwezesha kuamua hatua utakazochukua katika kila aina. Aina zingine (kwa mfano priklampsia ndogo na hipatensheni itokanayo na ujauzito - tazama Kisanduku 19.2 hapa chini) zina matatizo machache na yasiyo makali kwa mama na fetasi: aina zingine (kwa mfano, priklampsia kali na eklampsia) zinaweza kuwa na matatizo mabaya ila zidhibitiwe haraka.

19.2.1 Uainishaji wa prikilampsia

Priklampsia ndiyo aina ya magonjwa ya kihipatensheni inayotokea sana katika ujauzito na iliyoangaziwa sana katika majadiliano ya sehemu hii (tazama Jedwali 19.2 ). Hutokea katika nusu ya pili ya ujauzito (baada ya majuma 20 ya ujauzito, lakini hutokea sana baada ya majuma 28). Kuwepo kwa protini katika mkojo wa mwanamke (protinuria) ni ishara ya hatari. Protinuria nyingi hufafanuliwa kama kipimo chanya cha mkojo cha dipstick chenye matokeo zaidi ya au sawa na +2 kwenye kipimo cha dipstick hizo.

Jedwali 19.2 Sifa bainifu za aina za hipatensheni na priklampsia
AinaShinikizo la juu la damu (lililopimwa mara mbili, saa sita kati ya vipimo hivi)ProtinuriaDalili za ukali
Hipatensheni yaujauzito (hutokea katika ujauzito na kuisha baadaye)Zaidi ya kipimo cha 140/90 mmHgHakuna protinuria nyingiHakuna
Priklampsia ndogoKati ya 140/90 mmHg na 160/110 mmHgHakuna protinuria nyingiHakuna
Priklampsia kaliZaidi ya au sawa na 160/110 mmHgProtinuria inayoonekana iwepo au isiwepo (matokeo ya kipimo cha dipstick zaidi ya au sawa na +2)Maumivu ya kichwa, kiwaa, maumivu ya epigasriamu, kupungua kwa mkojo, kupungua au kutokuweko kwa kucheza kwa mtoto
Priklampsia zaidi juu ya iliyokuwepo awaliJuu kuliko kabla ya ujauzito kwa mwanamke aliye na hipatensheni suguProtinuria inayoonekana nyingi zaidi au inayozidi Kuwe au kusiwe na dalili za ukali

19.2.2 Dalili za kutambua eklampsia

Mchoro 19.1 Tukutiko ni ishara bainifu ya eklampsia katika ujauzito.

Eklampsia ndiyo aina kali sana ya magonjwa ya kihipatensheni. Utambuzi hufanyika mwanamke aliye na priklampsia (mara nyingi sana), au aina nyingine yoyote ya magonjwa ya kihipatensheni anapopata matukutiko (matukutiko, Mchoro 19.1) au koma (kupoteza fahamu kabisa). Tukutiko hili ni kama lile linalotokea kwa mtu aliye na kifafa (katika Kiamhari: Yemitil Beshita). Utajifunza mengi kuhusu aina hii ya tukutiko baadaye katika kipindi hiki.

19.3 Visababishi vya priklampsia/eklampsia

Katika hali nyingi, kutokea kwa priklampsia au eklampsia hakuwezi kutabirika na kisababishi hakijulikani. Hata hivyo, kuna visababishi vinavyojulikana kuhusiana na matatizo ya kihipatensheni ya ujauzito (Jedwali 19.1).

Kisanduku 19.1 Visababishi vya magonjwa ya kihipatensheni kwa wanawake wajawazito

 • Ujauzito wa mara ya kwanza kabla ya umri wa miaka 20 au baada ya miaka 35
 • Ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja (wawili au zaidi)
 • Historia ya priklampsia/ekilampsia katika familia kwa jamaa wa karibu
 • Historia ya priklampsia/eklampsia katika ujauzito wa hapo awali
 • Kisukari wakati huo
 • Unene wa kupindukia wakati huo (mwanamke ana uzani zaidi ukilinganishwa na urefu wake)
 • Ugonjwa wa figo wakati huo.

Kujua visababishi hivi kutakusaidia:

 • Kutarajia uwezekano wa kuwepo kwa magonjwa ya kihipatensheni na matatizo yake kabla hayajatokea.
 • Kutoa ushauri kwa mwanamke, mwenzi wake na familia kuhusu dalili za hatari za priklampsia/eklampsia kali ili waweze kuchukua hatua haraka ikihitajika.
 • Kufanya safari nyingi mwishoni mwa ujauzito kwa wanawake walio na visababishi hivi.

La muhimu pia ni kuwa unahitajika kujua ya kwamba mwanamke yeyote (bila kujali umri na idadi ya uzazi wa hapo awali) anaweza kupata magonjwa ya kihipatensheni katika ujauzito wowote. Kwa hivyo, ingawa ni vizuri kutarajia yatokee kwa wale walio na visababishi hivi, unaweza kuchukulia kuwa wanawake wote wajawazito wana uwezekano wa kupata hipatensheni.

19.4 Dalili za kiafya za priklampsia kali

Jinsi ulivyoona kaika Jedwali 19.2, priklampsia ndogo ni matokeo yanayoambatana na shinikizo la juu la damu kwa mwanamke asiye na dalili zingine za kihipatensheni. Hata hivyo, mwanamke aliye na priklampsia kali anaweza kuwa na lalamiko moja au zaidi ya dalili kali. Kutokana na maoni na masomo ya utafiti, hizi ndizo dalili za kiafya zinazotokea sana.

19.4.1 Maumivu ya kichwa

Ingawa kuna visababishi vingi vya maumivu ya kichwa katika ujauzito, hadi itakapothibitishwa kinyume, unapaswa kuchukulia kwanza kuwa maumivu ya kichwa yanaweza kutokana na aina kali ya hipatensheni. Edema ya ubongo (uvimbe kutokana na kiowevu kujikusanya ubongoni) na ongezeko la shinikizo ndani ya fuvu la kichwa (jina la kitiba la fuvu la kichwa ni kreniamu, kwa hivyo, madaktari huliita shinkizo la ndani ya kreniamu) ndivyo visababishi vikuu vya maumivu ya kichwa katika priklampsia kali.

19.4.2 Kiwaa/matatizo ya kuona

Kiwaa na matatizo ya kuona pia hutokana na ongezeko la shinikizo ndani ya kreniamu, pamoja na edema ubongoni na kwenye retina (kiungo kilicho nyuma ya mboni ya jicho).

19.4.3 Maumivu ya epigastriamu

Edema kwenye ini inaweza kuwa na maumivu sana kwa sababu ini limefunikwa na kapsuli ambayo hukaza na kuuma ini linapokusanya kiowevu kingi sana kwenye tishu zake. Ini liko nyuma ya sehemu ya epigastriamu ya fumbatio uliyojifunza kutambua katika Kipindi cha 15 (tazama Mchoro 15.4). Visababishi vingine vya maumivu ya epigastriamu ni nadra katika ujauzito, kwa hivyo ujumbe ni: kwanza fikiria hipatensheni kwa mwanamke mjamzito (hasa baada ya majuma 28 ya ujauzito) anayelalamikia maumivu ya epigastriamu.

19.4.4 Kupungua kwa mkojo

Kutolewa kwa mkojo hupunguka kwa kiwango kikubwa katika aina kali za hipatensheni inayohusiana na ujauzito. Kupungua kwa kiasi cha damu ya mama (kilichoelezewa katika Sehemu ya 19.1.1) hupelekea kupungua kwa damu inayofika kwenye figo na kutokana na haya, kutakuwa na upungufu mkubwa katika mkojo unaotolewa. Mwanamke huyo anaweza kukoma kutoa mkojo kabisa.

19.4.5 Kupungua au kutokuwepo kwa kucheza kwa fetasi

Hii hutendeka kwa sababu fetasi inapokea oksijeni na virutubishi kidogo kutokana na kupungua kwa damu inayopita kwenye plasenta, jinsi ilivyoelezwa hapo juu.

19.4.6 Edema ya mwili wote (ya patholojia)

Edema ya mwili wote hujulikana kwa kuenea kwa edema kwa mgongo, fumbatio, mikono na uso wa mwanamke. Edema huchukuliwa kuwa ya patholojia ikiwa mama anaongeza uzani wa zaidi ya kilo 1.0 kwa juma. Ongezeko la kawaida la uzani kwa juma katika ujauzito ni kati ya kilo 0.25 hadi 0.75 (wastani kilo 0.5).

19.5 Dalili za kiafya za eklampsia

Ekilampsia hutokea mwanamke akikosa matibabu bora akiwa na priklampsia kali. Hili ndilo tatizo hatari sana la priklampsia kali. Inaweza kutokea kabla ya leba, katika leba na baada ya kuzaa. Wakati mwingine eklampsia inaweza kutokea kwa muda wa hadi saa 24 baada ya kuzaa, hata kwa wanawake waliozaa wakiwa na shinikizo la damu la kawaida na bila dalili zozote za hatari kabla na katika leba. Kwa hivyo mwanamke akija kwako na historia ya tukutiko baada ya leba na kuzaa kikawaida na hata wakati mwingine nyumbani, tatizo la kwanza la kiafya unalofaa kuzingatia ni eklampsia. Lakini unapaswa pia kujua kuwa kuna visababishi vingine vya tukutiko, kama vile kiwango cha chini au juu sana cha sukari katika damu (hipo au hipaglisimia), malaria yanayoathiri ubongo, maambukizi ya bakteria kwenye ubongo (kwa mfano meninjitisi), kiharusi, madawa, au kusumishwa.

Jinsi ulivyojifunza hapo juu, utambuzi wa eklampsia hufanywa dalili za kiafya za priklampsia zikiwepo, pamoja na:

 • Tukutiko
 • Koma bila ya visababishi vingine.

Tukutiko katika eklampsia huwa la ghafla mwanzoni lakini katika visa vingine huenda kukawa na ishara na dalili za hatari zinazothibitisha kutokea kwa eklampsia (tazama Kisanduku 19.2).

Kisanduku 19.2 Ishara na dalili za hatari zinazoonyesha kuwa eklampsia inatokea

 • Maumivu yasiyodhibitiwa kwa urahisi/makali ya kichwa
 • Maumivu makali ya epigastriamu
 • Kiwaa au kutoona kabisa (kwa muda)
 • Uchovu au kuwashwa
 • Kutotambua wakati (saa), watu, na mahali katika mazingira yake
 • Kutofahamu mazingira
 • Kuonyesha tabia zisizo za kawaida.

19.5.1 Matukutiko katika eklampsia

Tukutiko katika eklampsia ni sawa na tukutiko kwa watu walio na kifafa. Kama tukutiko la kifafa, lina awamu nne:

Awamu ya utulivu

Sifa bainifu ya awamu ya kwanza ni kipindi cha utulivu (huenda kisichukue zaidi ya sekude 20) mtu anapokuwa na udhaifu wa misuli kwenye mwili wote, mkazo na mshtuko wa misuli, na macho yanayokodoa.

Awamu ya toni

Hii inaweza kudumu hadi sekunde 30 na huonyeshwa kwa aina kali ya mikazo ya misuli kwenye mwili wote ambapo misuli ya miguu na mikono hunywea sana na hata kuonekana thabiti kama kijiti kikavu. Katika awamu ya toni, mwanamke hukoma kupumua na kukosa oksijeni. Pia kuna kugeuzageuza macho na unaweza kuona sehemu ya juu ya sklera (sehemu nyeupe ya jicho).

Awamu ya kiklonasi

Awamu ya tatu inaweza kuchukua hadi dakika 2 na hasa ni mwendo wa mshtuko wa mwili wote kutokana na kunywea na kulegea kwa misuli. Katika awamu hii mwanamke anaweza kupumua na pia kutoa mate na mkojo.

Kipindi cha koma

Baada ya awamu ya kiklonasi, katika kisa dhahiri, mwanamke hupoteza fahamu kabisa kwa muda usiojulikana. Hata hivyo, mwanamke huyo anaweza kwenda katika koma mwanzoni kabisa (yaani, bila tukutiko hata moja). Muda wa hali ya koma hutegemea:

 • Idadi ya matukutiko ya hapo awali: Idadi ya matukutiko inavyokuwa kubwa ndivyo muda wa koma unavyokuwa mrefu, ambao hata unaweza kusababisha kifo. Kuwa na historia ya zaidi ya matukutiko kumi ni mojawapo ya ishara ya matokeo mabaya. Kwa hivyo, tukutiko linapodhibitiwa mapema ndivyo matokeo yatakavyokuwa bora kwa mama na mtoto.
 • Ukali wa edema ya ubongo: Nafasi kati ya fuvu la kichwa na ubongo ni ndogo sana. Kwa hivyo, hata ongezeko dogo kwa ukubwa wa ubongo wa mama kutokana na edema au kutokwa na damu litakuwa na athari kwa seli za ubongo kwa sababu shinikizo kwenye ubongo (shinikizo ndani ya kichwa) huongezeka sana.
 • Kiasi cha kutokwa na damu ndani ya kichwa (tazama hapa chini katika kipindi hiki): Jinsi ilivyoelezwa kuhusu edema ya ubongo, kutokwa na damu kwenye nafasi ndani ya kichwa kutaongeza shinikizo la ndani ya kichwa kwenye seli za ubongo. Pia, inaweza kusababisha kutoka zaidi kwa damu na kuweza kuleta mzunguko wa hali hii tena na tena.
 • Hipoglisimiahusika (kiwango cha chini cha sukari kwa damu): Kila tukutiko huhitaji nguvu. Hii ni kwa sababu karibu misuli yote ya skeletoni hunywea na kulegea mara mingi katika awamu za toni na kiklonasi. Matukutiko ya mara kwa mara humaanisha kutumika kwa nguvu nyingi, inayotoka kwenye sukari katika damu, ini na tishu. Mwanamke aliye na eklampsia hawezi kurudisha sukari iliyotumiwa na misuli haraka ifaavyo na kwa hivyo hukumbwa na kiwango cha chini cha sukari kwenye damu (hipoglisimia kali) ambayo baadaye hujionyesha kwa koma. Kwa kuwa kiwango chake cha sukari kwenye damu kiko chini, mwanamke aliye na eklampsia atapata nguvu kutoka kwa protini kwenye misuli yake kila wakati ili kumweka uhai. Usagaji wa protini hutoa ketoni ambazo zinaweza kutumika kama chanzo cha nguvu na zingine zitaonekana kwenye mkojo wake. Unaweza kupima kuwepo kwa ketoni kwa dipstick.

19.6 Je, unaweza kufanya nini ukitambua ugonjwa wa kihipatensheni kwa mwanamke mjamzito?

Jukumu la kwanza katika udhibiti wa magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito ni utambuzi wa mapema wa ishara na dalili za hatari na utoaji wa mara moja wa rufaa ya kwenda hospitalini au kituoni mwa afya. Ikiwezekana hakikisha usafirishaji wa haraka na mapokezi ya mwanamke huyo kwenye kituo hicho cha afya cha ngazi ya juu. Hatua zako zinapaswa kuzingatia utambuzi wako wa kiafya na ukali wa hipatensheni hiyo.

19.6.1 Hatua iwapo priklampsia si kali

Wanawake wajawazito wanaotambuliwa kuwa na:

 • priklampsia ndogo
 • hipatensheni sugu
 • hipatensheni ya ujauzito

wanapaswa kupewa rufaa bila wewe kujaribu kutatua, hasa siku ya utambuzi.

 • Je, kwa nini unafikiri rufaa ni muhimu angali hipatensheni hiyo si kali?

 • Hii ni kwa sababu wakati mwingine aina ya hipatensheni isiyo kali inaweza kuendelea na kuwa aina kali kwa muda wa kipindi kifupi.

  Mwisho wa jibu.

19.6.2 Kuwashawishi wananwake walioathiriwa kwenda kwa matibabu ya kiafya

Unapaswa kutoa ushauri kwa mwanamke na familia yake kuhusu hatari ya matatizo ya mama na fetasi na umuhimu wa kupata matibabu ya kitaalamu mara moja. Katika visa vya eklampsia, watu katika sehemu nyingi za mashambani huamini kuwa matukutiko yanahusiana na roho za kishetani. Mwanamke mjamzito aliyepata tukutiko kwenye tamaduni hizi huenda asitake kwenda kituoni mwa afya kwa sababu angependelea kwenda kwa maji matakatifu, kasisi au kiongozi mwingine wa dini, au madaktari wa kienyenji. Una jukumu muhimu sana kuhakikisha kuwa mwanamke huyo na familia yake wameelewa kuwa matukutiko hayo husababishwa na shinikizo la juu la damu analopitia. Mhakikishie kuwa matukutiko hayo yatakoma baada ya kuzaa.

19.6.3 .Matibabu saidizi ya priklampsia kali kabla ya rufaa 

Jukumu lako la pili ni kutoa matibabu saidizi ili kuzuia kuzorota kwa hali kabla ya mwanamke huyo kufika kituoni mwa afya. Utambuzi wako wa kiafya unapokuwa kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali 19.2 hapo awali:

 • priklampsia kali
 • priklampsia kali zaidi juu ya iliyokuwepo hapo awali

unapaswa uweze kuzuia kutokea kwa eklampsia kwa kuchukua hatua saidizi zilizo katika Kisanduku 19.2 hapa chini.

Kisanduku 19.2 Hatua za kuzuia kuendelea kwa priklampsia zaidi na priklampsia kali
 1. Mpe rufaa kwenda katika kituo cha afya cha ngazi ya juu mapema iwezekanavyo.
 2. Wasiliana na hospitali au kituo cha afya kinachompokea ili kuwafahamisha kuwa mwanamke aliye na Priklampsia kali anaenda huko kwa matibabu ya dharura.
 3. Mhakikishie mwanamke huyo na familia yake kuwa atakapofika katika kituo hicho cha afya, daktari atampa dawa za kupunguza shinikizo lake la juu la damu (dawa za kuzuia hipatensheni) na kumkinga dhidi ya matukutiko (dawa za kuzuia matukutiko)
 4. Huku usafiri unapoendelea kupangwa, dunga sindano katika vena kwenye mkono wa mwanamke huyo, jinsi utakavyosoma kufanya katika Kipindi cha 22 cha Moduli hii na katika vipindi vyako vya mafunzo ya kiutendaji. Unganisha sindano hii kwa mfuko ulio na angalau lita 1 ya kiowevu cha mshipani: kiowevu cha chumvi cha kawaida au mchanganyiko wa Ringer. Katu usimpe kiowevu cha deksitrosi.

19.6.4 Rufaa ya dharura ya eklampsia

Mchoro 15.2 Ni salama zaidi kumsafirisha mama kwenda hospitalini akiwa amelala kwa upande.

Ukigundua mwanamke mjamzito aliye na ekilampsia, unapaswa kuchukua hatua zilizoelezwa katika Kisanduku 19.2. Mpe rufaa mara moja ila akiwa yuko mwishoni mwa leba - katika hali hii unapaswa kuzalisha mtoto na umpe rufaa pamoja na mtoto kwenda hospitalini mara moja baada ya uzazi huo.

Unapomsafirisha mwanamke aliye na eklampsia kwenda katika kituo cha afya, hakikisha kuwa amelala kwa upande njia yake ya hewa ikiwa imefunguka (Mchoro 15.2). Usimruhusu kulala chali kwa sababu anaweza kupata ugumu katika kupumua akipata tukutiko jingine. Kulala kwa upande pia humaanisha kuwa akitapika ana uwezekano mdogo wa kuvuta matapishi kwenye mapafu yake.

Katika kipindi kifuatacho, utajifunza kuhusu hali nyingine inayoweza kuhatarisha maisha: utokaji mimba na kutokwa na damu mwanzoni mwa ujauzito.

Muhtasari wa Kipindi cha 19

Katika Kipindi cha 19 umejifunza kuwa:

 1. Magonjwa ya hipatensheni katika ujauzito ndiyo mojawapo ya visababishi vinanavyotokea sana vya maradhi na vifo vya kina mama na vya wakati wa kuzaa.
 2. Msongo wa mishipa ya damu mwilini mwote ni tukio la hipatensheni inayohusiana na ujauzito. Hii huleta kupunguka kwa kiasi cha damu ya mwanamke, kwani viowevu hutoka kwenye mishipa ya damu na kujikusanya kwenye tishu. Edema hutokea kwenye tishu na ogani tofauti (zikiwemo ubongo, ini na figo) na kusababisha kupungua katika uletaji wa damu kwenye sehemu tofauti za mwili wa mama na kwenye plasenta.
 3. Visababishi vya hatari vinavyojulikana vya hipatensheni inayohusiana na ujauzito ni: kuwa primigravida kabla ya umri wa miaka 20 na baada ya miaka 35, ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja, historia ya kibinafsi au kifamilia ya priklampsia au eklampsia, kuwa na ugonjwa wa kisukari au figo au, unene wa kupindukia.
 4. Priklampsia (shinikizo la juu la damu + protini nyingi) ndiyo aina inayotokea sana ya hipatensheni katika ujauzito. Priklampsia kali huonyeshwa kwa dalili za kiafya kama vile maumivu ya kichwa, kiwaa, maumivu ya epigastriamu, kupungua kwa mkojo, kupungua kwa kucheza kwa mtoto na kuwa na edema ya mwili wote.
 5. Eklampsia hutambulika mwanmke mjamzito anapopata tukutiko au koma bila visababishi vingine. Ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya kina mama na fetasi kati ya aina zote za magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito.
 6. Katika visa halisi, eklampsia ina awamu tatu: awamu ya utulivu, toni, kiklonasi na koma.
 7. Awamu ya koma inaweza kuwa ndefu iwapo kuna tukutiko la kujirudia, edema kubwa ubongoni, kutokwa na damu kwa wingi ndani ya kichwa, au hipoglisimia husika.
 8. Matatizo yanayotokea sana ya priklampsia kali ni eklampsia, anemia, kiwango cha chini cha pleteleti, kukosa kufanya kazi ghafla kwa ogani kadhaa (figo, ini, moyo, mapafu na macho).
 9. Matatizo ya fetasi ni kuachia kwa plasenta, asifiksia ya ndani ya uterasi, na asifiksia ya mapema ya mtoto mchanga (kutokana na kiwango cha chini cha oksijeni kwenye damu) uzuaji wa ukuaji kwenye uterasi na fetasi kufariki ndani ya uterasi.
 10. Katika udhibiti wa magonjwa ya kihipatensheni ya ujauzito, jukumu lako la kwanza ni kuwezesha rufaa mapema.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 19

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi umeweza kuyatimiza Malengo ya Somo la Kipindi hiki kwa kujibu maswali haya. Andika majibu katika Shajara yako na ujadiliane na Mkufunzi wako katika Mkutano saidizi wa Somo utakaofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na nakala kuhusu Maswali ya kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 19.1 (linatathmini Malengo ya Somo 19.1 na 19.2)

Je, ni gani kati ya kauli hizi si sahihi? Eleza kisicho sahihi kwa kila kauli.

 • A.Kuta za misuli za mishipa ya damu za mwili wote wa mwanamke zinaponywea, nafasi ndani ya mishipa huongezeka na hivyo shinikizo lake la damu kushuka.
 • B.Hipatensheni katika ujauzito hupunguza damu inayotoka kwenye ateri za endometria kwenye uterasi ya mama hadi kwa fetasi kupitia kwa plasenta.
 • C.Hipatensheni hupunguza kiwango cha kiowevu cha amnioni kinaichozunguka fetasi kwa sababu kiasi cha damu inayoingia kwenye figo za mtoto ni kidogo na hivyo hutengeneza kiasi kidogo cha mkojo.
 • D.Ukuaji wa fetasi hauzuiliwi kwa mwanamke mjamzito aliye na hipatensheni.
Answer

A si kweli. Kuta za misuli za mishipa ya damu za mwili wote wa mwanamke zinaponywea, nafasi ndani ya mishipa hii hupungua, hivyo shinikizo lake la damu hupanda.

B ni kweli. Hipatensheni katika ujauzito hupunguza damu inayotoka kwenye ateri za endometria kwenye uterasi ya mama hadi kwa fetasi kupitia kwa plasenta.

C ni kweli. Hipatensheni hupunguza kiwango cha kiowevu cha amnioni kinaichozunguka fetasi kwa sababu kiasi cha damu inayoingia kwenye figo za mtoto ni kidogo na hivyo hutengeneza kiasi kidogo cha mkojo.

D si kweli. Kuna uwezekano mkubwa wa ukuaji wa fetasi kuzuiliwa kwa mwanamke mjamzito aliye na hipatensheni kwa sababu viwango vya oksijeni, virutubishi na viowevu vinavyomfikia mtoto kutoka kwa plasenta kupitia damu hupungua.

Mwisho wa jibu.

Swali la Kujitathmini 19.2 (linatathmini Malengo ya Somo 19.1 na 19.3)

Kamilisha Jedwali 19.3 kwa vipimo ambavyo ungetarajia kupata kwa wanawake walioainishwa kuwa na aina za hipatensheni zilizoonyeshwa katika upande wa mkono wa kushoto.

Jedwali 19.3 kwa Swali la Kujitathmini 19.2
AinaShinikizo la juu la damu ProtinuriaDalili za ukali
Hipatensheni ya ujauzito
Priklampsia ndogo
Priklampsia kali
Priklampsia zaidi juu ya iliyokuwepo awali
Answer
Jedwali 19.3 lililokamilishwa limeonyeshwa hapa chini.
AinaShinikizo la juu la damu ProtinuriaDalili za ukali
Hipatensheni yaujauzito (hutokea katika ujauzito na kuisha baadaye)zaidi ya kipimo cha 140/90 mmHgHakuna protinuria nyingiHakuna
Priklampsia ndogoKati ya 140/90 mmHg na 160/110 mmHgHakuna protinuria nyingiHakuna
Priklampsia kaliZaidi ya au sawa na 160/110 mmHgProtinuria inayoonekana iwepo au isiwepo (matokeo ya kipimo cha dipstick zaidi ya au sawa na +2)Maumivu ya kichwa, kiwaa, maumivu ya epigasriamu, kupungua kwa mkojo, kupungua au kutokuweko kwa kucheza kwa mtoto
Priklampsia zaidi juu ya iliyokuwepo awaliJuu kuliko kabla ya ujauzito kwa mwanamke aliye na hipatensheni suguProtinuria inayoonekana nyingi zaidi au inayozidi Kuwe au kusiwe na dalili za ukali

Mwisho wa jibu.

Soma uchunguzi maalumu ufuatao kisha ujibu maswali yatakayofuata.

Uchunguzi Maalum 19.1 Kisa cha Zewditu

Zewditu ni mwanamke primigravida mwenye umri wa miaka 37 na ana ujauzito wa pacha. Yeye ana uzani wa kupita kiasi ikilinganishwa na urefu wake. Mama huyu alikuwa mwenye afya njema hadi ujauzito wake ulipofika juma la 22, alipoanza kulalamikia maumivu ya kichwa na kuvimba nyayo na vifundo.

Swali la Kujitathmini 19.3 (linatathmini Malengo ya Somo 19.1, 19.2, 19.3, 19.4, 19.5 na 19.6)

 • a.Je, Zewditu ana visababishi vyovyote vya hatari vya hipatensheni vinavyotokea sana. Iwapo ndio, ni vipi?
 • b.Je, ana mojawapo ya dalili za kiafya za hipatensheni? Iwapo ndio, ni dalili na ni nini kisababishi?
 • c.Je, ni matatizo yapi yanayoweza kuathiri mtoto wa Zewditu iwapo hatatibiwa hipatensheni?
 • d.Je, ni hatua zipi utakazochukua katika kisa cha Zewditu, na ni kwa nini?
Answer
 • a.Zewditu ana visababishi vitatu hatari vya hipatensheni vinavyotokea sana: yeye anapata mtoto wake wa kwanza baada ya umri wa miaka 35; anatarajia pacha; na ni mnene kupindukia.
 • b.Ana dalili mbili za kiafya za hipatensheni: maumivu ya kichwa na kuvimba kwa nyayo/vifundo. Dalili hizi mbili husababishwa na edema (kuvimba kutokana na kiowevu kujikusanya kwenye tishu). Maumivu ya kichwa hutokana na edema kwenye ubongo, angali, kuvimba nyayo na vifundo hutokana na edema kwenye tishu za miguu. Kisababishi cha edema ni shinikizo la juu la damu linalosukuma kiowevu kutoka kwa damu kupitia kuta za mishipa kisha kuingia kwenye tishu zilizo karibu.
 • c.Matatizo yanayoweza kumuathiri mtoto wa Zewditu asipotibiwa haraka ni kuachia kwa plasenta, asifiksia ya ndani ya uterasi, kuzuiliwa kwa ukuaji ndani ya uterasi, fetasi kufia ndani ya uterasi au upunguani baadaye maishani.
 • d.Hatua ya kwanza ni kumpima shinikizo la damu na kuchunguza kuwepo kwa protini katika mkojo wake. Hata ikiwa matokeo ni karibu na kawaida, anapaswa kupewa rufaa hadi kituo cha ngazi ya juu zaidi, bila wewe kujaribu utatuzi wowote, ikiwezekana apewe rufaa hii siku hiyo ya uchunguzi. Hii ni kwa sababu hata ikiwa hipatensheni yake ni ndogo wakati huo, inaweza kuendelea na kuwa priklampsia kali kwa kipindi cha muda mfupi.

Mwisho wa jibu.