Skip to main content
Printable page generated Saturday, 20 April 2024, 2:43 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Saturday, 20 April 2024, 2:43 AM

22. Kuanzisha matibatu ya udungaji wa viowevu mishipani na kuweka katheta ndani ya mwanamke mjamzito

Kipindi cha 22 Kuanzisha Matibabu ya Kudungia Viowevu Mishipani na Kumwingiza Katheta Mwanamke Mjamzito

Utangulizi

Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu mbinu mbili muhimu za utunzaji wa dharura kwa mwanamke mjamzito:

  • Anayevuja damu (kupoteza damu haraka sana kutoka kwa uterasi) kwa sababu zilizoelezwa katika kipindi cha 20 na 21 au
  • Asiyeweza kukojoa (kupitisha mkojo) kwa sababu ya kizuizi kinachomzuia kukojoa. Kwa kawaida, hii ni kwa sababu shinikizo la mtoto huzuia urethra- neli inayotoa mkojo kutoka kwa kibofu cha mama.

Kipindi hiki ni maandalizi ya mafunzo ya ujuzi wa kiutendaji kuhusu mbinu hizi zote utakazozipata katika kituo cha afya au hospitalini.

Hapa tutakutangulizia vifaa utakavyohitaji, na kukueleza jinsi ya kuanzisha na kudumisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani na pia jinsi ya kutia katheta kwenye kibofu cha mama mjamzito. Pia utajifunza jinsi ya kuzingatia utaratibu wa kudhibiti maambukizi unapotumia mbinu hizi.

Kabla ya kutekeleza mbinu yoyote kati ya hizi, hakikisha umemweleza mwanamke kwa lugha anayoelewa yale mtakayofanya na sababu za kuhitaji mbinu zenyewe.

Mfahamishe kuwa, punde tu utakapokamilisha utaratibu huu ni lazima aende katika kituo cha afya cha kiwango cha juu ili apate matibabu zaidi.

Hakikisha kuwa usafiri unatayarishwa unapoandaa matibabu ya kudungia viowevu mishipani wake au kutia katheta kwenye kibofu.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 22

22.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito (Maswali ya kujitathmini 22.1, 22.2 na 22.3)

22.2 Kueleza sababu za kumpa mwanamke mjamzito matibabu ya kumdungia viowevu mishipani au kumwingiza katheta ndani ya kibofu (Swali la Kujitathmini 22.1 na 22.3)

22.3 Kufafanua kuhusu vifaa utakavyotumia, maandalizi na utaratibu wa kuanzisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani pamoja na jinsi ya kuchagua sehemu bora ya kutoboa mshipa wa vena, kuweka na kutoa kanula kwenye mishipa. (Maswali ya Kujitathmini 22.1 na 22.2)

22.4 Kufafanua jinsi ya kufuatilia matibabu haya. (Swali la Kujitathmini 22.1)

22.5 Kufafanua kuhusu vifaa utakavyotumia, maandalizi na mbinu ya kuingiza na kutoa katheta ya mkojo. (Maswali ya Kujitathmini 22.1 na 22.3)

22.6 Kufafanua kuhusu taratibu za kudhibiti maambukizi zinazohitajika ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi yanayotokea kufuatia mbinu ya kudungia viowevu mishipani na kutia katheta kwenye kibofu. (Swali la Kujitathmini 22.1 na 22.2)

22.1  Kuanzisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani

22.1.2 Wakati bora wa kuanzisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani

Mwanamke mjamzito anayevuja damu atapata hali ya mshtuko kwa haraka sana; anaweza kupoteza fahamu na kisha kufa iwapo hautafanya lolote kwa haraka.

  • Je, dalili za mshtuko ni zipi? (Ulijifunza haya katika Kipindi cha 20.)

  • Mwanamke atapata uweupe hasa ndani ya vigubiko vya chini vya macho na viganja vya mikono yake; shinikizo lake la damu la kidiastoli (la kipimo cha chini) likiwa chini ya 60 mmHg- na wakati mwingine likiwa chini zaidi na mpigo wa moyo ukiwa juu; mara nyingi ukiwa zaidi ya midundo 100 kwa kila dakika.

    Mwisho wa jibu

Ili kuokoa maisha yake, unapaswa kufahamu jinsi ya kuanzisha matibabu ya kudungia viowevu mshipani (ambayo pia hujulikana kama ufufuzi wa kutumia viowevu vinavyodungiwa mishipani au kutia viowevu mishipani).

Hii inamaanisha kuingiza viowevu maalum ndani ya mzunguko wa damu kwa kutumia sindano iliyo na shimo inayoitwa kanula. Sindano hii huingizwa mishipani ili kutia viowevu vitakavyochukua nafasi ya sehemu ya viowevu vya damu vinavyopotezwa. Unapaswa kuyafanya haya kabla ya kumhamisha kwa dharura hadi kituo cha afya atakapopewa damu. Wanawake walio katika leba au muda tu baada ya kuzaa wanaweza kuvuja damu (kama utakavyojifunza katika Moduli ya Utunzaji katika Leba na Kuzaa). Unafaa kuanzisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani kwa haraka utakapogundua kuwa mwanamke anavuja damu.

22.1.2 Kutayarisha vifaa vya matibabu ya kudungia viowevu mshipani

Hatua ya kwanza katika mbinu hii ya kudungia viowevu kwenye mshipa ni kukusanya na kuchunguza vifaa utakavyohitaji (tazama Mchoro 22.1). Unaweza kuweka kila kitu kwenye sahani pana iliyo safi au kwenye sinia inayopatikana katika eneo hilo. Tutaeleza kwa ufasaha kuhusu vifaa hivi baada ya kutazama Mchoro 22.1

Mchoro 22.1 Vifaa vinavyohitajika katika matibabu ya kudungia viowevu mishipani. Nambari zilizo katika orodha iliyo hapa chini zinalingana na nambari zilizo kando ya vifaa vilivyo kwenye sinia
  1. Viowevu safi vya sindano zilizo ndani ya kifuko cha plastiki. Aina kuu ya viowevu huitwa Chumvi ya Kawaida na mchanganyiko wa Laktesi ya Ringer.
  2. Neli ya viowevu vya sindano (wakati mwingine hujulikana kama njia ya viowevu vya sindano) pamoja na kiunganishi katika upande mmoja ili kuunganishwa na kifuko cha viowevu na kiunganishi kingine katika upande mwingine ili kuiunganisha neli na kanula. Neli hii huwa imefungwa ndani ya kifurushi cha plastiki (ambacho hakijaonyeshwa katika Mchoro 22.1).
  3. Kanula safi ya sindano. Kanula hii huwa imefungwa ndani ya kifurushi cha plastiki (ambacho hakijaonyeshwa katika Mchoro 22.1). Mchoro mkubwa utakuwepo baadaye katika kipindi hiki (mchoro 22.6).
  4. Ili kudhibiti mtiririko wa viowevu kwenye neli, unahitaji klampu iliyo na umbo la duara ambayo utaunganisha na neli ya sindano kisha uikaze au uilegeze.
  5. Chupa yenye alkoholi utakayotumia pamoja na pamba (9) ya kupanguza eneo la ngozi ambapo kanula itaingiziwa. Ikiwa hauna alkoholi unaweza kutumia sabuni na maji.
  6. Glavu safi za upasuaji zilizofungiwa ndani ya kifuko. Fungua kifuko hiki kwa makini (kama inavyonyeshwa katika Mchoro 22.1), unaweza kuilaza karatasi hii safi kwenye sinia huku upande wa ndani ukielekea nje kisha uitumie karata kama sehemu safi. Ikiwa hauna glavu safi za kimatibabu, unafaa kutumia glavu safi kabisa za kawaida zilizopanguzwa kwa alkoholi au zilizosafishwa kwa sabuni na maji
  7. Mshipi, kamba, kipande cha nguo au bendeji ili kutumia kama fundo - kifaa unachohitaji kufungia mkono wa mtu ili kuzuia mtiririko wa damu kwa muda mfupi tu unapomdunga sindano iliyoko mwishoni mwa kanula kwenye mkono.
  8. Plasta ya kubandikia kanula kwenye mkono wake ili kuiimarisha salama mahali pake. Ikiwa huna plasta, unaweza kutumia bendeji safi au kifaa kinachopatikana kwa urahisi; kwa mfano, kipande cha nguo safi.
  9. Pamba au vipande vidogo vya nguo safi vya kutumia na alkoholi ili kupanguzia ngozi kabla ya kuingiza kanula.

22.1.3 Mbinu safi za matibabu ya kudungia viowevu mishipani.

Unapojitayarisha kumpa mtu matibabu ya kudunga viowevu mishipani yake, ni sharti kila kitu kiwe safi na utumie mbinu safi (zisizo na uchafuzi wa kiini cha maradhi) mara nyingi iwezekanavyo. Jambo hili linaweza kuwa gumu kufanya katika maeneo ya mashambani lakini ukifuatilia maelekezo yaliyo kwenye Kisanduku 22.1, unaweza kupunguza hatari ya maambukizi.

Kisanduku 22.1  Kuzuia maambukizi wakati wa matibabu ya kudungia viowevu mishipani
  • Hatua muhimu zaidi ni kunawa mikono kabisa kwa sabuni na maji safi kwa angalau dakika mbili kabla na baada ya kushika mgonjwa au kifaa chochote kisafi.
  • Tumia alkoholi kupanguza sinia au sahani utakayowekea vifaa vyako au (ikiwa haipatikani) safisha sinia kwa sabuni na maji na uhakikishe kuwa imekauka vya kutosha kabla ya kuitumia.
  • Vaa glavu safi au zilizosafiswa kabisa. Kwa kuwa utagusa damu ya mgonjwa huyu, ni lazima uvae glavu kila wakati.
  • Kanula, neli ya sindano ya mshipa na glavu za upasuaji huwa zimefungwa kwa plastiki safi au kifurushi cha karatasi. Pande za ndani za vifurushi hivi huwa safi hivyo zinaweza kufunguliwa na kutandazwa ili kutumika kama sehemu safi ya kuweka vifaa hadi utapovihitaji tena.
  • Mgonjwa anapaswa kuwa amelazwa kwa hali ya kutulia. Panguza ngozi yake kwa alkoholi au sabuni na maji kwenye sehemu ambayo kanula itaingizwa mishipani.
  • Fungua kifurushi safi kilichofunika neli ya kutilia viowevu kisha uiunganishe na kifuko cha viowevu. Tundika kifuko hiki kwenye kiopoo kilicho ukutani juu ya mgonjwa au uulize mtu yeyote akishikilie juu ya mgonjwa. Hakikisha kuwa sehemu ya mwisho ya neli itakayoshikanishwa na kanula imewekwa safi bila kuguswa.

22.1.4 Kuchagua kanula ya sindano

Unapaswa kuchagua kanula yenye ukubwa mwafaka kulingana na kusudi. Ukubwa wa kanula hujulikana kama geji ya kanula na kila ukubwa hupewa nambari - nambari ya juu huashiria kanula kubwa.

  • Unafikiri ni kwa nini ni mwafaka kuchagua geji kubwa ya kanula unapompa mwanamke mjamzito anayevuja damu matibabu ya kudungia viowevu mishipani?

  • Mwanamke huyu amepoteza kiasi kikubwa cha damu. Kwa hivyo, unahitaji kuingiza viowevu mbadala ndani ya mfumo wake wa damu haraka iwezekanavyo. Unahitaji kanula iliyo na geji kubwa zaidi ili uweze kutia kiwango kikubwa cha viowevu mishipani wake kwa muda mfupi.

    Mwisho wa jibu

22.1.5 Kuchagua sehemu ya kudungia

Mchoro 22.2 Sehemu za kudunga mshipa kwenye mkono na kigasha.

Hatua inayofuatia ni kutambua sehemu bora ya kudunga mshipa wa vena, yaani sehemu ambapo ‘utatoboa mshipa’ kwa kuingizia kanula ya kutilia viowevu. Mchoro wa 22.2 unaonyesha sehemu za kawaida zinazotumika kwenye mkono na kigasha.

Ili kuchagua eneo la kudunga mshipa wa vena:

  • Mwulize mgonjwa akuonyeshe mkono anaotumia mara nyingi, kwa mfano, kushikia kisu au chombo chochote kile. Ikiwa atasema ni 'mkono wa kulia', huu ndio mkono 'ulio na nguvu zaidi' na mkono wake wa kushoto 'hauna nguvu sana'.
  • Kwanza, tafuta sehemu utakazodunga kwenye mkono wake usio na nguvu ukizingatia sehemu ya juu katika mkono huu.
  • Chagua mshipa unaotoshea kanula huku ukiepuka maeneo yalio karibu na viungo kama vile kifundo au kiwiko.
  • Hakikisha kuwa baada ya kumwingiza mwanamke huyu kanula, kanula hii haitatizi uwezo wake wa kusongesha mkono.
  • Epuka eneo lililo na maumivu likiguswa

Uwezakano wa mshipa kuonekana unaweza kuimarishwa kwa kumhimiza mwanamke akunje na kukunjua vidole vyake mara kadhaa na kupeleka mkono wake chini huku ukisugua eneo la kudunga.Unapoendelea kupata ujuzi, itakuwa rahisi kwako kuchagua mshipa mwafaka unaoonekana vyema, ambao haujajipinda kisha mahali unafikiri unaweza kuingiza kanula yako kwa urahisi.

22.1.6 Kuingiza kanula ya kutia viowevu mishipani

Baada ya kuamua mahali utakapoingiza kanula ya sindano ya mshipa, funga fundo la takriban upana wa vidole vitatu juu ya sehemu uliyochajua kudunga kwenye mshipa. (Mchoro 22.3a). Ukitumia kidole kilicho na glavu, tafuta mshipa kwa kugusa (mchoro 22.3b). Safisha sehemu hiyo kwa alkoholi (mchoro 22.3c) au sabuni na maji.

Mchoro 22.3 Hatua za kuingiza kanula. (a) Fungilia fundo la kuzuia damu juu ya sehemu uliyoamua kudunga. (b) Tafuta mshipa mwafaka kwa kidole chako kilicho na glavu. (c) Safisha eneo hilo kwa alkoholi au sabuni na maji.

Tandaza ngozi iliyovutika kisha ulainishe mshipa ukitumia mkono wako usio na nguvu sana — hii inamaanisha uutandaze mshipa ili usisonge usije ukakosa kuulenga kwa sindano. Dunga ngozi kwa kuweka kanula juu ya mshipa ukiwa umeinamisha kwa pembe ya digrii 45; Kwanza, isukumie sindano ndani ya ngozi kisha ulenge mshipa (Mchoro 22.4). Unapokaribia mshipa huu, shusha pembe ya hadi digrii 10 kisha uingize kanula mishipani.

Mchoro 22.4 Tandaza ngozi ukitumia mkono wako usio na nguvu sana kisha uingize kanula mishipani (a) wa mkono wa mgonjwa (b) kwenye kigasha.

Angalia iwapo utaona 'kuwapo kwa damu' (damu ikichiriza nyuma kwenye mrija wa kanula). Hii itadhihirisha kuwa sindano imeingia mishipani. Kufikia hapa, achilia fundo la kuzuia damu kisha usukume kanula mishipani hadi uhakikishe imeingia inavyohitajika.

Kanula ni sindano ya chuma iliyofungiliwa plastiki, na sehemu ya plastiki ndiyo inayobaki mishipani. Ondoa sehemu ya chuma ya sindano kwa utaratibu huku ukiacha sehemu ya plastiki mshipani.

Mchoro 22.5 Kanula imeshikishwa mahali pake kwa plasta (au kifaa chochote kinachofanana na plasta) na kuunganishwa na mrija wa sindano.

Lainisha sehemu ya plastiki ya kanula kwa plasta, kamba safi au kipande cha nguo kilichofungilia eneo la kudunga mshipa (Mchoro 22.5).

Unganisha mrija na kifuko cha viowevu kisha ufungue klampu ya duara ili viowevu hivi viweze kutiririka chini kwenye mrija. Fanya hivi kabla ya kuunganisha upande mwingine wa mrija kwenye kanula. Kupitisha viowevu kwenye mrija uhakikisha kuwa hakuna viputo vya hewa ndani ya mrija kabla ya kuingiza viowevu ndani ya mgonjwa.

22.3 Ufuatilizi wakati wa matibabu ya kudungia viowevu mishipani

Baada ya kuunganisha mrija wa kuingiza viowevu kwenye kanula, sukuma kigurudumu hadi juu ya klampu (tazama mchoro 22.6). Hatua hii itaruhusu viowevu kuteremka kwenye neli hadi mshipani haraka iwezekanavyo. Kwa sababu mwanamke huyu anapoteza kiwango kikubwa cha damu, unafaa kuhakikisha kuwa kiwango cha mtiririko wa damu ni cha kasi sana. Dumisha kiwango hiki cha juu cha mtiririko wa viowevu hata unapomsafirisha hadi kituo cha afya. Hakikisha kuwa kifuko chenye viowevu kimeshikiliwa juu ya mkono wa mwanamke huyu, la sivyo kiwango cha mtririko kitapungua hata ikiwa klampu 'imefunguliwa' hadi mwisho.

Mchoro 22.6 Klampu hii inaweza 'kufungwa' (picha ya katikati) au 'kufunguliwa' ili kudhibiti kiwango cha mtiririko wa viowevu vinavyopitia kwenye mrija hadi mshipani kupitia kwenye kanula.

22.3.1 Kuanzisha utaratibu wa ufuatilizi

Utaratibu wa kufuatilia jinsi matibabu yanavyoendelea ni sharti uanzishwe; ukianzia kwenye kifuko kilicho na viowevu na kumalizia kwenye eneo la mshipa lililodungwa. Kwa muda wote utakapokuwa na mwanamke huyu, kiwango cha mtiririko kinafaa kutazamwa kila baada ya dakika 15. Ikiwa mtiririko huu umepungua kwa kasi, chunguza iwapo mrija unaopitisha viowevu umejipinda au mkono wa mwanamke huyu umejipinda hivyo kuzuia mtiririko, kisha uunyooshe. Kiwango cha mtiririko wa viowevu katika hali ya dharura kinafaa kuwa cha kasi sana.

Hakikisha kuwa umefuatilia mpigo wa moyo wa mwanamke huyu na shinikizo lake la damu kila baada ya dakika 15.

  • Iwapo lengo ya kumpa viowevu hivi ni kutibu mshtuko kufuatia kupoteza damu, unatarajia nini kifanyike katika kiwango cha mpigo wa moyo na shinikizo la damu punde viowevu hivi vinapoingia mishipani?

  • Kasi ya mpigo wa moyo itapungua na shinikizo la damu kuongezeka unapoingiza viowevu vya kutosha. (Baada ya kuingiza vifuko viwili au vitatu vya viowevu, kinachotarajiwa ni mpigo wa moyo kuwa wa polepole na shinikizo la damu kuongezeka kuelekea hali ya kawaida.)

    Mwisho wa jibu

Mara tu baada ya kumaliza maandalizi ya matibabu ya kumdungia viowevu mishipani, mpe mwanamke huyu rufaa hadi kwenye kituo cha afya cha kiwango cha juu haraka iwezekanavyo. Ukiweza, andamane naye.

22.3.2 Wakati unaofaa wa kusitisha kuingiza viowevu mshipani

Ukilinganisha na mkono mwingine, chunguza uvimbe wowote karibu na eneo la mshipa lililodungwa. Uvimbe huu unaweza kuashiria kuwa kanula imetoka na viowevu vinaingia kwenye tishu laini badala ya mshipa. Ukiona uvimbe huu, legeza plasta kisha utoe kanula. Chagua eneo jipya la kudunga mshipa kisha utumie kanula nyingine safi kudungia mshipa mwingine na uiunganishe tena na kifuko cha viowevu.

Kiowevu husitishwa kuingia mshipani iwapo mwanamke hahitaji viowevu zaidi, au sehemu iliyodungiwa kanula ikiambukizwa (ngozi iliyo karibu na eneo hili itakuwa nyekundu na mgonjwa atahisi maumivu ukimgusa). Wakati mwingine, wagonjwa wanaweza kupewa viowevu vingi kwa muda mfupi. Hatua hii inaweza kushinikiza moyo kwa sababu kiasi cha damu kimeongezeka. Pia viowevu vinaweza kuingia ndani ya mapafu, na katika matukio kama hayo mgonjwa anaweza kuwa na shida ya kupumua, kukohoa na wakati mwingine anachanganyikiwa. Jambo hili haliwezi kutokea iwapo utakuwa ukimhudumia mgonjwa huyu kwa sababu utampendekezea rufaa kwa dharura punde baada ya kuanzisha matibabu ya kupitishia viowevu mishipani. Lakini ukikabiliwa na tukio hili, unapaswa kusitisha viowevu na kumhamisha mwanamke huyo hadi kituo cha afya cha kiwango cha juu kilicho karibu ili apate matibabu zaidi.

Unaweza kusitisha viowevu kwa kufunga kigurudumu cha klampu hivyo viowevu havitashuka tena. Iache kanula ikiwa imepachikwa mkononi ili itolewe katika kituo cha afya kwa kuzingatia usafi unaohitajika.

  • Ili kusitisha upitishaji wa viowevu unahitaji glavu safi au zilizosafishwa mno, pamba safi iliyokauka, kipanguzio cha antiseptiki au pamba iliyotumbukizwa ndani ya alkoholi na plasta mpya.

Mweleze mgonjwa unachonuia kufanya, vaa glavu na 'uzime' klampu. Hakikisha kuwa mtiririko wa viowevu ndani ya mrija umesitishwa. Huku ukishikilia kanula kwa mkono wako ulio na glavu, ondoa plasta au chochote kinachoshikilia kanula kwa kutumia mkono huo mwingine. Ukitumia pamba safi isiyo na unyevunyevu kushikilia juu ya sehemu iliyodungwa, toa kanula kisha ufinye kwa vidole vyako kwenye sehemu hiyo kwa dakika moja au mbili. Pangusa sehemu hiyo kwa antiseptiki au alkoholi ili kuondoa viini vyovyote vinavyoweza kuwa vimekaribia shimo lilodungwa. Ngozi ikikauka, funika sehemu hiyo kwa plasta iwapo unayo.

Kila wakati, hakikisha kuwa kanula imetoka yote kisha uitupe salama kwenye chombo kisichoweza kutobolewa kwa urahisi.

22.4  Kuingiza katheta ndani ya kibofu

Mwanamke mjamzito aliye kwenye leba asiyeweza kukojoa kufuatia kufinyika kwa mrija wa kupisha mkojo (urethra) kutoka kwenye kibofu atasumbuka sana. Vile vile, kibofu kilichojaa kitazuia mtoto kuzaliwa kwa kuchukua nafasi kwenye pelvisi. Kwa, anahitaji katheta (mpira safi au neli ya plastiki) iingizwe ndani ya kibofu ili kuupisha mkojo kabla hujampa rufaa aende kwenye kituo cha afya cha kiwango cha juu. Mbinu hii huitwa uwekaji katheta. Utaratibu wa kuweka katheta unaweza kuruhusu uzalishaji kuendelea. Mwanamke hataweza kuzaa kwa njia ya kawaida bila utaratibu huu iwapo leba itaanza. Wanawake wanaokuwa na leba ya muda mrefu, pia wanaweza kuhitaji kuwekewa katheta ikiwa vibofu vyao vimezuiliwa. Kibofu cha mwanamke kilichovimba huhisi kama mfuko laini wa maji uliojitandaza juu ya mfupa wa kinena. Unaweza kuona kibofu chote kama mwinuko wenye umbo la duara akilala chali.

Mfahamishe utakachomfanyia na umueleze umuhimu wa utaratibu huo. Baadaye mwambie alale chali huku kichwa kikiinuliwa na kuikunja na kupanua miguu. Funika upande wa chini wa mwili wake kwa kitambaa safi isipokuwa eneo la ukeni ili asiaibike iwapo kuna watu wengine karibu.

22.4.1 Vifaa vya kuingizia katheta ndani ya kibofu

Kusanya vifaa unavyohitaji kufanyia utaratibu huu kisha uviweke kwenye sahani au sinia safi (tazama mchoro 22.7). Tutaeleza kwa kina kuhusu vifaa hivi baada ya kutazama mchoro 22.7

Mchoro 22.7 Vifaa vinavyohitajika wakati wa kuingiza katheta ndani ya kibofu.

Nambari katika orodha inayofuata zinalingana na nambari zilizo kando ya vifaa kwenye sinia

  1. Mrija safi wa kupitishia mkojo, pamoja na kifuko cha kukusanyia mkojo unaotoka kwenye kibofu. Mrija huu huwa katika kifurushi safi cha plastiki (ambacho hakijaonyeshwa katika Mchoro 22.7).
  2. Alkoholi au mchanganyiko wa antiseptiki ya kuoshea uke; ikiwa vifaa hivi havipo, tumia sabuni na maji.
  3. Pamba au vipande vidogo vya nguo safi.
  4. Glavu safi; ikiwa hauna unaweza kutumia glavu iliyosafishwa.
  5. Mrija ulio na mafuta ya kulainisha (jeli inayotelezesha ya kusaidia katheta kuingia ndani kwa urahisi).
  6. Sirinji iliyo na maji safi ya kupulizia puto ya katheta.
  7. Katheta safi yenye ukubwa sahihi; ukubwa wa katheta unaotumika kwa kawaida ni 16FK (FK au Foleyi ya Kathetha ni kipimo kinachotumika kuonyesha ukubwa wa katheta). Katheta huwa katika kifurushi safi cha plastiki (ambacho hakijaonyeshwa katika Mchoro 22.7). Tazama mrija wa upande unaounganishwa na puto inayoweza kupanuka kwenye ncha ya katheta.
  8. Chanzo bora cha mwangaza. Tochi inayotumia betri inaweza kutumika, lakini itakubidi umwambie mtu mwingine aishikilie
  9. Nguo ya kumfunika mwanamke sehemu ya chini ya mwili.

22.4.2 Hatua katika utaratibu wa kuingiza katheta

  • Je, ni jambo gani la kwanza unafaa kufanya kabla ya kufungua kifurushi chochote safi?

  • Kwa takriban sekunde 15, osha mikono yako kabisa kwa sabuni na maji.

    Mwisho wa jibu

Baada ya mgonjwa wako kuwa tayari na kufahamu matukio yatakayofuata, na vifaa vyako vimetayarishwa, vaa glavu safi kisha upanguze karibu na vulva na eneo la nje ya vulva ukitumia mchanganyiko wa antiseptiki au alkoholi, ukianzia kwenye uwazi wa urethra ukielekea upande (Mchoro 22.8a). Ikiwa hauna mchanganyiko wa antiseptiki, safisha eneo hili kikamilifu ukitumia sabuni na maji.

Mchoro 22.8 (a) Panguza sehemu ya karibu na vulva na periniamu kwa pamba iliyotumbukizwa ndani ya alkoholi. (b) Kwa upole, vuta labia kubwa ili kuona uwazi wa urethra kisha uingize katheta.
  • Unafikiri ni kwa nini ni muhimu kupanguza eneo hili ukianzia uwazi wa urethra kisha kuelekea upande wa nje?

  • Hatua hii huzuia kupanguza viini vya maradhi kutoka sehemu za periniamu kuelekea kwenye uwazi wa urethra. Ukipanguza kuelekea urethra, viini hivi vinaweza kubebwa hadi ndani ya mwili wakati katheta inapoingizwa.

    Mwisho ya jibu

Tumia mkono wako usio na nguvu nyingi kuvuta labia kubwa nyuma ili uwazi wa urethra uonekane. (Unaweza kurejelea mchoro wa kina kuhusu sehemu ya nje ya uke katika Mchoro wa 3.2 katika Kipindi cha 3. Lainisha katheta ya FK16 ikiwa una mafuta yanayofaa (usitumie kitu kingine) kisha uiingize polepole kwenye uwazi wa urethra (Mchoro 22.8b).

Punde tu baada ya katheta kuingia vizuri kwenye kibofu utaona mkojo ukitiririka kwenye katheta. Tumia sirinji kuingiza milimita 5 ya maji safi kwenye mrija unaoelekea kwenye puto; jambo hili litafanya kifuko hiki “kifure” na kusababisha katheta kushikilia kwenye kibofu hivyo haiwezi kutoka wakati mgonjwa anatembea (tazama Mchoro 22.9). Vuta katheta kwa utaratibu ili kuhisi jinsi ilivojishikilia kwenye kibofu.

Mchoro 2.9 Sehemu nusu ya kaviti ya pelvisi ya mwanamke ikionyesha katheta ilivyojishikilia kwenye kibofu kufuatia kufurishwa kwa puto la katheta.

Unganisha katheta na neli safi ya kupitishia mkojo ili mkojo utiririke kwenye kifuko cha kukusanyia. Hakikisha kuwa kifuko hiki kimewekwa chini ya kibofu, la sivyo mkojo hautatiririkia ndani ya kifuko. Ikiwa hauna kifuko safi cha kukusanyia, basi acha mkojo utiririkie kwenye chombo safi. Mbinu hii huitwa mfumo 'wazi' na huwa na hatari ya maambukizi kupitia katika njia ya mkojo hadi katika kibofu. Kwa kawaida, njia ya mkojo inafaa kuwa ya mfumo 'uliofungwa' huku mkojo ukitiririka ndani ya kifuko safi.

Punde tu baada ya kukamilisha utaratibu huu, mpe mwanamke huyu rufaa hadi katika kituo cha afya cha kiwango cha juu. Ikiwezekana, andamana naye.

22.4.2 Utunzaji wa ujumla wa mtu aliyeingizwa katheta

Unapomtunza mwanamke aliyeingizwa katheta, fahamu kuwa anaweza kuhisi usumbufu kwenye sehemu ya kibofu. Mtulize kwa kumweleza umuhimu wa katheta ili asiwe na wasiwasi.

Unapaswa pia kumdumishia usafi kwa kupanguza mkojo wowote uliovuja kutoka kwa katheta; mkojo huu unaweza kumlowesha na kumuaibisha, au kusababisha mwasho kwenye ngozi yake hivyo kuongeza wasiwasi.

22.4.3 Kuondoa katheta

Wakati wa kuondoa katheta ukifika, tayarisha vifaa muhimu kwenye sinia au sahani safi kabisa.

  • Vifaa utakavyohitaji ni glavu safi au zilizosafishwa, na sirinji ya kutoa maji ndani ya puto ya katheta.
  • Mweleze mgonjwa huyu kuwa utaondoa katheta hivyo anaweza kuhisi usumbufu mdogo. Vaa glavu na utumie sirinji kuvuta maji ili kuizima puto bila kutenganisha mrija wa kupishia mkojo. Baada ya kuvuta maji yote ndani ya sindano, vuta katheta nje kwa utaratibu.

Mweleze mwanamke huyu kuwa anaweza kuhisi uchungu mdogo anapokojoa kwa njia ya kawaida nyakati chache za kwanza, lakini kibofu chake kitafanya kazi kama kawaida baada ya muda mfupi.

22.5 Hitimisho

Huu ndio mwisho wa moduli ya Utunzaji katika Ujauzito. Umejifunza mambo mengi katika vipindi 22 vilivyopita kuhusu jinsi ya kumtunza mwanamke mjamzito aliye na afya njema na mimba yake inaendelea kwa kawaida. Pia umejifunza kuhusu hatua unazofaa kutekeleza unapotambua ishara na dalili zozote za hatari. Maarifa na ujuzi wako unaweza kuzuia matatizo mengi na kuokoa maisha ya wanawake na watoto wasiozaliwa wanaojipata kwenye matatizo. Katika moduli inayofuatia utajifunza kuhusu Utunzaji katika Leba na Kuzaa

Muhtasari wa Kipindi cha 22

Katika kipindi cha 22 umejifunza kuwa:

  1. Matibabu ya kudunga viowevu mishipani huhitajika kwa mwanamke mjamzito ili kuchukua nafasi ya viowevu vinavyopotezwa kufuatia kuvuja damu nyingi.
  2. Matibabu ya kudungia viowevu mishipani huhusisha; kufahamu jinsi ya kukusanya vifaa muhimu, kutambua sehemu ya kudunga mshipa, kuingiza kanula mishipani na kuidhibiti na kudumisha kiwango cha kasi ya mtiririko wa viowevu katika mfumo wa damu ya mwanamke.
  3. Sababu za kusitisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani ni pamoja na: shinikizo la damu na mpigo wa moyo kurejea hali ya kawaida, viowevu kuvujia ndani ya tishu na karibu na sehemu iliyodungwa badala ya kuenda mishipani, dalili za maambukizi karibu na sehemu iliyodungwa au mwanamke akipata viowevu vingi kupita kiasi na anaonyesha ishara ya kuwa moyo au mapafu yake yanaweza kuwa yameathirika.
  4. Kuingiza katheta ndani ya kibofu huhusisha kutia mpira safi au mrija wa plastiki ndani ya kibofu kupitia kwenye urethra ili kuondoa mkojo. Utaratibu huu ni muhimu kibofu kikifura kutokana na kizuizi kinachozuia mwanamke kukojoa kwa njia ya kawaida, kwa mfano, wakati wa leba iliyodumu kwa muda mrefu au iliyozuiliwa.
  5. Katheta hushikishwa kwenye kibofu kwa kudungia maji safi kwenye puto ya katheta ili kufurisha na kufanya ijishikishe ndani ya kibofu.
  6. Mfumo uliofungwa ni muhimu katika kukusanyia mkojo. Mfumo wazi unaweza kusababisha maambukizi kuingia ndani ya kibofu kupitia kwenye mrija.
  7. Utaratibu wa kudhibiti maambukizi unafaa kuzingatiwa kila wakati unapopeana matibabu ya kudungia viowevu mishipani au unapoingiza katheta ndani ya kibofu; Nawa mikono kabisa kabla na baada ya taratibu hizi, vaa glavu safi na upanguze sehemu ya ngozi inayokaribia eneo la kuingizia katheta au ya kudungia viowevu ukitumia mchanganyiko wa antiseptiki au alkoholi kabla ya kuingiza kanula au katheta ya mkojo.
  8. Hakikisha kuwa umemweleza mgonjwa yale unayotaka kufanya kabla ya kufanya taratibu hizi, na umweleze umuhimu wa kusaidiwa kwa njia hiyo.
  9. Punde tu baada ya kukamilisha matibabu haya, mpe mwanamke rufaa hadi katika kituo cha afya cha kiwango cha juu haraka iwezekanavyo. Ikiwezekana, andamana naye.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 22

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini jinsi ulivyofanikisha Malengo ya Somo hili kwa kujibu maswali yanayofuatia. Andika majibu yako kwenye Shajara yako ya Masomo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Kikao Saidizi kitakachofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na Muhtasari katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini la 22.1 (linatathmini Malengo ya Somo 22.1, 22.2, 22.3, 22.4, 22.5 na 22.6)

Ni maelezo yapi kati ya yafuatayo ambayo si kweli? Katika kila kauli, eleza lisilo la kweli.

  • A.Mwanamke aliye katika hali ya mshtuko kufuatia kuvuja damu nyingi anafaa kupewa rufaa haraka bila kuanzishiwa matibabu ya kudungia viowevu mishipani.
  • B.Ikiwa eneo lililodungwa litafura na kuwa chungu, ondoa kanula kisha uiweke mahali pengine.
  • C.Ikiwa hauna plasta ya kubandikia juu ya sehemu iliyodungwa, hakuna haja ya kudhibiti kanula mshipani.
  • D.Ikiwa shinikizo la damu na mpigo wa moyo wa mwanamke umerejea hali ya kawaida na havuji damu tena, unaweza kusitisha viowevu.
  • E.Sirinji hutumika kuingiza maji safi kwenye kifuko cha kukusanyia mkojo unaotoka kwenye kibofu na kupitia kwenye mrija.
  • F.Nawa mikono yako kabisa kwa sabuni na maji kabla ya kumgusa mgonjwa au kifaa chochote.
  • G.Kima cha mtiririko kinafaa kuwa cha haraka iwezekanavyo unapoanzisha matibabu ya kudungia viowevu mshipani mwa mwanamke aliye katika hali ya mshtuko.
Answer

A si kweli. Mwanamke aliye katika hali ya mshtuko (shinikizo la chini la damu na mpigo wa haraka wa moyo) kutokana na kupoteza damu huhitaji kuanzishiwa matibabu ya kudungia viowevu mishipani kabla ya kupewa rufaa.

B ni kweli. Ikiwa eneo lililodungwa limefura na ni chungu, unafaa kuondoa kanula na kuidungia mahali pengine. Hii inaonyesha kuwa viowevu vinaingia ndani ya tishu badala ya mshipa.

C si kweli. Ikiwa huna plasta ya kubandikia juu ya eneo lililodungwa, unapaswa kudhibiti kanula kwa kuifunga kwa nguo safi. Kanula inaweza kutoka nje ya mshipa ikiwa haitadhibitiwa.

D ni kweli. Ikiwa shinikizo la damu na mpigo wa moyo wa mwanamke umerejea hali ya kawaida na havuji damu tena unaweza kusitisha viowevu.

E si kweli. Sirinji ni ya kuingizia maji safi kwenye puto la katheta (si kwenye kifuko cha kukusanyia mkojo) ili kufurisha puto na kufanya katheta isalie ndani ya kibofu.

F ni kweli. Kabla hujamgusa mgonjwa au kifaa chochote, unafaa kunawa mikono kabisa kwa sabuni na maji.

G ni kweli. Kima cha mtiririko katika mwanamke aliye katika hali ya mshtuko kinafaa kuwa cha haraka iwezekanavyo punde tu unapomwanzishia matibabu ya kudungia viowevu mishipani wake.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 22.2 (linatathmini Malengo ya Somo 22.1, 22.3 na 22.6)

Panga upya orodha ifuatayo katika utaratibu sahihi wa hatua unazofaa kuchukua unapoanza matibabu ya kudungia viowevu mishipani.

Using the following two lists, match each numbered item with the correct letter.

  1. Nawa mikono yako.

  2. Mlaze mgonjwa

  3. Vaa glavu safi.

  4. Tambua sehemu unayoweza kuingizia kanula.

  5. Fungilia fundo la kuzuia damu hadi takriban upana wa vidole vitatu juu ya eneo hili.

  6. Safisha eneo utakalodunga ukitumia antiseptiki, alkoholi au sabuni na maji.

  7. Chukua kanula kutoka kwenye kifurushi safi kisha uiingize mishipani katika sehemu uliyochagua, kisha uondoe sindano huku ukiiacha kanula ya plastiki mishipani.

  8. Fungua kifurushi cha mrija safi kisha ukiunganishe na kifuko cha viowevu, halafu ukininginize juu ya mgonjwa au umwagize mtu yeyote akishikilie juu yake.

  9. Unganisha kanula na kifuko kilicho na viowevu kisha ufungue klampu ya duara.

  • a.5.

  • b.9.

  • c.8.

  • d.3.

  • e.1.

  • f.2.

  • g.7.

  • h.6.

  • i.4.

The correct answers are:
  • 1 = e
  • 2 = f
  • 3 = d
  • 4 = i
  • 5 = a
  • 6 = h
  • 7 = g
  • 8 = c
  • 9 = b

Swali la kujitathmini 22.3 (linatathmini Malengo ya Somo 22.1, 22.2 na 22.5)

Fasili kuingiza katheta na umuhimu wake kwa mwanamke mjamzito aliye katika leba. Orodhesha angalau vifaa vitano unavyohitaji ili kufanya utaratibu huu.

Answer

Kuingiza katheta ndani ya kibofu ni kutia mpira safi au mrija wa plastiki ndani ya kibofu kupitia kwenye urethra ili kuondoa mkojo wakati kibofu kimezuiwa. Kibofu kinaweza kuzuiliwa katika leba inayodumu kwa muda mrefu ama leba iliyozuiliwa mtoto akifinya urethra na kufunga mtiririko wa kawaida wa mkojo.

Vifaa unavyohitaji ni:

  • Katheta safi yenye ukubwa sahihi (FK16)
  • Mrija safi wa kufyonza na kifuko cha kukusanyia mkojo
  • Sirinji iliyo na maji safi ya kufurisha puto ya katheta
  • Glavu safi
  • Alkoholi au mchanganyiko wa antiseptiki na pamba.
  • Mrija wa mafuta ya kulainisha
  • Mwangaza
  • Nguo ya kumfunika mwanamke sehemu ya chini ya mwili

Mwisho wa jibu