Skip to main content
Printable page generated Wednesday, 29 Mar 2023, 12:06
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2023 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Wednesday, 29 Mar 2023, 12:06

8. Milalo Isiyo ya kawaida na mimba ya Zaidi ya mtoto mmoja

Kipindi cha 8 cha Somo Milalo Isiyo ya kawaida na mimba ya zaidi ya mtoto mmoja

Utangulizi

Vipindi vya masomo vya hapo awali vilitanguliza ufafanuzi, ishara, dalili na awamu za leba ya kawaida. Pia ulijifunza kuhusu fetasi kutanguliza veteksi kikawaida katika kuzaa. Katika Kipindi hiki cha somo utajifunza kuhusu milalo isiyo ya kawaida inayotokea sana (ya kutanguliza matako, bega, uso, au paji la uso). Pia utajifunza mbinu za kuitambua na hatua zinazohitajika kwa kuzuia matatizo yanayotokea katika leba. Wakati mwingine uzazi huzuilika kwa sababu mtoto yuko katika mlalo usio wa kawaida. Hatua ya dharura inaweza kuokoa maisha ya mama na mtoto wake. Pia utajifunza kuhusu uzazi wa pacha. Watoto hawa wawili hufungamana pamoja na hii humzuia yeyote kuzaliwa. Iwapo watoto watafungamana, matatizo yanaweza kutokea.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 8

Baada ya Kipindi hiki cha somo utaweza:

8.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandika kwa herufi nzito. (Maswali ya kujitathmini 8.1 na 8.2)

8.2 Kueleza jinsi ya kutambua fetasi iliyotanguliza veteksi. Tambua veteksi kwenye fetasi iliyo katika mlalo mbaya na isiyokuwa katika nafasi ya kawaida. (Maswali ya kujitathmini 8.1 na 8.2)

8.3 Kueleza visababishi na matatizo ya fetasi na mama kutokana na mlalo mbaya wa fetasi katika leba ya mimba iliyokomaa. (Swali la kujitathmini 8.3)

8.4 Kuelezea jinsi ya kutambua mimba ya zaidi ya mtoto mmoja na matatizo yanayoweza kutokea. (Swali la kujitathmini 8.4)

8.5 Kueleza lini na jinsi ya kumpa rufaa mwanamke mwenye leba kutokana na mlalo usio wa kawaida wa fetasi au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja. (Swali la kujitathmini 8.4)

8.1 Milalo ya kawaida na isiyo ya kawaida

8.1.1 Mlalo wa kutanguliza veteksi

Katika takriban asilimia 95 ya uzazi, sehemu ya fetasi inayotangulia ukingoni mwa pelvisi ni sehemu iliyo juu zaidi ya kichwa cha fetasi. Sehemu hii ya kichwa huitwa veteksi (Picha 8.1). Hali hii huitwa mlalo wa kutanguliza veteksi. Tambua kuwa kidevu cha mtoto kimepindwa kuelekea kwenye kifua chake. Veteksi ndiyo sehemu inayotangulia kuingia kwenye pelvisi ya mama. Katika nafasi na hali hii, kichwa cha mtoto husemekana kuwa “kimejikunja vizuri”.

Picha 8.1 Mtoto aliyejikunja vizuri katika mlalo wa kutanguliza veteksi kabla ya kuzaliwa, kuhusiana na pelvisi ya mama. (Imetolewa: Shirika la Afya Duniani, Kudhibiti Matatizo katika Ujauzito na Kuzaa.)

Mwanzoni mwa ujauzito, mtoto hugeuzwa upande mwingine. Upande wa chini wa mtoto huelekezwa chini kuelekea seviksi ya mama. Mlalo huu huitwa wa kutanguliza matako. Mwanzoni mwa kukua, kichwa cha fetasi huwa kikubwa kuliko matako yake. Mara nyingi kichwa huchukua kaviti pana zaidi, yaani fandasi ya uterasi. Fetasi inapoendelea kuwa kubwa, matako huwa makubwa kuliko kichwa. Mtoto hugeuza mlalo wake mwenyewe ambapo matako yake sasa huchukua fandasi. Kwa ufupi, mwanzoni mwa ujauzito fetasi nyingi huwa katika mlalo wa kutanguliza matako. Baadaye katika ujauzito, fetasi nyingi hujipindua na kutanguliza veteksi.

8.1.2 Milalo mibaya

Utajifunza kuhusu leba iliyozuiliwa katika Kipindi cha 9 cha Somo.

Mtoto anaweza kujitokeza kwenye pelvisi ya mama katika hali nyingine mbali na kutanguliza veteksi. Aina hii ya mlalo huitwa mlalo usio wa kawaida au mlalo mbaya. Milalo hii ina hatari zaidi ya kuzuiliwa na matatizo mengine ya uzazi kuliko mlalo wa kutanguliza veteksi. Aina za mlalo mbaya zinazotokea maranyingi ni kutanguliza matako, bega, uso au paji la uso. Tutajadili kila moja katika Kipindi hiki. Kumbuka kuwa mtoto anaweza kuwa “kichwa kikiwa chini” lakini katika mlalo usio wa kawaida. Mifano ni kutanguliza uso au paji la uso katika hali ambapo uso au paji la uso wa mtoto ndiyo kitangulizi.

8.1.3 Kutokuwa katika nafasi ya kawaida

Mtoto anaweza pia kuwa katika nafasi isiyo ya kawaida hata akiwa ametanguliza veteksi. Inaweza kuwa vigumu kugundua inapotendeka. Katika uzazi wa kawaida, wakati kichwa cha mtoto kimekabiliwa kwenye pelvisi, upande wa nyuma wa fuvu la kichwa cha mtoto huelekezwa upande wa mbele wa pelvisi ya mama. Upande wa nyuma wa fuvu la kichwa cha mtoto huitwa kisogo. Upande wa mbele ya pelvisi ya mama huitwa simfisisi ya kinena.Simfisisi ya kinena ni mahali ambapo mifupa miwili ya kinena inaungana pamoja. Hali hii ya fuvu la kichwa cha fetasi huitwa hali ya kisogo kuwa upande wa mbele (Picha 8.2a). Ikiwa kisogo cha fuvu la kichwa cha mtoto kinaelekea upande wa nyuma wa mama, hali hii ya kisogo kuwa upande wa nyuma (Picha 8.2b) ni veteksi kutokuwa katika nafasi ya kawaida. Ni vigumu zaidi kwa mtoto kuzaliwa akiwa katika hali hii. Uzuri ni kwamba zaidi ya takriban asilimia 90 ya watoto ambao veteksi haiko katika nafasi yake huzunguka na kuwa katika hali ya kisogo kuwa upande wa mbele na kuzaliwa kikawaida.

Ulijifunza nafasi za mwelekeo: mbele na nyuma katika Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito, sehemu ya 1, Kipindi cha 3.

Tambua kwamba fuvu la kichwa cha mtoto pia linaweza kulazwa upande wa kushoto au wa kulia katika hali ya kisogo kuwa upande wa mbele au upande wa nyuma.

Picha 8.2 Hali zinazowezekana za fuvu la kichwa cha fetasi mtoto atangulizapo veteksi wakati mama amelala chali: (a) Hali ya kawaida “isiyopinda” ya kisogo kuwa upande wa mbele ambapo mtoto anaweza kuzaliwa kwa urahisi sana. (b) Hali ya kutokuwa katika nafasi ya kawaida na “isiyopinda” ya kisogo kuwa upande wa nyuma hufanya kuzaa kuwe na ugumu zaidi. (Imetolewa: Kwa heshima ya Mikael Häggström, imefikiwa kwenye http://commons.wikimedia.org/ wiki/ File:Cephalic_presentation_-_straight_occipito-anterior.png)

8.2 Visababishi na athari za milalo mibaya na hali ya kutokuwa katika nafasi ya kawaida 

Unaweza kukosa kutambua ni kwa nini mtoto yuko katika mlalo usio wa kawaida au katika nafasi isiyo ya kawaida wakati wa kuzaa. Hata hivyo, hali hizihuongeza hatari ya mlalo mbaya na kutokuwa katika nafasi ya kawaida:

Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja ndio mahusiko ya sehemu ya 8.7 ya Kipindi hiki. Ulijifunza kuhusu plasenta privia katika Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito, Kipindi cha 21.

  • Kiowevu cha amnioni kingi au kidogo zaidi.
  • Tyuma kwenye uterasi inayozuia fetasi kupinduka kutoka katika mlalo wa kutanguliza matako hadi ule wa kutanguliza veteksi katika siku za mwisho wa ujauzito. (Tyuma ni tishu inayokua katika hali isiyo ya kawaida.)
  • Umbo lisilo la kawaida la pelvisi.
  • Rusu za misuli zilizolegea kwenye kuta za uterasi.
  • Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja.
  • Plasenta privia (plasenta iliyofunika mwanya wa seviksi kabisa au kwa kiasi).

Iwapo mtoto anajitokeza katika mlalo au nafasi isiyo ya kawaida, inaweza kuwa vigumu kukamilisha miendo saba mikuu. Ulijifunza kuhusu miendo hii katika Vipindi vya 3 na 5. Hatimaye, uzazi huwa mgumu zaidi na hatari ya matatizo haya huongezeka.

Ulijifunza kuhusu kupasuka kwa membrani kabla ya muda wake katika Kipindi cha 17 cha Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito, sehemu ya 2.

  • Kupasuka kwa membrani za fetasi kabla muda wake.
  • Leba kabla ya muda wake.
  • Mikazo ya polepole, isiyotabirika na unaodumu kwa muda mfupi.
  • Mikazo isiyopatana na yenye uchungu zaidi, na leba kuendelea pole pole au kutoendelea kabisa.
  • Leba iliyokaa kwa muda mrefu na iliyozuiliwa, inayoweza kusababisha kupasuka kwa uterasi (Vipindi vya 9 na 10).
  • Kutokwa na damu baada ya kuzaa (Kipindi cha 11) .
  • Kuathirika kwa fetasi na mama kunakoweza kusababisha kifo cha mtoto na/au mama.

Kumbuka matatizo haya unapojifunza kuhusu aina zinazotokea mara nyingi za mlalo mbaya na jinsi ya kuzitambua.

8.3 Mlalo wa kutanguliza matako

Katika mlalo wa kutanguliza matako, fetasi hujilaza matako yake yakiwa nyuma. Matako na/au miguu ndizo sehemu zinazotangulia wakati wa kuzaliwa. Mlalo wa kutanguliza matako hutokea katika takriban asilimia 3-4 za uzazi unaotendeka baada ya wiki 34 ya ujauzito.

  • Je, ni lini ambapo mlalo wa kutanguliza matako huwa nafasi ya kawaida kwa fetasi?

  • Mwanzoni mwa ujauzito, matako ya mtoto huelekezwa chini kuelekea kwenye seviksi ya mama. Kichwa ndicho sehemu kubwa zaida katika awamu hii ya ukuaji. Kichwa chake huwa kwenye fandasi ya uterasi, ambayo ndiyo sehemu pana zaidi ya kaviti ya uterasi.

    Mwisho wa jibu

8.3.1 Visababishi vya mlalo wa kutanguliza matako

Unaweza kuona kulala kingamo katika Picha 8.7 baadaye katika Kipindi hiki.

Katika hali nyingi, huoni sababu dhahiri inayoweza kuifanya fetasi kutanguliza matako baada ya muda kamili wa ujauzito. Mara nyingi mlalo wa kutanguliza matako wakati wa kuzaa huhusishwa na fetasi kulala kingamo mwanzoni mwa ujauzito. Kulala kingamo humaanisha kuwa fetasi imelala kwa upande kutoka upande mmoja hadi mwingine wa fumbatio ya mama, na imeangalia plasenta iliyojipandikiza kwa upande. Plasenta ikiwa mbele ya uso wa mtoto, inaweza kuzuia mchakato wa kawaida wa kupinduka. Wakati wa kupinduka mtoto hugeuza kichwa chini anapoendelea kuwa mkubwa katika ujauzito. Kutokana na haya, mtoto hugeuka kwa upande huo mwingine na kuishia katika mlalo wa kutanguliza matako. Mlalo wa kutanguliza matako katika leba unaweza pia kusababishwa na mambo haya:

  • Leba ya kabla ya muda wake ambayo huanza kabla ya mtoto kujipindua kutoka mlalo wa kutanguliza matako hadi ule wa kutanguliza veteksi.
  • Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja, inaweza kuzuia kupinduka kikawaida kwa mtoto mmoja au wote wawili.
  • Polihadromino: kiasi kingi cha kiowevu cha amnioni. Kichwa cha fetasi hakiwezi kukabiliana na seviksi ya mama.
  • Hidrosefalasi “maji kwenye ubongo”. Kichwa cha fetasi ni kikubwa kupita kiasi kutokana na kuongezeka kupita kiasi kwa kiowevu kwenye ubongo.
  • Plasenta privia.
  • Kuzaa mtoto aliyekuwa katika mlalo wa kutanguliza matako katika mimba ya hapo awali.
  • Uterasi isiyojengeka kikawaida.

8.3.2 Utambuzi wa mlalo wa kutanguliza matako

Kutambua mlalo wa kutanguliza matako, tomasa fumbatio. Hisi kichwa cha fetasi juu ya kitovu cha mama. Kichwa huhisika kama bonge gumu, laini na lenye umbo la mviringo utakalohisi likisonga kwa upole katikati ya mikono yako.

  • Je, kwa nini unafikiri kuwa bonge linalosonga hapo juu kwenye fumbatio ni dalili ya mlalo wa kutanguliza matako? (Ulijifunza haya katika Kipindi cha 11 cha Somo cha Moduli ya Utunzaji katika ujauzito.)

  • Kichwa cha mtoto kinaweza kutingika kidogo kwa sababu ya ulegevu wa shingo la mtoto. Kwa hivyo ukihisi bonge la mviringo linalosongakwenye upande wajuu wa kitovu cha mama, kuna uwezekano mkubwa kuwa ni kichwa cha mtoto. Ikiwa mtoto yuko “chini juu” katika mlalo wa kutanguliza veteksi, mgongo wake wote husonga ukijaribu kutikisa sehemu za fetasi zilizo kwenye fandasi (Picha 8.3).

    Mwisho wa jibu

Picha 8.3 (a) Mgongo wote wa mtoto aliyetanguliza veteksi husonga ukiutikisa kwenye fandasi; (b) Kichwa kinaweza kutingika ilhali mgongo usitingike katika mlalo wa kutanguliza matako

Baada ya fetasi kukabiliwa na leba kuanza, unaweza kuhisi matako ya mtoto yakiwa laini na yenye umbo lisilotabirika wakati wa uchunguzi wa ukeni. Huhisi tofauti na lile bonge la mviringo la fuvu la kichwa cha fetasi katika mlalo wa kutanguliza veteksi. Membreni za fetasi zinapopasuka, unaweza kuhisi matako na /au miguu dhahiri zaidi. Unaweza kuhisi mkundu wa mtoto. Unaweza kuona mekoniamu mbichi, nzito nyeusi kwenye kidole chako unachochunguzia. Ikiwa miguu ya mtoto imenyooka, unaweza kuhisi sehemu ya siri. Huenda ukaweza kujua jinsia ya mtoto huyo kabla ajazaliwa.

8.3.3 Aina za mlalo wa kutanguliza matako

Aina tatu za mlalo wa kutanguliza matako zimeelezewa katika Picha 8.4:

  • Wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi ya mama: Miguu imekunjwa kwenye viungo vya nyonga na magoti, ndiposa miguu imekunjwa chini ya mtoto.
  • Wenye matako ya mtoto juu ya seviksi ya mama: Ndiyo aina ya mlalo wa kutanguliza matako inayotokea sana. Katika mtako wazi, kiungo cha nyonga zimekunjwa na kiungo cha goti zimenyooshwa. Miguu yote ya mtoto imeelekezwa upande wa juu bila kupinda.
  • Wenye mguu au miguu ya mtoto juu ya seviksi ya mama: Mguu mmoja au yote imenyooshwa kwenye jointi za nyonga na magoti na mtoto kutanguliza “mguu kwanza”.
Picha 8.4 Aina tofauti za mlalo wa kutanguliza matako. (Imetolewa: Shirika la Afya Duniani, kama ilivyo katika Picha 8.1).

8.3.4 Hatari za mlalo wa kutanguliza matako

Wape rufaa wote walio na hali ambazo mtoto ametanguliza matako waende katika kituo cha afya cha ngazi ya juu kilicho karibu.

Aina zote za mlalo wa kutanguliza matako husababisha hatari kuu kwa mtoto:

  • Kichwa cha fetasi hukwama kabla ya kuzaliwa.
  • Leba huzuiliwa fetasi iwapo kubwa kutolingana na ukubwa wa pelvisi ya mama.
  • Prolapsi ya kiungamwana (kuchomoza kwa kiungamwana) inaweza kutokea. Kiungamwana kinasukumwa nje kabla ya mtoto na kinaweza kubaniwa kwenye ukuta wa sevikisi au uke.
  • Plasenta inaweza kutenganishwa kutoka mahali pa plasenta kabla ya muda wake. (Huitwa kuchubuka kwa plasenta.)
  • Mtoto kujeruhiwa anapozaliwa. Kwa mfano kuvunjika mikono au miguu, kuharibika kwa neva, kuumia kwa ogani za ndani na uti wa mgongo.

Uzazi wa mlalo wa kutanguliza matako unaweza kusababisha kujeruhiwa kwa njia ya uzazi ya mama au jenitalia za nje zinaweza kutanuliwa kupita kiasi kwa sababu sehemu za fetasi haziwezi kupita.

Prolapsi ya kiungamwana katika mlalo wa kawaida wa kutanguliza veteksi ilielezewa katika Kipindi cha 17 cha Somo cha Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito. Kuchubuka kwa Plasenta kulielezewa katika Kipindi cha 21 cha Somo.

  • Je, kuna athari gani kwa mtoto akikwama, leba imezuiliwa, kiungamwana kimechomoza au kukitokea kuchubuka kwa plasenta?

  • Matokeo ni haipoksia. Mtoto huyo hukoseshwa oksijeni na anaweza kukumbwa na kuharibika kwa ubongo kwa kudumu au afariki.

    Ulijifunza kuhusu visababishi na matokeo ya haipoksia katika Moduli ya utunzaji katika ujauzito.

    Mwisho wa jibu

8.4 Mlalo wa kutanguliza uso

Mlalo wa kutanguliza uso hutokea wakati shingo la mtoto limerefushwa (limekunjwa kuelekea nyuma) kiasi kwamba kisogo kinagusa uti wa mgongo wa mtoto huyo (Picha 8.5). Katika hali hii, uso wa mtoto ndio unaotangulia.

Picha 8.5 Mlalo wa kutanguliza uso. (a) Kidevu cha mtoto kimeangalia upande wa mbele wa pelvisi. (b) Kidevu kimeangalia upande wa uti wa mgongo wa mama (Imetolewa: Shirika la Afya Duniani, jinsi ilivyo katika Picha 8.1).

Mpe mama rufaa iwapo mtoto aliye katika mlalo wa kutanguliza uso huku kidevu chake kikiwa kimeangalia upande wa uti wa mgongo wa mama hatazunguka na hivyo basi leba kuendelea kwa muda mrefu.

Takribani mimba ya 1 kwa kila 500 inayotimiza muda kamili huwa katika mlalo wa kutanguliza uso. Picha 8.5 yaonyesha jinsi kichwa kilivyojikunja shingoni. Watoto wanaojitokeza katika hali ambapo kidevu kimeangalia upande wa uti wa mgongo wa mama (Picha 8.5b) kwa kawaida huzunguka wenyewe katika leba. Wanajiweka katika hali ya “kidevu mbele”, ambayo hurahisisha kuzaliwa kwao. Hata hivyo wasipozunguka na kujiweka katika hali ya kidevu upande wa mbele wa pelvisi, huenda wasizaliwe kupitia ukeni. Kidevu cha mtoto hukwama kwenye sakramu ya mama. (Sakramu ni mfupa uliobinuka nyuma ya pelvisi.) Mtoto aliye katika hali hii lazima azaliwe kupitia upasuaji.

8.4.1 Visababishi vya mlalo wa kutanguliza uso

Visababishi vya mlalo wa kutanguliza uso ni sawa na vile vya mlalo wa kutanguliza matako:

  • Ulegevu wa uterasi baada ya ujauzito mwingi uliokomaa hapo awali
  • mimba ya pacha
  • Polihadromino (kiowevu cha amnioni kingi kupita kiasi)
  • Matatizo ya kuzaliwa ya mtoto (kwa mfano anensefalia, yaani kukosekana au kutokua vizuri kwa mifupa ya fuvu la kichwa)
  • Umbo lisilo la kawaida la pelvisi ya mama

8.4.2 Utambuzi wa mlalo wa kutanguliza uso

Huenda usigundue mlalo wa kutanguliza uso unapotomasa fumbatio la mama. Ikiwa kidevu kimeangalia upande wa nyuma, ugunduzi ni mgumu. Unapochunguza fumbatio, unaweza kuhisi umbo lisilo la kawaida. Uti wa fetasi huwa umejipinda katika umbo la S. Unapofanya uchunguzi ukeni, unaweza kugundua mlalo wa kutanguliza uso kwa msingi wa sababu hizi:

  • Sehemu inayotangulia imeinuka, huwa laini na yenye umbo lisilotabirika.
  • Unaweza kugusa sehemu za uso seviksi ikiwa imepanuka kikamilifu. Unaweza kugusa vigongo vya obiti juu ya macho, pua au kinywa, fizi au mfupa wa kidevu.
  • Membreni zikipasuka, mtoto anaweza kunyonya kidole chako cha kuchunguzia!

Hata hivyo, leba inapoendelea, uso wa mtoto hupata edema (kufura kutokana na kujaa kwa viowevu). Hali hii hufanya iwe vigumu kuutofautisha na umbo laini unalogusa katika mlalo wa kutanguliza matako.

8.4.3 Matatizo ya mlalo wa kutanguliza uso

Matatizo kwa fetasi ni haya:

  • Leba iliyozuiliwa na uterasi iliyopasuka
  • Prolapsi ya kiungamwana
  • Majeraha ya uso
  • Kuvuja damu ubongoni (kutokwa na damu kwenye fuvu la kichwa)

8.5 Mlalo wa kutanguliza paji la uso

Picha 8.6 Mlalo wa kutanguliza paji la uso (Imetolewa: Shirika la Afya Duniani, jinsi ilivyo kwenye Picha 8.1)

Katika mlalo wa kutanguliza paji la uso, kichwa cha mtoto huwa kimerefuka kidogo shingoni (ikilinganishwa na kilivyo katika mlalo wa kutanguliza uso). Kwa hivyo, paji lake la uso ndiyo sehemu inayotangulia (Picha 8.6). Mlalo huu hautokei sana. Ni 1 tu kwa uzazi 1000 uliokomaa ambao huwa katika mlalo wa kutanguliza paji la uso.

8.5.1 Vinavyoweza kusababisha mlalo wa kutanguliza paji la uso

Umeona mambo haya yote kama visababishi vya milalo mingine mibaya:

  • Uterasi dhaifu kutokana na ujauzito komavu wa mara kwa mara
  • Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja
  • Polihadromino
  • Umbo lisilo la kawaida la pelvisi ya mama.

8.5.2 Utambuzi wa mlalo wa kutanguliza paji la uso

Mlalo wa kutanguliza paji la uso kwa kawaida haugunduliwi kabla ya mwanzo wa leba. Hata hivyo, wahudumu wa uzazi wenye uzoefu mwingi wanaweza kugundua mlalo wa kutanguliza paji la uso. Wakati wa uchunguzi wa fumbatio, kichwa huwa juu katika fumbatio la mama. Kichwa huonekana kikubwa mno na hakiteremki kuingia kwenye pelvisi, hata kukiwa na mikazo bora ya uterasi. Wakati wa kufanya uchunguzi ukeni, sehemu inayotangulia huwa juu na inaweza kuwa vigumu kuifikia. Unaweza kugusa mwanzo wa pua na macho. Lakini hauwezi kugusa kinywa, mwisho wa pua au kidevu. Pia unaweza kugusa fontaneli (utosi) ya mbele. Hata hivyo, baada ya saa fulani za kuwepo kwa leba, uvimbe mkubwa upande wa mbele ya fuvu la kichwa cha fetasi unaweza kuifunika alama hii.

Kumbuka wajihi wa uvimbe wa kawaida na fontaneli ya nyuma iliyoonyeshwa katika Picha 4.4.

8.5.3 Matatizo ya mlalo wa kutanguliza paji la uso

Matatizo ya mlalo wa kutanguliza paji la uso ni sawa na yale ya milalo mingine mibaya:

  • Leba iliyozuiliwa na uterasi iliyopasuka
  • Prolapsi ya kiungamwana
  • Kujeruhiwa kwa uso
  • Kuvuja damu ubongoni
  • Je, ni upi unoweza kukumbana nao: mlalo wa kutanguliza uso au paji la uso?

  • Mlalo wa kutanguliza uso hutokea sana. Huu hutokea katika mimba ya 1 kwa kila leba 500 zilizokomaa. Mlalo wa kutanguliza paji la uso hautokei sana, kwani hutokea katika ujauzito 1 kwa kila leba 1000 zilizokomaa.

    Mwisho wa jibu

8.6 Mlalo wa kutanguliza bega

Mlalo wa kutanguliza bega hautokei sana katika mimba iliyokomaa. Hata hivyo, mlalo wa kutanguliza bega hutokea iwapo fetasi imelala kingamano kwenye uterasi (Picha 8.7). Pengine haikukamilisha mvunguko ilipokuwa ikipinduka kutoka katika hali ya kutanguliza matako hadi kutanguliza veteksi. Labda imelala kingamano tangu mwanzoni mwa mimba. Mtoto akilala chali, huenda mgongo wake ndio kitangulizi. Iwapo mtoto amelala kifudifudi (ameangalia chini), mkono wake unaweza kujitokeza kupitia kwenye seviksi. Mtoto aliye katika hali ya kingamano hawezi kuzaliwa kupitia ukeni na leba hiyo huzuiliwa. Wape rufaa kwa haraka wenye watoto walio katika mlalo wa kutanguliza bega.

Usijaribu kumgeuza mtoto aliyeulalia upande wake.Isipokuwa mhudumu wa afya mwenye ujuzi amgeuze, mtoto huyo anafaa kuzaliwa kwa njia ya upasuaji.

Picha 8.7 Kujilaza kingamo (mlalo wa kutanguliza bega). Mtoto huyu hawezi kuteremka kwenye njia ya uzazi.

8.6.1 Visababishi vya mlalo wa kutanguliza bega

Mlalo wa kutanguliza bega unaweza kusababishwa na vipengele vinavyohusu mama au fetasi.

Vipengele vinavyomhusu mama ni:

  • Ulegevu (udhaifu) wa misuli ya fumbatio na uterasi: hasa baada ya mimba kadhaa za hapo awali.
  • Matatizo kwenye uterasi.
  • Pelvisi iliyokaza (nyembamba kupindukia).

Vipengele vinavyoihusu fetasi ni:

  • Leba kabla ya muda kamili wa mimba kutimia
  • Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja
  • Polihadromino
  • Plasenta privia
  • Je, “plasenta privia” na “polihadromino” huashiria nini?

  • Plasenta privia ni hali ya plasenta imeufunika mwanya wa seviksi kikamilifu au kwa kiasi. Polihadromino ni kiasi kingi cha kiowevu cha amnioni. Matatizo haya yote mawili yanaweza kusababisha milalo mibaya.

    Mwisho wa jibu

8.6.2 Utambuzi wa mlalo wa kutanguliza bega

Unapotomasa fumbatio uterasi huonekana kuwa pana na urefu wa fandasi ni mdogo kuliko inavyotarajiwa kwa kipindi hiki cha ujauzito. Urefu ni mdogo kwa sababu kichwa wala matako ya mtoto hayako kwenye fandasi. Kwa kawaida unaweza kuhisi kichwa kwenye upande mmoja wa fumbatio la mama. Wakati wa uchunguzi wa ukeni, huenda usihisi kitangulizi mwanzoni mwa leba. Lakini leba ikiendelea vizuri, unaweza kuhisi mbavu za mtoto. Bega linapoingia ukingoni mwa pelvisi, mkono wa mtoto unaweza kuchomoza na kuonekana nje ya uke.

8.6.3 Matatizo ya mlalo wa kutanguliza bega

Matatizo ni haya:

  • Prolapsi (kuchomoza) ya kiungamwana
  • Kuathirika kwa mkono uliochomoza
  • Leba iliozuiliwa na uterasi iliyopasuka
  • Haipoksia ya fetasi na kifo

Kumbuka kuwa mlalo wa kutanguliza bega una maana kuwa mtoto hawezi kuzaliwa kupitia ukeni. Ukigundua mlalo wa kutanguliza bega kwa mwanamke aliye tayari katika leba, mpe rufaa mara moja aende katika kituo cha afya cha kiwango cha juu.

Katika visa vyote vya mlalo mbaya au kutokuwa katika nafasi ya kawaida, usijaribu kumgeuza mtoto kwa kutumia mikono yako! Ni daktari au mkunga maalum aliyehitimu tu anayepaswa kujaribu kumgeuza mtoto. Mpe mama rufaa ili yeye pamoja na mtoto wake waweze kupata huduma ya dharura ya uzazi.

8.7 Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja

Sehemu hii inaeleza kuhusu mimba ya zaidi ya mtoto mmoja, ambayo ni zaidi ya fetasi moja kwenye uterasi. Zaidi ya asilimia 95 ya mimba ya zaidi ya mtoto mmoja ni pacha (fetasi mbili). Lakini unaweza pia kupata watatu (fetasi tatu), wanne (fetasi nne), watano (fetasi tano) na idadi zingine za juu. Uwezekano wa kupata zaidi ya fetasi moja hupunguka kulingana na ongezeko katika idadi ya fetasi. Visa vya kupata mapacha ni tofauti kwa kila nchi. Nchi zilizo Mashariki mwa Asia kama vile Japan na Uchina zina uwezekano mdogo wa visa vya upataji wa mapacha. Mashariki mwa Asia, 1 kati ya mimba 1000 ni pacha wa kidugu au pacha wasiofanana. Wafrika weusi wana uwezekano mkubwa wa kupata mapacha. Nchini Nigeria, 1 kati ya mimba 20 ni pacha wa kidugu. Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja huhusishwa sana na upotezaji wa mimba katika awamu ya kwanza na watoto kufariki wakati wa kuzaliwa, hasa kutokana na kuzaliwa kabla ya muda kamili wa mimba kumalizika.

8.7.1 Aina za mimba ya pacha

Mapacha wanaweza kufanana (wa monozaigoti) au wasifanane na wa kidugu (wa daizigoti). Mapacha wa monozaigoti hutokea kwenye yai moja lililotungishwa (zaigoti). Kwa hivyo wao huwa wa jinsia moja na hutumia plasenta moja. Kwa upande mwingine, mapacha wa daizigoti hutokana na zaigoti mbili tofauti. Kwa hivyo, wanaweza kuwa wa jinsia moja au la na pia wana plasenta tofauti. Picha 8.8 inaonyesha aina za mimba ya mapacha na mchakato wa kukua kwake.

Picha 8.8 Aina za mimba ya pacha: (a) Wa Kidugu au pacha wasiofanana ambao kila mmoja anayo plasenta yake. Hata hivyo, iwapo plasenta hizo zitakaribiana sana, zinaweza kuungana. (b) Pacha wanaofanana hutumia plasenta moja lakini kila mmoja anayo membreni yake ya fetasi.

8.7.2 Utambuzi wa mimba ya pacha

Wakati wa uchunguzi wa fumbatio, unaweza kutambua vitu hivi:

  • Uterasi ni kubwa zaidi ya inavyotarajiwa katika kipindi hicho mimba.
  • Uterasi inaonekana kuwa mviringo na pana na kusonga kwa fetasi kuonekana katika sehemu kubwa. (Muundo wa uterasi katika mimba iliyokoma wa mtoto mmoja aliye katika mlalo wa kutanguliza veteksi huonekana kuwa na umbo la moyo; kama mviringo upande wa juu na nyembamba upande wa chini).
  • Unaweza kuhisi vichwa viwili.
  • Midundo miwili ya moyo ya fetasi inaweza kusikika. Watu wawili wakisikiza kwa wakati mmoja na wasikie angalau midundo 10 tofauti, huenda kuna fetasi mbili (Picha 8.9).
  • Uchunguzi wa kutumia mawimbi sauti ya tiba unaweza kutoa utambuzi bora wa mimba ya pacha.
Picha 8.9 Watu wawili wanaweza kuwasikiza pacha, kwa kugonga kwa mwendo sawa na midundo ya mioyo ya hizo fetasi mbili.

8.7.3 Athari za mimba ya pacha

Wanawake walio na mimba ya pacha hutatizika sana na matatizo madogo madogo ya ujauzito kama vile kichefuchefu cha mjamzito asubuhi, kichefuchefu, na kiungulio. mimba ya pacha ni kisababishi kimoja cha hiparemisisi gravidaramu (kichefuchefu kingi na kutapika kupindukia katika ujauzito). Kina mama wa mapacha pia wamo katika hatari zaidi ya kupata anemia itokanayo na ukosefu wa ayoni na folati katika ujauzito.

  • Je, unaweza kupendekeza ni kwa nini anemia ni hatari kubwa katika mimba ya zaidi ya mtoto mmoja?

  • Lazima mama apate virutubishi vya kuwalisha watoto wawili (au zaidi). Ikiwa hapati ayoni na folati ya kutosha katika lishe yake au kupitia katika vyakula vya ziada, atapata anemia.

    Mwisho wa jibu

Matatizo mengine ni kama haya:

  • Matatizo ya hipatensheni yanayohusiana na ujauzito kama vile dalili zinazotangulia eklampsia (prekilampsia) na eclampsia (ugonjwa wa ujauzitoni) hutokea sana katika ujauzito.
  • Dalili za shinikizo zinaweza kutokea mwishoni mwa ujauzito kutokana na uzani na ukubwa ulioongezeka wa uterasi.
  • Leba kuanza yenyewe mapema na hatimaye kuzaa au membreni kupasuka kabla ya muda kamili wa ujauzito kutimia.
  • Ugumu katika kupumua (upungufu wa hewa kutokana na ukuaji wa haraka wa uterasi) ni tatizo jingine linalotokea sana.

Watoto pacha wanaweza kuwa wadogo ikilinganishwa na umri wa ujauzito huo. Watoto pacha wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo yanayohusiana na uzani wa chini wa kuzaliwa. (Matatizo haya ni kama kuwa wenye kuathiriwa na maambukizi kwa urahisi, kupoteza joto na ugumu katika kunyonya).

Utajifunza kwa kina kuhusu watoto waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini katika moduli ya Utunzaji baada ya kuzaa.

  • Mlalo mbaya hutokea sana katika mimba ya pacha. Pia, wanaweza kufungamana shingoni mmoja akiwa katika mlalo wa kutanguliza veteksi huku mwingine akitanguliza matako. Hatari zilizoelezewa hapo awali zinazohusiana na milalo mibaya pia zinaweza kutokea: prolapsi (kuchomoza) ya kiungamwana, minyweo duni ya uterasi, leba iliyokaa sana au iliyozuiliwa, kutokwa na damu muda tu baada ya kuzaa, na haipoksia ya fetasi na kufa.
  • Kupata pacha walioungana (pacha muungano, walioungana kwenye kichwa, kifua, fumbatio au mgongo) pia kunawezekana, ingawa ni nadra.

8.8 Utunzaji wa wanawake walio na milalo mibaya ya watoto au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja

Jinsi ulivyoona katika Kipindi hiki, mlalo wowote isipokuwa ule wa kutanguliza veteksi unazo hatari zake kwa mama na mtoto. Kwa sababu hii, wanawake wote wanaokumbwa na milalo isiyo ya kawaida au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja wanafaa kupata huduma bora kutoka kwa wataalam wakuu wa afya. Wanawake hawa wanapaswa kuhudumiwa katika kituo cha afya kilicho na uwezo wa kutoa huduma bora ya dharura ya uzazi. Utambuzi wa mapema na rufaa kwa mwanamke aliye na mojawapo ya hali hizi inaweza kuokoa maisha yake pamoja na ya mtoto wake.

  • Je, ni nini unachoweza kufanya ili kupunguza hatari zinazotokana na mlalo mbaya wa fetasi au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja kwa wanawake unaowatunza?

  • Katika utunzaji maalum wa manawake katika ujauzito, chunguza mlalo usio wa kawaida wa fetasi kila wanapokutembelea baada ya majuma 36 ya ujauzito. Ukigundua mlalo usio wa kawaida au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja, mpe mwanamke huyo rufaa kabla ya leba kuanza.

    Mwisho wa jibu

Muhtasari wa Kipindi cha 8

Katika Kipindi cha 8 cha somo, ulijifunza mambo haya:

  1. Mwanzoni mwa ujauzito, kwa kawaida watoto huwa katika mlalo wa kutanguliza matako. Katika asilimia 95 ya visa hivi, watoto hujigeuza na kutanguliza veteksi kabla ya leba kuanza.
  2. Mlalo mbaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida baada ya muda kamili wa ujauzito kukamilika huongeza hatari ya kuzuiliwa kwa leba na matatizo mengine ya uzazi.
  3. Visababishi vikuu vya milalo mibaya na fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida ni: kiasi kingi cha kiowevu cha amnioni, umbo na ukubwa usio wa kawaida wa pelvisi, tyuma kwenye uterasi, plasenta privia, ulegevu (udhaifu) wa misuli ya uterasi (baada ya ujauzito mwingi hapo awali); au mimba ya zaidi ya mtoto mmoja.
  4. Matatizo yanayotokea sana ni: upasukaji wa mapema wa membreni, leba kuanza kabla ya muda kamili wa ujauzito kukamilika, leba inayoendelea kwa muda mrefu au iliyozuiliwa, uterasi kupasuka, kutokwa na damu baada ya kuzaa, kuathirika kwa fetasi na mama, kunakoweza kusababisha kifo.
  5. Veteksi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida ni ambapo kisogo cha fetasi kimeangalia upande wa nyuma wa mama. Sehemu ya nyuma ya fuvu la kichwa cha fetasi inaangalia upande wa nyuma wa mama badala ya mbele ya pelvisi ya mama. Asilimia 90 ya fetasi zisizokuwa na veteksi katika nafasi yake ya kawaida huzunguka na mama kuzaa kikawaida.
  6. Mlalo wa kutanguliza matako (wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi, matako juu ya seviksi, mguu au miguu juu ya seviksi) ni ambapo matako ya mtoto ndiyo kitangulizi katika leba. Mlalo wa kutanguliza matako hutokea katika asilimia 3-4 za leba baada ya majuma 34 ya ujauzito. Mlalo wa kutanguliza matako unaweza kusababisha kuzuiliwa kwa leba, prolapsi (kuchomoza) ya kiungamwana, haipoksia, plasenta kujitenga kabla ya muda wake, na mtoto au njia ya uzazi kupata majeraha.
  7. Mlalo wa kutanguliza uso hali ya kichwa cha fetasi kujikunja sana kuelekea nyuma kiasi kwamba uso ndio kitangulizi katika leba. Mlalo wa kutanguliza uso hutokea kwa takriban mimba 1 kwa kila 500 iliyokomaa. Mlalo wa kutanguliza uso ambapo kidevu kimeangalia upande wa nyuma wa mama (“kidevu nyuma”) huzunguka na kuwa katika hali ya kidevu kuangalia upande wa mbele (pelvisi) wa mama (“kidevu mbele”) na kuzaliwa kikawaida. Huenda mama huyo ahitaji kuzaa kwa njia ya upasuaji iwapo mtoto hatazunguka kwa njia hii.
  8. Mlalo wa kutanguliza paji la uso ni ambapo paji la uso wa mtoto ndicho kitangulizi. Mlalo huu hutokea kwa takribani ujauzito 1 kwa kila 1000 uliokamilisha muda na ni vigumu kuugundua kabla ya leba. Upasuaji unaweza kustahili.
  9. Mlalo wa kutanguliza bega hutokea wakati fetasi imejilaza kingamo katika leba. Ukichunguza uke, baada ya leba kuendelea vizuri, utahisi mbavu za mtoto na pia mkono unaweza kuchomoza. Kuzaa kwa njia ya upasuaji huhitajika isipokuwa daktari au mkunga aweze kumgeuza mtoto ili kichwa kitangulie (“kichwa chini”).
  10. Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja huwa katika hatari kubwa ya mlalo mbaya wa fetasi. Kina mama wanahitaji utunzaji zaidi katika ujauzito huu. Pacha wamo katika hatari ya matatizo yanayohusiana na kuzaliwa wakiwa na uzani wa chini na kabla ya muda kamili wa mimba kukamilika.
  11. Mlalo wowote isipokuwa ule wa kutanguliza veteksi, baada ya wiki 34 ya mimba, husemekana kuwa na hatari kubwa kwa mama pamoja na mtoto wake. Usijaribu kumgeuza mtoto aliye katika mlalo mbaya au asiye katika nafasi yake ya kawaida! Mpe mama rufaa ili aweze kupata huduma ya dharura ya uzazi.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 8

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, jibu maswali haya ili kutathmini ulivyojifunza. Linganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 8.1 (linatathmini malengo ya Somo la 8.1, 8.2 na 8.4)

Je, ni maelezo yapi yaliyosahihi na yasiyosahihi? Andika maelezo sahihi kwa yale unayoona kuwa si kweli.

  • A.Fandasi: sehemu ya juu iliyo ya mviringo, ambayo ndiyo kaviti pana zaidi ya uterasi.
  • B.Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi: ambapo miguu imekunjwa kwenye kiungo cha nyonga na magoti na kukunjwa chini ya mtoto.
  • C.Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako juu ya seviksi: ambapo ni vigumu sana kuushughulikia mlalo huo wa kutanguliza matako kiasi kwamba ni lazima umweleze mama huyo bayana kuhusu jinsi uzazi huo utakavyokuwa mgumu.
  • D.Mlalo wa kutanguliza matako wenye mguu au miguu juu ya seviksi: ambapo mmoja au miguu yote imejinyoosha kiasi kwamba mtoto anatanguliza miguu ("miguu kwanza").
  • E.Haipoksia: mtoto anapopata oksijeni nyingi kupindukia.
  • F.Mimba ya zaidi ya mtoto mmoja: ambapo mama amekuwa na watoto wengi hapo awali.
  • G.Pacha wa monozaigoti: pacha wanaotoka kwenye ova moja iliyotungishwa (zaigoti). Wanaweza kuwa wa jinsia tofauti, lakini wanatumia plasenta moja.
  • H.Pacha daizaigoti (zaigotipacha): hutoka kwenye zaigoti mbili. Wana plasenta tofauti na wanaweza kuwa wa jinsia moja ua tofauti.
Answer
  • A.ni kweli. Fandasi ni sehemu ya juu iliyo ya mviringo, ambayo ndiyo kaviti pana zaidi ya uterasi.
  • B.ni kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako na miguu ya mtoto karibu na seviksi ni ambapo miguu imekunjwa kwenye kiungo cha nyonga na magoti, na kukunjwa chini ya mtoto.
  • C.si kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye matako juu ya seviksi ndiyo aina ya mlalo wa kutanguliza matako inayotokea sana na ni ambapo miguu ya mtoto imenyooshwa kuelekea juu (Picha 8.4).
  • D.ni kweli. Mlalo wa kutanguliza matako wenye mguu au miguu juu ya seviksi ni ambapo mmoja au miguu yote imejinyoosha kiasi kwamba mtoto anatanguliza miguu ("miguu kwanza").
  • E.si kweli. Haipoksia ni ambapo mtoto anakosa hewa na hua katika hatari ya kuharibika ubongo au kifo.
  • F.si kweli. mimba ya zaidi ya mtoto mmoja ni ambapo uterasi ina zaidi ya fetasi moja.
  • G.si kweli. Pacha wa monozaigoti hutoka kwenye ova moja iliyotungishwa (zaigoti). Huwa wa jinsia moja na hutumia plasenta moja.
  • H.ni kweli. Pacha wa daizaigoti (Zaigotipacha) hutoka kwenye zaigoti mbili tofauti, hutumia plasenta tofauti na wanaweza kuwa wa jinsia moja ua tofauti.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.2 (linatathmini malengo ya Somo la 8.1 na 8.2)

Je, tofauti kuu kati ya mlalo wa kawaida na usio wa kawaida wa fetasi ni zipi? Tumia istlahi sahihi za kitiba zilizo katika herufi nzito kwenye maelezo yako.

Answer

Katika mlalo wa kawaida, veteksi (sehemu ya juu kabisa ya kichwa cha fetasi) huwa ya kwanza kufika kwenye ukingo wa pelvisi ya mama. Kisogo (sehemu ya nyuma ya fuvu la kichwa cha fetasi) huangalia sehemu ya mbele ya pelvisi ya mama (kwenye simfisisi ya kinena).

Mlalo usio wa kawaida hutokea wakati ambapo veteksi haipo kwenye nafasi yake ya kawaida au mlalo mbayaukitokea. (Katika hali ambapo veteksi haipo kwenye nafasi yake ya kawaida katika mlalo wa kutanguliza veteksi, kisogo cha fetasi huangalia upande wa nyuma wa mama badala ya simfisisi ya kinena. Katika mlalo mbaya, sehemu yoyote ile isipokuwa veteksi hutangulia.) Kwa mfano, mlalo wa kutanguliza matako (matako kwanza), mlalo wa kutanguliza uso (uso kwanza), mlalo wa kutanguliza paji la uso (paji la uso kwanza), na mlalo wa kutanguliza bega (fetasi kulala kingamo).

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.3 (linatathmini malengo ya Somo 8.3 na 8.5)

  1. Orodhesha matatizo yanayotokea sana kutokana na milalo mibaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida mwishoni mwa ujauzito.
  2. Je, ni hatua ipi utakayochukua ukigundua kuwa fetasi iko katika mlalo mbaya ilhali leba haijaanza?
  3. Je, ni nini usichopaswa kujaribu kufanya?
Answer
  1. Matatizo yanayojikeza sana kutokana na milalo mibaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida ni: kupasuka kwa mapema kwa membreni, leba kuanza kabla ya muda kutimia, leba kukaa sana au kuzuiliwa, uterasi kupasuka, kutokwa na damu baada ya kuzaa, kuathirika kwa fetasi pamoja na mama kunakoweza kusababisha kifo.
  2. Mpe mama huyo rufaa aende katika kituo cha juu cha afya. Huenda akahitaji huduma ya dharura ya uzazi.
  3. Usijaribu kumgeuza mtoto. Ni daktari au mkunga aliyehitimu tu anayepaswa kujaribu kumgeuza mtoto. Mgeuze mtoto kwenye kituo cha afya tu.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.4 (linatathmini malengo ya Somo la 8.4 na 8.5)

Mwanamke mjamzito amehamia kwenye kijiji chako. Tayari amefikisha majuma 37 ya ujauzito. Hujawahi kumuona. Anakueleza kuwa alizaa pacha miaka mitatu iliyopita na anataka kujua ikiwa ana pacha tena.

  1. Je, utachunguzaje kua ana pacha?
  2. Je, ukitambua ana pacha, utafanya nini ili kupunguza hatari wakati wa leba na kuzaa?
Answer
  1. Jinsi ya kuchunguza ikiwa ujauzito huu ni wa pacha:
    • Je, uterasi ni kubwa zaidi ya inavyotarajiwa katika kipindi hicho cha ujauzito?
    • Je, utersi ina umbo lipi? Je, ni mviringo, ambayo ni ishara ya pacha? Au ina umbo la moyo, ambayo ni ishara ya mimba ya mtoto mmoja?
    • Je, unahisi zaidi ya kichwa kimoja?
    • Je, unasikia midundo miwili ya moyo iliyo na tofauti ya angalau mipigo 10? (Watu wawili wasikize kwa wakati mmoja).
    • Ikiwa unaweza kukifikia kituo cha afya cha juu na bado hauna uhakika, mpeleke mwanamke kwa ukaguzi wa mawimbi sauti ya tiba.
  2. Jinsi ya kupunguza hatari katika uzazi wa pacha:
    • Chunguza na uhakikishe kuwa mama huyo hana anemia.Mhimize apumzike na kuweka miguu yake juu ili kupunguza hatari ya ongezeko la shinikizo la damu au kuvimba kwa miguu na nyayo zake.
    • Kuwa macho ili kugundua na kukabiliana na ongezeko la hatari ya ugonjwa wa ujauzito.
    • Tarajia kuwa leba yake itaanza kabla ya muda kamili kutimia. Mpeleke kwenye kituo cha afya kabla ya leba kuanza. Enda naye ikiwezekana.
    • Wasiliana na kituo hicho cha afya mapema ili waweze kutarajia rufaa kutoka kwako.
    • Hakikisha kuwa usafiri unaweza kumpeleka katika kituo cha afya patokeapo hitaji.

Mwisho wa jibu