Skip to main content
Printable page generated Thursday, 18 April 2024, 11:19 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 18 April 2024, 11:19 PM

1. Utunzaji Baada ya Kuzaa katika Kituo cha Afya na katika Jamii

Kipindi cha 1 Utunzaji baada ya kuzaa katika kituo cha afya na katika Jamii

Utangulizi

Utunzaji wa baada ya kuzaa ni utunzaji anaopewa mama na mtoto wake mchanga mara tu baada ya kuzaa na kwa wiki sita ya kwanza ya maisha (Picha 1.1). Kipindi hiki hudhihirisha kuanzishwa kwa awamu mpya ya maisha ya kifamilia kwa wanawake na wenzi wao na mwanzo wa rekodi ya kiafya maishani mwa watoto wachanga (au watoto waliozaliwa - jina linalotumiwa mara nyingi na madaktari, wauguzi na wakunga).

Ingawa kipindi cha baada ya kuzaa hakina utata kwa wanawake na watoto wengi, utunzaji bora wa baada ya kuzaa pia inahusu kutambua mchepuko wowote dhidi ya upataji nafuu unaotarajiwa baada ya kuzaa, na kutathmini na kutatua ipasavyo kwa wakati ufaao. Ni jambo la kusikitisha kuwa katika nchi nyingi za Sahara ya Afrika chini ya asilimia 37 ya wanawake ndio huzalia kwenye vituo vya afya na chini ya asilimia 10 hupokea utunzaji wowote baada ya kuzaa katika muda wa siku mbili baada ya kuzaa. Kwa hivyo, jukumu lako kama mhudumu wa afya nje ya hospitali ni muhimu katika kuboresha hali hii, kutambua dalili za hatari na kupunguza athari mbaya kwa kina mama na watoto wachanga.

Katika kila nchi barani Afrika, kipindi cha baada ya kuzaa mara nyingi hutambulika kwa vitendo maalumu vya kitamaduni. Kuelewa imani na asasi za kijamii katika jamii yako ni jambo la kimsingi katika kuhakikisha utunzaji bora wa baada ya kuzaa. Katika Kipindi hiki cha kwanza cha somo, utajifunza kuhusu ni kwa nini huduma katika kipindi cha baada ya kuzaa ni muhimu sana na kuhusu umuhimu wa kushiriki na kujihusisha kwa jamii katika kutimiza utunzaji bora wa baada ya kuzaa. Tunatoa muhtasari wa baadhi ya mbinu za uhamasishaji wa jamii kwa kifupi na kujadili jinsi ya kujenga ubia na watu mashuhuri wanaoweza kukusaidia kuwatunza kina mama na watoto wao.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 1

Baada ya kusoma katika Kipindi hiki, unapaswa kuwa na uwezo wa:

1.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyochapishwa kwa herufi nzito. (Swali la kujitathmini 1.1)

1.2 Kueleza umuhimu wa utunzaji baada ya kuzaa kwa kuzingatia wakati ambapo kina mama wengi na watoto wachanga hufariki na visababishi vikuu vya vifo hivi. (Swali la kujitathmini 1.2)

1.3 Kueleza kwa kifupi mabadiliko makuu ya kifiziolojia kwa mama na mtoto mchanga katika kipindi cha baada ya kuzaa. (Swali la kujitathmini 1.3)

1.4 Kueleza dalili kuu za hatari kwa mama na mtoto mchanga katika kipindi cha baada ya kuzaa. (Swali la kujitathmini 1.3)

1.5 Kueleza umuhimu wa kujihusisha kwa jamii katika utunzaji wa baada ya kuzaa na kuelezea jinsi utakavyojenga ushirikiano na watu mashuhuri katika jamii hiyo. (Swali la kujitathmini 1.2)

1.1 Je, kwa nini utunzaji baada ya kuzaa ni muhimu?

Utunzaji bora baada ya kuzaa unaweza kuleta tofauti zaidi kwa afya na maisha ya kina mama na watoto wachanga mwanzoni mwa kipindi cha uchanga na siku saba za kwanza za maisha. Hata hivyo, kipindi hiki cha uchanga, tangu kuzaliwa hadi siku 28 baada ya kuzaliwa ni wakati wa kiwango cha juu cha hatari. Vifo vya watoto wachanga waliozaliwa wakiwa hai vitokeavyo katika kipindi cha siku 28 za kwanza huripotiwa na nchi zote ulimwenguni kama kiwango chavifo vya watoto wachanga kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai. Vile vile, ripoti za vifo vya kina mama vitokanavyo na ujauzito ni vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo yanayohusiana na matatizo ya baada ya kuzaa na sio tu yale yanayotokea wakati wa kuzaa. Viwango hivi vyote ni viashiria muhimu vya ubora wa utunzaji baada ya kuzaa.

Kipindi baada ya kuzaa ni wakati muhimu kwa mama na mtoto wake mchanga. Hii ndiyo sababu ya kwanza ya kukufanya ulenge utunzaji zaidi na mazingatio kwa kipindi hiki. Afrika, uwiano wa vifo vitokanavyo na ujauzito ni miongoni mwa wiano za juu zaidi ulimwenguni. Kina mama 673 hufariki kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai. Vile vile, kiwango cha vifo vya watoto mwanzoni mwa kipindi cha uchanga piakilikuwa juu sana ambapo watoto 39 walifariki katika juma la kwanza la maisha kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa wakiwa hai. Afrika ni mojawapo ya bara ambako nusu ya jumla ya vifo vya watoto wachanga hutokea.

Kipindi hiki chenye hatari ya juu pia ndio wakati ulio na kiwango cha chini cha matumizi ya huduma za kiafya kwa kina mama na watoto barani Afrika. Hii ndiyo sababu ya pili inayokulazimu kuzingatia sana utunzaji baada ya kuzaa.

Ikiwa watoto wote wachanga watapokea utatuzi bora na kwa gharama nafuu katika kipindi cha baada ya kuzaa, imekadiriwa kuwa vifo vya watoto wachanga vinaweza kupunguzwa kwa asilimia 10-27. Hii ina maana kuwa, kiwango cha juu cha matumizi ya utunzaji wa baada ya kuzaa kinaweza kuokoa maisha ya watoto wachanga 60,000 kila mwaka barani Afrika na kuisaidia nchi hiyo kutimiza Lengo la Milenia la Maendeleo la kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa theluthi mbili kufikia mwaka wa 2015.

Kwa kweli, utunzaji wa baada ya kuzaa ni bora ukitolewa katika kituo cha afya. Hata hivyo, kutokana na sababu nyingi za kijamii, kiuchumi na kitamaduni kama vile umbali na gharama ya kwenda kuhudumiwa, kina mama wengi vijijini huzalia nyumbani. Kwa hivyo, njia halisi zaidi ya kutoa utunzaji baada ya kuzaa katika siku za usoni barani Afrika huenda iwe ni kwa mhudumu wa afya kama wewe kuwatembelea nyumbani.

1.2 Je, ni wakati upi ambapo kina mama na watoto wachanga hufariki katika kipindi cha baada ya kuzaa?

Kina mama na watoto wao wachanga wamo katika hatari zaidi ya kufariki mwanzoni mwa kipindi cha uchanga, hasa saa 24 za kwanza baada ya kuzaa na katika siku saba za kwanza baada ya kuzaa (tazama Jedwali 1.1). Jinsi unavyoweza kuona katika jedwali, asilimia 45 hadi 50 ya vifo vya kina mama na watoto wachanga hutokea katika saa 24 za kwanza baada ya kuzaa. Asilimia 65 hadi 75 ya vifo vya kina mama na watoto wachanga hutokea katika muda wa juma moja baada ya kuzaa. Huu ni ushahidi unaolazimu utoaji wa utunzaji bora na kikamilifu kwa kina mama na watoto wachanga katika siku chache za kwanza baada ya kuzaa.

Jedwali 1.1 Makadirio ya vifo vya kina mama na watoto wachanga katika siku saba za kwanza baada ya kuzaa
Vifo baada ya kuzaaSaa 24 za kwanza (%)Siku saba za kwanza (%)
Vifo vya kina mama4565
Vifo vya watoto wachanga 5075

Kwa hali fulani zinazohatarisha maisha ya mama na mtoto mchanga, utunzaji bora baada ya kuzaa hutolewa katika saa na siku chache za kwanza au baadaye kwa kuchelewa. Hali hizi za kiafya zinapotambulika mapema ndivyo zinavyoweza kuthibitiwa kikamilifu; ndivyo mama na mtoto wanavyopewa rufaa ya kupata matibabu spesheli kwa haraka na ndivyo matokeo yatakavyokuwa mazuri. Nyingi za tatuzi hizi hutegemea sana wakati. Unapaswa kuzingatia haya unapotoa utunzaji kwa kina mama na watoto wao siku chache za kwanza za maisha baada ya kuzaa.

1.3 Je, kina mama na watoto wachanga katika kipindi cha baada ya kuzaa hufariki kutokana na nini?

Lengo kuu la kutoa utunzaji bora baada ya kuzaa ni kuzuia vifo vya kina mama na watoto wachanga na vile vile matatizo ya muda mrefu. Unapaswa kujua visababishi vikuu vya vifo katika kipindi cha baada ya kuzaa ili uweze kutoa utunzaji bora wa baada ya kuzaa na kwa wakati ufaao pale nyumbani na katika kituo cha afya.

Kujua ni nini hasa kinachosababisha vifo vya kina mama na watoto wachanga ni muhimu kwa kutambua hatua muhimu zinazowezakutatuavisababishi vikuu vya vifo katika kipindi baada ya kuzaa. Jedwali 1.2 linaonyesha asilimia ya vifo vya kina mama na visababishi vikuu vya vifo hivi kwa wanawake barani Afrika.

Ulijifunza kuhusu anemia, matatizo yanayosababisha shinikizo la damu, na uavyaji mimba katika vikao vya18, 19 na 20 vya somo katika Moduli ya utunzaji katika ujauzito. Vizuizi na kutokwa na damu nyingi wakati wa kuzaa vilifundishwa katika Vikao vya 9 na 11 vya moduli ya utunzaji katikauchungu wa kuzaa na kuzaa.

Jedwali 1.2 Visababishi vya vifo vya kina mama vitokanavyo na ujauzito barani Afrika.
Visababishi vya vifo vya kina mamaAsilimia (%)
Kutokwa na damu nyingi baada ya kuzaa34
Maambukizi ya sehemu fulani au yaliyosambaa (Sepsisi)16
Matatizo yanayosababisha shinikizo la damu katika ujauzito (ugonjwa wa ujauzito, eklampsia)9
VIRUSI VYA UKIMWI/ UKIMWI6.2
Vizuizi katika kuzaa4
Uavyaji mimba 4
Anemia4
Visababishi vingine vya vifo  30

Jedwali 1.3 linaonyesha visababishi vya vifo vya watoto wachanga barani Afrika. Utajifunza kuhusu utunzaji maalum kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na waliozaliwa na uzani wa chini katika Kipindi cha 8 cha somo cha Moduli hii.

Maambukizi, yakiwemo magonjwa ya kuhara na pepopunda, yameelezewa kwa undani katika Moduli juu ya magonjwa ya kuambukiza. Asifiksia ya kuzaliwa na uhaisho (urejeshaji uhai wa mtu mahututi) wa mtoto mchanga yaliangaziwa katika Kipindi cha 7 cha somo cha moduli juu ya utunzaji katika uchungu wa kuzaa na kuzaa.

Jedwali 1.3 Visababishivya vifo vya watoto wachanga barani Afrika
Visababishi vya vifo vya watoto wachanga Asilimia (%)  
Maambukizi:               47
  • Kuhara           
  • Pepopunda
  • Maambukizi mengine yakiwemo sepsisi

3

7

37

Asifiksia ya kuzaliwa 25
Kuzaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na kuzaliwa na uzani wa chini25
Ulemavu wa kuzaliwa4
Visababishi vingine vyote 7
  • Je, kwa nini ni muhimu sana uelewe visababishi vikuu vya vifo vya kina mama na watoto katika kipindi cha baada ya kuzaa?

  • Huenda ulifikiria sababu nyingi, lakini iliyo bayana zaidi ni tofauti kubwa inayoweza kuletwa na utoaji wa utunzaji bora wa baada ya kuzaa na kwa wakati ufaao kwa kiwango cha vifo vya watoto wachanga barani Afrika: kupungua kwa asilimia 10 hadi 27 ya vifo vya watoto wachanga au kuokoa maisha ya takribani watoto wachanga 60,000.

    Mwisho wa jibu

  • Fikiria kuhusu visababishi vikuu vya vifo vya kina mama na watoto wachanga. Je, ni vipi unavyotarajia kukumbana navyo unapotekeleza jukumu lako kama mhudumu wa afya nje ya hospitali?

  • Ukitumia takwimu zilizo kwenye Jedwali 1.2 na 1.3, basi huenda ulitaja kutokwa na damu nyingi baada ya kuzaa kwa kina mama, na aina fulani ya maambukizi kwa watoto na kina mama. Huenda pia ulichagua eklampsia na asifiksia ya watoto wachanga.

    Mwisho wa jibu.

1.4 Je, kwa nini wanawake na watoto wachanga wamo katika hatari kubwa katika kipindi cha baada ya kuzaa?

Saa 4-6 za kwanza baada ya kuzaa ndicho kipindi ambapo mama anaweza kuathiriwa sana na matatizo yatokanayo na kutokwa na damu nyingi. Visababishi huwa kupoteza damu nyingi kupitia katika eneo ambapo plasenta ilikuwa imejishikiza kwenye uterasi ya mama au kupasuka kwa uterasi wakati wa uchungu wa kuzaa na kuzaa. Kutokwa na damu kabla ya kuzaa pia kunaweza kuhatarisha maisha ya mtoto kwa kumkosesha oksijeni na virutubishi.

Mama pamoja na mtoto wamo katika hatari kubwa ya kukumbwa na matatizo mengine ikiwa marekebisho ya kifiziologia yanayotokea katika miili yao hayatatokea ifaavyo baada ya kuzaa. Hii inaweza kusababisha ukosefu wa utendaji kazi au ukatizaji wa usambazaji wa mahitaji muhimu ya oksijeni na virutubishi vinavyohitajika kudumisha maisha.

1.4.1 Mabadiliko ya kifiziolojia kwa mama baada ya kuzaa

Kuna kupoteza damu na viowevu vingine vya mwili (kwa mfano kupitia kutapika na kutokwa na jasho) kusikoweza kuepukika wakati wa uchungu wa kuzaa. Hata hivyo, wanawake wengi wanaweza kustahimili haya. Upotezaji huu wa viowevu ni kawaida kwa kiwango fulani. Aidha, wanawake wengi hubaki katika uchungu wa kuzaa kwa saa nyingi bila kula wala kunywa, jambo ambalo linaweza kuwafanya wakose maji mwilini. Wasipopewa maji mwilini kwa haraka baada ya kuzaa, wana uwezekano wa kupata matatizo ya kifiziolojia

Katika ujauzito, shughuli hubadilika katika karibu mifumo yote ya mwili wa mama, ikiwemo moyo, mapafu, kiasi cha damu na vilivyo kwenye damu, mfumo wa uzazi, matiti, mfumo wa kingamwili na homoni. Katika kipindi baada ya kuzaa, mifumo hii yote ya mwili yenye kubadilika sharti ibadilike kutoka katika hali ya ujauzito hadi hali ilivyokuwa kabla ya ujauzito. Kuna uwezekano wa hatari ya matatizo marekebisho haya yanapotendeka. Mifano ya matatizo yanayotokea sana ni maambukizi ya matiti na mivilio ndani ya vena (vibonge vya damu ndani ya vena za miguu), ambayo yameelezewa katika Kipindi cha 3 cha somo kwenye Moduli hii. Kipindi ambapo marekebisho haya ya kifiziologia hufanyika katika mwili wa mama aliyezaa huitwa puperiamu. Utajifunza kuhusu haya yote katika Kipindi cha 2 na cha 3 cha somo.

Aidha, uchungu wa kuzaa ni tukio lenye maumivu kwa wanawake wengi, hasa wale wanaozaa kwa mara ya kwanza. Wanawake pia hupata fadhaa na mhangaiko kuhusu jinsi matokeo ya uchungu wa kuzaa utakavyokuwa. Kuwa na mtoto ni furaha (Picha 1.1), lakini pia inaweza kuwa chanzo cha wasiwasi. Wanawake walio katika kipindi cha baada ya kuzaa mara nyingi hukabiliana na hali ya mfadhaiko na hivyo wanahitaji usaidizi wa kisaikolojia.

Picha 1.1 Kuwa na mtoto mwenye afya huleta furaha, jambo linaloweza kudumishwa na utunzaji bora baada ya kuzaa. (Picha: Nancy Durrell McKenna kwa Usalama wa Kina mama)

1.4.2 Matatizo kwa mtoto mchanga

Hatari ya maambukizi

Akiwa kwenye uterasi, mtoto huwa amelindwa vizuri na membreni za fetasi na kiowevu kizuia-bakteria cha amnioni ambamo fetasi hiyo huwa, vile vile na antibodi za mama zinazopitia kwenye plasenta na kuilinda dhidi ya maambukizi ambayo mama huyu ashakabiliana nayo. Antibodi kwenye kolostramu (maziwa ya kwanza ya mama) na maziwa komavu ya mama pamoja na vizuizi asilia kama vile ngozi ya mtoto humpa mtoto mchanga kiasi kikubwa cha kinga dhidi ya maambukizi anayopata mara tu anapozaliwa. Mfumo wa kingamwili wa mtoto huyu utachukua miezi kadhaa kabla ya kukua kikamilifu.

Hatari ya asfiksia

Mfumo wa mzunguko wa damu wa mtoto huyu mchanga ni mkumbwa na marekebisho kadhaa anapopumua kwa mara ya kwanza nje ya uterasi. Kiasi kidogo cha damu huenda kwenye mapafu mtoto akiwa ndani ya uterasi kwa sababu hapumui hewa. Mapafu ya fetasi hayawezi kutekeleza mbadilishano wa gesi (kufyonza oksijeni na kutoa dioksidi ya kaboni) unaofanyika tangu kuzaliwa na kuendelea.

  • Je, mbadilishano wa gesi hufanyika wapi kwa mtoto akiwa kwenye uterasi?

  • Oksijeni hufyonzwa katika damu ya fetasi kutoka kwa damu ya mama mifumo hii inapokaribiana katika plasenta; dioksidi ya kaboni kutoka kwa fetasi huingia katika damu ya mama na kutolewa kutoka kwa mwili wake kupitia katika pumzi yake.

    Ulijifunza kuhusu mbadilishano wa gesi kwenye plasenta katika Kipindi cha 6 cha somo kwenye moduli ya Utunzaji katika Ujauzito.

    Mwisho wa jibu

Mara tu baada ya kuzaliwa, mishipa ya damu inayopita kwenye mapafu hufunguka na kisha damu yote katika mzunguko wa mtoto iweze kupita kwenye mapafu, ambapo mbadilishano wa gesi hufanyika. Ni wakati muhimu sana kwa mtoto mchanga mapafu yanapoanza kufanya kazi. Kutopumua ni sababu ya kawaida ya asfiksia ya kuzaliwa. Pia watoto waliozaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha, mara nyingi huwa na ugumu wa kupata oksijeni ya kutosha kwa sababu mapafu yao hayajakomaa kikamilifu na kwa hivyo mbadilishano wa gesi hautafanyika ifaavyo.

Utajifunza mengi kuhusu ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga katika Kipindi cha 6 cha na pia kwenye moduli juu ya Udhibiti Unganifu wa Maradhi ya Watoto Wachanga na ya Utotoni.

Mtoto akiwa kwenye uterasi, kemikali nyingi zenye sumu au uchafu huondolewa mwilini mwake na plasenta inayozielekeza kwenye ini ambapo huharibiwa (mchakato unaoitwa uzimuaji sumu). Baada ya kuzaliwa, ini la mtoto hulichukua jukumu hili na kuzimua sumu kwenye uchafu wa kemikali unaotengenezwa mwilini au kuingiziwa mdomoni. Mojawapo ya majukumu yanayotekelezwa na ini ni kuizimua sumu kwenye protini iitwayo bilirubini. Protini hii hutolewa kwa seli zee nyekundu za damu zinapoharibiwa. Seli nyekundu za damu huishi kwa muda mfupi tu na kuharibiwa na kisha seli nyekundu mbadala kutolewa. Ini la mtoto lisipoweza kustahimili kiwango cha seli zee nyekundu zinazofaa kuharibiwa, bilirubini hulimbika katika mwili wa mtoto na kuifanya ngozi yake iwe na umanjano. Hali hii huitwa ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga na ni hatari sana hasa ngozi ya viganja vya mikono na nyayo za miguu inapoonyesha umanjano.

Figo za mtoto mchanga pia huchangia pakubwa katika uondoaji wa kemikali zenye sumu zinazoondolewa mwilini kupitia kwa mkojo. Uchanga katika utendakazi wa figo pia unaweza kusababisha matatizo kwa watoto wachanga kemikali zenye sumu zinapolimbika mwilini.

  • Dhania kuwa unazungumza na mama wa mtoto mchanga kisha akuambie kuwa mtoto alizaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha. Je, ni nini unachopaswa kutilia shaka na kushughulikia mara moja?

  • Kwanza chunguza ikiwa mtoto anakula vizuri. Fikiria kuhusu uchanga wa mapafu ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na uchunguze ikiwa mtoto huyu anaonyesha dalili zozote za matatizo ya kupumua. Pia zingatia uchanga wa figo na ini kisha uchunguze ikiwa ana dalili za ugonjwa wa manjano.

    Mwisho wa jibu

1.5 Utakayofanya katika kipindi cha baada ya kuzaa 

Hauwezi kusadiki kuwa kufanikiwa kwa mama katika kuzaa na ubora wa afya yake na ya mtoto wake mchanga mwanzoni mwa kipindi cha baada ya kuzaa ni kigezo kuwa wataendelea katika hali njema. Matatizo yanaweza kutokea kutokana na marekebisho ya kifiziolojia kwa mama na mtoto mchanga yaliyoelezewa hapo awali (ambayo tutajadili kikamilifu katika Kipindi cha baadaye kwenye moduli hii) na mabadiliko ya haraka ambayo sharti yafanyike kwa mtoto ili azoee maisha katika mazingira ya nje. Kwa hivyo, unafaa uchunguze kwa makini dalili za hatari mwanzoni na katika muda wa mwisho wa kipindi cha baada ya kuzaa. Kabla hujamruhusu mama na mtoto kwenda nyumbani (iwapo alizalia kwenye Kituo cha Afya) au kabla ya kuwaacha nyumbani kwao baada ya mama kuzaa, wachunguze kwa muda wa saa sita za kwanza baada ya kuzaa. Ikiwa haukuweza kuhudumia uzazi huo, watembelee mapema uwezavyo katika saa 24 za kwanza, na hasa katika saa sita za kwanza.

1.5.1 Kumkagua mama aliyezaa

Katika saa sita za kwanza, mkague mama huyo kwa dalili za hatari zifuatazo:

  • Uterasi kutopungua kikamilifu: Uterasi isiyopungua ipaswavyo ni dalili ya hatari; mpendekezee rufaa iwapo baada ya saa sita uterasi ni kubwa kuliko ukubwa wake wa kawaida baada ya wiki 20 ya ujauzito na haiwezi kuhisika kwa urahisi ukitomasa kwa sababu uterasi ni laini.
  • Kutokwa na damu mbichi ukeni: Ni kawaida kutokwa na kiowevu chenye damu (kiitwacho lokia) mwanzoni mwa kipindi cha baada ya kuzaa. Hata hivyo, kusiwe na kutoka kwa damu mbichi kunakoendelea.
  • Dalili kuu zisizothabiti au zinazoashiria mshtuko: Shinikizo la damu na mpwito wa ateri sharti viwe katika hali ya kawaida kabala ya kumuacha mama huyo. Ikiwa shinikizo lake la damu linapungua huku mpwito wa ateri ukipanda, mwanamke huyu anaweza kuwa anaelekea kuwa na mshtuko kutokana na kuvuja kwa damu ndani ya mwili. Ikiwa uterasi itabaki kuwa kubwa baada ya kuzaa na dalili kuu ziashirie mshtuko, inaweza kuwa ni kutokana na limbikizo la damu kwenye uterasi.

Mpe mama rufaa mara tu unapoona dalili zozote za hatari peleka mtoto pia.

1.5.2 Kumkagua mtoto mchanga

Unapaswa kumkagua mtoto mchanga kwa dalili zifuatazo katika saa sita za kwanza:

Unyonyeshaji umeelezewa kikamilifu katika Kipindi cha 7 cha somo.

  • Unyonyaji haba: Watoto waliozaliwa kabla ya muda wa ujauzito kutimia, waliozaliwa na uzito wa chini, wenye asfiksia au walio wagonjwa kwa kawaida hawawezi kunyonya maziwa matitini vizuri. Unyonyaji huzidisha utengenezwaji wa maziwa. Kwa hivyo, usimpinge mama huyo kunyonyesha iwapo hatoi maziwa ya kutosha mwanzoni. Mwongezee maji na umhimize mtoto kunyonya.
  • Ugonjwa wa manjano kwa mtoto mchanga: Umanjano kwenye ngozi ya mtoto mchanga ni ishara kuwa anahitaji rufaa kupelekwa kwenye kituo cha afya au hospitalini mara moja iwapo umanjano huu utaanza katika saa 24 za kwanza au akiwa na umri wa majuma mawili.
  • Kiwango cha juu cha joto, kutapika mara kwa mara, fumbatio kuvimba au kutotoa kinyesi baada ya saa 24: Kiwango cha juu cha joto (kiwango cha joto sawa na au juu ya nyuzijoto 37.5), kutapika na dalili zingine za hatari huashiria kuwepo kwa maambukizi hatari na/au kizuizi mahali fulani katika ufereji wa utumbo.
  • Hipothemia: Hipothemia ni hali ambapo mtoto ni baridi ukimgusa au ana kiwango cha joto chini ya nyuzijoto 35. Mweke mtoto katika hali ambapo ngozi yake itagusana moja kwa moja na ya mama kisha uwafungie kwenye blanketi iliyo vuguvugu na uweke chepeo au shali kwenye kichwa cha mtoto. Wape rufaa mara moja iwapo kiwango cha joto cha mtoto hakitapanda kwa haraka hadi hali ya kawaida.
  • Matatizo ya kupumua: Mtoto huwa na matatizo ya kupumua iwapo anapumua pumzi 60 kwa dakika, kifua kikijivuta ndani (mbavu kujivuta ndani mtoto anapotweta kwa kutafuta pumzi), midomo kuwa na rangi ya samawati na/au kipimo cha mpigo wa moyo kikiwa juu ya mipigo 160 kwa dakika.
  • Kutokwa na damu kwenye kitovu au sehemu nyingine: Kitovu kinaweza kutoka damu iwapo hakikufungwa kwa kukazwa kabla ya kiungamwana kukatwa, au mtoto anaweza kutokwa na damu mkunduni, ambayo huashiria kupoteza kwa damu kutoka kwa tumbo au matumbo.
  • Vigubiko vyekundu vilivyovimba au kutokwa na usaha machoni: Ikiwa tayari umeyatibu macho ya mtoto kwa kutumia lihamu ya tetrasaiklini wakati wa kuzaliwa, mpe mama huyo na mtoto wake rufaa kwa utunzaji maalumu.

Uzuiaji wa hipothemia kwa kutumia ‘kanuni ya msisimko fululizi’ umeelezewa kikamilifu katika Kipindi cha 7 cha somo.

Kiasi kamili cha damu kwa mtoto mchanga mwenye uzani wa wastani ni milimita 240 pekee; hata kupoteza milimita 30 za damu kunatosha kusababisha mshtuko.

1.5.3 Kufuatilia baada ya huduma ya mwanzoni mwa kipindi cha baada ya kuzaa

Katika safari ya kwanza ya utunzaji baada ya kuzaa, unapaswa kukumbuka:

  • Kumshauri mama na mumewe/mwenziwe kuhusu upangaji uzazi, chanjo na unyonyeshaji jinsi utakavyojifunza baadaye katika moduli hii.
  • Kumpa miadi aje katika kituo chako cha afya au umtembelee nyumbani kwake baada ya siku tatu, sita na majuma sita (Picha 1.2) ikiwa kila kitu kinaendele kikawaida.
  • Kumpa miadi zaidi ya kumtembelea nyumbani kwake baada ya siku mbili ikiwa kuna matatizo yoyote ambayo hayajasababisha rufaa au iwapo mtoto alizaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha, uzito wa chini au anaathiriwa na kiwango cha chini cha joto.

Watoto waliozaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na waliozaliwa na uzito wa chini ndio mada ya Kipindi cha 8 cha somo.

Picha 1.2 Uchunguzi katika kipindi cha baada ya kuzaa ni wakati mwafaka wa kuwashauri kina mama kuhusu chanjo na upangaji uzazi. (Picha: Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa/Indrias Getachew)

1.6 Uhamasishaji wa jamii kuhusu utunzaji baada ya kuzaa

Uhamasishaji wa jamii hufasiliwa kama shughuli zinazoanzishwa na jamii au watu wengine ambazo hupangwa, hutekelezwa na kutathminiwa na wanajamii, mashirika au vikundi ili kusuluhisha matatizo ya kiafya katika jamii. Katika Kipindi hiki cha somo tunalengo matatizo ya kiafya yanayotokea katika kipindi cha baada ya kuzaa. Uhamasishaji wa jamii ni mchakato endelevu na limbikizi wa mawasiliano, elimu na mpangilio ili kujenga nafasi za uongozi na utekelezaji.

1.6.1 Mbinu za kuhamasisha utendaji wa jamii

Kisanduku 1.1 linatoa muhtasari wa mbinu kuu za uhamasishaji wa jamii. Hapa tunaziangazia kwa kifupi kwa sababu ushakumbana na mbinu zote katika moduli juu ya Elimu ya Afya, Utetezi na Uhamasishaji wa Jamii.

Kisanduku 1.1 Mbinu za uhamasishaji wa jamii

Mabango: Mabango yaliyobuniwa vizuri na kuwekwa mahali panapofaa yanaweza kuwasilisha jumbe ili kuwakumbusha watu mara kwa mara kuhusu suala husika.

Uandikaji barua: Hii ni njia moja ya kuwasilisha jumbe za kiafya kwa wanajamii wasomi. Barua hutoa ujumbe sahihi na inaweza kuwekwa ili kurejelewa baadaye.

Kurasa zenye vielelezo: Picha ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe kwa watu wasioweza kuelewa barua kutokana na ujuzi wao haba wa kusoma(Picha1.3).

Kuwatembelewa nyumbani: Hii ndio njia bora zaidi ya kuihamasisha jamii kwa sababu unaweza kuwa na hakika kuwa ujumbe umewasilishwa.

Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa/Indrias Getachew
Picha 1.3 Kurasa zenye vielelezo katika lugha ya mahali pale zinaweza kusaidia kuwasilisha jumbe zako za kiafya kwa kina mama waliozaa.

Msingi wa uhamasishaji wa jamii ni kushiriki pakubwa kwa jamii ambako hufanyika wanajamii wanaposhiriki katika kutambua matatizo na mahitaji na kisha wapange, watekeleze, wasimamie na kutathmini shughuli za jamii ili kutatua tatizo hilo.

Kanuni ya kimsingi unayofaa kukumbuka ni kuwa hauko pale ‘kushurutisha’ ushiriki wa jamii. Wajibu wako ni kuchunguza, kujifunza kutoka kwa hekima ya jamii na kuelimisha na kuwarai wanajamii kuleta mabadiliko yatakikanayo - katika muktadha huu, kuboresha matokeo baada ya kuzaa. Neno na uamuzi wa mwisho huwa ya jamii.

1.6.2 Je, Kwa nini kushiriki kwa jamii ni muhimu sana?

Watu huwajibika wanapohusika na kushiriki katika shughuli fulani. Hii husaidia kwa kudumisha ari, shughuli na mipango. Pia ina manufaa haya:

  • Kuongezeka kwa upatikanaji wa raslimali wanajamii wanapotoa kwa hiari wakati na raslimali zao kwa yale wanayoyachukulia kuwa ari na shughuli zao.
  • Kuleta dhana ya umoja kati ya wanajamii.
  • Kuongezeka kwa matumaini mafanikio ya matoleo yao yanapoonekana.
  • Watu Kuwezeshwa kutumia ujuzi na talanta zao na kukuza uwezo wao.
  • Mbadiliko wa mienendo kuwa haraka na rahisi.
  • Urahisishaji wa uzuiaji wa asasi za kijamii zenye madhara.

1.6.3 Kujenga ushirikiano na watu mashuhuri katika jamii

Watu wa kwanza kulenga kwa utunzaji wa baada ya kuzaa ni mama, mtoto wake mchanga na baba. Hata hivyo kuna watu wa kulenga baadaye ambao ni watu mashuhuri katika jamii wanaoweza kushawishi uamuzi unaoathiri afya ya mama na mtoto. Unahitaji kuwahusisha watu hawa kutoka mwanzo unapotanguliza huduma za utunzaji wa baada ya kuzaa katika jamii yako. Zingatia kuhusisha:

  • Wasimamizi rasmi wa kijiji
  • Viongozi wa kidini, vikundi vya makanisa au misikiti
  • Viongozi mashuhuri na wazee wa kijiji
  • Mashirika au vyama vya wanawake
  • Mashirika ya vijana
  • Kamati za kijamii katika eneo hilo
  • Mashirika ya wakulima au ya ukulima
  • Wakunga na madaktari wa kienyeji
  • Wanao uza dawa vijijini
  • Wengineo unaoweza kufikiria ni muhimu kwa hali maalumu.

Bila ushirikiano wa watu binafsi na vikundi hivi, itakuwa vigumu kutoa utunzaji bora baada ya kuzaa. Hasa ni muhimu kuimarisha uhusiano bora na upatanishe juhudi zako na za wakunga wa kienyeji. Shughuli zifuatazo zitakusaidia kutimiza haya (Kisanduku 1.2)

Kisanduku 1.2 Kujenga ushirikiano na wakunga wa kienyeji
  • Wasiliana na wakunga wa kienyeji katika jamii yako kisha mjadiliane jinsi ya kusaidiana katika kutoa utunzaji wa baada ya kuzaa kwa wanawake, watoto wachanga na familia. Kwa pamoja mnaweza kuibuka na maarifa mapya yaliyo mwafaka zaidi kwa mahali pale.
  • Heshimu maarifa, uzofeu, maoni na ushawishi wao. Waulize waeleze maarifa wanayoshiriki na jamii.
  • Shiriki nao habari kuhusu utunzaji wa baada ya kuzaa. Toa nakala za elimu ya afya ambazo ungependa kusambaza kwa wanajamii na ujadiliane nao yaliyomo.
  • Wahusishe katika vikao vya kutoa ushauri kwa familia na wanajamii wengine. Wajumuishe katika mikutano yako na viongozi wa jamii na vikundi mashuhuri.
  • Jadili pendekezo kuwa kila uzalishaji unafaa kufanywa na mhudumu mwenye ujuzi kama wewe. Iwapo hili haliwezekani au halipendelewi na mwanamke huyo na familia yake, jadili jinsi wakunga wa kienyeji wanavyoweza kutoa utunzaji bora zaidi wa baada ya kuzaa, na ni katika hali zipi wanapopaswa kutoa rufaa ya dharura mwanamke huyo aje kwako au aende katika kituo cha afya cha juu.
  • Hakikisha wakunga wa kienyeji wamejumuishwa katika utaratibu wa kutoa rufaa na uwape majibu kuhusu wanawake waliowatuma kwako.
  • Je, kwa nini unafikiri ni muhimu kuwahusisha wakunga na madaktari wa kienyejii jinsi ilivyoelezewa hapo awali?

  • Wao ni wambia muhimu kwa sababu wanajua desturi za mahali pale, wanaheshimiwa na wanajamii na wana uzoefu mwingi wa kukabiliana na mengi ya matatizo ya kijamii yanayotokea katika kipindi baada ya kuzaa.

    Mwisho wa jibu

  • Dhania kuwa wewe ni mkunga wa kienyenji mwenye uzoefu wa miaka mingi. Muhudumu wa afya nje ya hospitali anaanza kufanya kazi katika kijiji chako kisha aombe usaidizi wako. Je, ni mambo gani yanayoweza kukufanya uweze kushirikiana naye kusaidia kazi yake?

  • Kwa kweli jibu sahihi si moja tu kwa swali hili jinsi tu ilivyo kwamba majibu yote hayatamfaa mkunga mmoja kwa usawa. Hata hivyo huenda ulitaja pia yafuatayo:

    • Anakutendea vyema kwa heshima na kama mwenzi.
    • Anaonyesha moyo wa kupenda kujua kuhusu uzalishaji wa kienyeji katika kijiji chako.
    • Unaweza kuona kuwa anathamini maarifa na uzoefu wako.
    • Anakupa fursa ya kujifunza kuhusu mbinu mpya za kuzalisha.
    • Anakusihi uungane naye kama mbia katika juhudi za pamoja ili kuboresha utunzaji baada ya kuzaa kwa wanawake na watoto wachanga katika kijiji chako.
    • Anakualika katika mikutano yake na viongozi wa kijiji na watu wengine mashuhuri ili kuhamasisha jamii kuunga mkono huduma za utunzaji baada ya kuzaa.

    Mwisho wa jibu

1.7 Kukagua wasifu wa jamii

Ulijifunza jinsi ya kukagua wasifu wa jamii katika Kipindi cha 1 cha somo cha utunzaji katika ujauzito.

Unapaswa kujua idadi kamili ya watu unaoenda kuhudumia na jinsi ya kukusanya takwimu muhimu kama vile za uzazi, vifo na habari kuhusu uhamaji na uhamiaji wa watu katika sehemu hiyo. Unahitaji pia kuweka kumbukumbu ya wanawake wote walio katika umri wa uzazi (takribani miaka 15 hadi 45) ambao wanaweza kupata ujauzito siku za baadaye na iadadi ya wanawake wajawazito wakati huo na wanapotarajiwa kuzaa

Unapaswa kuandika majina na anwani za wakunga wote wa kienyeji, madaktari wa kienyeji, wanaouza dawa vijijini na madaktari wengineo wa kibinafsi. Sajili mifumo yote ya kijamii inayoweza kukusaidia kwa uhamasishaji wa raslimali za kibinadamu, kifedha na kiusafiri iwapo rufaa za dharura zitahitajika kwa mama na mtoto. Utajifunza kuhusu mfumo wa rufaa katika Kipindi cha mwisho cha somo katika moduli hili. Habari hii yote inafaa kutengenezwa na kuboreshwa zaidi kila baada ya miezi minne hadi sita.

Huenda usihitaji kuendesha umahasishaji wa jamii kivyake kwa utunzaji wa baada ya kuzaa. Uhamasishaji huu unapaswa kufanywa kwa pamoja na wa huduma za afya kwa kina mama, watoto wachanga na watoto katika jamii. Kisanduku 1.3 Ni muhtasari wa shughuli za uhamasishaji wa jamii ili kuendeleza utunzaji wa baada ya kuzaa.

Kisanduku 1.3 Huduma za baada ya kuzaa katika jamii

  • Tembelea viongozi binafsi wa jamii, wakunga wa kienyeji, madaktari wa kienyeji ili kupata msaada wao
  • Panga mikutano ya maelekezo kwa viongozi na watu mashuhuri.
  • Pamoja na viongozi wa jamii na wakunga wa kienyeji andaa mikutano ya kuelimisha wanajamii kuhusu utunzaji baada ya kuzaa.
  • Zuru nyumba kwa nyumba ili kuwafundisha wazazi na watunzaji kuhusu utunzaji baada ya kuzaa (picha 1.4)
  • Sambaza vifaa vya habari, elimu na mawasiliano kwa viongozi na wanajamii.
Picha 1.4 kutembelewa nyumbani na mhudumu wa afya kunaweza kusaidia kina mama waliozaa kujifunza ujuzi mpya. (Picha: Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa)

Muhtasari wa Kipindi cha 1

Katika Kipindi cha 1 umejifunza kuwa:

  1. Uwiano wa vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na kiwango cha vifo vya watoto wachanga barani Africa viko miongoni mwa viwango vya juu sana ulimwenguni
  2. Takribani asilimia 45-50 ya kina mama na watoto wachanga hufariki katika saa 24 za kwanza baada ya uzazi na asilimia 65-75 ya vifo vya kina mama na vya watoto wachanga hutokea katika juma la kwanza.
  3. Utunzaji bora baada ya kuzaa katika saa sita za kwanza na baada ya siku mbili, sita na majuma sita unaweza kupunguza vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto wachanga kwa kiwango kikubwa.
  4. Visababishi vya mara kwa mara vya vifo vya kina mama muda mfupi baada ya kuzaa ni kutokwa na damu, eklampsia, maambukizi na kupasuka kwa uterasi.
  5. Visababishi vikuu vya vifo vya watoto wachanga ni maambukizi, asfiksia ya kuzaliwa, kuzaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na kuzaliwa na uzito wa chini
  6. Kipindi baada ya kuzaa ni wakati wa marekebisho ya haraka ya kifiziolojia kwa mama kurudi katika hali ya kutokuwa na ujauzito na kwa mtoto mchanga anayezoea maisha nje ya uterasi.
  7. Dalili za hatari kwa mama katika kipindi cha baada ya kuzaa ni uterasi kutopungua sawasawa, kutokwa na damu ukeni na mshtuko.
  8. Dalili za hatari kwa mtoto mchanga ni umanjano, ugumu katika kupumua, kiwango juu cha joto mwilini na dalili zingine za maambukizi, hipothemia, kutapika mara kwa mara na kutokwa na damu kutoka kwa kitovu au mkundu.
  9. Kabla ya kuanzisha huduma za utunzaji wa baada ya kuzaa, unapaswa kuendesha vikao vya uhamasishaji ili kuhakikisha kushiriki kikamilifu kwa jamii. Wahusishe viongozi wa jamii, wakunga na madaktari wa kienyeji. Pia zuru nyumba kwa nyumba ili kuwafundisha wazazi na watunzaji na usambaze vifaa vya habari, elimu na mawasiliano.

Maswali ya kujitathmini kwa Kipindi cha 1

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, unaweza kutathmini ni kwa kiwango kipi umeweza kuyatimiza malengo ya somo hili kwa kujibu maswali yafuatayo. Andika majibu yako katika shajara yako kisha ujadiliane na mkufunzi wako katika mkutano saidizi wa masomo utakaofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya maswali ya kujitathmini yaliyo mwishoni mwa moduli hii.

Swali la kujitathmini 1.1 (linatathmini Malengo ya Somo la 1.1)

Ifuatayo ni orodha ya maneno muhimu yaliyotumiwa katika Kipindi hiki cha somo. Kila neno na ufafanuzi. Ni ufafanuzi upi hapa chini ulio (i) sahihi kabisa (ii)sahihi kwa kiasi fulani na (iii) si sahihi. Andika sentensi fupi kwa kila mmoja wa ufafanuzi ulio sahihi kwa kiasi fulani au usio sahihi kwa kulitumia neno hilo kwa usahihi.

  • a.Mtoto mchanga - ni mtoto aliyezaliwa
  • b.Utunzaji baada ya kuzaa - utunzaji anaopewa mtoto mara tu baada ya kuzaliwa
  • c.Kiwango cha vifo vya watoto wachanga - idadi ya watoto wanaofariki katika siku 28 za kwanza za maisha yao kwa kila 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai.
  • d.Kipindi mwanzoni mwa uchanga - kipindi punde tu baada ya kuzaliwa hadi mwisho wa siku saba za kwanza za maisha.
  • e.Uwiano wa vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa - idadi ya kina mama wanaofariki kutokana na kuzaa.
  • f.Kiwango cha vifo vya watoto mwanzoni mwa uchanga - idadi ya watoto wanaofariki punde tu baada ya kuzaliwa.
  • g.Kipindi cha uchanga - kipindi tangu kuzaliwa hadi siku 28 baada ya kuzaliwa
  • h.Mbadilishano wa gesi - hali wanayojishughulisha nayo raia wa Marekani waendapo kwenye kituo cha petroli.
  • i.Umanjano kwa watoto wachanga - hali inayoweza kutokea ini la mtoto mchanga lisipoweza kuzimua sumu kikamilifu katika damu.
Answer
  • a.Sahihi: mtoto mchanga ni mtoto mchanga.
  • b.Sahihi kwa kiasi fulani: ni utunzaji unaotolewa kwa mtoto na mama yake mara tu baada ya kuzaa na kwa muda wa majuma sita ya kwanza ya maisha.
  • c.Sahihi: kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni vifo vya watoto wachanga katika siku 28 za kwanza za maisha kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai.
  • d.Sahihi : mwanzoni mwa kipindi cha uchanga ni tangu kuzaliwa hadi siku 7 za kwanza.
  • e.Sahihi kwa kiasi fulani: ni idadi ya kina mama wanaofariki wakati wa kuzaa na kutokana na matatizo yatokeayo mara tu baada ya kuzaa. Barani Afrika, kiwango cha vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa kiko juu sana kikiwa na takribani vifo 673 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai. Kumbuka kuwa kiwango cha vifo vya watoto wachanga hukadiriwa kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai ilhali Kiwango cha vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa hukadiriwa kwa kila watoto 100,000 wanozaliwa wakiwa hai.
  • f.Si sahihi: ni idadi ya vifo katika juma la kwanza la maisha kwa kila watoto 1,000 wanozaliwa wakiwa hai. Hii pia iko juu sana barani Afrika ambapo ni takribani vifo 39 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai.
  • g.Sahihi: kipindi cha uchanga ni tangu kuzaliwa hadi siku ya 28.
  • h.Si sahihi: ni mchakato ambapo mapafu yetu hufyonza oksijeni na kutoa monoksidi ya kaboni. Mchakato huu hutendeka tangu kuzaliwa.
  • i.Sahihi: Kwa undani zaidi, kinachotendeka ni kuwa ini hukosa kuitoa protini ya bilirubini ambayo hutolewa katika mchakato wa kuharibu seli zee nyekundu za damu. Dalili ya umanjano kwa mtoto mchanga (yaani malimbikizo ya bilirubini) ni ambapo ngozi huanza kuwa na rangi ya manjano hasa kwa viganja na nyayo za mtoto.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 1.2 (linatathmini malengo ya Somo la 1.2 na 1.5)

Dhania kuwa unajaribu kumshawishi Waziri wa Fedha wa bara Afrika kuweka pesa zaidi kwa utunzaji wa kiafya baada ya kuzaa na anataka ushahidi kuhusu sababu zake kufanya hivyo. Andika barua fupi ukieleza kwa muhtasari hoja kuu utakazosisitiza.

Answer

Kuna hoja nyingi unazoweza kumtolea Waziri huyo wa Fedha. Zifuatazo ni baadhi ya zile muhimu:

  • Afrika ina baadhi ya viwango vya juu sana vya vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto mwanzoni mwa kipindi cha uchanga duniani (unaweza kutaja tarakimu halisi).
  • Kipindi cha hatari kubwa (yaani, mara tu baada ya kuzaa na katika siku 7 za kwanza za maisha na hadi mpaka siku 28) pia ni wakati ambapo kuna kiwango cha chini cha matumizi ya huduma za utunzaji wa afya ya mama na mtoto katika Afrika.
  • Utunzaji bora zaidi wa baada ya kuzaa ni lazima utendeke katika saa chache za kwanza au utakuwa umechelewa sana. Utatuzi mwafaka katika kipindi cha baada ya kuzaa una uwezo wa kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 10-27. Hii itaisaidia Afrika kutimiza Malengo ya Millenia ya Maendeleo ya kupunguza vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto.
  • Tayari tunajua visababishi vikuu vya vifo katika kipindi cha baada ya kuzaa (unaweza kumpa orodha hii) na tunajua vyema cha kufanya kuhusu haya na hili hasa ni suala la kuwepo kwa mhudumu wa afya aliyehitimu ili kutekeleza hayo.
  • Unaweza pia kusisitiza kuwa ili uweze kufaa zaidi, utunzaji wa baada ya kuzaa huhitaji pia kuhusisha jamii (kuwafanya wahusike katika mchakato wote kuwezesha kubadilika kwa mienendo duni ya kitamaduni na mengineyo) kisha umuelezee jinsi utakavyokuwa ukiyatekeleza haya, kwa mfano kuzungumza na watu mashuhuri na utambulishe msaada wa wakunga wa kienyeji katika jamii.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 1.3 (linatathmini malengo ya Somo la1.3 na 1.4)

Umefanya kazi nzuri kumshawishi Waziri wa Fedha. Hata hivyo, amemtaka Waziri wa Afya achunguze na kuthibitisha ikiwa kweli unafahamu unachokizungumzia. Anakutaka uorodheshe dalili kuu za matatizo yanayoweza kutokea unazopaswa kuchunguza kwa mama aliyezaa na dalili kuu za hatari kwa mtoto mchanga. Je, utaandika nini katika orodha yako?

Answer

Dalili za hatari kwa mama aliyezaa:

Dalili kuu za kuchunguza ni ukosefu wa maji mwilini, uterasi isiyopungua ipaswavyo, kutokwa na damu upya, kupungua kwa shinikizo la damu na kupanda kwa mpwito wa ateri. Dalili za hatari za muda mrefu unazopaswa kujua ni kuganda kwa damu na dipresheni.

Dalili za hatari kwa mtoto mchanga

Unayopaswa kuchunguza kwanza ni: je, mtoto ananyonya vizuri, rangi ya ngozi ni ya kawaida au ni ya manjano, kuna joto la juu mwilini, mtoto ni baridi au vuguvugu sana akiguswa, kupumua ni kwa kawaida, kuna kutokwa na damu, vigubiko vya macho ya mtoto ni vyekundu au vimevimba? Pia utachunguza ikiwa mtoto alizaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha ili kutambua ikiwa yuko katika hatari zaidi ya kupata matatizo mengine. Huenda ulipata mengi ya haya. Ikiwa haukupata mengi ya haya au hauwezi kukumbuka yanayoashiria, soma tena sehemu 1.5.2 ‘kumtathmini mtoto mchanga’

Mwisho wa jibu.