Skip to main content
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 9:43 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 9:43 PM

2. Puperiamu ya Kawaida

Kipindi cha 2 Puperiamu ya Kawaida

Utangulizi

Katika Kipindi hiki cha somo, utajifunza kuhusu mabadiliko ya kawaida yanayotokea kwa wanawake katika majuma sita ya kwanza baada ya kuzaa. Kipindi hiki cha baada ya kuzaa pia kinajulikana kama puperiamu hasa kwa madaktari, wauguzi na wakunga. Mabadiliko haya huhusisha mchakato wa kawaida wa marekebisho ya kisaikolojia katika kipindi hiki. Je, unakumbuka mabadiliko ya kifiziolojia katika ujauzito uliyojifunza kwenye Kipindi cha 3 cha somo moduli ya Utunzaji katika Ujauzito? Hapa tunalenga urekebishi wa kawaida puperiamu, hasa mabadiliko yanayotokea katika mfumo wa uzazi na mifumo mingine ya mwili.

Wanawake wengine unaowahudumia baada ya kuzaa huenda wasielewe mabadiliko yote wanayoyapitia baada ya kuzaa. Wanaweza kushtuliwa na mabadiliko ambayo ni ya kawaida kabisa au wapuuze dalili ambazo kwa hakika ni za hatari. Wanawake wengine huona kulea mtoto mchanga kuwa jambo la kawaida na rahisi ilhali kwa wengine, jukumu hili ni gumu. Kama mhudumu wa afya anayeihudumia jamii nje ya hospitali, una fursa ya kipekee ya kuwasaidia kina mama na familia zao kustahimili marekebisho hayo katika kipindi cha baada ya kuzaa.

Malengo ya mafunzo ya Kipindi cha 2

Katika Kipindi hiki, utajifunza:

2.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote yaliyoandikwa katika herufi nzito (Swali la kujitathmini 2.1).

2.2 Kueleza kuhusu miitiko ya kifiziolojia inayotarajiwa katika puperiamu ya kawaida kwa kina mama waliozaa (Swali la kujitathmini 2.2).

2.3 Kueleza ushauri utakaowapa kina mama waliozaa ili waweze kujitunza nyumbani kwao katika puperiamu (Swali la kujitathmini 2.2).

2.1 Mabadiliko kwenye viungo vya uzazi katika puperiamu

Matukio muhimu ya kifiziolojia katika puperiamu ni kurudi kwa viungo vya uzazi na viwango vya homoni za kike katika hali ilivyokuwa kabla ya ujauzito. Tutaeleza kwa kifupi mabadiliko haya na kulenga yanayoweza kutarajiwa kwa mwanamke asiyepata matatizo baada ya kuzaa.

2.1.1 Uterasi

Uterasi ya mwanamke aliye na ujauzito uliokomaa huongezeka kwa ukubwa angalau mara kumi zaidi ilivyokuwa kabla ya ujauzito. Uterasi (bila kuongeza uzani wa mtoto, plasenta, guliguli aminio na kadhalika) huwa na uzani wa takriban kilo 1, ilhali uzani wake kabla ya ujauzito huwa kati ya gramu 50 hadi 100. Mara tu mtoto anapozaliwa, uterasi inaweza kutomaswa karibu na kitovu cha mwanamke huyo inaponywea ili kuondoa plasenta na membreni ya fetasi. Uterasi hunywea na kurudi katika hali yake ya awali ya kabla ya ujauzito katika wiki sita ya kwanza baada ya kuzaa. Hata hivyo, mwingi wa upunguaji huu wa uzani na ukubwa wa uterasi hufanyika katika majuma mawili ya kwanza. Kufikia wakati huu, uterasi inafaa kuwa imenywea kwa kiasi cha kuweza kutosha katika pelvisi ya mwanamke huyo chini ya kitovu.

Bitana ya ndani ya uterasi (endometriamu) hupona kwa haraka baada ya kuzaa ili kurejea katika hali yake ya kawaida uterasini mwote isipokuwa eneo la plasenta kufikia siku ya saba. Ndani ya uterasi, sehemu ambapo plasenta ilikuwa imejishikiza hukumbwa na mabadiliko ambayo hupunguza idadi ya kapilari za damu zinazoingia katika eneo hilo. Kapilari zitakazobaki huvuja kiowevu cha damu kwa muda fulani na husababisha kutoka kwa mchozo wa kawaida ukeni uitwao lokia. Mchozo huu mara nyingi huendelea kwa majuma kadhaa baada ya kuzaa. Lokia huwa na damu yenye rangi ya karibu kati ya kahawia na nyekundu katika juma la kwanza lakini hubadilika muda unaposonga na kuwa maji maji yanayotiririka. Mchozo huu huendelea kupunguka na rangi yake kubadilika kuwa manjano hafifu. Kipindi ambapo lokia huendelea kutoka hutofautiana. Hata hivyo, muda wa wastani ni takribani majuma matano unaoambatana na mabadiliko katika kiasi na rangi ya mchozo huu. Kila mwanamke anao mtindo wake mwenyewe ulio na awamu hizi mbalimbali za lokia zinazodumu kwa muda tofauti.

2.1.2 Seviksi

Mara tu baada ya kuzaa, kuta zenye misuli za seviksi hulegea, huwa nyembamba na zilizotanuka. Seviksi inaweza pia kuonekana iliyovimba na kuvilia kutokana na kuzaa. Pia inaweza kuwa na mikato midogo katika sehemu ambapo tishu iliraruka mtoto alipokuwa akizaliwa. Hata hivyo, seviksi kwa kawaida huwa imepungua na kurudi katika hali yake thabiti katika siku ya kwanza. Mwanya wa uke unafaa kuwa na kipenyo cha vidole viwili saa 24 baada ya kuzaa na kipenyo cha kidole kimoja ifikiapo mwisho wa juma la kwanza ukiuchunguza kwa kutumia mkono uliovishwa glavu.

2.1.3 Uke na vulva

Uke uliopanuliwa sana ili kumruhusu mtoto kupita hunywea pole pole ukirejea katika ukubwa na hali yake ya kawaida ilivyokuwa kabla ya ujauzito kwa kipindi cha takribani wiki tatu baada ya kuzaa. Kufikia wakati huu, upitaji zaidi wa damu na kuvimba kwa uke na vulva kunapaswa kuwa kumedidimia. Mwanamke huyo anaweza kuanza tena kushiriki ngono iwapo lokia imekoma, uke na vulva zimepona, hana maumivu na yuko tayari kihisia. Hali ya mwili kuwa tayari kwa kawaida huchukua takribani muda wa majuma matatu hadi matano. Hata hivyo, mwanamke huyo anaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kujisikia kuwa tayari kushiriki ngono na basi hapaswi kulazimishwa kukubali. Jukumu lako ni kuzungumza kwa upole na mwenzi wake ili kuhakikisha kuwa anaelewa na kuheshimu hisia za mwanamke huyo. Katika jamii nyingi kuna desturi inayothibiti wakati ambapo ngono inafaa kurejelewa na mara nyingi huwa baada ya puperiamu kuisha ambayo huwa baada ya majuma sita tangu kuzaa.

Kumbuka kuwa upangaji uzazi ni muhimu kwa kujikinga dhidi ya kupata ujauzito mwingine mara tu baada ya kuzaa. Ovulesheni ya kwanza haiwezi kutabirika na mwanamke anaweza kupata ujauzito tena hata kabla ya kurudi kwa hedhi yake ya kwanza.

Uzazi wa majira ulijadiliwa katika Kipindi cha 14 cha somo la moduli ya Utunzaji katika Ujauzito.

  • Je, ni nini manufaa ya kutumia njia ya kupanga uzazi baada ya kuzaa ili kutoa nafasi ya kuzaa watoto zaidi?

  • Muda wa angalau miaka miwili kati ya uzazi na hata bora zaidi muda huu ukiwa mrefu zaidi hupunguza hatari ya kupata matatizo katika ujauzito utakaofuata. Pia huongeza afya ya fetasi mpya na mtoto mchanga aliyezaliwa awali ambaye huenda bado anahitaji utunzaji na uangalifu wa mama (Picha 2.1).

    Mwisho wa jibu

Picha 2.1 Jukumu la mhudumu wa afya katika jamii ni kuwasaidia kina mama kutumia upangaji uzazi ili kuwe na nafasi kati ya watoto wao. (Picha: Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa/ Indrias Getachew)

2.1.4 Msamba

Msamba ni sehemu ya mwili iliyo kati ya mwanya wa uke na mwanya wa mkundu. Sehemu hii hutanuliwa na kujeruhiwa na wakati mwingine kuraruliwa katika kuzaa. Vile vile mkunga stadi anaweza kuukata kwa kukusudia kwa kutumia makasi yaliyotiwa kifisha vijidudu ili kuupanua mwanya na kumsaidia mtoto kutoka. Nyingi ya nguvu za misuli ya msamba hurejea katika muda wa majuma sita baada ya kuzaa na kuimarika zaidi katika miezi michache ifuatayo. Unaweza kumsaidia mama kurudisha nguvu za misuli kwa kumhimiza kukaza na kulegeza misuli ya msamba mara kumi mara tu anapoweza kufanya hivyo na kurudia zoezi hili mara kadhaa kila siku. Kuuimarisha msamba ni muhimu kwa sababu ndio unaotengeneza msingi wa kaviti ya pelvisi ambayo huhimili uterasi, uke na kibofu cha mkojo.

2.1.5 Ukuta wa fumbatio

Ukuta wa fumbatio hubakia laini na dhaifu sana kwa majuma mengi baada ya kuzaa, lakini huimarika muda unavyosonga. Jinsi uthabiti wa misuli unavyorejelea hali ilivyokuwa kabla ya ujauzito hutegemea kiasi cha mazoezi anayofanya mwanamke huyo anapopata nafuu kikamilifu. Kwa wanawake wa vijijini wanaofanya kazi katika mashamba na nyumbani, tatizo linaweza kuwa mavune kwenye misuli ya fumbatio (kwa mfano kwa kuinua vitu vizito) mara tu baada ya kuzaa.

2.1.6 Ovari

Ubadilikaji wa ovari na urudiaji hali yake ya kawaida ni wa kubadilika na huathiriwa pakubwa na unyonyeshaji wa mtoto huyo mchanga. Mwanamke anayemnyonyesha mtoto tu pasipo kumpa vyakula vingine vyovyote hukosa hedhi kwa kipindi kirefu na ovulesheni yake ya kwanza baada ya kuzaa huchelewa akilinganishwa na mama anayempa mtoto maziwa kwa chupa. Mwanamke asiyenyonyesha anaweza kutoa ova mapema kabisa kama vile majuma manne baada ya kuzaa na wengi wao hupata hedhi ifikiapo juma la kumi na mbili. Muda wa wastani kwa hedhi ya kwanza kwa mwanamke asiyenyonyesha ni majuma saba hadi tisa baada ya kuzaa.

Wakati wa kuanza kwa hedhi kwa mwanamke anayenyonyesha ni wa kubadilika sana na hutegemea vipengele kadhaa vikiwemo ni kwa kiasi kipi na ni mara ngapi mtoto huyo hulishwa, na ikiwa chakula hiki kimeongezwa maziwa bandia. Ovulesheni husitishwa kwa mwanamke anayenyonyesha na homoni itolewayo kwenye tezi ya pituitari iliyo ubongoni mtoto anaponyonya. Nusu hadi theluthi tatu za wanawake wanaowanyonyesha watoto wao pasipo kuwapa vyakula vingine vyovyote huanza kipindi chao cha kwanza cha hedhi katika majuma 36 baada ya kuzaa.

  • Je, ni ushauri upi unaoweza kumpa mama aliyezaa mara ya kwanza hivi karibuni na ananyonyesha akikuuliza anapoweza kuanza tena kushiriki ngono?

  • Unaweza kusema kuwa baada ya mchozo utokao ukeni (lokia) kukoma na kuwa wa rangi ya manjano hafifu (baada ya majuma matano hadi saba), anaweza kuanza tena kushiriki ngono ikiwa anahisi yuko tayari kimwili na kihisia. Unaweza pia kumweleza kuwa unyonyeshaji hufanya iwe vigumu kutabiri wakati atakapoanza kutoa ova tena. Pia, unaweza kumshauri kuwazia swala la upangaji uzazi kwa kufafanua hatari za ujauzito mwingine mara tu baada ya kuzaa na manufaa ya uzazi wa majira ya miaka miwili au zaidi.

    Mwisho wa jibu.

2.1.7 Matiti na mwanzo wa utungaji wa maziwa

Tukio jingine muhimu mara tu baada ya kuzaa ni mwanzo wa utungaji wa maziwa (kutengenezwa kwa kolostramu na kisha maziwa kwenye matiti) na kutolewa kwa viowevu hivi vyenye virutubishi mtoto anaponyonya chuchu ya mama. Matiti huanza kukuza uwezo wa kutengeneza maziwa ujauzito unapoendelea kukua kama mwitiko kwa homoni zinazozunguka katika damu ya mama. Kwa siku chache za kwanza baada ya kuzaa, matiti hutoa kolostramu (dutu yenye rangi ya malai). Kolostramu huwa na virutubishi vingi vya mtoto na pia antibodi za mama ambazo humkinga mtoto mchanga dhidi ya maambukizi. Kwa sababu hii, ni muhimu sana watoto wote walishwe kolostramu. Katika baadhi ya maeneo barani Afrika, tendo la kuwalisha watoto wachanga kolostramu linachukuliwa kuwa lisilo zuri na salama kiafya. Hata hivyo, jaribu kumshawishi mama huyo asiyatupe maziwa hayo hata akionekana mwenye kusita.

Antibodi ni protini maalumu zinazosaidia kutambua na kuharibu visababishi vya maambukizi.

Matiti huwa imara na kuanza kutoa maziwa siku tatu baada ya kuzaa kama mwitiko kwa mwongezeko wa homoni zitokazo kwenye tezi ya pituitari zinazochochea utengenezaji wa maziwa. Matiti hayo hufuka, huwa ngumu na yenye joto kwa haraka kutokana na ongezeko la damu, hali hii ya matiti huitwa kutuna, yaani, kuongezeka katika ukubwa wa ogani kutokana na mrundikano wa damu (Picha 2.2). Hali hii huendelea kwa muda wa takribani saa 24-48 na kisha kurudi katika hali yake ya kawaida kivyake. Baada ya haya, matiti kamwe si magumu na pia hayana joto bali huwa imara na laini yanavyojazwa maziwa kutoka safari moja ya unyonyeshaji hadi nyingine, na kuwa laini na kupungua katika ukubwa maziwa yanapoondolewa kupitia unyonyaji wa mtoto. Utengenezaji wa maziwa unaoendelea huchochewa na unyonyaji wa mtoto. Jinsi mtoto anyonyavyo ndivyo matiti yanavyoendelea kutengeneza maziwa.

Picha 2.2 Takribani siku tatu baada ya kuzaa, ukubwa wa matiti umeongezeka yanavyojazwa na maziwa kwa mara ya kwanza. (Picha:Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa)

Unapaswa kuwashauri kina mama waliozaa mara ya kwanza kuwa kuanza kunyonyesha mapema (katika saa moja baada ya kuzaa) na kumnyonyesha mtoto pasipo kumpa vyakula vingine vyovyote (mtoto asipewe vyakula wala viowevu vingine vyovyote) katika miezi sita ya kwanza ndio mwanzo mwema wa kilishe maishani. Mruhusu mtoto kunyonya kila anapotaka kula tangu siku ya kwanza na kuenedelea. Unyonyeshaji kamwe si rahisi wala haufanyiki tu wenyewe na huchukuwa muda mwingi kila siku mchana na pia usiku. Mama anahitaji nguvu nyingi kumnyonyesha mtoto wake kwa miezi sita bila kumpa chakula kingine chochote kile. Kutengeneza maziwa mengi yenye virutubishi vingi huhitaji nguvu nyingi za ziada. Mama huyu anahitaji virutubishi na viowevu zaidi. Kwa hivyo, mshauri anywe viowevu safi kwa wingi na ajaribu iwezekanavyo kula mlo zaidi kila siku katika muda wake wa kunyonyesha. Habari kamili kuhusu unyonyeshaji imeelezewa katika Kipindi cha 7 cha somo.

Ukomeshaji wa utungaji wa maziwa kwa wanawake wasionyonyesha

Kunazo hali ambapo mama hawezi au hatanyonyesha. Kwa mfano, ikiwa mtoto amezaliwa akiwa amefariki au akifariki katika majuma kadhaa ya kwanza, au mama anapostahabu kwa dhati kumlisha mtoto wake maziwa mbadala chupani, imependekezwa kuwa mwanamke huyo afungwe bendeji ya kubana katika kifua chake ikifunika matiti katika siku mbili hadi tatu za kwanza baada ya kuzaa ili kupunguza matatizo ya ukubwa unaoendelea wa matiti. Uangalifu unafaa kudumishwa ili matiti yasichochewe kwa njia yoyote ile kutengeneza maziwa. Vibonge vya barafu pia vinaweza kuwekwa kwenye matiti na mama kupewa dawa za kutuliza maumivu zilizo na aspirini au paracetamol ili kupunguza wepesi wa matiti kuumia.

2.1.8 Kuondolewa kwa viowevu vya mwili vya ziada

Mwili wa mwanamke huwa na viowevu vingi wakati wa ujauzito kuliko wakati ambapo hana ujauzito. Kiasi fulani cha maji haya ya ziada huwa kwenye tishu zake, mengine kwenye damu yake iliyoongezeka na mengine kwenye uterasi. Maji haya ya ziada huondolewa haraka baada ya kuzaa. Guliguli aminio hutokea kwenye uke. Kutoka siku ya pili baada ya kuzaa, kiasi cha mkojo kitaongezeka kwa siku kadhaa hadi lita tatu kwa siku lakini hurudi katika mkondo wake wa kawaida katika muda wa juma moja. Nafasi ya kibofu huongezeka na kuwa na ujazo wa mililita 1,000 hadi 1,500 za mkojo bila matatizo katika kipindi ambapo viowevu huondolewa mwilini. Kutakuwa na ongezeko la hatari ya maambukizi kwenye mfumo wa mkojo iwapo mkojo utabakizwa kibofuni kwa kipindi kirefu kutokana na urethra kufunga na kuvimba au kujeruhiwa kwa tishu baada ya kuzaa.

Ulijifunza kuhusu maambukizi ya mfumo wa mkojo katika Kipindi cha 18 cha Moduli ya Utunzaji katika ujauzito.

2.2 Habari muhimu kwa kina mama waliozaa mara ya kwanza

2.2.1 Kumtunza mtoto

Kina mama waliozaa kwa mara ya kwanza (na mara nyingi hata kina baba wa mara ya kwanza) wanafaa kufunzwa utaratibu wa kumtunza mtoto ukiwemo kumuogesha na kudumisha usafi wa mwili na nguo zake kutokana na kinyesi na mkojo. Wafundishe wazazi hawa wanachoweza kutarajia kutoka kwa mtoto kwa mujibu wa kulala, kukojoa, mwenendo wa matumbo, kula, na kulia. Sharti joto lidumishwe kwa mtoto. Hata hivyo, asifungwe kwa kukazwa. Anafaa kuchunguzwa kwa uangalifu mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hana baridi au joto jingi na anakula vizuri na kutoa kinyesi na mkojo wa kawaida mara kwa mara. Mengi kuhusu utunzaji wa mtoto mchanga yameangaziwa baadaye kwenye Moduli hii katika Kipindi cha 6 hadi cha 8 cha somo.

2.2.2 Kupumzika na kupona kwa mama

Ujauzito, uchungu wa kuzaa, kuzaa na utunzaji wa mtoto mchanga ni matukio yachokeshayo na yasababishayo mfadhaiko. Kwa hivyo, mama anahitaji pumziko la kutosha ndiposa apone. Pia, anahitaji habari kuhusu wakati mwafaka anapoweza kurejelea shughuli zake za kawaida. Mwambie kuwa anaweza kuanza tena kufanya baadhi ya shughuli za nyumbani katika siku mbili au tatu za kwanza baada ya kuzaa mradi hahisi uchungu au matatizo yoyote. Msingi wa kurejelea shughuli za kawaida si kufanya kazi kwa siku moja kiasi kwamba ajihisi mchovu kabisa siku itakayofuata.

2.2.3 Mbinu za kudhibiti uzazi

Mama pamoja na mwenzi wake wanapaswa kupewa ushauri kuhusu mbinu tofauti za kudhibiti uzazi. Huenda asiwe tayari kuamua mbinu yoyote lakini anafaa kuzijua mbinu tofauti zilizoko. Uamuzi wake utategemea vipengele kadhaa vikiwemo sababu za kutumia mbinu fulani, idadi ya watoto alionao na ikiwa ananyonyesha.

Kunazo mbinu nyingi tutakazozitaja kwa kifupi tu. Mbinu hizi zimeelezewa zaidi katika Moduli ya Upangaji uzazi.

  • Mbinu za kiasili zinahusisha kuchunguza hali ya kamasi la seviksi (ubora na kiasi). Hii inaweza kutumiwa vyema ili kuonyesha wakati ambapo mwanamke anatoa ova (ovulesheni). Hata hivyo, si njia mwafaka ya kuzuia ujauzito.
  • Kumnyonyesha mtoto bila kumpa vyakula vingine vyovyote na kumnyonyesha kila anapotaka kunaweza kutoa kinga dhabiti dhidi ya ujauzito kwa muda wa hadi miezi sita iwapo vipindi vya hedhi vya mwanamke huyu havijarejea.

  • Mbinu za kutumia vizuizi kwa uzuiaji ujauzito hutengeneza kizuizi kati ya mbegu ya kiume na uke au seviksi. Mbinu ya vizuizi inayotumika sana ni utumiaji wa kondomu za wanaume ambazo zinapatikana kote.
  • Mbinu za homoni za uzuiaji ujauzito ni tembe za kuzuia mimba, dawa za kuzuia ujauzito zinazoingizwa kwa sindano na vipandikizi (chuma kidogo sana kinachowekwa chini ya ngozi kilicho na homoni zinazotoka polepole ).
  • Vifaa vya kuzuia ujauzito vitiwavyo ndani ya uterasi hutiwa hapo ili kuzuia upandikizi wa kiinitete. Vinaweza kuwekwa mwishoni mwa puperiamu.
  • Mbinu za kudumu za kudhibiti uzazi ni kukata na kufunga mishipa ya falopio (inayotoka kwenye uterasi katika pande zote mbili ikielekea kwenye ovari) kwa wanawake na kukata mishipa inayosafirisha mbegu ya kiume kutoka kwa kende hadi kwa dhakari (vasektomi).
  • Bila kutazama nyuma katika sehemu zilizo hapo juu, jiandikie muhtasari mfupi wa hoja kuu utakazowaambia wazazi wa watoto wachanga ukiwashauri kuhusu jinsi ya kumtunza mtoto wao.

  • Sasa linganisha orodha yako na habari iliyo kwenye sehemu ya 2.2.1, 2.2.2 na 2.2.3Mwisho wa jibu.

2.3 Kwa kutamatisha

Kwa wanawake wengi, puperiamu hupita bila matatizo na huwa wakati wa furaha kwa mama na jamaa zake wengine kuwa na mtoto mgeni. Hata hivyo, ni muhimu kwa kina mama na wenzi wao kuelezwa yale ambayo hutendeka katika kipindi hiki na uhakikishe kuwa hakuna dalili za hatari zinazoweza kudhuru afya ya mama au ya mtoto mchanga. Tutajadili puperiamu isiyo ya kawaida katika Kipindi cha 3 cha somo cha moduli hii. Kumbuka kuwa unapaswa kumpa mama na mtoto wake rufaa katika kituo cha afya cha juu mara tu unapogundua matatizo wakati wa safari zako za kufuatilia ili wafanyiwe uchunguzi zaidi na kutibiwa.

Muhtasari wa Kipindi cha 2

Katika Kipindi hiki cha somo umejifunza kuwa:

  1. Kipindi cha wiki sita baada ya kuzaa huitwa puperiamu. Huu ni wakati ambapo mabadiliko ya kifiziolojia yaliyotendeka kwa mwili wa mama wakati wa ujauzito hurudi katika hali ya kawaida. Uterasi, seviksi, uke na vulva hupungua kwa ukubwa na viowevu zaidi vilivyobakizwa wakati wa ujauzito huondolewa haraka kupitia katika mkojo wa mama.
  2. Kina mama baaada ya kuzaa wana mchozo wa kawaida ambao ni mwekundu na majimaji uitwao lokia ambao hupungua pole pole wakati wa puperiamu na kubadilika rangi kuwa manjano hafifu.
  3. Mabadiliko kwa matiti ambayo huyatayarisha kwa unyonyeshaji hutokea katika muda wote wa ujauzito. Utengenezaji wa kolostramu huanza mara tu baada ya kuzaa na hufuatwa siku 3 baadaye na kutuna kwa matiti na utengenezaji wa maziwa halisi.
  4. Kolostramu inayotolewa kwa matiti katika siku mbili hadi tatu za kwanza baada ya kuzaa ina virutubishi na antibodi za mama. Ni lazima mtoto mchanga alishwe kolostramu hii.
  5. Unyonyeshaji unafaa kuanza katika saa ya kwanza baada ya kuzaa na kuendelea bila kumpa mtoto chakula kikingine chochote na kumnyonyesha kila anapotaka kwa miezi sita ya kwanza.
  6. Kina mama (na mara nyingine kina baba) huhitaji kusaidiwa ili kujizoesha na mahitaji ya kumtunza mtoto mchanga ukiwemo usaidizi wa kuanza kunyonyesha na kudumisha joto na usafi wa mtoto. Kina mama huhitaji muda wa kupumzika na kupata nafuu kabla ya kurejelea shughuli zao za kawaida.
  7. Mbinu tofauti zinazoweza kutumika katika upangaji wa uzazi baada ya kuzaa sharti zijadiliwe na wazazi wote wawili.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 2 Kwa kuwa umetamatisha Kipindi hiki, jibu maswali haya ili kujitathmini ulivyosoma.

Swali la kujitathmini 2.1 (linatathmini Lengo la Somo la 2.1)

Je, ni ipi kati ya kauli hizi isiyo sahihi? Kwa kila kauli, (i) eleza kisicho sahihi na (ii) fafanua neno lililoandikwa kwa herufi nzito.

  • A.Mwanamke wakati wa puperiamu hatatoa lokia kikawaida baada ya kuzaa.
  • B.Mwanzo wa utengenezaji wa maziwa na kolostramu hufuata mara tu baada ya kuzaa mtoto.
  • C.Utunaji wa matiti ni ishara kwamba unyonyeshaji unaweza kuanza.
  • D.Endometriamu inaweza kuchukua wiki 7 ili kupona baada ya kuzaa.
Answer
  • A.Si sahihi: wanawake wote baada ya kuzaa watakuwa na mchozo ulio majimaji na wenye rangi (lokia) kwa muda wa takribani majuma matano baada ya kuzaa. Huu ni takribani muda sawa na ule wa puperiamu ambao ni kipindi cha mabadiliko ya kifiziolojia yanayotokea katika majuma matatu hadi sita baada ya kuzaa.
  • B.Sahihi: kuanza kwa utengenezaji wa maziwa – yaani, utengenezaji wa kolostramu (‘maziwa ya kwanza’ ambayo ni malai na ya manjano na huwa na virutubishi na antibodi za mama) hufuata wenyewe mara tu baada ya kuzaa na kisha maziwa halisi kuanza baada ya takribani siku tatu.
  • C.Si sahihi kabisa: utunaji wa matiti ni mwitiko wa mwanzo wa utoaji wa maziwa na kwa kawaida hutendeka takribani siku tatu baada ya kuzaa. Kina mama wanahimizwa kuanza kunyonyesha katika saa moja ya kwanza baada ya kuzaa.
  • D.Si sahihi: endometriamu (ambayo ni bitana ya ndani ya uterasi) hupona haraka na ifikiapo siku ya saba huwa imerudi katika hali yake ya kawaida isipokuwa sehemu ya kondo.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 2.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 2.2 na 2.3)

Unamhudumia mwanamke aliyezaa mtoto wake wa pili siku 14 zilizopita. Mwanamke huyu anaonekana kuwa mwenye afya lakini mwenye wasiwasi kidogo. Eleza kwa ufupi vipimo vyote utakavyofanya kuhakikisha kuwa kila kitu kiko sawa na anapata nafuu kikawaida.

Answer

Kuna vipimo vingi unavyoweza kufanya - hivi ni baadhi ya vile vikuu.

  • Kwa kutomasa chini ya kitovu cha mwanamke unaweza kubainisha ikiwa uterasi imerudi katika hali yake ya kawaida.
  • Muulize ikiwa ana mchozo mwingi utokao ukeni na ni wa rangi gani.
  • Kwa kufanya uchunguzi ukeni, baini kuwa upana wa mwanya wa sevikisi umepungua hadi chini ya upana wa kidole kimoja.
  • Chunguza ikiwa uvimbe wa uke na vulva unapungua au u karibu kuisha.
  • Ikiwa msamba ulikatwa au uliraruka wakati wa kuzaaa, hakikisha unapona sawasawa, na ikiwa ni hivyo, mhimize mama kuanza kufanya mazoezi ya misuli yake ya msamba.
  • Chunguza ikiwa anayo matatizo katika kunyonyesha au (iwapo ameamua kutonyonyesha) anafanikiwa katika kupunguza utengenezaji wa maziwa.
  • Chunguza kuwa mtoto si baridi wala mwenye joto sana, anakula vizuri na anakunya mara kwa mara.
  • Uliza kwa hekima ikiwa mama huyo anahisi kushurutishwa na mwenzi wake kurejelea ngono kabla hajahisi kuwa tayari kufanya hivyo.
  • Jaribu kutathmini ikiwa amerejelea kazi nyingi mapema isivyotarajiwa.
  • Kwa kuukagua mwili wake, utatambua dalili kuu zitakazokufahamisha ikiwa puperiamu inaendelea kikawaida, na ikiwa ni hivyo, unaweza kumwondolea shaka mama huyo mwenye wasi wasi. Yale atakayoweza kusema kama majibu ya maswali ya kibinafsi yatakuwa magumu sana kutathmini. Utahitaji kutumia hisia zako na hekima ili kubainisha ikiwa kuna kitu kingine kinachoenda mrama.

Mwisho wa jibu.