Skip to main content
Printable page generated Friday, 26 April 2024, 6:55 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Friday, 26 April 2024, 6:55 AM

2. Kuendeleza Utunzaji katika Ujauzito

Kipindi cha 2 Kuendeleza Utunzaji katika Ujauito

Utangulizi

Katika somo hili utajifunza tofauti kati ya kuendeleza afya, elimu ya kiafya,uchunguzi wa kiafya na kuzuia magonjwa. Pia utajifunza njia tofauti za kuwasilisha jumbe za elimu ya kiafya kwa heshima na huruma.

Pia utajifunza jinsi ya kuelimisha na kushirikisha watu binafsi, vikundi, viongozi mashuhuri na wanajamii katika uendelezaji na utumiaji bora wa huduma za utunzaji katika ujauzito. Kanuni zizi hizi zinaweza pia kutumika katika kuendeleza utumiaji wahuduma za afya wakati wa uchungu wa kuzaa, katika kuzaa na baada ya kuzaa - utakavyoona katika moduli mbili zifuatazo. Hatimayetutakuonyesha hatua katika kupanga shughuli za elimu ya kiafya zinazolenga kupunguza vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto wazawa kwa kuongeza kiwango cha utunzaji katika ujauzito. Unaweza kutumia hatua zizi hizi kwa shughuli za kuendeleza afya ukiwa na malengo mengine, kwa mfano, ya kuongeza kiwango cha utumiaji wa huduma za kupanga uzazi.

Malengo ya Somo laKipindi cha 2

Baada ya kujifunza somo hili unapaswa uweze:

2.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito (Maswali ya kujitathmini2.1)

2.2 Kujadili manufaa ya kuendeleza huduma za utunzaji katika ujauzito katika jamii yako. (Maswali ya kujitathmini 2.2)

2.3 Kueleza mbinu mbalimbali tofautiza kuendeleza utunzaji katika ujauzito zikiwemo utetezi na uhamasishaji wa jamii, kampeni za kiafya, hafla za jamii, majadiliano ya vikundi au watu binafsi. (Maswali ya kujitathmini 2.3)

2.4 Kueleza hatua katika kuandaa hafla ya elimu ya kiafya ili kuendeleza matumizi ya huduma za utunzaji katika ujauzito katika eneo lako. (Maswali ya kujitathmini 2.4)

2.1 Uendelezaji wa afya

Uendelezaji wa afya ni shughuli zozote zinazosababisha afya bora katika jamii au nchi. Huhusisha jinsi ya kuwawezesha watu kuongeza udhibiti na uboreshaji wa afya yao. Lakini huenda zaidi ya kuzingatia mienendo ya mtu binafsi kuelekea utatuzi anuwai wa kijamii na kimazingira ambao huboresha afya. Uendelezaji wa afya huhusisha vitendo vyovyote vya watu binafsi, mashirika ya kijamii, ofisi za afya katika wilaya na maeneo, na serikali yanayolenga kuboresha afya ya watu wao. Kwa mfano, ujenzi wa hospitali zaidi na vituo vya afya, kufunza wahudumu wa afya zaidi ni shughuli za kuendeleza afya kitaifa. Vile vile ilivyokuhakikisha kuwa kila mmoja katika nchi anapata chakula cha kutosha, nyumba na maji safi.

Uendelezaji wa afya katika jamii huhusisha shughuli za aina tatu(jedwali 2.1). Tutaanza kwa kuangazia mifano ya kila moja ya aina hizi kwa zamu.

Jedwali 2.1 kuendeleza afya katika jamii kunahusisha elimu ya kiafya, uchunguzi wa kiafya na shughuli za kuzuia magonjwa.

Elimu ya kiafya ni uwasilishaji wa habari sahihi na muhimu za afya kwa wanajamii. Huwawezesha watu binafsi na vikundi kukuza maarifa yao ya masuala ya afya, kuongeza kujitegemea na uwezo wao wa kusuluhisha matizo yao ya kiafya kupitia ari yao yenyewe. Kibainishi kikuu cha afya bora au duni ni elimu ambayo watu wanayo kuhusu masuala ya afya, imani zao, mitazamo, mienendo yao na nia ya kusababisha mabadiliko ya kimienendo katika maisha yao.

Jukumu muhimu kwako kama muhudumu wa afya ni kutoa elimu mwafaka ya kiafya kwa watu katika jamii yako ili waweze kujadiliana nawe na miongoni mwao matatizo yao ya kiafya kisha wafanye uamuzi ufaao ili kuboresha afya yao na ya jamaa zao kwa juhudi zao wenyewe. Kwa hivyo elimu ya kiafya ni zana muhimu kwa kuwaleta watu katika utendaji. Ikiwa elimu ya kiafya itawasilishwa katika mpango uliopangwa na kuratibiwa vizuri na kuungwa mkono na kushiriki kwa jamii hakutakuwa na njia bora ya kuhimiza mienendo bora ya kiafya na kutatua au kuzuia matatizo mengi ya afya yanayotokea mara kwa mara.

  • Je, mienendo ni nini na hutokea wapi?

  • Mienendo ni kile watu wanatenda au kuzoea katika maisha yao ya kila siku. Chanzo chake ni maisha yetu ya kila siku, mazingira yetu na matukio tuliyolimbikiza na kufahamishwa na imani, tamaduni, mila na tabia zetu.

    Mwisho wa jibu

Mienendo ifaayo ya kiafya ni tendo lolote la mtu binafsi linaloboresha afya yake au afya ya wengine katika jamii.

  • Je, unaweza kupendekeza baadhi ya mifano ya mienendo ifaayo ya kiafya?

  • Unaweza kuwa umefikiria mifano kama vile kula lishe bora, kufanya mazoezi ya kutosha, kulala usingizi wa kutosha usiku na kujiepusha na mienendo inayoharibu afya kama vile kuvuta tumbaku, kunywa pombe kwa wingi au kushiriki ngono bila kondomu.

    Mwisho wa jibu

Sanduku la pili katika jedwali 2.1 linaonyesha uchunguzi wa kiafya ambao ni utaratibu wa kupimwa kwa watu binafsi ili kujua ikiwa wako katika hatari ya kukumbwa na tatizo la kiafya. Uchunguzi wa kiafya ni shughuli muhimu ya kuendeleza afya utakayofanya kama mojawapo ya huduma za utunzaji katika ujauzito. Kwa mfano, utapima halijoto, shinikizo la damu na mdundo wa moyo wa kila mwanamke mjamzito kila anapotembelea huduma hizi (tutakuonyesha jinsi ya kufanya haya katika Kipindi cha 9 cha somo) ili kujua ikiwa ana tatizo la kiafya linaloweza kumdhuru yeye au mtoto wake.

Sanduku la mwisho katika jedwali 2.1 linaonyesha uzuiaji wa magonjwa. Hii hurejelea tendo lolote linalofanywa kwa minajili ya kuzuia kukua kwa ugonjwa. kwa mfano, kumpa mwanamke mjamzito madini ya ziada kama mojawapo ya utaratibu wa utunzaji katika ujauzito ni tendo la kuzuia ukuaji wa anemia. Anemia ni hali inayoufanya mwili kutengeneza seli nyekundu za damu chache mno kwa sababu lishe ya mwanamke huyo haina madini ya kutosha. (Utajifunza jinsi ya kugundua na kutibu anemia katika vikao vya 9 na 18 vya somo katika moduli hii.)

Unaweza kuona katika majadiliano hapo juu ya kwamba kuendeleza afya huhusisha shughuli anuwai. Katika masomo yatakayofuata katika moduli hii, utajifunza mengi kuhusu elimu maluum ya kiafya, uchunguzi wa kiafya na shughuli za kuzuia magonjwa ambazo huchangia katika utunzaji katika ujauzito kwa wanawake wajawazito katika jamii yako. Katika Kipindi hiki cha somo tutaangazia kanuni za jumla za elimu ya kiafya kama kipengele muhimu cha kuendeleza afya katika utunzaji katika ujauzito.

2.2 Kuelimisha jamii yako kuhusu utunzaji katika ujauzito

Elimu ya kiafya huwawezesha watu kuelewa na kuchambua matatizo yao ya kiafya, kuwatia motisha na kuwaelekeza katika mkondo ufaao ili kutekeleza mabadiliko yanayotakiwa. Katika muktadha wa utunzaji katika ujauzito, elimu hii husaidia kuelimisha, kutia motisha na kuwahimiza wanawake wajawazito kutumia huduma hiyo kwa kutoa taarifa ambayo huwasaidia kufanya uamuzi mwafaka. Zaidi ya hayo, hupigania kukubalika pakubwa kwa huduma hizi na matumizi yake kwa kuielimisha jamii nzima. Matokeo ni kwamba kila mmoja anaelewa kuwa faida ya utunzaji katika ujauzito kwa jumla ni kuendeleza afya ya mama na mtoto mzawa na kuzuia magonjwa ya mara kwa mara na matatizo wakati wa ujauzito, uchungu wa kuzaa, kuzaa na kipindi baada ya kuzaa. Utunzaji katika ujauzito husaidia kugundua matatizo mapema na kisha udhibiti wa haraka ikiwa ni pamoja na rufaa katika hospitali yenye vifaa maalum ikibidi. Huwahimiza watu kufanya maandalizi ya uwezekano wa tukio la dharura wakati wa ujauzito na kuzaa na husababisha upungufu thabiti wa matatizo na vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto wazawa.

Jukumu lako ni kuhakikisha ufahamu wa jamii kuhusu huduma unayotoa ya utunzaji katika ujauzito kwa wanawake wajawazito, na kuwajulisha wanawake, jamaa zao na wanajamii kuhusu dalili za hatari na pa kutafuta huduma ya dharura. (Utajifunza kuhusu dalili za hatari katika vikao vya baadaye vya somo). Unafaa kuhakikisha kuwa kila mmoja katika jamii anafahamu kuhusu umuhimu wa kupanga mapema usafiri wa dharura kukitokea haja.

Bila shaka utaokoa maisha, ingawa afya ya wale walio karibu nawe kwa jumla haimo mikononi mwako wewe pekee. Hii ni kwa sababu watu huamua wenyewe jinsi ya kutumia ushauri wako na huchagua wenyewe watakalofanya kuhusu afya yao na ya jamaa zao. Kwa kufundisha na kujadiliana, unaweza kuwasaidia watu kufanya uamuzi wao wenyewe kwa busara. Kazi yako ya kwanza ni kuielimisha jamii yako na kuendeleza mienendo ifaayo ya kiafya.

Safari ya utunzaji katika ujauzito ni nafasi nzuri ya kuendeleza mazungumzo na wateja wako, na kuimarisha ujumbe wa afya unaofaa. Kwa hivyo, unahitaji kuwahimiza wanawake kuenda safari yao ya kwanza ya utunzaji katika ujauzito mapema wakiwa wajawazito. Utajifunza kuhusu mbinu bora za kutimiza lengo hili katika sehemu itakayofuata ya Kipindi hiki cha somo.

2.3 Mbinu za kuwasilisha jumbe za afya

2.3.1  Mbinu ya kutoa na kupokea habari

Ili kuendeleza matumizi bora ya huduma za utunzaji katika ujauzito, mawasiliano yafaayo hutekeleza wajibu muhimu. Mbinu za mawasiliano ni njia zote ambazo watu hutumia kwa kubadilishana mawazo, hisia na habari kupitia mazungumzo, chapa kama vile vitabu na kurasa zenye matangazo, mabango, redio, runinga na kwa kiwango kikubwa kupitia mtandao kukiweko vifaa. Elimu ifaayo ya kiafya huhusisha mazungumzo ya kutoa na kupokea habari.

  • Je, mawasiliano ya kutoa na kupokea habari ni nini?

  • Hutendeka wakati habari inabadilishwa kati ya angalau watu wawili kupitia kushiriki na majadiliano.

    Mwisho wa jibu

Mawasiliano ya kutoa na kupokea habari ni njia bora ya kuendeleza jumbe za elimu ya kiafya kwa watu binafsi au vikundi. Sharti kuwe na mtiririko huru wa mawasiliano kati ya wahusika wote. Kumbuka kwamba masikio yako ni baadhi ya zana zako muhimu. Hii ni muhimu hasa katika elimu ya afya kwa sababu inakuwezesha kupata majibu muhimu ya utekelezaji wa maazimio kutoka kwa kila mtu, kuelewa matatizo yao na kuyatatua kupitia majadiliano.

  • Je, ni wapi na lini elimu juu ya afya ya wanawake wajawazito hutolewa?

  • Inaweza kutolewa pahali popote na wakati wowote. Kwa mfano, wakati wa kupimwa katika utunzaji katika ujauzito, ukiwa unauliza maswali na kusikiliza majibu ya mwanamke, unaweza kujadili masuala ambayo ni muhimu kwake. Sokoni, katika mkutano wa jamii (Picha 2.2) au kila unapokutana na wanawake wajawazito au waume zao.

    Mwisho wa jibu

Picha 2.2 Mikusanyiko mbalimbali ya jamii ni nyakati nzuri za kupitisha jumbe za kiafya.

Wahusishe wanaume na wanawake katika kujadili faida za utunzaji katika ujauzito.

2.3.2 Chagua mbinu za mawasiliano zitakazoifaa hadhira yako

Kuendeleza afya si shughuli ya mara moja bali huendelea kulingana na shughuli zilizopangwa vizuri. Huwalenga wanajamii tofauti na hutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano ipasavyo. Uendelezaji wa afya huhusisha kushiriki kikamilifu kwa jamii nzima kwa msingi wa ukweli wa tamaduni, mila, lugha na rasilimali za eneo hilo. Watu hujifunza kwa njia tofauti, na kila mmoja hujifunza vyema akijifunza kitu hicho kwa njia tofauti. Baada ya kuzungumza na watu binafsi au vikundi kuhusu faida za utunzaji katika ujauzito, watashiriki waliyoyapitia na watu wengine katika jamii, kwa hivyo watakuwa mawakala wa mabadiliko mema.

2.3.3 Utetezi na uhamasishaji wa jamii

Utetezi ni kutetea au kutenda kwa niaba yako mwenyewe au mtu mwingine. Uhamasishaji wa jamii unarejelea mfumo mpana wa muungano wa kuwahusisha watu kushiriki katika kutimiza lengo maalum kupitia bidii za kibinafsi. Utetezi na uhamasishaji wa jamii utakusaidia kupata na kuendeleza ushirikishaji wa watu wenye ushawishi mkubwa, vikundi na sekta katika nyanja tofauti katika jamii watakaounga mkono mipango ya utunzaji katika ujauzito.

Mikakati hii imeangaziwa kwa kina katika moduli juu ya Elimu ya Afya, Utetezi na Uhamasishaji wa jamii.

Ukifanikiwa katika kuwafundisha watetezi kuongea kwa uwazi kuhusu utunzaji katika ujauzito na uhamasishaji wa uungwaji mkono pakubwa wa huduma hii, matokeo yanaweza kuwa;

  • Kuboresha uwezekano wa wanawake wajawazito kufikia huduma zifaazo katika ujauzito na kukubalika kwa huduma hizi katika jamii
  • Kuandaa mabaraza ya kujadili na kuratibu huduma zifaazo katika ujauzito
  • Uhamasishaji juu ya rasilimali za jamii kama vile usafirishaji, utoaji wa habari na fedha za dharura kwa wanawake wajawazito na wanaopata matatizo katika uchungu wa kuzaa yanayohitaji huduma ya kiafya kwa dharura.
Viongozi mashuhuri kama watetezi wa utunzaji katika ujauzito.

Kuhusisha usaidizi wa watetezi ambao ni viongozi mashuhuri au watu muhimu katika eneo lako ni jukumu muhimu. Wazee wanaojulikana na wenye kuheshima, viongozi wa kitamaduni au wa dini na watu wenye hekima ambao ushauri na maneno yao yana kibali katika jamii na wanaweza kuwashawishi wengine kuhusu faida za utunzaji katika ujauzito kwa kushinikiza jamii. Mazoea ya wanajamii kukubaliana nao ni muhimu kwa kuwasilisha jumbe za kiafya na kupata kibali kutoka kwa wengine.

Unaweza kutumia viongozi hawa walio heshimika kuwasilisha jumbe zifaazo kuhusu utunzaji katika ujauzito ikiwa utawapa habari ifaayo na uko tayari kuwatumia kama watetezi. Utetezi kutoka kwa viongozi walio heshimiwa unaweza kukuhakikishia kuwa watu wanazingatia na kuendeleza mienendo ifaayo uliyoleta kupitia elimu ya kiafya.

Jaribu kupata idadi ya juu zaidi ya watu wanaohusika katika uenezaji wa huduma za utunzaji katika ujauzito ili jamii iweze kuimarisha uungaji mkono wa afya ya wanawake wajawazito (Picha 2.3)

Picha 2.3 Uhamasishaji wa jamii kuunga mkono utunzaji katika ujauzito huhusisha jamii nzima, kwa sababu afya ya mwanamke mjamzito inaweza kukingwa au dhuriwa na yeyote.
Wanaume kama watetezi wa utunzajii ufaao katika ujauzito
  • Je, wanaume wana wajibu katika utunzaji katika ujauzito?

  • Ndio! Kuhusika kwao ni muhimu kwa sababu wanaume wanaweza kushawishi ikiwa wanawake wajawazito katika familia zao wanatembelea huduma za utunzaji katika ujauzito ili kupimwa mara kwa mara na kufuata ushauri wako.

    Mwisho wa jibu

Wahimize wanaume iwezekanavyo kushiriki katika kuboresha afya ya wanawake. Waume, kina baba, watoto wa kiume, viongozi wa jamii, viongozi wa kidini, mabosi na wanaume wengine wote huchangia jinsi afya ya wanawake itakavyokuwa kwa mujibu wa ujauzito, uchungu wakati wa kuzaa na katika kuzaa. Jamii nzima itafaidika ikiwa wanaume katika jamii watahisi kuwajibikia afya ya wanawake. Kwa hivyo wasaidie wanaume kuhusishwa katika kuendeleza utunzaji katika ujauzito.

Endeleza majukumu na ujuzi ambao wanaume tayari wanao. kwa mfano, katika jamii nyingi, wanaume hutazamiwa kama walinzi. Wasaidie wanaume wajifunze jinsi ya kulinda afya ya wanawake. Wahimize wanaume kushiriki katika majukumu ya ujauzito na malezi. Wanaume wanaweza kuwatunza watoto sawa na wanawake kwa kuliwaza, kuogesha, kuwapa chakula, kuwafunza na kucheza nao. Waalike wanawake na wanaume katika mikutano ya kijamii na uwahimize wanawake waongee. Wakati mwingine wanawake husita kuongea kuhusu ujauzito na mambo ya kuzaa mbele ya wanaume.

Shirikiana na wanaume walio na huruma kwa mahitaji ya wanawake. Wanaume hawa wanaweza kusemezana na wanaume wengine ambao huenda wamsikize mwanamume kwa makini kuliko mwanamke. Mnapojadiliana nao kuhusu utunzaji katika ujauzito, jaribu kuwapa mapendekezo tendaji. Wanaume wanaojali sana afya ya wanawake walio katika maisha yao waweza kuwa hawajui pa kuanzia. Kwa mfano;

  • Mwelezee mwanamume kuwa mkewe aliye mjamzito anahitaji kusaidiwa katika kazi zake za kila siku (tazama Picha 2.4)
Picha 2.4 Wanawake wanahitaji usaidizi wa ziada katika kazi zao wakati wa ujauzito.
  • Wahimize wanandoa kupanga kwa pamoja mipango ya kuzaa na wawe na ufahamu wa dalili za hatari katika ujauzito, wakati wa kuzaa na baada ya kuzaa. Washauri waweke akiba ya pesa fulani ikiwa watapatwa na tukio la dharura na kupangia usafiri ikiwa mwanamke atahitajika kuenda kwenye kituo cha afya au hospitali.
  • Hakikisha kuwa mume anaelewa kuwa ni lazima akuite mkewe akipata uchungu (ikiwa ujauzito wake umekuwa wa kawaida na hana dalili zozote za hatari) ili uweze kuwa hapo anapozaa.
  • Hakikisha kuwa anajua mahali pa kumpeleka mkewe katika kituo cha afya kwa utunzaji wa dharura ikiwa matatizo yatatokea.
  • Muonyeshe jinsi mume anavyomsaidia mkewe wakati wa uchungu wa kuzaa. Kwa mfano wapi na jinsi ya kumsugua mgongo ili kutuliza maumivu yake.
  • Waambie wanaume jinsi wanavyoweza kupimwa na kutibiwa maambukizi ya zinaa kwa sababu ikiwa ni mwanamke tu atakayetibiwa, ataweza kuambukizwa tena na mwenzi wake kwa haraka.

2.3.4 Kuandaa kampeni ya afya

Kampeni za kiafya hudumisha maarifa, ujuzi, mitazamo na maadili juu ya suala maalumu la kiafya. Pia zinaweza kutumika katika kutimiza mradi maalumu wa maendeleo ya jamii. Shughuli halisi za kampeni ya kijamii mara nyingi hufanyika kwa muda wa juma au mwezi mmoja. Kwa sababu hii, kampeni hizi mara nyingi huitwa‘Majuma ya Afya’.

Kampeni ya kiafya kwa kuendeleza matumizi ya huduma za utunzaji katika ujauzito inaweza kuandaliwa kutokana na suala au tatizo moja lililotambuliwa na wanajamii wenyewe. Kwa mfano, kueneza habari kuhusu manufaa ya huduma hizi kwa wanawake wajawazito kunaweza kuwa kampeni iliyopewa kipaumbele katika jamii ambapo kiwango cha matumizi ya huduma hizi kilikuwa chini. Ikiwa kuna kamati ya afya katika jamii hii, inafaa kushughulika katika kutambua masuala yanayopaswa kuandaliwa kampeni za kiafya na kupanga hatua inayofaa kuchukuliwa.

Picha 2.5 Nembo ya kampeni ya ‘Mwezi wa Umama Salama’ nchi mojawapo barani Afrika mwezi Januari mwaka wa 2010.

Kampeni za kiafya zinaweza pia kuendeshwa kitaifa. Kwa mfano, nchi mojawapo barani afarika kampeni iitwayo ‘Mwezi wa Umama Salama’ iliendeshwa mwezi Januari mwaka wa 2010. Lengo la kampeni hiyo lilikuwa ‘Hakuna mama anayepaswa kufariki wakati wa kuzaa’ (Picha 2.5).

Tatizo lililotambuliwa lilikuwa kiwango cha juu cha vifo vya kina mama na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kuzaa. Wakati huo huo, kulikuwa na kiwango cha chini cha matumizi ya huduma za afya kwa kina mama kama vile utunzaji katika ujauzito, wanawake kuzaa kwa kuhudumiwa na mtaalamu wa uzazi, na upangaji uzazi. Katika mwezi huo wote, kampeni za utetezi na uhamasishaji wa umma ziliendeshwa kwa kutumia mbinu tofauti za mawasiliano zikiwemo posta, runinga na redio. Kulikuwa na majadiliano ya jopo na washika dau, viongozi wa kidini, wabunge na wengineo kuhusu uzito wa tatizo la afya ya kina mama na kushirikiana katika utekelezaji mwafaka wa utoaji wa huduma hizi. Kampeni juu ya kupanga uzazi na kupewa mawaidha kuhusu Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kupimwa pia iliendeshwa katika mwezi huo.

2.3.5 Hafla spesheli za jamii

Kila jamii ina tamasha, maadhimisho na sherehe zake. Kwa mfano kuadhimisha majira spesheli ya mwaka kama vile wakati wa kupanda, kuvuna na Mwaka Mpya. Kuna tamasha na siku nyingi za kidini na siku za kukumbuka matukio ya kitaifa na mashujaa. Hafla zingine huwa za kujifurahisha na kutulia kama vile sherehe ya kahawa. Zingine huhitaji kufikiria sana na kutafakari kwa utulivu. Watu husherehekea kwa njia tofauti kulingana na tamaduni na kanuni za jamii hiyo. Jamii nzima hushiriki katika sherehe hizi bila kujali azma ya sherehe hizo. Hafla hizi zote zinaweza kuwa matukio mazuri kuwasilisha habari juu ya utunzaji katika ujauzito na kuendesha shuguli zinazoendeleza afya ya kina mama na watoto wazawa.

2.3.6 Vikundi vya majadiliano

Kikundi cha majadiliano ndiyo mbinu inayotumika sana katika kueneza elimu ya kiafya. Inahusisha mtiririko huru wa mawasiliano kati ya mwelekezi na washiriki wawili au zaidi (Picha 2.6).

Picha 2.6 Vikundi vya majadiliano hutoa fursa ya watu kubadilishana waliyoyapitia.

Manufaa ya vikundi vya majadiliano kama mbinu ya kuendeleza afya ni kuwa;

  • Huhimiza ushiriki sawa wa wanakikundi wote
  • Huongeza motisha ya kutekeleza ujumbe wa elimu ya kiafya
  • Husaidia wahusika kuelewa maarifa, mawazo mapya na ujuzi
  • Hutoa fursa saidizi ya kujifunza na kubadilishana matukio
  • Huendeleza kufikiria kwa pamoja ili kutambua na kutatua matatizo kwa kuleta pamoja maoni na ujuzi.

Vikundi vya majadiliano husaidia sana kama mbinu ya kueneza elimu ya afya ikiwa vina lengo sawa, mpango wa pamoja na utekelezaji wa hatua zitakazojitokeza. Jedwali 2.1 linakupa njia zifaazo za kuelekeza majadiliano ya kikundi.

Jedwali 2.1 Hatua za vikundi vya majadiliano bora
  1. Matokeo bora hutimizwa ikiwa kikundi ni kidogo. Ikiwa kikundi ni kikubwa sana, kiwango cha kushiriki kwa kila mtu kitakuwa chini. Ratibu kikundi ili kuwezesha kushiriki kamili kwa wanakikundi wote.
  2. Anza mawasilisho yako na mwazo dhahiri, utangulizi, malengo ya jumla na yale maalumu, na masuala fulani muhimu ya kujadiliwa ili kuendesha mazungumzo.
  3. Hakikisha kuwa majadiliano yana maana. Yaani, masuala yanayojadiliwa ni husika na dhahiri, watu hawakatizani katika maongezi na wanajadili tu mada waliyoafikiana.
  4. Ufaafu wa vikundi vya majadiliano unaweza kuimarishwa au kudhoofishwa na tofauti zilizoko katika usuli wa washiriki, kwa mfano katika tamadumi zao, mahali wanakoishi, hadhi ya kijamii na ya kiuchumi katika jamii, jinsia na rika. Tofauti hizi zinaweza kuwa na athari zinazofaa au zisizofaa kwa matokeo ya majadiliano. Na kwa hivyo unapaswa kufahamu haya.
  5. Wajibu wako kama mwelekezi ni kuwatia motisha na kuwahimiza washiriki kubadilishana mawazo kwa njia huru na kuafikiana.
  6. Hitimisha majadiliano kwa kufanya muhtasari wa matokeo, kukubaliana juu ya hatua zitakazofuata na kushukuru kila mmoja kwa kushiriki.

2.3.7 Elimu ya kibinafsi ya afya

Elimu ya kibinafsi ya afya hutokea unapobadilishana mawazo na habari na mtu mwingine. Ni yenye nguvu sana kuliko mbinu nyingine yoyote ya mawasiliano. Itakusaidia kuleta uelewano baina yako na huyo mwingine na muweze kujuana vyema. Huendeleza uwazi baina ya washiriki na kuwawezesha kupokezana mawazo na kupata majibu mara moja. Pia hutoa fursa ya kujadili matatizo nyeti na yanayohitaji kushugulikiwa kimaalumu, jinsi ilivyo mara nyingi katika ujauzito. Katika mawasiliano ya kibinafsi, ni muhimu kuanza kwa kujenga uhusiano bora. Jedwali 2.2 linakupa njia za kukusaidia kufanya haya.

Jedwali 2.2 Hatua za mawasiliano yafaayo ya kibinafsi
  1. Msalimie huyo mwingine kwa ukunjufu na kwa njia ya kirafiki.
  2. Kisha tengeneza mazingira mazuri ya kusoma kwa kumfanya astarehe na kutulia.
  3. Ujumbe wako unafaa kuwa wazi, rahisi na wa kueleweka ili kuepuka utata wowote.
  4. Tumia vielelezo mwafaka ikiwa vitakusaidia.
  5. Himiza kushiriki kwake kwa kumsihi awasilishe maoni yake juu ya mada hiyo, atoe masuala na kuuliza maswali.
  6. Fanya muhtasari wa ujumbe mwishoni mwa hipindi, kisha umkaribishe huyo mwingine ili aseme ikiwa ana maoni yoyote zaidi au maswali.

2.4 Kupanga hafla ya elimu ya afya

2.4.1 Maandalizi ni muhimu

Picha 2.7 Vitabu na utafiti hukusaidia kujiandaa kwa ajili ya hafla ya elimu ya kiafya.

Ikiwa unapanga hafla ya elimu ya kiafya ili kuendeleza matumizi ya huduma za utunzaji katika ujauzito au mada nyingine yoyote ya elimu ya kiafya, maandalizi kamilifu ni muhimu. Anza kwa kujiandaa vizuri mapema kwa kila kitu utakachohitaji kujua juu ya mada hiyo, kutafiti hoja kuu na kukusanya taarifa zote muhimu (Picha 2.7).

Tafakari kwa makini juu ya hadhira na ubaini wanachohitaji. Kwa mfano, ikiwa hadhira yako ni viongozi wa jamii, unahitaji kutayarisha ujumbe wako kulingana na maarifa na jukumu lao. Hafla hiyo kwa ajili ya wazee itahitaji jumbe tofauti na hafla ya wazazi wapya au mzazi mmoja wa kike na kadhalika. Zingatia mahitaji, hisia na matakwa ya hadhira maalum kisha ubaini ni hoja zipi huenda watataka uzingatie.

Chagua mahali na wakati mwafaka kwa watu kuweza kupatikana kwa wingi iwezekanavyo. Kwa mfano, ikiwa watu wengi wanapendelea kuhudhuria hafla hiyo Jumamosi saa tatu asubuhi katika ukumbi wa kebele, jaribu iwezekanavyo kukubaliana na chaguo lao.

2.4.2 Kuanza

Unapoendesha hafla au mkutano wa elimu ya kiafya, hakikisha kwamba kila mtu ameketi vizuri na yuko tayari kwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano. Tabasamu, na ujaribu kuangaliana ana kwa ana na kila mtu huku ukiwakaribisha kisha ujitambulishe. Sihi kila mmoja wao ajitambulishe.

Anza kwa kuzungumzia wanayo ya jua kuhusu huduma ya utunzaji katika ujauzito, kisha uongezee wasiyoyajua. Unaweza paswa kuwaambia kuhusu manufaa yake, mara ngapi na wakati upi mwanamke anapaswa kupimwa katika ujauzito na kadhalika.

Chagua mbinu utakayotumia kuwasilisha ujumbe wako kulingana na hali ya hadhira, idadi, umri, jinsia na kadhalika. Kwa mfano, kundi la wanawake wajawazito linaweza kufurahia ukilionyesha picha za uterasi iliyo na mtoto anayekua mle ndani au ukiwaonyesha jinsi mtoto anavyosonga chini kwenye njia ya uzazi, kwa kutumia mwanasesere. Viongozi wa jamii wanaweza kunufaika wakiona data juu ya vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa pamoja na vile vya watoto wazawa (jinsi ilivyo katika Kipindi cha 1 cha somo katika moduli hii), ili kuwashawishi kuhusu umuhimu wa utunzaji katika ujauzito.

2.4.3 Kuhusisha kila mmoja

Makinikia yale yanayoweza kufanywa na kutimizwa kwa muda uliopo wa hafla hiyo. Usijaribu kutoa habari mpya zote kwa pamoja, kwani watu wanaweza kujihisi wachovu kisha waache kusikiliza.

Kumbuka, mawasiliano ya kutoa na kupokea habari ndiyo njia bora zaidi! Washiriki wanafaa kuhimizwa kushiriki elimu na waliyoyapitia kisha watoe maoni na mapendekezo yao kwa uhuru.

Himiza kushiriki kikamilifu hasa kwa wanawake kwa sababu ndio wanaopaswa kuhimizwa kutumia huduma za utunzaji katika ujauzito. Watu wengine wana uzoefu wa kuzungumza katika vikundi wakati wengine huenda wawe wenye haya au woga. Kwa hivyo, unapaswa kuwahimiza wale wanawake ambao hunyamaza waweze kutoa mawazo yao.

Hakikisha kuwa kila mtu anapata nafasi sawa ya kushiriki. Kwa mfano, ikiwa kikundi cha wanawake fulani kinataka kujifunza kuhusu watakachokula wakati wa ujauzito na baada ya kuzaa, unaweza kuuliza kwanza kila mmoja wao aseme anachokijua. Wanawake wengi tayari wanajua kuhusu lishe bora kutoka vitabuni au madarasani, kwa kuzungumza na wanawake wengine au kutokana na waliyoyapitia. Hata hivyo wanawake wengine wanaweza kuwa wamepotoshwa kwa mfano kuhusu vyakula wanavyofikiri havifai kutumiwa katika ujauzito, angali kwa kweli vyakula hivyo ni bora kwa wanawake wajawazito ikiwa wanaweza kumudu kuvinunua (Picha 2.8).

Picha 2.8 Hafla za elimu ya kiafya zinaweza kufichua maoni mengi tofauti, kwa mfano juu ya lishe bora katika ujauzito.

2.4.4 Kuhitimisha hafla

Wakati wa kuhitimisha hafla hiyo unapowadia, fahamu ni maswali, maoni au masuala yapi aliyonayo mtu yeyote kisha uyajibu maswali hayo kikamilifu iwezekanavyo kabla ya mkutano kuisha. Kisha fanya muhtasari wa hoja zilizojadiliwa pamoja na maafikiano yoyote yale na hatimaye ufunge mkutano.

Washukuru wote kwa kushiriki na uwahimize kuwaambia wengine waliyojifunza.

Wanaweza kuwa watetezi wazuri wa utunzaji katika ujauzito.

Katika Kipindi cha somo kifuatacho, tunazingatia anatomi na fiziolojia utakazohitaji kujifunza ili uweze kutoa utunzaji bora ufaao katika ujauzito.

Muhtasari wa Kipindi cha 2 cha somo

Umejifunza katika Kipindi cha 2 cha somo kuwa:

  1. Azma kuu ya kuendeleza utumiaji wa utunzaji katika ujauzito ni kupunguza idadi ya vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa, vya watoto wazawa na matatizo.
  2. Utunzaji katika ujauzito ni fursa ya kuendeleza mazungumzo na wateja ili kuimarisha jumbe za afya ya kina mama kuhusu dalili za hatari katika ujauzito, kuzaa na muda baada ya kuzaa na kuhakikisha kila mmoja anajua ni wapi pa kutafuta utunzaji huo.
  3. Kuendeleza afya hujumlisha shughuli zozote zinazosababisha afya bora katika jamii au nchi. Pia inaweza kuhusisha vitendo vya watu binafsi, vikundi, mashirika, taasisi na serikali. Elimu ya kiafya, uchunguzi wa kiafya na uzuiaji wa magonjwa huchangia shughuli za kuendeleza afya.
  4. Elimu ya kiafya huwawezesha watu kuongezakudhibitina kuendeleza afya yao ya familia na jamii zao kwa vitendo na juhudi zao wenyewe. Huu ni mpango unaofululizwa kwa msingi wa shughuli zilizopangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia tamaduni, mila, lugha na raslimali za hadhira.
  5. Utetezi na uhamasishaji wa jamii husaidia kupata na kudumisha ushiriki wa watu binafsi wa matabaka mbalimbali, vikundi na sekta zilizo katika viwango tofauti katika jamii kwa kutimiza lengo linalokusudiwa.
  6. Kuelimisha viongozi watoa maoni wenye ushawishi, viongozi wa kidini, waume na kina baba ili wawe watetezi na wenzi katika kuendeleza afya ya wanawake wakati wa ujauzito, uchungu wa kuzaa na kuzaa. Hii ni muhimu sana.
  7. Kampeni za kuendeleza afya, hafla za mafunzo, vikundi vya majadiliano na mawasiliano na watu binafsi hufaa kuandaliwa kwa makini na kutumia njia tofauti za mawasiliano na uwasilishaji itakavyofaa.
  8. Majadiliano ya kikundi ndiyo mbinu inayotumika sana kwa kupitisha elimu ya kiafya. Huhusisha mawasiliano ya kutoa na kupokea habari ambapo washiriki hupewa nafasi sawa za kuwasilisha maoni yao na kubadilishana waliyoyapitia na mawazo yao.
  9. Msingi wa elimu ya kiafya ya kibinafsi ni kujenga uaminifu na maelewano, kuwezesha uwazi baina ya washiriki, uhuru wa kubadilishana mawazo na majibu ya mara moja kwa utekelezaji wa maazimio.
  10. Mahali pazuri pa kuanzia ni kuisikiza hadhira yako. Ukisha fahamu yale wanayoyajua unaweza kuwasaidia kujenga elimu waliyo nayo. Ukisikiliza utajifunza kutoka kwa wale unaowaelimisha.
  11. Toa nafasi zitakazoifanya huduma ya utunzaji katika ujauzito kuwa mpango wa jamii kwa kuendeleza utambuzi wa matatizo na suluhisho, upangaji na utekelezaji wa vitendo vifaavyo na kutathmini matokeo.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 2 cha somo

Kwa kuwa umekamilisha somo hili, unaweza kutathmini ni kwa kiwango kipi umetimiza malengo ya mafundisho haya kwa kujibu maswali haya. Andika majibu yako katika shajara ya masomo na uyajadili na mkufunzi wako katika mkutano ufuatao wa masoma ya kusaidiana. Unaweza kulinganisha majibu yako na muhtasari juu ya maswali ya kujitathmini mwishoni mwa moduli hii.

Maswali ya kujitathmini 2.1 (hutathmini malengo ya mafundisho 2.1)

Toa mfano mmoja wa:

  • a.Shughuli iliyoratibiwa ya uchunguzi wa kiafya inayoendeleza utunzaji katika ujauzito.
  • b.Shughuli iliyoratibiwa ya kuzuia ugonjwa inayoendeleza utunzaji katika ujauzito.
Answer
  • a.Huenda umependekeza shughuli zilizoratibiwa za uchunguzi wa kiafya kama vile kupima kiwango cha joto, mpwito wa ateri, shinikizo la damu au mkojo ili kubaini ikiwa una sukari ( Utajifunza jinsi ya kufanya haya yote katika vikao vya somo vya baadaye katika Moduli hii)
  • b.Huenda umependekeza kuwapa wanawake wajawazito tembe za elementi ya chuma ili kuzuia anemia au kuwapa neti za mbu zilizotibiwa ili kuzuia malaria. Kuna mifano minginemingi mizuri.

Mwisho wa jibu

Maswali ya kujitathmini 2.2 (hutathmini malengo ya mafundisho 1.2)

Taja faida kuu za kuendeleza utumiaji wa huduma za utunzaji katika ujauzito katika jamii yako.

Answer

Uendelezaji wa utunzaji katika ujauzito husaidia jamii kwa sababu:

  • Huhamasisha jamii nzima kuhusu huduma za afya zinazotolewa kwa wanawake katika ujauzito, wakati wa uchungu wa kuzaa, kuzaa na kipindi baada ya kuzaa.
  • Huwawezesha wanawake wajawazito na wenzi wao wa kiume kufanya uamuzi bora kuhusu utumiaji wa huduma hizi.
  • Huimarisha afya na ustawi wa wanawake wajawazito na kupunguza vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na vya watoto wazawa na matatizo.

Mwisho wa jibu

Maswali ya kujitathmini 2.3 (hutathmini malengo ya mafundisho 2.3 na 2.4)

Kisia kwamba una kikundi cha wanawake wajawazito katika eneo lako wanaotaka kujua kuhusu mahali pa kwenda kwa kuzaa. Je, ni mbinu ipi ya kuendeleza afya inayoweza kuwa bora katika mfano huu na ni hatua zipi utakazochukua kwa kuanda mpango wa elimu ya kiafya kwa wanawake hawa?

Answer

Majadiliano ya kikundi ndio mbinu bora zaidi katika mfano huu. Hatua unazopaswa kuchukua ni kama ifuatavyo:

  • Andaa maonyesho yako ili yatosheleze mahitaji ya hadhira maalumu, ambayo ni wanawake wajazito.
  • Tabasamu na ujaribu kuangaliana ana kwa ana na kila mtu. Jitambulishe na pia umsihi kila mwanamke ajitambulishe.
  • Anza na yale ambayo wanawake hawa tayari wanajua kuhusu mahali salama kwa kuzaa na uendeleze au uongezee wasiyoyajua, kwa mfano waeleze kuhusu dalili za hatari zinazoashiria kuwa wanapaswa kuzalia katika kituo cha afya.
  • Lenga kinachowezwa kufanywa na kutimizwa kwa muda uliopo.
  • Wahimize wanawake hao watoe maoni yao kwa uhuru. Wahimize wale wanawake ambao hunyamaza waweze kutoa mawazo yao. Husisha kila mmoja katika mawasiliano haya. Sikiliza kwa umaakini watakachosema.
  • Mwishoni mwa mkutano, fanya muhtasari wa hoja zilizojadiliwa pamojana maafikiano yoyote yale na hatimaye ufunge mkutano. Jaribu kuhakikisha kuwa maswali yote yaliyosalia yamejibiwa kisha umshukuru kila mmoja kwa kuhudhuria.

Mwisho wa jibu