Skip to main content
Printable page generated Thursday, 18 April 2024, 9:28 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 18 April 2024, 9:28 PM

3. Anatomia na Fiziolojia ya Mfumo wa Uzazi wa Kike

Kipindi cha 3 Anatomia na Fiziolojia ya mfumo wa Uzazi wa Kike

Utangulizi

Anatomia na fiziolojia kwa huduma ya kimsingi ya ukunga ni utangulizi katika masomo yako kwenye Moduli hii na nne zifuatazo, na pia ni maandalizi muhimu kwa mafunzo yako. Huduma ya ukunga ni utunzaji wa kiafya kwa wanawake katika ujauzito, leba, kuzaa na huduma ya baada ya kuzaa. Huduma hii huhitaji ufahamu mwafaka wa anatomia na fiziolojia ya mfumo wa uzazi wa kike. Anatomia ni taaluma ya viungo vya mwili wa binadamu, yaani, jinsi viungo, tishu na mifumo ya mwili inavyoundwa. Fiziolojia kwa upande mwingine, ni taaluma inayohusu jinsi viungo, tishu, na mifumo ya viumbehai inavyofanya kazi mwilini.

Katika Kipindi hiki, utajifunza kuhusu viungo vinavyounda Sehemu ya siri za nje za kike na viungo vya ndani vya uzazi. Katika Kipindi cha 4, tunakufunza kuhusu jinsi homoni zinavyoratibisha viungo vya ndani vya uzazi wa kike na mzunguko wa hedhi. Katika Kipindi cha 5, tunaeleza ovulesheni, utungisho, pandikizo la kiinitete kwenye uterasi ya mama, ukuaji wa fetasi, planseta na lishe ya fetasi. Katika Kipindi cha 6, utajifunza anatomia ya pelvisi ya kike na pia ya fuvu la fetasi, ambayo sharti ipitie kwenye pelvisi ya mama wakati wa kuzaa.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 3

Baada ya kusoma katika Kipindi hiki, unapaswa uweze:

3.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyochapishwa katika herufi nzito. (Maswali ya kujitathmini 3.1 na 3.2)

3.2 Kutambua na kueleza sehemu muhimu za kimsingi za anatomia ya Sehemu ya siri za nje za kike na viungo vya ndani vya uzazi. (Maswali ya kujitathmini 3.2, 3.3 na 3.4).

3.3 Kueleza majukumu ya viungo vikuu vya anatomia kwenye mfumo wa uzazi wa kike na umuhimu wao katika huduma ya ukunga. (Maswali ya kujitathmini 3.3 na 3.4)

3.1 Baadhi ya istilahi za kawaida katika anatomia na fiziolojia

Utakumbana na istilahi nyingi mpya katika kujifunza anatomia na fiziolojia kwa mara ya kwanza. Unaweza kuwa na ufahamu wa baadhi yao kutokana na somo lako la biolojia katika shule ya upili. Katika Kipindi hiki, tumejaribu kutumia istilahi rahisi iwezekanavyo ili kukusaidia kuelewa unachokisoma. Kufafanua nyingi za istilahi zinazotumika katika anatomia na fiziolojia ni zaidi ya Kipindi hiki, lakini kufafanua nyingi za istilahi muhimu zinazotumika katika huduma ya ukunga kutakusaidia kutimiza malengo ya somo la Kipindi hiki na Vipindi vya 4 hadi 6.

Istilahi zinazotumika katika anatomia ya binadamu mara nyingi ni zile zinazoonyesha mahali kilicho kiungo kimoja kwa kulinganisha na kingine au mwili wote (tazama Kisanduku3.1). Utakumbana na istilahi za mahali mara nyingi katika Moduli hii.

Kisanduku 3.1 Baadhi ya istilahi za kawaida za mahali zinazotumika katika anatomi

Juu ya

Chini ya

Ya mstari wa kati wa mwili (ya kati)

Pembeni mwa mstari wa kati wa mwili (pande, kingo, kando)

Mbele ya, kabla ya, mbeleni mwa

Nyuma au nyuma ya

3.2 Anatomia na fiziolojia ya viungo za uzazi za kike

Jukumu la wanawake katika uzazi ni changamani sana kuliko la wanaume:

  • Wanawake hutoa ova (mayai), zinazoweza kutungishwa na mbegu ya kiume.
  • Baada ya utungisho, wanawake pia hubeba na kulinda fetasi inayokua katika uterasi.
  • Baada ya kuzaa, matiti hutoa maziwa ya kumstawisha mtoto.

Kiasili, kila mmoja wetu ana hamu ya kujua jinsi tunavyokua katika uterasi za mama zetu, jinsi fetasi inavyokua katika miezi tisa ya ujauzito, jinsi inavyostawishwa na jinsi mzunguko wa hedhi unavyodhibitiwa. Ili kuelewa haya na maswali mengine husika kuhusu majukumu ya wanawake katika uzazi, unapaswa kujifunza kuhusu anatomia ya viungo vya uzazi vya kike na kuelewa fiziologia (jukumu) ya kila viungo.

Tunaanza na mahali pa kianatomia vilivyo viungo vya uzazi vya kike ukilinganisha na mfumo wa mkojo (figo na kibofu cha mkojo), mfumo wa utumbo na viungo vingine vya karibu katika kaviti ya Pelvisi, (tazama Jedwali 3.2 na Mchoro 3.1 hapa chini).

Jedwali 3.2 Kaviti katika mwili wa binadamu

Kaviti ni nafasi katika mwili wa binadamu iliyo na viungo, viowevu na viungo vingine. Kwa mfano, Kaviti ya fuvu ina ubongo, kaviti ya kifua ina mapafu na moyo, kaviti ya fumbatio ina tumbo, matumbo, ini, mafigo na viungo zinginezo, kaviti ya Pelvisi ina viungo vya uzazi na kibofu cha mkojo. Fahamu kuwa kaviti ya pelvisi ndiyo sehemu ya chini ya kaviti ya fumbatio na hakuna kizuizi baina yazo.

Mchoro 3.1 Sehemu nusu ya kaviti ya Pelvisi inayoonyesha viungo za uzazi wa kike, mwili ukitazama kushoto. Utajifunza zaidi kuhusu istilahi za anatomia zilizotambulishwa katika mchoro huu Kipindi hiki cha somo kinapoendelea.
  • Tazama kwa maakini, mchoro 3.1 kwa muda wa takribani dakika mbili ukuzingatia mahali vilivyo viungo vilivyotambulishwa. Chagua istilahi za mahali zilizo sahihi kutoka kwa Jedwali 3.1 kwa kuelezea mahali uterasi ilipo kwa kulinganisha na kibofu cha mkojo.

  • Kibofu cha mkojo kiko mbele ya uterasi, au unaweza kusema kuwa uterasi iko nyuma ya kibofu cha mkojo. Sehemu ya juu ya uterasi inainama juu ya kibofu hicho na iko juu yake au unaweza kusema kuwa kibofu cha mkojo kiko chini ya sehemu ya juu ya uterasi.

    Mwisho wa jibu

Nyuma ya uterasi, seviksi na uke katika mchoro 3.1, unaweza kuona sehemu ya koloni na rektamu ambapo uchafu mgumu huelekezwa nje ya mwili kupitia mkunduni. Kujua kuhusu mahali pa kianatomia vilivyo viungo hivi vyote ni muhimu sana katika ujauzito, leba na kuzaa. Kwa mfano, kwa mwanamke mjamzito, uterasi kuwa kubwa kutokana na fetasi inayokua itasukuma kibofu cha mkojo na koloni. Hii mara nyingi inaweza kusababisha kibofu kushindwa kudhibiti mkojo na hatimaye mwanamke huyo sharti akojoe mara nyingi zaidi na pia kufunga choo.

Unaposoma kuhusu mfumo wa uzazi wa kike, unafaa kujua kuwa viungo vyake vimegawanywa katika makundi mawili mapana. Viungo vilivyo nje ya uke vinasemekana kuwa Sehemu ya siri za nje za kike, ilhali vilivyo juu (ikiwa ni pamoja na mwanya wa uke) na ndani ya uke vinaitwa viungo za ndani za uzazi wa kike. Tayari umeona baadhi ya viungo katika makundi yote kwa kutazama kutoka upande mchoro 3.1. Sasa tutaangazia kila kundi kwa kina zaidi.

3.3 Sehemu ya siri ya nje ya uke

Tazama Picha 3.2 kwa makini. Viungo vyote vinavyoonekana kutoka nje, vinavyozunguka mianya ya urethra na uke, ikiwa ni pamoja na kinena, labia kubwa, labia ndogo, vestibuli na msamba, vinaunda Sehemu ya siri za nje za uke. Wakati mwingine viungo hivi kwa pamoja huitwa vulva.

Mchoro 3.2 Sehemu ya siri za nje za kike (au vulva).

Hamasa tofauti za hisi zinaweza kusababisha mwitikio kwenye neva zilizo katika viungo vya Sehemu ya siri za nje za kike kama vile mguso, maumivu, shinikizo na kiwangojoto. Hii huvifanya viungo hivi kuwa na hisia na kutiwa ashiki anapoguswa hasa na mwenzi wa kiume. Kufuatia haya, tendo la ngono kati ya mwanamume na mwanamke husababisha ushushaji wa manii kwenye viungo za uzazi za ndani za kike na kuanzisha mchakato wa utungisho, ujauzito, leba na kuzaa.

  • Tambua katika Mchoro 3.2 kuwa mwanya wa urethra, ​​wa uke na mkundu yote imekaribiana kwa pamoja kwenye vulva. Je, unafikiri uhusiano huu wa karibu una umuhimu gani wa kiafya kwa mwanamke mjamzito?

  • Jinsi ujuavyo, eneo karibu na mkundu huchafuliwa na bakteria kutoka kwa uchafu unaotoka kwenye ufereji wa utumbo. Kwa hivyo, maambukizi ya moja kwa moja ya vimelea vya bakteria kwenye mwanya wa urethra na uke hutokea kwa urahisi.

    Mwisho wa jibu

Ni muhimu sana kumshauri mwanamke mjamzito ahakikishe usafi kwenye eneo hili kwa kuzingatia usafi wa kibinafsi. Maambukizi kwenye kibofu cha mkojo na uke ni ya kawaida katika ujauzito, na ikiwa vimelea vya bakteria vitaingia katika uterasi yake, anaweza kumpoteza mtoto.

Sasa tutaangazia kila kiungo kilicho katika Mchoro 3.2, na tutaanza vile vilivyo kwenye kingo za nje, na kumalizia na vile vya kati.

3.3.1 Kinena

Kinena ni sehemu nene yenye mafuta na umbo la nusu mviringo iliyofunikwa na nywele. Sehemu hii iko juu ya kinena simfisisi. Simfisisi ni aina ya jointi thabiti isiyosogezeka na huwa kati ya mifupa. Jinsi utakavyoona katika Kipindi cha 6 cha somo (Mchoro 6.1), nusu mbili za mfupa wa kinena zimeunganishwa katikati na simfisisi ya kinena. Jukumu la tishu ya mafuta kwenye kinena ni kukinga eneo la kinena la mwanamke dhidi ya kuvilia anaposhiriki ngono.

3.3.2 Labia kubwa na labia ndogo

Labia kubwa ni mapindo mawili marefu ya ngozi yenye mafuta na yaliyofunikwa na nywele. Mapindo haya hufunika na kulinda viungo zingine za Sehemu ya siri za nje za kike.

Labia ndogo ni mapindo mawili madogo ya tishu yaliyofunikwa na labia kubwa. Hulinda mwanya wa uke na urethra. Labia ndogo kwa kawaida ni nyumbufu kiasili, sifa inayoziwezesha kutanuka na kunywea wakati wa ngono, leba na kuzaa.

  • Je, unyumbufu huu husaidiaje wakati wa kuzaa?

  • Labia ndogo zinaweza kutanuka ili kuruhusu kichwa cha mtoto kitoke.

    Mwisho wa jibu

Katika nchi zingine, zikiwemo sehemu fulani za Afrika, labia ndogo na kisimi (kilichoelezewa hapa chini) zinaweza kuondolewa na ukeketaji ambao ni mojawapo ya desturi zenye madhara.

Ukeketaji umejadiliwa katika moduli juu ya Afya ya Uzazi wa vijana.

3.3.3 Vestibuli

Vestibuli ni eneo kati ya labia ndogo lililo na kisimi, mianya ya urethra na uke.

Kisimi ni viungo vifupi vyenye uwezo wa kudisa iliyo juu ya vestibuli. Viungo hivi vina neva na mishipa ya damu kwa wingi. Jukumu lake ni kumsisimua mtu wakati wa ngono na ni nyepesi sana kuhisi hasa kwa mguso. Mahali ilipo kianatomi ni sawa na mahali ulipo uume kwa mwanamume.

Ikiwa kisimi na labia ndogo zitaondolewa kwa ukeketaji, mwanya wa uke hautapanuka kwa urahisi wakati wa kuzaa kutokana na kuwepo kwa kovu mahali ambapo tishu iliondolewa. Hii inaweza kusababisha ugumu wakati wa leba na kuzaa, kukiwemo kuvuja damu nyingi na kupasuka kwa tishu iliyojeruhiwa. Wakati mwingine hali hii husababisha fistula - shimo kwenye ukuta wa uke.

  • Ukeketaji unaohusisha labia ndogo na kisimi kwa kawaida hutekelezwa bila dawa ya ganzi. Je, kutatokea athari zipi kwa mwanamke?

  • Kutakuwa na uchungu mwingi kutokana na kuwepo kwa neva kwenye eneo hili. Hali hii inaweza kusababisha kuzirai.

    Mwisho wa jibu.

Pia, labia ndogo na kisimi huwa na mishipa ya damu kwa wingi kwa hivyo kuzikata husababisha kutoka kwa damu nyingi, ambayo inaweza kusababisha kuzirai na mshtuko.

Mwanya wa urethra ndio mdomo au mwanya wa urethra. Ni kiungo chenye muundo wa neli ambacho hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo. Katika Kipindi cha 22 mwishoni mwa Moduli hii, na katika madarasa yako ya mafunzo tendaji, utajifunza jinsi ya kuingiza neli ndogo iitwayo katheta kwenye mwanya huu ili kutoa mkojo kwenye kibofu. Hii inaweza kuwa ya muhimu wakati wa huduma ya dharura kwa mwanamke mjamzito, au wakati wa leba na kuzaa ikiwa hawezi kukojoa kivyake kwa sababu tishu za vestibuli zimevimba na kuibana urethra.

Mwanya wa uke ndio mlango wa ukeni. Hapa ndipo utakapoanza kuona sehemu ya mtoto inayotangulia kutoka mwanya huu unapopanuka na kufunguka leba unapodidimia.

3.3.4 Msamba na kizinda

Eneo lenye misuli lililofunikwa na ngozi kati ya mwanya wa uke na mkundu huitwa msamba. Eneo hili lina misuli dhabiti na neva na husaidia kwa kuegemeza viungo vilivyo kwenye kaviti ya pelvisi. Kizinda ni pindo la tishu nyembamba ya uke na hufunika sehemu fulani ya mlango wa uke kwa wasichana. Inaweza kuraruka wakati wa mazoezi yanayohitaji nguvu nyingi na vile vile kushiriki ngono kwa mara ya kwanza.

3.4 Viungo vya ndani vya uzazi wa kike

Katika kujifunza kuhusu ujauzito na kuzaa, ni muhimu kuelewa viungo vya kianatomi vinavyohusika kwa utoaji wa mayai (ova), utungisho, na ukuaji wa fetasi. Katika sehemu hii utajifunza jinsi ya kutambua na kueleza viungo vya ndani vya uzazi wa kike zinazohusika katika michakato hii. Kujua mahali zilipo na majukumu ya viungo hivi pia ni muhimu kwa kufanya uchunguzi sahihi wa kitabibu kwa wanawake wajawazito na kuzaa kwa usalama.

3.4.1 Mishipa ya falopio na ovari

Anza kwa kuutazama kwa makini mchoro 3.3. Jinsi unavyoona katika mchoro, kuna mishipa ya falopio miwili, mmoja kila upande wa uterasi. Miisho ya mishipa hii, iliyo mithili ya vidole (iitwayo fimbriae), iko karibu na ovari kwa upande huo huo na hufunguka kuelekea kwenye kaviti ya pelvisi. Hii ina maana kuwa kukiwa na maambukizi kwenye kaviti ya pelvisi yanaweza kuingia kwenye uterasi kupitia mishipa ya falopio. Vile vile, kukiwa na maambukizi kwenye uterasi, yanaweza kuenea katika mishipa ya fallopio hadi kwenye kaviti ya pelvisi kisha kwenye fumbatio nzima huku yakiathiri viungo vingine. Haya yanaweza kuwa hatari yasipotibiwa mapema.

Mchoro 3.3 viungo vya viungo za ndani za uzazi wa kike

Ovari ni jozi ya viungo za uzazi wa kike ambazo hutoa mayai (ova). Viungo hizi huwa kwenye kaviti ya pelviksi, moja kila upande wa uterasi chini ya mianya ya mishipa ya fallopio (tazama Mchoro 3.3). Viungo hizi hukaa mahala pake kwa kujishikiza kwenye ligamenti mbili. Ligamenti ni tishu za kuunganisha zenye unyuzi na uwezo wa kupindika zinazoshikilia viungo mbalimbali vya ndani ya mwili. Pia huunganisha mfupa mmoja kwa mwingine katika jointi.

Wanawake huzaliwa wakiwa na idadi isiyobadilika ya takribani mayai (ova) 60, 000 yasiyopevuka. Mayai haya huwa katika vishimo vidogo kwenye ovari viitwavyo foliko za ovari. Kila ova ina uwezo wa kupevuka na kuwa tayari kwa utungisho lakini ni mayai 400 tu yanayopevuka wakati wa maisha ya mwanamke. Kila mwezi foliko kadhaa za ovari huanza kuwa kubwa na ova iliyo ndani kuanza kupevuka, lakini kwa kawaida, ni moja tu itakayoachiliwa kutoka kwenye ovari. Utoaji wa ova huitwa ovulesheni. Foliko zingine zilizosalia kuanyeusi.

  • Je, ni nini kinachoweza kutendeka iwapo ova mbili zitaachiliwa kwa wakati mmoja?

  • Mwanamke huyo anaweza kupata ujauzito wa mapacha.

    Mwisho wa jibu

Foliko za ovari zinazokua pia hutoa homoni za uzazi wa kike ambazo ni estrojeni na projesteroni ambazo ni muhimu kwa kudhibiti mzunguko wa hedhi kila mwezi na katika ujauzito. Utajifunza mengi zaidi kuhusu homoni hizi katika vikao vya 4 na 5 vya somo.

Homoni ni kemikali za kutuma ishara ambazo hutengenezwa mwilini na kuzunguka katika damu. Homoni tofauti hudhibiti shughuli za seli au viungo tofauti.

Baada ya ovulesheni sehemu ya ndani ya hiyo foliko tupu hukua na kutengeneza kitu chenye rangi ya manjano ndani ya ovari kiitwacho kopasi luteamu, ambayo hufanya kazi kwa muda kama viungo ya kutoa homoni.

Kopasi luteamu hutoa estrojeni na projesteroni kwa takribani siku 14 zitakazofuata. Estrojeni hunenepesha tishu-mafuta kwenye kuta za uterasi kukiwa na mimba. Projesteroni husimamisha ovulesheni zaidi wakati wa mimba.

  • Je, kwa nini ni muhimu kuzuia ovulesheni zaidi mara tu mwanamke anapokuwa mjamzito.

  • Hii ina maana kuwa mwanamke huyo hawezi kupata ujauzito mwingine akiwa tayari ujauzito huu ndiposa virutubishi vyake vyote viweze kutumika katika kustawisha na kukinga fetasi ya kwanza inayokua katika uterasi yake.

    Mwisho wa jibu

Ikiwa ujauzito haukutokea katika siku 14 baada ya ovulesheni, kopasi luteamu kua nyeusi na kuacha kutoa projestoreni. Matokeo ya haya ni kukatizwa kwa damu inayoletwa katika tishu-mafuta hizi za ziada kwenye kuta za uterasi na kusababisha kusawijika pia kwa tishu hizi za ziada na hatimaye kutolewa kupitia ukeni kama hedhi. Viwango vya estrojeni vinaweza kuanza kupanda na ovulesheni inaweza kutokea tena kwa mwanamke huyo mwezi unaofuata.

Ovari inapoachilia ova pevu (ovulesheni), fimbriae za mshipa wa falopio hugwia ova hiyo na kuielekeza kwenye uterasi. Mbegu ya kiume husonga kwenye mishipa ya falopio, hutungisha mimba ikutanapo na ova iliyoachiliwa (jinsi utakavyoona kwenye vikao vya 4 na 5 vya somo). Bitana ya Mishipa ya fallopio na vinyeso vyake hudumisha ova na manii, hurahisisha utungisho na hurutubisha ova iliyotungishwa hadi itakapofika kwenye uterasi.

3.4.2 Uterasi

Uterasi ni viungo wazi yenye misuli ambamo ova iliyotungishwa hupandikizwa na kukua kuwa fetasi. Jukumu kuu la uterasi ni kukinga na kurutubisha fetasi hadi itakapozaliwa.

Wakati wa ujauzito, kuta za uterasi zenye misuli hunenepa na kunyumbuka ili kuhimili fetasi inayokua wakati wa ujauzito. Pia ni lazima uterasi iweze kuhifadhi kioevu zaidi cha amnioni (maji yanayozingira fetasi kwenye mfuko wa membreni za fetasi) na kondo (kiungo kinachopeleka virutubishi kutoka kwa mama hadi kwa fetasi). Utajifunza mengi zaidi kuhusu haya katika Kipindi cha 5 cha somo.

  • Je, unafikiri ni kwa nini kuta zenye misuli za uterasi hunenepa wakati wa ujauzito?

  • Rusu nene ya misuli ina nguvu za kuhimili fetasi inayokua na vitu vingine vilivyo kwenye uterasi ambavyo huendelea kuwa vizito ujauzito unapozidi kukua.

    Mwisho wa jibu

Uterasi ina sehemu nne za kianatomia zilizoonyeshwa katika Mchoro 3.4:

  • Mwili: Ndiyo sehemu kuu ambayo iko upande wa juu na ni theluthi mbili za uterasi nzima.
  • Fandasi: sehemu juu ya uterasi iliyotanuka na iko katikati ya mwungano wa mishipa ya falopio.
  • Kaviti ya endometria: hii ni nafasi yenye umbo la pembe tatu katikati ya kuta za uterasi.
  • Seviksi: ni shingo nyembamba iliyo mwisho wa upande wa juu wa uke.
Mchoro 3.4 Muundo wa uterasi tupu ukionyesha hizo sehemu nne kuu.

Ukuta wa uterasi una rusu tatu za tishu, mbili nazo zimeonyeshwa katika mchoro 3.4:

  • Perimetriumu: hii ni rusu ya nje kabisa iliyoundwa kwa membreni nyembamba na hufunika uterasi. (Si muhimu kwako kujua istilahi hii kwa mujibu wa utunzaji wa ukunga)
  • Miometriamu: hii ni rusu ya katikati ambayo ni nene na yenye misuli ilivyoonyeshwa katika mchoro 3.4.
  • Endometriamu: hii ndiyo rusu ya ndani kabisa ya uterasi ambayo ni nyembamba na hunenepa wakati wa mzunguko wa hedhi. Hii ndiyo tishu inayokua na kujilimbikiza kila mwezi kwa mwanamke aliye katika umri wa uzazi kutokana na athari za homoni za uzazi za kike.
  • Je, ni nini kinachofanyika kwa endometriamu homoni zikiacha kuzunguka baada ya ovulesheni?

  • Kuletwa kwa damu hukatizwa na endometriamu kusawijika na kutolewa mwilini kupitia ukeni kama hedhi ya kila mwezi.

    Mwisho wa jibu

3.4.3 Seviksi na uke

Seviksi ni shingo nyembamba ya upande wa chini wa uterasi inayotengeneza kijia chenye umbo la neli kinachoelekea katika upande wa juu wa uke(tazama Mchoro 3.4). kwa kawaida huwa na urefu wa takribani centimita 3 hadi 4.

Uke ni kijia chenye misuli, na urefu wa takribani centimita 8 hadi 10 kilicho kati ya seviksi na viungo vya uzazi vya nje. vioevu vinavyolainisha uke hutoka kwenye tezi zilizo katika sevikisi.

  • Uke una majukumu matatu. Je, unaweza kuyataja?

  • Ndiyo viungo inayoupokea uume wakati wa kushiriki ngono na ndipo manii yanapowekwa. Ndio njia ambapo hedhi hutokea kila mwezi kwa mwanamke asiyepata ujauzito. Pia ndiyo njia ambapo mtoto hupitia anapozaliwa.

    Mwisho wa jibu

Wanawake wajawazito wanapaswa kuhimizwa kutia nguvu misuli ya uke kwa kuibana kwa ukakamavu wanavyoweza kwa angalau mara kumi na kurudia zoezi hili kwa angalau mara nne kila siku. Mwanamke anaweza kujifunza jinsi ya kulifanya zoezi hili anapokojoa. Mwanamke anapaswa kuibana misuli ya uke anapokojoa, mkojo usimame, kisha ailegeze misuli hiyo mkojo utiririke tena. Mara tu anapojua jinsi ya kuibana misuli hii, anapaswa kulifanya tu zoezi hili wakati hakojoi. Kufanya zoezi hili la kubana kunaweza kusaidia katika:

  • Kuzuia kuvuja kwa mkojo
  • Kuzuia kuraruka kwa uke na msamba viungo hivi vinapotanuliwa wakati wa kuzaa
  • Kuharakisha uponaji baada ya kuzaa
  • Kuongeza furaha ya ngono

Katika Kipindi hiki umejifunza viungo na majukumu ya viungo katika mfumo wa uzazi wa kike na umuhimu wao katika utunzaji wa ukunga. Katika Kipindi kitakachofuata utaangazia udhibiti wa homoni kwa mzunguko wa uzazi kwa wanawake.

Muhtasari wa Kipindi cha 3

Katika Kipindi cha 3 umejifunza kuwa;

  1. Anatomia ni somo juu ya viungo vya mwili wa binadamu na fiziolojia ni somo juu ya majukumu patanifu ya viungo, tishu na mifumo ya mwili.
  2. Mfumo wa uzazi wa kike umegawanywa katika sehemu ya ndani ya genitalia (chini na nje ya mwanya wa uke) na viungo vya uzazi vya ndani (juu ya mwanya wa uke katika kaviti ya pelvisi)
  3. Viungo vya uzazi vya ndani viko karibu na kibofu, utumbo mkubwa na rektamu; mwanya wa nje wa uke uko karibu na ule wa urethra na mkundu. Uhusiano huu wa karibu huongeza uwezekano wa kuenea kwa maambukizi katika eneo la genitalia.
  4. Katika jamii zingine za kitamaduni, kisimi na labia ndogo mara nyingi huondolewa kwa ukeketaji; hii inaweza kusababisha athari za hatari kubwa (hata zinazoweza kusababisha kifo) kwa mwanamke huyo, hasa wakati wa leba na katika kuzaa.
  5. Ovari ni viungo za uzazi vya kike ambavyo hutoa ova moja kila mwezi katika miaka ya uzazi. Mmoja wa mishipa ya falopio hubeba ova kutoka kwa ovari hadi kwenye uterasi. Utungisho hufanyika katika mshipa wa falopio.
  6. Uterasi ni viungo vyenye misuli inayoipa fetasi inayokua ulinzi na chakula wakati wa ujauzito.
  7. Homoni za uzazi wa kike; estrogeni na projesteroni huelekeza upevukaji wa ova kwenye ovari, utoaji wa ova (ovulesheni) na unenepaji wa endometria (bitana yenye mafuta kutani mwa uterasi). Endometriamu hukwangulika na kutolewa kama hedhi ikiwa utungisho na ujauzito hautatokea.
  8. Uke ndiyo kiungo inayoupokea uume wakati wa kushiriki ngono. Ndiyo njia ambapo hedhi hutokea, na pia hutengeneza sehemu ya chini ya njia ya uzazi.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 3

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki, unaweza kutathmini ni kwa kiwango kipi umeweza kutimiza malengo yake kwa kujibu maswali haya. Yaandike majibu yako katika daftari lako na uyajadili na Mkufunzi wako katika Kipindi Kitakachofuata cha Masoma ya Kusaidiana. Unaweza kuyalinganisha majibu yako na muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la kujitathmini 3.1(linatathmini Malengo ya Somo 3.1 na 3.2)

Tazama mchoro 3.5. Andika majina ya viungo vya mwili vilivyopachikwa herufi ‘a’ hadi ‘i’.

Mchoro 3.5.Andika majina ya viungo vya ndani vya uzazi wa kike ili kukamilisha maswali ya kujitathmini 3.1.
Answer

Majibu sahihi ya majina kwa mchoro 3.5 ni kama ifuatavyo:

  • a.ni uke
  • b.ni seviksi
  • c.ni uterasi
  • d.ni ovari
  • e.ni fandasi
  • f. ni ligamenti inayoshikilia ovari
  • g.ni mshipa wa falopio
  • h.ni fimbriae
  • i.ni ligamenti ya ovari

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 3.2 (linatathmini Malengo ya Somo 3.1)

Chagua istilahi sahihi za sehemu kutoka katika jedwali 3.1 kueleza mahali panaporejelea zilipo uterasi na rectamu katika mcharo 3.1.

Answer

Uterasi iko mbele na juu ya rektamu. Njia nyingine ya kueleza sehemu hizi ni kusema kuwa rektamu iko nyuma na chini ya uterasi.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 3.3 (linatathmini Malengo ya Somo 3.2 na 3.3)

Je, ni viungo vipi vinavyoondolewa kwa ukereketaji na ni madhara yapi yanayoweza kumkumba mwanamke wakati wa leba na katika kuzaa?

Answer

Viungo vinavyoondolewa kwa ukereketaji ni kisimi na labia ndogo. Kovu inayotokea mikato inapoendelea kupona huzuia uwezo wa kawaida wa vulva kutanuka wakati wa kuzaa ili kuruhusu mtoto kupita kwenye njia ya uzazi. Kutokana na haya, kuzaa kunaweza kuzuiliwa kisha uke uraruke na kusababisha maumivu makali na upotezaji wa damu. Wakati mwingine nasuri (shimo kwenye ukuta wa uke) inaweza kuraruka na upotezaji wa damu unaweza kuhatarisha maisha ya mwanamke huyo.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 3.4 (linatathmini Malengo ya Somo 3.2 na 3.3)

Je, ni kauli ipi kati ya hizi isiyo kweli? Taja ni kwa nini kauli hiyo si kweli.

  • A.Maambukizi katika uterasi yanaweza kuingia kwenye kaviti ya pelvisi kupitia ukeni.
  • B.Msamba ni sehemu yenye misuli katikati ya mwanya wa uke na mkundu.
  • C.Upevukaji wa ova hudhibitiwa na homoni za uzazi wa kike.
  • D.Tezi zilizo kwenye seviksi hutoa vinyeso vinavyolainisha uke.
  • E.Fandasi ndiyo ‘shingo’ nyembamba iliyo kwenye upande wa chini wa uterasi.
Answer
  • A.Si kweli. Maambukizi kwenye uterasi yanaweza kuingia katika kaviti ya pelvisi kupitia katika mishipa ya falopio ambayo iko wazi upande wa mwisho. Maambukizi katika uterasi yanaweza kuenea ukeni na mara nyingi hujitokeza kama mchozo unaonuka kutoka kwenye mwanya wa uke katika vulva.
  • B.Ni kweli. Msamba ni sehemu yenye misuli katikati ya mwanya wa uke na mkundu.
  • C.Ni kweli. Upevukaji wa ova hudhibitiwa na homoni za uzazi wa kike.
  • D.Ni ukweli. Tezi zilizo kwenye seviksi hutoa unyeso unaolainisha uke.
  • E.Si kweli. Fandasi ndilo jina inayopewa sehemu yenye umbo la kuba juu ya uterasi. Shingo nyembamba kwenye sehemu ya chini ya uterasi huitwa seviksi.

Mwisho wa jibu.