Skip to main content
Printable page generated Thursday, 25 April 2024, 1:49 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 25 April 2024, 1:49 AM

5. Utungisho, Upandikizaji na Kuzunguka kwa Damu kwenye Fetasi na Plasenta

Kipindi cha 5 Utungisho, Upandikizaji, na Mzunguko wa Damu kwenye Fetasi na Plasenta

Utangulizi

Wakati kamili ambapo ova iliyotungishwa, embrio, fetasi, au mtoto mchanga huitwa binadamu ni jambo ambalo limekumbwa na utata. Jambo hili ni tofauti miongoni mwa watu binafsi, vikundi vya kidini, mifumo ya haki, na hata mataifa. Kipindi hiki hakizungumzii wazo hili gumu, bali kinazingatia kuhusu jinsi ova inavyotungishwa na kupandikizwa kwenye uterasi, na jinsi fetasi inavyolishwa wakati wa ujauzito. Kipindi hiki kitakusaidia kutambua vipengele vinavyoweza kupelekea matatizo wakati wa ujauzito.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 5

Katika Kipindi hiki utajifunza:

5.1 Kufasili na kutumia kisahihi maneno yote yaliyoandikwa kwa herufi nzito (Swali la Kujitathmini 5.1)

5.2 Kueleza kuhusu utungisho, upandikizaji kwenye uterasi wa ova iliyotungishwa, na vipindi vya mwanzo vya kukua kwa embrio na plasenta. (Swali la Kujitathmini 5.1 na 5.2)

5.3 Eleza jinsi mzunguko wa damu kwenye fetasi unavyofanyika na jinsi fetasi hupokea chakula kutoka kwa mama kupitia plasenta. (Swali la Kujitathmini 5.1 na 5.3)

5.1 Seli za uzazi za kiume na za kike

Ili kuelewa jinsi utungisho unavyofanyika, ni sharti uelewe muundo wa mbegu za kiume na ova ya kike.

5.1.1 Mbegu za uzazi za kiume: seli za uzazi za kiume

Seli ya mbegu ya kiume iliyokomaa (tazama Mchoro 5.1) ni seli ndogo ya kizazi ya kiume inayoogelea. Seli hii ina kichwa, mwili na mkia. Kichwa chake kimefunikwa na chepeo na kina kiiniseli cha chembe nzito za kijenetiki. Kichwa hiki kimeshikishwa kwenye sehemu iliyo na mitokondria, ambayo husambaza nguvu za kuiwezesha mbegu hii kutenda kazi. Mkia wa mbegu hii unaweza kukunjika na kunyooka, hivyo kuifanya isonge kwa mwendo kama wa wimbi.

Mchoro 5.1 Muundo wa mbegu za uzazi za kiume (seli ya uzazi ya kiume)
  • Tazama Mchoro 5.1. Je, unaweza kueleza jinsi mbegu ya uzazi ya kiume inavyosonga ukeni, uterasini, na kisha kwenye mishipa ya falopio?

  • Mkia wa mbegu ya kiume hujipinda kutoka upande hadi mwingine, hivyo kuisongesha mbele. Mitokondria ni oganeli zinazotolesha nguvu katika seli. Oganeli hizi husambaza nguvu kwenye mkia wa mbegu ya kiume ili kuiwezesha kusonga.

    Mwisho wa jibu.

Mbegu ya kiume hujumuisha takriban 5% pekee ya manii yanayotolewa na mwanaume wakati wa ngono. Takriban mbegu milioni 100 - 400 hutolewa kila wakati. Mbegu hizi hubebwa kwenye kiowevu kilicho na virutubishi (manii), kinachosaidia kuziweka hai. Mbegu za kiume ni ndogo sana. Mbegu moja ndiyo seli ndogo zaidi katika mwili wa mwanamume.

Mbegu mpya hukua katika kende (korodani) kuanzia kipindi cha kubaleghe hadi utu uzima wa mwanaume. Mbegu hukua hadi kupevuka kwa takriban siku 72. Kutoleshwa kwa mbegu za kiume huhitaji kiwangojoto cha mwili cha nyusi 3 – 5 chini ya kile cha kawaida. Hii ndiyo sababu makende huwa nje ya fumbatio. Makende yanapofikiwa na kiasi kingi cha joto, uzalishaji wa mbegu unaweza kutatizika na kusababisha ugumba.

5.1.2 Ova: mbegu za kizazi za kike

Kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 3, mtoto wa kike huzaliwa akiwa na ova zote atakazokuwa nazo maishani mwake, ingawa zikiwa bado hazijapevuka. Kila ova ni seli kubwa yenye membreni iliyo nje. Ova huwa imejaa kiowevu chenye wingi wa protini. Ova ina kiiniseli chenye chembe za kijenetiki za kike.

Ova huhifadhiwa kwenye foliko za ovari, na ova chache huanza kupevuka kila mwezi baada ya msichana kubaleghe afikiapo umri wa takriban miaka 12 -15. Utaratibu huu huendelea hadi wakati wa ukomohedhi, afikiapo takriban miaka 48 - 50, wakati ambapo vipindi vya hedhi hukoma.

  • Ni homoni zipi zinazosisimua ova ili kuiwezesha kupevuka?

  • Haipothalamasi iliyo ubongoni hutolesha homoni inayotoa gonadotropini (GnRH). Homonihii husisimua tezi ya pitituari (iliyo ubongoni pia) ili kutolesha homoni ya kusisimua foliki (HKF) na homoni ya lutea (HL). Homoni hizi mbili hutenda kazi kwa pamoja kwenye foliki za ovari na kusababisha baadhi ya foliki hizi kuanza kupevuka.

    Mwisho wa jibu

  • Ikiwa siku ya kwanza ya hedhi inaitwa Siku ya 1 ovari itaachilia ova iliyopevuka baada ya siku ngapi (ovulesheni)?

  • Kwa wanawake wengi, ovulesheni hufanyika takriban siku ya 14 baada ya hedhi.

    Mwisho wa jibu.

5.2 Utungisho

Utungisho ni kuunganika kwa kiiniseli cha mbegu za uzazi za kiume na kiiniseli cha ova. Ili utungisho utokee, ni sharti mbegu za kiume ziingie ukeni katika kipindi kisichozidi siku 3 kabla ya ovulesheni au katika kipindi kisichozidi siku moja baada ya ovulesheni. Kipindi cha ovulesheni ni kifupi kwa sababu mbegu za kiume na ova huishi kwa muda mfupi, na zote hufa zisipokutana na kuungana katika kipindi hiki. Kufuatia ovulesheni, ova huchukuliwa na fimbria ya mshipa wa falopio iliyo katika upande huo wa mwili ambapo ovari iliachilia ova. Ova hubaki kwenye mshipa wa falopio ikiwa ingali hai na inayotenda kazi vyema kwa muda wa saa 12 - 24. Mbegu za kiume zinaweza kuishi kwa muda mrefu zaidi kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke, kwa takriban saa 72, ingawa nyingi hufa mapema.

Mbegu za kiume ziingiapo ukeni huogelea kupitia katika seviksi huku zikiingia kwenye uterasi, kisha kuingia kwenye mishipa ya falopio. (Tazama tena Mchoro 3.3.) Utungisho wa ova hufanyika katika mshipa wa falopio. Kukazana kwa misuli ya kuta za uterasi na mishipa ya falopio husaidia kusongesha mbegu za kiume. Mbegu hizi zinaweza kuogelea milimita kadhaa kwa sekunde, hivyo zinaweza kufika katika mishipa ya falopio kwa muda wa takriban dakika 15. Hata hivyo mamilioni ya mbegu hizi hufa zikiwa zingali zinasonga.

Mchoro 5.2 Utungisho wa ova ya binadamu.

Mbegu moja tu kiume ndiyo hufaulu kutungisha ova (Mchoro 5.2) kwa kupenyeza hadi ndani ya membreni ya seli na kuwekeza chembe za kijenetiki za kiume kwenye seli ya kike, ambapo viiniseli hivi viwili huungana. Ova iliyotungishwa (zigoti) punde hupinga kupenyeza kwa mbegu nyingine. Baada ya utungisho, zigoti hubaki kwenye msipa wa falopio kwa takriban saa 72. Zigoti hii hukua upesi katika kipindi hiki.

5.3 Vipindi vya kwanza vya kukua kwa embrio

Kuanzia utungisho hadi miezi 8 ya ujauzito, mwanadamu anayekua huitwa embrio. Kwanza, embrio hugawanyika na kuwa seli mbili. Seli hizi hugawanyika tena na kuwa seli nne (tazama Mchoro 5.3). Seli hizi hugawanyika mara nyingi hadi mviringo wa seli uitwao morula kujitokeza baada ya siku tatu. Seli zilizo katika morula zinapoendelea kugawanyika, huanza kusongea pembeni mwa mviringo huu hadi mwanya kufanyika. Mviringo huu huitwa blastosisti katika takriban siku tano baada ya utungisho. Fahamu katika Mchoro 5.3 kuwa blastosisti ina bonge la seli kwenye sehemu moja ya mwanya.

Mchoro 5.3 Utaratibu wa utungisho na upandikizaji katika mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Embrio ya kwanza husongea kwenye mshipa wa falopio kuelekea uterasini pindi inavyoendelea kubadilika. Utaratibu huu huchukua muda wa siku 5 - 7

5.3.1 Upandikizaji

Siku 5 -7 baada ya utungisho, blastosisti hufika uterasini na kujishikisha kwenye endometriamu ilionenepa (sehemu ya ndani ya uterasi). Utaratibu huu hujulikana kama upandikizaji. Iwapo embrio itaendelea kuishi, kipindi cha ujauzito huanza. Hata hivyo, embrio huenda isijipandikize, au isidumu kwa siku nyingi. Ikiwa ni hivyo, embrio hutolewa uterasini huku endometriamu ikimenyeka, kisha kupitia ukeni kama damu ya hedhi. Mara nyingi, mimba ya siku chache huharibikia namna hii. Mwanamke anaweza kukosa kufahamu kuwa alikuwa mjamzito kwa kipindi kidogo.

Unapokisia kuwa mwanamke ana mimba ya kiektopi, mpe rufaa mara moja kwa...?

Mara kwa mara, upandikizaji hutokea kwenye mshipa wa falopio. Aina hii ya mimba, na ambayo ni hatari sana, huitwa mimba ya kiektopi. Embrio inapoendelea kukua, mshipa wa falopio unaweza kupasuka na kusababisha maumivu makali na damu kuvujia kwenye njia ya fumbatio.

Ikiwa blastosisti itafaulu kujipandikiza kwenye uterasi, seli huendelea kujigawa huku ikisongea kwenye sehemu mpya na kuchukua miundo miwili tofauti.

  • Seli tatu au nne za blastosisti hukua na kuunda sehemu ya ndani ya bonge la seli. Wiki chache baadaye, bonge hili huundika kuwa miundo maalum ya embrio ya binadamu iliyo na kichwa, moyo unaodunda na miguu na mikono midogo. Baadhi ya seli hizi pia hukua na kuwa membreni za fetasi, ambazo huunda mfuko wa maji uliozunguka embrio ili kuikinga.
  • Takriban seli 100 za blastosisti zinazosalia kutoka huunda trofoblasti ( hutengeneza trophoblasti ambayo huchangia kukua kwa plasenta ya mtoto). Awamu ya kwanza ya kukua kwa plasenta ni wakati seli za trofoblasti zinapoingia kwenye endometriamu.

Jedwali 5.1 linaeleza kwa muhtasari awamu muhimu za utaratibu wa kukua kwa binadamu kutoka utungisho hadi mwaka mmoja baada ya kuzaliwa.

Kisanduku 5.1 Awamu za kukua kwa binadamu baada ya utungisho

Utungisho: kuungana kwa ova na mbegu ya kiume katika siku ya kwanza

Morula: bonge la seli baada ya siku tatu

Blastosisti: bonge la seli lenye uwazi baada ya siku tano.

Trofoblasti: hutumika kuunda embrio katika vipindi vya kwanza, membreni ya fetasi na plasenta baada ya siku 5 -7.

Embrio: binadamu anayekua, kuanzia utungisho hadi wiki 8 za ujauzito.

Fetasi: Binadamu anayekua kuanzia wiki ya 9 ya ujauzito hadi kuzaliwa, baada ya wiki 40.

Mtoto mzawa: mtoto aliyezaliwa, kutoka siku ya kuzaliwa hadi siku 28.

Mtoto mchanga: mtoto aliye na umri chini ya mwaka mmoja.

5.4 Plasenta

Plasenta ni kiungo cha muda mfupi kinachohitajika wakati embrio na fetasi inapokua. Plasenta husaidia katika ubadilishanaji wa virutubishi na oksijeni baina ya mama na fetasi, na kusafirisha takamwili za fetasi hadi katika mwili wa mama ili ziondolowe na viungo vya mwili vya mama. Damu ya mama na ya mtoto haichanganyiki katika plasenta. Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu jinsi damu huzunguka kwenye fetasi na plasenta na jinsi fetasi hulishwa na kuondoa kinyesi chake. Mfumo wa damu katika plasenta pia hukinga fetasi kutokana na kemikali na viini vya maambukizi vilivyo katika damu ya mama.

Kama ilivyoelezewa hapo juu, plasenta huanza kukua kutoka trofoblasti baada ya embrio kujipandikiza kwenye uterasi. Plasenta hukua kikamilifu katika kipindi cha miezi 2, kisha kuendelea kukua hadi leba inapoanza. Ifikapo wakati wa mtoto kuzaliwa, plasenta huwa na uzito wa kadri gramu 600.

5.4.1 Mishipa ya damu ya mama na mtoto

Ili kuelewa jinsi damu ya mama na ya mtoto inavyoweza kukaribiana katika plasenta na isichanganyike, ni sharti kwanza ujifunze ukweli wa kimsingi kuhusu damu na mishipa ya damu. Mfumo wa moyo na mishipa unajumuisha moyo, mishipa ya damu, (veni na ateri - tazama Jedwali 5.2), na damu inayozunguka mwilini. Huu ndio mfumo wa uchukuzi unaosambaza oksijeni na virutubishi vilivyofyonzwa kutoka kwa mfumo wa tumbo na utumbo hadi kwenye seli zote, tishu na viungo vyote vya mwili wa mama na wa mtoto anayekua. Oksijeni na virutubishi husaidia mama na mtoto kupata nguvu wanayohitaji kutekeleza majukumu yao. Mfumo huu pia hurudisha dioksidi ya kaboni, ambayo ni mabaki ya pumzi, kwenye mapafu ambapo huondolewa. Utaratibu wa kikemikali unaofanyika mwilini hutolesha taka kwa wingi. Taka hizi husafirishwa kwa damu hadi kwenye figo na ini ambapo huondolewa. Majukumu mengine ya mfumo wa damu na mishipa ni pamoja na kudhibiti kiwangojoto cha mwili na kusafirisha homoni na ajenti zinginezo zinazodhibiti majukumu ya mwili.

Kisanduku 5.2 linaonyesha baadhi ya vidokezo muhimu kuhusu mwingiliano wa mifumo ya moyo na mishipa ya mama na mtoto, na jinsi unavyohusiana na kuzunguka kwa damu katika plasenta.

Kisanduku 5.2 Vidokezo muhimu kuhusu kuzunga kwa damu ya fetasi, mama na plasenta

Damu yenye oksijeni: Damu inayopeleka oksijeni na virutubishi vya kutosha hadi kwenye seli, tishu na ogani za mwili ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ifaavyo.

Damu isiyo na oksijeni: Ni damu iliyo na kiasi kidogo cha oksijeni na kiasi kikubwa cha taka zilizoyeyuka na dioksidi ya kaboni kuzidi damu yenye oksijeni.

Ateri za kiambakitovu: Kwa kawaida, ateri husafirisha damu yenye oksijeni, lakini ateri zote mbili za kiambakitovu (tazama Mchoro 5.4) huchukua damu isiyo na oksijeni kutoka mwilini mwa fetasi hadi kwenye plasenta. Damu iliyo katika ateri za kiambakitovu husambazwa kwenye plasenta na moyo wa fetasi.

Vena za mama: Vena za mama huchukua damu isiyo na oksijeni kutoka kwenye plasenta. Damu inapopitia kwenye ini na figo, taka zilizoyeyuka hutolewa, ikiwa ni pamoja na zile zilizochukuliwa na vena za endometria kutoka kwenye plasenta. Damu isiyo na oksijeni inapofika katika moyo wa mama husambazwa kwenye pafu zake ili kupata oksijeni zaidi.

Ateri za mama: Ateri za mama husafirisha damu yenye oksijeni ambayo husambazwa na moyo wake mwilini kote. Ateri zake za endometriamu\2 huleta damu kwenye uterasi na kisha kwenye plasenta, huku zikileta damu na virutubishi kutoka kwenye mfumo wa mama wa umeng’enyaji.

Vena ya kiambakitovu: Kwa kawaida, vena husafirisha damu isiyo na oksijeni, lakini vena ya kipekee ya kiambakitovu (tazama Mchoro 5.4) husafirisha damu yenye oksijeni na virutubishi kutoka kwenye plasenta hadi moyo wa fetasi, ambao huisambaza kote katika mwilini mwa fetasi.

Mchoro 5.4 Mzunguko wa damu kwenye fetasi na plasenta. Kumbuka kwamba kuna ateri mbili na vena moja ya kiambakitovu.

5.4.2 Mzunguko wa damu kwenye plasenta

Wakati wa kukua kwa fetasi, sehemu za plasenta huchomoza kwenye endometriamu ya mama. Michomozo hii midogo huitwa vili. Vili hutoa kemikali zinazomeng’enya, kuvunjavunja na kufungua kuta za ateri za mama kwenye endometiriamu, na kupelekea mianya kwenye endometiriamu kujaa damu yenye oksijeni na virutubishi kutoka kwenye ateri za endometiriamu za mama.

Hata hivyo, vidimbwi vya damu ya mama vilivyo kwenye plasenta havichanganyiki na damu ya fetasi. Kuta za ateri na vena ndogo zaidi (kapilari) zilizo katika plasenta hubakia nzima (hazimeng’enywi). Kapilari hizi hulowa kwa nje na damu ya mama, iliyotenganishwa na damu ya fetasi iliyo ndani ya kapilari na kuta za mishipa (Mchoro 5.5).

Mchoro 5.5 Mzunguko wa damu katika plasenta, unaoonyesha kapilari za fetasi zikiwa zimelowa damu ya mama.

Kapilari za fetasi katika plasenta zipo karibu sana na “dimbwi” la damu ya mama, iliyo na wingi wa oksijeni na virutubishi vilivyoyeyushwa, kuliko damu ya fetasi iliyo ndani ya mishipa ya fetasi.

  • Nini hutendetekea oksijeni na virutubishi vilivyo ndani ya damu ya mama katika hali hii?

  • Oksijeni na virutubishi huvuka kutoka ndani ya damu ya mama hadi katika damu ya fetasi kupitia kuta za kapilari. Utaratibu huu huitwa msambao. Kupitia utaratibu huu, mfumo wa mzunguko wa damu wa fetasi hupata oksijeni na virutubishi.

    Mwisho wa jibu.

  • Je, unafikiri takamwili zilizoyeyushiwa ndani ya damu ya fetasi hutolewa vipi zinapopitia kwenye plasenta?

  • Takamwili zilizoyeyushiwa ndani ya damu ya fetasi zinazoingia katika plasenta husambaa kupitia kuta za mishipa ya damu ya fetasi hadi katika damu ya mama. Damu ya mama kisha huzisafirisha taka hizi ili ziondolewe na maini na figo za mama.

    Mwisho wa jibu.

Plasenta ina sehemu kubwa inayosaidia kusafirisha dutu katika pande zote kupitia msambao, kama ilivyoelezwa hapo juu. Fahamu kwamba damu ya mama kamwe haichanganyiki na ya fetasi, bali huwa imetenganishwa kwa kuta za mishipa ya damu ya fetasi.

5.4.3 Plasenta kama kichungi

Mojawapo ya majukumu ya plasenta ni kutumika kama kichungi. Plasenta huruhusu chembe zenye manufaa kwa fetasi, kama vile oksijeni na virutubishi, kupita kutoka kwenye mfumo wa damu ya mama hadi wa fetasi. Hata hivyo, plasenta pia hujaribu kuzuia vitu vyenye madhara kupita. Kwa mfano, plasenta huruhusu protini na baadhi ya kemikali kubwa katika damu kupita, zikiwemo antibodi, ambazo ni kemikali zinazoundwa mwilini mwa mama ili kukumbana na viini vinavyosababisha maambukizi, kama vile bakteria. Kuachilia antibodi kuvuka kupitia kwenye plasenta hadi fetasi ni jambo la muhimu ili kukinga fetasi, na baadaye mtoto mzawa kutokana na viini hivi vinavyosababisha maambukizi.

Hata hivyo, plasenta haiwezi kuzuia alkoholi, baadhi ya dawa na virusi kuvuka hadi katika fetasi. Vitu hivi vinaweza kusababisha hitilafu za kuzaliwa, kama vile meno kugeuka rangi, hitilafu ya mifupa na kuharibika kwa ubongo. Ni muhimu kumshauri mama mjamzito kukomesha matumizi ya dawa zenye madhara na kuepukana na kemikali hatari. Ulijifunza mengi kuhusu maswala ya uhamasisho wa kiafya katika utunzaji wa wajawazito katika Kipindi cha 14.

5.4.4 Usanisi wa homoni katika plasenta

Plasenta ni ogani muhimu inayotoa homoni kwa muda mrefu wakati wa ujauzito. Plasenta hutoa gonadotropini za kikorioni za kibinadamu (GKK), ostrojeni na projestini. Uchunguzi wa kubaini ujauzito hutambua GKK katika mkojo wa mwanamke. Jukumu la homoni hizi ni kudumisha plasenta huku fetasi ikiendelea kukua, na kuzuia ovulesheni na muhula wa hedhi ili mwanamke asipate mimba tena hadi baada ya kuzaa.

Katika Kipindi kinachofuata, tutazingatia uhusiano ulio tofauti, kati ya anatomi ya fetasi na ya mama – miundo ya mifupa ya pelvisi ya mama na fuvu la fetasi.

Muhtasari wa Kipindi cha 5

Katika Kipindi cha 5 ulijifunza:

  1. Utungisho ni kuungana kwa seli ya uzazi ya kiume na za kike, mbegu ya kiume na ova, katika mishipa ya falopio.
  2. Mbegu za kiume zinaweza kusalia hai katika mfumo wa uzazi wa mwanamke kwa kipindi cha saa 72. Ova husalia hai kwa saa 12 hadi 24 tu. Ili utungusho ufanyike, ni sharti mbegu ya kiume ishushwe ukeni kwa kipindi kisichozidi siku tatu kabla ya ovulesheni, na kisichozidi saa 24 baada ya ovulesheni.
  3. Baada ya utungisho, seli hujigawa na kuunda hatua za embrio inayokua, zikiwemo morula (bonge la mviringo la seli) kisha blastosisti (mviringo wa seli wenye mwanya).
  4. Embrio hushuka kutoka katika falopio hadi uterasi kwa siku 5 -7.
  5. Embrio hupandikizwa katika endomitriamu (pembezoni) ya uterasi. Ikiwa itapandikizwa kwenye falopio, mimba ya kiektopi hutokea, na ni hatari sana kwa mwanamke.
  6. Eneo la trofoblasti ya blastosisti hupenya kwenye endomitriamu, na michomozo inayoitwa vili hutoa kemikali zinazoyeyusha mishipa ya damu ya mama. Damu ya mama hulowesha mishipa ya damu ya fetasi katika plasenta, kisha virutubishi, oksijeni na takamwili hubadilishanwa kati ya mama na fetasi.
  7. Damu ya mama na ya fetasi haichanganyiki katika plasenta.
  8. Plasenta hutenda kazi kama eneo la kusafirishia, kichungi cha kutenganisha dutu muhimu na hatari, na kiungo cha kutolesha homoni.

Maswali ya Kujitatmini ya Kipindi cha 5

Jitathmini jinsi ulivyojifunza kwa kujibu maswali haya. Andika majibu yako katika Shajara yako ya Masomo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi unaofuata. Unaweza kulinganisha majibu yako na maandishi kuhusu Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa moduli hii.

Swali la Kujitathmini 5.1 (linatathmini Malengo ya Somo 5.1, 5.2 na 5.3)

Kati ya maelezo yafuatayo, ni lipi lisilo sahihi? Katika kila kauli, eleza ni kwa nini si sahihi.

  • A.Nguvu zinzosongesha mkia wa mbegu ya kiume hutoka kwenye chembe za kijenetiki zilizo katika kichwa chake.
  • B.Mikazo katika misuli ya pembezoni mwa uterasi na mishipa ya falopio husaidia mbegu za kiume kusongea kuelekea kwenye ova.
  • C.Upandikizaji hutokea blastosisti inapoingia kwenye endomitriamu na kufanikiwa kuumba plasenta ya mwanzo.
  • D.Vena ya kiambakitovu husafirisha damu isiyo na oksijeni kutoka katika fetasi hadi plasenta.
  • E.Plasenta hufanya kazi kama kichungi kwa kuzuia dutu zote hatari kutoka kwa mwili wa mama hadi katika mfumo wa damu ya fetasi.
Answer

A si sahihi. Nguvu za kusongesha mkia wa mbegu za kiume hutoka kwenye mitokondria katika sehemu ya kati ya kichwa na mkia.

B ni sahihi. Mikazo katika misuli ya pembezoni mwa uterasi na mishipa ya falopio husaidia mbegu za kiume kusonga kwa kasi kuelekea kwenye ova.

C ni sahihi. Upandikizaji hutokea blastosisti inapoingia kwenye endomitriamu na kufanikiwa kuumba plasenta ya mwanzo.

D si sahihi. Vena ya kiambakitovu husafirisha damu yenye oksijeni kutoka kwa plasenta kurudi kwenye fetasi. Damu isiyo na oksijeni husafirishwa hadi kwenye plasenta na ateri mbili ya kiambakitovu.

E si sahihi. Plasenta haiwezi kuzuia kuvuka kwa dutu zote hatari kutoka kwa mwili wa mama hadi katika mfumo wa damu ya fetasi. Kwa mfano, pombe, dawa na kemikali zingine zinaweza kuvuka kupitia plasenta.

Mwisho wa jibu.

Swali la Kujitathmini 5.2 (linathmini Malengo ya Somo 5.2)

Soma Mfano 5.1 kisha uyajibu maswali yanayofuata.

Mfano 5.1 Ushauri kwa Bi. A baada ya kufanya ngono bila kinga.

Bi. A alifanya ngono bila kinga (bila kondomu) siku 17 baada ya siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho. Amekuja kituoni kubaini kama ametungika mimba.

Mweleze Bi. A uwezekano wake wa kutungika mimba kwa lugha anayoweza kuelewa.

Answer

Bi. A alifanya ngono bila kinga katika siku ya 18 ya muhula wake wa hedhi. Ovulesheni hutokea kwa wanawake wengi karibu siku ya 14, hivyo basi kuna uwezekano kuwa alifanya ngono katika siku tatu hadi nne baada ya ovulesheni. Ova husalia hai kwa saa 12 – 24 isipotungishwa. Kwa hivyo, ikiwa ovulesheni ilitokea kama inavyotarajiwa katika siku ya 14, basi hakuna uwezekano kuwa ova ilikuwa hai siku ya 18 alipofanya ngono. Hivyo basi, hakuna uwezekano kuwa ana mimba kwa wakati huu. Hata hivyo, ikiwa ovulesheni yake ilitokea ikiwa imechelewa, kuna uwezekano ametungika mimba. Mshauri kuhusu hatari za kufanya ngono bila kinga: yaani mimba isiyotakikana na maambukizo ya zinaa.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 5.3 (linatathmini Malengo ya Somio 5.3)

Soma Mfano 5.2 kuhusu Bi. P, kisha uyajibu maswali yanayofuata.

Mfano 5.2 Bi. P anataka kujua jinsi pombe na miraa inavyoweza kudhuru fetasi yake

Bi P ni mwanamke mjamzito wa umri wa miaka 38 aliye na uraibu wa pombe na kutafuna miraa. Alizuru kituo chako kuhudhuria Kipindi cha elimu ya afya kwa wajawazito kabla ya kuzaa. Alisikiliza ukieleza kuwa damu ya fetasi na ya mama haiguzani moja kwa moja. Baada ya mazungumzo, alikuuliza, “ Kwa nini unaniambia nikomeshe kunywa pombe na kutafuna miraa ikiwa damu yangu haiguzani moja kwa moja na damu ya mtoto wangu? Ikiwa damu yangu haiguzani na ya mtoto, basi pombe na miraa haiwezi kumfikia mtoto.”

Jibu lako ni nini? Mweleze kwa lugha anayoweza kuelewa.

Answer

Unapaswa kumwelezea Bi P kuwa ingawa damu yake haiguzani moja kwa moja na ya mtoto wake, damu yake na ya mtoto imepakana kwa karibu katika plasenta. Ni wembamba wa mishipa ya damu ya mtoto tu unaowagawanya. Kuta hizi za mishipa ni nyembamba sana hivi kwamba vidutu vidogo kama vya pombe na miraa vinaweza kuvukia kutoka damu yake hadi ya mtoto. Mfahamishe kuwa utaratibu huo ndio unaotumika kupitisha dutu muhimu kama oksijeni na virutubishi kutoka kwa damu yake hadi ya mtoto. Hivyo basi, kudumisha afya njema na kula chakula tosha ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto. Akikomesha kunywa pombe na kutafuna miraa, mtoto wake atakuwa na afya njema zaidi. Akiendelea kutumia vitu hatari, mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na hitilafu au hata afe.

Mwisho wa jibu.