Skip to main content
Printable page generated Monday, 28 Nov 2022, 02:11
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2022 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Monday, 28 Nov 2022, 02:11

6. Maumbile ya Pelvisi ya Mwanamke na Fuvu la Fetasi

Kipindi cha 6 Maumbile ya Pelvisi ya Mwanamke na Fuvu la Fetasi

Utangulizi

Katika Kipindi hiki, utajifunza kuhusu miundo ya kimifupa iliyo mihumu zaidi katika mwanamke mjamzito na mtoto atakayemzaa. Kazi kuu ya mifupa ya kiunzi ni kuegemeza uzito wa mwili na kutenda kazi kama sehemu za kuunganisha misuli. Lengo la somo hili ni kuhusu pelvisi ya mwanamke, ambayo huegemeza sehemu kubwa ya uzito wa uterasi inayobeba mimba, na fuvu la fetasi, ambalo ni sharti lipitie katika pelvisi ya mwanamke anapozaa.

Kuna sehemu kuu mahususi katika maumbile ya pelvisi ya mwanamke na fuvu la fetasi ambazo tutakuonyesha katika Kipindi hiki. Kufahamu sehemu hizi kuu kutakuwezesha kukadiria jinsi leba inavyoendelea, kwa kutambua mabadiliko katika hali zake linganifu huku mtoto akishukia katika njia ya uzazi. (Utajifunza kuhusu haya yote katika Moduli inayofuata ya Leba na Utunzaji wakati wa Kuzaa.)

Malengo ya Somo la Kipindi cha 6

Baada ya kipindi hiki, unapaswa kuwa na uwezo wa:

6.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Maswali ya Kujitathmini 6.1, 6.2 na 6.3)

6.2 Kueleza kuhusu pelvisi ya mwanamke na kutambua sifa muhimu za utunzaji wa kiukunga. (Maswali ya Kujitathmini 6.1, 6.2 na 6.3)

6.3 Kueleza sifa kuu za fuvu la fetasi na umuhimu wa sifa hizi katika leba na kuzaa. (Maswali ya Kujitathmini 6.1, 6.2 na 6.3)

6.1 Pelvisi ya mwanamke iliyo ya kimfupa

Pelvisi ni duara gumu la mifupa (tazama Mchoro 6.1), ambayo huegemeza na kukinga viungo vya pelvisi na viungo vilivyo ndani ya uwazi wa fumbatio. Misuli ya miguu, mgongo na fumbatio hushikilia pelvisi. Nguvu na uwezo wa misuli hii huufanya mwili kusimama wima na kuuwezesha kuinama na kupindika kiunoni, na pia kutembea na kukimbia.

Mchoro 6.1 Mifupa ya pelvisi ya mwanamke.

Pelvisi ya mwanamke imeumbwa kuhimili utaratibu wa kuzaa, na ina umbo bapa na pana zaidi kuzidi pelvisi ya mwanaume. Pelvisi hii ina jozi la mifupa iliyoungana kwa nguvu sana hivi kwamba ni vigumu kuona viunga hivi. Tutaeleza kila mojawapo ya mifupa hii na sifa zake kuu. Maelezo haya yatakuwezesha kufahamu kimawazo maumbile ya pelvisi iwapo utazidi kurejelea Mchoro 6.1.

6.1.1 Iliamu

Iliamu hutamkwa kama ‘il-a-mu’

Sehemu kuu ya pelvisi imeundwa kwa mifupa miwili, kila mojawapo ikiitwa iliamu - mfupa mmoja katika kila upande wa uti wa mgongo (au safu ya uti) kisha kupindika kuelekea upande wa mbele wa mwili. Ukiweka mkono wako kwenye kiuno kimoja, utakuwa umeshika kilele cha iliamu, ambao ni mpaka wa juu wa iliamu katika upande huo ulioshika. Katika sehemu ya mbele ya kilele cha iliamu, unaweza kushika na kuhisi chomozo la kimfupa liitwalo uti wa juu wa mbele wa iliamu (’chomozo’ ni kitu kinachobenuka nje, kama vile mlima au nundu).

 • Je, istilahi ya kimaelekezo ‘juu’ na ‘mbele’ yanatufahamisha nini kuhusu nafasi ya nyuti za iliamu? (Iwapo hukumbuki, rejelea Jedwali 3.1 katika Kipindi cha 3.)

 • ‘Mbele’ humaanisha kuwa nyuti za iliamu ziko katika sehemu ya mbele ya mwili. ‘Juu’ inaashiria kuwa nyuti hizi ziko juu ya sehemu kuu ya iliamu katika kila upande.

  Mwisho wa jibu

6.1.2 Iskiamu

Iskiamu ndiyo sehemu ya chini nene ya pelvisi iliyoundwa kwa mifupa miwili iliyoungana - mfupa mmoja katika kila upande. Mwanamke anapokuwa katika leba, mshuko wa kichwa cha fetasi inaposhukia katika njia ya uzazi hukadiriwa kwa kulinganishwa na nyuti za iskiamu, ambazo ni chomozo za iskiamu zinazoelekea ndani katika kila upande. Nyuti za iskiamu ni ndogo zaidi na za umbo la duara zaidi katika pelvisi ya mwanamke kushinda ile ya mwanaume. Katika Moduli ya Leba na Utunzaji wa wakati wa Kuzaa, utajifunza jinsi ya kuhisi nyuti za iskiamu ili kukuwezesha kukadiria jinsi kichwa cha fetasi kilivyoshuka katika njia ya uzazi.

Iskiamu hutamkwa kama ‘is-ki-amu’

6.1.3 Mifupa ya kinena na simfisisi ya kinena

Mifupa ya kinena katika kila upande huunda sehemu moja ya pelvisi. Mifupa yote miwili ya kinena huungana kwenye simfisisi ya kinena. (Simfisisi ni kiunga imara sana.) Simfisisi ya kinena iko punde chini ya kifusi kilichofunikwa kwa nywele ambacho hukinga sehemu za nje za uke (kama ilivyoonyeshwa kwenye Mchoro 3.2, iwapo utahitaji kukirejelea).

Kuhisi sehemu ya juu ya simfisisi la kinena ni hatua muhimu sana unapolichunguza fumbatio la mwanamke mjamzito. Katika Kipindi cha 10, utajifunza jinsi ya kukadiria urefu wa uterasi kutoka kwenye simfisisi ya kinena hadi kwenye fandasi (sehemu ya juu ya uterasi - tazama Mchoro 3.3 iwapo utahitaji kujikumbusha kuhusu nafasi ya fandasi. Vipimo hivi vitakusaidia kukadiria kipindi cha ujauzito, yaani, idadi ya wiki ambazo ujauzito huu umechukua, na iwapo fetasi hii inakua kwa kiwango cha kawaida.

6.1.4 Sakramu

Sakramu hutamkwa kama ‘sa-kra-mu’. Kokisiksi hutamkwa kama ‘koki siksi’.

Sakramu ni mfupa mrefu, wenye umbo la kabari ulio nyuma ya pelvisi, ambao una vetebra tano zilizoshikana (mifupa midogo inayounda safu ya uti wa mgongo au uti wa mgongo). Chini ya sakramu ni chomozo la kimfupa linalofanana na mkia liitwalo kokisiksi. Mpaka wa juu wa vetebra ya kwanza katika sakramu huchomoza na kuelekea upande wa mbele ya mwili. Chomozo hili ni promontori ya sakramu - ambayo ni sehemu muhimu katika leba.

6.2 Njia ya pelvisi

Uwazi mgumu wa duara uliofunikwa na mfupa wa kinena upande wa mbele na iskiamu wa nyuma, huitwa njia ya pelvisi - uwazi wa mifupa ambao mtoto hupitia. Njia hii ina umbo lililopindika kwa sababu ya tofauti ya ukubwa kati ya mipaka ya mbele na ya nyuma ya uwazi ulioachwa na mifupa ya pelvisi. Unaweza kuiona njia hii kutoka mtazamo wa upande kwenye Mchoro 6.2.

Mchoro 6.2 Njia ya pelvisi ikitazamwa kutoka upande mmoja, huku mwili ukielekea upande wa kushoto.

6.2.1 Ukubwa na umbo la pelvisi

Ukubwa na umbo la pelvisi ni muhimu katika leba na kuzaa. Wanawake wenye nguvu na afya nzuri, waliotumia lishe bora katika kipindi chao cha kukua cha utotoni, kwa kawaida huwa na pelvisi pana iliyoumbika vyema kumpitisha mtoto wakati wa kuzaa. Pelvisi ina ukingo wa duara na nyuti fupi, butu,za iskiamu. (Madaktari na wakunga huliita umbo hili pelvisi ya ‘jinaesidi’.) Sehemu hii hupelekea matatizo machache zaidi wakati wa kuzaa, almuradi fetasi ina ukubwa wa kawaida na njia ya uzazi haina ukuaji wa tishu zisizo za kawaida zinazozuia utaratibu wa kuzaa.

Kuna tofauti kubwa kati ya maumbo mbali mbali ya pelvisi, ambapo baadhi yake husababisha matatizo katika leba na kuzaa. Pelvisi nyembamba inaweza kupelekea ugumu wa mtoto kupitia katika njia ya pelvisi. Ukosefu wa madini muhimu kama iodini katika chakula wakati wa utotoni unaweza kusababisha matatizo ya ukuaji wa pelvisi. Kudumaa (kuwa mfupi kuliko wastani ikilinganishwa na umri) kwa sababu ya lishe bovu na/au magonjwa ya kuambukiza kunaweza pia kupelekea pelvisi nyembamba.

Pili, tutatazama umbo la njia ya pelvisi kwa kina, kisha tutofautishe kati ya kiingilizi cha pelvisi (uwazi mgumu wa umbo la duara ambapo kichwa cha mtoto huingia katika pelvisi - Mchoro 6.3), na kitokezi cha pelvisi (uwazi mgumu wa umbo la duara ambapo kichwa cha mtoto hutokea nje ya pelvisi. Kama utakavyoona katika kifungu kinachofuatia, kiingilizi na kitokezi cha pelvisi hazina usawa wa ukubwa.

6.2.2 Kiingilizi cha pelvisi

Kiingilizi cha pelvisi kimeundwa kwa ukingo wa pelvisi, kama ulivyoona katika Mchoro 6.1. Ukingo wa pelvisi ni wa duara isipokuwa sehemu ambapo promontari ya sakramu na nyuti za iskiamu huchomozea ndani ya pelvisi hii. Ukubwa wa kiingilizi cha pelvisi kwa sentimita; umeonyeshwa katika Mchoro 6.3 kutoka pande zote (juu hadi chini; na kwa kukingama au upande hadi upande). Ukitazama Mchoro 6.3, chukulia kuwa wewe ni mtoto aliye katika kichwa kuinama, huku ukitazama chini kwenye pelvisi kutoka upande wa juu, katika na nafasi unayofaa kujifinyilia ili upite! Nafasi hii ni ya upana wa sentimita 13 tu (kwa wastani) na sentimita 12 kutoka chini.

Mchoro 6.3 Vipenyo vya kiingilizi cha pelvisi, kwa kutazamwa kutoka juu.

6.2.3 Kitokezi cha pelvisi

Kitokezi cha pelvisi kimeundwa kwa mpaka wa chini wa mifupa ya kinena upande wa mbele na mpaka wa chini wa sakramu upande wa nyuma. Nyuti za iskiamu zimechomoza kuelekea pande zote mbili. Mchoro 6.4 kinaonyesha ukubwa wa nafasi ambayo ni sharti fetasi kupitia inapotoka katika pelvisi la mama. Unapotazama Mchoro 6.4, chukulia kuwa wewe ni mkunga anayetazama juu katika njia ya uzazi huku ukingonjea fetasi ichomoze kichwa.

Mchoro 6.4 Kipenyo cha kiingilizi cha pelvisi kikiangaliwa kutoka upande wa chini.
 • Je, unatambua nini unapolinganisha ukubwa wa kiingilizi cha pelvisi (Mchoro 6.3) na kitokezi cha pelvisi (Mchoro 6.4)? Ni gani nyembamba zaidi kati ya milango hii miwili?

 • Kipenyo chembamba zaidi cha kuiwezesha fetasi kupitia ni kitokezi cha pelvisi ambacho kina upana wa sentimita 11 pekee katika pelvisi ya mwanamke ya wastani.

  Mwisho wa jibu

Ni vigumu kutambua kutoka Mchoro 6.3 na 6.4, lakini ni sharti fetasi izunguke ili iweze kupitia katika njia ya pelvisi. Hii ni kwa sababu kiingilizi cha pelvisi ni sentimita 13 kwa upana ilhali kitokezi cha pelvisi ni sentimita 11 pekee kwa upana. Ili iweze kutoshea katika kitokezi cha pelvisi katika sehemu pana zaidi (sentimita 12.5 kutoka juu hadi chini), ni sharti fetasi izunguke ili iweze ’kutanguliza' kichwa chake kwenye upande ule mpana zaidi wa njia ya pelvisi katika kila sehemu wakati inapopita. Fuvu ndiyo sehemu iliyo kubwa zaidi ya fetasi, hivyo kichwa cha fetasi huzunguka kwanza, kisha mabega, halafu sehemu ya mwili iliyobakia kutanguliza. Utajifunza haya yote katika Moduli ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa. Kwanza, hebu tuutazame vyema muundo wa fuvu la fetasi.

6.3 Fuvu la fetasi

Fuvu la fetasi ndiyo sehemu iliyo na ugumu kupitia katika njia ya pelvisi ya mama kwa sababu imeundwa kwa mifupa. Kuelewa maumbile ya fuvu la kichwa na upenyo wake kutakusaidia kutambua jinsi leba unavyoendelea na ikiwa kichwa cha mtoto ‘kinatanguliza’ ifaavyo anaposhuka katika njia ya uzazi. Hii itakusaidia kuelewa ikiwa itawezekana mama ajifungue kwa njia ya kawaida au mama atahitaji rufaa kwa sababu mtoto hashuki ifaavyo.

6.3.1 Mifupa ya fuvu la fetasi

Mifupa ya fuvu hufunga na kukinga ubongo, ambao ni laini sana na unaweza kupata shinikizo wakati kichwa cha fetasi kinashuka katika njia ya uzazi. Kutanguliza kipenyo cha fuvu la fetasi katika kipenyo kikubwa zaidi cha pelvisi ya mama ni muhimu sana ikiwa ataendelea kuzaa kwa kawaida. Ikiwa kipenyo cha fuvu linalotanguliza ni kipana zaidi ya kile cha pelvisi ya mama, itahitaji uangalifu mkuu sana ili mtoto azaliwe kwa njia ya kawaida ya uke.

Unaweza kutazama mifupa mikuu ya fuvu katika Mchoro 6.5.

Mchoro 6.5 Mifupa ya fuvu la fetasi - kwa mtazamo wa kutoka kushoto.

Mifupa ya fuvu la fetasi ni kama ifuatavyo:

 • Mfupa wa mbele, unaounda paji la uso. Katika fetasi, mfupa wa mbele uko katika nusu mbili, ambazo huungana na kuwa mfupa mmoja baada ya umri wa miaka 8.
 • Mifupa miwili ya parieta, ambayo huwa katika pande zote mbili za fuvu huchukua takriban nafasi yote ya fuvu.

Parieta hutamkwa kama ‘pa-ri-eta’.

 • Mfupa wa oksipitasi, unaounda sehemu ya nyuma ya fuvu na pia sehemu ya msingi wake. Mfupa huu huungana na vetebra ya seviksi (mifupa ya shingo katika safu ya uti wa mgongo, au uti wa mgongo).
 • Mifupa miwili ya panja, mmoja katika kila upande wa kichwa, iliyo karibu zaidi na sikio.

Kuelewa sehemu muhimu na vipimo vya fuvu la fetasi kutakusaidia kutambua tangulizi za kawaida na zisizo za kawaida za fetasi wakati wa uchunguzi wa kabla ya kuzaa, leba na kuzaa.

6.3.2 Sucha

Sucha ni viunga vilivyo katikati ya mifupa ya fuvu. Katika fetasi, sucha hizi zinaweza 'kubonyeka' kidogo chini ya shinikizo kwenye kichwa cha mtoto anaposhukia kwenye njia ya uzazi. Mwanzoni mwa utotoni, sucha hizi huwa gumu na mifupa ya fuvu haiwezi kusonga ikilinganishwa na kila moja wake, jinsi inavyosonga ingawa kwa kiasi kidogo katika fetasi au mtoto mzawa. Katika masomo ya ukunga, ni jambo la kidesturi kufunza majina na maeneo ya mifupa hii. Unaweza kutambua pembenukta ya kichwa cha mtoto 'anapotanguliza' katika njia ya uzazi kwa kuhisi zilipo sucha kuu kwa vipimo vya vidole vyako. Unaweza kuona mahali zilipo sucha katika fuvu la fetasi katika Mchoro 6.6, na pia vipenyo vyake katika ncha mbili.

Sucha hutamkwa kama ‘su-cha’.

Mchoro 6.6 Maeneo na sehemu muhimu kwenye fuvu la fetasi zikielekea upande wa kushoto, kama zinavyoonekana kutoka juu. Makinika kuhusu vipenyo wastani vilivyoonyeshwa kwa rangi nyekundu.
 • Sucha la lamdoidi huunda muungano kati ya mfupa wa oksipitasi na mfupa wa paji.

Lamdoidi hutamkwa kama ‘lam doidi’. Sagita ni ‘sa-ji-ta’ ilhali korona ni ‘ko-ro-na’.

 • Sucha ya sajita huunganisha mifupa miwili ya parieta.
 • Sucha ya korona huunganisha mfupa wa paji na mifupa miwili ya parieta.
 • Sucha ya paji huunganisha mifupa yote miwili ya paji.
 • Unatambua nini kuhusu vipenyo vilivyopeanwa katika Mchoro 6.6, ukilinganisha na ukubwa wa njia ya pelvisi (Mchoro 6.3 na 6.4)?

 • Katika sehemu pana zaidi, fuvu la fetasi lina upana wa sentimita 9.5 (kwa wastani). Hii ni sentimita 3.5 chache zaidi kuliko kipenyo kipana zaidi cha kiingilizi cha pelvisi na sentimita 1.5 chache zaidi kuliko kipenyo kipana zaidi cha kitokezi cha pelvisi.

  Mwisho wa jibu

Hii ni kumaanisha, ikiwa pelvisi ya mama na fuvu la fetasi ni vya ukubwa wa wastani, kuna nafasi ya kutosha ya kichwa cha mtoto kupitia katika njia ya pelvisi ikiwa kichwa kitazunguka ili kutokea katika eneo kubwa zaidi la pelvisi.

6.3.3 Fontaneli

Fontaneli ni nafasi inayoundwa sucha mbili au zaidi zinapoungana. Fontaneli huwa imefunikwa kwa tando nene na ngozi ya kichwa cha mtoto, huku ikiukinga ubongo ulio chini yake ili usipate mathara kutoka nje. Kutambua fontaneli mbili kubwa juu ya fuvu la fetasi husaidia kujua pembenukta ambayo kichwa cha mtoto kinatanguzia wakati wa leba na kuzaa. Fontaneli zinaonyeshwa katika Mchoro 6.5 na 6.6. Fontaneli hizi ni:

 • Fontaneli ya mbele (pia inayojulikana kama bregma) ni nafasi yenye umbo la almasi inayoelekea katika sehemu ya mbele ya kichwa cha mtoto katika muungano wa sucha za sajita, korona na paji. Fontaneli hii ni laini sana na unaweza kuhisi mpigo wa moyo wa fetasi kwa kuviweka vidole vyako taratibu juu ya fontaneli hizi. Ngozi iliyo juu ya fontaneli inaweza kuonekana 'ikidunda' katika mtoto mzawa au mtoto mchanga.
 • Fontaneli ya nyuma (au lamda) ina umbo la pembetatu, na inapatikana kuelekea nyuma ya fuvu la fetasi. Fontaneli hii imeundwa kufuatia muungano wa lamdoidi na sucha za sajita.

6.3.4 Maeneo na sehemu muhimu katika fuvu la fetasi

Vielelezo 6.5 na 6.6 vinakuwezesha kutambua maeneo maalum na sehemu muhimu katika fuvu la fetasi, ambazo zina umuhimu maalum katika utunzaji wa kiukunga. Hii ni kwa sababu zinaweza kuunda sehemu maarufu kama sehemu tangulizi ya fetasi - ambayo ni sehemu inayoelekea chini ya njia ya uzazi.

 • Veteksi ni eneo la katikati ya fontenali ya mbele, mifupa miwili ya parieta na fontenali ya nyuma. Utangulizi wa veteksi hutokea wakati sehemu hii ya fuvu la fetasi inatangulia. Hii ndiyo njia ya kawaida na iliyo salama zaidi ya utangulizi wakati wa kuzaa kwa njia ya uke.
 • Paji ni eneo la fuvu linalotandaza kutoka fontaneli ya mbele hadi kwenye mpaka wa juu ya macho. Utangulizi wa paji ni hatari kubwa kwa mama na mtoto.
 • Uso hutandaza kutoka tuta la juu ya macho hadi kwenye pua na kidevu (kitaya cha chini). Utangulizi wa uso pia ni hatari kubwa kwa mama na mtoto.
 • Osiputi ni eneo la katikati mwa msingi wa fuvu na fontenali ya nyuma. Ni jambo lisilo la kawaida na hatari sana kwa osiputi kuwa sehemu inayotanguliza.

Utakaposoma moduli inayofuatia ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa, utajifunza kuhusu tangulizi za aina nyingine ikiwemo 'kutanguliza matako' (kichwa cha mtoto kinapoelekea juu na miguu yake au matako ndiyo sehemu inayotangulia), na 'bega' kwanza.

Kwa kuwa umejua sehemu kuu maumbile ya mfumo wa uzazi mwanamke, pelvisi ya mwanamke na fuvu la fetasi, sasa tuende katika Kipindi cha 7 ili tuweze kutazama mabadiliko makuu ya kifiziolojia yanayotokea katika mwili wa mwanamke wakati yu mjamzito.

Muhtasari wa Kipindi cha 6

Katika Kipindi cha 6 umejifunza kwamba:

 1. Mifupa ya pelvisi ni pamoja na iliamu, isikiamu, mifupa ya kinena, na sakramu.
 2. Ukubwa na umbo la pelvisi linaweza kuathiri urahisi au ugumu wa leba na kuzaa. Pelvisi pana hurahisisha kuzaa kuliko pelvisa nyembamba, ambayo inaweza kuzuia kushuka kwa mtoto katika njia ya kuzaa.
 3. Sehemu mahususi ambazo ni muhimu za maumbile ya pelvisi hutumika mara nyingi kukadiria jinsi mtoto alivyshuka wakati wa leba na kuzaa. Sehemu mbili zilizo muhimu zaidi ni nyuti za iskiamu na promontari ya iskiamu, ambayo inaweza kuhisika kwa vidole wakati wa kuchunguza uke.
 4. Kiingilizi cha pelvisi ni nafasi ambayo kichwa cha mtoto huingilia pelvisi. Mlango huu wa pelvisi ni mkubwa kuliko kitokezi cha pelvisi ambapo kichwa cha mtoto hutokea. Mtoto hulazimika kuzunguka anapopitia kwenye njia ya pelvisi, ili kuhakikisha amepata kipenyo kikubwa cha kiingilizi na kitokezi cha pelvisi.
 5. Fuvu la kichwa limeundwa kwa mifupa mingi iliyounganishwa na viunga viitwavyo sucha. Katika fetasi na mtoto mzawa, nafasi ziitwazo fontaneli ziko kati ya baadhi ya mifupa ya fuvu iliyo juu ya kichwa cha mtoto. Nafasi ya sucha na fontaneli inaweza kubainisha kuhusu pembenukta ya kutokeza kwa kichwa cha mtoto wakati wa leba na kuzaa.
 6. Kutanguliza veteksi (ambapo sehemu ya juu ya kichwa cha mtoto hutangulia) ni hali ya kawaida na salama zaidi katika uzazi wa kawaida wa kupitia uke. Hali zingine za kutanguliza huwa hatari zaidi kwa mama na mtoto.

Maswali ya Kujitathmini (MK) ya Kipindi cha 6

Kwa kuwa sasa umekamilisha Kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili kubaini jinsi ulivyotimiza Malengo ya Masomo ya Kipindi hiki. Andika majibu yako katika shajara yako ya masomo na uyajadili na mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi wa Somo unaofuata. Unaweza kudhibitisha majibu yako ukilinganisha na vidokezo ulivyoandika katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 6.1 (linatathmini Malengo ya Somo 6.1, 6.2 na 6.3)

Linganisha kila jina la kimaumbile na maelezo yaliyo sahihi.

Using the following two lists, match each numbered item with the correct letter.

 1. Mfupa wa nyonga katika pelvisi

 2. Jozi la mifupa linalounda sehemu ya mbele ya fuvu

 3. Viunga vilivyo kati ya mifupa ya parieta katika fuvu la fetasi.

 4. Vetebra zilizoungana za mgongo zilizo nyuma ya pelvisi

 5. Sehemu ya juu ya fuvu la fetasi katikati ya fontaneli mbili

 • a.Iliamu

 • b.Veteksi

 • c.Sakramu

 • d.Mifupa ya paji

 • e.Sucha wa sajita

The correct answers are:
 • 1 = a
 • 2 = d
 • 3 = e
 • 4 = c
 • 5 = b

Swali la Kujitathmini 6.2 (linatathmini Malengo ya Somo 6.1, 6.2 na 6.3)

Ni elezo lipi ambalo si kweli?? Katika kila kauli, eleza ni kwa nini sio sahihi.

 • A.Mifupa ya pelvisi ya mwanamke ni pana na bapa kuzidi ile ya mwanaume.
 • B.Kiingilizi cha pelvisi ni kidogo kuzidi kitokezi.
 • C.Ncha ya iliamu ni sehemu muhimu ya maumbile ya kubaini jinsi fetasi inavyoshukia ukeni.
 • D.Sucha katika fuvu la fetasi ni viunga vigumu na thabiti ambavyo hushikamanisha mifupa ya fuvu.
 • E.Mpwito wa mtoto mzawa unaweza kuonekana ikidunda katika fontaneli ya mbele.
Answer

A ni kweli Mifupa ya pelvisi ya mwanamke ni pana na bapa zaida ya ile ya mwanaume.

B si kweli. Kiingilizi cha pelvisi ni kipana (wala si chembamba) kuliko kitokezi.

C si kweli. Kilele cha iliamu ni chomozo lililo katika sehemu ya mbele ya mfupa wa kiuno. Kilele cha iliamu si sehemu muhimu ya kubaini jinsi fetasi inavyoshukia ukeni.

D si kweli. Sucha katika fuvu la kichwa cha fetasi ’hubonyea' kidogo kufuatia shinikizo la uke, hivyo mifupa ya fuvu la kichwa inaweza kuchezacheza kidogo. Jambo hili hufanya kichwa cha mtoto kupitia katika pelvisi ya mama kwa urahisi.

E ni kweli. Mpwito wa mtoto mzawa unaweza kuonekana ukidunda katika fontaneli ya mbele.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 6.3 (linatathmini Malengo ya Somo 6.1, 6.2 na 6.3)

Orodhesha sifa 4 zinazoweza kuwa za pelvisi na/au fuvu la fetasi ambazo zinaweza kutatiza leba au kuzaa.

Answer

Sifa za pelvisi na/au fuvu la fetasi zinazoweza kutatiza leba au kuzaa ni pamoja na (unafaa kutaja nne tu):

 • Pelvisi nyembamba au iliyoumbuka
 • Ukuaji wa tishu usio wa kawaida katika uwasi wa pelvisi
 • Fuvu kubwa la fetasi.
 • Fetasi kutanguliza paji, uso, matako au mabega.
 • Fetasi ambayo haiwezi kutanguliza sehemu pana zaidi la fuvu lake katika sehemu pana zaidi ya kiingilizi cha pelvisi, kisha kuzunguka na kufanya vivyo hivyo katika kitokezi.

Mwisho wa jibu