Skip to main content
Printable page generated Friday, 26 April 2024, 12:27 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Friday, 26 April 2024, 12:27 AM

7. Mabadiliko ya Kifiziolojia katika Ujauzito

Kipindi cha 7 Mabadiliko ya Kifiziolojia katika Ujauzito

Utangulizi

Wakati wa ujauzito, mwili wa mwanamke hubadilika kwa njia mbalimbali kufuatia athari za homoni. Wakati mwingine mabadiliko haya huwa sumbufu, lakini mara nyingi ni mabadiliko ya kawaida ambayo humwezesha mwanamke kulisha na kulinda fetasi, kuandalia mwili wake na kuandalia matiti yake ili yaweze kutoa maziwa.

  • Je, unakumbuka fasili ya homoni katika Kipindi cha 3?

  • Homoni ni kemikali ashirizi zinazozalishwa mwilini, ambazo husafirishwa katika damu. Homoni mbalimbali hudhibiti au kurekebisha utendakazi wa seli au viungo tofauti.

    Mwisho wa jibu

Katika Kipindi hiki, utajifunza kuhusu baadhi ya mabadiliko yanayotokea wakati wa ujauzito katika uterasi, seviksi na uke, mfumo wa moyo na mishipa ya damu, mfumo wa tumbo na utumbo mdogo na mfumo wa mkojo, na pia kuhusu mabadiliko kwenye matiti na ngozi. Pia utajifunza kuhusu madhara ya mabadiliko haya yote kama utavyohitaji kufahamu kama mhudumu wa afya anayeshughulikia afya ya wajawazito. Kwa kuelewa mabadiliko ya kawaida ya ujauzito, unaweza kumhakikishia mwanamke ikiwa ana wasi wasi, na pia kumchunguza na kumhudumia kwa haraka zaidi ikiwa utagundua chochote kisicho kawaida. Elimu ya kimsingi ya mabadiliko na virekebishi hivi pia ni muhimu katika kuelewa Malengo ya uchunguzi wa kimaabara unaoweza kufanywa katika kituo cha afya katika kipindi cha ujauzito.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 7

Baada ya kuhitimisha somo hili, unapaswa kuwa na uwezo wa:

7.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito.(Swali la Kujitathmini 7.6 )

7.2 Kueleza mabadiliko ya kifiziolojia ya mfumo wa uzazi wa mwanamke wakati wa ujauzito na athari za mabadiliko haya kwa mwanamke huyu mjamzito. (Maswali ya Kujitathmini 7.1 na 7.6)

7.3 Kueleza mabadiliko wastani ya uzito wa mwili wa mwanamke mjamzito. (Swali la Kujitathmini 7.2)

7.4 Kujadili kuhusu mabadiliko katika mfumo wa moyo na mishipa wakati wa ujauzito, na athari ya shinikizo la damu, utendakazi wa moyo, kiasi cha damu na ukolezi wa seli nyekundu za damu. (Maswali ya Kujitathmini 7.3, 7.4 na 7.6)

7.5 Kubaini mabadiliko ya kawaida na yasio ya kawaida katika mifumo ya pumzi, umeng’enyaji, na mkojo; na pia ngozi, na matiti, ikiwemo utoleshaji wa kolostramu. (Maswali ya Kujitathmini 7.5 na 7.6)

7.1 Mabadiliko ya kifiziolojia katika mfumo wa uzazi wa mwanamke wakati wa ujauzito

7.1.1 Mabadiliko katika estrojeni na projesteroni

Katika Kipindi cha 3, 4 na 5 ulijifunza kuhusu homoni kuu za mfumo wa uzazi wa mwanamke, estrojeni na projesteroni, na utendakazi wa homoni hizi katika kuandaa uterasi kudhibiti ujauzito. Vile vile, estrojeni na projesteroni ni homoni kuu katika kipindi chote cha ujauzito.

Mwanamke hutoa estrojeni nyingi wakati wa ujauzito kuliko wakati wowote maishani akiwa hana mimba. Wakati wa ujauzito, estrojeni huimarisha usafirishaji wa damu ya mama ndani ya uterasi na plasenta.

  • Je, estrojeni ina jukumu gani muhimu katika ukuaji wa fetasi?

  • Kwa kuimarisha usafirishaji wa damu ya mama katika uterasi na plasenta, estrojeni huhakikisha kuwa fetasi imesambaziwa virutubishi na oksijeni ili ikue, na kwamba takamwili la fetasi limetolewa kwenye damu ya mama. (Ulijifunza haya katika Kipindi cha 5.)

    Mwisho wa jibu

Pia kiwango cha projesteroni katika mwanamke mjamzito huwa cha juu sana. Miongoni mwa athari zingine, viwango vya juu vya projesteroni husababisha ukubwa wa baadhi ya viungo vya ndani ya mwili kuongezeka, ikiwa ni pamoja na uterasi, ili iweze kubeba mtoto aliyehitimu muhula wote wa ujauzito. Kiwango hiki pia kina athari zingine kwa mishipa ya damu na jointi, ambazo tutajadili baadaye katika Kipindi hiki.

7.1.2 Mabadiliko kwenye uterasi, seviksi na uke

Uterasi

Baada ya utungisho, uterasi hutoa mandhari yenye lishe na kinga ambapo fetasi itaweza kukua na kustawi. Uterasi huongezeka kutoka ukubwa sawa na wa pea ndogo wakati mwanamke hana mimba hadi iweze kubeba mtoto aliyehitimu muhula wote wa ujauzito katika wiki 40 za kipindi cha ujauzito. Tishu ambazo hutumika kuunda uterasi huendelea kukua kwa wiki 20 za kwanza na kuongezeka kwa uzito kutoka takriban gramu 50 - 1,000. Baada ya kipindi hiki, uterasi huwa haiongezeki kwa uzito, lakini itajivuta ili kumpa nafasi mtoto anayekua, plasenta na viowevu vya amniotiki. Ujauzito unapohitimisha mwisho wa muhula wake, uterasi itakuwa imeongezeka kwa ukubwa kwa takriban mara tano kuliko ukubwa wake wa kawaida:

  • Kwa urefu (juu hadi chini) kutoka sentimita 7.5 hadi 30.
  • Kwa upana (upande hadi upande) kutoka sentimita 5 hadi 23
  • Kwa urefu (mbele hadi nyuma) kutoka sentimita 2.5 hadi 20.
  • Ni nini husababisha mabadiliko haya?

  • Homoni ya projesteroni hasa husababisha mabadiliko haya.

    Mwisho wa jibu

Katika wiki ya 12 ya ujauzito (karibu mwisho wa trimesta ya kwanza ya ujauzito, yaani kipindi cha miezi mitatu) fandasi (pembeni mwa juu ya mwili wa uterasi) inaweza kupapasika (kuhisika) kupitia fumbatio, juu ya mfupa wa kinena (simfisisi ya kinena). Kwa kawaida, ukubwa wa uterasi hufikia kilele chake baada ya takriban wiki 36 za ujauzito (tazama Mchoro 7.1).

Mchoro 7.1 Urefu wa uterasi katika wiki mbalimbali za ujauzito.
  • Je, ni baada ya wiki ngapi za ujauzito ambapo fandasi ya uterasi inaweza kupapasika katika urefu wa kitovu (kitufe cha fumbatio) cha mwanamke, kulingana na Mchoro 7.1?

  • Kwa takriban wiki 20.

    Mwisho wa jibu

Kichwa cha fetasi kinapojitandaza kwenye pelvisi kwa maandalizi ya kuzaliwa, uterasi inaweza kushuka kidogo. Makinika kuhusu hali ya fetasi katika wiki 40, ambapo imeonyeshwa kwa alama ya mstari wa vitone kwenye Mchoro 7.1. Kushuka huku hujulikana kama 'kuwepesuka'. Hali hii huonekana wazi katika mama primigravida (mjamzito kwa mara ya kwanza) kuliko maltigravida (mwanamke aliyewahi kuwa mjamzito awali, bila kuzingatia Malengo ya ujauzito huu).

Seviksi

Seviksi hubakia na urefu wa sentimita 2.5 katika kipindi chote cha ujauzito. Katika kipindi cha mwishoni mwa ujauzito, seviksi hunyooka kufuatia mikazo isiyo chungu ya pembezo zake inayoongezeka.

Uke

Inapoakaribia mwisho wa ujauzito, uke pia huendelea kunyumbulika. Mabadiliko haya huwezesha uke kutanuka katika awamu ya pili ya leba, huku mtoto akishukia katika njia ya uzazi. (Utajifunza kuhusu haya yote katika Moduli inayofuata ya Leba na Utunzaji wakati wa Kuzaa.)

7.2 Mabadiliko ya mkao na viungo vinavyohusiana na ujauzito

Mtoto anapoendelea kukua, mkao wa kijumla wa mama mjamzito hubadilika. Fumbatio lake hubadilika kutoka hali bapa au ya kubonyea (kama bakuli) hadi kubinuka sana (kutokeza nje). Hali hii husababisha kuongezeka kwa mpindiko wa mgongo wake. Uzito wa fetasi, kuongezeka kwa uterasi, plasenta na kiowevu cha amniotiki (kifuko cha maji kinachozingira mtoto), pamoja na ongezeko la mpindiko wa mgongo wake, yote husukuma mifupa na misuli ya mwanamke. Kufuatia hali hii, wanawake wengi wajawazito hukumbwa na maumivu ya mgongo. Kusimama kwa muda mrefu mahali pamoja au kuinamia mbele kunaweza kusababisha maumivu ya mgongo, na vivyo hivyo pia kujishugulisha katika kazi ngumu. Aina nyingi za maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito ni kawaida, ingawa yanaweza kuwa viashirio hatari ya maambukizi ya figo. (Utajifunza jinsi ya kutambua maambukizi ya figo katika Kipindi cha 18.)

Vile vile, projesteroni husababisha ulegevu wa ligamenti na viungo katika mwili wote. Wanawake wajawazito wanaweza kuwa katika hatari ya kuteguka na kusukumika kwa sababu ligamenti zao ni legevu, na kwa kuwa mkao wake umebadilika.

7.3 Mabadiliko ya uzani katika ujauzito

Kuendelea kuongezeka kwa uzani wakati wa ujauzito hukisiwa kuwa mojawapo ya viashirio kuwa mwili wa mama unaanza kukubali mabadiliko na kukua kwa fetasi. Hata hivyo, upimaji wa uzani wa mama mara kwa mara wakati wa ujauzito kwa sasa umeonekana kutokuwa muhimu, kwa sababu haulingani vyema na Malengo ya ujauzito. Kwa mfano, mwanamke anaweza kushusha uzani wake kwa kiasi katika kipindi cha mwanzo wa ujauzito ikiwa alipata kichefuchefu na kutapika sana (mara nyingi huitwa‘ugonjwa wa asubuhi’). Utajifunza mengi kuhusu haya na matatizo mengine madogo ya ujauzito katika Kipindi cha 12, baadaye katika Moduli hii. Ongezeko la uzani linalotarajiwa katika mwanamke mwenye afya nzuri, aliye na mimba ya hali ya wastani na aliyebeba mtoto mmoja ni kama ifuatayo:

  • Takriban kilogramu 2.0 kwa jumla katika wiki 20 za kwanza.
  • Kisha takriban kilogramu 0.5 kila wiki hadi kipindi cha ujauzito kutimia wiki 40.
  • Jumla ya kilogramu 9-12 wakati wa ujauzito.

Mwanamke aliye na ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja atakuwa na ongezeko kubwa zaidi la uzani akilinganishwa na aliye na fetasi moja. Mwanamke huyu pia atahitaji chakula chenye kalori nyingi zaidi. (Utajifunza mengi kuhusu chakula na lishe bora na ujauzito katika Kipindi cha 14 katika Moduli hii.)

Ukosefu wa ongezeko bayana la uzito hautakuwa jambo la kusababisha wasiwasi kwa baadhi ya wanawake, lakini linaweza kuwa kiashirio kuwa fetasi haikui vyema. Daktari na wakunga wanaweza kuita jambo hili udumavu wa ukuaji wa mtoto katika uterasi.

7.4 Mabadiliko katika mfumo wa moyo na mishipa

Mfumo wa moyo na mishipa unajumuisha moyo, mishipa ya damu (vena na ateri), na damu inayozunguka mwilini. Huu ni mfumo wa usafirishaji mwilini unaofikisha oksijeni na virutubishi kutoka katika mfumo wa tumbo na utumbo mdogo hadi katika seli, tishu na viungo vya mwili ili kuwezesha kuzalisha nguvu zinazohitajika katika utendakazi wa mwili. Mfumo huu pia hurudisha dioksidi ya kaboni, ambayo ni aina ya takamwili inayofuatia pumzi, hadi kwenye pafu, ili kutolewa kwa njia ya kupumua. Taratibu za kikemikali zinazoendelea mwilini hutoa taka nyingi ambazo husafirishwa kwa damu hadi kwenye figo na ini ambapo huondolewa. Kazi zingine za mfumo wa moyo na mishipa ni pamoja na kudhibiti joto mwilini, kusafirisha na kufikisha homoni na chembechembe zingine zinazodhibiti utendakazi wa mwili. Kuna mabadiliko makubwa katika mfumo huu tata wakati wa ujauzito.

7.4.1 Moyo

Moyo unaweza kuongezeka kwa ukubwa wakati wa ujauzito kutokana na kuongezeka kwa kazi yake.

  • Unafikiri ni kwa nini kazi ya moyo ni sharti iongezeke?

  • Hii ni kwa sababu moyo unapaswa kusambaza damu kupitia plasenta, fetasi na uterasi na fumbatio la mwanamke mjamzito.

    Mwisho wa jibu

Kiwango cha damu kinachopigwa kutoka katika moyo kila dakika huitwa uzalishaji wa moyo. Jedwali 7.1 linaonyesha jinsi kazi ya moyo inavyoongezeka katika ujauzito.

Jedwali 7.1 Mabadiliko ya uzalishaji wa moyo katika ujauzito
Hali ya mwanamkeUzalishaji wa moyo (lita kwa kila dakikia)
Mwanamke asiye mjamzito, aliye katika hali tulivu2.5
Mwisho wa awamu ya kwanza ya ujauzito5
Mwisho wa awamu ya pili ya ujauzito6
Muhula wote wa ujauzito7

Ongezeko la uzalishaji wa moyo husababishwa na mabadiliko mawili katika jinsi moyo unavyotenda kazi:

  • Ongezeko la kima cha mapigo ya moyo katika hali ya kutulia, yaani idadi ya midundo ya moyo kwa kila dakika. Kima cha mapigo ya moyo ni takriban midundo 15 zaidi kwa kila dakika kwa mwanamke mjamzito.
  • Ongezeko la kiasi cha kipigo, yaani, kiasi cha damu kinachopigwa kutoka katika moyo kwa kila mdundo. Kiwango hiki ni takriban mililita 7 zaidi kwa kila mdundo katika mwanamke mjamzito.

Uzalishaji wa moyo hukokotolewa kwa kuzidisha kiwango cha upigaji moyo na kiasi cha kipigo.

Katika awamu ya pili ya ujauzito, mama akiwa ametulia, moyo wake hufanya kazi kwa asilimia 40 zaidi kuliko akiwa hana mimba. Kiwango kikubwa cha ongezeko hili hutokea kufuatia moyo unaotenda kazi kifasaha, ambao hupiga damu zaidi kwa kila mdundo.

7.4.2 Kiasi cha damu

Kiasi cha damu (kiasi cha jumla cha damu inayozunguka, kwa kipimo cha lita) huongezeka polepole kwa asilimia 30-50 katika mwanamke mjamzito. Hivyo basi, kufikia hatima ya ujauzito mwanamke huyu atakuwa na takriban lita 1.5 zaidi kuliko wakati hana mimba. Mwili huhitaji kiasi kikubwa cha damu inayozunguka ili kuwepo kwa damu ya ziada itakayopitia katika plasenta ili lishe na oksijeni ifikishwe kwenye fetasi. Ongezeko la kiasi cha damu husababishwa na mabadiliko mawili:

  • Kuongezeka kwa plazma ya damu (kiowevu cha damu).
  • Kuongezeka kwa seli nyekundu za damu katika mzunguko.

Kiwango cha plazma ya damu huongezeka baada ya takriban wiki ya sita ya ujauzito. Kuongezeka kwa damu hufikia kilele chake cha takriban asilimia 50 zaidi kuliko wakati mwanamke hana mimba ifikapo awamu ya pili ya ujauzito ambapo itabaki hivyo hadi hatima ya ujauzito.

Kiasi cha jumla ya seli nyekundu huongezeka kwa takriban asilimia 18 wakati wa ujauzito, kufuatia kuhitajika kwa oksijeni ya ziada katika tishu ya mama, plasenta na fetasi. Seli nyekundu za damu zina dutu inayosafirisha oksijeni, iitwayo hemoglobini, ambayo ina wingi wa elementi muhimu aina ya ayoni (tazama Jedwali 7.1). Matumizi ya dawa yenye elementi ya ayoni wakati wa ujauzito yanaweza kupelekea ongezeko la seli nyekundu za damu hadi asilimia 30 zaidi kuliko wakati mwanamke hana mimba.

Hemoglobini hutamkwa ' hem mo glo bini'

Jedwali 7.1 ayoni, hemoglobini, na anaemia

Ayoni hupatikana katika seli zote na ina kazi nyingi muhimu. Ayoni ni kipengele muhimu sana cha dutu hii inayosafirisha oksijeni yaani hemoglobini, ambayo hupatikana katika seli nyekundu za damu. Ni ayoni hii katika hemoglobini inayofanya seli hizi ziwe nyekundu. Ikiwa lishe lina kiwango cha chini sana cha ayoni, mtu hawezi kuzalisha seli nyekundu za kutosha. Pia, ayoni huhusika katika kuhifadhi na kutoa oksijeni kwenye misuli.

Anemia inafasiliwa kifasaha kuwa ukolezi duni wa hemoglobini katika damu, ingawa mara nyingi hujulikana kama ukolezi duni wa seli nyekundu za damu. Kiasi kidogo cha ayoni katika chakula ndicho kisababishi kikuu cha anemia.

Kipimo cha hemoglobini huonyeshwa kwa kutumia ishara zake za kemikali (Hb) na uzito wake kwa gramu (gm) kwa desilita (dl) moja ya damu. Desilita moja ni sawa na mililita (ml) 10. Shirika la Afya Duniani linapendekeza kuwa hemoglobini ya mwanamke mjamzito haipaswi kuwa chini ya gramu 11 ya hemoglobini kwa desilita moja ya damu (Hb 11g/dl). (Utajifunza mengi kuhusu anemia na matibabu yake katika Kipindi cha 18)

Ingawa kuna ongezeko endelevu katika idadi ya seli nyekundu za damu wakati wa ujauzito, ongezeko la kiasi cha plazma ni kubwa zaidi. Hata ingawa mwanamke mjamzito ana idadi kubwa zaidi ya seli nyekundu za damu kuliko alipokuwa bila mimba, seli hizi huzimuliwa katika kiasi cha plazma ya damu ambacho kwa sasa ni kikubwa.

  • Je, uzimulizi huu huathiri vipi ukolezi wa seli nyekundu na hemoglobini katika damu ya mwanamke mjamzito ikilinganishwa na wakati akiwa hana mimba?

  • Ukolezi wa seli nyekundu za damu na hemoglobini hushuka kwa sababu vipengele hivi huwa vimezimuliwa zaidi, hivyo basi damu ya mwanamke huyu itakuwa na kiwango kidogo cha hali ya anemia.

    Mwisho wa jibu

Athari hii hujulikana kama anemia ya kifiziolojia. Hivyo basi, tukio hili hueleza umuhimu wa chembechembe za ayoni kwenye chakula au kutokana na tembe wakati wa ujauzito.

7.4.3 Shinikizo la damu katika ujauzito

Awali tulijadili kuwa projesteroni husababisha ligamenti na jointi kulegea wakati wa ujauzito. Vile vile, homoni hii pamoja na kemikali zingine asilia mwilini husababisha pembezo za mishipa ya damu kulegea kidogo. Malengo yake ni kuwa mzunguko wa damu mwilini utafanyika bila kuzuiliwa sana, kwa sababu kiasi kile kile cha damu kinazunguka kupitia mishipa pana kiasi. Shinikizo la damu (SD) humaanisha jinsi ambavyo damu 'husukuma' pembezo za mishipa mikuu ya damu inapozunguka mwilini inapopigwa na moyo.

  • Ulegevu kiasi wa pembezo za mishipa ya damu unaathiri vipi shinikizo la damu la mwanamke mjamzito?

  • Shinikizo la damu la mwanamke huyu liko chini kuliko hali yake kabla ya kupata mimba, kwa sababu kiasi chicho hicho cha damu kina nafasi kubwa zaidi ya kuzungukia.

    Mwisho wa jibu

Shinikizo la chini la damu ni kawaida hususan katika kipindi cha mwanzo wa ujauzito. Wanawake wengi hukumbwa na kizunguzungu mara kwa mara katika kipindi cha kwanza cha ujauzito, kwa sababu kiwango kidogo cha damu na oksijeni hufikishwa kwenye ubongo. Projesteroni pia inaweza kusababisha ulegevu mkuu wa ghafla katika mishipa ya damu, hivyo kusababisha hisia za kizunguzungu za ghafla au hata kupoteza fahamu kwa muda mfupi.

Kisababishi kingine cha kizunguzungu kinaweza kuletwa na kulala chali. Jambo hili hufanyika mara nyingi baada ya wiki 24 ya ujauzito, lakini linaweza kutokea mapema kwa mwanamke aliyebeba mapacha au hali zozote zinazoongeza wingi wa kiowevu cha amniotiki (maji yanayozingira fetasi) Mwanamke mjamzito anapolala chali, uzito wa uterasi na vyote vilivyomo hufinya mishipa mikuu ya damu (vena kava) inayotoka upande wa chini wa mwili wake kuelekea moyoni. Mishipa ya damu inapojibana, uwezekano wa damu kusambaa nyuma hadi moyoni hupunguzwa, tukio ambalo litasababisha mkondo wa damu nje ya moyo hadi sehemu mbalimbali za mwili kupunguka.

  • Ikiwa kuna upungufu wa ghafla wa damu inayotoka moyoni, ni nini kitakachofanyikia shinikizo la damu la mwanamke, na je, atahisi vipi kufuatia tukio hili?

  • Kulala chali kunaweza kusababisha shinikizo la damu kushuka kighafla. Kizunguzungu au kupoteza fahamu kunaweza kutokea kwa sababu hakuna oksijeni ya kutosha inayofikia ubongo. Baada ya kukamilisha trimesta ya kwanza, wanawake wajawazito wanapendekezwa wasilale chali.

    Mwisho wa jibu

7.4.4 Mazoezi na mtiririko wa damu wakati wa ujauzito

Ongezeko la uzito katika mwanamke mjamzito huzidisha utendakazi wa mwili kufuatia mazoezi yoyote. Mazoezi taratibu yasiyo makali ni bora kwa mama kwa sababu mazoezi haya huandaa mwili wake kuhimili leba. Mazoezi makali ya ghafla, au kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika ni jambo linaloweza kumfanya ahisi kizunguzungu. Hisia hizi hutokea kwa sababu shinikizo la chini la damu na anemia ndogo ya kifiziolojia haiwezi kutosheleza kiwango cha ziada cha oksijeni kinachohitajika mwilini.

Kielelezo 7.2 Mwanamke mjamzito anafaa kujiepusha na mazoezi mazito au mepesi mno.

Mwanamke mjamzito hafai kufanya mazoezi ambapo amelala chali, kwa sababu mishipa mikuu inayorudisha damu moyoni itafinyika. Mazoezi makali yanaweza kupelekea upungufu wa damu inayotiririka kwenye uterasi kwa sababu damu itaelekezwa kwenye misuli, ingawa jambo hili halijaonekana kuwa na athari ya kudumu kwa mtoto. Wanawake wajawazito hawapaswi kufanya mazoezi makali katika msimu wa joto kali, au ikiwa mazoezi hayo yatamfanya asipumue vizuri au kama kuna hatari zozote zinazojulikana kama vile, historia ya utokaji mimba ghafla.

7.4.5 Edema wakati wa ujauzito

Edema hutamkwa kwa "ii diii mah".

Ikiwa mwanamke mjamzito atakumbwa na edema, kali ikiwemo kufura uso, hii ni dalili ya hatari inayohitaji mama kupelekwa kwa dharura hadi kituo cha afya kilicho karibu.

Ongezeko la uwezo wa mishipa midogo ya damu kupenyeka (yaani mishipa kuruhusu viowevu vingi kuvuja nje hadi katika tishu) na uzito wa ziada wa uterasi, na mvuto wa graviti hudhoofisha kima cha kusambaza damu kurudi moyoni kutoka katika sehemu ya chini ya mwili. Mara nyingi viowevu hukusanyika kwenye tishu ya miguu ya mwanamke mjamzito baada ya kipindi cha kwanza cha ujauzito, badala ya kufyonzwa iingie kwenye mfumo wa mzunguko wa damu. Kufura kunakosababishwa na mkusanyiko wa viowevu hivi huitwa edema.

Edema ni hali ya kawaida kwa wanawake wajawazito, hususan wakisimama kwa muda mrefu. Pia, edema ya mikono inaweza kutokea. Mshauri mama apumzike mara kwa mara na kuhakikisha ameiinua miguu yake akiwa ameketi. Jambo hili litaimarisha uwezo wa damu yake kurudi moyoni na pia kumsaidia kupunguza kufura kwa miguu.

7.5 Mabadiliko ya kipumzi

Wakati wa ujauzito, kiasi cha hewa inayoingia na kutoka katika mapafu huongezeka kwa karibu asilimia 50 kwa sababu hizi mbili:

  • Kila upumuo una kiasi kikubwa zaidi cha hewa
  • Kima cha kupumua (pumzi kwa dakika) huongezeka kwa kiasi kidogo.

Wakati wa ujauzito, wanawake wengi hutambua kwamba wanakumbwa na matatizo ya kupumua (hawawezi kuvuta ndani pumzi nyingi kama kawaida). Hii ni kwa sababu mtoto anayekua husukuma mapafu ya mama, hivyo ana nafasi ndogo zaidi ya kupumua. Lakini iwapo pia ni mnyonge na mchovu, ama amekosa hewa ya kutosha wakati huu wote, anafaa kuchunguzwa ili kubaini kama ana maradhi, matatizo ya moyo au lishe duni. Pata ushauri wa daktari iwapo unadhani kuwa anaweza kuwa na mojawapo ya hali hizi.

7.6 Mabadiliko katika mfumo wa tumbo na utumbo wakati wa ujauzito

Kama unavyoweza kukumbuka kutoka masomo yako ya shule ya upili ya bayolojia, chakula na viowevu huingia katika mfumo wa tumbo na utumbo kupitia mdomo, kisha kupitia umio, tumbo na utumbo, kisha taka ngumu ikatolewa katika kinyeo. Mkanda huu ulio mrefu sana kutoka mdomoni hadi kinyeo mara nyingi hujulikana kama ’utumbo’. Protini, mafuta na kabohidreti katika lishe huvunjwavunjwa (kumeng’enywa) katika utumbo hadi kuwa vipande vidogo sana vinavyoweza kufyonzwa kutoka utumboni hadi katika mishipa ya damu. Hii pia ndiyo njia ambayo dutu zenye rutuba, kama vile vitamini na madini huingia mwilini.

Wakati wa ujauzito, misuli ya pembezo za mfumo wa tumbo na utumbo hulegea kidogo, kisha kima cha kufinyia chakula nje ya tumbo na katika utumbo hupungua kidogo.

  • Je, unaweza kutaja sababu inayofanya upungufu wa mwendo wa chakula katika mfumo wa tumbo na utumbo kuwa na manufaa wakati wa ujauzito?

  • Upungufu huu wa mwendo wa chakula huongeza muda wa umeng’enyaji ili kuwezesha ufyonzaji wa kutosha wa virutubishi katika lishe.

    Mwisho wa jibu

Athari mbaya pia husababishwa na mwendo wa polepole wa kuondoa chakula katika tumbo na utumbo wote.

  • Hebu taja mojawapo ya athari hizi mbaya.

  • Wanawake wengi wajawazito hupatwa na hali ya kufunga choo (ugumu wa kuondoa kinyesi).

    Mwisho wa jibu

Kielelezo 7.3 Ukuaji wa mtoto huziba fumbatio la mama, jambo linaloweza kusababisha matatizo ya umeng’enyaji na kiungulia. Mwanamke huyu pia anaweza kushindwa kupumua vyema kwa sababu mtoto ameyasukuma mapafu.

Wanawake wengi pia huwa na kichefuchefu katika miezi ya kwanza ya ujauzito. Hisia za kuchomeka au maumivu tumboni au katikati ya matiti hujulikana kama ukosefu wa umeng’enyaji (au ’kiungulia’, ingawa moyo kwa kawaida haiathiriwi). Kiungulia hutokea kwa sababu pindi mimba inavyoendelea, mtoto anayekua hujaza fumbatio la mama hivyo kulisukuma juu kuliko kawaida (Kielelezo 7.3). Asidi zilizo katika fumbatio la mama zinazosaidia kumeng’enya chakula husukumwa hadi sehemu ya juu kifuani, ambapo zinasababisha hisia za kuchomeka. Hali hii si hatari na kwa kawaida huisha baada ya kuzaa.

Iwapo mama huyu ana matatizo ya kichefuchefu na umeng’enyaji, mshauri kula chakula kidogo mara nyingi. Mama huyu hafai kulala bapa kwa saa 1 - 2 baada ya kula, kwa sababu jambo hili linaweza kusababisha hali hizi. Katika Kipindi cha 12, utajifunza zaidi kuhusu matatizo madogo ya ujauzito kama hizi, na jinsi ya kumsaidia mwanamke huyu kuzidhibiti.

7.7 Mabadiliko katika mfumo wa mkojo wakati wa ujauzito

Mfumo wa mkojohuwa na figo (jozi la viungo katika pande zote mbili za fumbatio karibu na mgongo), mishipa inayounganisha figo hizi na kibofu ambapo mkojo huhifadhiwa, na mshipa unaojulikana kama urethra unaopitisha mkojo nje ya mwili. (Rejelea Kielelezo 3.1 katika Kipindi cha 3 ili kujikumbusha kuhusu nafasi ya kibofu na urethra.) Figo hutoa taka katika damu na kuligeuza kuwa mkojo. Ni sharti figo kufanya kazi ya ziada ili kulichunga taka la mama mwenyewe kutoka katika damu yake, na pia taka ya fetasi, na kisha kuliondoa kupitia mkojo wake. Kwa hivyo, pia kuna ongezeko la kiasi cha mkojo unaotolewa na mama wakati wa ujauzito.

Ni jambo la kawaida kwa mwanamke kukojoa mara nyingi, hasa katika miezi ya kwanza na ya mwisho ya ujauzito. Jambo hili hufanyika kwa sababu fetasi inasukuma kibofu. Mwishoni wa ujauzito, mara nyingi mwanamke huhitaji kuamka usiku ili kukojoa. Hii ni kwa sababu kiowevu kilichokusanyika miguuni na nyayoni wakati wa mchana (edema) hufyonzwa katika damu miguu yake inapoinuliwa kitandani. Figo hufyonza viowevu hivi vya ziada kisha kuvigeuza kuwa mkojo, hivyo kibofu hujazwa haraka zaidi wakati wa usiku.

7.8 Mabadiliko ya ngozi

Mabadiliko ya homoni za mwanamke na kupanuka kwa fumbatio na matiti yake husababisha mabadiliko kadhaa ya ngozi wakati wa ujauzito.

7.8.1 Linea nigra

Mstari huu mweusi unaweza kutokea katikati ya kitovu na simfisisi ya kinena (mfupa wa kinena); katika baadhi ya wanawake mstari huu unaweza kupanda hadi kwenye stanamu (mfupa ulio katikati ya matiti). Mstari huu ni utoleshaji wa hali ya juu wa dutu za rangi ya kunde katika seli za ngozi zilizo katika sehemu hii, utaratibu ambao husababishwa na homoni. Baada ya kuzaa, mstari huu huanza kufifia, ingawa huenda usiishe kabisa.

7.8.2 Kinyago cha ujauzito (kloasima)

Baadhi ya wanawake huwa na alama ya rangi ya kahawia usoni na kwenye paji la uso, ambayo hujulikana kama ’kinyago cha ujauzito’ (au kloasima). Hali hii humfanya kuwa na rangi ya shaba. Hali hii huanza katika wiki ya 16 ya ujauzito huku ikiongezeka polepole na kufifia baada ya kuzaa. Utajifunza kuhusu jambo hili katika Kipindi cha 8.

7.8.3 Alama za kuvutika

Huku uzito wa mwanamke huyu unapoongenzeka, ngozi huvutika katika maeneo yasiyoweza kukua zaidi - fumbatio, mapaja na matiti. Alama za kuvutika za rangi ya kahawia au waridi zinaweza kutokea katika baadhi ya wanawake, jambo linaloweza kutokea upesi sana. Alama hizi kwa kawaida hufifia baada ya kuzaa, ingawa huwa haziishi kabisa.

7.8.4 Tezi za jasho

Utendakazi wa tezi za jasho kote mwilini kwa kawaida huongezeka wakati wa ujauzito, jambo linalomfanya mwanamke huyu kutoa jasho jingi zaidi ya kawaida, hasa wakati wa majira ya joto au baada ya kufanya kazi ya sulubu.

7.9 Mabadiliko katika matiti

Katika vipindi vya kwanza vya ujauzito, matiti yanaweza kuwa na hisia za kujaa au kuchoma, huku yakiongezeka kwa ukubwa pindi ujauzito unavyoendelea. Areola (duara nyeusi ya ngozi yenye rangi) inayoizunguka chuchu huwa nyeusi zaidi huku kipenyo chake kikiongezeka. Tezi za Montgomery (vijinundu vilivyo katika areola) huongezeka kwa ukubwa na kuonekana kuchomoza. Mishipa ya damu ya sehemu ya juu ya titi inaweza kuanza kuonekana kufuatia ongezeko la kuzunguka kwa damu. Mishipa hii inaweza kuyapa matiti yangi ya waridi.

Kufikia wiki ya 16 (wakati wa simesta ya pili), matiti huanza kutoa dang’a. Hii ndiyo dutu inayotangulia maziwa ya titi. Dang’a ni dutu ya manjano inayotoka katika chuchu ambayo huwa nene zaidi pindi ujauzito unavyoendelea. Dang’a ina kiasi cha juu sana cha protini na huwa na antibodi (protini maalum zinazotolewa na mfumo wa kingamwili ya mama) ambazo husaidia kumkinga mtoto mzawa kutokana na maambukizi. Mwisho wa ujauzito unapokaribia, chuchu zinaweza kutoa dang’a nyingi kiasi cha kufanya majimaji kwenye nguo ya mama. Mhakikishie mama kuwa jambo hili ni la kawaida na ni ishara nzuri. Baada ya mtoto kuzaliwa, dang’a hutolewa kwa takriban siku tatu za kwanza, kabla ya maziwa halisi kuanza kutiririka. Hakikisha kuwa mama anamyonyesha mtoto kwa dang’a ili apate virutubishi vyote na antibodi anazohitaji.

Katika Kipindi cha 8, utakumbana tena na baadhi ya dalili za mabadiliko haya ya kifisiolojia ya ujauzito, ambapo utajifunza jinsi ya kutambua iwapo mwanamke ni mjamzito, na jinsi ya kukusanya habari kuhusu ’historia yake ya ujauzito’.

Muhtasari wa Kipindi cha 7

Katika Kipindi cha 7, ulijifunza yafuatayo:

  1. Vile vile, estrojeni na projesteroni ni homoni kuu katika kipindi chote cha ujauzito.
  2. Miongoni mwa athari zingine, viwango vya juu vya projesteroni husababisha ukubwa wa baadhi ya viungo vya ndani ya mwili kuongezeka, ikiwa ni pamoja na uterasi, ili iweze kubeba mtoto aliyehitimu muhula wote wa ujauzito.
  3. Ongezeko la uzito linalotarajiwa kwa mwanamke mwenye afya njema, aliye na mimba ya hali ya wastani na aliyebeba mtoto mmoja ni kama ifuatayo:
  4. Mwili huhitaji kiasi kikubwa cha damu inayozunguka ili kuwepo kwa damu ya ziada itakayopitia katika plasenta ili lishe na oksijeni ifikishwe kwenye fetasi.
  5. Ongezeko la kiasi cha damu huzidi ongezeko la seli nyekundu za damu, hivyo zinachujulika katika kiasi hiki kikubwa cha plazma ya damu, jambo linalosababisha anemia. Hii ni sababu moja inayofanya nyongeza ya ayoni mwilini kuwa muhimu sana wakati wa ujauzito.
  6. Shinikizo la chini la damu ni kawaida hususani katika kipindi cha mwanzo wa ujauzito. Jambo hili linaweza kupelekea kizunguzungu na hata kipindi kifupi cha kukosa ufahamu.
  7. Upungufu wa kurejea kwa damu moyoni ni jambo linaloweza kupelekea edema - kufura kwa miguu na nyayo kufuatia viowevu kukusanyika humu.
  8. Wakati wa ujauzito, wanawake wengi hukosa hewa ya kutosha kwa sababu mtoto anayekua husukuma mapafu ya mama hivyo ana nafasi ndogo zaidi ya kupumua. Mwanamke huyu pia anaweza kukumbwa na matatizo ya umeng’enyaji kwa sababu fumbatio lake husukumwa juu zaidi.
  9. Wakati wa ujauzito, misuli ya pembezo za mfumo wa tumbo na utumbo hulegea kidogo, kisha kima ambacho chakula husafirishwa tumboni hupungua kidogo. Jambo hili hupelekea virutubishi kufyonzwa kwa kiwango cha juu zaidi katika damu ya mama, jambo ambalo hunufaisha fetasi. Hata hivyo, mama huyu anaweza pia kupatwa na kichefuchefu au matatizo ya umeng’enyaji.
  10. Haja ya kukojoa kila mara ni jambo la kawaida, hasa katika mwezi wa kwanza na wa mwisho wa ujauzito. Hii ni kwa sababu uterasi inayokua husukuma kibofu. Kibofu hujaa upesi zaidi wakati wa usiku kwa sababu kiowevu (edema) kinachokusanyika miguuni wakati wa mchana hufyonzwa tena.
  11. Mabadiliko katika homoni za mwanamke na kupanuka kwa kimaumbile kwa matiti na fumbatio linalokua ni mambo yanayoweza kusababisha alama za kuvutika katika ngozi inayofukia maeneno haya wakati wa ujauzito. Mabadiliko mengine ya ngozi yanaweza kujumuisha rangi ya manjano na ongezeko la jasho.
  12. Katika simesta ya pili, matiti huanza kutoa dang’a - dutu ya rangi ya manjano ambayo huwa nene pindi ujauzito unavyoendelea. Dang’a ina wingi wa protini na antibodi za mama, hivyo inafaa kulishwa mtoto kila wakati.

Maswali ya Kujitathmini (MK) ya Kipindi cha 7

Kwa vile umekamilisha Kipindi hiki, jibu maswali haya ili kutathmini jinsi ulivyofanikiwa katika Malengo ya Mafunzo ya Kipindi hiki. Andika majibu yako katika shajara yako ya masomo na uyajadili na mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi wa Somo unaofuata. Unaweza kudhibitisha majibu yako ukilinganisha na vidokezo ulivyoandika katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini la 7.1 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.2)

Maumivu ya mgongo husababishwa na nini wakati wa ujauzito?

Answer

Maumivu ya mgongo hutokea mara nyingi katika wanawake wajawazito kwa sababu hali ya mwili wao hubadilika ili kutoa nafasi ya uterasi inayokua. Mgongo hujipinda ndani huku fumbatio likijipinda nje, hivyo kuusukuma mgongo, jambo linaloweza kusababisha maumivu.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 7.2 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.3)

Mwanamke mjazito aliongeza kilo 2 za uzito katika wiki 20 za kwanza za ujauzito, kisha kilo 0.5 kila wiki kwa wiki 10 zilizofuata, kisha kilo 0.1 katika wiki 10 za mwisho. Idadi ya jumla ya uzito alioongeza katika mwisho wa muhula wa ujauzito ni gani? Ongezeko hili linadokeza jambo gani linaloendelea?

Answer

Ongezeko la uzito wa mwanamke huyu lilikuwa kawaida katika wiki za kwanza 30 za ujauzito: yeye aliongeza kilo 2 katika wiki 20 za kwanza na kilo 0.5 kila wiki katika wiki 10 zilizofuata. Hata hivyo, mwanamke huyu anatarajiwa kuongeza kilo 0.5 kila wiki kutoka wiki 30 - 40, lakini ongezeko lake la uzito lilipungua hadi kilo 0.1 kwa kila wiki katika kipindi hiki. Haiwezekani kubaini iwapo ongezeko hili mwishoni mwa ujauzito ni dalili ya kuonyesha kuwa fetasi haikui vyema, lakini inafaa kuchunguzwa katika kituo cha afya. Baadhi ya wanawake huwa na mimba ya kawaida bila kuongeza uzito mwingi, lakini kwa wengine hii ni dalili ya kizuizi cha kukua kwa fetasi ndani ya uterasi.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 7.3 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.4)

Je, ni kwa nini ni muhimu kwa wanawake wajawazito kula vyakula vilivyo na ayoni kwa wingi au kutumia tembe za ayoni?

Answer

Wanawake wajawazito kwa kawaida hupata anemia ndogo ya kifisiolojia kwa sababu kiasi chao cha damu huongezeka kwa kasi kuzidi ongezeko la idadi ya seli nyekundu za damu. Ayoni huhitajika kwa utoleshaji wa hemoglobini, ambayo ni dutu inayobeba oksijeni katika seli nyekundu za damu. Iwapo mwanamke hana ayoni ya kutosha katika mwili wake, yeye hawezi kutolesha seli nyekundu za kutosha, hivyo anemia yake inaweza kuwa mbaya zaidi. Kula chakula kilicho na ayoni kwa wingi au kumeza tembe zilizo na ayoni ni hatua zinazomsaidia kutolesha seli nyekundu za kutosha kusafirisha oksijeni anayohitaji yeye na fetasi inayokua.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 7.4 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.4)

Ni kinachoweza kumfanyikia mwanamke mjamzito iwapo analala chali. Eleza jibu lako

Answer

Mwanamke mjamzito anapolala chali, uzito wa uterasi na vyote vilivyomo hufinya mishipa mikuu ya damu (vena kava) inayotoka upande wa chini wa mwili wake kuelekea moyoni. Jambo hili kwa upande mwingine hupelekea kiwango kidogo zaidi cha damu kupigwa kutoka katika moyo wake hadi sehemu zote za mwili, hivyo shinikizo lake la damu hushuka ghafla. Mwanamke huyu anaweza kupatwa na kizunguzungu au kupoteza fahamu kwa sababu hana oksijeni ya kutosha inayofikia ubongo wake.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 7.5 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.5)

Ni habari gani inayoweza kukusaidia kufanya uamizi kuhusu haja ya ushauri wa kiafya wakati mwanamke mjamzito amekumbwa na matatizo ya kupumua?

Answer

Matatizo ya kupumua hutokea mara nyingi katika ujauzito kwa sababu uterasi hukua na kuyasukuma mapafu ya mama, hivyo anakuwa na nafasi ndogo zaidi ya kupumulia. Lakini iwapo mwanamke huyu ni mnyonge, mchovu, na mwenye tatizo la kupumua wakati wote, unafaa kumpa rufaa ili kutafuta ushauri wa kiafya. Mwanamke huyu anaweza kuwa na anemia ama kukumbwa na matatizo ya moyo, au pengine lishe lake ni duni.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 7.6 (hutathmini Malengo ya Mafunzo ya 7.1, 7.2, 7.4 na 7.5)

Ni elezo lipi ambalo si kweli?? Katika kila kauli, eleza lisilo la kweli.

  • A.Mwanamke mjamzito huhimizwa kulala bapa baada ya kula kwa sababu hatua hii husaidia katika umeng’enyaji.
  • B.Kukojoa mara kwa mara katika vipindi vya mwishoni mwa ujauzito ni jambo la kawaida kwa sababu uterasi husukuma kibofu.
  • C.Kipimo cha mapigo ya moyo, kiasi cha mshtuko na utoleshaji wa moyo zote huongezeka wakati wa ujauzito.
  • D.Edema katika ujauzito huwa mbaya zaidi wakati wa usiku.
  • E.Rangi inaweza kutokea usoni, ama kama msitari mweusi kwenye fumbatio katika baadhi ya wanawake.
  • F.Watoto wazawa hawafai kulishwa kwa dang’a.
  • G.Projesteroni husababisha uterasi kuongezeka kwa ukubwa ili kuipa nafasi fetasi inayokua.
Answer

A si kweli. Mwanamke mjamzito hahimizwi kulala bapa baada ya kula na hali hii haisaidii katika umeng’enyaji. Vitu vilivyomo tumboni mwa mwanamke mjazito husukumwa kuelekea juu hadi kwenye umio katika kifua anapojilaza, huku asidi inayomeng’enya chakula chake ikisababishwa mwasho unaojulikana kama ‘kiungulia’.

B ni kweli. Kukojoa mara kwa mara katika vipindi vya mwishoni mwa ujauzito ni jambo la kawaida kwa sababu uterasi husukuma kibofu hivyo hakiwezi kuhifadhi kiasi kikubwa cha mkojo.

C ni kweli. Kipimo cha mapigo ya moyo, kiasi cha mshtuko na utoleshaji wa moyo zote huongezeka wakati wa ujauzito. Hii ni kwa sababu mwili wa mwanamke, ambao sasa ni mkubwa zaidi, uterasi na fetasi vyote huhitaji kiasi kukibwa zaidi cha damu ili kuvipa virutubishi na oksijeni.

D si kweli. Edema katika ujauzito kwa kawaida hupungua wakati wa usiku. Viowevu vinavyokusanyika miguuni mwa mwanamke wakati wa mchana hufyonzwa hadi ndani ya mkondo wa damu wakati miguu yake imeinuliwa kitandani wakati wa usiku.

E ni kweli. Rangi inaweza kutokea usoni, ama kama msitari mweusi kwenye fumbatio katika baadhi ya wanawake.

F si kweli. Watoto wazawa wanafaa kulishwa kwa dang’a kila mara. Dang’a ina kiasi cha juu sana cha protini na huwa na antibodi ambazo husaidia kumkinga mtoto kutokana na maambukizi.

G ni kweli. Projesteroni husababisha uterasi kuongezeka kwa ukubwa ili kuipa nafasi fetasi inayokua.

Mwisho wa jibu