Skip to main content
Printable page generated Wednesday, 4 Aug 2021, 16:51
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Wednesday, 4 Aug 2021, 16:51

18. Matatizo ya Kiafya ya Kawaida wakati wa Ujauzito

Kipindi cha 18 Matatizo ya Kiafya ya Kawaida wakati wa Ujauzito

Utangulizi

Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu matatizo matatu ya kawaida ya kiafya wakati wa ujauzito na athari zake kwa afya ya mjamzito: malaria, anemia na maambukizi kwenye njia ya mkojo na jinsi ya kutofautisha maambukizi ya njia ya mkojo (MNM) yanayoweza kutibiwa kutokana na yale yanayoendelea kwa kibofu cha mkojo na ugonjwa kali unoathiri figo. Tutakueleza visababishi, ishara, dalili, utambuzi, na udhibiti wa hali hizi, na wakati wa kumpa mama rufaa kwa kituo cha afya kwa uchunguzi na matibabu zaidi. Na utajifunza njia bora za kuzuia hali hizi zisitokee na umuhimu wa kufanya hivyo hasa wakati wa ujauzito.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 18

Ukimaliza kipindi hiki, unapaswa kuwa na uwezo wa:

18.1 Kufafanua na kutumia kwa ufasaha maneno yote muhimu yaliyochapishwa kwa herufi nzito. (Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 18.1 na 18.2)

18.2 Kueleza hatari kwa mama, fetasi na mtoto mchanga za malaria, anemia na maambukizi kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito. (Swali la Kujitathmini 18.1)

18.3 Kuwashauri wajawazito na waume zao jinsi ya kuzuia malaria, anemia, na maambukizi kwenye njia ya mkojo. (Swali la Kujitathmini 18.2)

18.4 Kutambua ishara na dalili za malaria kwa mjamzito, na kujua jinsi ya kudhibiti na wakati wa kumpa mama rufaa kwa kituo cha afya. (Swali la Kujitathmini 18.2)

18.5 Kutambua dalili za anemia kwa mjamzito, na kujua jinsi ya kudhibiti na wakati wa kumpa mama rufaa kwenye kituo cha afya. (Swali la Kujitathmini 18.2)

18.6 Kubainisha na kutofautisha kati ya ishara na dalili za maambukizi kwenye njia ya mkojo na ya figo wakati wa ujauzito, kudhibiti maambukizi yasiyokali kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito na dawa za kumeza na kutambua wakati wa kumpa mama aliye na maambukizi yanayoendelea rufaa kwenye kituo cha afya. (Swali la Kujitathmini 18.2)

Mchoro 18.1 Baadhi ya aina ya mbu wanaoweza kusambaza parasiti za malaria kwa watu.

18.1 Malaria wakati wa ujauzito

Malaria ni maambukizi ya seli nyekundu za damu inayosababishwa na parasiti iitwayo Plasmodiumu zinazobebwa na aina fulani ya mbu. Mbu hutoa parasiti za malaria katika damu ya mtu aliyeambukizwa anaponyonya damu 'chakula', na kisha kupitisha parasiti anapomwuma mtu mwingine (Mchoro 18.1). Parasiti hukua na kukomaa katika seli nyekundu za damu na mamilioni ya parasiti hukusanyika katika plasenta ya mjamzito.

Malaria inaweza kuwa kali zaidi kwa kina mama walio na magonjwa mengine. Malaria ni hatari zaidi kwa wajawazito kuliko watu wengine. Mjamzito aliye na malaria yuko katika hali ya kupata anemia (utakavyoona baadaye katika kipindi hiki), kuharibika kwa mimba (kutoka kwa mimba pekee yake kabla ya wiki 24 za ujauzito), kuzaa mapema, kupata mtoto mdogo zaidi, kuzaa mtoto aliyekufa (mtoto kuzaliwa akiwa amekufa baada ya wiki 24 za ujauzito) au kufa yeye mwenyewe (kifo cha mama).

18.1.1 Dalili za malaria

Dalili za ugonjwa huwa ishara kwa mwathiriwa na anazifahamu na kuwa na uwezo wa kukueleza kuzihusu; wanaweza kukuambia pekee yao, lakini unaweza kuuliza maswali yanayozihusu. Dalili za malaria ni kama vile:

 • Baridi (kuhisi baridi isiyo ya kawaida) na kutetemeka (vipindi vikali vya kutetemeka kwa dakika kadhaa na hudumu hadi saa 1), hii huwa dalili ya kwanza ya maambukizi
 • Maumivu ya kichwa na udhaifu mara nyingi huandamana na baridi
 • Joto jingi mwilini (halijoto ya juu); Joto jingi mwilini mara nyingi hufuatwa na baridi, na joto linaweza kwenda juu sana hivyo mtu anakabiliwa na deliriumu (kutokuwa katika hali sawa kiakili, kuona au kusikia mambo yasiyohalisi)
 • Kutokwa na jasho joto lishukapo
 • Katika baadhi ya hali zingine kuhara/kutapika kunaweza pia kushuhudiwa
 • Dalili nyingine ya kawaida ni maumivu ya misuli/viungo.

Vipindi vya joto jingi kwa kawaida hubadilishana na vile vya baridi na joto kwa malengo ambayo yanaweza kuwa kila siku, au baada ya siku 2-3. Dalili hizi zote zinaweza kutokana na kitu kingine chochote, lakini unapaswa kushuku malaria ikiwa yatatokea kwa mtu ambaye ameumwa na mbu katika eneo ambalo malaria hutokea kila mara.

Mchoro 18.2 Mtu aliye na joto jingi mwilini atahisi joto zaidi kukuliko.

Ishara za ugonjwa ni ishara kuwa mhudumu wa afya pekee ndiye atakaye jua, au kutambua kwa kufanya uchunguzi. Kwa mfano, ukishuku ni malaria, unapaswa kupima halijoto na kipimajoto ukiwa nacho (ulijifunza jinsi ya kutekeleza haya katika Kipindi cha 9 ), au kwa kulinganisha hali yako ya joto na ya mama (Mchoro 18.2). Mtu akiwa na malaria, joto mwili linaweza kwenda juu hadi sentigredi 39-40 au hata zaidi.

 • Ni ipi kiwango cha joto la mwili la kawaida na ishara ya joto jingi mwilini ni ipi?

 • Joto la mwili kwa kawaida ni sentigredi 37; ishara ya joto mwilini litakuwa sentigredi 38 au zaidi.

  Mwisho wa jibu

18.1.2 Utambuzi wa malaria

Kuna njia mbili kuu za kutambua malaria kwa kutumia uchunguzi wa damu. Njia rahisi ni kufanya uchunguzi wa haraka wa malaria ambao hutambua protini zinazotolewa na parasiti katika damu ya mgonjwa. Vifaa vya kuchunguza vinaweza kuwa aina ya vijiti vya kutumbukiza, plastiki, au kadi, ambazo hubadilisha rangi zinapopata tone la damu kutoka kwa mtu aliyeambukizwa - kwa kawaida huchukuliwa kutoka kwa kidole na shindano safi. Hata hivyo, vifaa vya kuchunguzia lazima vihifadhiwe kwa makini na kutunzwa kutokana na unyevu na joto jingi. Mafunzo kwa wahudumu wa afya yanahitajika kabla ya utambuzi sahihi wa ishara za malaria kwa malengo ya uchunguzi.

Njia nyingine ya kutambua malaria, ambayo inahitaji utaalamu wa mafunzo na vifaa, ni kutokana na uchunguzi wa damu kwa hadubini kwenye kioo, ambacho kimewekwa rangi ilikuonyesha parasiti. Vifaa vya kuchunguzia damu kwa hadubini kwa kawaida havipatikani katika Kituo cha Afya cha ngazi ya chini. Ikiwa umefunzwa kufanya uchunguzi wa malaria wa haraka na unaweza kutumia vifaa vya kufanyia uchunguzi, unapaswa kutoa utambuzi wa malaria kutokana na malengo ya uchunguzi huu. Ikiwa huwezi kutumia vifaa vya kuchunguza malaria kwa haraka, tekeleza utambuzi wako kwa msingi wa dalili (kwa mfano, maumivu ya kichwa, joto jingi mwilini, baridi, maumivu katika misuli /viungo), na joto jingi mwilini iliyopimwa na kipimajoto.

18.1.3 Matibabu ya malaria wakati wa ujauzito

Ni muhimu kwa wajawazito kuepukana na malaria - au kutibiwa haraka wakiwa wagonjwa. Dawa za kutibu malaria zinaweza kuwa na madhara, lakini ni afadhali kuliko kupatwa na malaria. Ikiwa mama ana dalili za malaria, anapaswa kutibiwa mara moja. Dawa inayotumika mara nyingi huitwa Artemether Lumifantrine (Inauzwa kama Coartem). Uharibu ukuaji wa parasiti katika seli nyekundu za damu za mtu.

Coartem inaweza kutumika kutibu malaria katika awamu ya pili na ya tatu ya ujauzito. Awamu ya pili ni wiki 13-27 tangu wakati wa mwisho wa mama kupata hedhi ya kawaida, na awamu ya tatu ni kutoka wiki 28 hadi wakati wa kuzaa, karibu wiki 40. Malengo ya uchunguzi yakionyesha kuwepo kwa malaria, au ukishuku kuwepo kwa malaria sana kulingana na ishara na dalili, na mama akiwa katika awamu ya pili ama ya tatu, mtibu kama ilivyoainishwa katika Kisanduku 18.1.

Kisanduku 18.1 Kutibu kwa kutumia Coartem katika awamu ya pili au ya tatu ya ujauzito
 • Tembe 4 za Coartem mara mbili kwa siku (baada ya masaa 12) kwa siku 3 (jumla ya tembe 24). Mshauri ameze na chakula, maziwa, supu au uji wa shayiri. Anaweza kuzivunja na kuzichanganya kwa kijiko cha chakula kama hii itakuwa rahisi kwake kumeza dawa. Mchoro 18.3 inaonyesha jinsi ya kueleza kina mama idadi ya tembe za kumeza.
 • Unaweza pia kumpatia tembe za paracetamol (miligramu 500-1000) kila baada ya saa 4-6 ili kupunguza joto jingi mwilini.
 • Kupanguza mwili wake kwa kitambaa kilichoingizwa ndani ya maji baridi pia husaidia akiwa na joto jingi.
 • Mshauri mama anywe maji mengi ili awe na maji ya kutosha mwilini. Anapaswa kunywa angalau kikombe1kubwa cha maji kila saa.

Wajawazito wanaoshukiwa kuwa na malaria katika awamu ya kwanza ya ujauzito, wanaoweza kusafiri, wanapaswa kupelekwa kwenye kituo cha afya kilichoko karibu kwa matibabu maalum.

Mama akiwa katika awamu ya kwanza ya ujauzito (yaani, hadi wiki 12 tangu wakati wa Mwisho wa mama Kupata Hedhi yake ya Kawaida), lakini anaugua sana kusafiri hadi kituo cha afya, mpe matibabu yaliyo katika Kisanduku 18.2. Hatari kwa maisha yake na ya fetasi kutokana na malaria, ni kubwa kuliko hatari ya kutumia dawa mapema wakati wa ujauzito. Mtume kwenye kituo cha afya haraka punde tu hali yake inapomruhusu kusafiri. Kumbuka kwamba dawa aina ya Artesunate huwekwa kwa kapsuli yenye umbo maalum - iitwayo sapozitori - katika njia ya haja kubwa kwa kusukuma polepole kupitia mkundu wake.

Picha 18.3 Mhudumu wa Afya anaonyesha chati chenye tembe za Coartem katika makundi manne. (Picha: hisani ya AMREF)
Kisanduku 18.2 Sidano ya Artemether na ya Artesunate kupitishwa kwenye mkundu

Sindano ya Artemether hudungwa kwa misuli kabla ya rufaa hali kali za malaria inaposhukiwa. Kwa kipimo cha miligramu 3.2 ya Artemether kwa kila kilo ya uzani wa mama, katika dozi moja kwenye misuli ya mkono wake upande wa juu.

Artesunate hupitishwa kwenye mkundu katika sapozitori kwa dozi zifuatazo kabla ya kupewa rufaa.

Uzani wa mamaDozi    Idadi ya sapozitori
Kilo 30-39Miligramu 50   1
Zaidi ya kilo 40Milingramu 4004

Kumbuka kwamba wajawazito wanaweza kuwa na uzani wa zaidi ya kilo 40 baada ya awamu ya kwanza ya ujauzito.

Jumla ya vifo vinavyotokana na malaria na magonjwa ya malaria zimepungua katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na jitihada kubwa za kuzuia malaria na matibabu ya haraka inapotokea. Mpango huu ni muhimu sana kwa kupunguza malaria hata zaidi, ikiwa ni pamoja na utambuzi na matibabu ya mapema kwa wajawazito wanaokuja kwenu kwa huduma ya ujauzito.

18.1.4 Kukinga malaria

Ili kukinga malaria, lazima ufanye lote uwezalo ili usiumwe na mbu. Unapaswa kushauri kila mtu katika jamii wajitokeze pamoja ili:

 • Kuondoa maji taka yanayoleta mbu; ondoa maji ya mvua kwenye choo; funika au ondoa makopo ya bati na sufuria zinazokusanya maji karibu na nyumba.
 • Usikae usiku katika maeneo yenye maji ambapo mbu huzalia.
 • Tumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua wadudu, kemikali inayoua mbu. Katika maeneo mengi, unaweza kusambaza vyandarua vilivyotiwa dawa ya kua wadudu (tazama Picha 18.4) kwa familia zinazozihitaji. Vyandarua hivi vinalinda watu ambao hulala ndani yao kutokana na mbu, na wao pia hupunguza hatari kwa wale wengine wanaolala katika chumba kimoja nao kwa sababu dawa hii hufukuza mbu wasiingie ndani ya nyumba.
Picha 18.4 Vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua wadudu hutoa kinga nzuri kutokana na mbu wanaosambaza malaria. (Picha: UNICEF / Indrias Getachew)

Kukinga malaria inapaswa kuwa wajibu wa mtu binafsi na jamii. Panga kufanya kampeni ya afya kwa lengo la kuhamasisha wana nchi namna ya kukinga malaria, kwa kutumia mbinu za kukuza afya ulizojifunza katika Kipindi cha 2 katika Moduli hii. Hakikisha kwamba wajawazito unao wahudumia wanajua kwamba, watoto wao ambao hawajazaliwa na walio chini ya miaka 5 wote wako katika hatari ya malaria.

18.2 Anemia katika ujauzito

Kina mama walio na anemia huwa na nguvu kidogo ya kuzaa na kuna uwezekano wa kuvuja damu sana baadaye (kuvunja damu nyingi baada ya kuzaa), wawe wagonjwa, au hata kufa baada ya kuzaa. Tayari umejifunza mengi kuhusu utambuzi na uzuiaji wa anemia katika vipindi vya mafunzo ya hapo awali katika Moduli hii, hivyo katika kipindi hiki tutazingatia tiba yake na kuimarisha ulichojifunza.

 • Je, anemia ni nini na nini hutokea katika mwili wa mtu aliye na anemia?

 • Mtu akiwa na anemia, kwa kawaida inamaanisha kuwa hajala vyakula vyenye ayoni ya kutosha. Seli nyekundu za damu huhitaji ayoni kutengeneza hemoglobini, kiungo kinachosaidia seli nyekundu za damu kubeba oksijeni kutoka kwa hewa tunayopumua hadi sehemu zote za mwili. Mtu aliye na anemia hawezi kutengeneza seli nyekundu za damu za kutosha, hivyo mwili wao una upungufu wa oksijeni.

  Mwisho wa jibu

Kumbuka kwamba baadhi ya aina ya anemia husababishwa na ugonjwa sio ukosefu wa ayoni na baadhi hurithiwa kutoka kwa wazazi (maumbile). Inaweza pia kusababishwa na parasiti fulani, ikiwa ni pamoja na malaria na minyoo. Katika kipindi hiki, tunashughulikia anemia inayosababishwa na upungufu wa ayoni kwa chakula. Wajawazito wengi wana anemia, hasa wanawake walio maskini ambao hawawezi kula vyakula vyenye ayoni ya kutosha, kama unavyojua kutoka Kipindi cha 14.

18.2.1 Utambuzi wa anemia

Chunguza anemia kwa wajawazito wote kila mara wanapotembelea kliniki, kwa kuuliza kuhusu dalili zake. Maswali muhimu ya kuuliza ni:

 • 'Je, unajihisi mdhaifu au kuwa mchovu kwa urahisi?'
 • 'Je, unashindwa kupumua (upungufu wa pumzi) unapofanya kazi za kinyumbani?'
 • 'Je, unapata kizunguzungu mara nyingi, na umewahi kuzirai (kukosa fahamu)?

Dalili hizi husababishwa na oksijeni ndogo katika damu ya kumpatia nguvu ya kufanya shughuli za kawaida. Mtu aliye na anemia hujihisi kuwa ana upungufu wa pumzi kwa sababu wanahitaji kupumua kwa haraka zaidi ili kupata oksijeni ya kutosha katika miili yao. Ikiwa ubongo hautapata oksijeni ya kutosha, atahisi kizunguzungu na kuweza kuzirai.

Ishara za anemia (kinachochunguzwa au kupimwa na mhudumu wa afya) ni:

 • Weupe: uweupe ndani ya kope la jicho, viganja vya mikono, kucha, na ufizi.
 • Kupumua kwa kasi (zaidi ya mara 40 kwa dakika; kawaida kiwango cha kupumua ni mara18-30 kwa dakika).
 • Mpigo wa haraka kwa mshipa (zaidi ya mipigo100 kwa dakika). Ulijifunza jinsi ya kupima kiwango cha mipigo kwa mshipa katika Kipindi cha 9 (Sehemu ya 9.4).

Kwa ziara ya kwanza wakati wa utunzaji katika ujauzito

Ukishuku kuwa mama ana anemia, mshawishi afanyiwe uchunguzi wa anemia ikiwa huduma hiyo inapatikana katika Kituo cha Afya kilicho karibu. Uchunguzi wa damu hupima kiasi cha hemoglobini (ayoni iliyoko katika damu) ili kutathmini ikiwa inatosha kubeba oksijeni inayohitajika kwa shughuli za kawaida na mahitaji ya mtoto ambaye hajazaliwa kwa ukuaji. Ikiwa uchunguzi wa damu haupatikani, tumia utathimni wako wa ishara na dalili maalumu (zilizotajwa hapo juu) kutambua anemia na kutoa matibabu kama ilivyoelezwa hapo chini.

Kwa ziara ya baadaye wakati wa utunzaji katika ujauzito

Ukiwa na wasiwasi kuwa mjamzito ana anemia na haonyeshi maendeleo yoyote, unapaswa kumpa rufaa kwenye Kituo cha Afya mara moja.

 • Chunguza weupe ndani ya kope la macho yake, mikononi, kucha, na ufizi.
 • Hesabu mipigo wa mshipa wake. Je, ni zaidi ya 100 kwa dakika?
 • Hesabu mipigo anazopumua katika dakika 1. Je, ni zaidi ya 40?

Anemia ni hatari sana kwa afya ya mama na mtoto, hasa mama anapokaribia kuzaa.

18.2.2 Ukingaji wa anemia katika ujauzito

Kula lishe bora

Wajawazito wote lazima washauriwe wale vyakula vilivyo na viwango vya kutosha vya ayoni na folate (vitamini, ambayo pia huitwa folic acid). Tayari unafahamu ni kwa nini anahitaji ayoni. Folate pia husaidia kukinga anemia kwa wajawazito au wanaonyonyesha, na inaweza kukinga baadhi ya hitilafu za kimaumbile kwa mtoto.

 • Rejelea Kipindi cha 13. Taja baadhi ya vyakula ambavyo vina ayoni nyingi.

 • Unaweza kuwa umefikiria baadhi ya vyakula hivi: kuku, samaki, alizeti, malenge na boga mbegu; maharagwe, mbaazi na dengu; mboga zenye rangi ya kijani kibichi; viazi vikuu; boga ngumu; nyama nyekundu (hasa ini, figo na nyama zingine za ogani); bidhaa za nafaka nzima kama vile mkate wa hudhurungi; mikate iliyowekwa ayoni (iliyoongezwa); karanga na kiini cha yai.

  Mwisho wa jibu

 • Taja baadhi ya vyakula vilivyo na folate nyingi.

 • Samaki; alizeti, malenge, na boga, mbegu; maharagwe na mbaazi; mboga zenye rangi ya kijani kibichi; nyama nyekundu (hasa ini, figo, na nyama nyingine); mchele wa hudhurungi; ngano nzima; uyoga na mayai.

  Mwisho wa jibu

Tembe za ayoni na folate

Unapaswa kumpatia mjamzito tembe za ayoni na folate za kutosha ili ameze tembe moja kwa siku, au tembe moja iliyounganishwa, hadi ziara ya utunzaji katika ujauzito inayofuata. Hakikisha unawaongeza kina mama tembe kila mara wanapozuru hospitali. Kipimo cha kuzuia ni:

 • Ayoni: Meza miligramu 300-325 za ferrous sulphate mara moja kwa siku, ikiwezekana na mlo. Kawaida kipimo hiki hutolewa kwa tembe moja iliyo pia na folate, lakini wakati mwingine inaweza kupeanwa kama matone ya ayoni.
 • Folate: Meza mikrogramu 400 za folic acid mara moja kwa siku, kwa kawaida imeunganishwa na ayoni.

18.2.3 Matibabu ya anemia wakati wa ujauzito

Mama akiwa na anemia kali (Uchunguzi unaonyesha ana hemoglobini iliyo chini ya gramu 8 kwa lita moja ya damu) katika miezi 9 ya ujauzito, anapaswa kuzaa mtoto wake katika hospitali.

Anemia ya kawaida inaweza kutibiwa kwa kula vyakula vyenye ayoni na folate nyingi, na pia vitamini C (kama vile matunda ya jamii ya machungwa na nyanya), na kwa kunywa tembe za ayoni na folate. Kipimo cha kutibu ni:

 • Ayoni: Meza miligramu 300-325 za ferrous sulphate mara mbili kwa siku (mara mbili ya kipimo kinachotumika kwa kuzuia anemia).
 • Folate: Meza mikrogramu 400 za folic acid mara moja kwa siku kwa kinywa (kipimo sawa na kile cha kuzuia).

Baada ya kuagiza tembe hizi na ushauri wa lishe, mjamzito anayeshukiwa kuwa na anemia anapaswa kuchunguzwa tena baada ya wiki 4. Ikiwa hakuna maendeleo yoyote, mpe rufaa kwa kituo cha afya. Anaweza kuwa na ugonjwa, au anahitaji tembe za kuongezwa ayoni.

Tembe za kuongeza ayoni lazima zitolewe kwa miezi 6 wakati wa ujauzito kina mama chini ya 40% katika jamii wakiwa anemia. Endelea kwa zaidi ya miezi 3 baada ya kuzaa ikiwa zaidi ya 40% ya kina mama wana anemia, na mteja wako ananyonyesha.

Madhara ya tembe za ayoni

Matumizi ya tembe za ayoni yanaweza kusababisha madhara-kama vile kichefuchefu kufungika kwa choo na kinyesi cheusi. Mwambie mama anaweza kuwa na madhara-haya, lakini ni muhimu aendelee kutumia tembe za ayoni. Akimeza tembe baada ya mlo inaweza kumsaidia kuzuia kichefuchefu na unywaji wa viowevu vingi na ulaji wa matunda na mboga nyingi husaidia kuzuia kufungika kwa choo. Mhakikishie mama kuwa rangi nyeusi ya kinyesi chake hakina madhara na itaisha akimaliza tembe za ayoni.

Mchoro 18.5 Dalili na ishara kuu za maambukizi ya njia ya mkojo. (Tayari umeona miundo hii yote katika Mchoro 3.1 katika Kipindi cha 3, isipokuwa figo na mishipa ya figo.)

18.3 Maambukizi kwenye njia ya mkojo

Njia ya mkojo (tazama Mchoro 18.5) inajumuisha figo, mishipa ya figo, kibofu cha mkojo na urethra (ufunguzi ambapo mkojo hutokea nje ya mwili). Zote zimeshikamana na hufanya kazi pamoja ili kuondoa uchafu kutoka kwenye damu. Kwanza figo husafisha damu na kugeuza uchafu kuwa mkojo. Halafu mkojo huteremka kwenye mishipa ya figo hadi kwenye kibofu cha mkojo. Mkojo una katika kibofu cha mkojo mpaka mtu akojoe (kutoa maji).

Maambukizi kwenye njia ya mkojo hutokea wakati vimelea vilio na madhara (bakteria) huingia katika urethra. Maambukizi yanaweza kuenea kwa urahisi kwa kibofu cha mkojo au figo. Mara nyingi madaktari huyaita maambukizi kwenye njia ya mkojo. Unapaswa kuchukulia kuwa maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kuhusisha ngazi zote za njia ya mkojo: urethra, kibofu cha mkojo na figo.

Mama anaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine zote. Maambukizi kwenye njia ya mkojo - hasa yanayofika kwenye figo - yanaweza kuwa hatari sana na pia kusababisha kuanza kwa leba mapema isipotibiwa mara moja. Ndio maana ni muhimu kuchunguza ishara za maambukizi katika kila ziara ya huduma ya ujawazito.

Mchoro 18.6 Kujipanguza kutoka mbele kuelekea nyuma baada ya kukojoa au kwenda haja kubwa husaidia kuzuia maambukizi kwenye njia ya mkojo.

18.3.1 Kuzuia maambukizi kwenye njia ya mkojo

Ili kuzuia maambukizi kwenye njia ya mkojo, wafunze kina mama jinsi ya kuweka vimelea kwa vinyesi vyao mbali na njia ya mkojo kwa kujipanguza kutoka mbele kuelekea nyuma baada ya kukojoa au kwenda haja kubwa (tazama Mchoro 18.6). Iwapo watajipanguza kutoka mkundu kuelekea njia ya mkojo, wanaweza kuweka vimelea katika sehemu za siri na vinaweza kuingia kwenye urethra. Wakumbushe kina mama na wenzi wao wanawe mikono na kuosha sehemu za siri kabla ya ngono. Kina mama wanapaswa pia kukojoa mara tu baada ya kufanya ngono. Kutumia kondomu pia husaidia kuzuia kuenea kwa maambukizi katika njia ya mkojo kutoka kwa mwanaume hadi kwa mwanamke.

Katika Sehemu ya 18.3.3 (hapa chini), utajifunza jinsi ya kuwapatia antibiotiki kina mama ambao huwa na maambukizi kwa kibofu cha mkojo ili kuzuia maambukizi wakati wa ujauzito.

18.3.2 Utambuzi wa MNM

Mama aliye na njia ya mkojo yenye afya si kawaida kuripoti maumivu, kuwashwa au uchungu wakati wa kukojoa. Hata hivyo, wakati mwingine mama anaweza kuwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo lakini akakosa kuwa na dalili. Ni muhimu kujaribu kutambua ikiwa maambukizi yamefikia kibofu cha mkojo au ikiwa yamekwenda zaidi katika njia ya mkojo na kufikia figo. Maambukizi ya figo ni makali zaidi na ni hatari kubwa kwa mama na mtoto ambaye hajazaliwa.

Kuchunguza MNM

Maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kutambuliwa kwa kuchunguza mkojo wa mama. Kuna uchunguzi tofauti ambazo kawaida hutekelezwa katika Kituo cha Afya. Kuna kijiti cha kutumbukiza ambacho hubadilisha rangi inapoingizwa katika mkojo iliyoambukizwa au bakteria zinaweza kuonekana kama mkojo unachunguzwa kwa hadubini au bakteria zinaweza kukuzwa (kukuzwa) katika vyombo maalum hadi zitambuliwe. Uchunguzi huu wote unahitaji sampuli ya mkojo safi 'wa katikati unapokojoa’.

 • Ulijifunza jinsi ya kukusanya sampuli ya mkojo wa katikati unapokojoa katika Kipindi cha 9. Unawezaje kumweleza mama jinsi ya kufanya hivyo?

 • Utamwambia aanze kukojoa, lakini baada ya kutoa mkojo wa kwanza achukue kwa chombo safi baadhi ya mkojo wa katikati anapokojoa.

  Mwisho wa jibu

Kuwashwa au uchungu unapokojoa inaweza pia kuwa ni ishara ya maambukizi ukeni au magonjwa ya zinaa. Ikiwa utampata mgonjwa na dalili hizi, mpe rufaa kwenye kituo cha afya kilicho karibu.

Kijiti cha kutumbukiza, hadubini na uchunguzi wa kukuza bakteria ndio njia sahihi ya kutambua maambukizi katika njia ya mkojo, lakini huwezi kutofautisha maambukizi ya kibofu cha mkojo na ya figo. Unaweza kufanya hivyo tu kwa kumuhoji mama kwa makini juu ya dalili zake.

Dalili za maambukizi ya kibofu cha mkojo

Uliza mjamzito ikiwa amekuwa na dalili zozote zifuatazo:

 • Kuhisi haja ya kukojoa, kukojoa kila mara
 • Maumivu au uchungu unapokojoa au pindi tu baadaye
 • Maumivu katika fumbatio la chini, nyuma na mbele ya pelvisi.

Ukishuku maambukizi ya figo, mpe mama rufaa mara moja kwenye kituo cha afya kilicho karibu.

Dalili za maambukizi ya figo

Mchoro 18.7 Maumivu ya upande wa mgongo yanaweza kuwa ya kawaida katika ujauzito, au kuwa ishara ya maambukizi ya figo.

Uliza mjamzito ikiwa anahisi yafuatayo:

 • Dalili zozote za maambukizi ya kibofu cha mkojo
 • Mkojo unalio kama mawingu au damu
 • Joto jingi mwilini, kuhisi joto sana na kutokwa na jasho
 • Kujihisi mgonjwa sana au mdhaifu
 • Maumivu ya upande wa mgongo (upande mmoja au pande zote mbili)
 • Kutapika mara kwa mara
 • Baridi, joto, au kutetemeka sana.

Dalili nyingine ni maumivu upande wa chini wa mgongo, wakati mwingine kwa upande (tazama Mchoro 18.7). Lakini kumbuka kwamba maumivu ya mgongo ni kawaida katika ujauzito na huenda yasiwe ishara ya maambukizi ya figo. Maumivu ya kawaida kwa mgongo katika ujauzito yanaweza kusaidiwa na kusugua au mazoezi. Maumivu yakitokana na maambukizi ya figo, kusugua au zoezi halitamaliza.

18.3.3 Kutibu maambukizi ya kibofu cha mkojo

Mshawishi mama anywe kikombe 1 kikubwa cha kinywaji safi na cha afya angalau mara moja kila saa kabla hajalala. Vinywaji husaidia kuondoa maambukizi kutoka kwenye njia ya mkojo. Maji ya kawaida na yale ya matunda ni mazuri hasa kwa kunywa. Mshawishi ale matunda ambayo yana vitamini C nyingi, kama vile machungwa, mapera ('zeituni') na maembe.

Maambukizi yasipopona haraka au mama akiwa na dalili yoyote ya maambukizi ya figo, mpe rufaa kwenye kituo cha afya, ambapo uchunguzi unaweza kufanywa ili kuthibitisha maambukizi na kuanza matibabu yanayofaa na antibiotiki (dawa za kuua bakteria). Unavyochelewa kutibu maambukizi, ndivyo itakuwa vigumu kutibu. Ukipata mafunzo ya kutibu magonjwa ya kibofu cha mkojo yasiyo makali na antibiotiki, kipimo ni:

 • Amoxicillin: Miligramu 500 kwa kinywa mara tatu kwa siku kwa muda wa siku 5; antibiotiki hii inaweza kutolewa katika tembe za miligramu 250 au 500, hivyo uwe makini unapotoa kipimo cha tembe sahihi. Kamwe usitoe antibiotiki nyingine – ila Amoxicillin tu.

Kutumia antibiotiki kuzuia maambukizi ya mara kwa mara katika kibofu cha mkojo

Mama akiwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo mara kwa mara hapo awali, unaweza kumpatia matibabu ya kinga pamoja na antibiotiki ili kuzuia maambukizi zaidi wakati wa ujauzito. Kipimo ni:

Amoxicillin: Miligramu 250 mara moja kupitia kinywa kila siku wakati wa kulala hadi mwisho wa ujauzito na kwa wiki 2 baada ya kuzaa.

Ikiwa matibabu ya antibiotikiyatashindwa kutibu dalili za maambukizi au mama akipata maambukizi mengine ya kibofu cha mkojo baadaye katika ujauzito, mpe rufaa kwenye Kituo cha Afya kwa uchunguzi. Anaweza kuhitaji matibabu na antibiotiki mbalimbali.

18.4 Hitimisho

Malaria, anemia na MNM ni tatu kati ya matatizo ya kawaida ya ujauzito. Katika kipindi hiki umejifunza jinsi ya kutambua, kukinga na kuyatibu. Katika vipindi vitatu vifuatavyo, utajifunza kuhusu matatizo mengine matatu ya afya yanayotishia maisha ya kina mama wajawazito yasipotambuliwa na mama kupewa rufaa mara moja: matatizo ya shinikizo la damu (Kipindi cha 19), kutokwa na damu mwanzo wa ujauzito (Kipindi cha 20), na kuvuja damu baada ya ujauzito (Kipindi cha 21).

Muhtasari wa Kipindi cha 18

Katika Kipindi cha 18, umejifunza kwamba:

 1. Malaria inasababishwa na parasiti ambayo huenezwa na mbu.
 2. Mjamzito aliye na maambukizi ya malaria ana uwezekano zaidi wa kuwa na anemia, kuharibika kwa mimba, kuzaa kabla ya wakati, mtoto mdogo, mtoto kufa kabla ya kuzaliwa), au afe yeye mwenyewe.
 3. Ni muhimu kwa wajawazito kuepukana na malaria - kwa mfano kwa kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua wadudu - na kutibiwa haraka akiugua.
 4. Dawa za kutibu malaria zinaweza kuwa na gharama kubwa na madhara lakini dawa hizi ni salama zaidi kuliko kupatwa na ugonjwa wa malaria hasa wakati wa ujauzito. Dawa ya kawaida ya kutibu malaria ni Coartem.
 5. Ayoni husaidia damu kubeba oksijeni kutoka kwa hewa tunayopumua hadi sehemu zote mwilini. Ayoni kidogo katika mlo wa mjamzito inamaanisha atakuwa na pumzi kwa sababu ana anemia.
 6. Kina mama walio na anemia wana nguvu kidogo ya kuzaa na wana hatari ya kuvunja damu sana, kuugua au hata kufariki baada ya kuzaa.
 7. Kula lishe iliyo na ayoni na folate na kutumia madini hayo muhimu kwa tembe kila siku wakati wa ujauzito inaweza kuzuia anemia na kutibu hali za anemia sizizo kali.
 8. Njia ya mkojo hujumuisha figo, mishipa ya figo, kibofu cha mkojo na urethra. maambukizi katika njia ya mkojo ni ya kawaida wakati wa ujauzito na yanaweza kuzuiliwa kwa usafi.
 9. Maambukizi ya kibofu cha mkojo na figo yanaweza kuwa hatari kwa mama na pia kusababisha leba kuanza mapema mno yasipotibiwa mara moja. Unywe vinywaji safi na bora mara nyingi ya kutosha kuondoa bakteria mwilini.
 10. Kuwasha au uchungu wakati wa kukojoa ni dalili ya kawaida ya maambukizi ya kibofu cha mkojo, maambukizi ya kibofu yasiyo makali yanayoweza kutibiwa kwa antibiotiki. Antibiotiki ya kawaida katika kituo cha ngazi ya chini za afya ni Amoxicillin.
 11. Maambukizi ya figo hasa ni hatari na mama lazima wapewe rufaa mara moja akiwa na mkojo unayofanana na mawingu au ukiwa na damu, joto jingi mwilini na maumivu katika upande wa chini wa mgongo.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi 18

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, unaweza kutathmini ulivyofaulu kutimiza Malengo ya Somo kwa kujibu maswali haya. Andika majibu yako katika shajara yako ya somo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Mkutano ujao wa Somo Saidizi. Unaweza kulinganisha majibu yako na matini kuhusu Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 18.1 (yanatathmini Malengo ya Somo 18.1, 18.2 na 18.3)

Ni taarifa zipi kati ya zifuatazo zisizokweli? Katika kila hali, eleza kile kilicho sahihi.

 • A.Hatari ya MNM inaweza kupunguzwa kwa kunawa mikono na kuosha sehemu za siri vizuri.
 • B.Mama anaweza kupata maambukizi ya urethra, kibofu cha mkojo, au ya figo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine.
 • C.Ni muhimu kumpatia mama tembe za ayoni ili kukinga anemia katika ziara ya kwanza ya huduma ya ujauzito.
 • D.Kumshawishi mama aliye na MNM anywe glasi 1 ya viowevu kila saa kabla hajala husaidia kupunguza maambukizi ya kibofu cha mkojo.
 • E.Malaria katika ujauzito huhusishwa na ongezeko la hatari ya kutoka kwa mimba pekee yake na mtoto kufa kabla ya kuzaliwa.
 • F.Maziwa ina folate nyingi, hivyo ukinywa maziwa mengi wakati wa ujauzito inaweza kukinga anemia.
Answer

A ni sahihi. Hatari ya MNM inaweza kupunguzwa kwa kunawa mikono na kuosha sehemu za siri vizuri.

B ni sahihi. Mjamzito anaweza kupata maambukizi ya urethra, kibofu cha mkojo, au ya figo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine.

C si sahihi. Tembe za ayoni zinapaswa kutolewa wakati wa kila huduma ya ujauzito ili kukinga anemia - si tu wa kwanza.

D ni sahihi. Kushawishi mama aliye na MNM anywe glasi 1 ya viowevu kila saa kabla hajalala husaidia kupunguza maambukizi kwenye kibofu cha mkojo.

E ni sahihi. Malaria katika ujauzito huhusishwa na ongezeko la hatari ya utokaji wa mimba bila hiari na kufa kwa mtoto kabla ya kuzaliwa.

F si sahihi. Maziwa ni nzuri kwa kina mama wajawazito kama sehemu ya lishe bora, lakini haina folate; kwa hivyo anatakiwa kula samaki wengi, maharagwe, mbaazi, mboga yenye rangi ya kijani kibichi, nyama nyekundu, mchele ya rangi ya hudhurungi, ngano nzima, uyoga, na mayai ili kuongeza folate katika mlo wake.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 18.2 (yanatathmini Malengo ya Somo 18.1, 18.4, 18.5 na 18.6)

Kamilisha visanduku vilivyotupu katika Jedwali 18.1.

Jedwali 18.1 la Swali la Kujitathmini 18.2.
Hali ya afyaIshara na dalili
Malaria
Anemia
Maambukizi ya kibofu cha mkojo
Maambukizi ya figo
Answer

Jedwali 18.1 Toleo lililokamilishwa linaonekana hapa chini.

Jedwali 18.1 Ishara na dalili za kawaida za ujauzito-zinazohusiana na matatizo ya afya
Hali ya afyaIshara na dalili
MalariaBaridi, kutetemeka, maumivu ya kichwa, udhaifu, joto jingi mwilini ikibadilishana na baridi, kutokwa na jasho joto inapopungua, wakati mwingine kuhara/kutapika, maumivu ya misuli/viungo. Uchunguzi wa damu unaonyesha kuwepo kwa parasiti ya malaria.
AnemiaWeupe, kupumua kwa haraka (ugumu wa kupumua), mpigo wa haraka wa mshipa (zaidi ya mipigo 100 kwa dakika), udhaifu, kizunguzungu, kuzirai mara kwa mara. Uchunguzi wa damu unaonyesha kuna upugufu wa hemoglobini.
Maambukizi ya kibofu cha mkojoHisia ya kukojoa kila mara, uchungu au maumivi wakati wa kukojoa, maumivu katika tumbo upande wa chini. Bakteria huonekana kwa uchunguzi wa mkojo.
Maambukizi ya figoKama ilivyo kwa maambukizi ya kibofu cha mkojo, pamoja na mkojo wa rangi ya mawingu au damu kwa mkojo, joto jingi mwilini, kujihisi mgonjwa sana au mdhaifu, maumivu kwa ubavu katika pande moja au zote mbili ambayo haihuondolewi kwa kusugua, kutapika mara kwa mara, baridi na kutetemeka sana.

Mwisho wa jibu