Skip to main content
Printable page generated Monday, 8 Aug 2022, 22:48
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Monday, 8 Aug 2022, 22:48

21. Kuvuja Damu katika Awamu za Mwisho wa Ujauzito

Kipindi cha 21 Kuvuja Damu katika Awamu za Mwisho wa Ujauzito

Utangulizi

Kuvuja damu baada ya wiki 28 za ujauzito hukisiwa kuwa kuvuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito. Ulijifunza kuhusu kuvuja damu katika awamu za mwanzo kabla ya wiki 28 za ujauzito katika Kipindi cha 20. Kuvuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito pia hujulikana na madaktari na wakunga kama kuvuja damu kabla ya kuzaa. Hali hii ni kisababishi kikuu cha vifo vya kina mama na fetasi, hivyo huhitaji usaidizi wa mtaalamu wa huduma ya afya haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya mwanamke na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.

Wewe kama mhudumu wa afya wa kwanza kufikiwa na wanawake wajawazito katika jamii yako, unapaswa kushirikiana nao katika maandalizi ya kuzaa na kufanya mpango unaoshugulikia matatizo yoyote katika ujauzito, kama vile kuvuja damu kwa wingi. Unapaswa kutoa huduma ya kwanza ya kiukunga kisha uhakikishe kuwa mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito amefikishwa kituoni cha afya ili apate huduma ya dharura. Hospitali ya Wilaya au Kituo cha Afya chenye uwezo wa kufanya upasuaji wa kiukunga kinaweza kuokoa maisha yake.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 21

Baada ya kukikamilisha kipindi hiki unatarajiwa:

21.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Maswali ya Kujitathmini 21.2 na 21.3)

21.2 Kufasili kuhusu dalili za hatari na visababishi vya mara nyingi vya kuvuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito. (Maswali ya kujitathmini 21.1, 21.2 na 21.3)

21.3 Kutoa huduma ya kwanza ya ukunga na kutambua wakati wa kupendekeza rufaa kwa mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito. (Maswali ya Kujitathmini 21.1 na 21.2)

21.1 Kuvuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito husababishwa na nini?

Kuvuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito au kuvuja damu kabla ya kuzaa mara nyingi husababishwa na kuvuja damu kutoka kwa plasenta, ingawa kuna visababishi vingine vichache vinavyotokea katika uterasi au sehemu zingine za mfumo wa uzazi. Kwanza, tutaorodhesha visababishi hivi kwa ufupi, kisha kufasili kwa kina kuhusu plasenta kujitenga kutoka pembezoni mwa uterasi, privia ya plasenta na kupasuka kwa uterasi, kwa sababu hizi ni hali zinazohitaji huduma ya dharura ili kuokoa maisha.

 • Kutengeka kwa plasenta: hali hii hutokea iwapo plasenta itatengeka kabla ya wakati (mapema sana) kutoka kwenye sehemu yake ilipojibandika kwa kawaida katika thuluthi mbili juu ya uterasi.
 • Privia ya plasenta: hali hii hutokea wakati plasenta imejibandika katika sehemu ya chini sana ya uterasi, ikikaribia seviksi sana, au hata kuifunika.
 • Kupasuka kwa uterasi: hali hii inaweza kutokea iwapo leba itadumu kwa muda mrefu au leba itazuiliwa, ambapo uterasi huraruka au kupasuka baada ya majaribio mengi ya kusukuma fetasi.
 • Kupasuka kwa vena ya varikosi katika eneo la uke: hii hutokea iwapo vena imejipinda na kupanuka. Hivyo basi, uterasi inaweza kujeruhiwa kwa urahisi na kuvuja, hasa katika leba na kuzaa.
 • Utetelezi mkuu: ute uliochanganyika na damu unaotoka ukeni kuashiria mwanzo wa leba huitwa utetelezi; wakati mwingine, kizibo hiki cha ute kinapotoka kinaweza kufuatiwa na uvujaji mkubwa wa damu unaoitwa utetelezi mkuu, ambao hukoma peke yake bila usaidizi wowote. Hata hivyo, mama anapaswa kupendekezewa rufaa kila wakati.

21.2 Kutengeka kwa plasenta:

Kutengeka kwa plasenta: humaanisha kutengeka kwa kipande cha plasenta au plasenta yote iliyojibandika kwenye sehemu ya thuluthi mbili za juu ya uterasi kabla ya wakati. Kwa kawaida, plasenta hutengana na uterasi baada ya kutolewa kwa fetasi, katika awamu ya tatu ya leba (Utajifunza kuhusu haya yote katika Moduli ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa). Mama na mtoto wanaweza kufa ikiwa sehemu ambapo plasenta ilitengana na pembezoni mwa uterasi itaanza kuvuja damu.

 • Ni kwa nini kuna uwezekano wa kuvuja damu sana ikiwa plasenta itatengana na pembezoni mwa uterasi kabla ya wakati? Ni kwa nini tukio hili huhatarisha maisha ya mama na fetasi? (Rejelea uliyoyasoma kuhusu muundo wa plasenta katika Kipindi cha 5 au uutazame tena Mchoro 5.5 katika Utunzaji kabla ya Kuzaa, Sehemu ya 1.)

 • Damu ya mama hutiririka hadi kwenye nafasi kubwa katika plasenta; sehemu zinazopakana na mishipa ya damu ya fetasi (Mchoro 5.5). Ikiwa plasenta itatengeka kutoka pembezoni mwa uterasi, damu ya mama itatiririkia kwenye uwazi wa uterasi, hivyo anaweza kufa kufuatia kupoteza damu nyingi. Kiwango cha virutubishi na oksijeni kinachoifikia fetasi kutoka katika damu ya mama kitapunguka, hivyo fetasi inaweza kufa au ubongo wake kuharibika.

  Mwisho wa jibu

Damu nyingi inayovuja kwenye sehemu ambapo plasenta imetengana na pembezoni mwa uterasi inaweza kupitia seviksi kisha kutiririkia ukeni. Damu hii kwa kawaida huwa na uweusi kwa kukosa oksijeni ya kutosha. Hii ni dalili kuu ya hatari.

Mchoro 21.1 Kuvuja damu kufuatia kutengeka kwa plasenta pembezoni mwa uterasi.

Hata hivyo, katika baadhi ya matukio, damu yote kutoka katika sehemu ambapo plasenta imejitenga inaweza kusalia ndani ya uterasi, kisha kuanza kujaa (Mchoro 21.1) Damu haitaonekana ikitokea ukeni kwa sababu kiasi kidogo sana cha damu hupenyeza na kutokea ukeni. Hata hivyo, mwanamke ataonyesha ishara za kuvuja damu ndani ya uterasi, ziitwazo mshtuko unaohusiana na kuvuja damu. Tulijadili hali hii kwa muhtasari katika Kipindi cha 20 kuhusu kuvuja damu katika nyakati za mwanzo za ujauzito. Tutarudia habari inayofuata hapa (Kitengo 21.2.1) kwa sababu kuna hatari zaidi ya mshtuko huu kutokea ikiwa mwanamke atavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito.

Dalili zingine za kutengeka kwa plasenta ni pamoja na:

 • Ikiwa mama tayari yuko katika leba, tambua kama ana uchungu kati ya mikazo, ambao unazidi kuwa mbaya wakati upitapo.
 • Fumbatio lake ni gumu, lina kidonda na ni chungu likiguswa.
 • Mpigo wa moyo wa mtoto unaweza kuwa wa kasi mno (zaidi ya midundo 180 kwa dakika), au wa chini sana (chini ya midundo 100 kwa dakika), au ikiwa mpigo wa moyo wa fetasi hausikiki, mtoto anaweza kuwa amekufa.
 • Mtoto hasikiki akicheza au anacheza mara chache.

21.2.1 Mshtuko unaohusiana na kuvuja damu

Hali zote zinazotokea kufuatia kutengeka kwa plasenta zinakuhitaji uchukue hatua ya dharura: tazama Kitengo 21.5.

Tukio la kutengeka kwa plasenta linaloambatana na kuvuja damu nje au ndani ya uterasi linaweza kusababisha mshtuko unaohusiana na kuvuja damu, ambapo damu huvuja kwa kiasi kikubwa hivi kwamba damu inayosalia katika mishipa ya mwanamke haitoshi kufikisha virutubishi na oksijeni inayohitajika kwenye seli zake.

 • Dalili za mshtuko unaohusiana na kuvuja damu ni zipi? (Rejelea Kisanduku cha 20.3 katika kipindi cha awali)

 • Mwanamke mwenye mshtuko ataparara na kulowa jasho huku akiwa na mrindimo hafifu lakini wa kasi (zaidi ya midundo 100 kwa dakika), kupumua kwa haraka, shinikizo la chini la damu au linaloshuka (shinikizo la kidiastoli — kiwango cha chini — halizidi 60 mmHg na wakati mwingine ni la chini sana); anasema ana kizunguzungu; anaonekana kuchanganyikiwa na hata kupoteza fahamu.

  Mwisho wa jibu

Unapaswa kutambua dalili kama vile kuparara: kucha, viganja vya mikono na sehemu ya ndani ya kigubiko cha macho huendelea kuwa nyeupe pindi anavyoendelea kupoteza damu. Mwanamke huyu anaweza kukwambia kuwa anachoka au kushindwa kuinua kichwa chake. Yeye pia huonekana kutotulia, pengine anaomba kunywa maji, na anaonekana kuchanganyikiwa. Kuchanganyikiwa hutokea kwa sababu ubongo haupati oksijeni ya kutosha. Madhara ya mshtuko yanayotokea mara nyingi kufuatia kuvuja damu ni pamoja na figo au moyo kushindwa kufanya kazi.

21.2.2 Hali kali ya kushindwa kwa figo

Kufuatia mshtuko huu na kupungua kwa kiwango cha damu inayotiririkia kwenye figo, figo zinaweza kushindwa kufanya kazi. Hivyo basi, mwanamke hutoa kiasi kidogo sana cha mkojo, hivyo taka ambalo lingeondolewa na figo kutoka kwenye damu kisha kuondolewa mwilini kwa mkojo husalia kwenye damu. Kulimbikazana kwa taka katika damu humfanya mwanamke kudhoofika kwa haraka, na kifo hufuata iwapo hali hii haitakabiliwa. Hali hii huitwa hali kali ya kushindwa kwa figo ('kali' humaanisha kuwa hali hii huwa hatari kwa maisha kwa ghafla).

21.2.3 Kushindwa kwa moyo

Mwanamke akivuja damu, moyo wake hupiga kwa kasi ukijaribu kufikisha damu ya kutosha kwenye sehemu muhimu za mwili, kama vile ubongo. Ikiwa amevuja damu nyingi, moyo wake hautaweza kupiga kwa kasi ifaavyo hadi kutosheleza kiwango cha damu kinachopotea, hivyo atakumbwa na hali ya kushindwa kwa moyo. Hii ni hali ambapo moyo hushindwa kufikisha damu ya kutosha kwenye tishu, hivyo kifo kinaweza kutokea.

21.3 Privia ya plasenta

Kisababishi kingine cha kuvuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito ni privia ya plasenta. Katika hali hii, plasenta huwa imejibandika karibu sana na seviksi, au hata kuifunika (Mchoro 21.2). Seviksi inapoendelea kupanuka, ncha ya plasenta inaweza kutengeka na kuanza kuvuja damu. Mwanamke mwenye hali hii kwa kawaida huwa na damu yenye rangi ng'avu nyekundu inayovujia ukeni. Kiwango cha damu inayovuja kinaweza kuwa cha chini ikilinganishwa na ile inayovuja kufuatia kutengeka kwa plasenta, lakini katika baadhi ya matukio, hali hii inaweza kuwa kali na hatari kwa maisha. Kuvuja damu mara nyingi huwa hakuandamani na uchungu, hivyo mwanamke anaweza kutotambua kwa muda mrefu, kwa mfano, usiku akilala. Kuvuja damu kunaweza kuanzishwa na ngono na kunaweza kurejea kila mara (kukikoma kisha kuanza tena).

Mchoro 21.2 Privia ya plasenta imeainishwa kulingana na jinsi ncha ya plasenta imekaribia seviksi. (a) Privia ya chini ya plasenta, lakini haikuziba seviksi.(b) Privia ya plasenta ya kadri. (c) Privia ya plasenta kamilifu.

Katika mwanamke aliyevuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito kufuatia privia ya plasenta, uterasi mara nyingi huwa laini kwa kumpapasa fumbatio. Hali hii ni kinyume na uterasi iliyo gumu wakati kuvuja damu kumesababishwa na kutengeka kwa plasenta.

Kwa kijumla, kichwa cha fetasi hakiko katika sehemu ya chini ya uterasi, ambayo utahisi ikiwa tupu. Hali hii ya mtoto kutanguliza vibaya inaweza kuwa dalili ya privia ya plasenta. Kwa kawaida, hali ya fetasi ni ya kawaida, hivyo unaweza kuhisi mpigo wa moyo wa fetasi ukisikiliza kwa fitoskopu. Mama pia huhisi fetasi ikicheza kama kawaida — lakini hali hii huwa tofauti wakati mwingine.

Utambuzi wa privia ya plasenta unaweza tu kuthibitishwa kwa kumchunguza mama kwa mtambo wa pichatiba unaoweza kuonyesha hali ya plasenta, au kwa kuchunguza uke katika chumba cha upasuaji. Kwa hivyo, unapaswa kumpendekezea rufaa hadi kituo cha afya kilicho na vifaa vinavyohitajika kufanyia utambuzi.

Wanawake wanaoshukiwa kuwa na privia ya plasenta wanapaswa kuhamishwa hadi katika Hospitali ya Wilaya au Kituo cha Afya chenye mtambo wa pichatiba au chumba cha upasuaji.

Usimchunguze uke wewe mwenyewe iwapo mwanamke anavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito. Hatua hii huzidisha hali hii na kuongeza hatari kwake na fetasi.

21.4 Uterasi iliyopasuka

Kuvuja damu kufuatia kupasuka uterasi kunaweza kutokea kupitia ukeni, hivyo unaweza kuona damu ikitiririka nje, au uterasi inaweza kuvujia damu ndani ya fumbatio ambapo haitaweza kuonekana. Ikiwa mwanamke mwenye leba iliyodumu kwa muda mrefu ataanza kuhisi maumivu katika fumbatio, (mauvimu yanayoendelea na kuzidishwa na mwendo wowote), au uterasi ikikoma kukazana katika jaribio la kumsukuma mtoto, au damu kuanza kuvuja ukeni ikiandamana na mshtuko, kuna uwezekano kuwa uterasi imepasuka. Ikiwa uterasi itakoma kukazana, fumbatio litakuwa laini na utaweza kuzihisi sehemu za mwili wa mtoto kwa urahisi kwa kulichunguza fumbatio. Ikiwa mtoto amekufa, hutaweza kusikia mpigo wa moyo wake hata kwa fitoskopu.

Utajifunza kwa kina kuhusu hali ya kupasuka uterasi katika Moduli inayofuata katika mtaala huu, kuhusu Utunzaji katika Leba na Kuzaa. Unapomhudumia mwanamke mwenye dalili za kupasuka uterasi, unafaa kuchukua hatua za dharura kama inavyoelezwa hapa chini.

21.5 Jinsi ya kushughulikia mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito

Ukitambua kwamba mwanamke anavuja damu na unashuku kuwa ana plasenta iliyotengeka, privia ya plasenta, uterasi iliyopasuka, au kuvuja damu kufuatia visababishi vingine, chukua hatua hizi:

 • Usimchunguze ukeni
 • Tathmini kwa haraka hali zote za mwanamke, pamoja na dalili muhimu: mrindimo, shinikizo la damu, pumzi na halijoto, baini kama ameparara, ana uchovu, kizunguzungu, na kuchanganyikiwa.
 • Ukikisia kuwa ana mshtuko, anza matibabu haraka iwezekanavyo kwa kumdungia viowevu vya Chumvi ya Kawaida au mchanganyiko wa kiowevu cha laktesi ya Ringer ndani ya mishipa. (Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika somo la nadharia katika Kipindi cha 22 na kuukuza ustadi wako katika mafunzo ya kiutendaji.)
 • Hata ikiwa hakuna ishara za mshtuko, utilie mshtuko maanani huku ukiendelea kutathmini hali ya mwanamke kwa kuwa inaweza kubadilika ghafla. Ikiwa mshtuko utatokea, chukua hatua zilizoelezwa hapo juu.
 • Kwa haraka, watafute watu wakusaidie, wajulishe kuhusu uzito wa hali hiyo na utekeleze mpango wa kushughulikia matatizo ambao uliandaa wewe na mwanamke kama sehemu ya utunzaji maalum katika ujauzito (Kipindi cha 15 cha Moduli hii). Kwa mfano, watafute wanakijiji wakusaidie kumsafirisha haraka hadi kituo cha juu cha afya; hakikisha kuwa watu wenye afya njema wameandamana naye ili kumtolea damu iwapo atahitaji.

Kumbuka kuwa damu inayovuja mwanzoni inaweza kuwa nyingi sana na hatari kwa maisha, hivyo mwanamke anaweza kufika katika Kituo cha Afya akibebwa na jamaa zake. Katika hali hiyo, baada ya kufanya uchunguzi wa haraka wa hali ya mgonjwa, andaa mrija wa kudungia dawa mishipani, andaa usafiri kisha umpe rufaa haraka iwezekanavyo hadi katika kituo cha afya kilicho karibu.

 • Ni hali gani salama zaidi ya kumsafirisha mwanamke? (Rejelea Mchoro 20.3 katika kipindi cha awali)

 • Mwanamke anapaswa kukilaza kichwa chake bapa — usiweke mto chini ya kichwa chake. Mwinue magoti na umwegemeze miguuni kwa kutumia mto au blanketi iliyokunjwa, ili miguu iinuke zaidi ya kichwa chake.

  Mwanamke anapaswa kupendekezewa rufaa kila mara na ni muhimu azalie katika kituo cha hali ya juu zaidi iwapo atavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito, hata ikiwa damu itasita kuvuja bila usaidizi wowote kabla ya leba kuanza.

  Mwisho wa jibu

Kwa kawaida, unapaswa kuandamana na mwakamke huyu ili kudhibiti viowevu alivyotiwa na uhakikishe kuwa umeshikilia kifuko cha kiowevu juu yake. Iwapo hutaweza kwenda naye, mweleze mtu atakayeandamana naye umuhimu wa kudumisha hali ya mwanamke na kifuko katika namna iliyoelezwa; pia mweleze mtu huyu jinsi ya kufunga sindano ya kutia viowevu mishipani wakati viowevu vilivyo katika kifuko vitamalizika. Kumbuka kumpa mwanamke huyu barua ya rufaa.

Katika kipindi cha mwisho cha Moduli hii, tunakufunza kwa nadharia jinsi ya kutayarisha viowevu vinavyotiliwa mishipani, na jinsi ya kuingiza katheta ya mkojo kwa mwanamke asiyeweza kukojoa kwa sababu ya matatizo ya ujauzito au leba.

Muhtasari wa Kipindi cha 21

Katika kipindi cha 21, umejifunza kwamba:

 1. Kuvuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito kunaweza kusababisha kifo cha mama na fetasi, hivyo hali hii inapaswa kuchukuliwa kama jambo la dharura linaloweza kuhatarisha maisha.
 2. Visababishi vya mara nyingi vya tukio la kuhatarisha maisha la kuvuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito ni kutengeka kwa plasenta kabla ya wakati, na privia ya plasenta, au kwa nadra sana linaweza kutokea kufuatia kupasuka uterasi.
 3. Hali isiyo kali sana ya kuvuja damu inaweza kutokea kufuatia vena ya varikosi ukeni, au damu kutokana na utetelezi mkuu, ambao husita bila usaidizi wowote.
 4. Kutengeka kwa plasenta kabla ya wakati kunaweza kutokea kama hali fiche ya kuvuja damu (kuvujia ndani) au hali wazi (damu inaonekana kwa nje) kutoka ukeni; damu hii kwa kawaida huwa na uweusi na mwanamke anaweza kuwa na maumivu ya fumbatio.
 5. Privia ya plasenta mara nyingi hudhihirika kama damu yenye wekundu mng’avu na isiyosababisha maumivu, na inaweza kuhusishwa na utangulizi mbaya ya fetasi. Kwa kawaida, (lakini sio kila mara) fetasi huwa katika hali ya kawaida.
 6. Usimchunguze uke wa mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito kwa sababu unaweza kuzidisha kuvuja damu.
 7. Hatua za kwanza muhimu katika kudhibiti mshtuko unaohusiana na kuvuja damu katika wanawake wanaovuja damu sana katika awamu za mwisho za ujauzito ni kufanya ukadiriaji wa mwanzoni wa ishara muhimu na kuanzisha matibabu ya kutia viowevu mishipani.
 8. Baada ya kumtia viowevu mishipani, mhamishe mwanamke huyu haraka hadi katika Hospitali ya Wilaya au kituo cha afya kilicho na chumba cha upasuaji, kwa sababu visa vingi huhitaji upasuaji.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 21

Kwa sababu umekamilisha somo hili, unaweza kutathmini ulivyofanikisha Malengo yake kwa kujibu maswali yafuatayo. Andika majibu yako katika shajara kisha ujadiliane na Mkufunzi wako katika mkutano utakaofuata wa Somo saidizi. Unaweza kulinganisha majibu yako na vidokezo kuhusu Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa moduli hii.

Swali la Kujitathmini 21.1 (linatathmini Malengo ya Somo 21.2 na 21.3)

Jamaa wa mwanamke mmoja wamekuita kumhudumia mwanamke anayevujia damu ukeni katika miezi 8 ya ujauzito.

 • a.Utafanya nini katika uchunguzi wako wa kwanza?
 • b.Utamwanzishia matibabu ya dharura na kumpendekeza rufaa aende katika kituo cha afya kilicho karibu? Eleza ni kwa nini ndivyo au sivyo.
 • c.Utaawaambia jamaa zake wafanye nini?
Answer
 • a.Uchunguzi wa kwanza utakuwa kutathmini haraka hali zote za mwanamke, pamoja na ishara kuu: mdundo wa moyo, shinikizo la damu, pumzi na halijoto; mchunguze kama ana hali ya kuparara, uchovu, kizunguzungu, au kuchanganyikiwa.
 • b.Matibabu ya dharura yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo kwa kumtia mishipani kiowevu cha Chumvi ya Kawaida au mchanganyiko wa Laktesi ya Ringer. Hatua hii itaokoa maisha yake kwa kuongeza chumvi na viowevu vilivyopotezwa kufuatia kuvuja damu, hivyo shinikizo lake la damu halitashuka sana hadi kiwango cha hatari.
 • c.Jamaa zake wanapaswa kufahamishwa watayarishe chombo cha kumsafirisha mwanamke hadi katika kituo kikuu cha afya kilicho karibu.

Mwisho wa jibu

Maswali ya Kujitathmini 21.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 21.1, 21.2 na 21.3)

Ni maelezo yapi yafuatayo yasiyo ya kweli? Katika kila kauli, eleza lisilo la kweli.

 • A.Unaweza kumchunguza uke wa mwanamke mjamzito aliyekuja kwako akivujia damu ukeni katika wiki ya 37 ya ujauzito.
 • B.Kutengeka kwa plasenta kabla ya wakati wake kwa kawaida husababisha kuvuja damu inayotokea ukeni.
 • C.Privia ya plasenta hutokea iwapo plasenta imejibandika karibu na seviksi au kuifunika.
 • D.Ikiwa damu itakoma kuvuja bila usaidizi wowote, unaweza kutompendekezea rufaa mwanamke anayevuja damu sana katika awamu za mwisho za ujauzito, au ana kuvuja kunakorejea.
Answer

A si kweli. Haupaswi kamwe kumchunguza uke wa mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho wa ujauzito.

B si kweli. B Kutengeka kwa plasenta kutoka mahali pake pa kawaida kabla ya wakati kunaweza kusababisha damu kuvujia nje, lakini pia kunaweza kusababisha damu kuvujia ndani.

C ni kweli. Privia ya plasenta hutokea wakati plasenta imejibandika katika sehemu inayokaribia seviksi au kuifunika.

D sio kweli. D Unapaswa kila wakati kumpendekezea rufaa mwanamke anayevuja damu kwa muda mrefu katika awamu za mwisho za ujauzito hata ikiwa damu itakoma kuvuja bila usaidizi wowote.

Mwisho wa jibu

Soma Kauli ya Somo 21.1 kisha ujibu maswali yanayofuata.

Unchunguzi Maalum 21.1 Bi. X ameletwa katika Kituo cha Afya

Bi X ameletwa katika Kituo chako cha Afya akiwa amebebwa na jamaa zake huku amelazwa kwenye kitanda cha mbao cha kujitengenezea nyumbani. Unafahamishwa kuwa ana ujauzito wa miezi 9. Alianza kwa kuumwa na fumbatio kisha kuvuja damu ukeni. Unapomchunguza, unatambua kuwa nguo zake zimelowa damu. Ana wasi wasi na kiu. Mapigo yake ya moyo ni midundo 120 kwa dakika, na shinikizo la damu ni 80/50 mmHg.

Swali la Kujitathmini 21.3 (linatathmini Malengo ya Somo 21.1 na 21.2)

 • a.Ni visababishi vipi vinavyoweza kupelekea kisa hiki? Fafanua jibu lako.
 • b.Je Bi X yoko katika hali ya mshtuko? Thibitisha utambuzi wako.
Answer
 • a.Visababishi vinavyoweza kupelekea kisa cha Bi X ni:
  • Kutengeka kwa plasenta
  • Privia ya plasenta
  • Uterasi iliyopasuka
  • Kupasuka kwa vena ya varikosi.
 • b.Bi X yuko katika hali ya mshtuko: yeye hatulii na ana kiu, mrindimo wake ni wa kasi mno (midundo 120 kwa dakika) na shinikizo lake la damu liko chini sana hata kumhatarishia maisha (80/50 mmHg).

Mwisho wa jibu