Skip to main content
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 10:01 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 10:01 PM

1. Kutambua Leba ya Kawaida

Kipindi cha 1 cha somo Kutambua Leba ya Kawaida

Utangulizi

Kwa kawaida, mhudumu mmoja wa afya ndiye anayefuatilia mwanamke mjamzito na mtoto wake tangu kuzuru kliniki ya wajawajazito hadi baada ya kuzaa. Jambo hili huitwa ufuatilizi wa huduma. Ulisoma moduli kuhusu huduma ya Kabla ya Kuzaa. Sasa utajifunza kuhusu Utunzaji wa Leba na Kuzaa. Leba nijina linalopewa mabadiliko ya kianatomi na kifisiolojia katika mkondo wa uzazi wa mwanamke. Mabadiliko haya hufanyika ili kutayarisha fetasi na plasenta kwa utaratibu wa kuzaa. Mara nyingi, leba hutokea wakati mtoto ameumbika kikamilifu, kufikia hatima ya wakati anaofaa kukaa mwilini mwa mama, yaani kati ya wiki 37-40 za ujauzito. Leba huashiria mwisho wa kipindi cha mtoto kukaa uterasini na mwanzo wa maisha nje ya mwili wa mama.

Kipindi hiki cha kwanza cha somo kinatanguliza moduli ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa. Lengo kuu ni kukusadia kubainisha kati ya leba halisi na ile bandia. Utajifunza kutambua dalili za awamu nne za leba. Utajifunza kuhusu leba na utaratibu wa kuzaa ili uweze kufanya uamuzi sahihi na uwe na ujasiri unapozalisha. Pia utajifunza namna ya kumtayarisha mwanamke mjamzito kutambua mabadiliko mwilini mwake yanayoashiria kuwa leba iko karibu kuanza. Utajifunza jinsi ya kumwelimisha juu ya kutambua mwanzo wa leba halisi ili aweze kutafuta msaada wako kwa wakati unaofaa.

Matokeo ya Somo la Kipindi cha 1

Baada ya Kipindi hiki utaweza:

1.1 Kufasili na kutumia vizuri maneno ya kina yalioandikwa kwa herufi nzito. (MK 1.1, 1.2, 1.3, na 1.4)

1.2 Kueleza dalili za leba halisi na kubainisha kati ya leba halisi na bandia. (MK 1.2 na 1.3)

1.3 Kumweleza mama jinsi ya kutambua mwanzo wa leba. (MK 1.2)

1.4 Kueleza viashirio na utaratibu wa awamu nne za leba. (MK 1.4)

1.5 Kueleza awamu saba kuu ambazo mtoto hupitia anaposhuka kwenye njia ya uzazi wakati wa leba ya kawaida. (MK 1.4)

1.1 Asilia isiyodhahiri ya leba

Leba inaweza kuanza wakati wowote. Ukweli huu ni mojawapo ya asilia ya leba “isiyodhihirika” hivyo basi unapaswa kuwa tayari kila wakati kuchukua awamu ifaayo. Licha ya kuimarika kwa sayansi ya afya ya mama na fetasi, hakuna ajuaye wakati maalum wa kuanza kwa leba.

Tashwishi hii ndiyo husababisha mwanzo wa leba utarajiwe katika wiki mbalimbali. (Katika kiwango cha kituo cha afya, kipindi ambacho leba hutarajiwa kuanza ni wiki 37 – 40. Katika kiwango cha hospitali, leba inaweza kuanza katika wiki 37 – 42, huku mama na mtoto wakifuatiliwa kwa karibu kwa kutumia uchunguzi wa “ultrasound”). Kokotoa siku ya kuzaa inayotarajiwa, ambayo ni wiki 40 tangu hedhi ya mwisho ya mama, ikiwa anajua siku ambayo hedhi ilitokea. (Wanawake wengi hawajui tarehe yao ya hedi ya mwisho). Hata hivyo, mfahamishe kuwa kuna uwezekano asizae katika siku iliyotarajiwa. Takriban 2% tu ya wanawake huzaa katika siku iliyotarajiwa, hata kwa wanawake wanaojua tarehe halisi za hedhi ya mwisho. Hivi ni baadhi ya viashirio vya leba visivyodhirika:

  • Ni nini huanzisha au kuchochea leba? Je, ni vipengele vinavyohusu fetasi, mama au wote wawili?
  • Kwa nini baadhi ya wanawake huanza leba kabla ya wakati sahihi.
  • Ni kwa nini matatizo ya leba yasiyotabiriwa hutokea?

Acha maswali hayo bila kuyajibu, kisha uzingatie leba inayotokea katika kipindi maalum.

1.1.1 Leba ya kawaida

Leba ya kawaida huwa na viashirio hivi:

  • Kuanza kighafla. (Leba ya kawaidahuanza kivyake bila usaidizi wowote wa kimatibabu)
  • Mikazo ya uterasi huwa yenye utaratibu na mpangilio maalum.
  • Mtoto kutanguliza utosi. (Utosi wa mtoto hutanguliza kupitia kwenye uwazi wa seviksi, kama vile ulivyojifunza katika Kipindi cha 6 cha moduli ya Utunzaji Katika Ujauzito.
  • Kuzaa kupitia uke hufanyika bila usaidizi wa kitaalam kwa muda wa chini ya saa 18 kwa mwanamke anayezaa kwa mara ya kwanza (mwanamke primigravida). Kwa mwanamke anayejifungua kwa mara ya pili (au zaidi) (maltigravida), kuzaa kupitia uke hutokea bila usaidizi zaidi wa kitaalam kwa muda wa chini ya saa 12.
  • Hakuna matatizo kwa mama ama fetasi.

Leba yoyote inayohitilafiana na viashirio hivi si ya kawaida. Leba isiyo ya kawaida huitaji kushughulikiwa na mtaalam. Vipindi vya 8 -11 vinaelezea jinsi ya kushugulikia aina mbalimbali za leba isiyo ya kawaida. Baadaye, utajifunza kuhusu dalili zinazokuashiria wewe na mama kuwa leba halisi imeanza.

1.2 Utajuaje kuwa leba halisi imeanza?

Wakati wa leba halisi, mikazo ya uterasi huwa yenye utaratibu, inayofuata mtindo maalum na yenye nguvu. Mikazo hii huongezeka na haiwezi kupunguzwa kwa dawa za kutuliza maumivu. Ikiwa mwanamke atatumia dawa za kutuliza maumivu, dalili za uchungu zinaweza kutulia kidogo, lakini leba halisi bado huendelea.

1.2.1 Mikazo tosha ya uterasi ni nini?

Wakati wa leba halisi, mikazo tosha ya uterasi hutokea. Mikazo ya uterasi hutathminiwa kwa kuzingatia viashirio vitatu: idadi ya marudio, muda inayochukua na makali ya mikazo:

  • Idadi ya marudio ya mikazo ya uterasi ni mara 3-4 kila dakika 10.
  • Kila mkazo huchukua sekunde 40-60, ambazo huitwa muda wa mikazo.
  • Mwanamke anasema kuwa anahisi mikazo ikiwa na kishindo. Kishindo hiki huitwa makali ya mikazo.

Ili kukadiria makali ya mikazo ya uterasi, chunguza kwa kupapasa fumbatio la mwanamke katika sehemu ya fandasi (juu) ya uterasi. (Kupapasa ni kugusa kwa mikono yako ili kuhisi). Unaweza kupapasa sehemu za fetasi kati ya vipindi vya mikazo uterasi unapotulia na misuli ya pembezoni mwa uterasi imelainika. Hata hivyo, mikazo mikali inapoanza, pembezoni mwa fumbatio juu ya uterasi hukazana hivyo hautaweza kuhisi viungo vya fetasi kwa kupapasa. Ukifinya kwa nguvu ukitumia vidole, mama huhisi uchungu.

Katika Kipindi cha 4 ulijifunza jinsi ya kurekodi marudio, muda na makali ya mikazo kwenye chati iitwayo

1.2.2 Damu tetelezi na kuvuja kwa kiowevu cha amnioni

Mara nyingi wakati wa ujauzito, uwazi mwembamba ulio seviksini huwa umezibwa na utetelezi. Katika siku chache za mwishoni mwa ujauzito, seviksi inaweza kuanza kufunguka. Wakati mwingine utetelezi huu na matone ya damu hutoka ukeni. Mchanganyiko huu wa damu na utetelezi huitwa damu tetelezi. Damu tetelezi hii inaweza kutoka yote kwa mara moja kama kizibo, au kuvuja pole pole kwa siku kadhaa. Ukiona damu tetelezi, fahamu kwamba seviksi inaanza kulainika, kuwa nyembamba na kuanza kufitia (kufunguka). Usidanganyike kati ya damu tetelezina mchozo wa kawaida (unyevunyevu kutoka ukeni) ambao wanawake wengi huwa nao wiki mbili kabla ya leba kuanza. Mchozo huo mara nyingi huwa ni utetelezi mwangavu wala si mwekundu kutokana na damu.

Leba halisi inaweza kuanza iwapo damu tetelezi ipo au haipo, ama kiowevu cha amnioni kinavuja au hakivuji. Kiowevu cha amnioni ni majimaji yaliyo kwenye membreni zinazozingira mtoto. Katika sehemu nyingi za Afrika, watu hufikiria kuwa leba haiendelei ikiwa hawajaona kuvuja kwa kiowevu cha amnioni ama kabla au baada ya leba kuanza. Fikira hii si kweli. Si lazima damu tetelezi na kiowevu cha amnioni kutoka ili leba ianze au iendelee.

Ikiwa leba haijaanza wala kuendelea sana katika kipindi cha saa 6 baada ya “maji kupasuka”, mhamishe mwanamke hadi kituo cha juu cha afya haraka iwezekanavyo.

Mfuko wa maji unapopasuka (kupasuka kwa membreni za fetasi), kiowevu cha amnioni kinaweza kububujika kutoka ukeni au kuvuja polepole. Kwa wanawake wengi, mfuko huu hupasuka katika vipindi vya kwanza vya leba. Ikiwa membreni ya fetasi itapasuka kabla ya leba kuanza, leba inafaa kuanza punde. Ikiwa leba haitaanza katika kipindi cha saa 6 baada ya mfuko wa maji kupasuka, maambukizi yanaweza kuingia kwenye uterasi. Hatari hii ya maambukizi huongezeka pindi wakati unapopita baada ya membreni kupasuka. Ulijifunza kuhusu kupasuka kwa membereni kabla ya wakati katika Kipindi cha 17 cha moduli ya Utunzaji wa katika Ujauzito. Kumbuka kuwa “kabla ya wakati” inarejelea kupasuka kwa membreni ya fetasi kabla ya leba kuanza. Katika muktadha huu “kabla ya wakati” hairejelei wakati wa kupevuka kwa mtoto, ambao unaweza kuwa kabla ya, wakati wa, au baada ya kupasuka kwa mfuko wa maji.

Ni kawaida kwa membreni za fetasi kupasuka baada ya leba kuanza. Walakini, hata katika kauli ya kawaida kama hii, jitahadhari na hatari zinazoambatana na kuvuja kwa kiowevu cha amnioni.

  • Hebu waza tena juu ya ulichosoma kuhusu kupasuka kwa membreni kabla ya wakati unaofaa. Ni hatari gani zinaweza kutokea ikiwa maji yatavuja wakati mwanamke yuko katika leba?

  • Matatizo yanayoweza kutokea membrani za fetasi zinapopasuka wakati wa leba ni:

    • Maambukizi: “mlango” wa uterasi umefunguka nawe unachunguza pelvisi kwa vidole baada ya kuvaa glavu mikononi ili kubaini jinsi leba inavyoendelea. Usipozingatia usafi unaweza kusambaza maambukizi kwenye uterasi (utajifunza mengi zaidi katika vikao vya masomo vitakavyofuata katika Moduli hii). Hatari hii huenea zaidi iwapo kipindi cha leba kitarefuka.
    • Kitovu kinaweza kutoka (kusukumwa nje kabla ya mtoto huku maji yakibubujika kupitia kwenye seviksi). Isitoshe, kitovu kinaweza kunaswa katikati mwa pembezo ya endometria na mtoto ambaye amesita kuelea kwenye kiowevu cha amnioni. Ikiwa kitovu kimefinywa, mtoto anaweza kupata hipoksia (kiwango kidogo cha oksijeni). Mtoto anaweza kufariki ama ubongo wake kuathiriwa iwapo damu itakwama kwenye kitovu.

    Mwisho wa jibu

1.2.3 Tofautisha kati ya leba halisi na leba bandia

Hali inayojulikana kama leba bandia inaweza kutokea wiki moja au mbili kabla ya leba ya kweli. Wakati wa leba bandia, mwanamke huhisi mikazo isiyo na utaratibu na iliyo na uchungu kiasi kidogo kuliko wa wakati wa leba ya kweli. Kwa kawaida, mikazo hii haiendelei. Jedwali1. 1 inalinganisha viashirio vya leba ya kweli na ile bandia. Mwanamke anapokuwa na leba bandia, mhimize asife moyo. Mweleze kuwa ingawa angali hajapata leba halisi, dalili hizi zinaonyesha kuwa itaanza hivi karibuni. Mshauri kuhusu dalili za leba halisi. Mueleze akuite au aje katika Kituo cha Afya punde dalili za leba halisi zikijitokeza. Dalili za leba halisi zimeelezwa katika jedwali 1.1 na Kipindi kinachofuata.

Jedwali 1.1 Viashirio vya leba halisi na bandia
ViashirioLeba ya kweliLeba ya bandia
Mikazo ya uterasiMikazo hutokea ikifuata utaratibu maalum lakini muda baina ya kila mkazo hupungua polepole.Mikazo hutokea bila kufuata utaratibu wowote.
MudaMuda wa kila mkazo huongezeka polepole. Muda haubadiliki, aidha kuwa mrefu au mfupi
MikazoMikazo huongezeka kwa nguvu na kasi. Mikazo haiongezeki kwa vyovyote.
Kupanuka kwa seviksiSeviksi huendelea kupanuka. Seviksi haipanuki, hubaki chini ya sentimita 2.
MaumivuMaumivu ya mgongo, ambayo hayatulizwi kwa dawa zenye nguvu ya kutuliza maumivu makali. Maumivu hayapo katika mahali popote mahususi na kawaida hutulizwa kwa dawa za kutuliza maumivu ama kwa kutembea.

1.2.4 Kumsaidia mama kutambua leba halisi

Hakuna anayeweza kujua wakati leba itaanza. Hata hivyo, baadhi ya dalili huashiria kwamba itaanza punde. Mara nyingi, watoto hushuka chini ya fumbatio takriban wiki mbili kabla ya kuzaliwa, hali inayojulikana kama kusahaulika. Kwa kawaida, mwanamke atahisi kuwa mtoto “haelei” kwenye fumbatio, na hasukumi juu tumbo la mama. Ikiwa mwanamke aliwahi kuzaa, huyu mtoto huenda asishuke hadi wakati wa kuanza kwa leba.

Dalili nyingine zinaweza kuanza siku moja au mbili tu kabla ya kuanza kwa leba. Kinyesi cha mama kinaweza kubadilika ama kiasi kidogo cha damu tetelezi (damu iliyochanganyika na utetelezi) kinaweza kutoka kwenye uke. Wakati mwingine, mfuko wa maji hupasuka kabla ya leba kuanza.

Kutambua leba halisi si jambo rahisi kwa mama, hasa kama mimba hii ni ya kwanza. Anaweza kukuita au kuja kwenye kituo cha afya mara nyingi akifikiria kuwa maumivu madogo ni mwanzo wa leba halisi. Kumshauri mama na jamii yake kuhusu kujitayarisha kuzaa ni sehemu ya lengo la utunzaji kabla ya kuzaa. (Kipindi cha 13 cha Somo cha moduli ya Utunzaji wa kabla ya Kuzaa). Unapomfunza jinsi ya kutambua dalili za leba halisi na awamu anazohitaji kuchukua, tumia lugha anayoweza kuelewa. Mweleze bayana kuhusu jinsi atakavyohisi kwenye fumbatio lake. Wajibu wako ni muhimu. Unasaidia kupunguza wasiwasi wa mama kuhusu leba. Unaweza pia kumsaidia kupunguza gharama na muda anaopoteza anapotembelea kituo cha afya kwa sababu ya leba bandia au maumivu madogo.

Mweleze viashirio hivi vya leba halisi:

  • Uchungu wa kusukuma chini unaongezeka pindi wakati unavyoendelea. Uchungu huu hutokea mara 3-5 kila dakika 10. (Hakikisha kama anafahamu au anaweza kukadiria muda wa dakika 10).
  • Kwa kawaida mwanamke huhisi uchungu unaosukuma chini, kwanza katika sehemu ya chini ya mgongo. Uchungu huu huzunguka hadi katika sehemu ya chini ya fumbatio chini ya kitovu.

Mweleze mambo haya kwa kutumia fumbatio lake:

  • Kitakachotokea kwa sababu ya kusahaulika.
  • Sehemu atakayohisi ugumu kwenye fumbatio wakati wa mikazo.
  • Sehemu atakayohisi uchungu zaidi unaosukuma chini.

1.3 Awamu za leba

Katika Kipindi hiki, utajifunza mawaidha ya msingi kuhusu awamu za leba na kuzaa. Kila awamu imeelezwa waziwazi katika vikao vya masomo vitakavyofuata katika moduli hii. Leba imeainishwa katika awamu hizi nne.

  • Awamu ya kwanza ya leba ni wakati seviksi hufunguka.
  • Awamu ya pili ni wakati wa kusukuma, ambayo huisha mtoto anapozaliwa.
  • Awamu ya tatu ni kuzaliwa kwa kondo.
  • Awamu ya nne ni masaa manne ya kwanza baada ya kuzaa.

1.3.1 Awamu ya kwanza ya leba

Wakati wa awamu ya kwanza ya leba, seviksi hufunguka pole pole kiasi cha kuwezesha mtoto kutoka kwenye uterasi. Kwa muda mrefu wakati wa ujauzito, hakuna chochote kinachoweza kuingilia au kutokea kwenye seviksi kwa sababu uwazi huo mdogo huwa umezibwa na utetelezi.

Wakati wa ujauzito, seviksi huwa ndefu na imara, kama kidole gumba cha mguu (Mchoro 1.1a) Uterasi ikikazana, seviksi hupanuka huku sehemu ya chini ya uterasi ikifupika. Pembezo za seviksi huvutwa nyuma na juu pole pole. Utaratibu huu hujulikana kama kufitika (Mchoro 1.1b na c)

Mchoro 1.1 Kufitika kwa seviksi. (a) Kabla ya leba kuanza, seviksi haijafitika. (b) 60% ya seviksi imefitika. (c) Seviksi imefitika kabisa.

Seviksi hupanuka (kipenyo huongezeka pole pole), hali inayoitwa kupanuka kwa seviksi. Kila mara inapokazana, uterasi huvuta juu sehemu ndogo ya seviksi na kuipanua. Katikati ya mikazo seviksi hulegea. Awamu ya kwanza imegawanywa katika awamu mbili: awamu fiche na awamu wazi. Awamu hizi zinatambuliwa kulingana na kiwango ambacho seviksi imepanuka.

Awamu fiche

Awamu fiche ni kipindi kati ya mwanzo wa mikazo inayofuata utaratibu hadi seviksi inapopanuka kwa kiasi cha sentimita 4. Katika awamu hii, mikazo inaweza kuwa chungu au isiyo chungu, na seviksi hupanuka pole pole. Awamu fiche huisha wakati seviksi inapoanza kupanuka kwa haraka zaidi. Ongezeko hili la kasi huashiria mwanzo wa awamu wazi.

Awamu wazi

Awamu wazi huanza wakati seviksi imepanuka zaidi ya sentimita 4. Mikazo hii hutokea kwa utaratibu maalum, mara nyingi na huwa chungu. Seviksi hupanuka haraka zaidi. Kipenyo cha seviksi kinaweza kuongezeka kwa kati ya sentimita 1.2 na 1.5 kwa saa. Kima cha kupanuka kinafaa kuwa sentimita 1 kwa kila saa. Katika awamu hii, nakili data katika patografu. (Utajifunza nakili data hii katika Kipindi cha nne katika moduli hii)

Seviksi huendelea kupanuka hadi kufika kipenyo cha sentimita 10, yaani kupanuka kabisa. Seviksi iliyopanuka kabisa ni pana vya kutosha kupitishia mtoto (Mchoro 1.2). Seviksi ikiwa na kipenyo kiasi hiki, huwezi kuihisi juu ya kichwa cha fetasi ukichunguza seviksi kwa vidole vilivyovalishwa glavu. (Uchunguzi wa uke umeelezwa baadaye katika Moduli hii na umeonyeshwa jinsi ya kuchunguza katika vikao vya mazoezi)

Mchoro 1.2 Seviksi iliyopanuka kabisa ina kipenyo cha sentimita 10.

1.3.2 Awamu ya pili ya leba

Awamu ya pili ya leba huanza wakati seviksi imepanuka kabisa (sentimita 10) na kuisha mtoto anapozaliwa. Baada ya seviksi kupanuka kabisa, mama kawaida hupata hisia za kutaka kusukuma. Mama akisukuma kulingana na mikazo ya uterusi, mtoto huteremkia kwenye seviksi na kushukia ukeni. Mwendo huu wa mtoto hujulikana kama kushuka kwa fetasi. Kiwango cha kushuka kwa fetasi ni kiashirio muhimu cha jinsi leba inavyoendelea. Habari hii imeelezwa kwa kina hapo baadaye. Muda wa awamu ya pili ni wastani wa masaa 1-2. Jedwali 1.2 inaeleza kwa muhtasari ishara na dalili za awamu ya kwanza na ya pili ya leba ya kawaida.

Jedwali 1.2 Viashirio vya awamu ya kwanza na ya pili ya leba ya kawaida
Dalili na isharaAwamuAwamu
Seviksi haijapanukaLeba bandia, mwanamke hayuko katika leba
Mikazo ya uterasi isiyo taratibu wala mikaliLeba bandia, mwanamke hayuko katika leba
Mikazo ya uterasi iliyo taratibu lakini isiyo mikaliYa kwanzaFiche
Seviksi imepanuka kiwango cha chini ya sentimita 4. Mikazo ni taratibu na mikali
Seviksi imepanuka kwa sentimita 4-9
Kima cha kupanuka kawaida ni sentimita 1 kwa kila saa au zaidi Ya kwanzaWazi
Fetasi inaanza kuteremka. Seviksi imepanuka kabisa (sentimita 10)
Fetasi inaedelea kuteremka. Ya piliYa vipindi vya mwanzo (haipelekei kuzaliwa)
Mama hana hamu ya kusukuma. Seviksi imepanuka kabisa (sentimita 10)
Sehemu tangulizi ya fetasi imefika sehemu ya chini ya pelvisiYa piliYa vipindi vya mwisho (inapelekea kuzaliwa)
Mama hana hamu ya kusukuma

Kuzaliwa kwa mtoto ni ishara ya mwisho wa awamu ya pili.

1.3.3 Awamu ya tatu ya leba

Katika awamu ya tatu ya leba, plasenta na membreni hutoka baada ya mtoto kuzaliwa. Kwa kawaida, awamu ya tatu huchukua hadi dakika 30. (Utajifunza zaidi kuhusu awamu hii katika Kipindi cha 6 cha Somo kwenye moduli hii.)

1.3.4 Awamu ya nne ya leba

Saa 4 za kwanza punde baada ya plasenta kutoka huwa muhimu. Baadhi ya wataalam wamekipa kipindi hiki jina awamu ya nne ya leba. Mwanamke anaweza kuvuja damu kwa wingi baada ya plasenta kutoka. Hii hutokea iwapo mikazo ya uterasi inasababisha kutofungika kwa mishipa ya damu iliyofunguka kufuatia kubanduka kwa plasenta kwenye pembezoni mwa uterasi. Kwa hivyo, unafaa uwe makini ili kutambua na kuthibiti damu inayovuja baada ya kuzaa. Damu hii inaweza kuwa dhahiri au iliyofichika. (Utajifunza zaidi kuhusu kuvuja damu baada ya kuzaa katika Kipindi cha 11 cha Somo kwenye moduli hii. )

Chunguza plasenta, membreni na kodo. Hakikisha kuwa vyote hivi ni vizima na vya kawaida (Kipindi cha 6). Rekodi kiwango cha shinikizo la damu na mpwito wa mishipa ya mama baada ya kuzaa na kila baada ya dakika 15 kwa saa 4 za kwanza. Kwa kawaida, baada ya plasenta kutoka, uterasi huwa ngumu kwa sababu inaendelea kukazika. Mwanamke anaweza kuhisi mikazo mikali baada ya kuzaa. Mwakikishie kuwa mikazo hii ni salama na kwamba inaweza kusaidia kusitisha kuvuja kwa damu.

1.4 Utaratibu wa leba ya kawaida

Miendo saba mikuu ni mabadiliko ya hali ya mtoto, ambayo yeye hufanya ili kuweza kushukia kwenye njia ya uzazi. (Neno ‘mikuu’ humaanisha ”muhimu sana”). Hali ya mtoto kabla ya miendo kuanza imeonyeshwa katika Mchoro 1.3 (mchoro wa 1) na miendo yote saba imeonyeshwa katika michoro ya 2-8. Unaposoma maagizo yanayofuatia, tazama Mchoro 1.3 tena.

Mchoro 1.3 Hali ya kwanza na miendo saba kuu ya mtoto anaposhuka kwenye njia ya uzazi. Picha hizi ndogo zinaonyesha hali ya kichwa cha mtoto, kana kwamba unatazama kwenda juu ya njia ya uzazi. Rejeleo: Shirika la Afya Duniani, 2008, {1} Moduli ya Elimu ya Ukunga: Usimamizi wa Leba ya muda mrefu na Tata, toleo la 2, Mchoro 1.5, uk 23)

Mabadiliko ya hali ambayo mtoto hufanya huwa bayana, ya hiari na mahususi. Mabadiliko haya huwezesha hata kipenyo kidogo kabisa cha mtoto kipitie kwenye njia ya pelvisi ya mama. Mkunga na mama hawahusiki kwa vyovyote katika mabadiliko haya. Mtoto mwenyewe hufanya miendo hii saba kuu.

1.4.1 Kufungamana

Kufungamana ni utaratibu ambapo kichwa cha fetasi huingia kwenye uwazi wa pelvisi. (Mchoro 1.3, mchoro wa 2). Kipenyo cha parietombili ni kipimo kutoka ncha moja ya sikio hadi nyingine kupitia juu ya utosi wa mtoto (Mchoro 1.4). Kichwa hufungamana wakati kipenyo cha parieto mbili hushuka kwenye uwazi wa pelvisi, nacho kisogo kipo katika upeo wa mifupa ya iskiamu katika pelvisi ya mama (Mchoro 1.5).

Mchoro 1.4 Fuvu la kichwa cha mtoto linaweza kufinyangika wakati wa kushuka kwa mtoto. Katika mfano huu, mojawapo ya mifupa ya parieto hupishana na ule mwingine kwenye sucha ya sajita. Kisogo na kipenyo cha mifupa miwili ya parieto vimeonyeshwa.
Mchoro 1.5 Uwazi wa pelvisi, ukitazamwa kutoka juu. Tazama hali ya mifupa ya iskiamu.

1.4.2 Kushuka

Kushuka ni mwendo endelevu wa chini wa mtoto ambapo sehemu (kwa kawida kichwa) hutokezea kupitia pelvisi. Ni sharti mikazo ya uterasi iwe dhabiti na itokee kwa utaratibu maalum. Ni sharti kichwa cha mtoto na nafasi ya pelvisi ya mama vitoshane kwa ukubwa ili mtoto aweze kupitia. Mtoto huendelea kushuka kwenye nafasi ya ndani ya pelvisi.

Nafasi ya pelvisi imezungukwa na mifupa ya pelvisi. Uterasi inaposukumika chini kwa kishindo, mifupa ya skalpu ya mtoto hupishana mara kwa mara katika mistari ya sucha. Hii hufanyika ili kichwa kipitie kwenye nafasi hii ndogo. Utaratibu huu wa kupishana hujulikana kama kufinyangika. Aina za kufinyangika zinazofanyika mara nyingi ni:

  • Mojawapo ya mifupa ya parieto hupishana na ule mwingine kwenye sucha ya sajita. (Mchoro 1.4)
  • Mfupa wa kisogo hupishana na wa panja.
  • Mfupa wa mbele hupishana na mifupa ya parieto.

1.4.3 Kukunjika

Kukunjika ni wakati kichwa cha mtoto hujipinda hadi kidevu kikagusa kifua (Mchoro 1.3, mchoro wa 2). Kukunjika hutokea wakati wa kushuka, kichwa kinaposukuma tishu laini na mifupa ya pelvisi ya mama. Mabadiliko haya huwezesha hata kipenyo kidogo kabisa cha mtoto kipitie kwenye pelvisi ya mama.

1.4.4 Kuzungukia ndani

Ili kuona vipenyo vya pelvisi vya kuingilia na kutokea, tazama vielelezo 6.3 na 6.4 kwa moduli ya Huduma ya kabla ya Kuzaa, sehemu ya 1.

Kichwa cha mtoto kinapofika kwenye sehemu ya chini ya pelvisi (Mchoro 1.3, mchoro wa 3). Katika kiingilio cha pelvisi, kipenyo cha pelvisi ni kipana kuanzia pande ya kulia hadi kushoto. Kwenye tundu la kutokea la pelvisi, kipenyo cha pelvisi ni kipana kuanzia mbele hadi nyuma. Kwa hivyo ni lazima mtoto azunguke kutoka hali ya kulala kwa upande hadi atazame uti wa mgongo wa mama. (Mchoro 1.3, mchoro wa 4). Mtoto akishakamilisha kuzunguka, kisogo chake husukuma sehemu ya mbele ya pelvisi ya mama). Sucha ya sajita iliyo kwenye fuvu la kichwa cha fetasi haipo tena kwenye pembe. Sucha ya sajita huelekea chini kwenye uti wa mgongo wa mama. Mwendo huu unaitwa kuzungukia ndani kwa sababu unafanyika wakati mtoto angali ndani ya uterasi.

1.4.5 Kutandazika

Baada ya mwendo wa kuzungukia ndani kukamilika, kichwa cha mtoto hupitia kwenye pelvisi. Leba husita kidogo wakati shingo la mtoto lingali chini ya pindo la kinena la mama. Baadaye, kutandazika kwa kichwa na shingo za mtoto hufuata. Shingo linatandazika ili kuzuia kidevu kusukuma kifua cha mtoto. Kilele cha kichwa, uso, na kidevu huzaliwa (Mchoro 1.3, mchoro wa 4 na 5).

1.4.6 Kuzungukia nje (kurejea)

Baada ya kichwa cha mtoto kutoka, leba husita kwa muda mfupi. Wakati huu leba inaposita, sharti mtoto azunguke. Uso wa mtoto huzunguka kutoka kutazama uti wa mgongo wa mama hadi kutazama sehemu ya ndani ya mojawapo ya mapaja ya mama (Mchoro 1.3, mchoro wa 6). Mwendo huu huitwa kuzungukia nje kwa sababu sehemu moja ya mtoto tayari iko nje ya mwili wa mama. (Mwendo huu pia huitwa kurejea). Ni muhimu mtoto kuzunguka hivi ili kuwezesha mabega yake kutoshea kwenye pande zote na chini ya mfupa wa kinena wa mama.

1.4.7 Kutolewa

Punde tu baada ya kuzungukia nje, bega la juu la mtoto hutoka kupitia chini ya mfupa wa kinena wa mama (Mchoro 1.3, mchoro wa 7). Msamba wa mama hupanuliwa na bega la juu (la pili), ambalo pia huzaliwa (Mchoro 1.3, mchoro wa 8). Sehemu ya mwili iliyobaki huzaliwa (kutolewa). Wakati wa kutolewa, mtoto husonga kwa mwendo wa juu huku akisaidiwa na mhudumu.

1.4.8 Hitimisho

Mwendo wa kushuka hufanyika katika kila awamu ya leba. Hususan, baada ya kichwa cha fetasi kutandazika, mtoto hushuka. Baada ya kuzungukia ndani, mtoto hushuka. Baada ya kutandazika, mtoto hushuka, na kadhalika. Utaratibu wa leba ya kawaida umeelezwa kwa kina zaidi katika Kipindi kinachofuata.

Muhtasari wa Kipindi cha somo la 1

Katika Kipindi cha somo la 1, ulijifunza yafuatayo:

  1. Leba halisi ni utaratibu asilia. Wakati wa leba, mikazo ya uterasi hutokea kwa utaratibu maalum, yenye kutabirika na mikali. Mikazo huendelea kuongezeka taratibu na kusababisha seviksi kufitika na kupanuka.
  2. Leba halisi inaweza kuanza bila damu tetelezi au maji kuvunjika (kupasuka kwa membreni za fetasi).
  3. Mwanamke aliye na leba bandia huwa na mikazo ya uterasi isiyo taratibu. Dawa za kutuliza maumivu zinazoweza kupunguza makali ya mikazo hii.
  4. Mwanamke mwenyewe anaweza kutambua akiwa katika leba ya kweli. Wakati wa leba, uchungu unaotokana na kusukuma chini hutokea mara 3-5 kila baada ya dakika 10, na kila mkazo huchukua sekunde 40-60.
  5. Kuna awamu nne za leba:
    • Awamu ya kwanza huanzia na leba halisi na kukamilika seviksi ikipanuka kabisa (sentimita 10). Awamu hii ina awamu fiche na wazi.
    • Awamu ya pili huanza wakati seviksi imepanuka kabisa na kuisha mtoto anapozaliwa.
    • Awamu ya tatu huanza mtoto anapozaliwa na kukamilika plasenta inapotoka.
    • Awamu ya nne ni masaa 4 ya kwanza baada ya plasenta kutoka. Katika awamu hii, mtazame mama kwa makini kama ufanyavyo wakati wa leba na kuzaa.
  6. Katika leba inayoendelea kwa kawaida, mtoto hufanya miendo saba mikuu huku akishuka chini kwenye njia ya uzazi: kufungamana, kushuka, kukunjika, kuzungukia ndani, kutandazika, kuzungukia nje (kurejea), na kutolewa.
  7. Fetasi hushuka kila wakati wa kila mwendo.
  8. Fuvu la kichwa cha mtoto linaweza kufinyangika linapopitia kwenye pelvisi ya mama. Nguvu ziletwazo na mikazo inayomsukuma kupita kwenye nafasi nyembamba inaweza kufinyanga fuvu la kichwa cha mtoto.

Maswali ya Kujitathmini (MK) ya Kipindi cha Somo la 1

Kwa vile umekamilisha Kipindi hiki, jibu maswali haya ili kutathmini jinsi ulivyofanikiwa katika malengo ya Somo la Kipindi hiki. Andika majibu yako katika shajara yako ya masomo na uyajadili na mkufunzi wako katika Mkutano Saidizi wa Somo unaofuata. Linganisha majibu yako na maandishi ya kukumbuka yaliyo katika Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa moduli hii.

MK 1.1 (linatathmini Malengo ya Somo 1.1)

Andika kwenye kijikaratasi kila mojawapo ya maneno yaliyoandikwa kwa herufi nzito yaliyoorodheshwa hapa. Kunja kila kijikaratasi kisha ukitumbukize kwenye kikapu au bakuli.

Chukua kila kijikaratasi kimoja baada ya kingine kisha ujaribu kufasili kila neno. Andika majibu yako kwenye Shajara yako ya Masomo. Mwisho, linganisha majibu yako na fasili iliyo kwenye Kipindi hiki cha somo. Rudia zoezi hili hadi uyafahamu maneno yote: leba halisi, kuvutika juu na kupanuka kwa seviksi baada ya kila mkazo, kupanuka, sehemu iliyotangulia, damu tetelezi, kupasuka kwa membreni, kufungamana, kushuka, awamu ya kwanza, awamu ya pili, awamu ya tatu, awamu ya nne

Answer

Angalia fasili yako ya maneno yaliyoandikwa kwa herufi nzito. Angalia kila neno katika Kipindi cha 1 cha Somo kisha ulinganishe uliyoyaandika kwenye Shajara yako ya Masomo na fasili iliyo katika Kipindi hiki. Iwapo kuna fasili yako yoyote ambayo haikulingana, jaribu Zoezi 1.1 tena hadi uyapate kwa usahihi.

Mwisho wa jibu

Soma Kauli ya Somo 1.1 kisha ujibu maswali yanayoifuata.

Kauli ya Somo 1.1 Bi. Abeba

Bi Abeba ana umri wa miaka 30 na anazaa mtoto wake wa kwanza. Ametembelea kituo cha afya kwa sababu masaa matatu yaliyopita alianza kuhisi uchungu wa kila mara unaosukuma kwenda chini. Anaeleza kuwa uchungu huu unaanzia mgongoni na kusonga hadi sehemu ya mbele ya fumbatio. Anaeleza kuwa kila mara, uchungu unadumu kwa takriban sekunde 40, na kuwa unatokea mara 2-3 baada ya kila dakika 8. Baada ya kumchunguza, unatambua kuwa seviksi yake imefitika na kupanuka kabisa na kwamba kipenyo chake kina upana wa sentimita 4. Mama mkwe wa Bi Abeba alimwambia kuwa leba haijaanza kwa sababu “damu tetelezi” ingali haijatoka.

MK 1.2 (linatathmini Malengo ya Masomo 1.2 na 1.3)

  1. Ni dalili zipi, kulingana na maelezo ya Bi. Abeba, zinazoonyesha kuwa yuko katika leba ya kweli?
  2. Je, amefika awamu ipi ya leba na umetambua vipi?
  3. Utamwambia nini Bi. Abeba ili atambue kwamba yuko katika leba halisi?
Answer
  1. Bi. Abeba yuko katika leba halisi kwa sababu uchungu wake ni dalili ya mikazo tosha ya uterasi. Mikazo inatokea kila mara (mara 2-3 kila baada ya dakika 8), na muda inayochukua ni sekunde 40, jambo ambalo linatarajiwa katika leba halisi. Seviksi yake imevutika na kupanuka kwa sentimita 4 baada ya saa 3 za mikazo kutokea.
  2. Yeye yuko katika awamu ya kwanza ya leba. Yeye yuko kati ya awamu fiche na iliyo wazi, ambayo hutokea wakati seviksi imepanuka hadi sentimita 4.
  3. Mhakikishie Bi. Abeba kwamba leba inaweza kuanza hata kabla ya damu tetelezi kuvuja. Mikazo yake imekuwa ikija kwa saa 3 bila kusita. Makali na utaratibu wa kikazo hii ni kama inavyotarajiwa katika leba ya kawaida.

Mwisho wa jibu

MK 1.3 (linatathmini Malengo ya Somo 1.2)

Jedwali 1.3 linaorodhesha tofauti baina ya leba halisi na bandia. Jaza mapengo haya kwa maelezo yafaayo.

Jedwali 1.3 Leba halisi na bandia
Leba halisiLeba bandia
Mikazo hutokea kwa nyakati zinazoweza kutabirika
Muda unaochukua kila mkazo huongezeka pole pole
Makali ya mikazo hayabadiliki
Seviksi huendelea kupanuka
Maumivu huondolewa kwa kutembea au na matibabu ya kuyapunguza.
Answer

Toleo lililojazwa la Jedwali 1.3 limeonyeshwa hapa.

Leba halisiLeba bandia
Mikazo hutokea kwa nyakati zinazoweza kutabirikaMikazo hutokea kwa nyakati zisizoweza kutabirika.
Muda unaochukua kila mkazo huongezeka pole pole Muda haubadiliki: iwapo ni mrefu au mfupi
Makali ya mikazo huzidiMakali ya mikazo hayabadiliki
Seviksi huendelea kupanukaSeviksi haipanuki
Maumivu hayatulizwi kwa matibabu ya kutuliza maumivuMaumivu huondolewa kwa kutembea au matibabu ya kuyapunguza.

Mwisho wa jibu

MK 1.4 (linatathmini Malengo ya Masomo 1.1, 1.4 na 1. 5)

Ni elezo lipi lisilo la kweli? Katika kila kauli, eleza lisilo la kweli.

  • A.Wepesi ni utaratibu ambapo mtoto huelea kwenye fumbatio muda mfupi kabla ya leba kuanza.
  • B.Awamu ya pili ya leba huisha mtoto anapotoka kwenye njia ya uzazi.
  • C.Awamu ya nne ya leba hudumu kwa saa 4 na kuanza punde plasenta na membreni zinapotolewa.
  • D.Kupishana kwa mifupa ya fuvu la kichwa cha mtoto wakati wa kushukia kwenye pelvisi ya mama hujulikana kama kukunjika.
  • E.Kichwa cha mtoto hufungamana kisogo kinapofika katika upeo wa mifupa ya iskiamu katika pelvisi ya mama.
  • F.Wakati wa kuzaa kwa njia ya kawaida, mabega yote hutokeza kwa wakati mmoja.
Answer
  • A.si kweli. Wepesi ni utaratibu ambapo mtoto hushuka hadi sehemu ya chini ya fumbatio, muda mfupi kabla ya leba kuanza.
  • B.ni kweli. Awamu ya pili ya leba huisha mtoto anapotoka kwenye njia ya uzazi.
  • C.ni kweli. Awamu ya nne ya leba hudumu kwa saa 4 na kuanza punde plasenta na membreni zinapotolewa.
  • D.si kweli. Kupishana kwa mifupa ya fuvu la kichwa cha mtoto wakati wa kushukia kwenye pelvisi ya mama hujulikana kama kufinyangika (wala sio kutandazika).
  • E.ni kweli. Kichwa cha mtoto hufungamana wakati kisogo kipo katika upeo wa mifupa ya iskiamu.
  • F.si kweli. Wakati wa kuzaa kwa njia ya kawaida, bega moja la mtoto hutoka kwanza, kisha lile lingine kufuata.

Mwisho wa jibu