Skip to main content
Printable page generated Thursday, 5 Aug 2021, 00:26
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Thursday, 5 Aug 2021, 00:26

3. Kumtunza Mama aliye katika Leba

Kipindi cha 3 Kumtunza Mama aliye katika Leba

Utangulizi

Katika kipindi kilichopita cha Moduli hii, ulijifunza kuhusu ufasili, ishara na dalili, na awamu za leba ya kawaida. Leba na kuzaliwa kwa mtoto ni tukio la kipekee katika maisha ya familia yoyote na pia huwa na umuhimu wa namna ya kipekee kwa mama binafsi. Kushirikiana na mwanamke mjamzito na umahiri wako katika kudhibiti utaratibu wa kuzaliwa huchangia kuwepo kwa hali ya kuridhisha pamoja na uaminifu wakati wa leba na kuzalisha. Hisia hizi huchangia katika matokeo bora. Ni lazima uwe msikivu unapomtunza mwanamke aliye katika leba. Ni lazima uelewe mahitaji yake na jinsi mama yule anavyofahamu leba.

Katika kipindi hiki utajifunza jinsi ya kumfadhili mwanamke katika kipindi chote cha kuzaa. Pia utapewa utangulizi wa kanuni za kimsingi za ufuatilizi wa mama na fetasi wakati wa leba. Utajifunza pia kuhusu kiwango cha usafi kinachohitajika ili kuzuia maambukizi na pia kuhusu vifaa unavyopaswa kutayarisha ili kuzalishia nyumbani au katika kituo cha afya.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 3

Baada ya kuhitimisha somo hili, unatarajiwa:

3.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 3.7)

3.2 Kukadiria mahitaji ya mwanamke aliye katika leba na kumtunza ifaavyo. (Maswali ya Kujitathmini 3.1 na 3.7)

3.3 Kumpa mwanamke aliye katika leba usaidizi wa kihisia na kisaikolojia. (Swali la Kujitathmini 3.1)

3.4 Kufuatilia hali ya mama na fetasi katika awamu ya kwanza na ya pili ya leba na kurekodi habari hiyo. (Maswali ya Kujitathmini 3.2, 3.3, 3.5 na 3.6)

3.5 Kutayarisha vifaa vya uzalishaji wa kawaida. (Swali la Kujitathmini 3.4)

3.6 Kutwaa hadhari za kiwango cha usafi kinachohitajika na kinga dhidi ya maambukizi katika utunzaji wa kuzalisha. (Swali la Kujitathmini 3.4 na 3.7)

3.1 Kukadiria mahitaji ya mwanamke aliye katika leba

Kila mwanamke huhitaji usaidizi wa aina tofauti. Hata hivyo wanawake wote huhitaji wema, heshima na usikivu. Mtazame na umsikilize ili ufahamu hisia zake. Mhimize ili ahisi kuwa mwenye nguvu na ujasiri wakati wa leba. Msaidie kutulia na kuanza kuipokea leba yake.

Mchoro 3.1 Msaidie mwanamke aliye katika leba kutulia.

3.1.1 Kuifadhili leba

Unapomfadhili mama wakati wa leba, unapaswa kumsaidia kutulia badala ya kuipinga leba (Mchoro 3.1). Ingawa kufadhili leba hakufanyi uchungu wake kuisha, kunaifanya leba kuwa rahisi, fupi na salama zaidi. Katika kipindi hiki, utajifunza mbinu mbalimbali za kufadhili leba, vikiwemo vitendo wazi (kama vile mguso na sauti) na usaidizi wa kisaikolojia na kihisia.

3.1.2 Kuikinga leba

Kukinga leba ni kuilinda dhidi ya madhara.

Hakikisha kuwa watu wote fidhuli na wasio wakarimu hawamsumbui mama. Mama huyu hapaswi kuhofishwa na shida za kifamilia. Wakati mwingine hata marafiki wa kufadhili na kuonyesha upendo wanaweza kudhuru leba. Wakati mwingine, mbinu mwafaka katika kuzalisha ni kuwaeleza watu wote waondoke chumbani ili mama asiwe na wasiwasi wakati wa leba.

Usitumie dawa au taratibu zisizohitajika! Usimpe mama dawa za kuharakisha leba kwa kuwa dawa hizi huongeza hatari.

Watu wengine huamini kwamba dawa, vifaa na uchunguzi zaidi kwa mama humfanya azae kwa njia salama zaidi. Kwa kawaida fikira hii si kweli. Hatua hizi zinaweza kufanya uzalishaji kuwa mgumu au kusababisha matatizo. Sindano au tembe zinazopewa akina mama ili kuharakisha kuzaa zinaweza kufanya leba kuwa chungu zaidi na hata kusababisha kifo cha mama na mtoto.

3.1.3 Mkao na mwendo

Kuna vipengele kadhaa vinavyoathiri uamuzi kuhusu mkao wa mama katika awamu ya kwanza ya leba. Kati ya mikao yote, ulio muhimu zaidi ni hiari ya mama - jinsi angependa kuzaa. Hata hivyo, baadhi ya wanawake huhitaji kuhimizwa kujaribu mikao tofauti.

Msaidie mwanamke kujisogeza wakati wa leba. Anaweza kuchuchumaa, kuketi, kupiga magoti au mikao mingineyo (Mchoro 3.2). Mikao hii yote ni mizuri. Seviksi hufunguka kwa usawa zaidi mama anapobadili hali ya mkao.

Mchoro 3.2 Kubadilisha mkao katika awamu ya kwanza humsaidia mama kustahimili leba zaidi.

3.1.4 Kumsaidia mama kudhibiti mikazo yake

Huenda mama aweze kupata usingizi katika vipindi vya kwanza vya leba. Wanawake wengi huhisi uchovu mikazo yao ikiwa dhabiti sana. Wao wanaweza kuhofia kuwa hawana nguvu za kutosha kumsukuma mtoto. Hata hivyo uchovu wa mwili ni hali ya mwili kumpuzisha na kumtuliza mama. Iwapo mambo yote ni salama, mama atakuwa na nguvu za kuzaa wakati utakapofika.

Ili kuhifadhi nguvu zake, mama anapaswa kutulia katikati ya mikazo na hata punde leba inapoanza. Hii inamaanisha kuwa mikazo inapokoma, mama anapaswa kuuacha mwili wake kupumzika, avute pumzi nyingi na wakati mwingine aketi au kulala.

3.1.5 Mguso

Usimpapase fumbatio. Kupapasa hakuwezi kuharakisha leba, bali kunaweza kusababisha kutengeka kwa plasenta kabla ya wakati. (Ulijifunza kuhusu kutengeka kwa plasenta kabla ya wakati na kuvuja damu katika awamu ya mwisho ya ujauzito katika kipindi cha 21, Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito Sehemu ya 2. Plasenta inaweza pia kutengeka mapema sana wakati wa leba.)

Leba inaweza kuwa ngumu zaidi iwapo mwanamke ana hofu au wasiwasi. Ili kumsaidia kupunguza hofu, mdhibitishie mwanamke huyu kuwa maumivu aliyo nayo ni ya kawaida. Ingawa mguso unaweza kumsaidia mwanamke aliye katika leba, fahamu aina ya mguso anayopendelea. Mifano ya miguso inayopendelewa mara nyingi na wanawake ni kama:

 • Kusukuma kwa udhabiti na utulivu kwenye sehemu ya chini ya mgongo wakati wa mikazo.
 • Mpapase baina ya mikazo, hasa miguu na mgongo.
 • Kijitambaa kilicho na joto au baridi kwenye sehemu ya chini ya mgongo au tumbo (Mchoro 3.3). Iwapo mama anatokwa na jasho, kuweka kijitambaa chenye ubaridi kwenye paji la uso humfanya kuhisi vyema.
Mchoro 3.3 Kijitambaa vuguvugu kilicho na unyevu au kupapasa taratibu kunaweza kupunguza maumivu ya leba.

3.1.6 Sauti

Mchoro 3.4 Unaweza kutoa sauti za chini mwenyewe ili kumwelekeza mama.

Kutoa sauti wakati wa leba kunaweza kusaidia kufungua njia ya uzazi. Mhimize mama kutoa sauti kwani sio wanawake wengi wanaopendelea kufanya hivi. Sauti za chini zinazoweza kumsaidia mama ni kama vile kutoa mingurumo kama mnyama au ndege. Wanawake wengine hukariri au kuimba. Mwanamke anaweza kutoa sauti ya juu kadri apendavyo.

Sauti zingine zinaweza kuwafanya wanawake kuwa na wasiwasi zaidi. Kwa kawaida, sauti kali au mayowe hazisaidii. Mama anapoanza kutoa sauti ya juu iliyo ya kuhofisha, msihi kutoa sauti ya chini (Mchoro 3.4)

3.1.7 Kupumua wakati wa leba

Namna ya kupumua kwa mwanamke inaweza kuathiri sana jinsi leba ilivyo. Katika awamu ya kwanza ya leba, mbinu mbali mbali za kupumua zinaweza kurahisisha leba zaidi. Zijaribu mbinu hizi za kupumua wewe binafsi kisha umwonyeshe mama jinsi ya kuzifanya. Msaidie kuchagua mbinu inayomfaidi zaidi ili kupunguza maumivu. Wahimize kina mama kujaribu mbinu tofauti za kupumua katika kipindi chote cha leba:

 • Kupuliza taratibu. Mshauri mwanamke huyu kuvuta pumzi taratibu kwa muda mrefu. Ili kutoa pumzi, mshauri kuunganisha midomo kisha kupuliza polepole. Kuvuta pumzi kupitia pua husaidia kupunguza kasi ya kupumua.
 • Kupumua kwa sauti ya ’juu’. Mwanamke huvuta pumzi nzito taratibu, kisha kupuliza pumzi fupi za haraka ili kutoa sauti laini ya "hiii, hiii".
 • Kuhema. Mwanamke huvuta pumzi nyepesi za haraka.
 • Kupuliza kwa nguvu. Mwanamke hupuliza kwa nguvu na kisi.

3.1.8 Kutumia vinywaji wakati wa leba

Mwanamke aliye katika leba hutumia nguvu nyingi na maji ya mwili kwa haraka. Katika awamu ya kwanza ya leba, mwanamke anapaswa kunywa angalau kikombe kimoja cha kinywaji kilicho na kiwango cha juu cha kalori kila saa, kama vile chai, vinywaji visivyolevya, supu au maji ya matunda. Mwanamke huyu asipokunywa vinywaji vya kutosha, anaweza kuishiwa na maji (kukosa maji ya kutosha mwilini). Jambo hili linaweza kufanya leba kuwa ndefu na ngumu zaidi na kumfanya kuhisi uchovu. Ukosefu wa maji mwilini pia unaweza kumfanya mwanamke huyu kujihisi mchovu.

Dalili za kuishiwa na maji ni pamoja na:

 • Midomo iliyokauka
 • Macho yaliyobonyea
 • Ngozi kupoteza unyoofu.
 • Homa ndogo (hadi nyusi 38)
 • Pumzi nzito na za haraka (pumzi za zaidi ya mara 20 kila dakika)
 • Mpwito dhaifu wa moyo, lakini wa haraka (zaidi ya midundo 100 kila dakika)
 • Mpigo wa moyo wa mtoto ni haraka kuliko midundo 160 kila dakika.

3.1.9 Kutunza kibofu

Mshawishi mama mjamzito kukojoa angalau mara moja kila baada ya saa 2 (Mchoro 3.5a). Mikazo huwa dhaifu na leba kuchukua muda mrefu zaidi, iwapo kibofu kimejaa. Kibofu kilichojaa kinaweza pia kusababisha maumivu, matatizo wakati wa kusukuma plasenta na kuvuja damu baada ya kuzaa. Mkumbushe mama kukojoa, kwa sababu anaweza kusahau.

Mchoro 3.5 (a) Mshawishi mama kukojoa angalau kila baada ya saa 2. (b) Kibofu kilichojaa kinaweza kusababisha maumivu na kufanya leba kuchukua muda mrefu zaidi.

Gusa sehemu ya chini ya tumbo ya mama ili kuchunguza kama kibofu kimejaa. Kibofu kilichojaa huwa kama mfuko wa plastiki uliojaa maji. Unaweza kuona umbo la kibofu chini ya ngozi ya mama ikiwa kimejaa sana (Mchoro 3.5b). Usingoje hadi kibofu chake kijae sana.

Ni lazima mama akojoe iwapo kibofu chake kimejaa. Ikiwa hawezi kutembea, jaribu kumwekea sinia au pedi chini yake na umwagize akojoe. Ili kumsaidia kuanza kukojoa, weka mikono yake ndani ya maji vuguvugu.

 • Unafikiri ni kwa nini kibofu kilichojaa kinaweza kutatiza hali ya kawaida ya leba? (Fikiri kuhusu yale unayojua kutoka katika vipindi viwili vya somo vilivyopita.

 • Katika awamu ya kwanza na ya pili ya leba, kibofu kilichojaa kinaweza kutatiza mikazo ya kawaida ya uterasi. Kibofu kilichojaa huweka kichwa cha mtoto nje ya ukingo wa uterasi.

  Mwisho wa jibu

Katika Kipindi cha 6, unajifunza kuwa katika awamu ya tatu ya leba kibofu kilichojaa kinaweza kuchelewesha kutolewa kwa plasenta. Kuchelewa huku huongeza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa (Kipindi cha 11).

3.1.10 Usaidizi wa kihisia na kisaikolojia kwa mwanamke aliye katika leba

Mwanamke aliye katika kipindi cha leba huhisi kwamba anajidhibiti unapompa ushauri wa kihisa na kisaikolojia. Msaidie kujihisi kuwa anapendwa, bila kuzingatia jinsi anavyo itihia au kutenda. Msaidie kutamatisha kipindi cha leba na ajihisi kuwa amefaulu, hata ikiwa matokeo yake siyo aliyotarajua. Toa usaidizi huu kwa njia kadhaa.

Kuandamana wakati wa leba

Usihudumu peke yako wakati wa leba. Usaidizi wa kila mara kutoka kwa mume wake, jamaa wa karibu au marafiki wanaweza kumsaidia mwanamke wakati wa leba. Hakuna sheria kuhusu nani anayepaswa kumsaidia, lakini lazima mjamzito awe na watu wa kumsaidia wakati wa kuzaa.

Mawasiliano bora

Mweleze mama mjamzito kuhusu jinsi leba inavyoendelea. Mama huyu ana haki ya kujua jinsi leba inavyoendelea na hali yake pamoja na ya mtoto. Mfahamishe mama na mtu anayemsaidia kuhusu utunzaji wa kimwili, hali ya kutulia na usaidizi wa kihisia.

Mfahamishe mwanamke huyu na msaidizi wake kuhusu wanachotarajia katika leba ya mapema, kabla ya mikazo kuwa chungu zaidi na baadaye mikazo inapokuwa thabiti zaidi (ikiwezekana). Mweleze kuwa mikazo huwa thabiti zaidi na kukaribiana zaidi anapokaribia muda wa kuzaa. Mweleze anachopaswa kutarajia wakati wa kuzaa. Mhakikishie mwanamke kuwa utakuwa naye katika hatua zote.

3.2 Ufuatilizi wa mama na fetasi wakati wa leba

Ni lazima umchunguze mama na fetasi vyema wakati wa leba. Njia pekee iliyobora ya kutathmini jinsi leba inavyoendelea na kutambua hali isiyo ya kawaida ni kumfuatila mama na mtoto.

3.2.1 Tathmini jinsi leba inavyoendelea

Leba huwa tofauti. Zipo leba za kasi na zingine taratibu. Jambo hili ni la kawaida. Lakini leba salama inafaa kuendelea. Kuendelea kunamaanisha kuwa leba inaendelea kuwa thabiti zaidi na seviksi hufunguka. Kisanduku 3.1 linatoa kwa muhtasari sifa kuu za leba inayoendelea kwa kawaida.

Mchoro 3.6 Mhakikishie mama huyu kuwa mikazo inazidi kuwa thabiti zaidi kwa sababu leba ni ya kawaida.
Kisanduku 3.1 Kuendelea taratibu kwa leba ya kawaida
 • Mikazo huchukua muda zaidi, kuwa thabiti zaidi na kufuatana kwa karibu zaidi.
 • Wakati wa mkazo, uterasi huwa ngumu zaidi ukiigusa (Mchoro 3.6).
 • Kiasi cha “utetelezi” huongezeka.
 • Mfuko wa maji hupasuka
 • Mama huteuka, kutoa jasho na kutapika, au miguu yake hutetemeka.
 • Mama huhisi haja ya kusukuma chini kupitia sehemu ya chini ya fumbatio

Katika Kipindi cha 4 cha Somo, unajifunza jinsi ya kutumia chati inayoitwa patografu. Chati hii hutumika kutathmini jinsi leba inavyoendelea na kunakili uchunguzi na vipimo vyako kwa usahihi. Lakini kwanza fahamu yanayoendelea mwilini mwa mwanamke. Pia unajifunza mambo muhimu ya kuchunguza wakati wa leba.

3.2.2 Mikazo ya Uterasi

Kagua na urekodi marudio, urefu na uthabiti wa mikazo kila baada ya nusu saa. Marudio huonyesha idadi ya mikazo anayopata mwanamke kwa dakika 10. Hesabu marudio haya. Urefu humaanisha muda ambao kila mkazo huchukua. Pima muda huu kwa saa yako (kama unayo). Udhabiti huonyesha ukali wa uchungu ambao mwanamke hupata katika kila mkazo. Mwulize mwanamke akueleze uthabiti wa mikazo yake.

Katika leba ya kawaida, marudio ya mikazo huongezeka, hudumu zaidi, na huwa thabiti zaidi (huwa chungu zaidi).

3.2.3 Kupanuka kwa seviksi

Kuendelea kwa leba hubainika kwa kiasi cha kupanuka kwa seviksi. Kupanuka kwa seviksi hutathminiwa kwa kuchunguza uke baada ya saa 4 na kwa kutumia vidole vyako ili kukadiria kiasi cha kufunguka kwa seviksi. (Kipindi cha 2 cha Somo kinaelezea jinsi ya kutathmini ilivyo seviksi iliyopanuka.) Katika leba ya kawaida, kiwango cha wastani cha kupanuka kwa seviksi ni sentimita moja baada ya kila saa (sentimita 1 kwa saa)

3.2.4 Kushuka kwa sehemu tangulizi

Ili kupima kushuka kwa sehemu tangulizi ya fetasi, ipapase fumbatio na uilinganishe na ukingo wa pelvisi. Vilevile, unaweza kuona sehemu tangulizi ilivyoshuka kwa kufanya uchunguzi wa uke. Kadiria na unakili kushuka huku baada ya kila saa mbili wakati wa leba.

3.2.5 Michozo kutoka ukeni

“Utetelezi” ni jina la damu iliyo na kamasi inayooenekana katika leba ya mapema. Mtiririko wa damu unaweza kutokea kufikia mwisho wa awamu ya kwanza. Kiowevu cha amnion kinaweza kutirika kutoka ukeni baada ya tando kuraruka. Kiowevu hiki kinaweza kuwa na mekoniamu. Huu ni mchozo wa rangi ya kijani kibichi, ambao ni kinyesi cha kwanza cha mtoto. Ikiwa kiowevu cha amnioni kina mekoniamu, basi fetasi inaweza kuwa katika hali ya kufadhaika. Kwa kawaida, mtoto mchanga hutoa kinyesi baada ya kuzaliwa. Baadaye katika Moduli hii, utajifunza hatua za kuchukua ikiwa fetasi au mama yuko katika hali ya kufadhaika.

3.2.6 Hali ya Fetasi

Ili kukadiria hali ya fetasi wakati wa leba, chunguza kima cha mpigo wa moyo wa fetasi na mpangilio wake ukilinganisha na mikazo. (Kima cha mpigo wa moyo wa fetasi ni hesabu ya mpigo kwa dakika moja). Chunguza mpigo wa moyo wa fetasi kila baada ya dakika 30 kwa kusikiliza (oskulitesheni). Ulijifunza jinsi ya kusikiliza mpigo wa moyo kwa kutumia stethoskopu katika Kipindi cha 11 cha Somo la Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito.

 • Je, unakumbuka kiwango cha kawaida cha mpigo wa moyo wa fetasi?

 • Mpigo wa moyo wa fetasi wa kawaida huwa ni kati ya mipigo 100-180 kwa dakika moja.

  Mwisho wa jibu

3.2.7 Hali ya mama

Hesabu mipigo ya moyo wa mama baada ya kila dakika 30 na upime shiniko la damu na halijoto kila baada ya saa 4. Ulijifunza jinsi ya kuchukua vipim hivi katika Kipindi cha 9 cha Somo cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito. Pia, nakili kwenye chati yako hesabu ya kula, kunywa na kukojoa.

Shinikizo la damu kushuka

Mwanamke huyu anapaswa kwenda hospitalini mara moja ikiwa shinikizo la damu litashuka ghafla!

Ikiwa shinikizo la damu la diastoli (nambari ya chini) litashuka ghafla kwa alama 15 au zaidi, mabadiliko haya ni athari ya hatari. Mabadiliko haya humaanisha kuwa mama anavuja damu sana. Ikiwa havuji damu kutoka ukeni, basi plasenta yake inaweza kuwa imetengeka na huenda akawa anavuja damu ndani ya uterasi (kuvuja damu wakati wa kuzaa).

Shinikizo la damu kupanda

Shinikizo la damu la mmHg 140/90 au zaidi ni ishara ya hatari. Mwanamke anaweza kuwa na priekilampsia. Priekilampsia inaweza kusababisha mitukutiko (eklampsia), kutengeka kwa plasenta, kuvuja damu ubongoni, au kuvuja damu nyingi sana. Mama na mtoto wanaweza kufa. Katika Kipindi cha 19 cha Somo cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito sehemu ya 2, ulijifunza kuhusu eklampsia na priekilampsia. Nakili shinikizo la damu na vipimo hivi vingine katika patografu. Utajifunza jinsi ya kufanya hivyo katika kipindi kijacho.

Sasa utajifunza kuhusu vifaa unavyopaswa kutayarisha ili utumie kuzalisha.

3.3 Jitayarishe kuzalisha

Jitayarishe kuzalisha punde mwanamke anapoingia katika awamu ya pili ya leba.

3.3.1 Ishara za awamu ya pili ya leba

 • Mikazo inakuwa thaniti zaidi na inayosukuma nje.
 • Kinyeo hupanuka na kuacha kipenyo. (Sfinikta ya kinyeo hufunguka wakati wa mkazo.)
 • Sehemu ya fetasi inayotangulia hutokea chini ya vulva.
 • Seviksi hupanuka kabisa hadi sentimita 10.

3.3.2 Tayarisha mahali pa kuzalishia

Ukishadhibitisha kuwa mwanamke yuko katika awamu ya pili ya leba, fanya maandalizi ya kwanza ya kuzalisha. Chumba cha kuzalishia kinafaa kuwa na kiwango mwafaka cha joto na mwangaza ili kuhakikisha kuwa msamba na vulva inaonekana vyema. Fuata utaratibu wa kuzuia maambukizi kama ilivyoelezwa katika Sehemu ya 3.5 ili kuandaa mahali safi pa kumpokea mtoto (Mchoro 3.7). Tandika vazi linalozuia maji kitandani na sakafuni . Hakikisha kuwa nguo za kumpasha mtoto joto zimetayarishwa.

Mchoro 3.7 Vifaa vya kuandaa mahali safi na salama pa mama kuzalia.

3.3.3 Vifaa na nyenzo unazohitaji ili kuzalishia

Hakikisha kuwa una nyenzo na vifaa unavyohitaji ili kuzalisha (Kisanduku 3.2 na Mchoro 3.8) katika Kituo cha Afya. Iwapo utamzalisha mwanamke nyumbani, nenda na vifaa hivyo. Ingawa mwanamke anaweza kuwa na vifaa vidogo vidogo, kama vile sabuni na vitambaa safi, unafaa kuwa umejiandaa vya kutosha. Tumia Kisanduku 3.2 kama orodha ya kukagulia. Hakikisha kuwa vifaa vyote viko unapapakia.

Kisanduku 3.2 Orodha ya kukagua vifaa vya kuzalisha
 • Maji safi, sabuni na taulo ya mkononi.
 • Aproni, miwani, kinyago na gauni.
 • Glavu safu.
 • Uzi safi mpya wa kufungia kitovu.
 • Wembe mpya au makasi yaliyotakaswa.
 • Fosepsi mbili aina ya klempu za kushikilia kambakitovu kabla ya kuikata.
 • Kitega kamasi au balbu ya kufyonzea kamasi kutoka kwenye matundu ya pua la mtoto (iwapo itahitajika).
 • Shashi iliyotakaswa, kijitambaa cha pamba na pedi ya kiafya ya mama kutumia.
 • Taulo mbili za mtoto zilizosafi na kavu, na vitambaa viwili vya kufunikia.
 • Stethoskopu na sijafu ya kupimia shinikizo la damu.
 • Kiowevu cha antiseptiki ili kusafishia msamba na viungo vya uzazi.
 • Vipimo 10 vya dawa ya kudungwa aina ya oxytocin ama mikrogramu 600 za tembe za misoprostol. Dawa hizi hutumika kuzuia damu kuvuja baada ya kuzaa. Oxytocin ndiyo dawa inayopendekezwa zaidi ingawa misoprostol inaweza kutumika ikikosekana. (Utajifunza zaidi kuhusu dawa katika Kipindi cha 6 cha Somo.)
 • Lihamu ya macho aina ya Tetracycline. (Antibiotiki hii ya macho hutumika kumkinga mtoto mzawa dhidi ya maambukizi ya macho.)
 • Ndoo tatu au vijibakuli vitatu vilivyo na kiowevu cha klorini au cha sabuni na maji safi katika kila kimoja. (Unaweza kutumia Berekina kutayarisha 0.5% ya kiowevu cha klorini. Soma ukolezi wake kwenye chupa. Iwapo ukolezi ni 5%, unaweza kutayarisha kiowevu chenye ukolezi wa 0.5% kwa kuchanganya kikombe 1 cha Berekina na vikombe 9 vya maji safi.)
 • Bakuli ya plastiki ya kumpokea mtoto.
Mchoro 3.9 Vifaa unavyohitaji ili kuzalisha.

3.4 Kuzuia maambukizi unapozalisha

Maambukizi husababisha magonjwa na hata kuua. Maambukizi ni baadhi ya visababishi vya vifo baada vingi baada ya kuzaa. Hatua nyingi unazochukua wakati wa leba na kuzalisha zinaweza kuwa salama iwapo tu utafuata kanuni za kimsingi za kuzuia maambukizi. Kanuni hizi zinaweza kuorodheshwa kwa muhtasari kama ”safi tatu”: mikono safi, mahali safi (pa kuzalisha) na vifaa safi. Tayari unafahamu kuwa unafaa kusafisha kabisa mahali pa kuzalisha. Hali kadhalika, fuata kanuni zingine za usafi kama zilivyoelezwa katika sehemu ifuatayo.

3.4.1 Kunawa mikono

 • Je, kunawa mikono huzuia maambukizi vipi?

 • Kunawa mikono ni mojawapo ya mambo muhimu zaidi unaweza kufanya ili kuzuia maambukizi. Kunawa mikono hukuzuia kueneza viini vya magonjwa kwa watu wengine na kukukinga dhidi ya viini wewe mwenyewe.

  Mwisho wa jibu

Iwapo kuna jambo unalohitaji kufanya ili kuzuia maambukizi, basi ni kunawa mikono (Mchoro 3.10 na Kisanduku 3.3).

Mchoro 3.10 Jinsi ya kunawa mikono kwa dakika 2.
Kisanduku 3.3 Nawa mikono kila wakati kwa dakika mbili
Kabla yaBaada ya
Kuguza uke wa mama.Kusafisha uke baada ya kuzalisha.
Kunchunguza uke au pelvisi.Kuguza damu au viowevu vyovyote vingine.
Kumtoa mtoto.Haja ndogo au Haja kubwa.
Kumchunguza mtoto.
Kinawa mikono cha gliserini na alkoholi

Iwapo huna maji ya kunawia mikono, unaweza kuandaa kinawa mikono rahisi kinachojulikana kama kisugua mikono. Kinawa mikono hiki huua viini vilivyo mikononi iwapo kitatumiwa vyema.

Changanya mililita 2 za gliserini na mililita 100 za ethili au kileo aina ya aisopropili (ukolezi ni 60% hadi 90%). Kama sivyo, unaweza kutumia alkoholi yoyote inayotumika kusafisha ngozi kabla ya kudunga sindano.

Sugua mililita 5 hivi (kijiko 1 kidogo) za kisugua mikono ili kuisafisha mikono. Sugua mikono kwa makini huku ukisafisha sehemu za katikati ya vidole na ndani ya kucha. Endelea kusugua hadi mikono ikauke. Usikamue mikono yako au kuipanguza kwa kitambaa.

Ili kuzuia kuongezeka kwa kinawa mikono kwenye mikono, nawa mikono kwa sabuni na maji baada ya kukitumia mara 5-10.

Usitumie kisugua mikono iwapo mikono yako imechafuliwa na viowevu vya mwili ama ina uchafu unaoonekana; badala yake, nawa mikono kwa sabuni na maji.

3.4.2 Vaa mavazi ya kujikinga

Aina tofauti za glavu huwa na matumizi mbalimbali. Tumia glavu nzito kushika vifaa vichafu, vitambaa na uchafu wa mwili; kufanya shughuli za kinyumbani; na kusafisha maeneo machafu. Tumia glavu zilizotakaswa na ambazo zimetumika mara moja tu unapoguza tando za ute ambazo hazijapasuka (unapochunguza uke). Pia, tumia glavu zilizotakaswa na ambazo zimetumika mara moja tu iwapo utahitaji kushika damu au viowevu vingine vya mwili. Tumia glavu zilizotakaswa kwenye taratibu zote unapogusa tishu zilizo chini ya ngozi au kwenye mfumo wa damu.

Vaa glavu unapoguza uke wa mama, damu au kiowevu cha mwili. Baada ya kuzitumia, zitupe glavu kwa uangalifu.

Kinyago, miwani, aproni au kanzu

Vaa kinyago usoni, miwani ya kulinda macho na aproni safi unapochagua na kusafisha vifaa na vitambaa. Unashauriwa kuvivaa unapozalisha kupitia ukeni na unapokata kambakitovu. Vifaa vya kulinda macho hujumuisha miwani kubwa, ngao ya macho na miwani za kawaida.

Kinga za miguu

Ili kuikinga miguu yako, vaa viatu au buti zinazofunika miguu na ambazo zimetengenezwa kwa mpira au ngozi. Iwapo viatu au buti hizi ni za ngozi, zifunike kwa karatasi za plastiki. Viatu au buti humkinga aliyevaa kutokana na majeraha yanayosababishwa na vifaa vizito au vyenye ncha kali. Karatasi za plastiki inakukinga dhidi ya damu ama viowevu vingine vya mwili vilivyotapakaa sakafuni.

3.4.3 Safisha na uvitakase vifaa kwa kiwango cha juu

Takasa vifaa vyote kabla na baada ya mtoto kuzaliwa kwa kutumia kiowevu cha klorini chenye ukolezi wa 0.5%. Lowesha vifaa kwa dakika 10, vioshe kwa kiowevu cha sabuni kisha uvikamue kwa maji. Tumia kijiburashi kuvisugua. Baada ya kuondoa viini kwenye vifaa, takasa vifaa kwa kutumia mtambo wa kutakasa, au uvichemshe kwa dakika 20. (Iwapo unatumia mtambo wa kutakasa, fuata kwa utaratibu maagizo yaliyopeanwa).

3.4.4 Mahali safi pa kuzalisha na utaratibu mwafaka wa kutupa uchafu

Sugua mahali pa kuzalisha hadi pawe safi. Hakikisha kuwa vitambaa vyote, taulo na vitambaa vya kufunikia ni safi na kavu. Shuka zote anazolalia mama na zile unazomfunikia mtoto wakati wa kumwosha zinafaa kuwa safi kabisa.

Baada ya kuzalisha, weka uchafu wote kwenye chombo kisichovuja kama vile mkebe wenye kifuniko imara. (Uchafu huu ni kama vile damu, shuka chafu, tando na plasenta.) Kitupe chombo hiki mahali salama ambapo hakiwezi kuonekana. Choma au uzike uchafu. Ni muhimu kuzuia maambukizi yaliyo kwenye uchafu huu kuenea kwenye jamii.

Jitahadhari na sindano. Weka sindano ndani ya kijisanduku salama baada ya kutumia sirinji inayotupwa. Usiwache sindano kutapakaa ovyo.

3.5 Hitimisho

Ulijifunza jinsi ya kumsaidia mwanamke aliye katika leba, vifaa vinavyohitajika na jinsi ya kutupa uchafu. Katika kipindi kijacho, utajifunza kuhusu kuzaa kwenyewe na jinsi ya kutumia patografu.

Katika Kipindi cha 3, ulijifunza yafuatayo:

 1. Wanawake huhitaji utunzaji wa kibinafsi wakati wa leba na kuzaa. Wanawake wajawazito wanafaa kutafuta msaada kwa mhudumu aliyehitimu.
 2. Mpe mwanamke aliye katika leba pamoja na mtu aliyeambatana naye usaidizi wa kimwili, kihisia na kisaikolojia.
 3. Msaidie kutumia mikao tofauti, kujaribu njia tofauti za kupumua, kukubali kusuguliwa mgongo na kutoa sauti ndogo wakati wa leba. Hatua hizi hupunguza uchungu na kudhibiti mikazo.
 4. Mshauri kunywa angalau kikombe kimoja cha kiowevu kila siku. Msaidie kukojoa angalau mara moja kila baada ya masaa 2.
 5. Mjulishe jinsi leba inavyoendelea ili atulie na awe mjasiri.
 6. Fuatilia hali ya fetasi. Chunguza mpigo wa moyo wa fetasi kila baada ya dakika 30. Kiwango cha mpigo wa moyo kinafaa kuwa cha kawaida.
 7. Fuatilia hali ya mama. Pima kiwango chake cha shinikizo la damu na kiwango joto cha mwili kila baada ya masaa 4, na mpigo wa mishipa kila baada ya dakika 30.
 8. Chunguza jinsi leba inavyoendelea. Chunguza urefu, uthabiti na marudio ya mikazo ya uterasi kila baada ya dakika 30. Chunguza jinsi kichwa kinavyoshuka kila baada ya saa 2. Chunguza jinsi seviksi inavyopanuka kila baada ya saa 4.
 9. Tayarisha vifaa unavyohitaji kutumia kuzalisha. Jumuisha nguo za kujikinga mwenyewe. Sugua au utakase kila kitu kinachoguzana na tishu au viowevu vya mwili.
 10. Tumia sabuni na maji safi kunawa mikono. Nawa mikono ili kupunguza hatari ya kumwambukiza mama na mtoto wakati wa leba na kuzaa.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 3

Kwa kuwa sasa umekamilisha kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili kubaini jinsi ulivyotimiza Malengo ya Somo ya kipindi hiki. Andika majibu yako kwenye Shajara yako ya Masomo na uyajadili na Mkufunzi wako katika Somo Saidizi kijacho. Unaweza kulinganisha majibu yako na uliyoandika kwenye Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Uchunguzi Maalum 3.1. Woizero Almaz

Woizero Almaz ni mwanamke aliye katika hatima ya kipindi cha ujauzito. Alikuja katika Kituo cha Afya akiwa na maumivu na kutokwa na mchozo ulio na damu ukeni mwake. Maumivu yalianza saa 5 zilizopita. Ana wasiwasi kuhusu mimba yake, kwa sababu ni yake ya kwanza. Unapomchunguza, unatambua kuwa yuko katika awamu yake ya kwanza.

Swali la Kujitathmini 3.1 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.2 na 3.3)

Ni usaidizi gani unaoweza kumpa Woizero Almaz ili kumtuliza kuhusu hali yake?

Answer

Ili kumhakikishia Almaz, kuwa mkarimu na uziheshimu mila na kaida zake ili akuamini. Onyesha kuhusika katika hali yake. Mweleze kinachoendelea kuhusu leba yake. Mhimize kuuliza maswali na kujieleza kuhusu mawazo na wasiwasi alionao. Mweleze kuhusu hali ya mtoto. Mruhusu msaidizi kukaa naye. Mweleze kuhusu kila hatua kabla ya kuitekeleza.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.2 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.4)

Ni vifaa gani vya kukadiria unavyotumia kuchunguza jinsi leba yake inavyoendelea? Vifaa hivi vinakusaidia aje?

Answer

Pima shinikizo la damu, halijoto na mpigo wa mishipa ya Almaz ili kufahamu kuhusu hali yake. Chunguza mpigo wa moyo wa fetasi kubaini ikiwa anafadhaika. Fuatilia mikazo, kupanuka kwa seviksi na kushuka kwa kichwa cha mtoto ili kutathmini jinsi leba inavyoendelea. (Ulijifunza kuhusu patografu katika Kipindi cha 4 cha Somo. Kifaa bora zaidi cha kufuatilia jinsi leba inavyoendelea na kubaini tatizo lolote kwa haraka ni patografu).

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.3 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.5 na 3.6)

Katika kipindi cha kwanza cha leba, ni aina gani ya chakula unachomshauri atumie? Ni mara ngapi unajaribu kumshawishi ale?

Answer

Katika awamu ya kwanza ya leba, mwanamke anashauriwa kula chakula kilicho na kiwango cha juu cha kalori. Baadhi ya mifano ni kama chai, vinywaji vyepesi, supu na maji ya matunda. Almaz anapaswa kunywa kikombe kimoja angalau baada ya kila saa 1.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.4 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.5 na 3.6)

Unapomhudumia Almaz wakati wa leba, unazuia vipi maambukizi?

Answer

Unapochunguza uke na kuzalisha, tumia hatua za kawaida za tahadhari na uzuiaji wa maambukizi. Kabla ya na baada ya kila hatua, nawa mikono angalau kwa dakika 2. Tumia sabuni na maji safi au kinawa mikono cha alkoholi. Vaa nguo za kujikinga kama vile aproni, miwani, kinyago, glavu na viatu. Tumia njia mwafaka za kutupa uchafu (kuzika au kuchoma). Tumia mchanganyiko wa klorini ya 0.5% kwa dakika 10 kusugua, kuondoa vimelea au kutakasa vifaa vya chuma au glasi. Kisha safisha vifaa kwa maji moto na yenye sabuni au utumie mashine ya kutakasa.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.5 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.4)

Unachunguza nini (na ni mara ngapi) ili kuchunguza jinsi leba ya Almaz inavyoendelea.

Answer

Pima ishara muhimu za mwanamke: shinikizo la damu na halijoto baada ya kila saa 4, na mpigo wa mshipa baada ya kila dakika 30.

Chunguza marudio, urefu na uthabiti wa mikazo yake baada ya kila dakika 30. Mikazo hutokea kila mara, kali na ya haraka leba yake inapoendelea kukua.

Chunguza uke wa mwanamke mjamzito baada ya kila masaa 4 ili kutathmini upanuzi wa seviksi . kiwango cha kawaida cha kupanuka kwa seviksi ni angalau senitmita 1 kwa saa 1 katika leba.

Chunguza kushuka kwa sehemu tangulizi baada ya saa 2. Gusa fumbatio ili huhisi kichwa cha fetasi ukilinganisha na ukingo wa pelvisi, au uchunguze uke.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.6 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.4)

Ni ishara gani inayoonyesha kuwa mtoto ana ufadhaiko?

Answer

Uwepo wa mekoniamu ya rangi ya kijani kibichi katika kiowevu cha amnioni inayotoka ukeni mwa Almaz inaashiria kuwa fetasi iko katika hali ya kufadhaika. Mekoniamu ni kinyesi cha kwanza cha mtoto na kwa kawaida huwa hatoi kinyesi hadi azaliwe. Kima cha mpigo wa moyo wa mtoto anafadhaika wakati wa leba na kuzaliwa kinaweza kuwa juu au chini zaidi ya kiwango cha kawaida cha 100 -180 kwa dakika.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 3.7 (linatathmini Matokeo ya Somo la 3.1, 3.2 na 3.6)

Ni yapi kati ya kauli hizi ambayo si kweli? Katika kila mmojawapo, eleza isiyo sahihi.

 • A.Hiari ya mjamzito inamaanisha uheshimu namna ambavyo mjamzito angependa kuzaa
 • B.Mwanamke hapaswi kunywa chochote iwapo atatapika katika kipindi cha kwanza cha leba.
 • C.Marudio ya mikazo yanaashiria jinsi mikazo ilivyochungu.
 • D.Kutoka kwa mekoniamu ukeni ni ishara kuwa fetasi inafadhaika.
 • E.“Safi tatu” ni: mikono safi, mahali safi (pa kuzalishia) na vifaa safi.
Answer
 • A.Ni kweli. Kuheshimu hiari ya mjamzito inajumuisha namna ambavyo angependa kuzaa.
 • B.Si kweli. Mjamzito anapaswa kunywa angalau kikombe kimoja cha kiowevu baada ya kila saa 1 ili asipoteze maji mwilini, katika kipindi cha kwanza cha leba.
 • C.Si kweli. Marudio ya mikazo inamanisha ni mara ngapi yanakuja kwa muda wa dakika 10 wakati wa leba. Marudio haimaanishi jinsi mikazo ilivyo na uchungu, ambayo ni uthabiti wa mikazo.
 • D.Ni kweli. Mekoniamu inayotoka ukeni ni ishara kuwa fetasi iko katika hali ya ufadhaiko.
 • E.Ni kweli.“Safi tatu” ni: mikono safi, mahali safi (pa kuzalisha) na vifaa safi.

Mwisho wa jibu