Skip to main content
Printable page generated Saturday, 20 July 2024, 6:55 AM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Saturday, 20 July 2024, 6:55 AM

5. Kutekeleza Uzalishaji wa Kawaida

Kipindi cha 5 Tekeleza Uzalishaji wa Kawaida

Utangulizi

Katika masomo ya vikao vya awali, ulijifunza ufafanuzi, dalili na hatua za leba. Ulijifunza jinsi ya kutumia patografu. Aidha ulijifunza jinsi ya kumtunza mjamzito aliye katika leba. Katika Kipindi hiki, utajifunza jinsi ya kumsaidia mjamzito aliye katika hatua ya pili ya leba ya kawaida na jinsi ya kumtoa mtoto. Katika hatua ya pili ya leba, mama humsukuma mtoto chini kutoka kwenye uterasi kuelekea kwa uke na mtoto huzaliwa. Hatua ya pili huanza wakati seviksi ipanukapo kabisa. Hatua hii ya pili hukamilika mtoto azaliwapo.

Mjamzito haonyeshi hisia kwa muda mrefu katika hatua ya kwanza ya leba. Katika hatua ya pili, hali hiyo hubadilishwa na nguvu kali za mwili zitumikazo kwa muda mfupi. Mjamzito na msaidizi wake wawe na ushupavu, uvumulivu na matumaini kutoka kwa mkunga. Lazima utoe huduma bora na uwe na uhusiano nzuri na mama.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 5

Baada ya Kipindi hiki cha somo, utaweza:

5.1 Kueleza na kutumia kwa usahihi maneno muhimu yaliyo kwenye herufi nzito. (Maswali ya kujitathmini 5.1, 5.2 and 5.3)

5.2 Kueleza dalili za hatua ya pili ya leba. Kueleza kitendekacho kwa mama na mtoto ateremkapo chini kuelekea kwenye uke. (Maswali ya kujitathmini 5.1 na 5.2)

5.3 Kueleza jinsi ya kukadiria iwapo hatua ya pili itaendelea katika hali ya kawaida. Kueleza jinsi ya kutambua dalili za kuonya kwamba leba haiendelei ipasavyo.

5.4 Kueleza jinsi ya kutekeleza kuzaliwa kawaida kwa mtoto aliye na afya na kumpatia huduma mara tu azaliwapo.

5.5 Kufafanua jinsi ya kusaidia kujenga uhusiano mwema kati ya mama na mtoto mchanga baada ya kuzaliwa. (Swali la kujitathmini 5.5)

5.1 Kutambua dalili za hatua ya pili ya leba

Njia ya kipekee na hakika ya kutambua hatua ya pili ya leba ni kupanuka kabisa kwa seviksi. Njia pekee ya kutambua kuwa seviksi imepanuka kabisa ni kuchunguza uke. Lakini kumbuka urudiaji wa uchunguzi wa uke unaweza kusababisha maambukizi. Ni bora kutochunguza uke zaidi ya mara moja kila masaa 4. Hata hivyo pima upanuzi kabisa katika hali hizi:

 • Unapohesabu mipigo ya moyo ya fetasi na iwe kiwango cha kawaida cha mipigo ya 120-160 kwa dakika).
 • Kuna umwagikaji wa ghafla wa kiowevu cha amnioni ambacho kinadhihirisha hatari ya prolapsi ya kambakitovu au kuachilia kwa plasenta.
 • Utagundua dalili za hatua ya pili ya leba kabla ya wakati uliopangwa kwa uchunguzi wa uke. (Kisanduku 5.1 linaorodhesha dalili za hatua ya pili ya leba)

Ukiwa na tajriba huhitaji uchunguzi wa uke kufahamu wakati mjamzito yuko karibu kusukuma.

Kisanduku 5.1 Dalili za hatua ya pili

Iwapo mama ana dalili mbili au zaidi ya hizi, kuna uwezekano kuwa ana hatua ya pili ya leba:

 • Anahisi uchungu wa kusukuma ambao hawezi kuuzuia (anasema kuwa ni lazima apitishe kinyesi).
 • Anazuia pumzi au mguno wa kujivuta.
 • Anaanza kutoa jasho.
 • Hali yake inabadilika. Anaanza kulala au kuwa na makini zaidi.
 • Viungo vyake vya uzazi vya nje au mkundu huanza kupanuka na maumivu ya misuli.
 • Anahisi kichwa cha mtoto kikianza kusonga kuelekea kwenye uke.

Mstari wa zambarau huonekana katikati ya matako ya mama yatawanyikapo kutokana na msukumo wa kichwa cha mtoto.

5.1.1 Ni nini hutendeka katika hatua ya pili ya leba?

Katika hatua ya pili, wakati mtoto yuko kwenye uke, viungo vya uzazi vya mama hupanuka kwa kujikaza. Mkundu wake hufunguka kidogo. Katikati ya maumivu ya misuli viungo vya uzazi hupumzika. (Mchoro 5.1)

Mchoro 5.1 Viungo vya uzazi hupumzika katikati ya mikazo

Kila mikazo ya misuli (na kila mama asukumapo) mtoto husonga chini. Katikati ya mikazo, uterasi ya mama hupumzika na kuvuta mtoto juu kidogo. (Mtoto hayuko juu sana kuliko vile alivyokuwa kabla ya mikazo)

Baada ya muda mdogo, utaona kichwa cha mtoto kwa kila mkazo. Mtoto husonga kama wingu la bahari; ndani na nje, lakini kila mara akiwa karibu kuzaliwa. (Vielelezo 5.2a-d)

Mchoro 5.3 Kichwa cha fetasi hunyosha mlango wa uke kwa kiasi cha kiganja chako.

Kichwa cha mtoto kinyooshapo mlango wa uke kwa kiasi cha kiganja chako, kichwa hukaa katika mlango. (Mchoro 5.3) Kichwa kikaapo kwa mlango hata katikati ya mikazo, kichwa kinafanikiwa. Baada ya kichwa kuzaliwa, mwili wote hutoka nje kwa urahisi kwa msukumo mmoja au miwili.

5.1.2 Mtoto husongaje kupitia kwa njia ya uzazi?

Mchoro 5.4 kinaonyesha jinsi mtoto asongapo kupitia kwa njia ya uzazi. Mtoto husonga hivi iwapo kichwa kiko sawa mahali pake na mgongo ukielekea kwenye fumbatio la mama. Lakini watoto wengi hawakai jinsi hii. Mtoto ambaye huangalia upande wa mbele wa mama au atangulizaye matako, husonga kwa njia tofauti. Tazama kila uzazi kwa karibu uone jinsi watoto husonga katika hali tofauti tofauti.

Mchoro 5.4 Miendo saba mikuu ya mtoto katika leba na uzaaji.

5.2 Msaidie mama na mtoto wawe na uzaaji ulio salama

Endelea kuangalia dalili muhimu za mama ulivyofanya katika hatua ya kwanza ya leba.

Mchoro 5.5 Angalia mpigo wa moyo wa fetasi katika hatua ya pili ya leba.

5.2.1 Angalia mpigo wa moyo wa mtoto

Mpigo wa moyo wa mtoto husikika kwa ugumu katika hatua ya pili. Kwa kawaida moyo wa mtoto huwa chini katika fumbatio la mama. Ikiwa una ujuzi, unaweza kusikia mpigo wa moyo wa mtoto katikati ya mikazo. Unaweza kuusikia vizuri chini ya fumbatio la mama, karibu na mfupa wa kinena (Mchoro 5.5). Mpigo unaweza kuwa kiwango cha chini ya midundo 100 kwa dakika wakati wa mikazo mama anaposukuma. Lakini kinapaswa kurudi kwa kiwango cha kawaida mara tu mikazo inapoisha.

 • Je, mpigo wa fetasi wa kawaida ni upi?

 • Kwanzia mipigo 120 hadi 160 kwa dakika.

  Mwisho wa jibu

Ikiwa mpigo wa moyo wa mtoto hautarudi kwa kiwango cha kawaida ndani ya dakika 1, anaweza kuwa na matatizo. Au iwapo mpigo utabakia kiwango ya chini ya mipigo 100 kwa dakika, mtoto anaweza kuwa na matatizo. Mweleze mama alale kwa upande, na upime mpigo wa moyo wa mtoto tena. Ikiwa kwa kiwango cha chini, mwambie mama asisukume wakati wa mikazo michache. Hakikisha anavuta pumzi sana ili mtoto apate oksijeni ya kutosha.

5.2.2 Msaidie mama wakati anaposukuma

Mchoro 5.6 Kwa upole mhimize mama kusukuma anapohisi haja hiyo.

Seviksi ikipanuka kikamilifu, mwili wa mama husukuma mtoto nje. Baadhi ya wahuduma wa afya hupatwa na furaha sana wakati wa hatua ya kusukuma. Wanampigia mama kelele, "Sukuma! Sukuma "! Lakini kina mama kawaida hawahitaji kusaidiwa ili kusukuma. Miili yao husukuma kwa kawaida. Wakati wanahimizwa na kuungwa mkono, mara nyingi wanawake husukuma kwa jinsi sawa na kutoa mtoto nje.

Ikiwa vigumu kwa mama kusukuma, usimkemee au kumtisha. Kamwe usimtusi au kumpiga mama ili kumfanya asukume. Ikiwa mama amekasirika au ana uoga, kuzaa kunaweza kuendelea polepole. Badala yake muelezee jinsi ya kusukuma vizuri ( Mchoro 5.6). Kila mkazo wa uterasi ni nafasi mpya. Msifu kwa kujaribu.

Mwambie mama unapoona sehemu zake za siri zinapotokezea nje. Mueleze kwamba mtoto anasonga chini. Utakapoona kichwa, uliza mama aiguse. Anaweza kusukuma bora zaidi.

Mwache mama achague upande anahisi ndio nzuri kwake. Ulijifunza kuhusu pande mbalimbali katika kipindi cha kwanza katika Kipindi cha 3 cha Somo. Kumbuka kwamba si vizuri kwa mama kulala chali katika uzaaji wa kawaida. Iwapo analala chali, mishipa inayopelekea mama na mtoto damu hufinywa. Uzaaji unaweza kuendelea polepole.

Mchoro 5.7 Hali tofauti tofauti katika hatua ya pili ya leba.

Tazama dalili za hatari

Usisukume uterasi chini ili kusaidia mama kusukuma mtoto. Kusukuma uterasi kunaweza kusababisha plasenta kutengana au kupasuka kwenye uterasi.

Tazama mwendo wa kila uzalishaji. Iwapo uzalishaji utachukua muda mrefu mno, mpeleke mama hospitalini. Mpeleke mama hospitalini ili kuzuia matatizo makubwa au hata kifo akiwa katika leba.

Watoto wa kwanza wanaweza kuchukua saa 2 kamili ya mikazo na kusukuma vizuri ili azaliwe. Watoto wa pili na wa baadaye kwa kawaida huchukua chini ya saa 1. Tazama mwendo wa kichwa cha mtoto kinavyosonga chini kwa njia ya uzazi. Katika uzalishaji wa kawaida na ulio na afya, mtoto anaendelea kusonga chini (polepole sana), na mpigo wa moyo wa mtoto ni ya kawaida. Mama ana nguvu ya kutosha. Mhimize mama kusukuma mpaka kichwa kitokee.

Ikiwa mama atasukuma kwa muda mrefu bila maendeleo, matatizo makubwa yanaweza kutokea. Leba ambayo haiendelei inaweza kusababisha fistula, kupasuka kwa uterasi, pia kifo cha mtoto au mama. (Katika Kipindi cha 10, ulijifunza kuhusu kupasuka kwa uterasi.) Viungo vya uzazi vya mama vinapaswa kuvimba baada ya mama kusukuma kwa nguvu kwa dakika 30. Ikiwa viungo vya uzazi havivimbi, au uvimbe mdogo hautazidi, kichwa kinaweza kuwa hakisongi chini. Iwapo mama atasukuma kwa muda wa saa 1 na mtoto hasongi chini, atahitaji usaidizi.

Iwapo kipindi cha leba kitazidi wakati huu bila maendeleo yanayofaa, mpe mama rufaa mara moja:

 • Saa 1 bila maendeleo yanayofaa (multigravida)
 • Saa 2 bila maendeleo yanayofaa (primigravida)

Wakati kipindi cha pili cha leba kinapoendelea vizuri, utaona mabadiliko muhimu pahali pa kichwa cha mtoto. Mpe mama rufaa ya hospitali au kituo cha afya mara moja ukiona dalili hizi:

 • Mama yuko katika kipindi cha pili cha leba, lakini mtoto hajashuka.
 • Kaputi au ufinyanzi wa fuvu uliozidi kutokea kwa mtoto.

5.3 Tekeleza uzalishaji wa mtoto

Ujuzi na maamuzi yako ni muhimu ili kupunguza wasiwasi kwa mama na kuhakikisha uzalishaji ulio salama kwa mtoto. Ulipata ujuzi na uamuzi kupitia uzoefu. Hata hivyo ni lazima uchukue hatua hizi hata ikiwa una ujuzi:

 • Tazama leba inavyoendelea.
 • Zuia maambukizi.
 • Mpe mama utulizo wa kihisia na wa kimwili.
 • Tarajia matukio ya kawaida.
 • Tambua leba isiyo ya kawaida au tatizo la fetasi.

5.3.1 Zuia kuraruka kwa ufa wa uke

Kutokea kwa kichwa cha mtoto kinaweza kurarua ufa wa uke wa mama. Shikilia uke ili kuzuia miraruko. Ukeketaji wa wasichana huwa kawaida katika baadhi ya jamii. (Kutahiriwa kwa wanawake pia huitwa ukeketaji.) Kitendo hiki cha kitamaduni kinachodhuru husababisha kovu zisizopanuka kutoshea mtoto kupita. Au kovu inaweza kuraruka mtoto anapozaliwa.

5.3.2 Toa kichwa cha mtoto wakati anapozaliwa

Mchoro 5.8 Msaidie kutoa kichwa cha mtoto.

Nawa mikono vizuri na uvae glavu safi na vifaa vingine vya kukinga vimelea.

Safisha eneo la msamba kwa kutumia antiseptiki na uweke nguo safi juu ya mapaja ya mama.

Finya msamba kwa kutumia mkono mmoja kwa uthabiti. (Msamba ni ngozi iliyo kati ya ufa wa uke na mkundu.) Mkono huu huweka kidevu cha mtoto karibu na kifua chake. Katika mtindo huu, kichwa hutoka kwa urahisi (Mchoro 5.8). Funika mkundu wa mama na kipande cha nguo. Mara kwa mara mama husukuma kinyesi (mavi) anaposukuma mtoto.

Kwa utaratibu, tumia mkono wako mwingine kufinya kichwa cha mtoto kiteremke chini. Kufinya huku kwa utaratibu, huweka kichwa cha mtoto kiiname chini.

Baada ya kichwa kutokea ukeni, uso hujitokeza kwenye msamba.

Safisha pua na kinywa cha mtoto. Inaweza kubidi usafishe pua na kinywa cha mtoto kabla ya mwili wote kutoka ili aweze kupumua. Ikiwa mtoto ana kamasi au maji kwa pua au kinywa chake, funga kidole kwa kitambaa safi na uyapanguze kwa utaratibu.

5.3.3 Angalia kama kambakitovu iko shingoni mwa mtoto

Mara nyingi mapumziko huwa kati ya kutokwa kwa kichwa na wa mabega wakati wa kuzaa. Katika mapumziko haya, hisi kambakitovu shingoni mwa mtoto.

 • Kambakitovu inaweza kufungwa ikiwa kimelegea shingoni mwa mtoto. Kitoe kichwani au kwa mabega ya mtoto.
 • Kambakitovu kinaweza kuwa kimejikaza mno au kinaweza kuwa kimezunguka shingoni mwa mtoto zaidi ya mara moja. Jaribu kuilegeza na uitoe kupitia kichwani.
 • Labda huwezi kulegeza kambakitovu. Pengine kambakitovu inamzuia mtoto kutoka. Uiunganishe na uikate kambakitovu.

Tumia kemikali ya tiba inayotumiwa kusitisha kutoka kwa damu na makasi ambayo si kali kushikilia na kukata kambakitovu. Au utumie uzi safi na wembe mpya. (Kemikali ya tiba inayotumiwa kusitisha kutoka kwa damu hushikilia.) Shikilia au ufunge vipande viwili kisha ukate katikati (Mchoro 5.9). Usikate mama au shingo ya mtoto.

Ikiwa utakata kambakitovu kabla ya mtoto kuzaliwa, lazima mama asukume kwa nguvu na umtoe mtoto haraka. Bila kambakitovu, mtoto hukosa oksijeni hadi aanze kupumua.

Mchoro 5.9 Kukata kambakitovu ikiwa imezunguka shingo ya mtoto.

5.3.4 Toa mabega ya mtoto

Baada ya kichwa kutoka, mtoto hugeuka na kutazama miguu ya mama. Ngoja mikazo ya baadaye. Mwambie mama asukume kwa utaratibu atakapohisi mikazo. Kwa kawaida, mabega ya mtoto hutoka nje. Ili kuzuia miraruko, jaribu kutoa bega moja kwa wakati ( Mchoro 5.10).

Usiinamishe kichwa cha mtoto sana. Elekeza kichwa lakini usikivute!

Mchoro 5.10 Kutoa mabega wakati wa uzalishaji mama akiwa kwa upande mbalimbali.

5.3.5 Kuzalisha mwili wa mtoto

Baada ya mabega kutolewa, mwili kwa kawaida hutoka nje bila matatizo. Na ukumbuke kwamba watoto huwa wameloa na watelezi. Kuwa mwangalifu usimwangushe mtoto!

Mweke mtoto juu ya fumbatio ya mama. Panguza mtoto na nguo safi na umfunike na blanketi mpya iliyosafi. Mpatie mtoto joto. Funika kichwa cha mtoto kwa kofia au blanketi. Ikiwa mtoto anaonekana yuko sawa, mruhusu mtoto anyonye mara moja. Hauhitajiki kusubiri hadi plasenta itoke au kambakitovu ikatwe.

5.3.6 Kata kambakitovu

Kawaida huhitajiki kukata kambakitovu mara moja. Iwache ikiwa imeshikilia ili kumsaidia mtoto kumpatia madini ya iron ya kutosha katika damu yake. Baadhi ya damu hutoka kwa plasenta kupitia kambakitovu hadi kwa mtoto. Unaposubiri kukata kambakitovu, lazima mtoto akae juu ya fumbatio ya mama, ambapo ndipo pahali pazuri zaidi kwa mtoto. Subiri hadi kambakitovu iache kudunda na ionekana kama ikiwa tupu.

Hata hivyo, ikiwa mama ana maambukizi ya VVU au hali yake haijulikani, kata kambakitovu mara tu baada ya kukauka na kupata joto.

Mchoro 5.11 Kata kambakitovu.

Tumia uzi au klampu safi kufunga kwa nguvu au uweke klampu kwa kambakitovu kwa upana wa vidole viwili kutoka fumbatio ya mtoto. (Hatari ya mtoto kupata maambukizi ya pepopunda ni makubwa wakati kambakitovu imekatwa mbali na mwili.) Funga fundo la mraba (Mchoro 5.11).

Weka uzi nyingine safi au klampu kwa upana wa kidole kimoja mbali na fundo la kwanza. Iwapo huna klampu kwenye kambakitovu karibu na mama, ongezea fundo la tatu vidole viwili kutoka kwa fundo la pili. Kuweka fundo mara mbili kwa kambakitovu hupunguza hatari ya kutokwa na damu.

Tumia makasi au wembe safi kukata kambakitovu baada ya fundo la pili. (Kwa mfano, fundo la kwanza liko sentimita 3 kutoka fumbatio la mtoto na la pili liko kwa umbali wa sentimita 5.)

5.4 Huduma ya mtoto baada ya kuzaliwa

Sehemu hii inaelezea huduma muhimu kwa mtoto. Utajifunza jinsi ya kumpatia pumzi mtoto ambaye hawezi kupumua katika Kipindi cha 6 cha Somo.

5.4.1 Kuzuia maambukizi na utunzaji wa kambakitovu

Ili kuzuia maambukizi kwa mama na mtoto, fuata hatua hizi:

 • Nawa mikono yako.
 • Safisha msamba wa mama.
 • Usiweke vitu visivyo safi katika uke.
 • Safisha pahali pa kuzalia.
 • Tumia vifaa safi kufunga na kukata kambakitovu.

Weka gutu ya kambakitovu safi na iliyokauka ili kuzuia maambukizi. Safisha tu kwa sabuni na maji safi iwapo imechafuka. Kumbuka:

 • Usifunike au kuweka kitu chochote.
 • Kama kambakitovu inavuja damu, ifunge tena.

Gutu kwa kawaida huanguka siku 4-7 baada ya kuzaa. Wakati gutu bado imeshikilia, iweke nje ya napi na mbali na mkojo na kinyesi.

Usiweke uchafu au kinyesi cha mnyama kwenye gutu la kambakitovu! Uchafu au kinyesi cha mnyama hazilindi gutu, bali husababisha maambukizi hatari.

5.4.2 Kagua mtoto

Watoto wengi huwa macho na wana nguvu wanapozaliwa. Wengine huanza polepole, lakini muda unapoendelea, wanapumua na huendelea vizuri zaidi. Wanapata nguvu na ngozi ya bluu hupunguka. Mara tu baada ya kuzaliwa, safisha njia za kupumua na uamshe mtoto wakati unapompanguza. Ili kufahamu hali ya afya ya mtoto, tathmini mambo haya:

 • Upumuaji: Watoto wanapaswa kuanza kupumua kwa kawaida baada ya sekunde za kuzaliwa. Watoto ambao hulia baada ya kuzaliwa kawaida wanaweza kupumua vizuri. Watoto wengi hupumua vizuri na hawalii.
 • Rangi: ngozi ya mtoto inapaswa kuwa rangi ya kawaida. Mtoto hapaswi kuwa na ngozi nyeupe au bluu.
 • Mkazo wa misuli: Mtoto anapaswa kusongesha mikono na miguu kwa nguvu.

Kagua mambo haya yote ndani ya dakika za kwanza baada ya kuzaliwa.

5.4.3 Joto na upatanaji

Watoto wachanga wanaweza kupatwa na baridi sana. Mshauri mama awe na mgusano kati ya ngozi yake na ya mtoto. Wafunike wote wawili na blanketi safi, iliyokauka mara tu baada ya kuzaliwa kabla ya kukata kambakitovu.

Mwili wa mama humpatia mtoto joto. Harufu ya maziwa ya mama humtia mtoto hamu ya kunyonya. Kuwa mwangalifu na mtoto mchanga. Saa ya kwanza ndio bora zaidi ya mama na mtoto kuwa pamoja. Wasitenganishwe kukaa pamoja wakati huu husaidia kuanzisha unyonyeshaji wa mapema iwezekanavyo.

5.4.4 Unyonyeshaji wa mapema

Mchoro 5.12 Unyonyeshaij ni nzuri kwa mama na mtoto.

Iwapo kila kitu ni sawa baada ya kuzaa, muulize mama amnyonyeshe mtoto mara moja (Mchoro 5.12). Baadhi ya kina mama wanahitaji usaidizi hapo mwanzoni. Maziwa ya kwanza ina rangi ya manjano na huitwa kolostramu. Baadhi ya kina mama hudhani kuwa kolostramu ni mbaya kwa mtoto na hivyo hawanyonyeshi siku ya kwanza. Lakini kolostramu ni muhimu sana! Kolostramu imejaa protini na hulinda mtoto dhidi ya maambukizo.

 • Unyonyeshaji hufanya uterasi ipate mikazo. Mikazo husaidia plasenta kutoka na huzuia kutokwa na damu nyingi.
 • Unyonyeshaji humsaidia mtoto kutoa kiowevu kutoka kwa pua na kinywani chake hivyo hupumua kwa urahisi zaidi.
 • Unyonyeshaji humsaidia mama na mtoto kujuana.
 • Unyonyeshaji humfariji mtoto.
 • Unyonyeshaji unaweza kumsaidia mama kupumzika na kuhisi vizuri kuhusu mtoto wake.

Iwapo mtoto hawezi kunyonya, chunguza kama ana kamasi kwenye pua yake. Ili kumsaidia kamasi kutoka, mweke mtoto kwa kifua cha mama kichwa chake kikiwa chini zaidi kuliko mwili. Gonga mgongo wa mtoto polepole kutoka kiunoni hadi kwa mabega. Baada ya kamasi kutoka, msaidie mama kumweka mtoto kwenye titi tena. Utajifunza kuhusu unyonyeshaji katika Moduli ya huduma baada ya kujifungua.

Muhtasari wa Kipindi cha 5

Katika Kipindi cha 5, ulijifunza mambo haya:

 1. Hatua ya pili ya leba inaanza wakati seviksi imepanuka kabisa na huisha wakati mtoto amezaliwa. Toa uzingatiaji wa karibu, huduma yenye ujuzi, na hatua ya haraka kwa uzalishaji salama, safi.
 2. Dalili hizi zinaonyesha hatua ya pili ya leba: mama anahisi hamu isiyozuilika ya kusukuma na anashikilia pumzi yake au kupumua kwa nguvu wakati wa mikazo. Mama anaanza kutoa jasho na hali ya sununu yake inageuka. Viungo vya uzazi vya nje au mkundu wa mama hujitokeza nje wakati wa mikazo. Mama anahisi kichwa cha mtoto kikisongea kwenye uke. Mstari wa zambarau unajitokeza katikati ya makalio ya mama.
 3. Angalia dalili muhimu za mama. Angalia mpigo wa moyo wa fetasi na kiwango cha uteremkaji wa kichwa cha mtoto. Angalia mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba leba inaendelea kwa kawaida.
 4. Chunguza dalili za hatari ya kuwa leba haiendelei na umpe mama rufa.
 5. Msaidie mama wakati anasukuma na kuzaa mtoto.
 6. Ikiwa kambakitovu imezungushwa shingoni mwa mtoto, ikate kabla ya mwili kuzaliwa. Halafu hakikisha kwamba mama anasukuma kwa nguvu ili mtoto atoke nje haraka.
 7. Dumisha usafi wakati wote wa leba na wa kuzaa. Usafi huzuia maambukizi kwa mama na mtoto.
 8. Mpatie mtoto mchanga joto na uhakikishe kuwa anapumua vizuri.
 9. Anzisha unyonyeshaji wa mapema.

Maswali ya kujitathmini ya Kipindi cha 5

Sasa kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, jibu maswali haya kutathmini ulichojifunza. Angalia majibu yako na nakala juu ya Maswali ya kujitathmini hapo mwisho.

Maswali ya kujitathmini 5.1 (Malengo ya Somo la 5.1, 5.2, na 5.3)

Ni maelezo gani ambayo si kweli? Katika kila hali, eleza ni lipi lisilo sahihi.

 • A.Upanuzi kamili wa seviksi hadi sentimita 10 ndio ishara muhimu zaidi kwamba hatua ya pili ya leba imeanza.
 • B.Katika hatua ya pili, sehemu za siri za mama hutokea wakati wa mikazo na hupungua katikati ya mikazo.
 • C.Kujichomozani wakati kichwa cha mtoto huzaliwa kabisa.
 • D.Katika uzaaji wa kawaida, mtoto huteremka kwenye njia ya uzazi akiangalia upande wa mbele wa mwili wa mama. Mgongo wa mtoto ukiangalia upande wa uti wa mama
 • E.Wakati mtoto yuko katika njia ya uzazi, Mpigo wa moyo huongezeka wakati wa mkazo.
 • F.Katika hatua ya pili ya leba, mruhusu mama kuchagua ni upande gani ule anahisi angependelea kukaa wakati anapopata hisi ya kusukuma.
Answer
 • A.ni kweli. Upanuzi kamili wa seviksi hadi sentimita 10 ndio ishara muhimu zaidi kwamba hatua ya pili ya leba imeanza.
 • B.ni kweli. Katika hatua ya pili, viungo vya uzazi vya mama hutokea wakati wa mikazo na hupungua katikati ya mikazo.
 • C.si kweli. Kujichomoza ni wakati kichwa cha mtoto hupanua ufunguzi wa uke hadi ukubwa wa kiganja chako. Kichwa hukaa katika ufunguzi hata kati ya mikazo.
 • D.si kweli. Katika uzaaji wa kawaida, mtoto huteremka kwenye njia ya uzazi na huangalia nyuma ya mwili wa mama. Mgongo wa mtoto huangalia upande wa fumbatio yake.
 • E.si kweli. Wakati mtoto akiwa katika njia ya uzazi, mpigo wa moyo wa fetasi huenda chini (sio haraka) ikiwa na mkazo.
 • F.ni kweli. Katika hatua ya pili ya leba, mruhusu mama kuchagua ni upande gani ule anahisi angependelea kukaa wakati anapopata haja ya kusukuma.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 5.2 (Malengo ya Somo la 5.3)

Orodhesha dalili 4 za kuonyesha kuwa hatua ya pili ya leba haiendelei kwa njia ya kawaida.

Answer

Dalili za kuonyesha kwamba hatua ya pili haiendelei kawaida ni pamoja na hizi:

 • Mpigo wa moyo wa fetasi inakaa zaidi au chini ya kiwango cha kawaida (midundo 120-160 kwa dakika) hata kati ya mikazo.
 • Amnioni Kutoka kwa ghafla ukeni, ambayo inaweza kuonyesha hutokaji wa kambakitovu au kuachilia kwa plasenta.
 • Mama aliye Multigravida anasukuma kwa saa 1 na mtoto hajateremka kwa njia ya uzazi. Au mama aliye primigravida anasukuma kwa saa 2 na hakuna maendeleo mazuri.
 • Mtoto hateremki na ukuaji wa kaputiau ufinyanzi mwingi wa fuvu ya fetasi.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 5.3 (Malengo ya Somo la 5.4)

Fikiria kwamba kichwa cha mtoto kimezaliwa. Subiri mkazo ujao ili kutoa mabega ya mtoto wakati wa uzalishaji. Unapaswa kufanya nini ikiwa kambakitovu imezunguka shingo ya mtoto?

Answer

Kwanza, jaribu kulegeza kambakitovu na uipitishe juu ya kichwa cha mtoto. Iwapo huwezi kuilegeza na inazuia mtoto kutoka, weka klampu kwa kambakitovu katika maeneo mawili. (Au ifunge na uzi iliyofishwa vimelea.) Kata kambakitovu katikati ya klampu. Usimkate mama au shingo ya mtoto.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 5.4 (Malengo ya Somo la 5.4 na 5.5)

Panga upya hatua hizi katika mpangilio sahihi wa uzalishaji wa mtoto na mara tu baadaye.

 • A.Baada ya kichwa cha mtoto kutolewa wakati wa kuzaa, panguza pua na kinywa ili kumsaidia kupumua.
 • B.Nawa mikono yako vizuri na uvae glavu safi na mavazi mengine ya kujikinga.
 • C.Ili kuzuia kuraruka kwa msamba wa mama, toa mabega ya mtoto mmoja kwa wakati.
 • D.Finya msamba wa mama kwa nguvu na mkono mmoja.
 • E.Wakati mtoto amezaliwa, mweke juu ya fambatio ya mama na umpanguze na nguo safi.
 • F.Safisha sehemu ya msamba wa mama kwa antiseptiki.
 • G.Weka klampu au funga kambakitovu katika maeneo mawili na ukate katikati ya hizo klampu.
 • H.Tumia mkono wako mwingine polepole kuweka pumzi ya kueleka juu ya kichwa cha mtoto ili kujipinda chini.
 • I.Funika mtoto ili kumpatia joto na umnyonyeshe mara moja.
 • J.Tumia kipande cha nguo au shashi kufunika mkundu wa mama ikiwa kinyesi chochote kitatoka nje wakati anaposukuma.
 • K.Chunguza kama kambakitovu haijazunguka shingo ya mtoto.
Answer

Mpangilio huu ndio sahihi:

 • B Nawa mikono yako vizuri na uvae glavu safi na mavazi mengine ya kujikinga.
 • F Safisha sehemu ya msamba wa mama na antiseptiki.
 • D Bana msamba wa mama kwa nguvu na mkono mmoja.
 • J Tumia kipande cha nguo au shashi kufunika mkundu wa mama ikiwa kinyesi chochote kitatoka nje wakati anaposukuma.
 • H Tumia mkono wako mwingine kuweka polepole pumzi ya kuelekea juu ya kichwa cha mtoto kwelekea chini ili kujipinda chini. A Baada ya kichwa cha mtoto kuzaliwa, mpanguze pua na kinywa ili kumzaidia kupumua.
 • K Chunguza kama kambakitovu haijazunguka shingo ya mtoto.
 • C Ili kuzuia kuraruka kwa msamba wa mama, toa mabega ya mtoto mmoja kwa wakati.
 • E Wakati mtoto amezaliwa, mweke juu ya fambatio ya mama na umpanguze kwa nguo safi.
 • I Funika mtoto ili kumweka joto na humnyonyeshe mara moja.
 • G Weka klampu au funga kambakitovu katika maeneo mawili na ukate katikati ya hizo klampu.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 5.5 (Malengo ya Somo 5.5)

Ni kwa jinsi gani unaweza kuhamasisha mama na mtoto wake kujuana?

Answer

Ili kusaidia mama na mtoto wake kujuana, weka mtoto haraka juu ya fumbatio ya mama mara tu anapozaliwa. Mnyonyeshe mapema. Usitenganishe mama na mtoto wake katika saa la kwanza baada ya kuzaliwa.

Mwisho wa jibu