Skip to main content
Printable page generated Tuesday, 16 April 2024, 8:04 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Tuesday, 16 April 2024, 8:04 PM

7. Uhaishaji wa Mtoto mchanga

Kipindi cha 7 cha somo Uhaishaji wa mtoto mchanga

Utangulizi

Mara tu mtoto anapozaliwa, lazima mkunga amchunguze mtoto huyo mchanga haraka ili kuamua ikiwa anahitaji usaidizi wa kupumua. Ni sharti utambue dalili za jumla za hatari kwa mtoto huyo kwa sekunde chache. Kumshughulikia mtoto kwa haraka huzuia matatizo mabaya au hata kifo iwapo mtoto huyo hapati oksijeni ya kutosha. Watoto wengi hupumua wenyewe mara tu wanapozaliwa. Unahitaji tu kuzifuata hatua za utunzaji wa kimsingi wa mtoto mchanga zilizotolewa katika Kipindi cha 5 cha Somo. Utazisoma kwa kina katika Moduli ya Utunzaji wa baada ya ujauzito. Hatua hizi zimeelezewa tena katika Moduli ya Udhibiti Changani wa Maradhi ya Watoto wachanga na ya Utotoni.

Kipindi hiki cha somo kinaangazia watoto wachanga wasioweza kupumua vizuri. Utajifunza jinsi ya kuwahaisha na kuwasaidia kupumua kikawaida. Pia, utajifunza jinsi ya kutofautisha kati ya mtoto mwenye afya na yule aliye na asifiksia kwa kadiri au kwa kiwango kikubwa. Asifiksia humaanisha kukosa oksijeni kutokana na matatizo katika kupumua. Pia utajifunza kuhusu hatua mwafaka utakazochukua. Kipindi hiki cha somo ni maalum, kwani habari nyingi zinatolewa kwa njia ya michoro (Mchoro).

Malengo ya Masomo ya Kipindi cha 7

Baada ya Kipindi hiki cha somo, utaweza:

7.1 Kufafanua na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyo katika herufi nzito. (Swali la kujitathmini 7.2)

7.2 Kutoa kwa muhtasari dalili za asifiksia ya watoto wachanga zinazoashiria kuwa unapaswa kuanza uhaishaji (uhaisho) wa mtoto mchanga. (Swali la kujitathmini 7.1)

7.3 Kueleza jinsi ya kutumia mbinu za wastani za uhaisho kuwasaidia watoto wachanga kupumua. (Maswali ya kujitathmini 7.1 na 7.2)

7.4 Kutambua vifaa unavyopaswa kuwa navyo ili kumhaisha mtoto mchanga na jinsi ya kuvitumia ifaavyo. (Swali la kujitathmini 7.3)

7.5 Kueleza vitu usivyotakiwa kufanya unapomtathmini mtoto kwa matatizo ya kupumua. (Swali la kujitathmini 7.4)

7.6 Kutoa muhtasari wa hatari kuu za kiafya na huduma muhimu kwa watoto wachanga. (Swali la kujitathmini 7.5)

7.1 Upumuaji na uhaishaji wa mtoto mchanga

Sehemu hii inaanza kwa muhtasari wa kile kinachofanyika iwapo ni sharti mtoto apumue kivyake. Ni lazima mtoto mchanga apitie na azoee mabadiliko kutoka kwa maisha ya ndani ya uterasi ya mama hadi ya nje.

7.1.1 Jinsi mtoto mchanga mwenye afya anavyopumua

Kwa kawaida, mtoto mwenye afya hupumua mwenyewe mara tu baada ya kuzaliwa (Picha 7.1). Iwapo kupumua kulianza kwenyewe na mtoto anapumua bila kusaidiwa, mambo haya ni kweli:

  • Fetasi haikupata asifiksia ilipokuwa kwenye uterasi.
  • Mfumo wa kupumua unafanya kazi vizuri.
  • Mfumo wa moyo na mishipa ya damu unafanya kazi vizuri.
  • Ubongo unaratibu mizunguko inayohitajika kwa mfululizo wa upumuaji bora. (Ubongo unafanya kazi vizuri.)
Picha 7.1 Mtoto mchanga aliyezaliwa baada ya kutimiza muda kamili wa ujauzito na anayepumua vizuri ana ngozi yenye rangi ya waridi na mikono na miguu iliyokunjwa kiasi. Amebadilika vyema kutoka kwa uterasi ya mama hadi nje. (Picha: Dr Mulualem Gessese)
  • Je, unachunguza vipi hali njema ya mtoto wakati wa leba na kuzaa?

  • Fetasi yenye afya ina midundo ya moyo kati ya 120 na 160 kwa dakika. Membreni za fetasi zinapopasuka, kiowevu cha amnioni kinachovuja kutoka ukeni mwa mama huyo ni angavu. Kiowevu hakina rangi nyekundu ya damu au rangi ya kijani au nyeusi ya mekoniamu. (Mekoniamu ni kinyesi cha kwanza cha mtoto.)

    Mwisho wa jibu.

Umechunguza mdundo wa moyo wa fetasi mara kwa mara katika kipindi chote cha leba. Uliyaandika matokeo kwenye patografu jinsi ulivyojifunza katika Kipindi cha 4 cha somo. Ulimpa mama rufaa iwapo mtoto ambaye hajazaliwa alionyesha dalili za kuathirika. Kwa hivyo, usishughulikie uzazi wa mtoto aliye na asifiksia. Hata hivyo, matatizo katika uzazi yanaweza kutokea bila kutarajiwa au unaweza kuitwa kumhudumia mwanamke aliye katika kipindi cha pili cha leba. Kwa hivyo, ni lazima ujue jinsi ya kumhaisha mtoto mchanga iwapo utashughulikia uzazi wa mtotot aliye na asifiksia.

7.1.2 Asifiksia ya mtoto mchanga

Jinsi ulivyojifunza katika Kipindi cha 4 cha somo, asifiksia ni uhaba wa oksijeni. Asifiksia kwenye uterasi husababishwa wakati ambapo damu ya mama haina oksijeni ya kutosha. Asifiksia kwenye uterasi pia husababishwa na tatizo kwenye plasenta. Asifiksia kwenye uterasi inaweza kusababisha mambo haya:

  • Asifiksia wakati wa kuzaliwa (kidogo, kiasi, au kali).
  • Ugumu katika kusoma au kudhoofika kwa ufahamu. Haya yote huonekana mtoto anapokua. Seli za ubongo huharibiwa kutokana na ukosefu wa oksijeni katika leba na kuzaa.
  • Kifo cha mtoto huyo mchanga.

Mbadilishano wa gesi hutendeka kwa kila pumzi. Oksijeni kutoka kwa hewa iliyovutwa ndani hufyonzwa ndani ya damu inapopita kwenye mapafu. Dioksidi ya kaboni hutolewa kwenye damu hadi kwenye hewa inayotolewa nje.

Hata hivyo, asifiksia ya mtoto mchanga husababishwa na mambo matatu:

  • Mtoto kukosa kupumua baada ya kuzaliwa.
  • Moyo wa mtoto huyo mchanga hauwezi kusukuma damu ya kutosha kwenye mapafu kwa mbadilishano wa gesi.
  • Mtoto huyo mchanga ana viwango vya chini vya hemoglobini (anemia) na kwa hivyo hawezi kutoa oksijeni ya kutosha mwilini mwake.

Mtoto asiyeweza kupumua vyema hawezi kuishi kivyake nje ya mwili wa mama yake. Uhashaji wa mtoto mchanga humsaidia aweze kupumua mwenyewe na kupeleka oksijeni kwenye ogani na tishu zake. Ni lazima ubongo upate oksijeni haraka au uharibike. Unaweza kuhitaji kumhaisha mtoto aliye na anemia kali kutokana na kupoteza damu wakati wa leba na kuzaa. Huenda uhitaji kumhaisha mtoto anayeendelea kuwa na sinosisi hata kama anapumua vizuri. Sinosisi ni ugeukaji wa rangi ya midomo na ngozi kuwa samawati. Sinosisi hutokea wakati ambapo damu haina oksijeni ya kutosha (Picha 7.2).

Picha 7.2 Mtoto aliyezaliwa kabla ya kutimiza muda kamili na mwenye matatizo: Anaonekana mwenye sinosisi (samawati). Mikono na miguu yake ni laini kwa sababu misuli yake ni dhaifu. Ana matatizo ya kupumua. (Picha: Dr Mulualem Gessese)

Ili kuepuka matatizo ya mara moja na ya muda mrefu ya asifiksia, lazima umsaidie mtoto yeyote mchanga asiyeweza kupumua vizuri.

7.2 Aina za uhaishaji wa mtoto mchanga

Jifunze hizi aina tatu za uhaishaji wa mtoto mchanga.

Upitishaji wa hewa safi: Tumia mfuko wa ambu unaotumika kwa mkono (Picha 7.3). Iweke barakoa kwenye pua na mdomo wa mtoto na usukume hewa kwenye mapafu ya mtoto huyo. (Wakati mwingine wataalamu wa afya hutumia neno “uwekaji mfuko wa ambu” kumaanisha upitishaji wa hewa safi.)

Picha 7.3 Mbinu ya kuhaisha ya upitishaji hewa safi ikijaribiwa kwa mwanasesere wa kusomea kwa kutumia mfuko wa ambu. (Picha: Dr Yifrew Berhan)
  • Ufyonzaji: Tumia sirinji ya balbu kuondoa kamasi na viowevu kwenye pua na kinywa cha mtoto.
  • Usingaji wa moyo: Finya kifua cha mtoto kwa mkazo mkali na hafifu ili kuchochea mpigo wa moyo (Picha7.4).
Picha 7.4 Mbinu ya usingaji wa moyo ikijaribiwa kwa mwanasesere wa kusomea. Unaweza kuona chombo cha kupitisha hewa upande wa juu wa kulia wa picha hii. (Picha: Dr Yifrew Berhan)

7.2.1 Vifaa vya kimsingi vinavyohitajika kwa uhaishaji wa mtoto mchanga

  • Vitambaa viwili safi vya kitani au pamba: kimoja cha kumpanguzia mtoto huyo mchanga na kingine cha kumfunikia mtoto baadaye.
  • Sirinji ya plastiki aina ya balbu ya kuondolea viowevu kwenye kinywa na pua, hasa akiwa na mekoniamu.
  • Mfuko wa ambu na barakoa vya kumpa mtoto oksijeni moja kwa moja kwenye mapafu.
  • Mtu kama wewe aliyehitimu katika uwanja wa uhaishaji.
  • Ikiwezekana, kifaa cha kutoa joto, kwa mfano taa.

7.2.2 Kabla ya uhaishaji

Kabla ya kuanza aina yoyote ya uhaishaji, chunguza mambo haya:

  • Ikiwa mtoto yuko hai: Iwapo mtoto mchanga haonekani kuwa hai, kwanza kisikize kifua chake kwa stethoskopu. Usiposikia mpigo wa moyo, mtoto tayari amefariki (Jedwali 7.1).
  • Ulitambua kiwango cha asifiksia. Ikiwa unaweza kusikia mpigo wa moyo, lakini unaukadiria kuwa chini ya mipigo 60 kwa dakika, kwanza msinge moyo. Kisha, pitisha hewa safi ukisita na kuendelea, hadi mipigo ya moyo iwe zaidi ya 60 kwa dakika (Jedwali 7.1).
  • Mtoto hajachafuliwa na mekoniamu: Iwapo mtoto amechafuliwa na mekoniamu (Picha 7.5), kwanza fyonza kwenye kinywa, pua na maeneo ya koromeo. Au iwapo kaviti za kinywa na pua zimejaa kiowevu chenye mekoniamu (Picha 7.5), kwanza fyonza kwenye kinywa, pua na maeneo ya koromeo. Upitishaji wa hewa hufanya tatizo kuwa baya zaidi. Upitishaji wa hewa huingiza kiowevu chenye mekoniamu kwenye mapafu ya mtoto. Kiowevu kwenye mapafu huzuia mbadilishano wa gesi.
Picha 7.5 Mtoto huyu hapumui. (Kifua na pua havisongi.) Mekoniamu iko kwenye mwili wote. (Picha: Dr Mulualem Gessese)

7.3 Tathmini kiwango cha asifiksia

Watoto walio na asifiksia kiasi au kali wanahitaji huduma makini ya uhaishaji. Jifunze jinsi ya kutambua kiwango cha asifiksia kwa mtoto mchanga. Tathmini kama mtoto yuko hai au amefariki katika sekunde 5 baada ya kuzaliwa. Iwapo yuko hai, kadiri kiwango cha asifiksia. Huenda mtoto aliye na asifiksia kali asipumue kabisa. Hasongezi mikono wala miguu yake. Rangi ya ngozi yake ni samawati sana au nyeupe sana. Mtoto asiyeweza kupumua au anayetweta ili kupata hewa anahitaji huduma ya dharura. Mtoto anayepumua chini ya pumzi 30 kwa dakika pia anahitaji huduma ya dharura. Mtoto asipopumua punde tu baada ya kuzaliwa, ubongo wake unaweza kuharibika au kufariki. Ukiwahaisha watoto vizuri na kwa haraka, wengi wao wanaweza kuongoka.

Jedwali 7.1 linaorodhesha mambo utakayochunguza ili kutathmini kiwango cha asifiksia kwa mtoto mchanga. Pia, tazama picha za watoto wachanga walio na viwango tofauti vya asifiksia (Picha 7.1, 7.2 na 7.5).

Mtoto mchanga anayetweta anaweza tu kuvuta pumzi chache na kwa ugumu. Mitweto mikubwa kati ya kila pumzi pia ni tatizo. Mtoto mchanga anayetweta, kwa kawaida huwa karibu kufariki.

Jedwali 7.1 Tathmini kiwango cha asifiksia.
DaliliHakuna asifiksiaAsifiksia ndogoAsifiksia kiasiAsifiksia kali
Mpigo wa moyoZaidi ya mipigo 100 kwa dakikaZaidi ya mipigo 100 kwa dakikaZaidi ya mipigo 60 kwa dakikaChini ya mipigo 60 kwa dakika
Rangi ya ngoziWaridiBuluu kidogoBuluu wastaniBuluu sana
Mkondo wa kupumuaKuliaKuliaKupumua lakini sio sanaKutopumua wala kutweta
Kusonga kwa miguu na mikonoInasonga vizuriKusonga kidhaifuKutosongaKutosonga
Kuchafuliwa na mekoniamuLaLaLabdaKawaida
UhaishajiHakuna hajaMwitiko wa harakaMwitiko mzuriAnachukua muda mrefu kuitika

Tathmini kiwango cha asifiksia chini ya sekunde 5. Fanya hivyo haraka lakini usiwe na hofu.

Lazima utoe huduma ya kumhaisha mtoto katika muda wa dakika moja baada ya kuzaliwa. Kwa hivyo, ni rahisi kukadiria mpigo wa moyo kuliko kuhesabu. Ni rahisi na haraka kutazama mkondo wa pumzi zake kuliko kuhesabu kiwango cha pumzi. Jedwali 7.2 linaorodhesha dalili zinazoonyesha kilicho na kisicho cha kawaida baada ya kuzaliwa.

Jedwali 7.2 Ugunduzi wa kawaida na usio wa kawaida kwa mtoto mchanga mara tu baada ya kuzaliwa.
IsharaUgunduzi wa kawaidaUgunduzi usio wa kawaida
RangiYafaa kuwa waridi

Buluu au yenye sinosisi (ukosefu wa oksijeni ya kutosha)

Nyeupe, (weupe) anemia

Umanjano

PumziPumzi 40-60 kwa dakika

Hakuna pumzi

Kiwango cha kupumua ni chini ya 30 kwa dakika

Mitweto (pumzi chache mno na zenye ugumu)

Kiwango cha mpigo wa moyoMipigo 120-160 kwa dakika

Hakuna mpigo wa moyo

Mpigo wa moyo ni chini ya 100 kwa dakika

 
Siha ya misuliMikono na miguu ya mtoto aliyezaliwa baada ya kutimiza umri kamili wa ujauzito imeyojikunja kidogoKujikunja duni kwa miguu na mikono, dhaifu (Picha 7.2), inayoashiria asifiksia kali inayoathiri ubongo
MatendohiariMtoto huhisi na kuitika kidole kinapowekwa kwenye kaakaa la kinywa chakeMtoto hahisi wala kuitika unapoligusa kaakaa la kinywa chake.

“Chini ya” inaweza kubadilishwa na alama , kwa mfano > 30 kwa dakika.

7.4 Utaratibu wa uhaishaji wa mtoto mchanga

Kabla ya kwenda kuzalisha, hakikisha una vifaa utakavyohitaji katika kuhaisha na kumpa mtoto mchanga huduma ya haraka. Sehemu hii inaeleza hatua utakazochukua baada ya kutathmini kiwango cha asifiksia.

7.4.1 Sekunde tano za kwanza

Jedwali 7.3 linatoa muhtasari wa mambo utakayofanya ukiona dalili za asifiksia katika sekunde 5 za kwanza baada ya mtoto kuzaliwa. Habari zaidi zimetolewa baada ya maelezo haya ya jumla.

Jedwali 7.3 Vitendo kama mwitiko kwa dalili za asifiksia ya mtoto mchanga
Mtoto mchanga anafanya niniTathminiKitendo
Analia na kusongesha miguu na mikono Labda mtoto ni mwenye afyaUhaishaji hauhitajiki
Anapumua kidhaifu, hasongeshi mikono wala miguu, ana sinosisi kiasiLabda ana asifiksia kiasi

Pitisha hewa safi ukisita

Kadiria kiwango cha mpigo wa moyo

Halii, hapumui, hatweti wala kusongesha mikono na miguu. Mikono na miguu ni dhaifu. Ana sinosisi au mwili wake una mekoniamuLabda asifiksia kali

Ita msaidizi (jamaa au mtu mwingine).

Tumia sirinji ya balbu. Fyonza kwenye kinywa, pua na maeneo ya koromeo chini ya sekunde 5.

Pitisha hewa ukisita

Halii, hapumui, hatweti wala kusongesha mikono na miguu. Mikono na miguu ni dhaifu. Ana sinosisi au mwili wake una mekoniamuKiwango cha mpigo moyo ni zaidi ya 60 kwa dakika
Halii, hapumui, hatweti wala kusongesha mikono na miguu. Mikono na miguu ni dhaifu. Ana sinosisi au mwili wake una mekoniamu Kiwango cha mpigo moyo ni chini ya 60 kwa dakikaTekeleza vitendo vyote vilivyo kwenye jedwali hili na pia uusinge moyo (Picha 7.4).

7.4.2 Chunguza kiwango cha mpigo wa moyo wa mtoto mchanga

Mpigo wa moyo wa apeksi ni jina la mpigo wa moyo unaosikika kwa moyo kwenye upande wa kushoto wa kifua kwa kutumia stethoskopu (Picha 7.6). Unaitwa “wa apeksi” kwa sababu utausikia moja kwa moja kutoka juu ya moyo.

  • Je, idadi ya mipigo ya moyo kwa kila dakika inayopimiwa kwenye sehemu zingine mbali na moyo huitwaje?

  • Huitawa mpwito wa ateri.

    Mwisho wa jibu

Njia nyingine ya kuhesabu mipigo ya moyo wa mtoto mchanga ni kuhisi mpwito mwanzoni mwa kiungamwana (Mchoro 7.6).

Mchoro 7.7 Tazama na uhesabu mipigo ya apeksi na uhisi mpwito chini ya kiungamwana.

7.4.3 Shughuli za kwanza

Fanya shughuli hizi kwa watoto wote wachanga bila kuzingatia kiwango cha asifiksia:

  1. Kwa haraka mpanguze mtoto asiwe na viowevu juu ya mwili wake (Mchoro 7.7).
  2. Hakikisha mtoto ana joto.
  3. Ondoa vizuizi vyovyote kwenye mdomo na pua (Picha 7.9).
  4. Mpapase kwa upole ili kuchochea aanze kupumua au kumsaidia katika kupumua (Mchoro 7.10).
  5. Wakati huo huo, kadiria kiwango cha asifiksia (Majedwali 7.1 hadi 7.3).
  6. Mweke mtoto kwa nafasi bora tayari kwa uhaishaji ukiona dalili za asifiksia (Picha 7.11).

Chunguza kila picha kwa makini. Soma muhtasari na maelezo yazo.

7.4.4 Mpanguze mtoto kwa haraka na uhakikishe anapata joto

Mlalishe mtoto mahali penye joto mbali na vitu. Tumia taa yenye joto au vifaa vingine vya kupasha joto juu ya kichwa ikiwa vipo. Kisha, mpashe mtoto joto (Mchoro 7.8).

Mchoro 7.8 Mlalishe mtoto chali na umpanguze kikamilifu. Ondoa kitambaa hicho kilicholowa. Geuza kidevu chake kiasi cha kumweka mtoto katika hali ifaayo na uhakikishe kuwa njia zake za kupisha hewa zimefunguka.

Mweke mtoto karibu sana na mama kiasi kwamba ngozi zao zinagusana kisha uwafunike na blanketi lenye joto. Funika kichwa cha mtoto na kofia au shali yenye joto.

7.4.5 Ondoa vizuizi kwenye kinywa na pua

Ikiwa sirinji aina ya balbu ipo:

Fyonza kwenye kinywa kwanza, kisha pua (Mchoro 7.9).

Usifyonze kwa kina kwa sirinji aina ya balbu! Ufyonzaji wa kina unaweza kupunguza kiwango cha mpigo wa moyo (bradikadia).

Ondoa vinyeso kwenye kinywa na pua kwa kitambaa safi kikavu.

Mchoro 7.9 Fyonza mtoto mchanga kwa sirinji aina ya balbu ili kuondoa kamasi kwenye njia yake ya upande wa juu ya hewa. Fyonza kinywa kwanza kisha pua.

7.4.6 Mguse kwa upole ili kumchochea kuanza upumuaji au kumsaidia katika kupumua

Mchoro 7.10 Mpe mguso chochelezi kwa upole. Sugua fumbatio la mtoto ukienda juu na chini. Papasa upande wa chini wa nyayo kwa vidole vyako.

Usimchochee kwa vitendo hivi.

Aina hizi za kuchochea ni hatari na zinaweza kumjeruhi mtoto huyu mchanga.

  • Usimpige kofi mgongoni.
  • Usimminye ngome ya mbavu.
  • Usisukume mapaja ya mtoto kwenye fumbatio lake.
  • Usitanue msuli (sfinkta) wa mkundu.
  • Usitumie vishinikizo moto au baridi wala kumwogesha kwa maji moto au baridi.
  • Usitingize kiungamwana.

7.4.7 Iwapo utatambua asifiksia, anza uhaishaji!

Mlalishe chali mtoto huyu mchanga huku shingo lake likiwa limenyooshwa kidogo jinsi ilivyoonyeshwa kwenye picha ya kwanza katika mchoro 7.11. Fyonza kinywa na pua kwa sirinji aina ya balbu. Kufyonza hufungua njia ya hewa (Picha 7.9).

Mchoro 7.11 Weka kichwa katika nafasi ambapo njia yake ya hewa itakuwa wazi: Mchor wa kwanza ni sahihi. Kidevu kimegeuzwa kiasi kifaacho. Katika mchoro wa katikati, kichwa kimeinamishwa nyuma sana. Shinikizo linabana umio wa pumzi (trakea) shingoni mwake. Katika mchoro wa mwisho, kichwa hakijainamishwa vya kutosha. Kidevu kimekaribia kifua sana na njia ya hewa imebanwa.
  • Simama upande wa kichwa cha mtoto (Mchoro 7.12).
Mchoro 7.12 Nafasi mwafaka ya kumweka mtoto mchanga unapotumia mfuko wa ambu.

Ikiwa mpigo wa moyo wa apeksi ni zaidi ya mipigo 60 kwa dakika:

  • Pitisha hewa kwa barakoa yenye ukubwa ufaao na mfuko wa ambu unaopitisha hewa wenyewe. Barakoa inafaa kutosha jinsi ilivyoonyeshwa katika Mchoro 7.13. Tengeneza kizibo imara kati ya barakoa na uso wa mtoto ili hewa isipite kutoka kwa barakoa hiyo. Usilazimishe barakoa kwenye uso wa mtoto, kwani unaweza kusukuma kidevu kuelekea kwenye kifua cha mtoto na uishie kubana njia yake ya hewa. (Mchoro wa tatu katika Mchoro 7.11.)

Ikiwa mpigo wa moyo wa apeksi ni chini ya mipigo 60 kwa dakika:

  • Usinge moyo (Mchoro 7.4) na upitishe hewa safi kwa kusita kwa mfuko wa ambu.
Mchoro 7.13 Ukubwa unaofaa na usiofaa wa barakoa: Mchoro ulio upande wa juu ni sahihi: barakoa inafunika kinywa, pua na kidevu. Mchoro ulio chini upande wa kushoto si sahihi: barakoa ni kubwa sana na inafunika macho huku ikiendelea na kufunika kidevu pia. Mchoro ulio chini upande wa kulia si sahihi: barakoa ni ndogo sana na haifuniki pua wala mdomo.

7.4.8 Pitisha hewa safi kwa kiasi cha pumzi 40 kwa dakika

Hesabu kwa sauti: “pumzi-mbili-tatu” huku ukipitisha hewa safi (Mchoro 7.14). Finya mfuko huku ukisema “pumzi” na uachilie shinikizo kwa mfuko huku ukisema “mbili-tatu”. Hesabu hii hukusaidia kupitisha hewa safi ukitumia wizani kwa kiwango kinachofaa kwa mapafu ya watoto wachanga.

Kiasi cha hewa unayoingiza na kutoa ndani ya mapafu ni sawa na takriban pumzi 40 kwa dakika. Tumia shinikizo la kutosha ili kutimiza mwinuko na mshuko mpole kwa kifua cha mtoto. Pumzi chache za kwanza zinaweza kuhitaji shinikizo la juu. Shinikizo litakuwa jingi sana iwapo mtoto ataonekana kupua kwa nguvu sana.

Mchoro 7.14 Pima muda wa kiwango cha kupitisha hewa huku ukisema “pumzi-mbili-tatu”.

7.4.9 Chunguza motto huku ukumpitishia hewa

Dalili bora ya upitishaji mzuri wa hewa na ubora wa hali ya mtoto ni ongezeko katika kiwango cha mpigo wa moyo hadi mipigo 100 kwa dakika.

  • Je, ni mabadiliko yapi mengine utakayotarajia kuona kwa mtoto unapompa hewa ikiwa uhaishaji unaendelea vizuri?

  • Utatarajia kuona ngozi ya mtoto ikibadilika kutoka rangi ya samawati au buluu hafifu sana hadi rangi bora ya waridi. Mtoto anaanza kusonga kidogo, anaanza kukunja mikono na miguu yake na haonekani mdhaifu sana.

    Mwisho wa jibu

Je, unapoacha kumpa hewa safi kwa muda, mtoto huyo anaweza kupumua au kulia bila kusaidiwa? Dalili hizi ni nzuri. Watoto wengi hupata nafuu haraka sana baada ya muda mfupi wa kupewa hewa safi. Hata hivyo, endelea kumchunguza mtoto hadi utakapohakikisha kuwa anapumua vizuri mwenyewe.

Ikiwa mtoto anabaki mdhaifu au anapumua kwa kusita baada ya dakika 30 za kupewa hewa safi, mpe mama na mtoto rufaa haraka. Wape rufaa waende katika kituo cha afya au hospitali ambapo watoto wasiopumua vizuri husaidiwa. Enda nao na umpe mtoto hewa safi safarini hadi mtakapofika. Hakikisha mtoto ana joto wakati wote. Watoto wachanga hupoteza joto kwa urahisi. Mtoto asiyepumua vizuri mwenyewe anaweza kupata baridi nyingi na afariki. Mchoro 7.15 Inatoa muhtasari wa hatua katika uhaishaji wa mtoto mchanga ulizosoma katika sehemu ya 7.4.

Mchoro 7.15 Muhtasari wa hatua katika uhaishaji wa mtoto mchanga

7.5 Utunzaji muhimu wa mara moja wa mtoto mchanga

Sehemu ya mwisho ya Kipindi hiki cha somo inakukumbusha kuhusu utunzaji muhimu wa mtoto mchanga. Toa utunzaji huu kwa watoto wote pasipo kujali iwapo wana dalili za asifiksia. Kiungamwana kinapokatwa, mabadiliko mengi ya kifisiolojia mwilini mwa mtoto humsaidia kuzoea maisha ya nje ya mwili wa mama yake. Ni vigumu sana kumudu nje kuliko ndani ya uterasi ambapo ni salama. Toa utunzaji wa kimsingi kwa mtoto mchanga ili kumsaidia kujikinga dhidi ya hatari za kiafya zilizoorodheshwa katika Kisanduku 7.1.

Kisanduku 7.1 Hatari za Kiafya kwa watoto wachanga

Watoto wachanga huhitaji utunzaji ili kuzuia matatizo haya:

  • Damu kutoka yenyewe kwenye ufereji wa utumbo kutokana na ukosefu wa vitamini K
  • Kutokwa na damu kutokana na majeraha yanayotokana na uzazi (hujitokeza baadaye zaidi baada ya kuzaa ambapo skalpu hufura na kuhitaji rufaa ya haraka)
  • Maambukizi ya macho kutokana na Klamidia trakomati na Kisonono cha Neiseria. (Bakteria hizi ni visababishi vikuu vya maambukizi ya zinaa. Mtoto anaweza kupata maambukizi haya anapopita kwenye njia ya uzazi.)
  • Baadhi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama polio na kifua kikuu.
  • Hipothemia (kuwa baridi sana)
  • Hipoglisimia (kiwango cha chini cha glukosi kwenye damu)
  • Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama hadi kwa mtoto iwapo mama ana VVU.

Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo yamejadiliwa kwa kina katika Moduli ya Magonjwa ya kuambukiza, Vikao vya 3 na 4 vya Somo.

Uzuiaji wa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama hadi kwa mtoto umeelezewa katika Moduli ya Utunzaji katika ujauzito, Kipindi cha 17 cha Somo. Dawa na utaratibu wa uzuiaji wa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama hadi kwa mtoto umeelezewa katika Moduli ya Magonjwa ya kuambukiza, Kipindi cha 27 cha Somo.

Kwa kuzingatia hatari za kiafya zilizo kwenye Kisanduku 7.1, wape watoto wote utunzaji huu muhimu:

  • Funga kiungamwana upana wa vidole viwili kutoka kwa fumbatio la mtoto. Funga maara ya pili upana wa vidole viwili kutoka kwa kifungo cha kwanza. Kata kiungamwana katikati ya kifungo cha kwanza na cha pili. Hakikisha kuwa shina la kiungamwana halitoki damu na si fupi sana.
  • Weka lihamu ya tetrasiklini kwenye macho mara moja tu. Lihamu hii hukinga dhidi ya maambukizi ya macho.
  • Dunga sindano iliyo na miligramu 1 ya vitamini K kwenye msuli upande wa mbele katikati mwa paja. Vitamini K huzuia damu kutoka yenyewe.
  • Mpe kipimo cha kwanza ya chanjo ya polio kwa kinywa na dawa ya chanjo dhidi ya kifua kikuu (BCG).
  • Mweke mtoto kwenye fumbatio la mama katika hali ya mgusano wa ngozi kwa ngozi na mama. Wafunike kwa blanketi na uweke kofia au shali yenye joto kwenye kichwa cha mtoto. Ni lazima kiwango cha joto cha mtoto kisalie zaidi ya sentigredi 36.
  • Hakikisha kuwa mtoto ananyonya vizuri na mama anatoa maziwa ya kutosha. Iwapo maziwa ya mama hayapendelewi, hakikisha kuwa chakula mbadala cha kutosha kipo. Anzisha unyonyeshaji mapema bila kumpa chakula kingine chochote ila kuna sababu mwafaka za kutonyonyesha. Kwa mfano, mama aliye na VVU hawezi kunyonyesha.
  • Iwapo mama ana VVU, mpe mtoto matibabu ya kumkinga dhidi ya VVU.

Ratiba ya uchanjaji ya chanjo zote zilizo kwenye Moduli ya Uchanjaji.

Utajifunza yote kuhusu unyonyeshaji katika Moduli yaUtunzaji baada ya kuzaa. Unyonyeshaji na VVU vimeelezewa katika Moduli ya Magonjwa ya kuambukiza, Kipindi cha 27 cha Somo.

Muhtasari wa Kipindi cha 7

Katika Kipindi cha 7, umejifunza mambo haya:

  1. Dalili za asifiksia kwa watoto wachanga wakati wa kuzaliwa ni: ugumu katika kupumua, kutweta, au kutopumua, mpigo wa moyo usio wa kawaida, udhaifu wa misuli (miguu na mikono dhaifu), kukosa kusonga, ngozi kuwa na rangi ya samawati (sinosisi) au kuchafuliwa na mekoniamu.
  2. Tathmini kiwango cha asifiskia katika sekunde 5 za kwanza baada ya mtoto kuzaliwa, wakati sawa na utakapoanza kutoa utunzaji wa kimsingi kwa mtoto mchanga. (Kwa mfano mpanguze mtoto, hakikisha anapata joto, kisha ufunge na ukate kiungamwana.)
  3. Kwa mtoto asiyepumua vizuri, fyonza mdomo na pua haraka na uanze kumhaisha.
  4. Chunguza kuhakikisha kuwa mtoto yuko hai. (Sikiliza mpigo wa apeksi wa moyo.) Chunguza kuhakikisha kuwa kiwango cha mpigo wa moyo ni zaidi ya mipigo 60 kwa dakika. (Ikiwa kiwango hiki ni chini ya mipigo 60 kwa dakika, usinge moyo kabla ya uhaisho.) Chunguza kuwa mtoto hajachafuliwa na mekoniamu. Fyonza uondoe mekoniamu kabla ya kumhaisha mtoto.
  5. Mweke mtoto katika hali ambapo shingo lake litanyooka ili kuzifungua njia za hewa. Mwekee barakoa ya kuingiza hewa safi inayotosha sawasawa juu ya mdomo na pua lake. Mpe hewa safi kwa kiwango cha pumzi 40 kwa dakika.
  6. Chunguza dalili zozote za nafuu: chunguza; rangi ya waridi, kusonga, na uwezo wa kupumua bila usaidizi. Usipoona nafuu baada ya dakika 30 za kumpa hewa safi, mpe rufaa haraka iwezekanavyo.
  7. Fanya shughuli zote za utunzaji muhimu kwa mtoto mchanga. Utunzaji kwa kiungamwili. Mdunge sindano ya vitamini K na lihamu ya macho ya tetrasaiklini. Anzisha kunyonyesha mapema na pasipo kumpa mtoto chakula kingine chochote. Hakikisha dawa za kuzuia VVU zimepeanwa ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 7

Kwa kuwa umekamilisha Kipindi hiki cha somo, jibu maswali haya ili utathmini kujifunza kwako. Linganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya Kujitathmini mwishoni mwa Moduli hii.

Kwanza soma Uchunguzi Kifani 7.1 kisha ujibu maswali yanayofuata.

Uchunguzi Maalum 7.1 Mtoto hawezi kupumua

Atsede, mwanamke wa umri wa miaka 25, aliletwa katika Kituo chako cha Afya. Alikuwa katika leba nyumbani kwake kwa muda wa saa 38. Muda tu baada ya kufika kwako, akazaa mtoto mvulana aliyetimiza umri kamili wa ujauzito. Ulimtathmini na kugundua haya: hakujaribu kupumua, hakusongesha miguu wala mikono yake, mwili wake wote ulikuwa umefunikwa na mekoniamu yenye kiowevu cha amnioni, bado hakujaribu kupumua ulipompanguza na kumpa mguso wa kumsisimua.

Maswali ya kujitathmini 7.1 (yanatathmini Malengo ya Masomo 7.2 na 7.3)

  • a.Je, mtoto huyu ana asifiksia? Iwapo ndiyo, asifiksia imefika kiwango kipi?
  • b.Je, hatua zako za mara moja ni zipi? Utafanya nini baadaye?
  • c.Je, matatizo ya kuzaliwa kwa mtoto huyu mchanga yangezuilika, na iwapo ndiyo, kivipi?
Answer
  • a.Mtoto huyu ana asifiskia kali. Unaona dalili nyingi za hatari. Hakujaribu kupumua. Hakusongesha mikono wala miguu yake. Alikuwa amefunikwa na mekoniamu na mguso wa kumsisimua haukusaidia.
  • b.Hatua itakayofuata ni kumpanguza haraka na kumfunika gubigubi. Ondoa mekoniamu kwenye mdomo na pua lake kwa sirinji aina ya balbu na kitambaa safi. Sikiliza mpigo wa moyo wa apeksi. Ikiwa mpigo huu uko chini ya mipigo 60 kwa dakika, singa moyo. Singa moyo na kupitisha hewa safi kwa zamu kwa kiwango cha takriban pumzi 40 kwa dakika.
  • c.Matatizo ya kuzaliwa kwa mtoto huyu mchanga yangeweza kuzuiliwa. Mtaalamu wa uzazi angemsaidia Atsede mapema katika leba yake. Mhudumu angechunguza ishara za kuathirika kwa fetasi na kumpa rufaa kwa utunzaji wa dharura. Saa 38 ni nyingi sana kungoja.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 7.2 (linatathmini lengo la Somo 7.4)

Orodhesha vifaa vya kimsingi unavyopaswa kuwa navyo ili kumhaisha mtoto mchanga asiyeweza kupumua.

Answer

Unahitaji vifaa hivi vya kimsingi kwa kumhaisha mtoto mchanga asiyeweza kupumua:

  • Vitambaa viwili safi vya kitani au pamba: kimoja cha kumpanguza na kingine cha kumfunika baadaye
  • Sindano ya plastiki aina ya balbu ya kuondoa vinyeso kwenye mdomo na pua hasa kama kuna mekoniamu
  • Mfuko wa ambu na barakoa za kumpa hewa safi moja kwa moja hadi mapafuni mwake
  • Mtu aliyehitimu katika uwanja wa uhaishaji wa mtoto mchanga (kama wewe)
  • Kifaa cha kutoa joto (taa) ili kumpa joto, ikiwezekana

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 7.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 7.1, 7.2, 74, 7.5 na 7.6)

Je,ni kauli ipi isiyo sahihi? Eleza kisicho sahihi kwa kila kauli.

  • A.Mtoto mchanga akilia mara tu baada ya kuzaliwa ni isahara kuwa asifiksia ilitokea kabla ya kuzaa.
  • B.Sinosisi inamaanisha kuwa mtoto amefunikwa na mekoniamu.
  • C.Mpigo wa moyo wa apeksi unaweza kugunduliwa kwa kusikiliza kifua cha mtoto kwa stethoskopu.
  • D.Mbadilishano wa gesi mapafuni hutendeka dioksidi ya kaboni inapoingizwa huku oksijeni ikitolewa nje.
  • E.Sindano ya vitamin K kwa watoto wachanga huzuia maambukizi ya macho.
  • F.Kiwango kilichopendezwa cha kuwapa watoto wachanga hewa safi ni pumzi 40 kwa dakika.
Answer

A si sahihi. Mtoto mchanga akilia mara tu baada ya kuzaliwa huwa ishara kuwa asifiksia haijatokea au haikutokea kabla ya kuzaliwa.

B si sahihi. Sinosisi inamaanisha kuwa ngozi ina rangi ya samawati kutokana na upungufu wa oksijeni (asifiksia).

C ni sahihi. Mpigo wa moyo wa apeksi unaweza kugunduliwa kwa kusikiliza kifua cha mtoto kwa stethoskopu.

D si sahihi. Mbadilishano wa gesi mapafuni hutendeka dioksidi ya kaboni inapotolewa nje huku oksijeni ikiingizwa.

E si sahihi. Sindano ya vitamini K kwa watoto wachanga ni ya kuzuia kutokwa na damu. Lihamu ya tetrasiklini inayopakwa machoni huzuia maambukizi ya macho.

F ni sahihi. Kiwango kilichopendekezwa cha kuwapa watoto hewa safi ni pumzi 40 kwa dakika.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 7.4 (linatathmini lengo la Somo 7.4)

Je, njia zilizopendekezwa za kumsisimua mtoto mchanga ni zipi? Je, ni njia zipi zilizo hatari na zisizoruhusiwa?

  • Mpige kofi kwa mgongo.
  • Fikicha fumbatio kwa upole juu na chini.
  • Finya ngome ya mbavu.
  • Sukuma mapaja kwenye fumbatio.
  • Papasa nyayo za mtoto kwa vidole vyako.
  • Panua msuli wa mkundu.
  • Mwekee vishinikizo moto au baridi, au umwogeshe kwa maji moto au baridi.
  • Tingisha kiungamwana.
Answer

Ni njia mbili tu zilizopendekezwa kumsisimua mtoto kwa upole:

  • Fikicha fumbatio kwa upole juu na chini.
  • Papasa nyayo za mtoto kwa vidole vyako.

Hizo njia zingine zote ni hatari. Usizitumie.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 7.5

Kisanduku7.1 ni muhtasari wa baadhi ya hatari za kiafya zinazotokea sana kwa watoto wachanga na utunzaji muhimu wa mara moja kwa uzuiaji wa matatizo hayo. Baadhi ya majedwali yameachwa na mapengo ili uyakamilishe.

Kisanduku 7.1 la kutumiwa kwa Swali la Kujitathmini 7.5
Hatari ya kiafya kwa mtoto mchanga Utunzaji muhimu wa mara moja kwa Mtoto mchanga
Maambukizi ya macho
Damu kutoka yenyewe
Hipothemia
Hipoglisimia
Answer

Kisanduku 7.1 lililokamilishwa ndilo hili.

Kisanduku 7.1 Lililokamilishwa
Hatari ya kiafya kwa mtoto mchanga Utunzaji muhimu wa mara moja kwa Mtoto mchanga
Maambukizi ya machoWeka lihamu ya tetrasiklini
Damu kutoka yenyeweDunga sindano ya miligramu 1 ya vitamini K kwenye msuli
Hipothemia Mgusano wa ngozi kwa ngozi na mama, blanketi, na kofia
Hipoglisimia Unyonyeshaji wa mapema au chakula mbadala cha kutosha

Mwisho wa jibu