7. Uhaishaji wa Mtoto mchanga

Kipindi cha 7 cha somo Uhaishaji wa mtoto mchanga

Utangulizi

Mara tu mtoto anapozaliwa, lazima mkunga amchunguze mtoto huyo mchanga haraka ili kuamua ikiwa anahitaji usaidizi wa kupumua. Ni sharti utambue dalili za jumla za hatari kwa mtoto huyo kwa sekunde chache. Kumshughulikia mtoto kwa haraka huzuia matatizo mabaya au hata kifo iwapo mtoto huyo hapati oksijeni ya kutosha. Watoto wengi hupumua wenyewe mara tu wanapozaliwa. Unahitaji tu kuzifuata hatua za utunzaji wa kimsingi wa mtoto mchanga zilizotolewa katika Kipindi cha 5 cha Somo. Utazisoma kwa kina katika Moduli ya Utunzaji wa baada ya ujauzito. Hatua hizi zimeelezewa tena katika Moduli ya Udhibiti Changani wa Maradhi ya Watoto wachanga na ya Utotoni.

Kipindi hiki cha somo kinaangazia watoto wachanga wasioweza kupumua vizuri. Utajifunza jinsi ya kuwahaisha na kuwasaidia kupumua kikawaida. Pia, utajifunza jinsi ya kutofautisha kati ya mtoto mwenye afya na yule aliye na asifiksia kwa kadiri au kwa kiwango kikubwa. Asifiksia humaanisha kukosa oksijeni kutokana na matatizo katika kupumua. Pia utajifunza kuhusu hatua mwafaka utakazochukua. Kipindi hiki cha somo ni maalum, kwani habari nyingi zinatolewa kwa njia ya michoro (Mchoro).

Malengo ya Masomo ya Kipindi cha 7