Skip to main content
Printable page generated Sunday, 28 Nov 2021, 11:27
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Sunday, 28 Nov 2021, 11:27

10. Uterasi Iliyoraruka

Kipindi cha 10 Uterasi Iliyoraruka

Utangulizi

Kuraruka kwa uterasi hutokea uterasi inaporaruka au kupasuka kutokana na shinikizo litokanalo na leba iliyozuilika. Urarukaji wa uterasi hutokea sana katika nchi zinazoendelea barani Afrika. Barani Afrika, asilimia 94 ya uzazi hufanyika nyumbani na bila kushughulikiwa na mtaalamu wa afya mwenye ujuzi. Leba ikikamilika kwa kuraruka kwa uterasi, mwanamke huyo anaweza kufariki. Ikiwa mwanamke huyo ataongoka, anaweza kumpoteza mtoto au uterasi yake.

Takribani visa vyote vya urarukaji wa uterasi hutokea kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja hapo awali ambao wamezaa angalau mara moja baada ya ujauzito wao kutimiza umri wa majuma 28. Urarukaji wa uterasi unaweza pia kutokea kwa wanawake walio na kovu kwenye uterasi. Uterasi huraruka tishu ya kovu hili inapofunguka. Hata hivyo, katika nchi zinazostawi, karibu visa vyote vya urarukaji wa uterasi hutokea kwa wanawake wasio na kovu kwenye uterasi ambao leba yao ilizuilika palipokosa utatuzi. Katika kipindi hiki, utasoma kuhusu mambo ya hatari na ishara za kitabibu za uterasi iliyoraruka. Utasoma kuhusu athari kwa mama na mtoto. Utasoma pia jinsi ya kuanza utatuzi unaoweza kuokoa mama na mtoto wake.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 10

Baada ya kipindi hiki, utaweza:

10.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyo kwenye herufi nzito. (Maswali ya kujitathmini 10.1 na 10.2)

10.2 Kueleza mambo yanayoongeza hatari ya urarukaji wa uterasi. Kufafanua ni kwa nini wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wamo katika hatari kubwa zaidi kuliko wale wanaozaa kwa mara ya kwanza. (Swali la kujitathmini 10.2)

10.3 Kueleza ishara za hatari na ishara za kitabibu za urarukaji wa uterasi. Kueleza matatizo yanayotokea sana kutokana na urarukaji wa uterasi. (Maswali ya kujitathmini 10.3 na 10.4)

10.4 Kufafanua jinsi ya kufanya utatuzi kwa wanawake wanaoraruka uterasi ili kuokoa maisha yao. Kueleza hatua utakazochukua ili kupunguza hatari ya urarukaji wa uterasi katika leba. (Swali la kujitathmini 10.4)

10.1 Mambo yanayoongeza hatari ya urarukaji wa uterasi

Ikiwa uzazi umezuilika huku uterasi ikiendelea kunywea, inaweza kuraruka. Tayari unajua kuhusu matatizo ya leba na kuzaa kutoka kwa Vipindi vya 8 na 9. Unapaswa uweze kujibu swali hili.

 • Je, ni mambo yapi yanayoongeza hatari ya urarukaji wa uterasi?

 • Ikiwa leba imezuilika kutokana na visababishi hivi, uterasi inaweza kuraruka:

  • Kutolingana kwa sefalopelvisi: kichwa cha fetasi ni kikubwa sana au pelvisi ya mama ni ndogo sana. Mtoto hawezi kuteremka kwenye njia ya uzazi.
  • Mlalo mbaya wa fetasi au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida: Kwa mfano, mtoto yuko katika mlalo wa kutanguliza matako, uso, paji la uso au bega. Au mtoto yuko katika mlalo wa kutanguliza veteksi ilhali kisogo chake kiko upande wa nyuma wa mama (Kisogo-nyuma ni kwamba kisogo cha mtoto kiko upande wa nyuma wa pelvisi ya mama.)
  • Ujauzito wa zaidi ya fetasi moja: Pacha au watoto zaidi hasa ikiwa “wameshikamana” shingoni au waliounganika.
  • Kizuizi cha kimaumbile: Kitu kitokanacho na maumbile kuzuia mtoto kuteremka. (Kwa mfano, tyuma kwenye fumbatio au uterasi.)
  • Kovu za uterasi.

  Mwisho wa jibu

Visababishi vinne vya kwanza vimeshajadiliwa kwa kina katika vipindi vya hapo awali. Kipindi hiki kinaeleza kutokea kwa kovu kwenye uterasi na visababishi vingine vya urarukaji wa uterasi.

10.1.1 Uterasi yenye kovu

Mwanamke aliyefanyiwa upasuaji kwenye uterasi ana tishu ya kovu mahali ambapo ukuta wa uterasi umepona. Kwa mfano, upasuaji kwa ajili ya kuzaa mtoto au kutoa tyuma kwenye uterasi huacha tishu ya kovu. Tishu ya kovu si nyumbufu kikamilifu kama sehemu ya ukuta wa uterasi isiyo na kovu. Tishu ya kovu haiwezi kutanuka kulingana na minyweo ya leba. Leba ikizuilika kwa muda mrefu, minyweo ya misuli kwenye ukuta wa uterasi inaweza kusababisha kuraruka kwa tishu ya kovu. Uterasi inaweza pia kuwa na kovu ikiwa ilitobolewa katika utoaji wa mimba hapo awali.

10.1.2 Seviksi yenye kovu

Seviksi inaweza kuwa na jeraha kutoka katika uzazi wa awali. Kwa mfano, labda fosepsi zilitumika kusaidia katika uzazi wa mtoto ambaye hakuendelea kutoka baada ya kichwa kujichomoza kwenye vulva. Au uharibifu wa seviksi unaweza kutokea ikiwa vyombo vya upasuaji viliingizwa ndani ya uterasi kupitia ukeni. Wakati mwingine vyombo hutumiwa kudhibiti kutoka kwa damu baada ya kuzaa au kutibu tatizo kwenye uterasi. Matatizo kama haya yanaweza kuwa inflamesheni kwenye bitana ya uterasi. Katika hali hizi, seviksi iliyojeruhiwa hupata tishu ya kovu inayoweza kupasuka na kufunguka katika leba iliyozuilika.

 • Je, unakumbuka majina ya rusu ya misuli kwenye uterasi na bitana ya ndani ya uterasi kutoka katika Moduli ya Utunzaji katika Ujauzito? (Bitana ya ndani ni ambapo plasenta hukua.)

 • Rusu hiyo ya misuli huitwa miometriamu nayo bitana ya ndani ni endometriamu.

  Mwisho wa jibu

10.1.3 Fistula iliyokarabatiwa hapo awali

Ulisoma kuhusu fistula katika Kipindi cha 9. Fistula ni mojawapo ya matatizo makali ya leba iliyozuiliwa. Fistula imeenea sana katika maeneo ya mashambani barani Afrika. Wakati mwingine, mwanamke hupata fistula katika leba ya hapo awali na kisha ikarabatiwe kwa njia ya upasuaji. Fistula inapopona, kovu kubwa zinaweza kutokea na kuzuia kuzaliwa kwa mtoto atakayefuata.

 • Je, ni sehemu ipi ya njia ya uzazi inayopata kovu kutokana na ukarabati wa fistula?

 • Uke. Fistula ni mwanya unaopasuka katikati ya uke na labda kibofu cha mkojo, rektamu, urethra, au ureta.

  Mwisho wa jibu

Washauri kwa dhati wanawake walio na kovu kwenye uterasi, seviksi, au uke kuzaa mtoto wao atakayefuata katika kituo cha afya. Mwanamke huyu anaweza kuhitaji damu na vyombo vya upasuaji, pamoja na ujuzi wa kufanya upasuaji wa kuzaa.

10.2 Kwa nini wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wako katika hatari kubwa ya urarukaji wa uterasi?

Mwanamke aliyezaa mara mbili au zaidi amezaa angalau mtoto mmoja baada ya majuma 28 ya ujauzito. Umri wa ujauzito ni muhimu. Baada ya majuma 28, fetasi hutimiza ukubwa na uzani halisi. Uterasi ya mwanamke huyu tayari imetanuka. Kuzaa kunatarajiwa kuwa rahisi katika ujauzito utakaofuata. Licha ya ukweli huu, ikiwa leba zao zitazuilika, wanawake waliozaa mara mbili au zaidi wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na urarukaji wa uterasi kuliko wale wanaozaa mara ya kwanza.

 • Je, unaweza kupendekeza sababu ya tokeo hili lisilotarajiwa?

 • Sababu moja ni kuwa kina mama wa mara ya kwanza hawana historia ya hapo awali ya matatizo ya ujauzito. Mwanamke aliyezaa mara mbili au zaidi anaweza kuwa na kovu kwenye uterasi au sehemu zingine za njia ya uzazi. Kovu hizi ni visababishi vya hatari ya urarukaji wa uterasi.

  Mwisho wa jibu

10.2.1 Inesha ya uterasi

Sababu nyingine ya wanawake waliozaa mara mbili au zaidi walio na leba iliyokaa kwa muda mrefu au iliyozuilika kuwa katika hatari zaidi ya urarukaji wa uterasi ni kuwa wana minyweo mikali ya leba kwa muda mrefu zaidi kuliko wale wanaozaa kwa mara ya kwanza.

Kwa wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, minyweo ya uterasi huwa mikali kwa takribani saa 24 za kwanza za leba. Baada ya saa 24, minyweo hii hufifia kwa ukali na kuwa mifupi. Baada ya takribani saa 36, uterasi imeishiwa nguvu. Wanawake hawa wanaozaa kwa mara ya kwanza hupata inesha ya uterasi. Ukali wa minyweo hii hufifia kabisa. Minyweo hii hudumu kwa muda mfupi na kutenganishwa na muda mrefu baina ya mnyweo mmoja na mwingine. Kwa kina mama hawa wa mara ya kwanza, minyweo ya uterasi imekaribia kuisha na kwa hivyo urarukaji wa uterasi ni nadra. Kwa upande mwingine, minyweo ya uterasi kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja hubaki mikali, thabiti na ya mara kwa mara kwa muda mrefu zaidi. Wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wanapokuwa katika leba, kuna uwezekano mkubwa wa kuraruka kwa uterasi.

Wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza hukumbwa na matatizo mengine makali. Inesha ya uterasi humaanisha kusalia kwa kichwa cha fetasi kwenye pelvisi ya mama kwa muda mrefu. Hatari ya hipoksia ya fetasi huongezeka, ambayo ni uhaba wa oksijeni kwa fetasi. Hatari ya kutokea kwa fistula huongezeka, ambayo husababisha ubakizaji wa mkojo na maambukizi kwenye kibofu cha mama kilichozuilika.

10.2.2 Usingaji wa kiasili wa fumbatio

Katika sehemu fulani za Afrika, usingaji wa fumbatio katika leba ni tendo la kawaida la kijamii. Usingaji wa fumbatio hufanywa sana leba inapokaa kwa muda mrefu. Wakunga au wanawake wa kijiji hutumia siagi na mafuta ya kulainisha kusugua fumbatio. Wao huminya fandasi ya uterasi ili kujaribu kumsukuma mtoto upande wa chini. Kitendo hiki cha kijamii ni cha kudhuru sana. Usingaji wa fumbatio unaweza kusababisha urarukaji wa uterasi hasa kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja.

10.2.3 Utumiaji mbaya wa vichochelezi vya toni ya uterasi

Ili kudhibiti kipindi cha tatu cha leba, unaweza kutumia dawa ya toni ya uterasi, ambayo huifanya uterasi kunywea. (Dawa hizi ni misoprostol, oxytocin au ergometrine. Zote zimeelezewa kwa kina katika Kipindi cha 6.) Kabla ya kupeana dawa ya toni ya uterasi, hakikisha kuwa uterasi haina fetasi nyingine. Ukimpa dawa ya toni ya uerasi kukiwa na fetasi ndani ya uterasi, uterasi hii inaweza kuraruka na mtoto kupata asfiksia.

 • Je, kwa nini kina mama waliozaa zaidi ya mara moja wamo katika hatari zaidi ya kuraruka kwa uterasi kuliko wenzao wanaozaa mara ya kwanza?

 • Kovu kwenye uterasi ni kisababishi kikuu cha hatari kwa urarukaji wa uterasi. Tishu ya kovu si nyumbufu sana na inaweza kuraruka minyweo inapotokea. Mwanamke aliyezaa zaidi ya mara moja anaweza kuwa na kovu kutokana na upasuaji wa kuzaa au uzazi wenye matatizo ulioijeruhi njia ya uzazi. Uterasi yake pia hunywea kwa muda mrefu. Mwanamke huyu hapati inesha ya uterasi hata ikiwa leba imezuilika.

  Mwisho wa jibu

10.3 Ishara za kitabibu na athari za urarukaji wa uterasi

Urarukaji wa uterasi unaweza kuzuilika ikiwa leba iliyokaa sana itadhibitiwa vyema na hatua ifaayo kuchukuliwa kabla ya uterasi kuraruka.

10.3.1 Ishara za hatari za uterasi inayoelekea kuraruka

Jedwali 10.1 linaonyesha ishara za hatari zinazotokea sana uterasi inapoelekea kuraruka. Ishara hizi ndivyo viashiria bora zaidi kuwa leba imezuilika na kuwa uterasi inaweza kuraruka karibuni. Urarukaji unaweza kutokea ila mtoto azaliwe haraka kwa njia ya upasuaji.

Kisanduku 10.1 Ishara za hatari za kuraruka kwa uterasi
 • Minyweo mikali na ya mara kwa mara ya uterasi inayotokea zaidi ya mara 5 kwa kila dakika 10 na/ au kila mnyweo kudumu kwa sekunde 60 - 90 au zaidi.
 • Kiwango cha mpigo wa moyo wa fetasi kilicho juu ya mipigo 160 kwa dakika au chini ya mipigo 120 kwa dakika, kinachoendelea kwa zaidi ya dakika 10. Ishara hii, mara nyingi, ndiyo huwa ya kwanza kabisa kuonyesha kuwa kuzuilika kunaiathiri fetasi.
 • Kutengenezwa kwa kizingo cha Bandl (Kipindi cha 9 na Mchoro 10.1).
 • Maumivu kwenye sehemu ya chini ya uterasi.
 • Kotokwa na damu ukeni kunaweza pia kuashiria kuraruka kwa uterasi.
Mchoro 10.1 Umbo la kawaida la fumbatio (upande wa kushoto) na uterasi iliyozulika iliyo na kizingo cha Bandl (upande wa kulia), ambacho ni kiashiria cha hatari ya urarukaji unaoelekea.
 • Je, patografu inawezaje kukusaidia kujua kuwa uterasi inaelekea kuraruka?

 • Tumia patografu kuchora idadi ya marudio na muda ambao minyweo itadumu. Chora mabadiliko kwa kiwango cha mpigo wa moyo wa fetasi. Kwa hivyo utagundua haraka ikiwa mojawapo ya idadi hizo zipo katika eneo la hatari lililoonyeshwa katika Jedwali 10.1.

  Mwisho wa jibu

10.3.2 Ishara Zinazoonyesha kuwa uterasi imeraruka

Ishara ya kwanza kuwa uterasi imeraruka ni kukoma kabisa kwa minyweo ya uterasi. Dalili zingine hufuata haraka.

Fumbatio lililofura na lenye maumivu

Maumivu haya huhisika unapoligusa fumbatio. Fumbatio lina maumivu kwa sababu ya kuraruka kwa uterasi na kero lisababishwalo na damu inayojikusanya kwenye kaviti ya fumbatio. Fumbatio linaonekana kuwa lililofura kwa sababu uterasi imejifunga kwa mwili wa fetasi na damu kumwagika ndani ya kaviti ya fumbatio. Kusonga kwa utumbo kumepungua au kumekoma, na kwa hivyo huwezi kusikia sauti za kusonga kwa utumbo kwa stethoskopu. (Kusonga kulikopungua au kulikokoma kwa utumbo huitwa enteroflejia.) Kibofu pia kinaweza kuzuilika, hali inayochangia kufura na maumivu. Muda unaposonga, maambukizi yanaweza kukua kwenye fumbatio na kusababisha kufura zaidi.

Sehemu za fetasi zinazoweza kutomasika kwa urahisi, fetasi kutosonga, na sauti za mpigo wa moyo wa fetasi

Fetasi haiwezi kuishi kwa muda mrefu ndani ya uterasi iliyoraruka. Kwanza, uterasi hujifunga kwa mkazo kwenye mwili wa fetasi. Kisha sehemu fulani za fetasi zinaweza kupita kwenye mikato. Au fetasi nzima iweze kupita hadi kwenye kaviti ya fumbatio. Ukitomasa fumbatio, ni ukuta wa fumbatio tu ulio katikati ya mkono wako na fetasi. Kwa hivyo, unaweza kuhisi sehemu za fetasi kwa urahisi. Ikiwa mtoto amefariki, mama hawezi kumhisi akisonga na huwezi kusikia mpigo wa moyo wake.

10.3.3 Athari kwa mama

Athari za kuraruka kwa uterasi kwa mama hutegemea mambo matatu. Mambo haya ni kiasi cha damu iliyopotea, muda uliopita baada ya mraruko kutokea, na ikiwa kaviti ya fumbatio na mfumo wake wa mzunguko wa damu vimeambukizwa.

Kiasi cha damu iliyopotea

Kuraruka kwa uterasi ni kero linalorarua misuli ya uterasi na mishipa ya damu. Ikiwa mraruko huo utahusisha mishipa mikuu ya damu, hasa ateri za uterasi, damu inayopotea ni nyingi sana. Pasipofanyika utatuzi wa dharura haraka, upotezaji huo wa damu unaweza kusababisha kufariki kwa fetasi. Mama naye atakumbwa na mshtuko kutokana na upotezaji wa damu na kisha afariki. Mraruko ukitokea katika eneo la uterasi ambapo mishipa mikuu ya damu haijahusishwa, mwanamke ana nafasi kubwa ya kuongoka.

Muda uliopita baada ya mraruko kutokea

Wakati mwingine, wanawake hawatokwi na damu sana wala kuwa na hali inayohatarisha maisha. Wanawake hawa hubaki nyumbani kwa saa na hata siku kadhaa baada ya uterasi kuraruka. Hata hivyo, jinsi mwanamke anavyokawia kutibiwa kwa ajili ya uterasi iliyoraruka, ndivyo kiwango cha kupoteza damu , kutofanya kazi kwa figo na maambukizi yanayoenea mwilini mwake yanavyoendelea kuongezeka.

Kuwepo kwa maambukizi

Uterasi iliyoraruka hutoa mwingiliano wa moja kwa moja kati ya njia ya uzazi na kaviti ya fumbatio. Viungo vingine vya ndani vinaweza kujeruhiwa na kuvuja ndani ya fumbatio. (Sehemu za matumbo, rektamu na kibofu zinaweza kujeruhiwa.) Kutokana na haya, viini huenea kwa urahisi kwenye kaviti ya fumbatio. Viini hivi huingia kwenye mzunguko wa damu kupitia kwenye mishipa ya damu iliyoraruka. Ukuaji wa maambukizi kwenye kaviti ya fumbatio huitwa peritonitisi. Maambukizi yanayosambazwa mwilini kwenye mzunguko wa damu huitwa septisemia. Wakati mwingine, mwanamke hustahimili mraruko wa kwanza, bali hatibiwi kwa zaidi ya saa 6. Hatari ya kutokea kwa moja au matatizo haya yote yapo juu sana. Kwa hivyo, unafaa kutambua mapema kuwa mraruko umetokea. Ni lazima umpe mwanamke huyu rufaa haraka. Hatua hizi mbili ni muhimu sana kwa kuokoa maisha ya mama huyo.

Matatizo yanategemea kiasi cha damu iliyopotea, muda uliopita baada ya uterasi kuraruka na hali ya maambukizi yoyote yale. Mwanamke aliye na uterasi iliyoraruka anaweza kukumbwa na baadhi au matatizo haya yote.

Mshtuko utokanao na upotezaji wa damu

Mshtuko utokanao na upotezaji wa damu unaua kwa haraka sana. Mama huwa anahisi dalili hizi:

 • Kupoteza fahamu, kizunguzungu, udhaifu au kuchanganyikiwa
 • Kukwajuka kwa ngozi, na jasho baridi
 • Mpwito wa haraka wa ateri (zaidi ya mipigo 100 kwa dakika) au haraka sana hadi kutoweza kunakiliwa
 • Shikiniko la damu linaloshuka kwa kasi au lisiloweza kunakiliwa
 • Kupumua kwa haraka (zaidi ya pumzi 30 kwa dakika)
 • Wakati mwingine kupoteza fahamu
 • Kupungua sana au kutokuwepo kwa mkojo
Mshtuko wa sepsisi

Mshtuko wa sepsisi hutokea iwapo mraruko au kutokwa na damu kumesababisha septisemia. Ishara zinafanana na zile za mshtuko utokanao na upotezaji wa damu, bali pamoja na kiwango cha juu sana cha joto mwilini (zaidi ya sentigredi 38).

Matatizo mengine
 • Peritonitisi: maambukizi kwenye kaviti ya fumbatio.
 • Kutofanya kazi kwa figo kutokana na kiasi kidogo cha damu.
 • Takribani visa vyote viletwavyo hospitalini hudhibitiwa na histerektomi. (Katika histerektomi, uterasi huondolewa) Kwa hivyo mwanamke hawezi kupata watoto zaidi.
 • Je, ni nini kinachofanyika kwa fetasi uterasi inapoelekea kuraruka na punde baada ya kuraruka?

 • Kabla ya mraruko, kiwango cha mpigo wa moyo kiko zaidi ya mipigo 160 kwa dakika au chini ya mipigo 120 kwa dakika. Baada ya mraruko, uterasi hujifunga kwenye mwili wa fetasi. Damu humiminika kwenye kaviti ya fumbatio na fetasi kufariki haraka ila upasuaji wa haraka uitoe.

  Mwisho wa jibu

10.4 Utatuzi wa uterasi iliyoraruka

Tumia miongozo hii ili kuzuia au kupunguza hatari ya kuraruka kwa uterasi kwa wanawake walio katika leba:

 • Tumia patografu kufuatilia kuendelea kwa mwanamke aliye katika leba. Patografu huhakikisha kuwa unapata dalili mapema ikiwa leba haitaendelea kikawaida. (Ulisoma jinsi ya kutumia patografu katika Kipindi cha 4).
 • Wape wanawake rufaa haraka ukishuku kuwa leba imekaa sana au imezuilika.
 • Wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wanaweza kuwa na kovu kwenye uterasi kutokana na matatizo ya uzazi wa hapo awali. Washauri wazalie katika kituo cha afya ambapo wanaweza kutiwa damu na kufanyiwa upasuaji. Toa ushauri huu kwa mwanamke yeyote aliyetolewa tyuma kwenye uterasi.
 • Waeleze wanajamii kwa nini kutosinga uterasi ni muhimu wakati wa leba au kutoweka shinikizo kwenye uterasi ili kujaribu kuharakisha uzazi. Waambie wasifanye msingo huu hata ingawa ni mazoea ya kiasili.
 • Tumia dawa za toni ya uterasi kusaidia kutoa plasenta lakini tu baada ya kuhakikisha kuwa fetasi ya mwisho imezaliwa.

10.4.1 Kigezo cha rufaa kwa leba iliyokaa sana

Usiache mwanamke akawie katika kipindi cha kwanza au cha pili cha leba kwa muda mrefu. Wape wanawake hawa rufaa haraka.

 • Je, ni lini unapopaswa kumpa rufaa mwanamke aliyezaa zaidi ya mara moja au anayezaa kwa mara ya kwanza ambaye leba yake imekaa kwa muda mrefu? (Kumbuka Kipindi cha 9.)

 • Wape rufaa wanawake walio na ishara hizi za leba iliyokaa sana:

  • Kipindi cha kwanza cha leba fiche kinachokaa zaidi ya saa 8 kabla ya kuingia katika kipindi cha kwanza cha leba dhahiri.
  • Kipindi cha kwanza cha leba dhahiri kinachokaa zaidi ya saa 12 kabla ya kuingia katika kipindi cha pili.
  • Kipindi cha pili cha leba kinachokaa zaidi ya saa moja kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja au zaidi ya saa mbili kwa wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, ila kuzaa kunaelekea kutendeka.

  Mwisho wa jibu

Wajibu wako mkuu ni uzuiaji wa kimsingi. Hakikisha kuwa iwapo leba itazuilika, unaweza kumpeleka mwanamke huyu katika kituo cha afya apate utunzaji wa dharura kwa wakati unaofaa ili kuzuia kuraruka kwa uterasi. Hata hivyo, sababu nyingi zinaweza kuhitaji kuwa umpe mwanamke aliye na uterasi iliyoraruka utunzaji wa dharura. Kisha jukumu lako ni uzuiaji wa baadaye wa maambukizi yanayohusiana na urarukaji wa uterasi.

10.4.2 Uzuiaji wa kimsingi: fika katika kituo cha afya kwa utunzaji wa dharura kabla ya uterasi kuraruka

 • Kumbuka ulichosoma katika moduli ya utunzaji katika ujauzito (Kipindi cha 13) na majadiliano kuhusu jinsi ya kutoa rufaa. Je, ni nini unachopaswa kukumbuka kufanya?

 • Fanya mambo haya unapotoa rufaa:

  • Andika barua ya rufaa iliyo na habari nyingi iwezekanavyo.
  • Andaa mpango wa dharura wa usafirishaji wa jamii kwa mama huyu. Ukiweza, enda naye.
  • Ikiwezekana, wajulishe wahudumu katika kituo hicho cha afya wamtarajie mama huyu. Vituo vingi vya afya vinaweza kuwa katika umbali sawa. Tambua ni kituo kipi kinachoweza kumfanyia upasuaji wa dharura na kumwongeza damu na kisha umtume huko.

  Mwisho wa jibu

10.4.3 Uzuiaji wa baadaye: utunzaji wa dharura kwa mwanamke aliye na mshtuko

Mwanamke aliye kwenye mshtuko anahitaji usaidizi wa haraka. Mtibu haraka ili kuokoa maisha yake.

Mshtuko ni athari isiyoepukika ya uterasi iliyoraruka. Mpe rufaa haraka aende katika kituo cha afya kilicho karibu chenye huduma zinazofaa za utunzaji wa dharura. Njiani, hakikisha kuwa mwanamke amelala miguu yake ikiwa juu kidogo kuliko kichwa chake na kichwa chake kimekunjwa kuelekea upande mmoja (Mchoro 10.2). Hakikisha anapata joto na ametulia.

Mchoro 10.2 Namna ya kumsafirisha mwanamke aliye kwenye mshtuko kwenda hospitalini. Mfunike kwa blanketi ili apate joto.

Ikiwa umefundishwa kufanya haya, anza kwa kumpa viowevu mishipani. Ulisoma jinsi ya kufanya hivi katika Moduli ya utunzaji katika ujauzito, Kipindi cha 22 na katika mafunzo yako ya ujuzi tendaji. Ikiwa ana fahamu, anaweza kunywa maji au viowevu vya kumwongezea maji (chumvi za mdomoni za kuongeza maji). Ikiwa hana fahamu, usimpe kitu chochote mdomoni. Usimpe dawa, kinywaji au chakula.

Unafaa kuwa ulishatimiza matayarisho haya:

 • Hakikisha kuwa ushauri wako wakati wa ujauzito ulimfafanulia kinaganaga jinsi ilivyo muhimu kupata usaidizi maalum anapoenda katika leba.
 • Shawishi familia na jamii ya mwanamke huyu kupangia dharura zinazoweza kutokea. Msaada wa kifedha na usafiri unaweza kuhitajika.
 • Hakikisha kuwa unaweza kufanya utambuzi wa mapema na ufanye taratibu za dharura kabla ya rufaa.
 • Hakikisha kuwa watu wawili wazima wenye afya wanaoweza kumtolea damu wameenda naye. Enda naye ukiweza.

Hatimaye jaribu kupunguza kuchelewa, jambo linaloweza kuwa ndilo tofauti kati ya uhai na mauti. Wanawake wengi waafrika hufariki kutokana na urarukaji wa uterasi kwa sababu wanasita kutafuta usaidizi maalum wakati wa kuzaa. Kisha wanachelewa kutafuta usaidizi wa kimatibabu baada ya urarukaji wa uterasi. Matibabu yanacheleweshwa zaidi kwa sababu ya umbali wa kituo cha afya au ukosefu wa vifaa na wahudumu mwanamke anapofika kwa utunzaji wa dharura.

Kumbuka mambo haya yote ili kuhakikisha kuwa mwanamke huyu amepewa rufaa ya kwenda katika kituo mwafaka haraka kwa utatuzi na utunzaji wa dharura.

Muhtasari wa Kipindi cha 10

Katika Kipindi cha 10, ulisoma yafuatayo:

 1. Barani Afrika, urarukaji wa uterasi mara nyingi hutokana na kupuuzwa kwa leba iliyozuilika. Kwa utatuzi wa mapema na utunzaji ufaao, urarukaji wa uterasi unaweza kuzuiliwa.
 2. Visa zaidi vya urarukaji wa uterasi hutokea kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja kuliko wale wanaozaa kwa mara ya kwanza. Sababu moja ni kuwa, kwa wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, inesha ya uterasi hutokea. Inesha ya uterasi hupunguza nguvu na marudio ya minyweo isababishayo kuraruka kwa uterasi.
 3. Inesha ya uterasi kwa wanawake wanaozaa mara ya kwanza ina hatari zingine: Kichwa cha fetasi hukawia kwenye pelvisi kwa muda mrefu. Hatari ya hipoksia ya fetasi, kuanza kwa fistula, mkojo kubakizwa na maambukizi kwenye kibofu kiko juu sana.
 4. Kisababishi kikuu cha urarukaji wa uterasi ni leba iliyozuilika. Leba iliyozuilika husababishwa na kutolingana kwa sefalopelvisi, mlalo mbaya au fetasi kutokuwa katika nafasi yake ya kawaida, ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja, tyuma kwenye uterasi, au kovu. Mambo mengine yaongezayo hatari ya urarukaji wa uterasi ni fistula iliyokarabatiwa hapo awali, utumizi mbaya wa dawa za toni ya uterasi na usingaji wa fumbatio na wakunga wa kiasili katika leba.
 5. Ishara za kitabibu za uterasi inayoelekea kuraruka ni minyweo ya uterasi inayoendelea kutokea na inayodumu kwa muda wa sekunde 60-90 au zaidi, minyweo inayotokea zaidi ya mara 5 kwa kila dakika 10, na mpigo duni wa moyo wa fetasi. (Mpigo wa moyo wa fetasi unaoendelea kuwa juu ya mipigo 160 kwa dakika au chini ya mipigo 120 kwa dakika.) Dalili zingine ni kutokea kwa kizingo cha Bandl, maumivu kwenye fumbatio ukitomasa na pengine kutokwa na damu ukeni.
 6. Kukoma kabisa kwa minyweo ndiyo ishara muhimu zaidi ya kuwa uterasi imeraruka.
 7. Ishara zingine za uterasi iliyoraruka zinaweza kuwa maumivu kwenye fumbatio ukitomasa, sehemu za fetasi zinazotomasika kwa urahisi, kuvimba kwa fumbatio, kutosonga kwa fetasi na kutokuwepo kwa mpigo wa moyo wa fetasi.
 8. Hali ya kiafya ya mwanamke mwenye uterasi iliyoraruka hutegemea kiasi cha damu iliyopotea, muda tangu iliporaruka na kuwepo kwa maambukizi yaliyokithiri.
 9. Matatizo yatokeayo sana ya urarukaji wa uterasi ni kifo cha fetasi, na cha mama, maambukizi na mshtuko utokanao na upotezaji wa damu na/au sepsisi, peritonitisi, figo kutofanya kazi na upasuaji wa kutoa uterasi.
 10. Baadhi ya sababu za kufariki kwa wanawake wengi waafrika kutokana na urarukaji wa uterasi ni: kusita kutafuta usaidizi maalum wakati wa kuzaa na kisha kuchelewa kutafuta usaidizi wa kimatibabu baada ya uterasi kuraruka; kuchelewa zaidi katika kupata matibabu kwa sababu ya urefu wa safari ya kufikia kituo cha afya; au ukosefu wa vifaa na wahudumu waliohitimu mwanamke huyu anapofika kwa utunzaji wa dharura.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 10

Kwa kuwa umekamilisha kipindi hiki, jibu maswali haya ili kutathmini ulivyosoma. Unaweza kulinganisha majibu yako na Muhtasari juu ya Maswali ya Kujithmini mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la kujitathmini 10.1 (linatathmini Malengo ya Somo la 10.1 na 10.2)

Ni mambo yapi yanayoweza kumfanya mwanamke apate urarukaji wa uterasi?

Answer

Mambo haya yanaongeza hatari ya kuraruka kwa uterasi: (Maneno muhimu yako kwenye herufi nzito.)

 • Leba iliyozuilika kutokana na: kichwa cha fetasi kuwa kikubwa zaidi au pelvisi ya mama kuwa ndogo zaidi (kutolingana kwa sefalopelvisi); mtoto kutoweza kuteremka kwenye njia ya uzazi; mlalo mbaya na fetasi kutokuwa katika nafasi yake; au ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja (Kipindi cha 8).
 • Vizuizi vingine vya kimaumbile kama vile tyuma au kovu kutokana na uzazi wa hapo awali. (Kwa mfano, fistula, ambao ni mkato kati ya uke na kibofu, rektamu, urethra au ureta.)
 • Mazoea ya kiasili kama vile msingo usiofaa wa fumbatio au kusukuma chini kwenye fandasi katika leba.
 • Utumiaji mbaya wa dawa ya toni ya uterasi. (Dawa hii hutumiwa kusababisha minyweo.)

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 10.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 10.1 na 10.2)

Kwa nini wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wako katika hatari kubwa ya urarukaji wa uterasi kuliko wale wanaozaa mtoto wa kwanza?

Answer

Wanawake wanaozaa mtoto wa kwanza wanazaa kwa mara ya kwanza. Katika uzazi wa kwanza, kuna uwezekano wa leba kuwa ndefu. Hata hivyo, kwa wanawake hawa, inesha yauterasi hutokea baada ya takribani saa 36. Minyweo huwa dhaifu na mifupi, na yenye muda mrefu baina yake. Inesha ya uterasi hupunguza hatari ya urarukaji wa uterasi kwa kiwango kikubwa .

Kwa upande mwingine, wanawake waliozaa zaidi ya mara moja wamepata angalau mtoto mmoja baada ya majuma 28 ya ujauzito. Uterasi ya wanawake hawa hunywea mno kwa muda mrefu zaidi kuliko uterasi ya wale wanaozaa kwa mara ya kwanza. Ikiwa uzuio utazuia kuzaa kwa muda mrefu, hasa ikiwa kuna kovu kutokana na matatizo ya uzazi wa hapo awali, kuna uwezekano mkubwa wa uterasi kuraruka.

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini 10.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 10.3)

Kamilisha Jedwali 10.1. Ongeza maelezo ya dalili za hatari za urarukaji wa uterasi unaoweza kutokea.

Jedwali 10.1 Dalili za hatari za uwezekano wa urarukaji wa uterasi.
Hatua Dalili za hatari
Pima muda wa vipindi vya leba
Pima minyweo ya uterasi
Chunguza kiwango cha mpigo wa moyo wa fetasi
Chunguza fumbatio
Chunguza uke
Answer

Jedwali 10.1 lililokamilishwa ndilo hili hapa.

Jedwali 10.1 Dalili za hatari ya uwezekano wa urarukaji wa uterasi (iliyokamilishwa
Hatua Dalili za hatari
Pima muda wa vipindi vya lebaLeba ndefu sana: kipindi cha kwanza cha awamu fiche kinadumu zaidi ya saa18; kipindi cha kwanza cha awamu ya leba dhahiri kinadumu zaidi ya saa 12; kipindi cha kinadumu zaidi ya saa 1 kwa wanawake waliozaa zaidi ya mara moja, au zaidi ya saa 2 kwa wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza
Pima minyweo ya uterasi Minyweo ya uterasi inayoendelea kutokea inayodumu kwa muda wa sekunde 60 - 90 au zaidi, inayotokea zaidi ya mara 5 kwa kila dakika 10
Chunguza kiwango cha mpigo wa moyo wa fetasiKiwango cha mpigo wa moyo wa fetasi kinaendelea kuwa zaidi ya mipigo 160 kwa dakika au chini ya mipigo 120 kwa dakika
Chunguza fumbatioSehemu ya chini ya uterasi ni nyororo ukitomasa; kizingo cha Bandl kipo
Chunguza ukeKunaweza kuwa na kutokwa na damu

Mwisho wa jibu

Swali la kujitathmini (linatathmini Malengo ya Somo la 10.3 na 10.4)

 • a.Ni matatizo gani yanayoweza kufuata urarukaji wa uterasi?
 • b.Ni hatua zipi unazopaswa kuchukua iwapo urarukaji wa uterasi utatokea?
Answer
 • a.Matatizo ya urarukaji wa uterasini:
  • Kifo cha fetasi ila upasuaji wa haraka ufanywe kuitoa.
  • Mama kutokwa na damu nyingi na kupatwa na mshtuko kutokana na upotezaji huu wa damu, ambayo husababisha kifo cha mama ila apate matibabu ya haraka. (Kutokwa na damu nyingi sana na mshtuko utokanao na upotezaji huu wa damu hutambulika kwa upotezaji wa fahamu, ngozi kukwajuka, mpwito wa haraka wa ateri, shinikizo la damu linalopungua, upumuaji wa haraka, kuanza kupoteza fahamu na utoaji wa kiasi kidogo cha mkojo.)
  • Maambukizi: peritonitisi (maambukizi ya kaviti ya fumbatio) na/au septisemia (maambukizi ya damu yatokanayo na bakteria), ambayo husababisha uwezekano wa mshuto wa sepsisi unaoweza kusababisha kifo.
  • Figo kukosa kufanya kazi (kwa sababu ya kupoteza kiasi cha damu).
  • Histeroktomi.
 • b.Hatua muhimu zaidi ni kumpeleka mwanamke huyo katika kituo cha afya kilicho karibu kinachoweza kutibu uterasi iliyoraruka haraka iwezekanavyo. Hakikisha anapata joto na ametulia. Anafaa kulala miguu yake ikiwa juu kidogo kuliko kichwa chake na kichwa chake kikiwa kimekunjwa kuelekea upande mmoja. Mpe viowevu mshipani. Ikiwa hana fahamu, usimpe chochote mdomoni.

Mwisho wa jibu