Skip to main content
Printable page generated Sunday, 28 Nov 2021, 12:43
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Printable page generated Sunday, 28 Nov 2021, 12:43

11. Kuvuja Damu baada ya Kuzaa

Kipindi cha 11 Kuvuja Damu baada ya Kuzaa

Utangulizi

Takriban wanawake 127,000 kote duniani hufa kila mwaka kutokana na kuvuja damu baada ya leba na kuzaa. Hali hii hujulikana kama kuvuja damu baada ya kuzaa. Hali hii ni kisababishi kikuu cha vifo vya kina mama vinavyohusiana na kuzaa, nayo husababisha robo ya vifo vyote vya kina mama vinavyohusiana na kuzaa. Kila mwaka, visa milioni 14 vya kuvuja damu hutokea wakati wa ujauzito na kuzaa. Hali hii hutokea mara nyingi kwa sababu uterasi haikujikaza vyema baada ya plasenta kutoka. Katika Kipindi cha 6, ulijifunza kuhusu jinsi ya kudhibiti awamu ya tatu ya leba. Awamu ya tatu ya leba huanza kwa kuzaliwa kwa mtoto na kukamilisha kutoa kwa plasenta na membreni za fetasi.

Katika kipindi hiki, utajifunza kuhusu kuvuja damu baada ya kuzaa na jinsi ya kuidhibiti hali hii. Kuvuja damu baada ya kuzaa ni hali hatari zaidi inayohitaji matibabu ya dharura. Hatua zako za haraka zinaweza kuokoa maisha ya watu wengi. Usisahau kuwa kuvuja damu baada ya kuzaa (kuvuja damu kupita kiasi kabla ya leba kuanza) kunaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Ulijifunza kuhusu kuvuja damu nyakati za mwanzo na za mwisho wa ujauzito katika Kipindi cha 20 na 21 cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujazito.

 • Je, unaweza kukumbuka vipengele viwili ambavyo mara nyingi husababisha kuvuja damu katika kipindi cha mwisho wa ujauzito?

 • Vipengele viwili ambavyo mara nyingi husababisha kuvuja damu katika kipindi cha mwisho wa ujauzito ni privia ya plasenta na kutengeka kwa plasenta. Privia ya plasenta hutokea wakati plasenta imekaribia seviksi au kuifunika. Plasenta hujitenga seviksi inapoanza kupanuka wakati leba inapoanza. Kutengeka kwa plasenta hutokea plasenta inapokuwa katika pahali pake pa kawaida katika thuluthi mbili za juu ya uterasi, lakini imetengeka kabla ya mtoto kuzaliwa.

  Mwisho wa jibu

Malengo ya Somo la Kipindi cha 11

Baada ya kipindi hiki, unatarajiwa:

11.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 11.1)

11.2 Kueleza visababishi na vipengele hatari vya hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na jeraha na uterasi kutojikaza vyema. (Swali la Kujitathmini 11.2)

11.3 Kueleza hatua zinazoweza kusaidia kuzuia kuvuja damu baada ya kuzaa. Jumuisha hatua utakazochukua wakati wa ujauzito na awamu ya pili na tatu ya leba. (Swali la Kujitathmini 11.3)

11.4 Kufafanua jinsi ya kudhibiti hali ya dharura katika wanawake wanaovuja damu baada ya kuzaa. (Swali la Kujitathmini 11.3)

11.1 Kuvuja damu baada ya kuzaa ni nini?

Kuvuja damu baada ya kuzaa ni hali ya kuvuja damu kupita kiasi kutoka kwenye njia ya mfumo wa uzazi wakati wowote baada ya kuzaa hadi wiki sita baadaye. Takriban asilimia 70-90 ya matukio ya hali hii hutokea wakati wowote katika saa 24 za kwanza baada ya kuzaa. Matukio haya hutokea kwa sababu uterasi haikujikaza vyema baada ya plasenta kutengeka. Mikazo dhabiti ni muhimu ili kuziba mishipa ya damu kwenye shina la plasenta.

Vipengele hatari ni hali zilizopo zinazofanya hali hii kuwa, na uwezekano wa juu wa kutokea au kuwa na hatari zaidi kwa hali hii.

Kuvuja damu baada ya kuzaa ni hali isiyotabirika na ya kasi inayosababisha vifo vya kina mama. Hali hii haitabiriki kwa sababu thuluti mbili ya wanawake waliokabiliwa na tatizo hili hawana vipengele vya hatari vinavyojulikana. (Kiwango hatari cha hali hii hujulikana na madaktari kama hali idiopathiki ikiwa kisababishi chake hakijulikani.) Katika matukio mengine, wanawake wanaovuja damu baada ya kuzaa huwa na mojawapo au zaidi ya vipengele vya hatari vinavyojulikana. Au damu huvuja kwa sababu mhudumu wa kiafya ameidhibiti vibaya awamu ya tatu ya leba. (Tutavidurusu vipengele vya hatari baadaye katika kipindi hiki.)

11.1.1 Ni kiwango gani cha kuvuja damu kilicho cha “kupita kiasi”?

Ulijifunza jinsi ya kupima shinikizo la damu na mrindimo katika Kipindi cha 9 cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujawazito. Tulijifunza kuhusu visababishi na jinsi ya kudhibiti mshtuko unaohusiana na kuvuja damu katika Kipindi cha 20–22 cha Moduli hiyo.

Kwa kawaida, mama hupoteza kiwango kidogo cha damu wakati wa kuzaa. Mama kwa kawaida hupoteza takriban mililita 150 (kikombe 1), za damu wakati wa kuzaa na baada ya plasenta kutolewa. Ikiwa kiwango hiki kitazidi mililita 300 (vikombe 2), hali hii inaaminiwa kuwa kuvuja damu kupita kiasi (Mchoro 11.1) Kuvuja damu kupita kiasi hufasiliwa kama kuvuja damu zaidi ya mililita 500. Hata hivyo, kwa wanawake wenye anemia kali, kuvuja damu ya hata mililita 200–250 kunaweza kusababisha kifo. Kwa sababu hiyo, ufasili bora zaidi wa kuvuja damu baada ya kuzaa ni " kiwango chochote cha kuvuja kinachosababisha hali ya mwanamke kudhoofika na kusababisha dalili za mshtuko unaohusiana na kuvuja damu." (Dalili hizi ni shinikizo la chini la damu, mrindimo wa kasi, kuparara, unyonge, au utatanishi.)

Mchoro 11.1 Kuvuja damu kwa wingi ni zaidi ya mililita 300; Kuvuja damu kupita kiasi ni zaidi ya mililita 500.

11.1.2 Uainishaji wa kuvuja damu baada ya kuzaa

Kuvuja damu huainishwa kulingana na wakati wa kuvuja damu baada ya mtoto kuzaliwa, na kisababishi cha kuvuja kwenyewe.

Uainishaji kulingana na wakati wa kuvuja damu:

 • Kuvuja damu kwa baada ya kuzaa kwa kiwango cha kimsingi ni hali ya kuvuja damu kupita kiasi inayotokea katika awamu ya tatu ya leba au katika saa 24 baada ya kuzaa.
 • Kuvuja damu kwa baada ya kuzaa kwa kiwango cha upili (pia huitwa kuvuja damu kwa baada ya mtoto kuzaliwa) hujumuisha kuvuja damu kupita kiasi kwa kati ya saa 24 baada ya mtoto kuzaliwa na wiki 6 baadaye.

Uainishaji kulingana na kisababishi cha kuvuja hujulikana kama hali inayohusiana na mikazo au inayohusiana na jeraha. Tutajadili kuhusu kila aina na jinsi ya kuidhibiti katika somo linalofuata.

11.2 Kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo

Neno "kutojikaza" linamaanisha "ukosefu wa mikazo ya kimisuli au uwezo wa kujikaza". Kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo hutambulika kwa kuvuja damu kupita kiasi kufuatia uterasi kukosa kujikaza vyema baada ya kuzaa, na kuwa laini, legevu na iliyokosa mikazo ya misuli.

Kwa ufasaha zaidi, katika hali ya kuvuja damu inayohusiana na mikazo, miometriamu haiwezi kujikaza na kuifinya mishipa ya damu ya mama iliyoraruka baada ya plasenta kutengana na pembezo za uterasi. (Miometriamu ni pembezo ya uterasi iliyoundwa kwa misuli.) Mara nyingi kuvuja damu baada ya kuzaa hutokea kwenye sehemu ambapo plasenta ilikuwa imejibandika hapo awali. Ikiwa miometriamu haitajikaza kwa nguvu, haitaweza kuifinya mishipa ya damu ili kudhibiti kuvuja damu.

11.2.1 Visababishi vya kuvuja damu kunakohusiana na mikazo

Hali yoyote inayotatiza mikazo ya uterasi huongeza hatari ya kuvuja damu kupita kiasi. (Hali hizi ni plasenta iliyosalia, mabaki ya tishu za plasenta, au kusalia kwa tando za amanioni au kuganda kwa damu ndani ya uterasi.) Ikiwa plasenta imejitenga lakini ingali imebakia uterasini, hata kama ni kipande kidogo, uterasi haiwezi kujikaza. Hata kipande kidogo cha plasenta au donge la damu lililosalia ndani ya uterasi linaweza kufanya uterasi kutojikaza. Uterasi isipojikaza, mishipa ya damu ya mama itaendelea kuvuja. Mwanamke atapoteza damu haraka.

Tatizo kuu la kuvuja damu baada ya kuzaa ni kuwa huwezi kubashiri ni nani atakayevuja damu kupita kiasi baada ya kuzaa. Hali hii ngumu husababishwa na ukweli kwamba thuluti mbili ya wanawake waliokabiliwa na tatizo hili hawana vipengele vya hatari vinavyojulikana. Hivyo basi, ni sharti ukumbuke kuwa wanawake wote wamo katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili. Kukinga kuvuja damu baada ya kuzaa ni sehemu ya lazima katika kila tukio la kuzaa. Ufuatao ndio muhtasari wa vipengele vikuu vya hatari vinavyojulikana.

Kutatizwa kwa uwezo wa uterasi kujikaza

Mhudumu hawezi kubashiri wala kuzuia uterasi isiyoweza kujikaza. Hata hivyo, ukifahamu vipengele vinavyopelekea uwezekano wa kuvuja damu, unaweza kujitayarishia dalili hizi zinazoweza kutokea za hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na mikazo:

 • Kizuia privia ya plasenta au kutengeka mapema kwa plasenta: Katika hali zote mbili, nyuzi za misuli ya miometriamu huwa zimejeruhiwa katika sehemu ya plasenta.
 • Plasenta iliyosalia: Plasenta yote au kipande chake husalia ndani ya uterasi. Plasenta iliyosalia uterasini hutatiza mikazo ya kawaida ya misuli katika sehemu ya plasenta.
 • Kutengeka nusu kwa plasenta: Sehemu ya plasenta hutengeka kutoka katika pembezo za uterasi huku sehemu nyingine ikisalia imebandikika humo.
 • Kibofu kilichojaa: Uterasi imekaribiana na kibofu. Kibofu kikijaa kinaweza kutatiza mikazo ya kawaida ya uterasi katika wakati wote wa leba na baada ya kuzaa.
 • Usawa wa ujauzito: Mwanamke aliyewahi kupata mimba zaidi ya mara tano. Misuli ya miometriamu inaweza kukosa uwezo wa kujikaza kwa udhabiti kwa sababu imejikaza mara nyingi.
 • Mimba nyingi:Ni sharti uterasi ipanuke ili kutoa nafasi ya watoto wawili au zaidi (Kipindi cha 10). Baada ya kuzaa, uterasi iliyopanuka sana inaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kujikaza kabisa.
 • Polihidramniosi: Kiowevu kingi cha amanioni (zaidi ya lita 3) kinachomzingira mtoto kinaweza kupanua uterasi kupita kiasi kama vile katika mimba nyingi.
 • Mtoto mkubwa: Mtoto mwenye uzito zaidi ya kilogramu 4.0 anaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
 • Leba iliyodumu kwa muda mrefu: Leba inapochukua zaidi ya saa 12 (Kipindi cha 9), misuli ya miometriamu inaweza kuchoka. Muda mrefu wa mikazo hufanya misuli kukosa kujikaza vyema (utepetevu wa uterasi).
Anemia katika mama

Anemia ni ukosefu wa seli nyekundu za damu kufuatia kiwango cha chini cha hemoglobini. Anemia humweka mama katika hatari ya kupata hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa, kwa kuwa damu yake haiwezi kuganda haraka kama vile katika mtu asiye na anemia. Kupoteza damu ni hatari mno kwa mtu mwenye anemia. (Ulijifunza jinsi ya kutambua na kudhibiti anemia wakati wa ujauzito katika kipindi cha Somo cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito.)

Udhibiti duni wa awamu ya tatu ya Leba

Kipindi cha 6 kinaeleza jinsi ya kudhibiti kikamilifu utaratibu wa kutoa plasenta na mambo yanayofaa kuepukwa.

 • Je, mbinu sahihi ya kuhusika kikamilifu katika kusaidia kutoa plasenta imepewa jina gani?

 • Mbinu hii huitwa kuvuta kambakitovu taratibu.

  Mwisho wa jibu

 • Je, ni hatua gani isiyo sahihi ambayo mkunga anapaswa kuepuka katika awamu ya tatu ya leba inayoweza kusababisha kuvuja damu baada ya kuzaa?

 • Usijaribu kutoa plasenta kabla haijatengana na pembezo za uterasi. Usiisukume fandasi ya uterasi unapovuta kambakitovu. Unapaswa kungojea mkazo kabla ya kuvuta kambakitovu taratibu. Unapaswa kuweka shinikizo pinzani kwenye fumbatio ya mama. (Soma Kipindi cha 6 tena ikiwa una tashwishi kuhusu jinsi ya kutekeleza mbinu ya kuvuta kambakitovu taratibu.)

  Mwisho wa jibu

11.3 Kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na jeraha

Katika kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na jeraha, kuvuja damu kupita kiasi hutokea kufuatia jeraha kwenye njia ya uzazi baada ya mtoto kuzaliwa. Jeraha linaweza kutokea kwenye seviksi, uke, periniamu, au kinyeo. Jeraha pia linaweza kuwa kupasuka kwa uterasi (Kipindi cha 10). Dalili za hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na jeraha ni damu inayovujia ukeni lakini uterasi imejikaza vyema (ni ngumu).

Jeraha kwenye mfumo wa uzazi linaweza kuzuilika. Ujuzi na udhibiti taratibu uhitajika wakati wa kuzalisha. Ikiwa leba imedumu kwa muda mrefu au fetasi imetanguliza vibaya au iko katika hali mbovu, pendekeza rufaa haraka iwezekanavyo (Kipindi cha 8).

11.4 Punguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa

Katika kitengo hiki, tutazingatia hatua za kuchukua katika kila hatua ili kupunguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Anza kumhudumia mwanamke mjamzito kabla ya leba kuanza.

11.4.1 Hatua za dharura katika utunzaji wa waakati wa ujauzito

Wapangie wanawake walio na vipengele hatari vinavyojulikana (kama ilivyoelezwa katika hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na mikazo ya uterasi) wazalie kituoni cha afya. Humo kituoni, hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa inaweza kudhibitiwa kwa urahisi. Ikiwa kuvuja kutatokea, hatua ya dharura inaweza kuchukuliwa. Katika matukio ya privia ya plasenta, hali mbovu ya fetasi, au mapacha, upasuaji unaweza kuhitajika. Baadhi ya wanawake wanaweza kuwa hawataki kwenda kwenye kituo cha afya. Hata hivyo, unapaswa kuwafafanulia kwa ufasaha na kwa umakinifu kina mama walio hatarini zaidi kwa nini kuzalia nyumbani si salama. Ikiwa watakataa, hakikisha kuwa mpango ya rufaa uko tayari. Hakikisha kuwa umewatayarisha watu wa kumtolea mwanamke damu ikiwa ataihitaji.

Hatari kubwa ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na anemia ni mojawapo ya sababu ya umuhimu wa kuchunguza anemia kila unapotoa huduma ya wajawazito (na baada ya kuzaa). Chukua hatua kuzuia anemia.

 • Utafanya nini ili kuzuia anemia katika wanawake wajawazito unaowahudumia?

 • Washauri kuhusu lishe bora. Zingatia kuhusu chakula kinachopatikana chenye wingi wa madini ya chuma na foleti (kama vile mboga mbichi, nafaka nzima, nyama nyekundu, na mayai). Wape virutubishi mbadala ya chuma/foleti.

  Ulijifunza kuhusu mambo haya katika Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito kama kitengo cha utunzaji maalum wa kabla ya kuzaa (Kipindi cha 13), lishe katika ujauzito (Kipindi cha 14), na ukingaji na matibabu ya anemia (Kipindi cha 18).

  Mwisho wa jibu

 • Utachukua hatua gani ili kuzuia anaemia inayosababiswa na malaria na mnyoo?

 • Wahimize wanawake kutumia neti iliyotiwa dawa ili wajikinge dhidi ya mbu wanaoambukiza viini vya malaria. Wape wananwake dawa (mebendazole) baada ya kipindi cha kwanza cha ujauzito iwapo wanaishi katika maeneo yenye mnyoo.

  Mnyoo na ugonjwa wa malaria umeelezwa kwa kina katika Moduli ya Magonjwa ya Kuambukiza.

  Mwisho wa jibu

11.4.2 Hatua za dharura katika awamu ya pili ya leba

 • Tumia pathograpu kufuatilia na kudhibiti leba na kuzuia leba kuchukua muda mrefu (Kipindi cha 4).
 • Mhimize mwanamke ahakikishe kuwa kibofu chake ni kitupu.
 • Usimkubalie mama kusukuma mtoto kabla ya seviksi kupanuka vyema.
 • Usifinye juu ya uterasi (shinikizo la fandasi) ili kusaidia kuzaliwa kwa mtoto.
 • Msaidie mwanamke kuzaa kwa kudhibiti kichwa na mabega ya mtoto ili kuzuia majeraha (Kipindi cha 3). Weka vidole vya mkono wako mmoja kwenye kichwa cha mtoto ili kukilegeza. Tumia mkono wako mwingine kushikilia periniamu. Mfunze wanawake mbinu za kupumua ili kusukuma au kukoma kusukuma.

11.4.3 Hatua za dharura katika na baada ya awamu ya tatu ya leba

Kwa wanawake wasio na hatari zinazojulikana, unaweza kupunguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Ili kufanya hivyo, dhibiti awamu ya tatu ya leba kwa umakinifu (Kipindi cha 6). Kwa muhtasari, kumbuka vidokezo hivi vikuu:

 • Baada ya mtoto kuzaliwa, hakikisha hakuna mtoto mwingine uterasini. Mpe mama dawa ya misoprostol mikrogramu 600 ya kumeza au 10 (vipimo vya kimataifa) vya oxytocin kwa kuidungia ndani ya misuli. Dawa hizi huisaidia uterasi kujikaza.
 • Usisukume fandasi ili kusaidia kutolewa kwa plasenta.
 • Isugue uterasi punde tu baada ya plasenta kutolewa. Ili kuhakikisha kuwa uterasi imejikaza vyema, isugue kwa angalau kila dakika 15 kwa saa 2 za kwanza baada ya kuzaa. Mfunze mama kupapasa na kuchunguza uterasi yake ili kuiweka dhabiti. Mwambie atafute usaidizi ikiwa uterasi yake ni laini au ikiwa kiwango cha kuvuja damu kitazidi (Mchoro 11.2).
Mchoro 11.2 Isugue uterasi ili kuchochea mikazo ya uterasi baada ya plasenta kutoka.
 • Chunguza kwa umakinifu ili kutambua kama kuna michibuko ya uke, periniamu au kinyeo.
 • Chunguza kwa umakinifu kama plasenta imetoka yote (Kipindi cha 6).
 • Msaidie mama kunyonyesha mtoto punde tu atakapozaliwa. Anza kunyonyesha hata kabla ya plasenta kutoka (Mchoro 11.3). Mtoto akinyonya, mwili wa mama hutolesha oksitosini. Oksitosini huchochea uterasi kujikaza na vichirizi vya maziwa kujikaza ili kutiririsha maziwa kinywani mwa mtoto. Kunyonyesha husaidia kutolewa kwa plasenta na kupunguza kuvuja damu baada ya kuzaa.
Mchoro 11.3 Anza kunyonyesha punde tu mtoto atakapozaliwa ili kupunguza kuvuja damu baada ya kuzaa.
 • Mhimize mwanamke ahakikishe kuwa kibofu chake ni kitupu baada ya kuzaa. Uterasi inaweza kuwa laini kwa sababu kibofu cha mama kimejaa. Mama akikosa kukojoa, chururiza maji vuguvugu juu ya fumbatio lake. Hatua hii isipofaulu, anaweza kuhitaji kuingizwa katheta (neli ya plastiki) kibofuni mwake ili kumsaidia kukojoa.

Ulijifunza kuhusu jinsi ya kutumia katheta katika Kipindi cha 22 cha Moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito, na katika mafunzo yako ya kiutendaji.

 • Kwa haraka, orodhesha hatua za dharura unazoweza kuchukua kabla, wakati wa na baada ya leba ili kupunguza hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa.

 • Ili kudhibitisha jinsi ulivyojibu, soma tena Vifungu vya 11.4.1, 11.4.2 na 11.4.3.

  Mwisho wa jibu

Hata hivyo, kumbuka kuwa hata ukichukua hatua za dharura zozote zile, kuvuja damu baada ya kuzaa kunaweza kutokea baada ya kuzaa kokote kule. Kila wakati unafaa kuwa tayari kuchukua hatua ya dharura.

11.5 Udhibiti wa dharura wa kuvuja damu baada ya kuzaa

Iwapo mama ataanza kuvuja damu kupita kiasi baada ya kuzaa, chukua hatua ya haraka na umsafirishe hadi katika kituo chochote cha afya kilicho karibu. Kuvuja damu baada ya kuzaa kunaweza kusababisha kifo. Wahudumu wengi wa afya hupuuza kiwango cha damu anachopoteza mwanamke. Ukikumbana na tatizo hili, kwanza paza sauti ukiomba usaidizi. Paza sauti uwaite familia au majirani wakusaidie kumpeleka katika kituo kilicho karibu cha afya (Mchoro 11.4).

Mchoro 11.4 Usikawie kumpa rufaa mwanamke aliyevuja damu nyingi baada ya kuzaa.

11.5.1 Dawa za kukazisha uterasi na viowevu vya mishipa ya vena katika kudhibiti kuvuja damu kwa baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo

Kuna uwezekano kwamba utasubiri usafirishaji wa dharura. Ikiwa mama anavuja damu nyingi sana, mpe kipimo kingine cha dawa za kukazisha uterasi. Mpe kipimo kingine cha oxytocin 10 UI kwa kumdunga sindano ndani ya misuli. La sivyo, mpe kipimo kingine cha mikrogramu 400 za misoprostol kupitia rektamu au uzitie tembe hizi chini ya ulimi wake ambapo zitaweza kuyeyuka polepole. (Ili kumpa dawa kupitia rektamu, sukuma tembe hizi taratibu ndani ya rektamu kupitia kwenye kinyeo cha mwanamke huyu ) Ikiwa ulimpa oxytocin kwanza, usimpe misoprostol zaidi.

Usizidishe mikrogramu 1000 za misopropol! Ikiwa utampa mikrogramu 600 kupitia mdomo punde baada ya mtoto kuzaliwa, kipimo cha pili hakifai kuzidi mikrogramu 400 kupitia rektamu.

Ikiwa umefunzwa kufanya haya, anza kutilia viowevu vya mishipa ya vena kabla ya kumpeleka rufaa ili kuzuia na kutibu mshtuko. Tia asilimia 9 ya Chumvi ya Kawaida au mchanganyiko wa kiowevu cha lakteti cha Ringer, huku kikiwekwa katika mtiririko wa kiwango cha haraka iwezekanavyo. Hakikisha kuwa mfuko ulio na mchanganyiko wa kiowevu cha mishipa ya vena umeshikiliwa juu ya kichwa cha mwanamke muda wote. Mfuko huo unafaa kushikiliwa juu ya kichwa chake hata anaposafirishwa katika kituo kilicho karibu cha afya.

Ulisoma kuhusu kanuni za kutia kiowevu cha mishipa ya vena katika Kipindi cha 22 kwenye moduli ya Utunzaji wa Wakati wa Ujauzito na mafunzo yako ya kiustadi ya utendaji.

11.5.2 Tumia mbinu ya shinikizo la mikono miwili kwenye uterasi

Ikiwa damu inatoka kwa wingi na kusugua hakusimamishi kuvuja huku kwa damu, jaribu shinikizo la mikono miwili kwenye uterasi (Mchoro 11.5). Chota uterasi, ikunje upande wa mbele kisha uifinye kwa nguvu. (Ulionyeshwa jinsi ya kufanya hivyo katika masomo ya ustadi ya utendaji). Shikilia mkono mmoja juu ya uterasi. Weka mkono wako mwingine kwenye mfupa wa kinena na uisukume uterasi mbele kuelekea katika mkono wa kwanza. Ifinye uterasi katikati ya mikono yako.

Ikiwa umefunzwa kufanya hivi, unaweza kuifinya uterasi kwa mikono miwili kwa kufuata mbinu hii. Ingiza mkono wako mmoja ulio na glavu kwenye uke kisha ukaze mkono wako nyuma ya seviksi. Finyilia huo mkono mwingine kwenye fumbatio ili kuibana uterasi.

Mchoro 11.5 Shinikizo la mikono miwili juu ya uterasi linaweza kukomesha kuvuja damu baada ya kuzaa.

Punde tu damu itakapopungua kuvuja na unahisi kuwa uterasi iko dhabiti, sitisha shinikizo hili la mikono miwili taratibu. Ikiwa damu itaendelea kuvuja, mpe rufaa mwanamke huyu hadi katika kituo kilicho karibu cha afya. Jaribu kutumia shinikizo la mikono miwili juu ya uterasi wakati unamsafirisha mama huyu. Usimwache mtoto nyumbani. Hakikisha kuwa mtu mwingine amembeba mtoto. Hakikisha umeandamana na watu wanaoweza kumtolea mwanamke damu kutoka kwa jamaa yake. Mwanamke huyu anaweza kuhitaji kuongezwa damu.

11.5.3 Udhibiti wa dharura wa kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na jeraha

Mwanamke huyu anaweza kuwa na jeraha, kama vile mchibuko kwenye periniamu au uke. Ili kusitisha kuvuja kwa damu kutoka kwenye jeraha, weka shinikizo juu ya sehemu inapovujia damu. Kunja vipande 10 hadi 15 vya shashi iliyotakaswa au kitambaa kidogo kilichotakaswa katika pedi nene. Ifinyilie pedi hii kwa nguvu kwenye sehemu ya mchibuko inayovuja damu. Ishikilie pedi humo kwa dakika 10. Kwa umakinifu, iondoe shashi hii kisha udhibitishe kama damu ingali inavuja. Ikiwa mchibuko bado unavuja damu, ifinyilie shashi hii tena kwenye sehemu inayovujia kisha umpeleke mwanamke huyu katika kituo kilicho karibu cha afya. Endelea kuweka shinikizo juu ya mchibuko huu hadi utakapofika katika kituo cha afya. Ikiwa mwanamke huyu ana mchibuko mrefu au ulioingia dani sana, mpeleke katika kituo cha afya ambapo mchibuko huu unaweza kurekebishwa. Mpeleke hata ikiwa damu inavuja kwa kiwango cha chini kutoka kwenye mchibuko huu.

11.6 Orodha ya ithibati za rufaa ya dharura

Tunakaribia mwisho wa Moduli hii katika Leba na Utunzaji wakati wa Kuzaa. Jedwali 11.1 linatoa kwa muhtasari baadhi ya mambo muhimu ya kukumbuka wakati wa rufaa ya dharura wakati mwanamke anapovuja damu nyingi baada ya kuzaa. Habari hii inasaidia katika hali nyinginezo za dharura zinazotishia maisha kama zilivyoelezwa katika vipindi vya hapo awali. Katika moduli inayofuatia, uendeleshaji wa utunzaji huendelea hadi Utunzaji wa baada ya Kuzaa.

Jedwali 11.1 Mambo muhimu ya kufanya wakati wa kumsafirisha mwanamke hospitalini

Azimia kudumisha mambo haya:Hatua
Mkazo wa uterasiPapasa uterasi taratibu, au uisukume kwa mikono miwili na uendelee kuisukuma hivyo wakati wa rufaa.
Kibofu kitupuIkiwa mwanamke hawezi kukojoa, ingiza katheta inayojishikilia ili kutoa mkojo na uiache ndani ya kibofu wakati wa rufaa.
Kiasi kinachotosha cha damuIkiwa mwanamke anavuja damu au ana mshtuko, mpe viowevu vya mishipa ya vena na uendelee kupima viowevu hivi wakati wa rufaa.
Dalili muhimuChunguza rangi, mrindimo wa damu, shinikizo la damu, halijoto, kupoteza damu na kiwango cha kujifahamu.
JotoMfunike mwanamke huyu kwa blanketi.
NafasiMwanamke huyu anafaa kulala bapa, huku miguu yake ikiinuka juu ya kipeo cha kichwa chake ili kumsaidia kudumisha shinikizo lake la damu.
UjasiriMpe mwanamke huyu usaidizi wa kihisia na uhakikisho. Mtulize iwezekanavyo.
Nakala sahihi na maagizo ya rufaaOrodhesha matokeo yako yote na hatua za dharura ulizochukua katika maagizo ya rufaa. Jumuisha pia historia ya mwanamke huyu na habari za kina kuhusu utambulisho wake.
 • Ni vidokezo vipi viwili muhimu zaidi vya kukumbuka kuhusu kuvuja damu baada ya kuzaa?

 • Kumbuka vidokezo hivi viwili:

  • Ingawa vipengele vya hatari huhusishwa na kuvuja damu baada ya kuzaa, theluthi mbili ya wanawake wanaokumbwa na hali hii hawana vipengele vya hatari vinavyojulikana. Haiwezekani kutabiri ni wanawake wepi watakaokumbwa na hali hii ya kuvuja damu baada ya kuzaa.
  • Fahamu kuwa mwanamke yeyote yule anaweza kukumbwa na hali hii akiwa chini ya utunzajii wako anapozaa. Hali hii ni hatari kwa maisha, hivyo unafaa kujiandaa kuchukua hatua inayofaa ya dharura. Hatua hii ni pamoja na kumpa rufaa ya haraka hadi katika kituo cha afya.

  Mwisho wa jibu

Muhtasari wa Kipindi cha 11

Katika Kipindi cha 11, umesoma yafuatayo:

 1. Hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vinavyotokana na kuzaa katika nchi zinazostawi. Ni vigumu kutabiri ni wanawake wepi watakaokumbwa na hali hii, kwa hivyo unafaa kuwa tayari kuidhibiti kila unapozalisha.
 2. Visa vingi vya hali hii vinaweza kuzuiliwa kupitia utunzaji wa kiustadi wakati wa ujauzito, leba na kipindi kinachofuatia kuzaa.
 3. Wakati wa utunzaji wa kabla ya kuzaa, wanawake wote wajawazito wanafaa kupokea ushauri kuhusu lishe na kinga dhidi ya malaria. Wanawake wote wajawazito wanafaa kupokea matibabu dhidi ya mnyoo. Wanawake hawa pia wanafaa kupokea nyongeza ya virutubishi vya madini ya chuma/foleti ili kuzuia anemia, ambayo ni kipengele hatari cha kuvuja damu baada ya kuzaa.
 4. Mpe rufaa mapema ikiwa leba itakawia. Dhibiti jinsi kichwa kinavyotoka wakati wa kuzaa katika awamu ya pili ili kuzuia kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na majeraha.
 5. Baada ya mtoto kuzaliwa, mpe mama misoprostol au oxytocin ili kuzuia kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo, kisha upapase uterasi baada ya plasenta kutoka.
 6. Kuvuja damu baada ya kuzaa kukiendelea, tambua kisababishi cha kuvuja huku. Ikiwa kuvuja damu baada ya kuzaa kumesababishwa na uterasi isiyojikaza (iwe plasenta imesalia au la), ipapase uterasi ukitumia mikono miwili. Ondoa mkojo kutoka kibofuni (ikiwa inahitajika, tumia katheta) na uandae kiowevu cha vena. Mpe ama kipimo cha pili cha oxytocin 10 IU kwa kumdunga ndani ya misuli au kipimo cha pili cha misoprostol miligramu 400 kupitia rektamu au uzitie tembe hizi chini ya ulimi wake.
 7. Ikiwa hali hii inasababishwa na majeraha, tumia shinikizo dhabiti kwa dakika kumi kwenye sehemu inayovujia damu ukitumia pedi safi. Ikiwa damu itaendelea kuvuja, anzisha tena shinikizo na umpe rufaa hadi katika kituo cha afya ambapo jeraha hili linaweza kutibiwa.
 8. Kaa na mwanamke huyu katika kituo cha afya ambapo umempeleka rufaa. Chunguza dalili muhimu, dumisha shinikizo la uterasi na umpe joto na usaidizi wa kihisia.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 11

Kwa kuwa sasa umekamilisha kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili kubaini jinsi ulivyojifunza. Unaweza kudhibitisha majibu yako ukilinganisha na vidokezo ulivyoandika katika Maswali ya Kujitathmini yaliyo mwishoni mwa Moduli hii.

Swali la Kujitathmini 11.1(linatathmini Matokeo ya Somo la 11.1)

Unahitajika kuandika habari iliyoonyeshwa hapa ili kuituma pamoja na ilani ya rufaa kwa mama aliye na hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Mkurufunzi mwenzako mchanga amekuuliza umweleze ulichoandika. Eleza dondoo lako la rufaa ili mwenzako aweze kuelewa. Jumuisha maneno yote yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.

“Nataka kumpa rufaa Mebrihit. Yeye ni mama aliye na usawa wa kiwango cha juuna anatokwa nadamu kupita kiasi. Naamini kuwa ana hali ya kimsingi ya kuvuja damu baada ya kuzaa. Nilikuwa mwangalifu ili kumkinga dhidi ya jeraha nilipomsaidia kuzaa. Kumpapasa huashiria kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo, hali ambayo nakisia kuwa imesababishwa na matatizo ya miometriamu.

Answer

Unaweza kumwelezea mkurufunzi mwenzako dondoo lako la rufaa namna hii:

"Nataka kumpa rufaa Mebrihit. Yeye amekuwa na zaidi ya mimba 5 (usawa wa kiwango cha juu) na akatokwa na damu ya zaidi ya mililita 500 (kuvuja damu kupita kiasi) katika saa 24 za kujifungua (hali ya kimsingi ya kuvuja damu baada ya kuzaa ). Nilikuwa makini ili kumkinga na jeraha lolote (jeraha) wakati wa kuzaa. Ninapoliguza fumbatio lake (kupapasa), nilihisi kuwa uterasi yake ni laini na haijajikaza vyema baada ya kuzaa (kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo). Nashuku kuwa misuli ya pembezo za uterasi yake (miometriamu) haikazani vyema ili kuweza kuifunga mishipa ya damu katika sehemu ambapo plasenta ilitengana na uterasi.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini la 11.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 11.2 na 11.3)

Unamchunguza mwanamke mjamzito aliye chini ya utunzaji wako ili kubaini iwapo ana hatari ya kuvuja damu baada ya kuzaa.

 • a.Ni maswali gani utakayomuuliza na ni nini utayokumbuka kuchunguza kama sehemu ya ziara zako za utunzaji wa wakati wa ujauzito?
 • b.Ni uchunguzi na huduma zipi za dharura utakazomtolea wakati wa leba na kuzaa?
Answer

Uliza maswali haya na pia ufanye mambo haya. Unaweza kutaja mengine zaidi.

 • a.Utunzaji wa wakati wa ujauzito: Maswali ya kuuliza na mambo ya kubaini:
  • Je, amezaa kwa mara ya kwanza (primipara) au tayari amezaa mara mbili au zaidi (maltipara)? Kina mama maltipara wako katika hatari ya juu zaidi ya kupata hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa inayohusiana na mikazo.
  • Ikiwa mama ni maltipara, je, mtoto wake wa awali alikuwa mzito sana (zaidi ya kilogramu 4) au alipata mapacha? Mojawapo ya mambo haya yanaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
  • Je, mama huyu anakumbuka ikiwa alikuwa na kiowevu kingi zaidi cha amnioni katika ujauzito wake wa hapo awali (polihidrominiosi)? Zaidi ya lita 3 inaweza kupanua uterasi kupita kiasi.
  • Je, umefanya uchunguzi wa kutumia picha kubaini kama ana anemia? (Fanya uchunguzi wa kutumia picha kuchunguza anemia katika utunzaji wa baada ya kuzaa pia). Ikiwa ana anemia, umemshauri kuhusu lishe bora?
  • Je, mpango wa usafirishaji wa kijamii uko tayari iwapo rufaa ya dharura itahitajika?
 • b.Wakati wa, na baada ya kuzaa: Hatua za dharura za kuchukua na mambo ya kuchunguza:
  • Hakikisha kuwa anakojoa mara nyingi. (Kibofu kitupu hakitatizi mikazo ya kawaida ya uterasi) Pia anafaa kukojoa punde tu baada ya kuzaa.
  • Tumia patografu ili kufuatilia jinsi leba inavyoendelea. Patografu hii inakuwezesha kutambua kwa haraka dalili zozote zinazoweza kupelekea hali ya kuvuja damu baada ya kuzaa. (Kwa mfano, kizuizi kinaweza kusababisha kupasuka kwa uterasi).
  • Usimshauri mama huyu kusukuma mtoto nje kabla ya seviksi kupanuka hadi mwisho. Toa usaidizi wa kuvuta kichwa na mabega ya mtoto taratibu ili kuzuia majeraha.
  • Mshauri na umsaidie mama huyu kunyonyesha haraka iwezekenavyo. (Mama ataanza kujitolea oxytocin yake itakayochochea uterasi kujikaza.)
  • Hakikisha kuwa plasenta imetengana kabisa na kuwa ni nzima. Isugue uterasi kila dakika 15 katika saa 2 za kwanza ili kuwezesha uterasi kujikaza vizuri.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 11.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 11.4)

Gelila alizaa dakika 40 zilizopita. Ulimpa miligramu 600 za misoprostol kwa njia ya mdomo muda tu baada ya kuzaa lakini plasenta bado haijatoka. Amekojoa. Baada ya dakika 10 plasenta yake inatoka na unahakikisha kuwa ni nzima, lakini Gelila anaanza kuvuja damu kwa wingi. Utafanya nini?

Answer

Fanya mambo haya:

 • Paza sauti mara moja kuwaita familia na majirani wa Gelila. Washauri kuandaa usafirishaji iwapo ataendelea kuvuja damu kwa wingi na ni sharti aende katika kituo cha afya kilicho karibu.
 • Chunguza kiwango chake cha kuvuja damu. Hali hii isipopungua kwa haraka, chukulia kuwa ni kuvuja damu baada ya kuzaa kunakohusiana na mikazo.
 • Ikiwa alipata miligramu 600 ya misoprostol baada ya kuzaa, mpe kipimo cha pili cha miligramu 400 ya misoprostol kupitia rektamu au chini ya ulimi ili kuwezesha uterasi kujikaza. Ikiwa alipewa oxytocin hapo awali, mpe UI 10 nyingine kwa kumdunga sindano ndani ya misuli.
 • Mlaze Gelila chali huku miguu yake ikiwa katika kipeo cha juu ya kichwa, mfunike kwa blanketi na uhakikishe kuwa ana joto.
 • Ikiwa umefunzwa kufanya haya, mdunge sindano iliyo na viowevu vya vena kabla ya rufaa.
 • Isugue uterasi ili kuiwezesha kujikaza. Ikiwa hatua hii haifaulu, jaribu kufinya uterasi yake kwa kutumia mikono miwili. Ikiwa damu itakoma kuvuja na uterasi ianze kuwa dhabiti, ondoa shinikizo pole pole. Ikiwa damu haitakoma kuvuja, endelea na utaratibu wa kutoa rufaa na umfikishe mama huyu katika kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
 • Andamana na Gelila hadi katika kituo hicho cha afya. Chunguza dalili zake kuu na uendelee kumtilia viowevu ndani ya mshipa. Hakikisha kuwa mtoto wake pia analetwa hospitalini na kuna watu wanaofaa wa kumtunza na kumtolea damu.
 • Nakili kila hatua uliyochukua katika dondoo zako za rufaa. Jumuisha pia historia ya Gelila na habari za kina kuhusu utambulisho wake.

Mwisho wa jibu