Skip to main content
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 2:38 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Thursday, 28 March 2024, 2:38 PM

6. Uchunguzi wa Kidesturi wa Watoto Wachanga ili Kubaini Hali Hatari

Kipindi cha 6 Uchunguzi wa Kidesturi wa Watoto Wachanga ili Kubaini Hali Hatari

Utangulizi

Katika Kipindi hiki, tutarejelea dalili hatari za kijumla zinazoonyesha kuwa mtoto mchanga yuko hatarini, kama zilivyoorodheshwa kwa kifupi katika Kipindi cha 1. Sasa tutalenga kwa kina zaidi uchunguzi na uainishaji wa hali hizi hatari. Pia tutazungumzia hatua unazohitaji kuchukua ili kuzuia na kutibu matatizo ya mtoto mchanga yanayotokea mara nyingi. Tutalenga maambukizi ya mfumo wa pumzi, macho na kitovu, na pia dalili hatari kama vile umanjano na pepopunda. Kumhusisha mama katika utaratibu huu ni sehemu muhimu ya utunzaji wa baada ya kuzaa. Mama anaweza kuokoa maisha ya mtoto wake kwa kutia juhudi na kuwa tayari kutafuta msaada wako anapotilia shaka hali ya mtoto.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 6

Baada ya masomo ya Kipindi hiki, unatarajiwa:

6.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 6.1, 6.2 na 6.3)

6.2 Kutaja maswali muhimu unayohitaji kumuuliza mama ili kubaini hali ya mtoto wake mchanga.

6.3 Kutambua dalili hatari za kijumla za mtoto mchanga kisha kueleza hatua zinazohitaji kuchukuliwa. (Swali la Kujitathmini 6.2)

6.4 Kueleza jinsi ya kuzuia au kupunguza hatari ya mtoto mchanga kuambukizwa. (Swali la Kujitathmini 6.3)

6.1 Hatua za kwanza kabla ya kumchunguza mtoto mchanga

Kabla ya kuanza kumchunguza mtoto mchanga, vua virembesho kama vile pete, bangili au mapambo yoyote mengine, kisha unawe mikono vyema kwa maji safi na sabuni kwa angalau dakika 2. Kunawa mikono ni mojawapo ya hatua muhimu zaidi unayoweza kuchukua ili kuzuia maambukizi. Hakikisha kuwa unabeba sabuni na taulo yako mwenyewe katika kila ziara, na ufuate maagizo yaliopeanwa kwenye Mchoro 6.1.

Kisanduku 6.1 Jinsi ya kunawa mikono vyema kabla ya kufanya uchunguzi wa baada ya kuzaa.

Pia unafaa kumwonyesha mama jinsi ya kunawa mikono yake vyema, na umkumbushe kunawa mikono:

  • Kabla ya kunyonyesha
  • Kabla ya kumvisha au kumvua mtoto nguo.
  • Kabla ya kumsafisha au kumwosha mtoto.
  • Baada ya kumbadilisha mtoto nepi na kutupa kinyesi.
  • Baada ya mama kubadilisha padi zake mwenyewe zinazotumika kufyonzea mchozo wa damu kutoka ukeni.
  • Baada ya kutumia choo.
  • Kabla au baada ya kuandaa chakula.

Unapoendelea kunawa mikono, mwambie mama aanze kunyonyesha. (Katika Kipindi kijacho, tutakufunza kwa kina kuhusu utaratibu mwafaka wa kunyonyesha). Mama anaponyonyesha, utachukua fursa hiyo kubaini kama kuna matatizo yoyote yanayohusiana na kunyonyesha. Kunyonyesha pia humtuliza mtoto unapomchunguza. Iwapo mtoto atalia unapomchunguza, Malengo ya uchunguzi huo yanaweza kuathirika. Hivyo basi, jaribu kila mara kuwatuliza watoto unapowachunguza.

6.2 Kumkagua mtoto ili kubaini dalili hatari za kijumla

Katika ziara ya kwanza, jambo muhimu zaidi ni kuwachunguza watoto wote Wachanga ili kubaini uwepo wa dalili hatari za kijumla katika watoto Wachanga (Kisanduku 6.1). Dalili hizi tayari zimeorodheshwa kwa kifupi katika Kipindi cha 1. Kila wakati, kumbuka kuzingatia uangalifu, wepesi wa kutambua na utaratibu unapomchunguza na kumhudumia mtoto mchanga, hasa katika siku za kwanza za uhai wake. Pia, muda wote unapomhudumia mama na mtoto mchanga, unashauriwa kuwa makini ili kutambua uwezekano wa kuwepo kwa dalili kuu hatari.

Matatizo yanayohusiana na kula yamezungumziwa kwa kina katika Kipindi cha 7.

Kisanduku 6.1 Dalili hatari za kijumla kwa watoto Wachanga

  • Historia ya ugumu wa kula, au mtoto hawezi kula kwa sasa - muulize mama kuhusu jinsi mtoto anavyokula.
  • Historia ya mitukutiko, au mtoto anatukutika kwa sasa - muulize mama kama mtoto ameshawahi kupata mitukutiko ya maungo.
  • Mtoto mchanga anaonekana mlegevu au amepoteza fahamu.
  • Mtoto anasonga tu iwapo amesisimuliwa.
  • Kupumua kwa haraka.
  • Kifua kubonyea ndani sana.
  • Homa.
  • Hipothemia (ukimguza, unahisi kuwa mtoto ana baridi)
  • Mtoto amekuwa na rangi ya manjano kabla ya kufikisha umri wa saa 24. Umanjano unaoonekana kwenye viganja vya mikono na nyayo za miguu.
  • Macho yamefura au yanatoa mchozo.
  • Usaha unatoka kitovuni.
  • Zaidi ya pustuli (madoa) 10 zinaonekana ngozini.

6.2.1 Je, unaweza kutambua vipi kuwa mtoto mchanga ana mtukutiko?

Apnea ni dalili hatari sana. Iwapo unakisia kuwa mtoto amepata mtukutiko, au unatambua dalili za mtukutiko wakati wa ziara, mpe mama na mtoto rufaa ya dharura hadi katika kituo cha hali ya juu cha afya.

Katika mtoto mchanga, mtukutiko (mtukutiko wa maungo) unaweza kudhihirika kama:

  • Mtetemo wa kiungo cha mwili (kama vile mkono), sehemu ya mwili, au mwili wote (mtukutiko wa mwili wote).
  • Mtandaziko wa (spazimu ya) kiungo cha mwili (kama vile mkono) au mwili wote.
  • Miendo isiyo ya kawaida (kama vile ya mdomo, kugeuza macho upande mmoja au miendo ya miguu kana kwamba anaendesha baiskeli).
  • Apnea (vipindi virefu vya kukosa kupumua).

Mara nyingi ni vigumu kutambua mtukutiko katika watoto Wachanga kwa sababu mwili na viungo vyao havitandaziki kwa pamoja au mwili kushtuka kama ilivvyo kwa mitukutiko ya watoto wakubwa na watu wazima. Kwa hivyo, ni muhimu sana kuwa makini ili kutambua dalili zozote zisizo za kawaida, hata kama dalili hizi si wazi mwanzoni.

6.2.2 Je, mtoto mchanga amelegea au amepoteza fahamu?

Mtoto aliyepoteza ufahamu anafaa kupelekwa rufaa kwenye kituo cha afya mara moja.

Tazama miendo ya mtoto huyu mchanga. Je, mtoto anacheza kama inavyotarajiwa kwa mtoto mwenye afya bora au la? Je, mtoto anachezesha viungo anapochangamshwa tu (amelegea?) Iwapo mama amewahi kuzaa tena, au kina mama wengine wenye tajiriba wako mle nyumbani, waulize kama wanafikiri mtoto huyu amelegea. Iwapo mtoto hachezeshi viungo au hajibizi changamsho kama kawaida, basi yuko katika hatari.

6.2.3 Je, mtoto huyu anapumua kwa kasi sana?

Mpe rufaa mtoto anayeonekana kuwa na matatizo ya kupumua.

Hesabu idadi ya kadri mtoto anavyopumua kwa dakika moja. Je, anapumua kama kawaida au kwa kasi sana? Kupumua kwa kasi ni kupumua mara 60 au zaidi kwa dakika. Mtoto mchanga hupumua mara 40 - 60 kwa dakika. Kimo hiki hupimwa mara mbili kwa kipindi cha dakika moja kila wakati. Chunguza ili utambue kama mtoto ana kifua kinachobonyea sana. Hii inamaanisha kuwa mtoto anapovuta pumzi, sehemu ya chini mwa mbavu ‘hufyonzeka’ ndani sana (Mchoro 6.2).

Mchoro 6.2 Kubonyea kwa kifua ni dalili kuwa mtoto mchanga ana matatizo ya kupumua.

6.2.4 Je, jotomwili la mtoto ni la kawaida?

Pima kiwango cha jotomwili la mtoto, hasa ukitumia themometa iliyoingizwa taratibu kwenye rektamu kupitia kinyeoni, au utumie themometa ya kawaida iliyoshikiliwa taratibu kwapani mwa mtoto (hii hujulikana kama jotomwili la kwapani). Kumbuka kuwa themometa hii inafaa kuwa safi kabisa kabla ya kuitumia. Ioshe themometa kwa maji safi kabla na baada ya kuitumia, kisha uisugue kwa swabu iliyolowa alkoholi au kiowevu kingine cha kutakasa. Iwapo hauna themometa, tumia mkono wako kuguza kichwa na mwili wa mtoto kubaini kama ana homa au kiwango cha chini cha jotomwili. Hii ni kwa kulinganisha hali ya mtoto na yako au ngozi ya mama.

Mpe rufaa mtoto aliye na homa au hipothemia, iwapo kiwango chake cha jotomwili hakijarejea hali ya kawaida upesi.

Homa hufasiliwa kama kiwango cha jotomwili cha nyusi 37.5 au zaidi. Iwapo unakisia kuwa mtoto ana joto jingi kutokana na joto la mama, mpunguzie joto kwa kuondoa blanketi zake kisha upime kiwangojoto tena baada ya dakika 15. Iwapo kiwango cha jotomwili hakitarejea hadi kawaida kwa upesi, au kinazidi nyusi 37.5, mpeleke rufaa haraka. Kiwango cha juu cha jotomwili ni dalili hatari ya maambukizi, ambayo yanafaa kutibiwa haraka. Habari zaidi kuhusu maambukizi ya mtoto mchanga zimepeanwa katika Kifungu 6.4 cha Kipindi hiki.

Mchoro 6.3 Njia bora zaidi ya kumpasha joto mtoto aliye na baridi ni kumshika huku mwili wake ukiguzana moja kwa moja na wa mama.

Hipothemia hufasiliwa kama kiwango cha jotomwili cha nyusi 35.5 au zaidi, ingawa kiwango hiki ni cha chini sana na hatari kwa mtoto mchanga. Iwapo mtoto ana baridi, usigonje kiwangojoto kishuke hadi chini ya nyusi 36.5 kabla ya kuchukua hatua ya dharura ili kumpasha joto. Mvue nguo kisha umweke huku mwili wake ukiguzana na wa mama, katikati ya matiti akiwa amefunikwa kwa nguo. (Mchoro 6.3) Mfunike mama na mtoto kwa blanketi, huku ukifunika kichwa cha mtoto kwa chepeo au kijiblanketi. Iwapo mtoto hajavishwa sokisi, ifunike miguu yake (hii hujulikana kama Utunzaji wa Mama wa aina ya Kangaruu, kama utakavyojifunza katika Kipindi cha 8.) Iwapo kiwango cha jotomwili cha mtoto hakianzi kupanda hadi kile cha kawaida baada ya dakika 30, au ki chini ya nyusi 35.5, au midomo ya mtoto ni ya rangi ya samawati, mpeleke mtoto rufaa mara moja.

Baada ya kumchunguza mtoto ili kutambua dalili kuu kama ilivyoelezwa hapo juu, hatua inayofuata ni kumchunguza ili kutambua dalili hatari za maradhi ya watoto Wachanga.

6.3 Je, mtoto ana umanjano?

Dalili za maradhi ya umanjano ni uwepo wa rangi ya manjano ngozini na kwenye sklera (sehemu nyeupe ya macho). Hata hivyo, ni vigumu kuiona sklera ya watoto Wachanga, basi rangi ya ngozi hutumika kutambua umanjano. Kwanza muulize mama kama aliona rangi yoyote ya manjano ngozini mwa mtoto kabla hajafikisha umri wa saa 24. Baada ya hilo, chunguza mwenyewe huku ukikadiria kama viganja vya mikono na nyayo za miguu zina rangi ya manjano. Umanjano husababishwa na wingi wa hakiba ya pigmenti za manjano zinazojulikana kama bilirubini (hali hii pia hujulikana kama hipabilirubinemia, ‘bilirubini iliyopita kiasi’). Umanjano hujitokeza ngozini wakati hemoglobini kupita kiasi (protini inayobeba oksijeni) na iliyo katika seli nyekundu za damu imemenywa, au wakati ini halitendi kazi vyema, hivyo haliwezi kupunguza bilirubini, au wakati mshipa wa kutoa nyongo umezibwa. (Nyongo ni kiowevu kinachosaidia kumenya bilirubini na ambacho hutoleshwa na tezi za nyongo).

Mtoto mchanga asipotibiwa, bilirubini iliyopita kiasi huathiri sana ubongo wake, na hata kusababisha kifo. Isipotibiwa, inaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu ya neva (matatizo yanayohusiana na kuathiriwa kwa mfumo wa kati wa neva, kama vile kupooza kwa baadhi ya sehemu za mwili, msoto au ugumu wa kujifunza)

6.4 Maambukizi kwa mtoto mchanga

Maambukizi hutokea mara nyingi katika watoto Wachanga. Maambukizi haya ni baadhi ya visababishi vikuu vya vifo vya watoto.

  • Je, unaweza kukumbuka (kwa mfano, kwa kurejelea Kipindi cha 1) ni kwa nini kuna hatari zaidi ya watoto Wachanga kuambukizwa ikilinganishwa na watoto wakubwa au watu wazima?

  • Sababu moja kuu ni kutokomaa kwa mfumo wa kinga ya mwili. Utaratibu huu huchukua miezi kadhaa baada ya kuzaliwa hadi kufikia kiwango cha kuukinga mwili dhidi ya maambukizo.

    Mwisho wa jibu

Kipindi cha 17, Moduli ya Utunzaji katika ujauzito kinafunza kuhusu kupasuka kwa membreni za fetasi kabla ya wakati. Habari kuhusu leba inayochukua muda mrefu au iliyokinzana imetolewa katika Kipindi cha 9 cha Moduli ya Utunzaji wa Leba na Kuzaa.

Hii inamaanisha kuwa watoto Wachanga wako katika hatari kuu zaidi ya kuathiriwa na viini vya maambukizi wakati wa ujauzito, wanapozaliwa nyumbani na baada ya kuzaliwa. Vipengele vinavyosababisha hatari zaidi kwa watoto Wachanga ni wakati membreni za fetasi zimepasuka muda mrefu kabla ya wakati, leba imechukua muda mrefu, na maambukizi ambayo yamekuwepo katika sehemu ya chini ya njia ya uke wa mama. Kwanza tuzingatie maambukizi ya macho kwa watoto Wachanga.

6.4.1 Je, dalili za maambukizi ya macho ni gani?

Iwapo njia ya uzazi ya mama ina bakteria zinazosababisha magonjwa ya zinaa (hasa klamidia na kisonono), viini vya maambukizi haya vinaweza kuingia machoni mwa mtoto wakati wa kuzaliwa na hivyo vinaweza kusababisha upofu. Chunguza ubaini kama kuna uvimbe wa kope, wekundi kwenye sehemu ya ndani ya macho au mchozo kutoka machoni. Unaweza kumpa profilaksisi (matibabu ya kuzuia maambukizi) punde anapozaliwa. Matibabu haya yanaweza kufanywa kwa kutumia tetracycline au lihamu nyingine ya macho iliyopendekezwa, kama ilivyoonyeshwa katika Mchoro 6.4. Lakini iwapo mtoto huyu ameambukizwa macho baada ya kuzaliwa, mpeleke rufaa hadi hospitalini au katika kituo cha afya kwa uchunguzi au matibabu ya kina.

Mchoro 6.4 Desturi iliyopo ya kutunza macho ya mtoto mchanga ili asiambukizwe ni kupaka tetracycline mara moja punde baada ya kuzaliwa.

6.4.2 Je, dalili za maambukizi ya kiungamwana ni gani?

Mpeleke rufaa hadi hospitalini au kituoni mtoto anayeonyesha dalili zozote za maambukizi ya kitovu. Usitumie poda ya antibayotiki. Usimtie asprin kitovuni, wala dawa zozote za kutayarishiwa nyumbani.

Chunguza kiungamwana: je, ni chekundu au kinatoa usaha? Maambukizi ya kitovu huonyesha dalili hatari zifuatazo:

  • Kiungamwana kinachotoa uvundo na usaha.
  • Kiungamwana kinachobakia laini na chenye unyevunyevu na wala hakikauki vyema.
  • Wekundu wa ngozi inayozunguka mzizi wa kitovu.

Utunzaji bora wa kiungamwana unaweza kuzuia kutokea kwa maambukizi ya kiungamwana. Kinga dhidi ya maambukizi hujumuisha:

  • Kunawa mikono vyema
  • Usafi bora wa kibinafsi, wa mama na mtoto
  • Kufunga kiungamwana kwa uzi safi uliotakaswa na kukikata kwa vifaa vilivyotakaswa
  • Kuhakikisha kuwa kitovu ni safi na kikavu

6.4.3 Je, dalili za maambukizi ya ngozi ni gani?

Aina mbili kuu za maambukizi ya ngozi ya mtoto mchanga ni:

Mpeleke rufaa hadi hospitalini au kituoni mtoto anayeonyesha dalili za impetigo au upele wa moniliaisisi.

  • Maradhi ya impetigo husababishwa na bakteria iitwayo Staphylococcus iliyo ngozini. Maradhi haya hujitokeza kama uvimbe wenye usaha (pustuli) na kwa kawaida huonekana yamekizunguka kitovu au sehemu inayofungwa nepi. Je, kuna pustuli zozote? Pustuli zaidi ya 10 ni dalili ya kijumla ya hatari.
  • Upele wa moniliasisi husababishwa na fangasi (za daraja la Kandida au Monila). Mara nyingi, maradhi haya hutokea katika sehemu inayofungwa nepi. Dalili zake ni madoadoa mekundu yaliyofura kidogo, na yaliyokithiri mikunjoni mwa ngozi.

Kinyume na haya, upele unaotokana na nepi unaosababishwa na muwasho wa ngozi kwa sababu ya mkojo au kinyesi kwa kawaida huathiri sehemu wazi za ngozi wala sio mikunjo. Iwapo upele huu haujaambatana na maambukizi, kwa kawaida utadhibitiwa kwa kudumisha usafi wa hali ya juu, kumwosha mtoto mara nyingi kwa maji vuguvugu na kuacha ngozi ikauke kabisa.

Upele unaotokana na jasho, unaosababishwa na kutoa jasho jingi, unaweza kufanana na maambukizi, lakini sio maambukizi. Upele huu hujitokeza kwenye paji la uso kama vimbe dogo zisizo na rangi yoyote, au upele mwekundu kabisa shingoni na katika kiwiliwili. Mhakikishie mama kuwa hili si tatizo kuu, kisha umshauri amwoshe mtoto kwa maji vuguvugu na amkinge kutokana na joto jingi.

6.4.4 Tetanasi ya watoto Wachanga ni nini?

Mhamishe kwa darura mtoto aliye na dalili za tetanasi hadi hospitalini au kituo cha afya kilicho karibu. Mkiwa safarini, mkinge mtoto kutokana na hipothemia na umpe maziwa ya mama.

Tetanasi inayoathiri watoto Wachanga husababishwa na bakteria (Clostridium tetani) inayoambukiza tishu zilizokufa kama vile kitovu. Bakteria za tetanasi hupatikana kwenye udongo na kinyesi cha wanyama. Bakteria hizi zinaweza kuambukiza kiungamwana au vidonda vingine, kama vile kupitia desturi hatari za kimila. Bakteria hizi hutoa toksini (sumu) kali zinazoathiri mfumo wa neva. Itakisiwa kuwa mtoto ana tetanasi iwapo ataonyesha dalili zifuatazo:

  • Kuongezeka kwa mikazo ya misuli (spazimu), hususan katika misuli ya taya na fumbatio.
  • Spazimu ya misuli ya mwili wote na mtukutiko wa maungo unaosababishwa na vichocheo kama vile kushikwa au kelele. Mtoto anaweza kujipinda nyuma wakati wa spazimu (Kielelezo 6.5)
  • Watoto wengi walioambukizwa tetanasi hukumbwa na ugumu wa kupumua na wengi hufa hata wakiwa wamehudumiwa kimatibabu.
Mchoro 6.5 Mfano dhahiri wa spazimu ya misuli ya mtoto mchanga aliyeambukizwa tetanasi

6.4.5 Utawakinga vipi watoto wachanga dhidi ya maambukizi ya tetanasi?

Njia bora ya kumkinga mtoto dhidi ya maambukizi ni kuzalia katika kituo cha afya na kuzalishwa na mhudumu wa afya aliyehitimu, akitumia vifaa safi vilivyotakaswa. Hata hivyo, jambo hili mara nyingi haliwezekani mle vijijini mwa Afrika ambapo wanawake wengi huzalia nyumbani. Kwa sababu hiyo, jukumu lako la kupunguza maambukizi kwa watoto Wachanga ni muhimu mno. Kuna njia nyingi rahisi zinazoweza kutumika kuzuia maambukizi ya watoto wachanga. Unapaswa kufahamu kwa kina kuhusu njia hizi kwa kurejelea vikao vya awali vya moduli hii:

  1. Hakikisha hakuna msongamano nyumbani na ikiwezekana, waweke pamoja na mama zao watoto Wachanga wasioambukizwa.Usiwatenganishe watoto Wachanga na mama zao isipokuwa ikihitajika mno.
  2. Himiza unyonyeshaji: maziwa ya mama yana antibodi zinazosaidia kumkinga mtoto mchanga dhidi ya maambukizi.
  3. Jaribu kumshawishi mama asimwoshe mtoto katika saa 24 baada ya kuzaliwa. Veniksi (unyesho kama magandi au jabini unaofunika ngozi ya mtoto mchanga) ina chembechembe zinazozuia bakteria, hivyo basi inapaswa kuachwa ili ifyonzwe na ngozi ya mtoto.
  4. Kila wakati, kabla ya kumshika mtoto mchanga, nawa mikono yako vizuri kwa sabuni. Kunawa mikono hususan ni njia muhimu zaidi ya kuzuia uenezaji wa maambukizi.
  5. Msaidie mama kuzingatia usafi na unadhifu wake wa kibinafsi, na pia utie juhudi kuhakikisha kuwa chumba anamoishi mama na mtoto ni safi.
  6. Kila mara, tumia vifaa safi vya kukatia kiugamwana na uhakikishe kuwa kitovu ni safi na kimekauka. Visafishe kwa alkoholi vifaa vyote vinavyotumiwa katika utunzaji wa mama na mtoto kabla ya uchunguzi wowote.
  7. Kumbuka kuwa huduma ya profilaksisi ya macho kwa kutumia lihamu ya macho (tetracycline) yenye antibiotiki punde tu baada ya mtoto kuzaliwa huzuia maambukizi ya macho, lakini unapaswa kuitumia mara moja tu.
  8. Usisahau chanjo: wajawazito wote wapaswa kupewa chanjo ya tetanasi angalau mara mbili (na ikiwezekana hadi tano) ili kuzuia tetenasi kwa mtoto.

6.5 Orodha ya kukadiria hali hatari ya watoto wachanga

Baada ya kumuuliza mama kuhusu matatizo yoyote ya mtoto mchanga na kufanya uchunguzi wa kimsingi wewe mwenyewe, unaweza kumuainisha mtoto kulingana na orodha ya uchunguzi inayofuata (Jedwali 6.1).

Baada ya kumchunguza mtoto ili kubaini hali tata, kumbuka kuchunguza tena kuhusu dalili zote sizizo za kawaida alizozaliwa nazo/au dalili zote za majeraha ya wakati wa kuzaliwa (kwa mfano hitilafu mgongoni, kufura kwa kichwa, vilia vingi). Dalili hizi zinaweza kusababisha uhaba wa ghafla wa damu hivyo kupelekea kutokea kwa anemia.

Katika Kipindi cha 7, tutaeleza yote ambayo inakupasa wewe na mama kufahamu kuhusu kunyonyesha. Kubaini kuwa mtoto ananyonya vizuri na mama anaweza kumnyonyesha inavyofaa ni lengo moja la ziara ya nyumbani ya baada ya mama kuzaa. Unapaswa pia kumpima mtoto uzani kila mara unapomzuru nyumbani ili kuhakikisha kuwa anaongeza uzani kikawaida. Jambo hili ni muhimu hasa kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati (wiki 37 hadi 42 za ujauzito), au wale waliozaliwa na uzani wa chini ya kiwango cha kawaida (sawa na au zaidi ya gramu 2,500).

Watoto waliozaliwa kabla ya kukamilika kwa kipindi cha ujauzito (waliozaliwa katika wiki ya 32 – 36 ya ujauzito), watoto waliozaliwa muda mrefu kabla ya kukamilika kwa kipindi cha ujauzito (walizaliwa kabla ya wiki 32 za ujauzito), na watoto walio na uzani wa chini (chini ya gramu 1,500) wanaweza kuwa na dalili hatari za ziada kwa sababu hawajapata uwiano wa kumeza na kupumua, hivyo hawawezi kunyonya vyema. Utajifunza kuhusu utunzaji maalum wa watoto hawa wadogo sana katika Kipindi cha 8.

Jedwali 6.1 Orodha ya uchunguzi wa watoto Wachanga: chati ya ‘kuchunguza na kuainisha.
Uliza na uchunguzeAinishaHatua
  • Historia ya ugumu wa kunyonya au hawezi kunyonya sasa.
  • Historia ya mtukutiko wa maungo au anatukutika maungo sasa.
  • Mtoto mchanga ni mlegevu au amepoteza fahamu.
  • Mwendo hutendeka tu anapochochewa.
  • Kupumua kwa kasi
  • Kubonyea sana kwa sehemu ya chini ya kifua
  • Homa
  • Hipothemia

Ikiwa kuna mojawapo ya dalili hizi hatari za kijumla, ainisha kama:

MAAMBUKIZI HATARI YANAYOWEZA KUWEPO

Hamisha mtoto KWA DARURA hadi hospitalini au kituo cha afya

Hakikisha mtoto amepashwa joto la kutosha na umpe maziwa ya mama mkiwa safarini.

  • Mtoto kubadilika na kuwa manjano kabla ya saa 24 za umri wake.
  • Umanjano katika viganja na nyayo.
  • Kufura kwa macho au mchozo kutoka machoni.
  • Kutokwa na usaha kitovuni
  • Kupatikana kwa pustule zaidi ya 10 kwenye ngozi
  • Hakuna dalili zozote zilizotajwa hapo juu.

Ikiwa kuna mojawapo ya dalili hizi hatari, ainisha kama:

MAAMBUKIZI YANAYOWEZA KUWEPO AU UMANJANO

Hamisha mtoto KWA DARURA hadi hospitalini au kituo cha afya

Hakikisha mtoto amepashwa joto la kutosha na umpe maziwa ya mama mkiwa safarini.

MTOTOASIYE NA MATATIZOKumnyonyesha na kumtunza ili kumkinga dhidi ya maambukizi na kuhakikisha amepata joto la kutosha.

Muhtasari wa Kipindi cha 6

Katika Kipindi cha 6 umejifunza kuwa :

  1. Lengo muhimu la ziara yoyote ya nyumbani ni kumchunguza mtoto mchanga ili kubaini dalili zote za hatari, zikiwemo: kukosa kunyonya, mtukutiko wa maungo, ulegevu au mwendo wa mwili usio wa kawaida, kupumua kwa kasi na kubonyea kwa kifua, vidonda vya ngozi vikiwemo maambukizi ya kitovu, mchozo machoni na tetanasi ya mtoto mchanga.
  2. Maandalizi yanayofanywa kila mara kabla ya kumchunguza mtoto ni kunawa mikono yako vyema na kumuagiza mama aanze kunyonyesha ili uchunguze jinsi mtoto anavyonyonya, na pia kumtuliza mtoto unapoendelea kumchunguzi.
  3. Kumuuliza mama hali ya mtoto wake ni jambo muhimu linalokupasha habari utakayotumia katika uchunguzi.
  4. Hakikisha umemwelezea mama njia anazoweza kutumia kuzuia mtoto wake kuambukizwa, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kuhakikisha mtoto ni safi, na kwamba kitovu ni safi na kimekauka. Pia anafaa aepukane na msongamano au hali zisizo safi katika mahali wanamoishi.
  5. Kulingana na chati ya ‘Chunguza na Uainishe’ (Jedwali 6.1), orodha zinazoweza kupatikana ni: uwezekano wa maambukizi hatari, uwezekano wa maambukizi au umanjano, au mtoto asiyeambukizwa. Uainishaji utakusaidia kufanya uamuzi wa busara kuhusu hatua utakayochukua.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 6

Kwa kuwa sasa umekamilisha Kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili linatathmini jinsi ulivyojifunza. Kwanza, soma Mfano 6.1 kisha uyajibu maswali yanayofuata.

Mfano 6.1 Uchunguzi wa mtoto mchanga wa kike

Mtoto wa kike alizaliwa na mama wa umri wa miaka 32 katika kipindi cha wiki 39 za ujauzito. Ulimchunguza mtoto saa 28 baada ya kuzaliwa. Ana uzani wa kuzaliwa wa gramu 3,000 na ana historia ya mtukutiko wa maungo. Mtoto huyu pia hawezi kabisa kunyonya na kiwango chake cha jotomwili ni nyusi 38.5

Maswali la Kujitathmini 6.1(yanatathmini Malengo ya Somo la 6.1 na 6.3)

  • a.Utamuainishaje mtoto huyu ukizingatia umri wake wa ujauzito?
  • b.Utamuainishaje kulingana na uzani wake wa kuzaliwa?
  • c.Orodhesha dalili jumla za hatari zinazodhiirishwa na mtoto huyu.
  • d.Je una wazo gani kuhusu kiwago cha joto cha mwili cha mtoto huyu?
  • e.Utatoa uainisho gani wa tamati kuhusu mtoto huyu na jinsi gani utadhibiti hali yake?
Answer
  • a.Katika wiki 39 za ujauzito, mtoto huyu huainishwa kama mtoto aliyehitimu muhula wa kawaida.
  • b.Uzani wa kuzaliwa ni gramu 3,000, ambao huainishwa kama uzito wa kawaida wa kuzaliwa
  • c.Dalili hatari za jumla ni: kutonyonya, historia ya mtukutiko wa maungo na joto jingi mwilini.
  • d.Kiwango cha jotomwili (nyusi 38.5) si cha kawida na mtoto ana homa. Kiwango cha jotomwili cha kawaida kwa mtoto mchanga ni zaidi ya nyusi 36.5 hadi chini ya nyusi 37.5
  • e.Mtoto huyu ana dalili tatu kuu za hatari (kutonyonya, mtukutiko wa maungo na homa) na huainishwa kama aliye na uwezekano wa maambukizi. Njia iliyo bora ya kumhudumia mtoto huyu ni kumhamisha kwa dharura hadi hospitalini au katika kituo cha afya huku ukipendekeza kuwa mtoto amepata joto la kutosha na kumpa maziwa ya mama mkiwa safarini.

Mwisho wa jibu.

Sasa soma Mfano 6.2 kisha uyajibu maswali yanayofuata

Mfano 6.2 Uchunguzi wa mtoto mchanga wa kiume

Unamchunguza mtoto mchanga wa kiume mwenye umri wa saa nane, aliyezaliwa na mama mwenye umri wa miaka 27 katika kipindi cha wiki 31 za ujauzito. Mama huyu alikuwa anazaa kwa mara ya kwanza. Mtoto huyu ana uzani wa kuzaliwa wa gramu 1,300, anadhiirisha kima cha pumzi cha mara 72 kwa dakika na kifua kinabonyea. Kiwango cha jotomwilini nyusi 34.5

Maswali ya Kujitathmini 6.2 (yanatathmini Malengo ya Somo la 6.1 na 6.3)

  • a.Utaainisha vipi umri wa ujauzito wa mtoto huyu?
  • b.Utaainisha vipi mtoto huyu kulingana na uzani wake wa kuzaliwa?
  • c.Je kima cha pumzi mara 72 kwa dakika ni cha kawaida au la? Je kupumua kawaida ni kwa kiwango gani?
  • d.Je kuna nini kuhusu kiwango cha jotomwili cha mtoto huyu ni cha kawaida?
  • e.Utamdhibiti vipi mtoto huyu?
Answer
  • a.Kwa sababu mtoto alizaliwa akiwa na wiki 31 ya ujauzito, ataainishwa kama aliyezaliwa muda mrefu kabla ya wakati.
  • b.Uzani wa kuzaliwa ni gramu 1300, hivyo ataainishwa kama aliye na uzani wa kuzaliwa wa chini mno.
  • c.Kima chake cha pumzi cha mara 72 kwa dakika si cha kawaida. Mtoto huyu anapumua kwa kasi. Kima cha kawaida cha kupumua ni mara 40-60 kwa dakika.
  • d.Kiwango cha jotomwili (nyusi 34.5) ki chini mno. Mtoto ana hipothemia. Kiwango joto cha kawaida cha mtoto mchanga ni juu ya nyusi 36.5 hadi chini ya nyusi 37.5.
  • e.Kwa sababu alizaliwa muda mrefu kabla ya wakati na yuko na uzani wa chini sana, pia akiwa na dalili mbili kuu za hatari (kupumua kwa kasi na hipothemia), mtoto huyu anaainishwa kama aliye na uwezekano wa kuambukizwa. Hatua abora ya kumhudumia ni kumhamisha kidharura hadi hospitalini au katika kituo cha afya ukipendekeza hakikisho la kuwa mtoto amepata jotola kutosha na kumpa maziwa ya mama wakiwa safarini.

Mwisho wa jibu.

Maswali ya Kujitathmini 6.3 (yanatathmini Malengo ya Somo la 6.1, 6.2 na 6.4)

Tuseme ni siku yako ya kwanza kumzuru mama aliyezaa salama. Unamchunguza mtoto mchanga kama yuko salama, ikiwemo kuchunguza dalili za maambukizi.

  • Utamuuliza nini mama kabla ya kuanza kumchunguza mtoto mchanga?
  • Ni kitu gani utakachohakikisha kubaini utakapokuwa ukimchunguza mtoto huyu?

Tumia Jedwali 6.2 lililo hapa chini ili kupanga majibu yako

Jedwali 6.2 Kumchunguza mtoto mchanga
Maswali kwa mamaVitu vya kuchunguza katika mtoto mchanga

Answer
Jedwali 6.2 Kumchunguza mtoto mchanga (Jedwali lililokamilishwa).
Maswali utakayomuuliza mamaVitu vya kuchunguza katika mtoto mchanga
Je, mama anakumbuka kunawa mikono kabla ya kunyonyesha na kuzingatia usafi wake na wa mtoto?Je mama na mtoto wanaonekana safi na wazima. Je chumba ki safi na nadhifu?
Je mama amegundua mwendo wowote usio wa kawaida, spazimu ya mkono au mwili wote?Ikiwa ndivyo, chunguza kwa makini kubaini ikiwa mtoto anaweza kuwa ana mtukutiko wa maungo
Je mtoto anapumua taratibu bila ugumu?Kama mama ana wasiwasi, chunguza kuhusu kubonyea kwa kifua (kifua cha mtoto kubonyea ndani katika mbavu za chini) pia chunguza dalili za mtukutiko wa maungo.
Je mama anatunza kitovu kwa kuhakikisha ni safi na kimekauka? Je amegundua uvundo wowote kutoka kitovuni?Chunguza kama kuna mchozo au wekundu wa ngozi uliozunguka kitovu. Mkumbushe mama umuhimu wa kutunza kitovu kwa kuhakikisha ni safi na kimekaushwa.
Je, amegundua wekundu wowote au uozo kutoka kwa macho ya mtoto?Je tetracycline (au dawa yoyote ile ya macho iliyoidhinishwa) ilipakwa machoni mwa mtoto alipozaliwa.
Je mtoto anonekana mwenye baridi au mwenye joto jingi?Ikiwa mtoto anaonekana mwenye joto jingi, pima kiwango chake cha jotomwili (kwa kutumia themometa safi) na pia uchunguze kama amefunikwa vizuri. Ikiwa yuko baridi, chunguza kama ana hipothemia.
Je mama ana tatizo lolote akinyonyesha? Ikiwa ndivyo, chunguza kama chuchu za mama zimepasuka au ana joto jingi katika matiti (mastitisi au jipu). Kama anasita kunyonyesha mkumbushe umuhimu wa maziwa kwa mtoto, kwani yana virutubishi na hukinga mtoto dhidi ya maambukizi.
Je mtoto ana dalili zozote za upele? Ikiwa ndivyo, ni upele unaohusiana na nepi au jasho? Je kuna pustuli (malengelenge yenye usaha) ikiwa ni hivyo, malengelenge hayo yanazidi 10?
Je, yeye au mtoto alifanyishwa tambiko lolote hatari la kitamaduni kufuatia uzazi?Ikiwa ndivyo, chunguza mtoto kubaini dalili zozote za tetanasi (k.m spazimu ya misuli) na umwulize mama kama amechanjwa dhidi ya tetanasi.
Je mama anajihisi mzima kwa kijumla? Je, anakabiliana vyema na changamoto za kumtunza mtoto mchanga?Je mama anapata usaidizi wa kutosha, na mtoto anapata utunzaji wote anaohitaji?

Mwisho wa jibu