Skip to main content
Printable page generated Friday, 19 April 2024, 1:03 PM
Use 'Print preview' to check the number of pages and printer settings.
Print functionality varies between browsers.
Unless otherwise stated, copyright © 2024 The Open University, all rights reserved.
Printable page generated Friday, 19 April 2024, 1:03 PM

8. Utunzaji Maalum kwa Watoto Waliozaliwa kabla ya Kuhitimu Muhula na Waliozaliwa wakiwa na Uzani wa Chini

Kipindi cha 8 Utunzaji Maalum kwa Watoto Waliozaliwa Kabla ya Kuhitimu Muhula na Waliozaliwa wakiwa na Uzani wa Chini

Utangulizi

Katika Kipindi hiki, utajifunza kuhusu huduma maalum na ya ziada inayohitajika na watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini. Tutaleleza kwa kina sababu za watoto hawa kuhitaji utunzaji maalum, na jinsi unavyoweza kuwahudumia. Pia tutaeleza jinsi ya kuwashauri kina mama na watu wengine wa familia kuhusu kuwahudumia watoto hawa. Lengo letu ni kudhibiti matatatizo yanayohusiana na kuwalisha watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini, na jinsi ya kuwapasha joto. Utajifunza hasa kuhusu njia mwafaka na inayochukuliwa kuwa ya kisasa ya kudhibiti jotomwili la mtoto mkembe au mwenye kimo kidogo sana. Njia hii hujulikana kama Utunzaji wa Mama wa aina ya Kangaruu.

Malengo ya Somo la Kipindi cha 8

Baada ya somo hili, unatarajiwa:

8.1 Kufasili na kutumia kwa usahihi maneno yote muhimu yaliyoandikwa kwa herufi nzito. (Swali la Kujitathmini 8.2 )

8.2 Kueleza ni kwa nini watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au wakiwa na uzani wa chini wanahitaji utunzaji maalum, kisha uorodheshe matatizo yanayoweza kuwakumba mara nyingi. (Swali la Kujitathmini 8.1 )

8.3 Kutoa uainisho wa watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula kwa kurejelea umri wa ujauzito na uzani wa wakati wa kuzaliwa, na ueleze mikakati mwafaka ya kudhibiti hali hizi katika kila kauli. (Swali la Kujitathmini 8.2 )

8.4 Kueleza jinsi unavyoweza kumshauri mama kuhusu jinsi ya kumlisha mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula au akiwa na uzani wa chini. (Swali la Kujitathmini 8.3 )

8.5 Kueleza jinsi ya kuwakinga watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au wakiwa na uzani wa chini kutokana ha hipothemia, ukijumuisha kumshauri mama na familia yake kuhusu Utunzaji wa Mama wa aina ya Kangaruu. (Swali la Kujitathmini 8.4 )

8.1 Je, ni kwa nini watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au wakiwa na uzani wa chini wanahitaji utunzaji maalum?

Watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au wakiwa na uzani wa chini wako katika hatari zaidi ya kufa kutokana na hipothemia, maambukizi, matatizo ya kupumua na kutokomaa kwa viungo muhimu. Kinachofuatia ni kuwa watoto hawa hushindwa kukabiliana na maisha nje ya uterasi. Sababu kuu zinazowafanya wahitaji utunzaji maalum zimeandikwa kwa muhtasari katika Jedwali 8.1

Kisanduku 8.1 Sifa bainifu za watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa nauzani wa chini

  • Baadhi ya sehemu za mfumo wao wa neva hazijakua vyema.
  • Watoto hawa wana kiwango kidogo cha mafuta ya ngozi, hasa mafuta ya rangi ya kahawia. Mafuta haya ni muhimu sana katika kutolesha joto kwa mtoto mzawa. Mafuta haya hupatikana mabegani, mgongoni, shingoni, kwapani na figoni.
  • Watoto hawa hawachezi, hivyo hawatoleshi joto, ambalo hutoleshwa kwa kucheza sana.
  • Watoto hawa wana uwiano mkubwa wa uzani na sehemu ya juu ya mwili ikilinganishwa na ule wa mtoto mkubwa au mtu mzima. Kwa hivyo, watoto hawa hupoteza joto kwa haraka kupitia ngozini.
  • Watoto hawa wana mapafu ambayo hayajakomaa, hivyo wana matatizo ya kupumua.
  • Watoto hawa hawana kingamwili imara, hivyo wako katika hatari kuu zaidi ya kuambukizwa.
  • Vena za ubongo wao ni nyembamba na hazijapevuka hivyo zinaweza kuvuja damu kwa urahisi.
  • Watoto hawa wanaweza kuwa dhaifu sana hata wasile vyema.

Mfano mmoja wa sababu inayowafanya watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au wakiwa na uzani wa chini kuhitaji utunzaji maalum ni kuwa wana uwezo mdogo kupindukia wa kukabiliana na maradhi ambukizi. Hii ni kwa sababu kingamwili yao haijakomaa vyema. Kwa hivyo, kando na linalohitajika kwa watoto wote, wewe na mama mnafaa kuwa waangalifu kuhusu usafi na hatua za kuzuia maambukizi (kama ilivyoelezwa katika Kipindi cha 6). Yeyote anayemshika mtoto anafaa kwanza anawe mikono vyema kabisa, kisha amshike kwa uangalifu. Ngozi ya mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula au akiwa na uzani wa chini inaweza kuchibuka kwa urahisi, hivyo kusababisha maambukizi kuingilia mle.

8.2 Uainishaji wa sifa bainifu za watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini

Jinsi mtoto mzawa alivyo na uzani wa chini na umri mdogo ndivyo alivyo katika hatari kuu ya kukumbwa na matatizo, na hata kufa, na ndivyo anavyohitaji utunzaji maalum zaidi. Utunzaji anaohitaji unafaa kuzingatia uainishaji wa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na wakiwa wadogo sana kama ilivyoelezwa hapa chini.

8.2.1 Uainishaji kwa kuzingatia uzani wa wakati wa kuzaliwa

Kwa kuzingatia uzani wa wakati wa kuzaliwa, watoto wengi huzaliwa wakiwa na uzani wa chini au uzani wa chini sana, kama ilivyoainishwa hapa chini:

Uzani wa chini wa wakati wa kuzaliwa Watoto wanaozaliwa wakiwa na uzani wa gramu 1,500-2,499. Watoto hawa wanaweza kuhudumiwa vyema nyumbani kwa kuzingatia utunzaji na usaidizi zaidi.

Uzani wa chini sana wa wakati wa kuzaliwa Watoto wanaozaliwa wakiwa na uzani wa chini ya gramu 1,500. Tatizo lililo hatari kwa usalama wa watoto wadogo kiasi hiki ni kuwa hawawezi kunyonya, kumeza na kupumua kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, watoto hawa huhitaji uangalifu maalum ili kuwalisha kwa njia ifaayo na salama. Watoto hawa pia wanakumbwa na ugumu wa kudhibiti kiwangojoto cha mwili, hivyo wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa hipothemia. Watoto hawa huhitaji usaidizi wa kimaisha wa hali ya juu, hivyo wanafaa kupewa rufaa ya dharura hadi katika hospitali iliyo na vifaa maalum vya kuwatunza watoto walio wadogo kupindukia. Hata hivyo, kwa sasa, inawezekana kuwa vifaa kama hivi havipatikani katika familia zinazoishi baadhi ya sehemu za mashinani mwa Afrika.

8.2.2. Uainishaji kwa kuzingatia umri wa ujauzito

Mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula ni aliyezaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito kuisha. Kwa kuzingatia umri wa ujauzito, watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula wameainishwa zaidi kama ifuatavyo:

Mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula: Watoto waliozaliwa katika umri wa ujauzito wa wiki 32 - 36, kama ilivyokokotolewa kutokana na tarehe ya mwisho ya kipindi cha hedhi ya mama. Watoto hawa wanaweza kuhudumiwa vyema nyumbani kwa kuzingatia utunzaji na usaidizi zaidi. Utajifunza kuhusu haya baadaye katika Kipindi hiki.

Mtoto aliyezaliwa siku nyingi kabla ya kuhitimu muhula: Watoto waliozaliwa katika umri wa ujauzito wa wiki 28-31, kama ilivyokokotolewa kutokana na tarehe ya mwisho ya kipindi cha hedhi ya mama. Watoto hawa wana matatizo ya kula na kudhibiti kiwangojoto cha mwili wao kama watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula, na kwa sababu sawa na zao. Ikiwezekana, wanafaa kupewa rufaa mara moja ili kupewa utunzaji maalum hospitalini.

Jedwali 8.1 inaainisha kwa muhtasari yale ambayo tumeeleza, pamoja na hatua unazo hitaji kuchukua.

Jedwali 8.1 Uainishaji wa watoto wazawa kwa kuzingatia uzani wa wakati wa kuzaliwa na umri wa ujauzito.
Uzani wa wakati wa kuzaliwa na umri wa ujauzitoUainishajiHatua
Uzani wa chini ya gramu 1,500. Uzani wa chini sana wa wakati wa kuzaliwaMpe rufaa ya DHARURA hadi hospitalini, na uhakikishe amepashwa joto wakati wa kusafiri
Umri wa ujauzito wa chini ya wiki 32Mtoto aliyezaliwa siku nyingi kabla ya kuhitimu muhula:Hakikisha mtoto huyu amepashwa joto na umpe rufaa mara moja.
Uzani wa gramu 1,500 - 2,500.Uzani wa chini wa wakati wa kuzaliwaIwapo hakuna tatizo lingine, mshauri mama kuhusu kunyonyesha mwafaka, kuzuia maambukizi na kumpasha mtoto joto.
Umri wa ujauzito wa wiki 32- 36Mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhulaNi kama ilivyoelezwa kuhusu mtoto aliyezaliwa na uzani wa chini wa wakati wa kuzaliwa
Uzani ulio sawa na au zaidi ya gramu 2,500 na umri wa ujauzito ulio sawa na au zaidi ya wiki 37Uzani wa kawaida na kipindi cha kuzaliwa kilichokamilikaNi kama ilivyoelezwa kuhusu mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula na akiwa na uzani wa chini wa wakati wa kuzaliwa.

8.3 Ushauri kuhusu jinsi ya kuwalisha watoto waliozaliwa kabla ya wakati na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini

Maziwa ya matiti yanayotolewa na mama wa mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula yana virutubishi zaidi ya yale yanayotolewa na mama aliyezaa katika kipindi cha kawaida. Kwa hivyo, maziwa ya mama aliyezaa kabla ya kuhitimu muhula au aliyezaa mtoto mwenye uzani wa chini ndiyo bora. Hivyo basi, hayafai kutupwa kwa sababu hakuna maziwa mengine yanayoweza kuchukua nafasi yake.

8.3.1 Kunyonyesha na kunywesha kwa kikombe

Katika wiki ya kwanza ya maisha ya mtoto, mama anahitaji usaidizi wako na wa familia yake. Hii ni ili kumhimiza aanze kumnyonyesha mtoto bila kumpa vyakula vingine na kuendelea kunyonyesha hadi mtoto wake aliye mdogo kupindukia aweze kunyonya bila tatizo. Watoto wanaozaliwa katika wiki ya 34 - 36 ya ujauzito wanaweza kunyonya vyema, lakini wale waliozaliwa siku nyingi kabla ya kuhitimu muhula wanaweza kukumbwa na tatizo la kunyonya. Kumnyonyesha mtoto aliyezaliwa mapema sana kabla ya kuhitimu muhulanhuwa changamoto. Mtoto huyu anafaa kunyonya kila baada ya saa 2, ikiwa ni pamoja na usiku.

Iwapo watoto waliozaliwa kabla ya wiki 34 hawawezi kunyonya vyema, wanaweza kupewa maziwa yaliyokamuliwa, kwa kutumia kikombe safi kabisa. (Tutaeleza jinsi ya kufanya hivi katika kifungu kijacho.) Watoto wadogo kwa kimo au waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula ambao wanaweza kunyonya pia wanaweza kuhitaji kupewa maziwa kwa kikombe ili kuhakikisha kuwa wanapata lishe la kutosha. Watoto wote wanaopewa maziwa kwa kikombe wanafaa kupewa takriban ml/kilo 60 kwa siku (yaani mililita 60 kwa kila kilo ya uzani wa mtoto kila siku). Kiwango hiki kinafaa kuongezwa kwa ml/kilo 20 jinsi mtoto anavyohitaji kulishwa zaidi.

Watoto waliozaliwa baada ya wiki 32 za ujauzito huenda wasiweze kunyonya hata kidogo, hivyo wanahitaji kuanzishiwa kupewa vinywaji vinavyotiwa kwa mipira. Hii ni sababu mojawapo wa zinazosababisha mtoto aliyezaliwa kabla ya wiki 32 za ujauzito anafaa kupelekwa rufaa hadi katika kituo cha afya mara moja.

8.3.2 Vidokezo vya kumsaidia mama kumnyonyesha mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula au aliyezaliwa akiwa na uzani wa chini.

Mchoro 8.1 Mpe mtoto titi lote ili kumhimiza kunyonya.

Kamulia matone machache ya maziwa midomoni mwake ili kumsaidia kuanza kunyonya. Ili mtoto anyonye kwa mafunda makubwa, mpe titi lote, wala sio chuchu tu (Mchoro 8.1). Mpumzishe kwa kifupi anaponyonya. Kunyonya huwa jambo gumu kwa mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula au aliye mdogo kupindukia.

Iwapo mtoto atakohoa, kutapika au kutema maziwa anapoanza kunyonya, huenda maziwa yanachuruza kwa kasi sana hivi kwamba hawezi kuyadhibiti. Mfunze mama kumwondolea mtoto titi iwapo jambo hili litafanyika. Mshikilie mtoto ukimuegeza kifuani mwa mama hadi aanze kupumua vyema tena, kisha umpe titi tena baada ya funda la kwanza la maziwa kupita.

Iwapo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula hana nguvu za kunyonya kwa muda mrefu, nfunze mama jinsi ya kukamua maziwa yake kisha amnyweshe mtoto kwa kikombe.

8.3.3 Kukamua maziwa ya titi la mama

Inaweza kumchukua mama dakika 20-30 kukamua maziwa ya titi, au hata muda zaidi mwanzoni, lakini mama huongeza kasi ya kukamua pindi anavyopata uzoefu. Kwanza mshauri mama anawe mikono na kuosha matiti kwa sabuni na maji, kisha aikaushe kwa taulo taulo safi kabisa. Kiandae kikombe safi kilichochemshwa au chupa iliyo na mdomo mkubwa. Iwapo hawezi kuchemsha kikombe chote, kitie maji yanayochemka na uyaache mle hadi muda mchache kabla ya kutia maziwa. Kisha yamwage yale maji. Maziwa hukingwa dhidi ya bakteria kwa kufanya hivi.

Mama anafaa kuketi vyema kisha aegemee kikombe. Mwonyeshe jinsi ya kushika titi kwa ‘mshiko wa C’ (mkono wake ukichukua umbo la C kubwa; Kielelezo 8.2a). Finya nyuma kidole gumba na vidole vingine kuelekea kifuani (Kielelezo 8.1b), kisha ukizungushe kidole gumba kwenda mbele kana kwamba unatolesha alama za kidole. Hii ni ili kuyatoa maziwa kutoka sehemu zote za titi. Kamua titi moja kwa angalau dakika 3 - 4 hadi maziwa yapungue, kisha ukamue hilo lingine. Kuwaza kuhusu mtoto wake anapokamua kunaweza kufanya maziwa yachuruze kwa urahisi zaidi.

Mchoro 8.2 Kukamua maziwa ya titi (a) Shika titi kwa mshiko wa C; (b) zungusha vidole na kidole gumba kwenda nyuma na mbele ili maziwa yachuruze kutoka chuchuni hadi ndani ya kikombe kilichotakaswa.

Maziwa yaliyokamuliwa kisha yakawa baridi au yaliyowekwa kwa saa 6 yanafaa kutupwa

Maziwa ya titi yanaweza kuhifadhiwa katika kiwango joto cha chumbani kwa saa 6 iwapo chumba hicho hakina joto jingi, na maziwa yamehifadhiwa ndani ya kifaa kilichotakaswa. Hata hivyo, maziwa haya yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi ndani ya friji, iwapo mama anayo. Popote yalipohifadhiwa, maziwa yanafaa kupashwa joto hadi kiwango cha joto la mwili kabla ya kumpa mtoto. Kitie ndani ya bakuli yenye maji moto kifaa kilicho na maziwa yaliyohifadhiwa ili kuyapasha joto. Usichemshe maziwa ya matiti ya mama! Virutubishi na antibodi za maziwa ya mama huharibiwa yanapochemshwa.

8.3.4 Mwonyeshe mama jinsi ya kumnywesha mtoto kwa kikombe

Mchoro 8.3 Kumnywesha mtoto aliye mdogo kupindukia huhitaji uangalifu na subira.

Mwonyeshe mama na watu wengine wa familia jinsi ya kumshika mtoto kwa karibu huku wakiwa wameketi wima. Shikilia kwenye mdomo wa chini wa mtoto kijikombe safi sana cha maziwa ya mama yaliyokamuliwa. Mtoto anapoamka na kufungua kinywa, shikilia kikombe midomoni mwake ukimwacha anywe kwa utaratibu. Mpe mtoto wakati wa kumeza na kupumzika kila baada ya kupiga funda. Mtoto anapokunywa vya kutosha na kukataa kunywa zaidi, muweke begani kisha umfanye apige mbweu kwa kumsugua mgongoni taratibu ili kuitoa hewa ambayo huenda aliimeza pamoja na maziwa.

  • Je, ni vidokezo na mitindo gani ya kunyonyesha unayofaa kumweleza au kumfunza mama aliyezaa kabla ya kuhitimu muhula?

  • Unafaa kumwarifu kuhusu:

    • Umuhimu wa kunywesha mtoto kwa maziwa yake kila wakati.
    • Kukamulia matone machache ya maziwa midomoni mwake ili kumshawishi kuanza kunyonya.
    • Jinsi ya kukamua maziwa yake na kuyahifadhi vyema.
    • Jinsi ya kumnywesha mtoto kwa kikombe

    Mwisho wa jibu

8.4 Utunzaji maalum ili kuhakikisha mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula na aliyezaliwa akiwa na uzani wa chini amepashwa joto

Watoto hawa hukumbwa na ugumu wa kudhibiti kiwangojoto cha mwili. Watoto hawa hupoteza jotomwili kwa urahisi, hivyo wapo katika hatari ya kupata hipothemia katika hali hii. Kila mara, fuata kanuni ya ’warm chain’ unapomhudumia mtoto yeyote, bila kuzingatia uzani au umri wake, kama ulivyojifunza katika Kipindi cha 7. Hata hivyo, watoto waliozaliwa muda mrefu kabla ya kuhitimu muhula na walio wadogo sana wanafaa kupewa huduma maalaum ifuatavyo:

  • Punde baada ya kuzaliwa, mlaze mtoto huyo ngozi yake ikiguzana na ya mama, kisha ufuatilishe Utunzaji wa Mama wa aina ya Kangaruu, iliyoelezwa hapa chini.
  • Blanketi au shuka za ziada zilizotengezwa kwa pamba zinahitajika ili kumfunika mama na mtoto. Jambo muhimu la kukumbuka (linalosahaulika mara nyingi) ni kwamba kichwa cha mtoto kinahitaji kufunikwa vyema. Hii ni kwa sababu zaidi ya 90% ya jotomwili hutokea kichwani kisipofunikwa vyema.
  • Chumba anapotunziwa mtoto kinafaa kuwa na kipasha joto cha ziada.
  • Kawisha kumwosha mtoto kwa angalau saa 28 baada ya kuzaliwa, ukitumia maji vuguvugu kila unapomwosha.
  • Anzisha kumnyonyesha mtoto au kumnywesha kwa kikombe muda mfupi iwezekanavyo baada ya kuzaliwa. Mnyweshe mtoto kila baada ya saa 2.
  • Ni jabo gani unalofaa kuzingatia ili kuhakikisha kuwa mtoto amepashwa joto?

  • Unakumbuka kama tulivyo jifunza katika Kipindi cha 7 kuwa ni muhimu kumkinga mtoto kutokana na baridi - hivyo basi, hakikisha kuwa milango na madirisha yote yamefungwa.

    Mwisho wa jibu

8.5 Utunzaji wa aina ya Kangaruu wa Mama kwa Mtoto

Utunzaji wa aina ya Kangaruu wa Mama kwa Mtoto (UKM) ni njia ya utunzaji iliyopewa jina kwa kurejelea jinsi kangaruu wanavyowatunza ndama wao. Njia hii imetambulika kuwa bora sana katika kuwatunza watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini. Njia hii huhusisha kumshika mtoto huku mwili wake ukiguzana na wa mama mchana na usiku. Mtu mwingine anaweza kuchukua nafasi ya mama iwapo hawezi kumshika namna hii wakati wote.

Utafiti unaonyesha kuwa njia ya UKM inapotumika, husaidia kudhibiti kima cha mdundo wa moyo na kupumua kwa watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini. Njia hii pia husaidia kupunguza maambukizi na kumwezesha mtoto kuongeza uzani ifaavyo. Njia hii humsaidia mama kwa kuzidisha utoleshaji wa maziwa, na pia kufanikisha kunyonyesha bila kutumia vyakula vya ziada.

8.5.1 Utaratibu wa UKM

Baada ya ya kumwelezea mama kuhusu utaratibu wa UKM (ama mhudumu mwingine kufanya hivyo) unafaa kufuata hatua zilizopeanwa katika jedwali 8.1

Kisanduku 8.1 Matayarisho ya UKM
  • Hakikisha kuwa chumba ni safi na chenye kiwangojoto mwafaka.
  • Hakikisha kuwa mama yuko faraghani hivi kwamba anaweza kufungua sehemu ya mbele ya nguo yake na kutoa matiti yake.
  • Mshauri mama aketi au kuegemea barabara.
  • Mvue mtoto nguo zote kwa utaratibu isipokuwa chepeo, nepi na sokisi.
  • Mlaze mtoto tambarare, huku akimtaza mama kwa hali ya uwimawima na kutandazika katikati mwa matiti ya mama, mwili wake ukiguzana na wa mama.
  • Geuza kichwa cha mtoto upande mmoja ili kufungua njia za kupumua. Mweke mtoto katika hali hii kwa saa 24 kila siku, isipokuwa kwa vipindi vifupi vya mapumziko.
  • Mfunike mtoto kwa shuka au gauni la mama, umfunge kwa blanketi ya ziada, kisha umvishe chepeo kichwani.
  • Mnyonyeshe mtoto mara kadhaa, angalau mara 8 -12 kila siku.
Mchoro 8.4 Mtoto na mama wanaweza kulala panoja wakati wa UKM.

Mhakikishie mama kuwa mtoto anaweza kupokea utunzaji muhimu wa kila siku, ikiwa ni pamoja na kunyonyesha, wakati wa UKM. Mtoto huondolewa kutoka hali ya kuguzana na mama wakati wa kumbadilisha nepi, usafi wa jumla wa kimwili, utunzaji wa kitovu na uchunguzi wakati wa ziara. Mama anahitaji kulala kitandani siku 3 - 5 tu za kwanza baada ya kuzaa. Hali ya mtoto inapokuwa dhabiti, mama anaweza kutembea na kufanya kazi zake za kawaida huku mtoto akiwa katika UKM, na wanaweza kulala pamoja usiku wakifuata njia ya UKM.

8.5.2 Kubaini kama mtoto yuko salama katika UKM

Katika kila ziara ya baada ya kuzaa unafaa:

  • Kukadiria kima cha kupumua cha mtoto, ukihakikisha kuwa hapumui kwa kasi sana.
  • Kuhakikisha kuwa mtoto analishwa vyema.
  • Kupima kiwangojoto cha mwili cha mtoto kwapani, ukihakikisha kuwa ni cha kawaida.
  • Kama mtoto yuko salama, Kuidhibitishia familia, iwapo mtoto yuko salama, lakini uwaarifu watafute msaada wako punde wanapokumbwa na tatizo lolote.

8.5.3 Kumshauri mama na familia kuhusu umuhimu wa UKM

Njia ya UKM inaweza kuonekana kama njia isiyo ya kawaida ya kumtunza mtoto. Kwa hivyo, ni muhimu kuchukua muda unapomshauri mama, baba na familia kuhusuvipengele vya njia hii na manufaa yake. Mama (na familia) wanapaswa kushawishika na kukubali kutumia njia hii kwa siku nyingi mfululizo. Baba na watu wengine wa familia pia wanapaswa kuwa tayari kutoa usaidizi wa kimwili na kihisia kwa mama anapotumia njia ya UKM

Umuhimu wa UKM ni nini?

Kunyonyesha: UKM huimarisha kima cha unyonyeshaji na muda wa kunyonyesha.

  • Udhibiti wa joto mwilini: kuguzana kwa muda mrefu kwa mwili wa mama na mwanawe aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula wa ujauzito/aliye na uzani wa chini husaidia kudhibiti kiwango cha joto mwilini mwa mtoto na pia kupunguza hipothemia.
  • Kuongezeka kwa uzani mapema: watoto wembamba huongeza uzani wakitumia UKM kuliko wakitumia utunzaji wa kawaida baada ya kuzaliwa
  • Vifo kupunguka: watoto wanaotumia huduma hii ya UKM wanapumua kwa ubora zaidi na uwezekano kukoma kupumua ni wa kima cha chini. Njia hii pia humkinga mtoto dhidi ya maambukizi.

Kwa kweli inaweza kuwa vigumu kwa kina mama wote kutumia UKM. Kwa hivyo, ni sharti uhakikishe kuwa mama hana matatizo au maradhi yoyote yanayoashiria kuwa anakosa nguvu za kutumia njia hii bila kusaidiwa. Ikiwa anakumbwa na matatizo haya, unapaswa kubaini kama baba au jamaa yeyote wa familia anaweza kushirikiana na mama kutoa utunzaji huu au kumtunza mtoto kwa njia hii wakati wote iwapo mama anaugua. Hatimaye, kina mama ambao wameweza kutoa utunzaji huu kikamilifu wana ujasiri mwingi mbali na kuridhika kuwa wanaweza kuwafanyia jambo spesheli watoto wao.

8.5.4 UKM inafaa kufanywa kwa muda gani?

Ikiwa mama na mtoto wanaridhika kutumia njia hii, inafaa kueendelezwa kwa kipindi kirefu kama inavyowezekana au mpaka mtoto ahitimu muhula wa kuzaliwa (wiki 40) ama mpaka mtoto apate uzani wa gramu 2,500. Iwapo mtoto ana uzani unaozidi gramu 1 800 na kiwango chake cha jotomwili ni dhabiti, hana matatizo yoyote ya kupumua na ananyonya vizuri, anaweza kulishwa kupitia UKM kabla ya wiki 40. Mtoto anapotosheka na UKM humdhiirishia mama yake kupitia, kugaagaa, kuchezacheza, kuondoa miguu na mikono yake kutoka kwenye nguo zilizomfunika na kulia hadi afunuliwe.

Hatimaye, ukifuata maagizo haya na kuwasaidia familia zako kutunza watoto wao waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula au waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini kama ilivyoelezwa katika Kipindi hiki, ni hakika kuwa utaokoa maisha ya watoto wengi wachanga. Kunalo jambo muhimu kuliko hili?

Muhtasari ya Kipindi cha 8

Katika Kipindi cha 8 umejifunza kuwa:

  1. Watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na wale wenye uzani wa chini wamo katika hatari ya kufa kufuatia maambukizi, matatizo ya kupumua na hipothemia kwa kuwa hawajakomaa.
  2. Punde tu wanapozaliwa ni muhimu kuainisha watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na wale waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini kulingana na umri wao wa ujauzito na uzani wao wa kuzaliwa, na kupendekeza rufaa kwa wale waliozaliwa wakiwa na umri wa ujauzito wa chini mno na wale walio na uzani wa chini sana.
  3. Unaweza kumshauri mama kikamilifu kuhusu namna ya kumnyonyesha mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliyezaliwa akiwa na uzani wa chini, ikiwemo kumlisha baada ya kila saa mbili. Unafaa pia kumfunza jinsi ya kujikamua na namna ya kumnywesha mtoto kwa kikombe ikiwa mtoto hawezi kunyonya vyema kwa kuwa hajakomaa.
  4. Unaweza kumfunza mama na familia yake jinsi ya kutoa Utunzaji wa aina ya Kangaroo ya Mama kwa Mtoto (UKM) na kuwaelezea manufaa ya njia hii, ambayo ni pamoja na kuendeleza kunyonyesha, kudhibiti jotomwili la mtoto, kuongeza uzani mapema, kupumua vyema zaidi na upungufu wa kima cha maambukizi.
  5. UKM huendelezwa usiku na mchana hadi mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula anapofikisha umri wa wiki 40 au mtoto aliyezaliwa akiwa na uzani wa chini anapofikisha angalau gramu 1,800. Mama atahitaji usaidizi zaidi ili kukabiliana na changamoto za UMK.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 8

Kwa vile sasa umekamilisha Kipindi hiki, jibu maswali yafuatayo ili kutathmini jinsi ulivyojifunza.

Swali la Kujitathmini 8.1(linatathmini Malengo ya Somo la 8.2)

Ni viashirio vipi muhimu vinavyoonyeshwa na watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na wale waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini ambavyo hudhiirisha kuwa wanahitaji utunzaji spesheli?

Answer

Vidokezo vikuu vinavyoashiria kuwa watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na wale waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini huhitaji utunzaji spesheli ni:

  • Kutokomaa kwa mfumo wa kingamwili hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa.
  • Kuwa na hatari ya kupata matatizo ya utendakazi ya mfumo wa neva na mapafu
  • Hatari ya kupata hipothemia, kwa sababu wana kinga ndogo inayotolewa na mafuta ya mwili, na kuna uwiano mkubwawa sehemu juu ya mwili ikilinganishwa na uzani wa mwili na kutoweza kujizalishia joto.
  • Uwezekano wa ugumu wa kunyonya, hivyo ukosefu wa virutubishi, unaweza kusababisha unyonge na hata kudhoofika kwa kingamwili na mwili kukosa joto.
  • Kuwa hatari ya kushika vibaya, kwa mfano kusasbabisha kuharibika kwa ngozi yake dhaifu ambapo husabisha viingizi vya maambukizi.

Mwisho ya jibu

Swali la Kujitathmini 8.2 (linatathmini Malengo ya Somo la 8.1 na 8.3)

Jaza mapengo katika Jedwali 8.2

Jedwali 8.2 Uainishaji wa watoto wazawa kulingana na uzani wa kuzaliwa na umri wa ujauzito, na hatua za kuchukuliwa.
Uzani wa kuzaliwa na umri wa ujauzitoUainishajiHatua za kuchukuliwa
Uzani wa chini ya gramu 1,500
Walizaliwa wakiwa na umri wa ujauzito wa chini mno
Umri wa ujauzito wiki 32-36Ikiwa hukuna tatizo jingine, mshauri kuhusu kunyonyesha kikamilifu, kuzuia maambukizi na kuhakikisha mtoto amepata joto la kutosha.
Uzani wa kawaida na muhula yote ya ujauzito
Answer

Rejelea Kisanduku 8.1 katika Kitengo cha 8.2.1 na ulinganishe na yale uliyoandika katika jedwali 8.2

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.3 (linatathmini Malengo ya Somo la 8.4)

Ulimzuru mama aliye na mtoto aliyezaliwa akiwa na uzani wa gramu 2,000 kwa mara ya kwanza saa 12 baada ya kuzaa. Yamkini ana uwezo wa kunyonya, ingawa sio kwa muda mrefu, na mama yake ana wasi wasi kuwa hawezi kupata maziwa ya kutosha. Je utamshauri vipi?

Answer

Kwa kuwa ana uzani wa gramu 2,000 mtoto huyu ana uzani wa chini, lakini anaonekana kuwa na uwezo wa kunyonya. Hata hivyo, ikiwa mama yake anafikiria kuwa mtoto hapati maziwa ya kutosha kwa sababau anachoka haraka akinyonya, unapaswa kumpendekezea ampatie lishe ya ziada ya maziwa ya mama ya kujikamua na kumnywesha kwa kikombe. Kwanza unapaswa umfafanulie jinsi ya kujikamua na namna ya kuhifadhi maziwa (rejelea Kitengo cha 8.3.3 kama huwezi kukumbuka), kisha umwonyeshe jinsi ya kumnywesha mtoto kwa kikombe.

Mwisho wa jibu

Swali la Kujitathmini 8.4 (linatathmini Malengo ya Somo la 8.5)

  • a.Ni mambo gani muhimu ambayo haupaswi kumfanyia mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula ili kumkinga dhidi ya hipothemia.
  • b.Utunzaji aina ya Kangaruu wa Mama kwa Mtoto una manufaa gani katika kuzuia hipothemia?
Answer
  • a.Ili kumkinga mtoto aliyezaliwa kabla ya kuhitimu muhula au aliyezaliwa akiwa na uzani wa chini asipoteze joto, unapaswa kujiepusha:
    • Kumuosha mtoto hadi baada ya angalau saa 48 baada ya kuzaliwa
    • Kumuacha mtoto bila kofia (90% ya joto hupotezwa kupitia kichwa ikiwa kimefunuliwa)
    • Kumuacha mtoto chumbani bila milango au madirisha kufunguliwa
    • Kusahau kuweka kipasha joto cha ziada chumbani ambamo mtoto amelazwa.
    • Kumvua nguo zote ili kubadilisha nepi.
  • b.Manufaa ya UKM ni:
    • Mtoto hushikwa huku mwili wake ukiguzana na wa mama mchana na usiku, jambo ambalo litahakikisha kuwa kiwango cha jotomwili la mtoto kimedibithiwa kikamilivu.
    • Desturi ya kumshika mtoto huku mwili wake ukiguzana na wa mama husitishwa tu kwa sababu maalum (kubadilishia nepi, kumchunguza kama kitovu kinakauka kama kawaida) hivyo basi kupunguza hatari ya kuachwa kwenye chumba kilicho na baridi.
    • Mtoto hunyonya vizuri na kuongeza uzani haraka (hivyo huzalisha mafuta ya mwili yanayomsaidia kupata joto)
    • Manufaa ya UKM ni kuwa huduma hii unaweza kutolewa na mtu mwingine katika familia ikiwa mama ni mgonjwa au anahitaji kupumzika.

Mwisho wa jibu