Utangulizi

Utangilizi wa Moduli ya Utunzaji wa Baada ya kuzaa

Jinsi unavyojua kutoka katika moduli zilizopita juu ya utunzaji katika ujauzito, uchungu wa kuzaa na, muda punde tu baada ya kuzaa ni kipindi cha hatari kubwa kwa kina mama na watoto wazawa.Takribani asilimia 65 ya vifo vya kina mama kabla, katika na muda mfupi baada ya kuzaa na asilimia 75 ya vifo vya watoto wazawa hutokea katika siku saba za kwanza baada ya kuzaa na takribani nusu ya vifo hivi hutokea katika saa 24 za kwanza. Mtoto mchanga huwa na uwezekano wa takribani mara 500 zaidi kufariki katika siku ya kwanza ya maisha yake kuliko akiwa na umri wa mwezi mmoja. Kwa hivyo kipindi cha baada ya kuzaa ni wakati ambapo uangalifu wako wa karibu na utunzaji unaweza kuboresha pakubwa nafasi za maisha ya wanawake na watoto katika jamii yako.

Vifo mwanzoni mwa uchanga (vifo vya watoto wachanga katika siku 7 za kwanza) huchangia pakubwa katika jumla ya idadi ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano. Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa imeonyesha kuwa vifo vya mwanzoni mwa uchanga pekee huchangia takribani asilimia 40 ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano na karibu asilimia 60 ya vifo vya watoto wachanga walio chini ya mwaka mmoja. Watoto wazawa ambao mama zao wamefariki wakati wa uchungu wa kuzaa, au katika kipindi cha baada ya kuzaa wako katika hatari kubwa ya kufariki. Hatari hii hutokana na ukosefu wa utunzaji wa baada ya kuzaa kutoka kwa mama kwa kiasi fulani lakini pia kwa sababu visababishi vya vifo vya kina mama kabla na, katika muda mfupi baada ya kuzaa pia humhatarisha mtoto pakubwa.

Kwa hivyo utunzaji wa kistadi unaotolewa wakati wa uchungu wa kuzaa na kuzaa lazima uendelee kutolewa mwanzoni mwa kipindi cha baada ya kuzaa kwa mama na mtoto hasa na mhudumu yuyo huyo wa afya. Utunzaji huu usiokatizwa unafaa uhusishe kuwashauri kina mama jinsi ya kutambua matatizo yanayohitaji kushughulikiwa haraka kwao au kwa watoto wao na msaada wa kiutendaji ili kuhakikisha kufikia kwa haraka utunzaji wa dharura kwa mama na mtoto iwapo utahitajika. Hii inamaanisha kujenga uhusiano bora kati ya kina mama waliozaa, familia zao na vituo vya afya ya juu vilivyo karibu, na kati ya vituo vya afya na jamii ili kuimarisha utunzaji huo usiokatizwa na utambuaji wa mapema na utoaji wa rufaa kwa matatizo ya baada ya kuzaa.

Kwa kweli, hata mwanamke azalie nyumbani au katika kituo cha afya, kwa hali nyingi huduma za utunzaji wa baaada ya kuzaa hazipatikani kikawaida barani Afrika. Hata ikiwa huduma hizi zipo, mara nyingi hazitekelezwi ifaavyo kutokana na wahudumu wa afya kukosa maarifa na ujuzi, na wakati mwingine kutokana na ukosefu wa vifaa na ruzuku muhimu. Moduli hii ya utunzajibaada ya kuzaa imenuia kujaza pengo la maarifa kwa kukufundisha habari na ujuzi wa kimsingi wa kuwapa mama na mtoto mchanga utunzaji mara tu baada ya kuzaa na kueneza ufahamu wa utunzaji bora baada ya kuzaa kwa wengine nyumbani na katika jamiii kwa jumla. Ina vikao tisa vya somo vinavyoangazia mada zifuatazo:

  • Kuhusika kwa jamii katika utunzaji wa baada ya kuzaa
  • Dalili za kawaida na zisizo za kawaida kwa mama na mtoto mchanga katika kipindi baada ya kuzaa
  • Utathmini na utunzaji wa mtoto mchanga
  • Kushauri juu ya unyonyeshaji
  • Kuhakikisha mtoto anapata joto
  • Kuzuia maambukizi na mambo mengine
  • Utunzaji maalum kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wa ujauzito kuisha na waliozaliwa na uzito wa chini

Inamalizika kwa mwongozo juu ya kujenga mfumo wa njia mbili wa rufaa kati yako katika jamii na wahudumu katika kituo cha afya ya juu ili uchunguzi na utatuzi maalumu baada ya kuzaa uweze kufanyika haraka iwapo utahitajika.

Kanuni na mbinu zote zilizofundishwa katika moduli hii zitaimarishwa na kufafanuliwa katika mafunzo yako ya juzi tendaji na pia katika moduli ya baadaye juu ya Uthibiti Ambatano wa Maradhi ya Watoto wachanga na ya Utotoni. Kuunganisha nadharia na utendaji wa utunzaji wa baada ya kuzaa na Uthibiti Ambatano wa Maradhi ya Watoto Wazawa na ya utotoni kutakuwezesha kuboresha afya na kudumu kwa kina mama, watoto wazawa, wachanga na wakubwa katika jamii yako.