2.1.1 Uterasi

Uterasi ya mwanamke aliye na ujauzito uliokomaa huongezeka kwa ukubwa angalau mara kumi zaidi ilivyokuwa kabla ya ujauzito. Uterasi (bila kuongeza uzani wa mtoto, plasenta, guliguli aminio na kadhalika) huwa na uzani wa takriban kilo 1, ilhali uzani wake kabla ya ujauzito huwa kati ya gramu 50 hadi 100. Mara tu mtoto anapozaliwa, uterasi inaweza kutomaswa karibu na kitovu cha mwanamke huyo inaponywea ili kuondoa plasenta na membreni ya fetasi. Uterasi hunywea na kurudi katika hali yake ya awali ya kabla ya ujauzito katika wiki sita ya kwanza baada ya kuzaa. Hata hivyo, mwingi wa upunguaji huu wa uzani na ukubwa wa uterasi hufanyika katika majuma mawili ya kwanza. Kufikia wakati huu, uterasi inafaa kuwa imenywea kwa kiasi cha kuweza kutosha katika pelvisi ya mwanamke huyo chini ya kitovu.

Bitana ya ndani ya uterasi (endometriamu) hupona kwa haraka baada ya kuzaa ili kurejea katika hali yake ya kawaida uterasini mwote isipokuwa eneo la plasenta kufikia siku ya saba. Ndani ya uterasi, sehemu ambapo plasenta ilikuwa imejishikiza hukumbwa na mabadiliko ambayo hupunguza idadi ya kapilari za damu zinazoingia katika eneo hilo. Kapilari zitakazobaki huvuja kiowevu cha damu kwa muda fulani na husababisha kutoka kwa mchozo wa kawaida ukeni uitwao lokia. Mchozo huu mara nyingi huendelea kwa majuma kadhaa baada ya kuzaa. Lokia huwa na damu yenye rangi ya karibu kati ya kahawia na nyekundu katika juma la kwanza lakini hubadilika muda unaposonga na kuwa maji maji yanayotiririka. Mchozo huu huendelea kupunguka na rangi yake kubadilika kuwa manjano hafifu. Kipindi ambapo lokia huendelea kutoka hutofautiana. Hata hivyo, muda wa wastani ni takribani majuma matano unaoambatana na mabadiliko katika kiasi na rangi ya mchozo huu. Kila mwanamke anao mtindo wake mwenyewe ulio na awamu hizi mbalimbali za lokia zinazodumu kwa muda tofauti.

2.1 Mabadiliko kwenye viungo vya uzazi katika puperiamu

2.1.2 Seviksi