2.1.3 Uke na vulva

Uke uliopanuliwa sana ili kumruhusu mtoto kupita hunywea pole pole ukirejea katika ukubwa na hali yake ya kawaida ilivyokuwa kabla ya ujauzito kwa kipindi cha takribani wiki tatu baada ya kuzaa. Kufikia wakati huu, upitaji zaidi wa damu na kuvimba kwa uke na vulva kunapaswa kuwa kumedidimia. Mwanamke huyo anaweza kuanza tena kushiriki ngono iwapo lokia imekoma, uke na vulva zimepona, hana maumivu na yuko tayari kihisia. Hali ya mwili kuwa tayari kwa kawaida huchukua takribani muda wa majuma matatu hadi matano. Hata hivyo, mwanamke huyo anaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kujisikia kuwa tayari kushiriki ngono na basi hapaswi kulazimishwa kukubali. Jukumu lako ni kuzungumza kwa upole na mwenzi wake ili kuhakikisha kuwa anaelewa na kuheshimu hisia za mwanamke huyo. Katika jamii nyingi kuna desturi inayothibiti wakati ambapo ngono inafaa kurejelewa na mara nyingi huwa baada ya puperiamu kuisha ambayo huwa baada ya majuma sita tangu kuzaa.

Kumbuka kuwa upangaji uzazi ni muhimu kwa kujikinga dhidi ya kupata ujauzito mwingine mara tu baada ya kuzaa. Ovulesheni ya kwanza haiwezi kutabirika na mwanamke anaweza kupata ujauzito tena hata kabla ya kurudi kwa hedhi yake ya kwanza.

Uzazi wa majira ulijadiliwa katika Kipindi cha 14 cha somo la moduli ya Utunzaji katika Ujauzito.

  • Je, ni nini manufaa ya kutumia njia ya kupanga uzazi baada ya kuzaa ili kutoa nafasi ya kuzaa watoto zaidi?

  • Muda wa angalau miaka miwili kati ya uzazi na hata bora zaidi muda huu ukiwa mrefu zaidi hupunguza hatari ya kupata matatizo katika ujauzito utakaofuata. Pia huongeza afya ya fetasi mpya na mtoto mchanga aliyezaliwa awali ambaye huenda bado anahitaji utunzaji na uangalifu wa mama (Picha 2.1).

    Mwisho wa jibu

Picha 2.1 Jukumu la mhudumu wa afya katika jamii ni kuwasaidia kina mama kutumia upangaji uzazi ili kuwe na nafasi kati ya watoto wao. (Picha: Hazina ya Dharura ya Watoto ya Umoja wa Mataifa/ Indrias Getachew)