Somo la 1

Mara nyingi watoto wadogo huona ni rahisi zaidi kutambua tofauti kuliko ufanano. Katika sehemu hii, tutaonesha njia mbili za kupanga wanafunzi zitakazowasaidia kuchunguza tofauti na ufanano baina yao.

Wataweza:

  • kujifunza jinsi ya kubadilishana taarifa kwa ushirikiano na kuchangia kwenye mijadala;

  • kujifunza kuhusu wao wenyewe na wenzao;

  • kujiheshimu zaidi kadiri wanavyotambua kuwa mawazo yao yanathaminiwa kama yale ya wenzao.

Ukiwa mwalimu, ni muhimu kwako ulihimize hili. Iwapo wanafunzi wako wote wataelewa kufanana kwao na kuheshimu tofauti baina yao, watatendeana kwa wema zaidi. Lazima uwe mfano wa kuigwa, kwa kuwatendea wanafunzi wako kwa haki na kwa usawa.

Kabla ya kuanza, ni vyema ufikirie kama unawatendea wanafunzi wako kwa heshima. Je, imeshatokea ukawa na siku mbaya unapowapigia kelele bila sababu? Je, una wanafunzi “vipenzi” unaowatendea kwa wema zaidi ya wengine? Kama unaweza kujibu maswali haya kwa dhati, unaweza kuchukua hatua kuhakikisha kuwa wanafunzi wako wote wanatendewa kwa haki na heshima.

Kufanya kazi kwa namna hii, unahitaji kujiuliza maswali ya kukusaidia kupanga shughuli hizi. Kwa mfano: Ni maswali gani ambayo wanafunzi wataulizana? Ni taarifa zipi watahitaji kuzipata? Watafanya kazi kwa

vikundi? Wawili wawili? Shughuli hii utaipangaje? Utawapatiaje maelekezo kufanya shughuli hizi? Angalia mwalimu anachofanya katika Uchunguzi Kifani 1 kabla ya kujaribu kufanya Shughuli 1 na darasa lako.

Uchunguzi Kifani ya 1: Kufanya kazi katika vikundi kuchunguza kufanana

Chanda anafundisha kwenye shule ya msingi ya kijijini huko Mwenda, Zambia. Anashirikiana na wanafunzi ili ajenge mazingira mazuri darasani. Anaangalia ufanano na tofauti baina ya wanafunzi na anawaelekeza wafikirie namna wote wanavyofanana.

Kwanza, darasa zima linafanya mazoezi ya kuunda sentensi, k.m.: ‘Sote hupenda chakula’; ‘Sote huenda shule’. Kisha, anawagawa katika vikundi vya watano watano, na anawaelekeza wafikirie sentensi tano zinazoanza na: ‘Sote …’ ; mwanafunzi mmoja katika kila kikundi aandike sentensi kwenye kipande cha karatasi.

Baada ya dakika kumi, kila kikundi kinasoma sentensi moja moja. Kama darasa linakubaliana na sentensi, mwalimu Chanda anaiandika ubaoni.

Kwa kutumia sentensi, analionesha darasa namna mbalimbali wanafunzi walivyo sawa:

  • k.m. kimwili –‘Sote tuna ngozi’;

  • k.m. namna tunavyopata hisia zile zile –‘Sote hufurahi’;

  • k.m. hali –‘Sote ni wanafunzi’.

Chanda anayafurahia mawazo ya darasa lake na anapanga kutumia msingi huu kuchunguza tofauti baina yao.

Shughuli ya 1: ‘Sote ni sawa?’

Soma Nyenzo-rejea 1: Ufanano na Utofauti, kabla ya kufanya shughuli hii.

  • Kuanza kuongelea wazo la “kuwa sawa” kwa kuuliza maswali rahisi. Shika penseli mbili na kuwauliza wanafunzi: ‘Je, ziko sawa? Kwa nini?’

  • Shika peni na penseli. Uliza: ‘Je, ziko sawa? Kwa nini?’

  • Rudia, kwa kutumia vitu mbalimbali.

  • Waombe watoto wawili waje mbele. Uliza: ‘Je, wako sawa?’

  • Kuwa mwangalifu. Kama ni wasichana, wanafunzi wanaweza kusema ‘Ndiyo!’. Kama ni msichana na mvulana, wanaweza kusema ‘Hapana!’. Lakini pia wanaweza kutoa majibu mengine, k.m. wanaweza kuwa na urefu ule ule au kuwa na

  • jina lile lile.

  • Ligawe darasa katika vikundi vya wawili wawili. Waelekeze wachunguzane kwa kuzingatia sifa kama urefu, ukubwa wa mguu na ikiwezekana nywele, macho, n.k. na waorodheshe namna wanavyofanana.

  • Washirikiane katika kutoa mawazo, kila kikundi kikitoa wazo moja moja.

Je, walisikilizana? Je, walikubali wazo la kufanana na wakati huo huo kutofautiana? Una ushahidi gani kwa jibu lako?

Sehemu ya 1: Njia za kuchunguza jinsi wanafunzi walivyo