Namba ya moduli 1: Kuchunguza maisha

Sehemu ya 1: Kuainisha viumbe hai

Swali Lengwa muhimu: Utawasaidiaje wanafunzi wapange uchunguzi wao wa viumbe hai?

Maneno muhimu: ainisha; modeli; duru ya maisha; wanyama; mimea; uchunguzi;

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kukusanya na kuonesha vitu halisi kwa mpangilio wa kimantiki darasani kwako ili kusaidia ujifunzaji wa wanafunzi wako juu ya kuweka viumbe hai katika makundi;
  • kutumia uundaji wa modeli kama njia ya kurekodi mambo ambayo wanafunzi wako wanajua juu ya mimea na wanyama mbalimbali;
  • kuwapanga wanafunzi wako wawiliwawili au katika vikundi vidogovidogo ili wafanye kazi miradi za utafiti juu ya duru mbalimbali za maisha.

Utangulizi

Wanafunzi wanahitaji kukua wakiheshimu na kujali ulimwengu wetu wa maumbile; katika hali iliyo bora, sote tunahitaji kuwa wana-maumbile. Wanamaumbile ni watu wenye shauku, wachunguaji, wadadisi na wanaothamini maumbile –watu wanaojifunza na wanaojali ulimwengu wao daima. Wana taswira wazi na pana katika akili zao kuhusu jinsi mambo yafanyavyo kazi katika maumbile. Matokeo ya uchunguaji mpya yatapata nafasi katika taswira yao pana.

Walimu huwasaidiaje wanafunzi wapate taswira hii pana kuhusu jinsi maumbile yafanyavyo kazi? Sehemu hii inatalii jinsi unavyoweza kuwasaidia wanafunzi wapangilie na kupanua maarifa yao kuhusu viumbe hai. Utaleta vitu hai darasani kwako, kuandaa maonesho, kuunda modeli na kufanya utafiti na wanafunzi wako.