Somo la 3

Kuthamini kufanana na kutofautiana baina ya wanafunzi wako kutakusaidia kuwa mwalimu bora zaidi. Utaweza kupanga vizuri zaidi kulingana na mahitaji yao. Endapo wanafunzi wako pia wanajielewa wao wenyewe na kuwaelewa wengine, watajiamini zaidi katika ushiriki wao darasani.

Jinsi wanafunzi wanavyotambua namna wanavyotofautiana na watu wengine, ni muhimu wasijisikie kuwa wametengwa au kuachwa. Sehemu ya wajibu wako ni kuwasaidia waelewe kuwa kukubaliana na watu katika jambo moja na kutokukubaliana katika mambo mengine ni jambo linalokubalika na si sababu ya ugomvi.

Watoto wanapoonekana kuwa tofauti kutokana na maumbile au wanavyotenda, watoto wengine wanaweza kuwaonea au kuwatania. Kuonewa kunaweza kuwafanya watoto wakose raha. Hali hii inaharibu kazi za shule na kuwazuia kupata marafiki.

Watoto wanahitaji kujifunza jinsi ya kushirikiana na wengine. Wajibu wako ukiwa mwalimu ni muhimu katika kuwasaidia kuelewa tofauti kati ya mema na mabaya.

Unawezaje kuhimiza jambo hili? Soma Nyenzo-rejea ya 4: Kuwachunguza wanafunzi wako kwa dokezo la awali. Hapa chini kuna baadhi ya mawazo ambayo unaweza kuyatumia. Yajaribishe. Yanafaa? Umepata matatizo yoyote?

Uchunguzi Kifani ya 3: Kuwasaidia wanafunzi kuheshimu tofauti za kila mmoja

Bibi Bulengo ana mvulana ambaye ni zeruzeru darasani kwake. Siku moja, aliwaona baadhi ya wasichana wakimcheka na kumtania kwa kumpa majina. Baada ya masomo, aliwauliza: ‘Kwa nini mlikuwa mnatenda vile?’ Aliwauliza wangejisikiaje kama mtu angewatania wao, na walifikiri mwenzao alijisikiaje baada ya kutaniwa. Kwa maswali kama haya aliwasaidia kufikiria kuhusu tabia zao. Kwa kutafakari kwa namna hii, baadaye, aliamua kuwasaidia wanafunzi wake kuheshimu tofauti za kila mmoja.

Siku iliyofuata, darasani, alitumia hadithi ya mtoto mwenye polio kuanzisha majadiliano kuhusu jinsi ambavyo wanafunzi wake wangejisikia kama wangekuwa na polio. Pia alitumia maneno na mawazo ya kuzungumzia vitu wanavyopenda, wasivyopenda na hisia alipohitaji kuzungumza na wanafunzi kuhusu tabia zao.

Wavulana wawili walipokuwa wanapigana, Bibi Bulengo alizungumza nao, mmoja mmoja, kuchunguza kwa nini walichukiana na kuwasaidia kusuluhisha mgogoro wao. Mtoto mmoja alipokuwa amekaa mwenyewe aliwaambia wenzake wachunguze ni kwa nini anakaa peke yake na wafanye naye urafiki. Kwa njia hii, wanafunzi wake walianza kujaliana shuleni na kwingineko. Bibi Bulengo alifurahi sana.

Shughuli muhimu: Wigizo kifani kuhusu tofauti

Soma Nyenzo-rejea muhimu: Tumia wigizo kifani/mazungumzo/tamthilia darasani

  • Wapange wanafunzi katika vikundi vya watu watano watano.

  • Kiambie kila kikundi kifikirie kaka wawili na dada wawili ambao vitu wanavyovipenda na wanavyovichukia ni kinyume. Waambie wafikirie mgogoro baina yao.

  • Waambie waigize igizo kifani kuhusu mgogoro huo. Wanafunzi wawili kutoka katika kikundi watakuwa kaka au dada. Wengine wanaweza kuwa mama, baba na babu/bibi.

  • Kwanza, ni lazima waigize kuhusu mgogoro, kisha wajadili pamoja mgogoro huo. Halafu, wafanye igizo kifani kuhusu njia za kusuluhisha mgogoro huo ambazo ni lazima ziwe za amani.

  • Halafu, kikundi lazima kijadili mawazo yao kuhusu chanzo cha mgogoro na suluhisho.

Mwishoni, kielekeze kila kikundi kiigize igizo kifani lake darasani, na pia waeleze wamejifunza nini. Kusanya mafunzo haya, na uyabandike ukutani ili kumkumbusha kila mmoja.

Nyenzo-rejea ya 1: Kufanana na kutofautiana