Nyenzo-rejea ya 1: Kufanana na kutofautiana

Usuli/welewa wa somo kwa mwalimu

Kuna njia nyingi ambazo kwazo watu hufanana, kuanzia sifa za maumbile ya nje mpaka haiba. Pia, kuna njia nyingi ambazo kwazo tunatofautiana. Hata hivyo, kwa wanafunzi vijana, mara nyingi ni muhimu zaidi wao kujisikia wako sawa na wengine, na kuwa sehemu ya kikundi.

Kwa kuelewa njia ambazo sisi sote tunafanana, tunapiga hatua ya kwanza ya kujielewa wenyewe. Pia, tunaanza kuona jinsi ambavyo sisi ni sehemu ya kikundi au jumuiya. Kuwasaidia wanafunzi kuelewa kuwa wao na wanafunzi wenzao wote ni sawa na ni lazima watendeane haki, ni sehemu muhimu ya jukumu la msingi la mwalimu.

Kufanana na kutofautiana kwa maumbile

Njia ya wazi zaidi ambayo watu wanatofautiana ni katika maumbile yao. Wengine ni warefu, wengine ni wafupi. Wengine ni wanene, wengine ni wembamba. Kama unawafundisha wanafunzi wako kuwaeleza ufanano na utofautiano baina ya watu, basi kuangalia sifa za maumbile ni mwanzo rahisi.

Lakini ni lazima uwe mwangalifu: kama ilivyo kwa watu wazima, watoto pia wanajali sana maumbile yao yalivyo; kwa hiyo ni lazima ujaribu kuhakikisha kuwa husemi jambo ambalo linaweza kumfanya mwanafunzi ajisikie kuwa ameaibishwa. Badala yake, lenga kwenye ufanano kama vile, Wote tunavaa nguo’. Utahitaji kuwa makini hasa endapo una watoto ambao wana ulemavu wa viungo katika darasa lako.

Vilevile, wakati mwingine watoto huwatania au kuwaonea watoto wengine, na kuelekeza makini kwenye tofauti za kimaumbile darasani kunaweza kuchochea tabia ya namna hiyo nje ya darasa. Kwa hiyo, pamoja na kuwasaidia kutambua tofauti zao za kimaumbile, ni lazima pia kusisitiza kiasi cha ufanano kilichopo. Endapo wanafunzi wataweza kuona uwiano baina yao na wenzao, kuna uwezekano wa kuwatendea kwa heshima wenzao.

Kufanana na kutofautiana katika haiba

Wakati ni rahisi kuona ufanano na utofautiano baina ya watu kimaumbile – jinsi tunavyoonekana – yumkini ni muhimu zaidi kwa wanafunzi kuelewa kufanana na kutofautiana kwa haiba baina ya watu – jinsi tunavyofikiri, tunavyohisi na tunavyotenda.

Maoni na hisia zetu zinaathiri jinsi tunavyowatendea watu wengine. Kwa muhtasari, tunaweza kusema:

  • 'Maoni’ hujumuisha watu wanavyofikiri kuhusu vitu – endapo wanapenda au hawapendi kitu fulani, au wanakubaliana au hawakubaliani na jambo fulani. Tofauti za maoni wakati mwingine husababisha mabishano na mapigano, iwe ni kwa watoto au watu wazima. Maoni yanaweza kutokana na ujuzi ambao unaonekana wazi na ni wa kweli au uvumi ambao kila mara hauna uhakika.

  • ’Hisia’ hujumuisha mihemko ya watu – endapo kitu fulani kinawafanya wafurahi, wahuzunike, wakasirike au waogope, n.k. Wakati mwingine ni vigumu kueleza hisia, na kama mtu ana hisia tofauti kuhusu kitu fulani kinachokuhusu wewe, inaweza kuwa vigumu wewe kukielewa.

Kadiri watoto wanavyokua, ni muhimu kwao kuweza kuelewa hisia na mihemko yao, kushirikiana na watu wengine, na kutambua mahitaji ya wengine. Ni muhimu kwa watoto kujifunza kuwa si kila mtu hufikiri na kuhisi kwa namna ileile kama wao. Mawazo, hisia na maoni ya kila mtu yatakuwa yameathiriwa na mazingira ya nyumbani kwao, uzoefu na walezi. Aina hizi za tofauti zisichukuliwe kama ni tatizo – isipokuwa pale zinapokwenda kinyume na tabia zinazokubalika kisheria.

Shughuli zilizo katika moduli hii zitawasaidia wanafunzi kuanza kuthamini tofauti hizo, zikiwa ni msingi wa urafiki na kufanya kazi pamoja.

Ukiwa mwalimu, unahitaji kuelewa hisia za wanafunzi wako na kuhakikisha kwamba unazingatia hisia na tofauti zao unapopanga mafunzo yao. Lazima uzingatie ukweli kwamba baadhi ya wanafunzi watafurahia shughuli fulani – kwa mfano, kuzungumza mbele ya darasa – na wengine hawatafurahia.

Hata hivyo, lazima uwatendee wanafunzi wako kwa haki na usawa. Ukimtendea kila mwanafunzi tofauti darasani, watoto wataliona hilo na wataanza kufanya hivyohivyo, ndani na nje ya shule.

Nyenzo-rejea ya 2: Kuuliza maswali kuhusu hisiai