Nyenzo-rejea ya 2: Kuuliza maswali kuhusu hisiai

Taarifa ya msingi/ welewa wa somo wa mwalimu / nyenzo-rejea za mwalimu za kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Unatakiwa kuwa makini unapouliza maswali yanayohusu hisia. Si wakati wote wanafunzi hupenda kuzungumza hadharani kuhusu hisia zao. Unatakiwa kuuliza aina ya maswali yatakayowapa wanafunzi nafasi kujibu wanavyohisi kwa utulivu.

Njia mojawapo ya kufanikisha hili ni kuuliza maswali kwa darasa zima badala ya kumwuliza mwanafunzi mmoja mmoja. Uliza maswali kama vile; ‘Nani anapenda…’ na ‘Nani hapendi…’ huku wanafunzi wakinyoosha mikono. Kama wakijiona ni sehemu ya kundi la darasa, wanafunzi watajisikia kutoaibika katika kutoa hisia zao.

Unaweza kufanya hivyohivyo kwa kutumia mbinu ya uchangiaji wa majibu ya maswali kutoka darasa zima. Kwa mfano, uliza: ‘Kitu gani kinakuogopesha?’ kisha, kwa haraka, andika mawazo ya wanafunzi ubaoni. Kwa kutumia mbinu hii, huwezi kumfanya mwanafunzi mmoja mmoja ajihisi amefichuliwa sana hisia zake.

Kama unataka wafanye mazungumzo kwa undani zaidi kuhusu hisia zao, wapange katika vikundi vya wawili wawili na wafanye mazoezi yanayofanana. Bila shaka wataona ni rahisi kuzungumza kwenye kundi dogo.

Aidha, unaweza kutumia hadithi kuchunguza mawazo nyeti – hii husaidia wanafunzi kuzungumza kwa uhuru zaidi kwa vile hawajihisi kama wanazungumza kuhusu yaliyowapata wao wenyewe.

Unaweza kutunga hadithi yako mwenyewe na kuisimulia kwa wanafunzi wako. Au unaweza kutumia hadithi ya watoto wa mitaani wa Kitanzania iliyopo hapa chini ili kuchochea majadiliano. Ama toa nakala ya karatasi – moja kwa kila kikundi – au soma kwa darasa zima kutoka katika nakala yako.

Baada ya wanafunzi kusikia hadithi kutoka Arusha Times, waulize jinsi wanavyojihisi kuhusu maisha ya watoto. Je, yanafanana au yanatofautiana na maisha yao wenyewe? Wangejisikiaje kama wangeishi maisha hayo? Wangependa nini na wasingependa nini kuhusu maisha ya aina hiyo?

Caption Kabla watoto hawajaja mitaani, wanakuwa wameachwa katika hali iliyowafanya wasiwe na furaha nyumbani, shuleni au katika jamii yao.

Wakati mwingine ukimwona mtoto wa mitaani, fikiria anakotoka

Imeandikwa na Hannah Johnson na Caroline Ellson

Asasi isiyo ya Kiserikali ijulikanayo kama Mkombozi kwa Watoto wa Mitaani inayo furaha kuwa na makala mpya itakayotoka mara kwa mara katika Arusha Times. Katika wiki zijazo, tutakuwa tunajadili masuala mbalimbali yanayowahusu watoto wa mitaani, ikiwa ni pamoja na sababu za watoto kukimbilia mitaani, maisha ya mitaani na mikakati mbalimbali ya kushughulika na watoto wa mitaani.

Jamii haipendi kuona watoto wa mitaani wakiombaomba katika mitaa ya Arusha. Mtoto unayemwona akiomba pesa mara nyingi hana njia nyingine na asingependelea kuishi maisha ya mitaani.

Kila mtoto huondoka nyumbani kwao kutokana na sababu mbalimbali; na Mkombozi inaamini kwamba watoto wanaoondoka majumbani kwao ni watoto walio katika mazingira hatarishi.

Kabla watoto hawajaja mitaani huwa wameachwa katika hali iliyowafanya wasiwe na furaha nyumbani, shuleni au katika jamii yao. Mkombozi inaamini kwamba watoto wanaoishi katika umaskini, waliodhalilishwa au kutelekezwa, ambao mama zao ni wahanga wa ugomvi wa majumbani au waliodhalilishwa katika nyumba zao, wapo katika hatari ya kwenda mitaani. Mara nyingi watoto wa mitaani hutoka katika familia ambamo ugomvi na kupigana ni jambo la kawaida kuliko upendo na uangalizi; ambamo fedha za familia hutumika vibaya na hazitumiki kwa ajili ya watoto; na ambamo watoto hawapati fursa ya kwenda shuleni.

Watoto wanapojiona wapo kwenye hali kama hizi, hujihisi hawana njia nyingine isipokuwa kuondoka majumbani kwao, kutafuta maisha bora zaidi. Wanaweza kusafiri mpaka Arusha na kuambulia patupu - hakuna kazi wala nafasi ya kusoma, hivyo wanalazimika kufanya uhalifu mdogomdogo na kuombaomba.

Tunapowaangalia watoto wetu wenyewe, tunatamani kamwe wasingefanya uamuzi huo wa kukimbilia mitaani. Tunatamani kamwe wasingelazimika kuishi maisha ya kutojua mlo wao utakaofuata utatoka wapi. Tunataka watoto wetu waishi bila kudhalilishwa na tunataka wapate fursa za elimu na kazi.

Watoto wanaoishi mitaani ni kama watoto wako na wangu, lakini hawa hawakupata msaada wa kuwa na nyumbani kwenye usalama na upendo. Watoto wengi unaowaona Arusha tayari wameshapatwa na madhara mengi kuliko umri wao. Wakati mwingine ukiwaona watoto wa mitaani, jaribu kukumbuka kwa nini wako hapo. Maisha hayajawapa nafasi ya kutosha ya kuwa mahali pengine.

Jaribu kukumbuka kuwa kila mtoto ni mtu pekee. Wanayo ya kusimulia na wamejilea wenyewe, wengine ni wadogo kiasi cha umri wa miaka minne. Wengi wao wanatoka katika familia zenye maisha yaliyo mabaya kuliko ya mitaani.

Ni lazima tukumbuke kwamba watoto wanaoishi mitaani wako katika hatari; na kwamba tunatakiwa kuwapa upendo, uangalizi na fursa. Tunapowaona watoto wa mitaani tunahitaji tutambue vyema kwamba wao ni watoto tu, kama walivyo watoto wetu.

Kama unataka kuwasaidia, badala ya kuwapa pesa, watoto wa mitaani wangefurahi zaidi kupata chakula na watu wa kuzungumza nao, badala ya kuwapuuza kila mara.

Mkombozi inajishughulisha na watoto wa mitaani na vijana tangu 1997 na ufadhili wao unawafikia watoto zaidi ya 1,000 kila mwaka katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro nchini Tanzania.

Hannah Johnson na Caroline Ellson ni Watumishi wa Kujitolea wa Mkombozi.

Vyanzo vya asili:Mkombozi Centre for Street Children, Website

Vyanzo vya asili: The Arusha Times, Website

Nyenzo-rejea ya 1: Kufanana na kutofautiana

Nyenzo-rejea ya 3: Jinsi ya kuendesha uchunguzi wa darasa