Nyenzo-rejea ya 3: Jinsi ya kuendesha uchunguzi wa darasa

Taarifa za msingi/Welewa wa somo wa mwalimu

Uendeshaji wa uchunguzi ni mbinu muhimu sana kwa wanafunzi wako kujizoeza stadi nyingi mbalimbali. Hizi hujumuisha:

  • kuuliza maswali;

  • kuweka kumbukumbu za aina mbalimbali za taarifa;

  • kulinganisha majibu;

  • kusema na kuandika;

  • kudadisi zaidi kuhusu kila mmoja.

Hata hivyo, unahitaji kufikiri na kuandaa kwa uangalifu sana kuhusu uendeshaji wa uchunguzi katika darasa lako, na pia jinsi utakavyouelezea kwa wanafunzi wako.

1. Uchunguzi ni nini?

Uchunguzi ni namna ya kukusanya taarifa kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu mada fulani. Inaweza kuchunguza maoni mbalimbali katika kikundi, na kusaidia kudadisi zaidi kuhusu mtu mmoja mmoja.

Katika kukusanya taarifa, kwa kawaida uchunguzi hutumia jedwali kuweka kumbukumbu za majibu. Jedwali hapa chini ni mfano ambapo majibu yanaweza kurekodiwa kwa urahisi na kwa haraka:

Jina:........................................
1. Unapenda…?
2. Unapenda …?
3. Unapenda …?

Uchunguzi ni mbinu inayowavutia wanafunzi kujizoeza katika kujitafutia taarifa.

Kwa kuwa uchunguzi huhusu hatua nyingi mbalimbali, itachukua somo zima au zaidi kumaliza, ikiwa wanafunzi watawauliza watu wengine nje ya shule. Kutoa muda ili ukusanyaji wa data ufanyike ni muhimu sana katika kumhusisha kila mmoja na kumfanya aweze kuona mchakato mzima kwa vitendo.

2. Kuchagua Mada

Wakati wa kuamua kufanya uchunguzi na darasa lako, unatakiwa kufikiri kwa uangalifu kuhusu jambo litakalofanyiwa uchunguzi – taarifa gani unataka kuichunguza? Kwa ufafanuzi, uchunguzi lazima ulingane, kwa namna fulani, na mada ya darasani. Kwa mfano, kama unafundisha kuhusu chakula, uchunguzi wa aina mbalimbali za vyakula vinavyopendwa na watu utatoa taarifa muhimu za kuanza majadiliano kuhusu vyakula vinavyopendwa na visivyopendwa. Wanafunzi wanaweza kutoa mawazo – hii itawafanya washiriki zaidi katika shughuli hiyo.

Katika hatua hii, ni muhimu kufikiri kuhusu stadi ambazo watoto wanapaswa kuzikuza na kuzifanyia mazoezi. Panga uchunguzi ambao utalandana na madhumuni yako ya ufundishaji.

3.Uandikaji wa Maswali

Ni vizuri kwa wanafunzi kufikiri na kuandika maswali yao wakati wa kufanya utafiti wa aina yoyote ile. Kila mwanafunzi au kundi la wanafunzi wanapaswa kuwa na mawazo yao. Lakini unahitaji kufikiri namna ya kuwapanga wanafunzi kutekeleza jambo hili. Watalifanya kipekee, wakiwa wawili wawili au wakiwa katika vikundi?

Ili kuwasaidia wanafunzi katika kufanya utafiti unaweza kuhitaji kuamua (ama wewe mwenyewe au pamoja na wanafunzi):

  • wafanyeje kazi k.m. kipekee, wakiwa wawili wawili au wakiwa katika vikundi;

  • waaandike maswali mangapi (kwa kawaida maswali 3-5 yanatosha);

  • waulize maswali ya aina gani (toa mifano yako na waelekeze watoe mifano zaidi ili kubaini kama wameelewa)

  • watumie muda gani katika kuandikia maswali hayo – dakika 10-15 zinatosha kwa maswali 3-5.

Ni muhimu kufanya yote yaliyotajwa hapo juu na darasa zima kabla ya kuanza kufanya kazi.      Wakati wa kufanya kazi hiyo, zunguka darasani ili kuona wanavyofanya kazi zao na kuhakikisha kuwa kweli wameelewa.

Aina ya maswali watakayoandika yatategemea aina ya taarifa wanazotaka kutafuta. Kwa mfano, kama lengo la utafiti ni kupata taarifa ya idadi ya wanafunzi wanaofikiri, au wanaopenda au kutaka kufanya jambo fulani, basi wataandika maswali yanayohitaji majibu ya ‘Ndiyo au Hapana’: k.m. unapenda kucheza mpira?

Lakini kama lengo la utafiti ni kupata taarifa ya mambo wanafunzi wanayopenda darasani, basi aina ya maswali itakuwa ni ile ya kupata maelezo: k.m ‘Unapendelea michezo gani?’ Watapaswa kufikiria jinsi ya kurekodi majibu.

4. Uulizaji wa maswali

Kila mwanafunzi anapaswa kufanya mazoezi ya kujibu maswali. Fikiria jinsi utakavyoendesha somo hili. Hapa kuna mapendekezo machache:

Wanafunzi hawahitaji kuzungumza na kila mmoja darasani. Hili laweza kuchukua muda mrefu na laweza pia kujirudiarudia. Sampuli ya wanafunzi watono hivi wanatosha, na wasizidi kumi kwa kutegemea ukubwa wa darasa.

Kama watakuwa wameandika maswali hayo wawili wawili au katika vikundi, basi wasiulizane maswali. Badala yake waulize maswali wanafunzi wengine darasani au shuleni. 

Kuwaongoza wanafunzi katika vikundi ili kufanya utafiti kunaweza kufanikiwa ikiwa una darasa kubwa. Pia unapaswa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanashiriki katika kuandika na kuuliza maswali. (Ona Nyenzo-rejea muhimu: Utumiaji wa kazi za vikundi darasani).

5. Uandikishaji wa kumbukumbu za majibu

Wanafunzi wanapaswa kufahamu kuhusu majibu wayaandikayo na wayaandike kwa ufupi, kwa kadri inavyowezekana.

Kwa mfano, kama wanauliza maswali yanayohitaji majibu ya maelezo, basi wanaweza kuandika majibu ya neno moja: Swali: Unapenda mchezo gani?

Jibu: Mpira wa miguu/kukimbia/kuruka.

Kama wanauliza maswali yanayohitaji jibu la Ndiyo au Hapana, wanaweza kuandika N au H kama jibu.Kama wanakusanya taarifa zinazohusiana na tarakimu, wanaweza kuweka idadi, kwa alama moja ikimwakilisha mtu mmoja: k.m.

Michezo inayopendwaMpiraKukimbiaKurukaKudaka
IdadiIIIIIIIIIIIIIIIIII

Ni vizuri kupanga utaratibu huu kwa makini, na waelezee wanafunzi kabla ya kukusanya data zao. Ili ugundue kama wameelewa, basi ni vyema uwatake wakueleze walivyoelewa.

6. Ulinganishaji wa Majibu

Baada ya wanafunzi kuuliza maswali na kurekodi taarifa, basi ni vyema kwao kujadiliana wawili wawili au katika vikundi kuhusu data zao na kulinganisha majibu yao. Data hii inaweza kutumika kujadili michezo wanayoipenda na wasiyoipenda na wanaweza kuchora matokeo kwa njia ya grafu ili kurahisisha kuona tofauti ambazo zinawawezesha kujadili maana yake.

Kuonesha wazi wazi matokeo au kuwataka kuandika kuhusu waliyoyapata kutakuwezesha kutambua uelewa wao na kutawapa nafasi ya kufikiri kwa makini zaidi kuhusu data zao.

Nyenzo-rejea ya 2: Kuuliza maswali kuhusu hisiai

Nyenzo-rejea ya 4: Uchunguaji wa wanafunzi