Somo la 1

Ni muhimu kujiandaa kwa ajili ya masomo kwa kupima welewa wako mwenyewe katika somo. Soma nyenzo-rejea 1: Utangulizi wa ukuaji wa kimwili kwa ajili ya kujikumbusha welewa wako. Unahitaji kufikiri kwa makini jinsi utakavyotambulisha mada hii. Kusoma tu maelezo na kudhani kuwa wanafunzi wanaelewa si njia nzuri sana kwa wengi wao katika kujifunza. Unahitaji kupanga somo lako kwa makini, tafakari kuhusu kitakachotokea katika kila hatua ya somo na chunguza kitu ambacho tayari wanafunzi wanakijua na kukifikiria. Angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Kup anga na kuandaa masomo yako kwa maelezo zaidi. Kila somo lazima liwe na matokeo maalum ya kujifunza (nia). Kwa sababu hii, unataka wanafunzi waweze kutambua mambo manne ya msingi yanayochangia ukuaji bora wa kimwili.Kwa kila hatua ya somo, unahitaji kujibu maswali matatu: Ni kwa jinsi gani shughuli hii inachangia katika matokeo ya kujifunza?Wanafunzi watakuwa wanafanya nini kitakachowasaidia kujifunza? Nitakuwa ninafanya nini ili kuwasaidia?Angalia michezo na kazi unazoweza kutumia. Ni izipi zitakazosaidia katika matokeo yako ya kujifunza?

Uchunguzi Kifani ya 1: Fikiria kuhusu ukuaji wa mwili wakati wa kupanga darasa lako

Biduga anafundisha katika shule ndogo kijijini , nchini Tanzania. Muhula huu, mwalimu mwenzake, Maria yuko katika likizo ya uzazi, kwa hiyo Biduga anafundisha darasa kubwa, lenye wanafunzi 85 wenye viwango tofauti kutoka darasa la 3 -6. Hii inamaanisha kuwa analazimika kuwa na watoto walio katika hatua tofauti za ukuaji wa kimwili. Biduga anajua kuwa anahitaji kufikiria hili anapoandaa darasa lake.

Ameshaona kuwa watoto wakubwa mara kwa mara wanawasaidia watoto wadogo kazi. Kwa hiyo, anapanga darasa katika vikundi, kila kikundi kikiwa na jina na `kiongozi’ wa darasa la 6. Kiongozi anahakikisha kuwa kila mtoto yupo, na anaandaa kikundi chake tayari kwa masomo.

Vilevile, amegundua kuwa watoto wadogo wanapenda kuwa na kazi nyingi tofauti katika somo. Anaandaa masomo yakiwa na kazi zenye mitizamo miwili: mmoja kwa ajili ya darasa la 5 -6 na mwingine kwa ajili ya darasa la 3 -4.

Kwanza, anawapa wanafunzi wa darasa la 5 -6 kazi ya kikundi au mazoezi marefu zaidi.

Kisha, anakaa kwa muda na wanafunzi wa darasa la 3 -4, kwa kuwapa kazi fupi zaidi ikiwa ni pamoja na michezo.

Hii inamaanisha kuwa anatakiwa kuandaa masomo yenye hatua nyingi zaidi kwa darasa la 3 –4. Angalia

Nyenzo-rejea Muhimu: Kufanya kazi na kundi kubwa na/au madarasa yenye viwango mbalimbali.

Kwa njia hii, Biduga amegundua tofauti za ukuaji wa kimwili kwa wanafunzi wake na anazitumia katika kumsaidia kuandaa ufundishaji wake.

Shughuli ya 1: Kuandaa somo kuhusu ukuaji wa kimwili

Nyenzo-rejea 1 inahusisha kanuni nne zinazochangia katika ukuaji wa kimwili. Andika andalio la somo linalotoa utangulizi kuhusu hizi kanuni nne kwa wanafunzi wako.

Bainisha shughuli na nyezo-rejea utakazotumia. Unaweza kutumia shughuli zilezile au tofauti ulizotumia katika sehemu ya 1 ya moduli hii lakini angalia kufanana na kutofautiana katika maendeleo ya ukuaji wa kimwili, k.m urefu, ukubwa wa viatu, mkono na urefu wa mkono.

Panga somo lako hivi:

Utangulizi wa somo na matokeo ya kujifunza yaliyokusudiwa. Tambulisha mawazo yaliyo katika Nyenzo-rejea 1, kwa kutumia maarifa ya awali.

Katika vikundi au wawili wawili, wanafunzi wafanye kazi hiyohiyo na nyingine tofauti au kazi yako mwenyewe.

Wanafunzi wafanye kazi nyingine kama hiyo ili uweze kupima welewa wao.

Nyenzo-rejea 2: Kupanga njia za kutoa utangulizi wa kanuni nne za ukuaji wa kimwili kunakupa mwongozo zaidi katika kupanga somo na kukusanya nyenzo-rejea za kukusaidia katika ufundishaji.

Baada ya somo, andaa muhtasari kwa ajili yako kuhusu jinsi somo lilivyofanyika:

Limefanikiwa? Wanafunzi wako walijifunza nini?

Je, kuna kipengele chochote ambacho hakikufanyika vizuri? Kama kipo, kwa nini ?

Utafanya kitu gani tofauti wakati mwingine?

Sehemu ya 2: Kupanga vipindi vya ukuaji na maendeleo ya kimwili