Somo la 2

Katika sehemu ya kwanza ya eneo hili, ulitafakari njia za kupanga ili kuwafundisha wanafunzi wako kuhusu ukuaji wa kimwili. Sasa tutaangalia kipengele kimojawapo: mazoezi ya viungo kwa wanafunzi wanayoweza kuyapata wakiwa shuleni au nyumbani.

Kwanza, somo Nyezo-rejea 3: Matumizi ya michezo na mazoezi ya viungo kwa ajili ya kupata utambuzi.

Unapopanga kutumia michezo katika ufundishaji wako, unahitaji kufikiria kuhusu:

maudhui ya mchezo, ili yaweze kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo ya kujifunza uliyopanga katika somo lako; mpangilio wa mchezo:

Unachezaje mchezo?

Utawapaje maelekezo wanafunzi wako? Utapimaje kama wanaelewa jinsi ya kucheza? Watacheza wawili wawili , kwa vikundi au kama darasa? Watachezea wapi –nje au ndani ya darasa?

Watacheza kwa muda gani?

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia michezo inayopendwa na wanafunzi

Amani, mwalimu wa Dar es Salaam alitaka kutumia michezo ya wanafunzi katika somo lake. Kwa hiyo, alipanga somo ambapo :

  • watabainisha michezo wanayoipenda;

  • wataeleza jinsi ya kuicheza;

  • kutumia michezo kujifunza kuhusu dhana na mada mbalimbali kama vile kushirikiana pamoja na namba.

Mwanzo wa somo, alitumia njia yauchunguzi wa ‘ninayopenda’ na ‘nisiyopenda’ kupata michezo wanayojua wanafunzi wake. Ili kuokoa muda, alipanga kufanya yafuatayo:

  • kufanya uchunguzi kwa kutumia darasa zima kwa wakati mmoja

  • mwalimu mwenyewe kurekodi maelezo ubaoni.

Kisha, aliwataka wanafunzi kufanya jambo fulani wenyewe. Aliamua kuwa, katika vikundi, wangeandika maelezo kuhusu mchezo wanaopenda, lakini pia wangeandika majibu kwa maswali lengwa yatakayoeleza jinsi ya kucheza mchezo huo. Aliweka maswali kama: Unauchezea wapi? Watu wangapi wanaweza kucheza? Vifaa gani vinahitajika? Sheria zake ni zipi ?

Mwishoni, alitoa nafasi kwa kila kikundi kueleza mchezo wao darasani. Wangepiga kura na kucheza mchezo mmoja kila wiki.

Somo Nyenzo-rejea 4: Jinsi Amani alivyofundisha somo lake kwa maelezo zaidi kuhusu mambo aliyofanya Amani.

Shughuli ya 2: Mchezo rahisi wa namba

Jaribu mchezo huu na darasa lako. Mchezo unazoeza kujumlisha namba 1 mpaka 10 na kuwapa wanafunzi mazoezi ya viungo.

  • Wanafunzi wanaunda duara. Unasimama katikati na kuwapa jumla rahisi, k.m 2 +3.

  • Wanafunzi wanaruka na kuunda vikundi ambavyo idadi yao inatoa jibu la jumla inayotakiwa: k.m 2 +3 =5; wanaruka katika vikundi vya wanafunzi 5

  • Mtu mpya anasimama katikati, na kutoa jumla na mchezo huendelea.

Endapo darasa lako ni kubwa, tengeneza mduara zaidi ya mmoja au mchezo ufanyikie nje ili kupata nafasi zaidi. Kama una kundi lenye madarasa tofauti, tengeneza mduara kwa kila darasa. Kwa madarasa ya chini, wanaweza kufanya mazoezi ya kujumlisha na kutoa. Kwa madarasa ya juu wanaweza kufanya mazoezi ya kuzidisha na kugawanya.

Wanafunzi wako walisema nini kuhusu mchezo huu?

Wamejifunza nini?

Unawezaje kutumia mchezo huu katika kuandaa somo la sayansi au Kiingereza? Marekebisho gani utakayofanya ili kuuandaa, na wakati huohuo, uendelee kuhusisha mazoezi ya viungo?