Nyenzo-rejea ya 2: Kutumia michezo na mazoezi ya viungo

Taarifa za msingi/Welewa wa somo wa mwalimu

Mazoezi ya viungo yanasaidia katika kazi nyingi. Kama tujuavyo, yanasaidia watoto katika kuwajengea uimara na ustahimilivu. Lakini yanaweza pia kuwasaidia wanafunzi kukuza stadi za kijamii, kiubunifu na za uongozi. Yanaweza kuwasaidia wanafunzi kupata marafiki na kujifunza vitu vipya, na yanaweza kuchangia katika afya zao kihisia.

Fikiria kuhusu wigo wa michezo na mazoezi ya viungo ambapo kuna:

  • Mashindano ya riadha mf. mpira wa miguu, mieleka;

  • Michezo mf. Kuruka kamba, dansi, kukimbizana;

  • Michezo ya maneno na namba mf. Kuimba, kukariri.

Watoto watabuni na kuchezo michezo pamoja na wengine bila kuambiwa na unaweza kuchukulia zoezi hili kama sehemu ya ufundishaji wako.

Utumiaji wa michezo na mazoezi ya viungo kama sehemu ya ufundishaji wako kutawahamasisha wanafunzi wafurahie kujifunza na hivyo kujenga hamu kubwa ya kwenda shuleni.

Kwa kutumia michezo kama sehemu ya ufunzaji wako, utawahamasisha wanafunzi wajifunze stadi mpya na tabia mbalimbali.

Stadi hizi zinaweza kujumuisha:

  • Kujifunza kwa kushirikiana;

  • Ujuzi wa kufikiri;

  • Kushirikiana na kubadilishana nyenzo rejea;

  • Hamasa na kushiriki katika ujifunzaji.

Zote hizi ni sifa ambazo unatakiwa uzihamasishe darasani, kwani wanafunzi watashiriki katika ujifunzaji bora.

Hapa chini utaona mifano ya michezo kutoka Tanzania na sehemu za Afrika ambayo inahusu mazoezi ya viungo.

SIMBA, SIMBA

Lengo:

Kumkamata ‘swala’

Zana:

Hakuna, ingawa kitambaa cha kufunga macho kutumika badala ya kufumba tu macho.

Idadi ya wachezaji:

Watano (5) na kuendelea

Kanuni:

Wachezaji wote huunda mduara.

Wachezaji wawili huanzisha mchezo. Mmoja ni Simba na mwingine ni Swala.

Simba na Swala wanakuwa wanafungwa macho kwa kitambaa au wanafumba macho yao na wanawazunguka wengine. Wachezaji katika mduara wanaanza kwa kuita ‘Simba, Simba’. Wanaita kwa nguvu na kwa haraka wakati Simba anapomkaribia Swala na wanaita kwa taratibu na kwa sauti ya chini sana wakati Simba anapokuwa mbali na Swala.

Ikiwa Simba atamkamata Swala – au ikiwa Simba hatamkamata Swala ndani ya dakika moja – anachaguliwa Simba mwingine.

NYOKA

Lengo:

Kuwafanya wachezaji wote washiriki kama sehemu ya ‘nyoka’

Zana:

Hakuna, ingawa unaweza kuweka alama kwenye mipaka ili kuonesha eneo la kuchezea.

Idadi ya wachezaji:

Watatu (3) na kuendelea.

Kanuni:

Mchezaji mmoja anachaguliwa kuwa kichwa cha nyoka. Huyu ‘nyoka kichwa’ anajaribu kumkamata mchezaji mwingine, na anapofanikiwa, huyo mchezaji mwingine anakuwa ‘nyoka mkia’ na wanashikana mikono.

‘Nyoka kichwa’ na ‘nyoka mkia’ wanawakimbiza wachezaji wengine, na kuwazuia kila upande, hivyo kufanya kichwa kipya au mkia mpya kwa kukamatwa kwa mchezaji mwingine.

Mchezo unaendelea hadi wachezaji wote wanakuwa ni sehemu ya ‘nyoka’.

KURUKA MFUKO WA MAHARAGE

Lengo:

Kuwa mchezaji wa mwisho anayeweza kuruka mfuko wa maharage.

Zana:

Kamba, mfuko wa maharage au gunia lingine la aina hii

Idadi ya wachezaji:

Watano (5) na kuendelea

Kanuni:

Ifunge kamba kuzunguka gunia, na acha kamba ya kutosha ya kulifanya gunia libembee popote.

Mchague mchezaji awe ‘mbembeeshaji’ (mbembeeshaji atatakiwa aweze kulifanya gunia libembee likiwa na mfuko wa maharage pande zote ardhini). Kila mchezaji lazima aruke mfuko huo kabla ya kumfikia.

Kama kamba itampiga mchezaji, mchezaji huyo atatolewa kwenye mchezo. Mchezo unaendelea hadi anabakia mchezaji mmoja tu akiwa amesimama, na huyu anakuwa ndiye mshindi.

Kutofautiana:

Urefu wa kamba huweza kupishana/kutofautiana.

Mbio anazotumia ‘mbembeshaji’ zinaweza kutofautiana.

KAMATA MKIA WAKO

Lengo:

Kukamata mkia wa timu nyingine.

Zana:

Leso za mkononi au skafu. Pia unaweza kuweka alama kuonesha eneo la kuchezea.

Idadi ya wachezaji:

Wanne (4) au zaidi

Kanuni:

Wachezaji wanajigawa katika timu. Kila timu inatengeneza msafara. Kila wachezaji (katika miisho yote miwili) ya kila msafara huning’iniza leso ya mkononi au skafu kwenye mfuko au mkanda wao.

Mtu wa kwanza katika mstari anaongoza timu katika ufukuzaji, na anajaribu kuukamata ‘mkia’ wa mtu wa timu nyingine.

Timu inashinda wakati wanapokamata ‘mkia’ kutoka timu nyingine

Imerekebishwa toka: Motherland Nigeria Games, Website, and CanTeach African Songs, Chants, and Games

Nyenzo-rejea ya 2: Kupanga njia za kutoa utangulizi kuhusu kanuni nne za ukuaji wa kimwili.

Nyenzo – Rejea 4: Jinsi Amani alivyofundisha somo lake