Somo la 2

Umewafundisha wanafunzi mawazo kadhaa juu ya vyakula na lishe na kuwapa nafasi ya kuchangia mawazo yao.

Hata hivyo, katika kuzungumzia kuishi kiafya, unahitaji pia kuwahamasisha wakuze tabia za kiafya, kwa kutekeleza wanachojua. Kwa kutumia majadiliano, unaweza kuwahimiza wafikirie tabia zao za kila siku na kupambanua jinsi ya kuziboresha.

Zifuatazo ni baadhi ya mada zinazoweza kujadiliwa:

  • mazoezi;

  • kula mlo kamili kwa kadiri iwezekanavyo;

  • kuhifadhi chakula kibaki salama;

  • kudumisha usafi.

Kuandaa majadiliano huhitaji upangaji makini. Vikundi vitafanyia kazi wapi? Nani atakuwa katika kikundi kipi? Unaweza kutaka kuwa na vikundi vyenye mchanganyiko wa watu wenye haiba tofautitofauti ili kusaidia majadiliano na mwingine kushika nafasi ya kiongozi wa majadiliano.

Kuwatia moyo wanafunzi washiriki, vipangie vikundi maswali matatu au manne. Kuwahimiza wanafunzi washiriki, vipangie vikundi maswali matatu au manne. Swali moja au mawili yanaweza kuwa rahisi kujibu –k.m. Taja tabia tatu za kiafya –na maswali mengine yawahimize kueleza mawazo yao –k.m. Unadhani ni tabia ipi ambayo ni muhimu kabisa? Kwa nini unasema hivyo?

Ni muhimu kwamba kila mwanafunzi aheshimu mawazo ya wengine, na kila mwanafunzi awasikilize wengine kwa makini.

Uchunguzi kifani ya 2: Majadiliano ya Darasani kuhusu kuishi kiafya

Bibi Mmasi alitaka kukuza mawazo ya wanafunzi wake kuhusu kuishi kiafya. Aliamua kupanga majadiliano juu ya mada tofauti, mada moja kila wiki kwa wiki tatu.

Katika majadiliano, alianza mada kwa kutumia picha au hadithi na aliwauliza maswali rahisi ili waanze kufikiri. Kisha aliwaweka katika vikundi vidogovidogo vya watu wanne au watano kujadili mada inayohusiana na hiyo, k.m. Kwa nini tunahitaji kuwa wasafi kadiri iwezekanavyo?

Wakati wanafunzi wakizungumza, alizungukazunguka akisikiliza na mara nyingine akishiriki na kusaidia kuendeleza majadiliano.

Baada ya dakika tano au kumi za majadiliano ya vikundi, alikiuliza kila kikundi walichojadiliana na kuwataka waeleze mawazo yao.

Mwishowe, kwa kushirikiana na wanafunzi, aliandika orodha ya mazoea mazuri ubaoni ili waweze kuyaandika na kuyakumbuka. Siku iliyofuata, aliwataka waitazame orodha tena na kupendekeza yapi walidhani ni muhimu kuliko mengine.

Kisha, Bibi Mmasi aliwapa wanafunzi mada ya wiki inayofuata na kuwataka wafikirie mawazo yao kabla ya somo.

Shughuli ya 2: Kupanga na kuandaa majadiliano

Kwa kutumia darasa lako, utaandaaje majadiliano ya kikundi juu ya kuishi kiafya?

  • Chagua mada ya kujadili au andaa orodha ya mada ili wanafunzi wachague. Panga utangulizi wako.

  • Fikiria watakavyofanya shughuli –wawiliwawili, katika vikundi au kama darasa zima? Andaa kazi –ama kujadili jibu la swali au watake wanafunzi wapange kazi juu ya namna ya kudumisha afya.

  • Tayarisha maelekezo yako. Utahakikishaje kuwa wameelewa?

  • Watazungumza kwa muda kiasi gani? Dakika 10-15 au zaidi? Watakuwa wakifanya nini wakati wa kuzungumza?

  • Mwishoni mwa majadiliano, watake watoe mawazo yao. Fikiria maswali unayoweza kuwauliza kuwasaidia. Utawauliza wangapi? Panga utakavyotoa muhtasari wa mawazo yao bora, labda kwa kuchora ‘ramani ya mawazo’. Tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia ramani za mawazo na kubunga-bongo katika kutalii mawazo.

  • Jadiliana na wanafunzi jinsi watakavyokumbuka na kutumia mawazo hayo.

Tumia maswali haya kupanga somo lako juu ya mada ya kuishi kiafya. Baada ya somo, jiulize jinsi somo lilivyoenda na jinsi ya kuliboresha kwa ajili ya siku nyingine.