Somo la 3

Yapo mambo mengi ambayo watoto wanapaswa kufahamu ili waendelee kuwa na afya. Baadhi ya haya wanaweza kujifunza wakiwa shuleni, lakini wanaweza kujinza mambo mengi nyumbani au katika jumuiya.

Kuwahamasisha wajifunze mengi zaidi kutoka kwenye jumuiya, unaweza kuandaa njia za kuwasaidia kutafuta watu ambao wanafunzi wanaweza kujifunza kutoka kwao. Hili litawatia moyo watake kujifunza. Njia mojawapo ni kuwapa kazi ya nyumbani watoto ambapo watawauliza wazazi au babu/bibi zao kuhusu jambo fulani. Utawasaidiaje watoto wafanye hili? Kwa mfano, ni taarifa gani watakusanya? Ni maswali yapi watauliza? Watarekodije taarifa hizo?

Njia nyingine ni kukaribisha darasani watu katika jumuiya wanaofahamu kuhusu mazoea ya kiafya ya mahali hapo. Hili ndilo analofanya mwalimu katika Uchunguzi kifani 3. Tazama pia Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia jumuiya/mazingira kama nyenzo-rejea .

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia mwenyeji kujifunza juu ya vyakula vya mahali hapo

Bwana Lupogo anamwomba Bibi Mwenda kuzuru darasa lake kuzungumzia vyakula vya mahali hapo. Bibi Mwenda ni mke wa kwanza wa mtemi wa hapo na kila mwaka hutembelea shule kuwasaidia watoto wajifunze juu ya jinsi vyakula vinavyopikwa na kuhifadhiwa.

Analeta unga wa mhogo, unga wa mahindi, samaki wakavu na nyama kavu shuleni na kuwaambia wanafunzi kuhusu jinsi ya kuchemsha vyakula hivi na kuvikausha juani.

Wanapambanua vyakula vyote vinavyopatikana mahali hapo. Tazama Nyenzo-rejea 3 kwa picha za vyakula vya Tanzania. Wanafunzi wanasisimka kwa ugeni huu na wanasikiliza kwa makini. Wanafurahia kuonja vipande vidogovidogo vya ndizi anavyowapikia.

Bibi Mwenda anazungumzia vuno la ngano, ghala la mahali hapo litatosha kwa muda gani, na wanafunzi wanafahamishwa juu ya jinsi vyakula vingine vya mahali hapo vinavyolimwa na kuhifadhiwa.

Bwana Lupogo aliona jinsi namna mpya ya kujifunza ilivyowahamasisha wanafunzi kwa kuwa siku iliyofuata wengi wao walikuja nakumwambia jinsi wazazi wao wanavyopika na kuhifadhi vyakula vyao.

Shughuli muhimu: Kutumia wawezeshaji wenyeji

Shughuli hii inahusu kupanga na kuendesha somo ambapo unamwalika mtaalam mwenyeji darasani. Kupanga jambo hili kwa ufanisi, unahitaji kufikiria yafuatayo:

Wawezeshaji wenyeji wapi wanaweza kuzuru darasa lako? Watahusika na mada ipi ya fya? Kwa mfano:

  • mkulima kuzungumza juu ya vyakula vya kienyeji;

  • mganga wa kienyeji kuzungumza juu ya mimea yenye manufaa;

  • mama wa nyumbani kuzungumzia kuhifadhi na kupika chakula;

  • muuguzi anayeweza kueleza mazoea ya kiafya ya kila siku.

Utahitaji:

  • kupanga shughuli ya kutalii maarifa ambayo wanafunzi wanayo juu ya mada;

  • kujadiliana na wanafunzi maswali gani watamwuliza mgeni;

  • kumwambia mgeni mambo ya kuongelea na muda kiasi gani;

  • kupanga shughuli ya wanafunzi baada ya ugeni kutalii mawazo zaidi.

Katika shughuli ya mwisho, unaweza kutathmini ni kiasi gani wanafunzi wamejifunza kwa kuwataka waandike hadithi au kufanya maigizo kifani na kulishirikisha darasa. Sasa endesha somo lako kama ilivyopangwa hapo juu na fikiria ufanisi wake. Unaweza kuendeleza matokeo ya kazi ya wanafunzi yawe wasilisho la darasani kwa ajili ya mkutano wa shule.

Nyenzo-rejea ya 1: Mazoea ya Kuishi Kiafya