Somo la 2
Watu, hususan vijana, hujisikia vizuri na salama wanapokuwa sehemu ya kundi. Hii ni kweli hasa nje ya familia. Shuleni, kwa mfano, makundi ya marafiki ni muhimu kwa vijana. Mara nyingi makundi ya marafiki huwa na matokeo chanya, lakini wakati mwingine yanaweza kuwa na athari hasi kwa baadhi ya vijana ambao hawakushirikishwa au wanaoonewa na wengine. Katika sehemu hii, utatumia igizo kifani na mbinu ya utatuzi wa matatizo ili kuwasaidia wanafunzi wako kutambua makundi yao na athari zinazosababishwa na makundi hayo katika maisha yao ya kila siku.
Utahitaji kutumia muda kiasi ukitayarisha maigizo kifani yanayofaa kwa kuzingatia umri wa wanafunzi wako darasani. Baadhi ya mapendekezo yametolewa katika Nyenzo-rejea 3: Maigizo kifani katika kutambua mtandao wa shule. Mapendekezo hayo yatakusaidia kuanza, lakini unaweza kufikiria mazingira halisi unayoweza kutumia. Wafikirie kwa makini wanafunzi wako darasani, fikiria matatizo yaliyokwisha tokea na hivyo kuwa makini unavyopanga maigizo.kifani.
Kwa vijana wadogo, ni muhimu kuwasaidia kujenga uhusiano mzuri na urafiki ili wajihisi kuwa kuja shuleni ni kunawaongezea ujuzi chanya. Kutumia hadithi kuhusu mazingira mbalimbali ni njia ambayo inaweza kuhamasisha mawazo ya jinsi ya kusaidiana.
Uchunguzi Kifani 2 inaonesha yaliyotokea wakati mwalimu mmoja alipotumia maigizo kifani na mbinu ya utatuzi wa matatizo darasani mwake.
Uchunguzi kifani ya 2: Makundi ya kirafiki
Mwalimu Mazura alitaka kuwasaidia wanafunzi wake wa darasa la 5 kujadili athari za makundi ya kirafiki. Kwanza alitayarisha kadi zenye matatizo halisi yanayozingatia umri wa wanafunzi wake. Alitumia muda mwingi akifikiria matatizo wanayoweza kuyapata wanafunzi wake, wenye umri wa miaka 11 hadi 12. Alijua kuwa hii ni miaka ya matatizo kwa vijana ambao wameanza kubadilika kimwili na wanaanza kuwa na muongezeko wa homoni. Alitaka pia kushughulikia tatizo kubwa alilokuwa nalo kuhusu kundi la wasichana ambao mara kwa mara walikuwa wakimsumbua msichana mmoja.
Katika mfulululizo wa masomo matatu, mwalimu Mazura aliyauliza makundi matatu kuwasilisha igizo ili kuonesha matatizo aliyoyaonesha katika kadi. Darasa lilikuwa na majadiliano ya kufurahisha baada ya kila wasilisho. Wakati mwingine kulitokea mabishano wakati wanafunzi walipokuwa na mawazo tofauti kuhusu utatuzi wa matatizo, lakini mwalimu Mazura aliwahimiza wasikilizane na waheshimu tofauti zao.
Kwa upande wa kazi ya nyumbani, mwalimu Mazura alilitaka darasa kufanya kazi wawili wawili na watatu watatu ili kufikiria mazingira ambamo wangependa kuigiza kwa ajili ya majadiliano darasani. Jambo hili lilikuwa nyeti, kwa kuwa mwalimu Mazura hakujua hali itakayojitokeza- na hivyo hakujitayarisha. Igizo lilihusisha michezo ya uonevu, kuwa na njaa, na kutokuwa na marafiki shuleni. Mwalimu Mazura alifurahia maigizo yao na alifurahi zaidi kwa kuwa hapakuwa na matatizo au hali ya mshangao.
Shughuli ya 2: Utatuzi wa matatizo katika muingiliano wa darasani
Makundi ya marafiki sio makundi pekee waliyonayo vijana shuleni. Hapa tunaonesha njia nzuri ya kupambanua makundi tofauti unapokuwa na darasa kubwa. Njia hii inahusisha vijana wote wakizunguka darasa wakati uleule, hivyo unahitaji kutunga kanuni ili kudhibiti darasa hilo. Utajikuta kuwa unahitaji filimbi.
Anza kwa kuwauliza wapo katika makundi yapi shuleni. Kila kijana anaandika jina la kundi alilomo katika kipande cha karatasi. Anakifunga nguoni mwake upande wa mbele. Kwa kutoa ishara wanafunzi wanazunguka darasani na kumtafuta kijana mwenzie wa kundi lake. Wape muda wa dakika tatu. Chunguza na kumsaidia kijana asiyekuwa na kundi au ambaye hakupata mwenzie. Piga filimbi tena na kila watu wawili watafute wenzi wao-wape dakika tatu pia. Endelea hivyohivyo mpaka makundi yote yaundwe. Watake wanafunzi wahesabu makundi na wayaandike ubaoni ili kubaini kundi lenye watu wengi/wachache, wasichana/wavulana wengi, n.k.
Watake wanafunzi wako wakae katika madawati yao. Halafu watake waandike wamegundua nini, kwa kumia taarifa iliyoandikwa ubaoni. Unaweza kuwa na majadiliano kuhusu kundi lipi linapendwa zaidi na kwa nini. Au ni kundi lipi lina wanafunzi wachache. Labda wanakundi hili wanaweza kuwasilisha taarifa fupi kuwaeleza wanafunzi wenzio darasani kuhusu shughuli zao. Ungeweza kuwahimiza baadhi yao kujiunga katika kundi jipya.
Kwa vijana wadogo utapenda kurudia haya kwa kufanya na kundi moja baada ya jingine na kuendeleza shughuli hiyo kwa wiki nzima, huku wewe ukiandika mawazo yako.
Somo la 1