Nyenzo-rejea 3: Igizo la kutambua mtandao wa shule
Nyenzo-rejea ya Mwalimu ya kutumia katika kupanga au kurekebisha pamoja na wanafunzi
Haya ni mawazo ya kukusaidia wakati unapofikiria kuhusu maigizo kifani. Kwa fikra zaidi, utaweza kutumia mawazo haya na kufikiria juu ya igizo kifani linalowafaa wanafunzi wako. Kumbuka kufikiria juu ya maswali kwa ajili ya darasa lako, baada ya wanafunzi kumaliza kucheza igizo kifani lao. Inabidi uhakikishe kuwa wanajua wanachotakiwa kufanya na kusema. Hakikisha pia kuwa kila mmoja anapata nafasi ya kuigiza. Unaweza pia kuwauliza wanafunzi kama wanafikiri mwalimu naye ahusike katika mojawapo ya matatizo haya.
Watoto wadogo
1. Fatima na Rose wamekuwa marafiki tangu darasa la kwanza. Sasa wako katika darasa la tatu. Mwanafunzi mgeni, aitwaye Elizabeth amejiunga na darasa hilo. Fatima ameamua kuwa hatakuwa rafiki na Rose zaidi kwa kuwa anaenda nyumbani kwa Elizabeth kucheza na mbwa wao. Rose anakosa raha kwa sababu Fatima si mtu mwenye huruma kwake. Anatumia muda wake mwingi wakati wa mapumziko kulia.
Rose afanye nini ili kutatua tatizo lake?
Fatuma afanye nini kama kweli anamjali Rose?
Elisabeth afanye nini kutatua hali hii?
2. Ahmed ni kijana mwenye soni. Anavaa miwani mizito kwa kuwa haoni vizuri. Hapendi michezo kwa kuwa si hodari wa michezo. Hamna kijana yeyote darasani kwake anayependa kufanya urafiki naye kwa kuwa hachezi mpira.
Mara nyingi yuko peke yake na anachukia shule kwa kuwa hana rafiki.
Unamshauri vipi Ahmed?
Wanafunzi wakubwa
- Isaac anapenda kushirikiana na vijana wanaojiita ‘Timu A’. Wanaonekena kuwa na furaha na wanazungukwa na wasichana. Baadhi huvuta sigara na kunywa pombe. Wanaiba pesa kutoka kwa wazazi wao kununua vitu hivi. Kama hawatapata pesa wanaiba kutoka katika duka la Allen Mushi. Wanasema kuwa kama Isaac anataka kuungana nao, basi lazima alete sigara na fedha.
- Isaac afanye nini?
- Basma amekutana na mvulana ambaye ni mkubwa kwake. Basma ana umri wa miaka 13 na mwenzie ana umri wa miaka 16. Anampenda sana na anafikiria aolewe naye. Anataka kufanya mapenzi naye, lakini Basma hana hakika. Anataka akae naye kama mpenzi wake wa kiume lakini pia ana wasiwasi kuhusu kupata UKIMWI au kupata mimba. Anataka kujiunga na Chuo Kikuu.
- Basma afanye nini?
Nyenzo-rejea ya 2: Muingiliano (Mtandao) wa familia