Somo la 1
Kujadiliana na kuandika hadithi huwasaidia wanafunzi kusema wanachokifikiria kuhusu hali mbalimbali. Hadithi zinaweza kusaidia wakati unapotaka wafikirie masomo magumu.
Lakini pia inachukua muda kuziandaa; unatakiwa ufikirie kuhusu jumuiya wanakotoka wanafunzi wako na uandae hadithi yako kwa uangalifu.Katika Uchunguzi Kifani 1, tunajifunza kuhusu Bibi Oto ambaye anafundisha darasa la sita katika shule kubwa ya msingi iliyopo Kampala.
Aliwataka wanafunzi wake wafikirie kuhusu mahusiano ya kijumuiya yaliyopo katika mazingira ya mji wao na kisha wachunguze kuhusu jumuiya iliyopo kijijini.
Kama unafanya kazi katika mazingira ya kijijini, unaweza ku wataka wanafunzi wako wachunguze hali ya mjini au ya mji.Shughuli 1 hutumia kujifunza kwa uvumbuzi ili kuwasaidia wanafunzi wako ‘kuvumbua’ zaidi kuhusu jumuiya zao wenyewe.
Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia uzoefu wako katika kujadili maisha ya jumuiya
Kwa kuwa Bibi Oto ametokea kijijini kilomita zaidi ya 200 kutoka Kampala, anajua vizuri mambo mengi kuhusu maisha ya kijijini. Kutokana na uzoefu wake wenyewe, aliweza kutunga hadithi kuhusu maisha yake ya pale na kisha kuzitumia na wanafunzi wake. Kutumia uzoefu wake wenyewe kulikuwa muhimu kwa Bibi Oto katika ufundishaji kwani ilimaanisha kuwa alikuwa anajiamini sana kuhusu ujuzi wa somo lake.
Bibi Oto aliwaambia wanafunzi wawili kutoka katika darasa la sita la shule ya msingi wasome hadithi alizoziandika kuhusu jumuiya moja ya kijijini kilichopo nchini Uganda na kisha wanafunzi wengine wawili wasome hadithi
moja kuhusu jumuiya ndogo ya mjini aliyoifahamu yeye. Alizichagua hadithi hizi kwa sababu zilikuwa na vipengele vingi vilivyofanana.Baada ya kusoma kila hadithi, aliwaambia wanafunzi wake wajadiliane katika vikundi vyao kimadawati kuhusu:
- shughuli mbalimbali wanazozifanya watu katika kuendesha maisha yao; watu wanaowasaidia watu wengine katika jumuiya; matatizo ya kila jumuiya –matatizo yapi yanafanana? Matatizo yapi yaliyotofautiana?; viongozi wa jumuiya.
Bibi Oto alivi ambia vikundi kutoa mawazo yao na aliandika vipengele muhimu ubaoni. Walijadiliana kama darasa kuhusu mafanikio na matatizo ya jumuiya mbalimbali na jinsi ambavyo matatizo haya yangeweza kutatuliwa.Kama kazi ya nyumbani, Bibi Oto aliwaambia wanafunzi wafikirie kuhusu jumuiya zao wenyewe. Somo lililofuata, baada ya kila kikundi kuwa kimeshafanya utafiti kwa kiasi fulani (tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kufanyia utafiti darasani ) kila kikundi cha wanafunzi wannewanne kiliandika maelezo ya kikundi chao wenyewe juu ya jumuiya zao. Baadhi ya wanafunzi walilisomea darasa zima maelezo haya
Shughuli ya 1 :Kujifunza kwa njia ya uvumbuzi katika jumuiya husika
Liambie darasa lako libunge bongo kuhusu baadhi ya makundi makuu katika jumuiya husika. Makundi haya yanaweza kujumuisha AZISE, makundi ya kidini, marafiki, familia, viongozi wa jumuiya n.k.
Lipange darasa lako katika vikundi vyenye ukubwa wa kutosha. (Vikundi hivi vinaweza kufuata umri, uwezo au njia nyingineyo).
Waeleze kwamba watatakiwa kujua taarifa ya kundi mojawapo kati ya makundi hayo.
Kiruhusu kila kikundi kichague kundi la jumuiya. Kikundi zaidi ya kimoja kinaweza kuchunguza kundi au asasi hiyo hiyo moja kwani nia na maoni yatatofautiana.
Unaweza kuhitaji kufanya utafiti wewe mwenyewe au wanafunzi wako wanaweza kufanya wao ili kujua zaidi kuhusu kila kundi au kila asasi. Wewe au wao mnaweza kukusanya maandiko ya kuwasaidia katika chunguzi zao. Pia kila kikundi kinaweza kuandaa dodoso na kuwahoji watu wa asasi hiyo. Tazama Nyenzo-rejea 2: Sampuli ya maswali ambayo wanafunzi wanaweza kuuliza ili kujua zaidi kuhusu makundi ya jumuiya husika.
Wapatie wanafunzi muda wa kufanya uvumbuzi, au utafiti.
Somo linalofuata, kiambie kila kikundi kiandae wasilisho kuhusu asasi yao –wasilisho linaweza kuwa kwa njia ya andiko, bango, picha au njia nyingine yo yote ile ya onesho.
Kwa wanafunzi wadogo, ungeweza kuchunguza kundi moja tu na kumwalika mtu kutoka kwenye asasi hiyo kuzungumza na darasa na kutengeneza bango kwa pamoja. Ungeweza kurudia utaratibu huu baada ya muda fulani ili wanafunzi wako wapate kujua kuhusu asasi mbalimbali.
Sehemu ya 2: Kuchunguza nafasi yetu katika jumuiya