Somo la 2
Kwa bahati mbaya, kwa kadiri baadhi ya wanafunzi wanavyokua wanaweza kukutana na uhusiano uliojaa unyanyasaji. Aina hii ya uhusiano unaweza kuathiri vibaya ukuaji wao wa kijamii, kihisia na kimwili, na inachukua muda na juhudi nyingi kuwasaidia washinde uharibifu uliokwisha fanyika.
Dhana ya ‘unyanyasaji’ isichanganywe na lugha ya matusi na karaha. ‘Unyanyasaji’ kwa maana hii hutokea pindi watu wawatumiapo wengine kwa njia isiyo sahihi na isiyofaa. Mahusiano ya namna hii huacha kovu la kudumu la kisaikolojia, kihisia na kimwili kwa mtu aliyenyanyaswa. Kuna aina kadhaa za unyanyasaji, kwa mfano unyanyasaji wa kimwili na wa kiakili. Kuna mifano ya unyanyasaji wa aina hizi katika Nyenzo-rejea 2: Aina za unyanyasaji , ambayo huna budi kuisoma .
Ukiwa mwalimu, wajibu wako ni kuwasaidia wanafunzi kujifunza. Kama hawana furaha au wananyanyaswa, hawatajifunza. Dhima yako ni kuwalinda wanafunzi wako na unaweza kuhitaji kuwahusisha wengine wenye utaalamu zaidi na wanaoweza kutoa ushauri-nasaha. Nyenzo-rejea 3: Dhima ya walimu wa shule inatoa maelezo zaidi juu ya wajibu wako.
Njia bora ya kusaidia ni kutalii na wanafunzi wako mambo wanayofahamu kuhusu tabia sahihi na zisizo sahihi katika mahusiano. Hata hivyo, huna budi kufanya hivi kwa makini na uangalifu. Nyenzo-rejea 4: Kutafiti mambo ambayo wanafunzi wanafahamu tayari kuhusu mahusiano inaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyofanya jambo hili. Unaweza kutumia mbinu hii na wanafunzi wako..
Uchunguzi kifani ya 2: Ajira ya Watoto
Bwana Sele, mwalimu wa Darasa la 5 Shule ya Msingi Mlimani, alimleta Afisa wa Ustawi wa Jamii wa wilaya kuzungumza na darasa juu ya unyanyasaji.
Afisa wa Ustawi wa Jamii alianza kwa kuwaambia wanafunzi kwamba kuwatumia vijana kufanya kazi za biashara na shambani lilikuwa jambo la kawaida katika sehemu nyingi Afrika. Ilikuwa ni njia ya kuwakuza vijana wajifunze stadi na uwajibikaji, na kuweza kujitegemea.
Lakini baada ya ‘Mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Mtoto’ (tazama Utangulizi) kupitishwa, serikali haikuridhika na utumiaji wa watoto kama watembeza bidhaa mitaani na walimaji mashamba, ambako walinyonywa na kulazimishwa kufanya kazi kwa masaa mengi. Ni hatari kwa afya zao, na mara nyingine husababisha kifo. Watoto huachishwa shule na elimu, na mara nyingine husukumizwa kwenye uhalifu.
Afisa Ustawi wa Jamii alisema kuwa wazazi mara nyingine hutoa hoja kwamba wanawahitaji watoto kuleta chakula na fedha kwa ajili ya familia. Hata hivyo, alisema, serikali hulichukulia jambo hili kuwa kinyume na sheria, kwa kuwa watoto wote wana haki ya kupata elimu ya bure, na kwamba kila jumuiya inahitaji kushughulikia suala hili.
Kufuatia hotuba ya afisa wa ustawi wa jamii, siku iliyofuata, darasa la Bwana Sele liliwasilisha igizo kifani juu ya unyanyasaji wa watoto. Walilionesha kwanza kwa shule nzima, na kisha kwa kamati ya Chama cha Wazazi na Walimu (tazama Nyenzo-rejea 5: Jinsi igizo kifani lilivyopokewa) .
Shughuli ya 2: Igizo kifani juu ya unyanyasaji wa watoto
Andaa igizo kifani linalohusika na suala la unyanyasaji wa watoto kwa ajili ya darasa lako. Unahitaji kufikiri kwa makini juu ya hili. Linaweza kuwa suala nyeti sana kwa vijana, hivyo utahitaji kuwa mwangalifu katika uandaaji wa shughuli hii.
Kwanza, orodhesha aina mbalimbali za unyanyasaji wa watoto na matokeo yake. Chagua aina unayotaka kushughulikia darasani.
Fikiria jinsi utakavyoanzisha masuala haya darasani. Kuhusu igizo kifani, amua kuhusu nafasi mbalimbali za wanafunzi. Masuala yapi yanahusika na kila nafasi?
Panga ni wanafunzi wangapi watakuwa katika kila kikundi, na jinsi watakavyoandaa na kuigiza igizo kifani. Utawaelezaje jambo hili?
Mwisho, utaandaaje muhtasari wa mambo muhimu na wanafunzi baada ya kumaliza kuigiza igizo kifani? Utakuwa na mjadala? Utausimamiaje?
Kukusaidia, tumia Nyenzo-rejea kwa ajili ya sehemu hii na Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia igizo kifani/mazungumzo/tamthiliya darasani.
Somo la 1